STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, October 15, 2013

Abdallah Juma haamini kafunga hat trick, apewa mpira tofauti na Tambwe

Abdallah Juma (kulia) alipokuwa Simba. Hii ni mechi moja wapo kati ta mbili anazodai alizitumikia katika Ligi ya msimu uliopita akiwa na Wekundu hao wa Msimbazi.
MSHAMBULIAJI wa Mtibwa Sugar, Abdallah Juma, amesema bado haamini kama ni yeye aliyefunga 'hat-trick' juzi Jumapili hasa baada ya kutoka katika kipindi kigumu cha kutothaminiwa na klabu ya Simba, huku akibainisha kwamba alikabidhiwa uwanjani mpira wake baada ya kufunga magoli hayo matatu.
Mchezaji huyo alifunga mabao matatu wakati Mtibwa ilipoisambaratisha Oljoro JKT kwa magoli 5-2 katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani na kuwa mchezaji wa kwanza mzawa kufanya hivyo tangu msimu wa 2010-2011.
Katika msimu huo, aliyekuwa mshambuliaji wa Polisi Dodoma, Juma Semsue alifunga mabao matatu na kuwa mchezaji pekee kufunga 'hat-trick' katika ligi kuu ya Bara kwa misimu miwili iliyopita.
Mrundi Amisi Tambwe wa Simba alizindua tukio hilo kwa kufunga mabao manne wakati walipoisambaratisha Mgambo JKT kwa magoli 6-0.
Juma alisema hadi sasa bado anashindwa kuamini kama ni kweli amefunga 'hat-trick' hiyo ya kwanza katika maisha yake ya soka kwa vile msimu uliopita alipokuwa na Simba hakupewa nafasi na alifikia kuanza kukata tamaa ya kucheza soka.
"Kwa kweli nimefurahishwa mno na pia najishangaa kama ndiye mimi yule yule ambaye nilipokuwa Simba sikuaminiwa na msimu mzima nilichezeshwa katika mechi mbili tu tena kwa muda usiozidi dakika 15," alisema. na kzuitamba mechi anazokumbuka aliichezeshwa ni ile dhidi ya African Lyon na JKT Ruvu.
Juma aliyewahi pia kung'ara na timu za AFC Arusha, Kagera Sugar na Ruvu Shooting, alisema kuaminiwa na kupewa nafasi na makocha wake ndiyo kulikomrejesha katika kiwango chake kilichowavutia Simba msimu mmoja uliopita.
"Kuaminiwa na makocha ndiyo siri ya kurejea kwa makali yangu, na huu ni mwanzo tu kwani kiu yangu ni kuendelea kufunga mabao ili nije kuitwa Taifa Stars," alisema.
Aliongeza kuwa tofauti na tukio la aibu la kunyimwa mpira lililomkumba Tambwe wa Simba baada ya kupiga 'hat-trick', yeye katika mechi yao ya juzi alikabidhiwa mpira wake uwanjani na mwamuzi mara baada ya kumalizika kwa mechi hiyo.
"Nashukuru mimi nilipewa mpira wangu," alisema.
Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alitoa ufafanuzi wa tukio la Juma kupewa mpira wake uwanjani tofauti na ilivyokuwa kwa Tambwe akisema ilitokana na hekima ya mwamuzi wa mchezo huo.
"Tulishatoa ufafanuzi tangu mwanzo kwamba hakuna kanuni wala sheria ya jambo hilo zaidi ya kuwapa motisha wachezaji na hivyo alichokifanya mwamuzi huyo ni kwamba ametumia busara na inakubalika," alisema.

No comments:

Post a Comment