Bondia Ramadhani Kido aliyefungiwa na TPBO |
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Rais wa TPBO-Limited, Yassin 'Ustaadh' Abdallah', Kido alifanya udanganyifu kwa kujiangusha ulingoni sekundu chache baada ya pambano lake na Chipindi kufanyika kwenye ukumbi wa Dar Live na kusababisha usumbufu mkubwa.
Ustaadh, alisema Kido alijiangusha na kugoma kuendelea na mchezo wakati mpinzani wake alipomrushia konde ambalo hata hivyo alikumpata na kufanya mashabiki waliofurika ukumbini kurusha chupoa za maji na kutukana kitu ambacho alisema TPBO haikikubali.
Alisema kilichofanyika ni udanganyifu kama aliowahi kuufanya Francis Cheka kwa kukataa kucheza na Japhet Kaseba na wao kumfungia kwa muda kabla ya kumasamehe, hivyo hata kwa Kido hali itakuwa hivyo kwa vile ameonyesha siyo wanamichezo.
Ustaadh alisema mara baada ya kumalizwa kwa pambano hilo kwa Kido kupigwa kwa KO ya sekunde 23, alimhoji sababu ya kufanya uhuni ule na kwa maelezo yake alimwambia kuwa mpinzani wake alipanda na 'jini' ulingoni lililomdhibiti kitendo alichodai ni kuingiza ushirikina katika michezo.
"Vitendo kama hivi huwa hatukubaliani navyo, tunaamini kabisa bondia huyu hakutaka kupigana ila aliingia mkataba na waratibu ambao ni Global Publishers, hivyo mbali na kumfungia pia tunamtaka arudishe fedha alizochukua kwa pambano hilo," alisema Ustaadh.
MICHARAZO halikubahatika kumpata Kido kusikia maoni yake juu ya tuhuma hizo na adhabu aliyopewa na TPBO, ingawa mashuhuda wa pambano hilo ambalo lilifuatiwa na pigano kali kati ya Francis Miyeyusho aliyemnyuka Mzambia Fidelis Lupapa, ni kwamba Kido alijiangusha.
"Sijawahi kuona bondia anaanguka na kugoma kucheza bila hata kuguswa na ngumi, huu ni uhuni na tumeibiwa fedha zetu. Mambo haya ndiyo yanayofanya ngumi za Tanzania zisiendelee kwa vile zinakatisha tamaa waaandaaji na mashabiki," alisema Ally Kisa 'Kingkong' mmoja wa mashuhuda wa michezo hiyo ya Eid Mosi aliyezungumza na MICHARAZO mapema leo.
No comments:
Post a Comment