Francis Cheka 'SMG' |
BINGWA wa IBF Afrika, Francis Cheka ameendeleza ubabe mbele ya mabondia wenzake baada ya usiku huu kumshinda kwa pointi Mmalawi Chiotcha Chimwemwe katika pambano lisilo la ubingwa lililochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.
Cheka amepata ushindi huo katika pambano hilo la raundi 8 japo baadhi ya mashabiki wamedai Mtanzania huyo amebebwa tena kama ilivyokuwa mjini Arusha alipomtwanga Chimwemwe na kutetea taji lake la IBF Desemba mwaka jana.
Ushindi huo umeendeleza rekodi ya Cheka ya kutopigwa katika ardhi ya Tanzania tangu Agosti, 2003 na kwa sasa atakuwa akijiandaa na mchezo wake mwingine lakini wa kimataifa kuwania mkanda wa WBF dhidi ya Mmarekani, Phil Williams atakayepigana naye Agosti 30 katika ukumbi wa Diamond Jubilee.
Pia ushindi huo wa Cheka umekuja saa chache baada ya Mtanzania mwingine na bingwa wa UBO Afrika, Francis Miyeyusho kumtwanga Mzambia Fidelis Lupapa katika pambano lisilo la ubingwa lililofanyika jana kwenye ukumbi wa Dar Live, Mbagala Dar es Salaam.
Miyeyusho alimtwanga Mzambia huyo kwa KO ya raundi ya 8 kati ya 10 zilizopangwa zichezwe katika kusindikiza sherehe za sikukuu ya Eid el Fitri.
No comments:
Post a Comment