STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, March 29, 2014

Shule ya Joyland yasaidia yatima msaada wa thamani ya Sh. Mil.5

Mkuruigenzi wa Shule ya Joyland Pre & Primary, Fred Otieno (wa pili kulia) na mmoja wa walimu wa shule hilo wakikabidhi sehemu ya msaada wao kwa Baba Mlezi wa Kityo cha Kulelea Yatima cha Yatima Trust Fund, Haruna Mtandika (kushoto) huku wakisaidiwa na baadhi ya yatima wa kituo hicho.
Mmoja wa walimu wa Shule ya Joyland, Madam Anna akiwa amempakata mmoja wa yatima wanaolelewa kwenye kituo cha Yatima Trust Fund, mara baada ya kukabidhi msaada wao kwa kituo hicho kilichopo Chamazi.
Mmoja wa yatima, Halima Seif akitoa shukrani zake na kuililia serikali na watu wengine kuwasaidia kuwaendeleza kielimu.
Viongozi wa Shule ya Joyland wakiongozwa na Mkurugenzi wao, Fred Otieno (wa nne toka kulia) wakikabidhi sehemu ya msaada walioutoa leo kwa kituo cha Yatima Trust Fund
Ngojeni tuwasaidie kupeleka ndani! Baadhi ya wasaidia wa kituo cha Yatima Trust Fund wakipelekea misada waliyopewa ndani ya stoo yao
Huu ni mwanzo tu, tutawaletea zaidi
Mkurugenzi wa Joyland Pre& Primary, Fred Otieno akizungumza na vyombo vya habari baada ya kukabidhi msaada wao kwa yatima leo jijini Dar es Salaam.
Baba Mlezi na mmoja wa waasisi wa Yatima Trust Fund, Haruna Mtandika akitoa shukrani zake wakati akizungumza na wanahabari
 UONGOZI wa Shule ya Joyland Pre & Primary ukishirikiana na wazazi wa watoto wanaosoma shule iliyopo Tuangoma, Kigamboni umetoa msaada wa vyakula na vitu mbalimbali wenye thamani ya zaidi ya Sh. Mil. 5 kwa kituo cha kulelea yatima cha Yatima Trust Fund.
Msaada huo ulikabidhiwa leo mchana na uongozi wa Shule hiyo kwa viongozi wa kituo hicho kilichopo Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam katika hafla fupi iliyofanyika kwenye kituoni hapo.
Mkurugenzi wa shule hiyo, Fred Otieno alisema uongozi wa shule yao ambayo haina muda mrefu tangu ianzishwe ukishirikiana na wazazi waliamua kujitolea msaada huo kama sehemu ya kuonyesha namna wanavyoguswa na yatima nchini.
Otieno alisema ingawa walichokitoa ni kidogo, lakini anaamini kitawasaidia yatima hao na kutoa wito kwa watu wengine kujitolea kwa hali na mali kuwasaidia yatima sehemu yoyote walipo.
"Kama sehemu ya jamii tunaguswa na matatizo ya yatima na ndiyo maana tukaamua kuchangishana kuanzia walimu, uongozi wa shule, wazazi na hata wanafunzi ili kuja kuwafariji yatima hawa." alisema.
Otieno alisema yatima hawapaswi kuachwa, hawakupenda kuwapoteza wazazi, hivyo wafarijiwe kwa kusaidia kwa hali na mali na wao wameonyesha mfano ili wengine waige.
Naye Baba mlezi na muasisi wa kituo hicho, Haruna Mtandika aliyepokea msaada huo kwa niaba ya uongozi na yatima wanaolelewa kituoni hapo waliushukuru uongozi wa shule ya Joyland.
Mtandika alisema Yatima Trust Fund iliyoasisiwa mwaka 1996 na kusajiliwa rasmi mwaka 2001 wamefariji kwa kukumbukwa kwa msaada huo na kuwaomba watu waige mfano wa shule hiyo.
"Tunawashukuru sana Joyland kwa kuonyesha moyo wa huruma kwa yatima hawa, na Mungu awabariki zaidi kwani nimesikia shule yenu haina muda mrefu tangu muianzishe lakini umeonyesha mfano wa kuigwa," alisema
Pia alidokeza kwenye risala yao changamoto wanayokabiliana nayo ikiwamo uhaba wa samani kwa ajili ya malazi, chakula, ada na sare kwa watoto wanaowasomesha, ambapo Mkurugenzi wa Joyland, aliahidi kuwasomesha watoto wawili toka kituoni hapo.
Otieno, alisema watoto hao mmoja mmoja wa kike na mwingine wa kiume watasomeshwa kwa kugharamiwa na uongozi wa shuleni kuanzia chekechea hadi darasa la saba.
Naye mmoja wa watoto wanaolelewa kituoni hapo, Halima Seif (16) pamoja na kuushukuru uongozi wa Joyland, pia alitoa wito kwa watu wengine wenye uwezo kuwasaidia kusomeshwa.
"Nilikuwa naomba watu watusaidie, kwa mfano mimi napenda shule, lakini sijaendelea na masomo ya sekondari kwa sababu sina wa kunilipia ada hiyo nawaomba watu wengine watuangalie sisi yatima," alisema Halima huku akimwaga chozi la uchungu.
Mara baada ya makabidhiano hayo, uongozi wa shule, walimu na waalikwa wengine walijumuika kula na kuburudika na muziki na yatima hao kama njia ya kuwafariji jambo lililonekana kufurahiwa na watoto hao.

No comments:

Post a Comment