Kava la albamu ya Afande Bright kama linavyoonekana kwa anayehitaji kupata burudani hiyo anaweza kuwasiliana naye kupitia namba zinazoonekana pembeni au barua pepe |
Afande Bright Mbwilo katika pozi |
Kiu kubwa ya mafanikio katika soka ndiyo iliyomfanya Bright Job Mbwilo kuanza kucheza tangu akisoma Shule ya Msingi Magoye-Makete na baadaye Songwe Mbeya.
Hata alipojiunga na masomo ya Sekondari katika Shule ya Kilombero Day ya Ifakara na baadaye Iyula-Mbozi bado alikuwa akisakata kandanda na kuamini ndoto zake zitatimia.
Haikuwa ajabu kwake kuanza kupata umaarufu akiwa Songwe Stars akicheza kama mshambuliaji na wakati mwingine kiungo au beki wa kati kabla ya kutua Oljoro JKT iliyomsaidia kupata mafunzo ya kijeshi.
Mafunzo hayo yaliyofahamika kama Operesheni Kasi Mpya yalimpa ajira JKT kabla ya kuhamishiwa Mafinga JKT.
Kambi ya Mafinga ilikuwa na kikundi cha sanaa na Mbwilo maarufu kama Afande Bright alianza kujifunza kuimba baada ya wenzake kugundua kipaji kikubwa cha muziki alichonacho.
Kipindi kifupi alijipatia umaarufu na kuteuliwa kuwa mwalimu kwa wenzake katika masuala ya utunzi baada ya kutunga nyimbo za Uhamasishaji za 'Mwanzilishi wa JKT' na 'Naipenda Nchi Yangu'..
"Safari yangu kimuziki ilianzia hapo na kujitosa muziki wa kizazi kipya kabla ya mwishoni mwa mwaka jana hasa nilipoteuliwa na Shaibu Issa kujiunga JKT Ruvu nikitokea Rhino ya Mafinga mwaka 2007."
KIPAJI
Mwaka 2008 alinyakuliwa na Prisons Mbeya na kupata mafunzo Magereza huku akiichezea timu hiyo katika Ligi Kuu msimu wa 2009 kabla ya kuhamishiwa Iringa.
Akiwa Iringa alijiunga na Polisi Iringa kabla ya kwenda kusomea Ukutubi Chuo cha Sanaa cha Bagamoyo na kuanza kushiriki matamasha ya muziki na kufunguliwa neema.
Matamasha hayo yalimfanya apate nafasi ya kurekodi wimbo wake wa kwanza wa Bongofleva uitwao 'Tanzania' aliomshirikisha Mirror.
Baada ya hapo alirekodi nyimbo nyingine kadhaa zilizokuja kuzaa albamu yake ya kwanza iliyofahamika kama Tanzania iliyokuwa na nyimbo nane.
Baadhi ya nyimbo hizo ni; 'Ndani ya Dancehall', 'Zako Style', 'Kiza Kinene', 'Jakaya', 'Nimedata', 'Hawapendi', 'Watanzania', 'Nikiachwa leo' na 'Leave Me Alone'.
Novemba mwaka alipohitimu Stashahada ya Ukutubi, alirejea kwao Mbeya na kuwa miongoni mwa wachezaji waliojaribiwa na Mbeya City kwa ajili ya usajili.
Hata hivyo kwa namna ya ajabu wakati akiendelea na mazoezi ili kusubiri kutangazwa watakaosajiliwa aliugua ghafla kichwa.
MATESO
Mbwilo anayezishabikia Chelsea, Barcelona na JKT Ruvu anasema kichwa kilimpa mateso makubwa, licha ya kuzunguka hospitali kadhaa kubwa ikiwamo ya Aga Khan.
"Mateso niliyopata kwa maumivu ya kichwa yaliyoshindwa kubainika katika hospitali zote nilizoenda kutibiwa kiasi cha kukata tamaa na kutamani kujiua kwa kujirusha ghorafani."
Anasema siku aliyokusudia kujiua ilitokea miujiza kwa kuokolewa na mama zake kabla ya kupelekwa kanisani kuombewa na ndipo ikawa sababu ya kupona kwake na kumpokea Yesu.
"Baadhi ya waumini wa kanisa hilo walibaini mimi nilikuwa mmoja wa waimbaji wa muziki wa kizazi kipya na kunishawishi kumuimbia Bwana na sikuwa na hiyana," anasema.
Anasema kupitia ufadhili wa Papaa Delinson alirekodi albamu nzima ya Asante Bwana yenye nyimbo nane ambazo ameanza kuzitengenezea video kupitia kampuni ya HMC ya mjini Moshi.
Nyimbo za albamu ya msanii huyo anayeshukuru soka kumpa ajira jeshini ni 'Asante Bwana', 'Upendo', 'Vita', 'Hamjui', 'Itakuwaje', 'Twakuheshimu', 'Jinsi Gani' na 'Vita Remix'
Mbwilo anasema ndoto zake kumtumikia Mungu kwa kadri awezavyo ili kurejesha shukrani kwa wema aliomtendea kwa kumuokoa na kifo na tayari ameanzisha kundi liitwalo Makomandoo wa Yesu.
Kundi hilo linalotoa huduma katika makongamano na makanisani linaundwa na wasanii watatu akiwamo yeye (Afande Bright), mdogo wake Robert Mbwilo na Eliah Michael.
Pia anatamani kulitanua kundi hilo na kusaidia wasanii wenye vipaji vya sanaa ili kuisaidia serikali kupunguza tatizo la ajira kwa madai kuwa asilimia kubwa ya vijana kwa sasa wamejiajiri kwenye sanaa.
WITO
Mbwilo mwenye ndoto za kufika mbali kisanii anawataka wasanii wenzake kuwa wabunifu na kuacha kujikita kwenye matumizi ya dawa za kulevya kadhalika wajitambua kama waelimishaji umma.
Pia ameiomba serikali kutunga sheria kali zitakazoweza kumkomboa msanii kupitia jasho lake sawia na kumwezesha kujiweza kisha ndipo wawakamua 'kodi' kinyume na inavyofanyika sasa.
"Huwezi kumkama Ng'ombe bila kumpa malisho, serikali imekuwa ikimbana na kumkamua msanii kupitia stika bila msanii kuanza kukusanya mapato, hii ni ajabu na inakatisha tamaa," anasema.
Mbwilo mwenye mke na mtoto mmoja hupenda kula wali kwa maharage na kunywa Fanta anamshukuru familia yake yote hasa mama yake mzazi Mwalimu Nesi Mziho, Papa Delinson na Enock Masanja wa HMC Production aliyebeba jukumu la kumrekodi video.
"Namshukuru sana Enock Masanja kwa kukubali kubeba jukumu la kurekodi na kusambaza video ya albamu yangu, pia Papaa Denilson na familia yangu nzima kwa kunisapoti kwa hali na mali pamoja na wanasoka wenzangu wote." anasema askari Magereza huyo.
No comments:
Post a Comment