STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, August 11, 2013

Yanga, Sc Villa hapatoshi leo taifa, Javu kuendeleza dozi?

Kikosi cha Yanga
TIMU ya soka ya Yanga, inatarajiwa kushuka dimbani jioni ya leo kuvaana na SC Villa ya Ugannda huku mashabiki wakielekeza macho yao kwa Hussein Javu kuona atawafanyizia vipi wageni hao katika mechi hiyo ya leo.

Javu aliyetua Jangwani hivi karibu akitokea Mtibwa Sugar, ameanza na moto kwa kufunga katika mechi zake mbili za awali akiisiaidia Yanga kuisulubu Mtibwa kwa mabao 3-1 na kuizamisha 3 Pillars ya Nigeria kwa bao pekee katika mechi iliyoichezwa katikati ya wiki.

Villa iliyochezea kichapo cha aibu jana toka kwa Simba, itaikabili Yanga itakayotumia mchezo huo kujiweka vyema kabla ya pambano lake la Ngao ya Hisani dhidi ya Azam litakalofanyika siku ya Jumamosi.

Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema jana kuwa maandalizi ya mechi hiyo yamekamilika na kila mchezaji yu tayari kuonesha uwezo wake.

Kwa upande wa Yanga, si tu itaitumia mechi hiyo kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu itakayoanza Agosti 24, pia kunoa makali ya kuikabili Azam FC katika mechi ya Ngao ya Hisani itakayochezwa Agosti 17.

Mechi ya Ngao ya Hisani ambayo ni ishara ya ufunguzi wa Ligi Kuu, itachezwa ikiwa ni siku nne tangu Azam warejee nchini wakitokea nchini Afrika Kusini walikokwenda kusaka makali kwa ajili ya msimu mpya tangu Agosti 3, wakicheza mechi za kirafiki.

Wakati Azam wakitokea Afrika Kusini, Yanga wao tofauti na msimu uliopita ambapo walikwenda kujinoa nchini Uturuki kabla ya kuanza kwa ligi hiyo, safari hii wameamua kujifua nyumbani.

Kwa mujibu wa tovuti ya Yanga, Kocha Mkuu wake, Ernie Brandts, amefurahia kwisha salama kwa mazoezi ya nyota wake hadi jana asubuhi, huku akisema hakuna majeruhi hata mmoja kuelekea mechi ya leo.

“Mechi ya kesho (leo) dhidi ya Villa, itakuwa kipimo kizuri kwetu kwani itakuwa ya mwisho kabla ya kuikabili Azam katika mechi ya Ngao ya Hisani na kuanza kwa Ligi Kuu ya Vodacom,” alisema Brandts.

Kwa mujibu wa tovuti ya Yanga, viingilio vya mechi ya leo ni sh 20,000 kwa jukwaa la VIP A; sh 15,000 kwa VIP B; sh 10,000 kwa VIP C na sh 5,000 kwa viti vya rangi ya machungwa, bluu na kijani.

Wapenzi wa soka na mashabiki wa klabu ya Yanga wameombwa kujitokeza kwa wingi kujionea uwezo wa timu yao kuelekea vita ya kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu ya Vodacom ambao iliutwaa msimu uliopita.

Wakati Yanga iliyoanzishwa mwaka 1935 ikimaliza msimu uliopita na ubingwa ukiwa wa 24 tangu mwaka 1965, Villa ni mabingwa mara 16 tangu ianzishwe mwaka 1975, ambapo mara ya mwisho kuonja ubingwa wa Uganda ni mwaka 2004.

No comments:

Post a Comment