STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, April 29, 2014

Elias Maguli ajinadi Simba, Yanga, Azam

Elias Maguli
MSHAMBULIAJI nyota wa Ruvu Shooting, Elias Maguli amesema yupo tayari kutua klabu yoyote kati ya Simba, Yanga au Azam, iwapo ataridhishwa na dau atakalowekewa mezani na klabu hizo.
Maguli aliyeshika nafasi ya pili kwa ufungaji sambamba na Kipre Tchjetche na Mrisho Ngassa, wakiwa nyuma ya Amissi Tambwe aliyeibuka Mfungaji Bora, alisema haoni tatizo kuihama Ruvu Shooting kama kuna klabu inayomhitaji.
Alisema, ingawa mpaka sasa hakuna timu yoyote iliyomfuata kumshawishi kujiunga nayo kwa msimu ujao, lakini amekuwa akisoma na kusikia tetesi tu kuwa Simba inamnyemelea na kusema milango i wazi kwao kama wanamtaka.
Maguli, alisema siyo Simba tu bali hata kama ni Yanga, Azam au Mbeya City inamhitaji yupo tayari kujiunga nayo mradi taratibu zifuatwe na masilahi yawe ya kuridhisha kwa sababu maisha yake yanategemea soka kama ajira.
"Nisiwe muongo zijafuatwa na klabu yoyote mpaka sasa, lakini nasikia tu tetesi za kuhitaji na moja ya klabu kubwa nchini, ila mimi nategemea soka klabu yoyote iliyoridhishwa nami milango i wazi waje tuzungumze," alisema.
Kuhusu kushindwa kuendelea na kasi ya ufungaji kama ilivyokuwa kwenye msimu wa kwanza, Maguli alisema matatizo aliyokuwa nayo kwenye duru la pili ikiwamo kuuguliwa na mama yake na sakata lake la kutimka umangani kusaka soka la kulipwa lilichangia kumfanya aachwe mbali na Tambwe.
Maguli aliyekuwa akishika nafasi ya pili nyuma ya Tambwe katika duru la kwanza wakitofautiana bao moja, Tambwe akiwa na 10 yeye akiwa na 9 alijikuta akiachwa mbali na mpinzani wake huyo aliyefunga bao 19 huku yeye na wenzake wawili wakimaliza msimu na mabao 13 tu.
Aidha Maguli amesema anamshukuru Mungu kwa kuweza kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa, chini ya kocha mpya kutoka Uholanzi, Mart Nooij, akidai ni furaha kwake na kuahidi kutomuangusha.
"Namshukuru Mungu, nilikuwa likizo nyumbani Mara na sasa naelekea Mbeya kwenye kambi, nimefurahi sana kocha mpya kunijumuisha kikosini.

No comments:

Post a Comment