STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, April 6, 2014

Yanga, JKT Ruvu vita ya 'wajuanao', mambo yapo Tanga!

Yanga yenye mtihani mzio kwa JKT Ruvu
MABINGWA watetezi leo wataikabili JKT Ruvu katika mechi inayotazamwa kama 'vita' na mtihani wake wa kwanza kuendelea kuipa presha Azam kwenye mbio za kunyakua taji lao la kwanza, lakini pia ni pambano linalokutanisha timu zinazofundishwa na makocha wanaofahamiana.
Fred Felix Minziro aliyekuwa kocha Msaidizi wa Yanga kwa sasa ndiye kocha mkuu wa JKT akichukua nafasi ya Charles Boniface Mkwasa aliyemrithi nafasi yake Yanga, kitu ambacho ni wazi timu hizo zinakutana huku kila mmoja akifahamu udhaifu na uimara wa adui yake.
Pambano hulo ambalo litatoa picha halisi kwa Yanga kama inautema ubingwa au itaendelea kusubiri mpaka mechi zake nyingine tatu, litachezwa kwenye uwanja wa Taifa.
Ingawa ina mechi moja mkononi dhidi ya viongozi wa ligi kuu ya Bara, kimahesabu Yanga iliyo nafasi ya pili imeshavuliwa ubingwa kutokana na kuwa nyuma ya Azam (53) kwa tofauti ya pointi saba kwenye msimamo wa ligi kuu ya Bara.
Matumaini pekee ya Yanga (46) kutetea taji hilo ni kuomba Azam ipoteze angalau mechi mbili katika michezo yake mitatu iliyobaki. Tatizo ni kuwa 'Wauza Koni' hao hawajafungwa msimu mzima.
Aidha, kwa kuwa kocha msaidizi wa Yanga mpaka Desemba mwaka jana, Minziro amesema anajua siri za udhaifu wa mabingwa watetezi hao na atajaribu kuzitumia katika mchezo wa leo.
Yanga ambayo ilikuwa ikipaa kwenye ligi ya kuu ya Bara, imepoteza uelekeo tangu itolewe kwa taabu na Al Ahly ya Misri kwenye Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mwanzoni mwa mwezi uliopita, ikishinda mechi moja tu kati ya nne zilizopita.
Tangu kushinda 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo wake wa mwisho kabla ya kuikabili Ahly, Yanga imetoka sare na Mtibwa Sugar na Azam, kukifunga kibonde Rhino na kulazwa 2-1 na timu dhaifu ya Mgambo JKT iliyocheza na watu 10 kwa saa moja.
Hata hivyo kocha msaidizi wa Yanga Cherles Boniface Mkwasa alisema licha ya kuwa katika mazingira magumu timu yake haijakata tamaa ya kutetea ubingwa huo hata hivyo.
"Kikubwa ni kushinda michezo yote iliyobakia. JKT Ruvu ni timu nzuri lakini naamini sisi ni wazuri zaidi yao na tunaomba ushindi Jumapili," alisema Mkwasa na kueleza zaidi:
"(Kimsingi) tumezidiwa kwa pointi nne na Azam lakini bado hatujakata tamaa kwa sababu kwenye mpira lolote linaweza kutokea."
Ingawa maandalizi ya Yanga kwa ajili ya mchezo huo yalifunikwa na taarifa za kutimuliwa kwa baadhi ya wachezaji muhimu na Emmanuel Okwi kugomea mazoezi, uongozi wa Yanga ulikanusha taarifa hizo za kwenye vyombo vya habari.
Mechi nyingine za ligi kuu ya Bara leo zinakutanisha Coastal Union na Mgambo JKT, JKT Oljoro na Prisons, na Rhino Rangers na Mtibwa Sugar.
Pambano la jijini Tanga baina ya wanadugu Coastal na Mgambo ndilo lenye mvuto kutokana na Mgambo kuonyesha ukali wake kwa vigogo kwa kuwatungua Simba na Yanga, huku Coastal yenyewe ikionekana imeridhika na nafasi iliyonayo baada ya makeke yao ya awali kuwatumbukia nyongo mashabiki wake.
Mgambo inahitaji ushindi ili ijiondoe kwenye janga la kushuka daraja na Coastal itataka kushinda kuendelea ubabe kwa vijana hao na pia kulinda heshima yake.

No comments:

Post a Comment