STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, January 4, 2015

Prisons-Mbeya, Ndanda nani kumcheka mwenzake leo?!

Prisons-Mbeya
Ndanda Fc
WAKATI vigogo vya Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, Yanga, watetezi Azam na vinara Mtibwa Sugar wakiwa visiwani Zanzibar kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi na kulazimisha mechi zao kuchezwa katikati ya wiki, leo ligi hiyo itahsuhudia pambano moja ambalo litazikutanisha timu 'vibonde' Prisons-Mbeya itakayoikaribisha Ndanda ya Mtwara.
Pambano hilo litakalochezwa kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya ndilo pambano pekee la ligi hiyo kwa leo baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupangua ratiba na kuahirisha mechi za 'vigogo' ili washiriki vema kwenye michuano ya Mapinduzi iliyoanza siku ya Alhamisi.
TFF ilipangua mechi nne zilizokuwa zichezewe jana na leo zinazohusu timu hizo ambazo sasa zitalazimika kucheza katikati ya wiki kwa wiki inayoanza kesho na wiki ijayo kabla ya mashindano hayo kumalizika Januari 13.
Hata hivyo pambano la Prisons-Mbeya na Ndanda lililokuwa liwe miongoni mwa michezo miwili iliyokuwa imepangwa kucheza leo zenyewe zitaendelea na ligi hiyo, huku kila timu ikiwania pointi tatu kujiondoa maeneo ya mkiani.
Ndanda inayocheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza ipo mkiani ikizibeba timu zote ikikusanya pointi sita tu katika mechi nane ilizocheza itaivaa Prisons ikiwa na kumbukumbu ya kuchezea kichapo toka kwa Mbeya City waliokuwa wakiburuza mkiani tangu ligi iliposimama Nov 9.
Timu hiyo ilikung'utwa bao 1-0 na Mbeya City ambayo leo itakuwa miguu juu kutokana na pambano lao la dhidi ya Yanga kuahirishwa hadi katikati ya wiki.
Wenyeji wao yaani Prisons wapo nafasi ya 13 wakiwa na pointi saba wakitoka kulazimishwa suluhu kwa mabingwa wa zamani Coastal Union katika pambano la wiki iliyopita lililochezwa kwenye uwanja wa huo wa Sokoine.
Timu hizo zinazofundishwa na makocha wazawa David Mwamaja wa Prisons na Meja Abdul Mingange watakuwa na kazi za kuhakikisha vijana wao wanapata ushindi ili kujiweka katika mazingira mazuri kadri ligi inavyozidi kushika kasi.
Prisons ni miongoni mwa timu mbili ambazo zimeshinda pambano moja katika ligi ya msimu huu ikiwa sambamba na Simba ambayo itavaana na Mgambo katikati ya wiki.
Kucheza kwao kwenye uwanja wa nyumbani unaweza kuwa na faida kwao, iwapo kama watagangamala vinginevyo wanaweza kuwapokea Ndanda nafasi ya mikiani kwani iwapo Ndanda itashinda itafikisha jumla ya pointi 9 zinazoweza kuwafanya kuiporomosha hata Simba waliopo nafasi ya tisa kwa sasa.
Hata hivyo kwa namna Prisons inavyocheza soka lake inaweza kuipa mtihani Ndanda iliyoimarisha kikosi chao kwenye usajili wa dirisha dogo, licha ya kuanza kwa kipigo mbele ya Mbeya City.
Baadhi ya wachezaji waliongezwa katika kikosi cha Ndanda kupitia dirisha dogo ni viungo wa zamani wa Yanga, Omega Seme, Kiggi Makassy, Stamili Mbonde na Raymond Zabron wote kutoka Villa Squad, Issa Said, MOhammed Masoud 'Chile' na Zubeir Ubwa waliokuwa huru.

No comments:

Post a Comment