STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, March 4, 2013

Rage: Libolo wametucheleweshea mkutano mkuu

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage



MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Ismail Rage amesema mechi yao ya marudiano ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Recreativo de Libolo ndiyo iliyoikwamisha kamati yake ya utendaji kutangaza mapema tarehe rasmi ya mkutano mkuu wa dharura wa wanachama wa klabu hiyo.
Kamati ya Utendaji ya Simba iliyokutana jijini Dar es Salaam baada ya timu yao kupoteza pambano lao la marudiano la Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa goli 1-0 dhidi ya mabingwa wa Tanzania Bara 1999 na 2000, timu ya Mtibwa Sugar, iliridhia kuitisha mkutano huo wenye ajenda moja tu ya kujadili mwenendo wa timu yao katika michuano mbalimbali inayoshiriki.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Rage alisema kamati yake ya utendaji itatangaza tarehe rasmi ya kufanyika kwa mkutano huo muda wowote baada ya mechi hiyo kuchezwa jana. Alisema uongozi wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, baada ya kuchezwa kwa mechi ya jana, utakuwa na wakati mzuri zaidi wa kuandaa mpango ya fedha na ukumbi ambao mkutano huo utafanyika. 
“Kwa sasa mawazo yetu yako kwenye mechi za kimataifa ndiyo maana inakuwa vigumu hata kutaja tarehe rasmi ya kufanyika kwa mkutano huo. Baada ya mechi ya leo (jana) nafikiri ndiyo tutakuwa na nafasi nzuri ya kuangalia bajeti yetu ikoje kuelekea kwenye mkutano huo,” alisema Rage.
Kamati ya utendaji ya klabu hiyo imefikia maamuzi hayo baada ya timu ya ‘Wekundu wa Msimbazi’ kuwa na matokeo yasiyoridhisha katika michuano mbalimbali iliyoshiriki na inayoshiriki msimu huu ikiwamo ya Kombe la Mapinduzi, ligi kuu ya Bara na Klabu Bingwa Afrika.
Wakati timu hiyo ikiendelea kusuasua katika mbio za kutetea ubingwa wake wa Bara, kumekuwa kukiibuka makundi ndani ya klabu yanayoshinikiza mwenyekiti huyo aachie ngazi kwa madai kuwa ni sehemu ya matokeo mabovu ya timu yao.
Baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo Novemba mwaka jana huku Simba ikikumbwa na matokeo ya sare nyingi na kipigo cha 2-0 kutoka kwa Mtibwa, Tawi la Mpira Pesa liliibuka na kumtaka Rage kama mwenyekiti wa Simba, aitishe mkutano mkuu wa dharura ili kujadili mwenendo wa timu yao katika ligi hiyo.
Rage alipinga vikali maombi ya tawi hilo na kuamua kulifuta kwa mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa katiba ya klabu hiyo kongwe nchini iliyoanzishwa 1936.
Simba inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi kuu ya Bara ikiwa na pointi 31 baada ya kucheza mechi 18 ikizidiwa kwa pointi 11 na mabingwa wa soka Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame na mahasimu wao wa jadi, Yanga waliooko kileleni mwa msiamo baada ya kujikusanyia pointi 42 katika mechi 18 walizocheza.
Nafasi ya pili inakamatwa na mabingwa wa Kombe la Mapinduzi, Azam FC wenye pointi 36 baada ya kushuka dimbani mara 18 pia.


CHANZO: NIPASHE

MWIMBAJI nyota wa muziki wa Injili nchini, Upendo Nkone, ni miongoni mwa wasanii wa ndani watakaopamba Tamasha la Pasaka Machi 31 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Upendo anakuwa msanii wa tatu wa ndani kutangazwa kuwa atashiriki katika tamasha hilo baada ya Rose Muhando na John Lissu ambao walitangazwa Ijumaa na Jumamosi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama alisema mwaka huu katika tamasha hilo wanawapa mashabiki kile wanachokitaka. “Tunakusanya maoni kutoka kwa mashabiki wetu wapendekeze wasanii gani watumbuize, hivyo hao watatu ndiyo mpaka sasa wameshika nafasi za juu kwa kupendekezwa sana na mashabiki. Wengine tutawatangaza kadri mambo yatakavyokuwa mazuri na pia tukiwa tumezungumza nao juu ya ushiriki wao,” alisema Msama.
Tamasha la Pasaka litafanyika Dar es Salaam Machi 31, kisha siku inayofuata itakuwa Uwanja wa Sokoine Mbeya, Aprili 3 itakuwa Uwanja wa Samora Iringa na Aprili 6 Uwanja wa Jamhuri Dodoma na Aprili 7 Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Tamasha la mwaka jana baadhi ya waimbaji mahiri waliokuwapo ni Rose Muhando, Rebecca Malope, Christina Shusho, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Solomon Mukubwa, Atosha Kissava, Ephraim Sekeleti na kundi la Glorious Celebration. Kwaya ya Kinondoni Revival, Mwinjilisti Faraja Ntaboba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zilikuwa miongoni mwa burudani zilizokuwapo siku hiyo.

Mbishi Real sasa ana mboga saba


MSANII wa muziki wa kizazi kipya nchini, Fred Kaguo 'Mbishi Real' amevunja ukimya kwa kuachia wimbo mpya uitwao 'Mboga Saba' ambao umeanza kuchezwa hewani tangu mwishoni mwa wiki.
Akizungumza na MICHARAZO, Mbishi aliyewahi kutamba na vibao kama 'Tozi wa Mbagala' alisema wimbo huo mpya ni wa kufungua mwaka 2013 na ni moja ya kazi alizopanga kuzitoa katika mwaka huu.
Mbishi alisema ameachia wimbo huo wakati akitafakari kuitolea video au la kutokana na kukwazwa na mfumo mpya wa urushaji matangazo wa digitali ambao umefanya kazi za wasanii zisitangazike kama zamani.
"Nimeachia wimbo wangu mpya wa 'Mboga Saba' ambao utaanza kusikika hewani Machi 1, pia nipo katika kizungumkuti kama niutolee video au la," alisema.
Baadhi ya kazi za msanii huyo anayejishughulisha na umachinga ni pamoja na 'Business', aliyomshirikisha marehemu Complex, 'Pombe' aliomshirikisha Q Jay , 'Nimesomeka' alioimba na Bwana Misosi na 'Amebaka' alioimba na Chege na Jay Mo.

Dogo Rama ndivyo alivyo nje ya Twanga Pepeta

Dogo Rama akiwa katika pozi

MTUNZI na muimbaji wa bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta', Ramadhani Athuman 'Dogo Rama' anajiandaa kufyatua albamu ya pili binafsi baada ya albamu ya ile ya kwanza ya 'Kilomita 10,000' kufanya vema sokoni.
Akizungumza na MICHARAZO, Dogo Rama ambaye pia ni rapa wa bendi hiyo alisema mpaka sasa tayari ameshakamilisha nyimbo tatu, mmoja ukiwa umetolewa video yake.
Alizitaja nyimbo hizo zilizokamilika kuwa ni 'Chuki Bila Sababu' alioutolea video akiwa ameimba kwa kuwashirikisha Nyoshi El Saadat, Isha Ramadhan 'Isha Mashauzi', Barnaba na Papi Catalogue, 'Ndivyo Nilivyo' na 'Umaskini Wangu'.
Mwanamuziki huyo aliyekuwa jijini Mwanza kumuuguza mwanae, alisema anatarajia kufikia katikati ya mwaka huu atakuwa ameishakamilisha albamu hiyo nzima aliyopanga iwe na nyimbo zisizopungua nane.
"Nipo katika maandalizi ya kupakua albamu yangu ya pili binafsi itakayochukua nafasi ya 'Kiliomita 10,000 na tayari nimesharekodi nyimbo tatu mpaka sasa," alisema.
Alisema kama ilivyokuwa albamu yake ya awali, albamu ijayo amepanga kushirikisha vichwa mahiri vya muziki wa dansi nchini kwa nia ya kuipa ladha nzuri na tofauti ili kuifanya albamu hiyo iwe ya kipekee.
"Kama ilivyokuwa albamu iliyopita, hii nimepanga kuwashirikisha wanamuziki nyota tofauti ili kuipa ladha zaidi, lengo likiwa kukonga nyoyo za maashabiki wangu," alisema.
Mkali huyo aliyewahi kuzipigia bendi kama Tabora Matata, Msuka na Mwanza Carnival kabla ya kutua Twanga, aliongeza kuwa ana nyimbo zaidi ya tatu kwa ajili ya albamu ya bendi inayotamba na albamu ya 'Shamba la Twanga'.

Muumin aiotabiria makubwa Victoria Sound

Muumin (mwenye shati ya kijani) akiwajibika jukwaani na wanamuziki wa Victoria Sound

UONGOZI wa bendi ya Victoria Sound umetamba kuwa umejiandaa vilivyo kukabiliana na changamoto pamoja na ushindani uliopo kwenye fani hiyo kwa sasa nchini.
Victoria iliyojiimarisha ikiundwa na wanamuziki wakali chini ya rais Mwinjuma Muumin, imedai inatambua muziki wa sasa una ushindani mkubwa, lakini wenyewe wamejiandaa vya kutosha kukabiliana nao.
Muumin alisema bendi yao ilishasoma hali ya upepo na kujipanga na hivyo haiogopi changamoto inazotarajiwa kukabiliana nazo kwani wanajiamini.
Mtunzi na muimbaji huyo aliyewahi kutamba na bendi mbalimbali ndani na nje ya nchi alisema kwa kutambua hali hiyo wapo tayari kwa lolote kuweza kusimama kama zilivyo bendi nyingine zilizozoeleka nchini.
"Hatuna hofu licha ya kuwapo kwa ushindani, Victoria Sound tumejiandaa vya kutosha tukitegemea kazi zetu na wanamuziki tulionao, muhimu mashabiki watupe sapoti wapate burudani waliyoikosa kwa muda mrefu," alisema.
Muumin alisema makali ya bendi yameanza kuonekana kupitia nyimbo walizoachia hewani na zile zilipigwa kwa mara ya kwanza kwenye uzinduzi uliofana wa bendi hiyo uliofanyika siku ya Ijumaa kwenye ukumbi wa Mango Garden, jijini Dar es Salaam.
"Kifupi ni kwamba tumekuja kuwashika, tupo fiti tofauti na watu wanavyofikiria, tuna wasanii wenye vipaji na uwezo mkubwa sambamba na nyimbo kali ambazo tunaamini zitawapa burudani mashabiki wa dansi," alisema Muumin.

Simba yavuna ilichopamba, Azam haoooooooooo!

Kikosi cha Simba kilichoaga michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika

MABINGWA wa soka nchini Simba jana ilikiona cha moto baada ya kutandikwa mabao 4-0 na wenyeji wao Libolo na kuiaga michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wakiwaacha wawakilishi wa Kombe la Shirikisho Azam ikipeta kwa kupata ushindi wa mabao 5-0 Sudan Kusini dhidi ya Al Nasir Juba.
Simbe imeng'olewa katika michuano hiyo kwa jumla ya mabao  5-0 baada ya kulala nyumbani Tanzania kwa bao 1-0 kwenye mechi ya awali.
Ikicheza bila nahodha wake, Juma Kaseja, Simba ilienda mapumziko ikiwa nyuma kwa bao 1-0 kabla ya kufanya mabadiliko yaliyowagharimu kwa kuruhusu mabao mengine matatu yaliyozima ndoto za klabu hiyo kurejea historia ya mwaka 1979 na 2003 katika michuano hiyo.
Katika miaka hiyo Simba iliweza kupata ushindi mnono wa mabao 5-0 Zambia dhidi ya Mufurila Wanderers waliokuwa wamewafunga uwanja wa nyumbani mabao 4-0 na pia mwaka 2003 walienda kuitoa Zamalek ya Misri kwa penati.
Kikosi cha timu kinatarajiwa kuwasili nchini leo ili kuja kuendelea na mbio zake za kutetea taji lake la Ligi Kuu Tanzania, ambapo Jumamosi wanatarajiwa kuvaana na Coastal Union wanaolingana nao pointi.
Wakati Simba wakiaga kwa aibu, wawakilishi wengine wa Tanzania Bara kwenye michuano ya kimataifa Azam imesonga mbele kwa jumla ya mabao 8-1 baada ya kuisambaratisha Al Nasir Juba ya Sudan Kusini jana kwa magoli 5-0 katika mechi ya marudiano wiki mbili baada ya kuilaza mabao 3-1 jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Azam walioenda Sudan Kusini wakiwa kama wamefuzu yalipachikwa wavuni na nyota wake, Mcha Khamis 'Vialli', aliyefunga mabao matatu, John Bocco 'Adebayor' na Salum Abubakar 'Sure Boy Jr' waliofunga bao moja moja.
Kikosi cha Azam wawakilishi pekee wa Tanzania waliosonga mbele kwenye michuano ya Afrika
 Nao wawakilishi pekee wa Zanzibar katika michuano ya Ligi ya Mabingwa, Jamhuri imeaga kwa aibu michuano hiyo kwa kufumuliwa jumla ya mabao 8-0, baada ya jana kucharazwa mabao 5-0 wiki mbili tangu wafumuliwe kwa mabao 3-0 mjini Zanzibar na timu ya Kedus Giorgis ya Ethiopia.

SARAH RAMADHAN AWATOA KIMASOMASO WATZ KILI MARATHON

Kocha wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) akimaliza mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon za Kilomita 21 zilizofanyika leo mjini Moshi. (Picha: Executive Solutions)

Meneja wa Bia ya Kiliamanjaro, Geogre Kavishe akimpongeza Edina Joseph mmoja wa washiriki wa Mashindano ya Kilimanjaro Marathon, yaliofanyika leo, Moshi Mkoa wa Kilimanjaro. (Picha: Executive Solutions)

MWANARIADHA wa Kitanzania, Sarah Ramadhani, jana aliibuka shujaa katika mashindano ya mwaka huu ya mbio ndefu za Kilimanjaro Premium Lager Marathon, baada ya kuibuka mshindi katika mashindano ya kilomita 21, (nusu marathon), kwa upande wa wanawake katika mbio zilizofanyika mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.

 Sarah alishinda mbio hizo baada ya kukimbia kwa dakika 1:13:05 na kujipatia medali ya dhahabu baada ya kuwabwaga wenzake wakiwemo Wakenya ambao wamekuwa wakitawala mbio hizo katika miaka ya hivi karibuni.

 Katika mbio hizo ambazo mwaka huu zimeweka rekodi ya kuwa na washiriki zaidi ya 6,800, Vicoty Chepkemoi, kutoka Kenya alishika nafasi ya pili baada ya kukimbia kwa dakika 1:14:34, ambapo Mtanzania mwingine Failuna Matanga, alishika nafasi ya tatu kwa kukimbia kwa dakika 1:15:35.

Hata hivyo wakenya waliendeleza ubabe wao, baada ya wanariadha wake kushika nafasi ya kwanza katika mbio za kilomita 42 na kilomita 21 wanaume, pamoja na nafasi ya kwanza katika kilomita 42 upande wa wanawake.

Katika mbio za kilomita 42 wanaume, Kipsang Kipkemoi alishika nafasi ya kwanza kwa kukimbia dakika 2:14:56 na kufuatiwa na mkenya mwenzake Julius Kilimo, aliekimbia kwa dakika kwa dakika 2:15:44 ambapo mkenya mwingine Dominic Kiangor alishika nafasi ya tatu kwa kukimbia dakika 2:16:25.

Kwa upande wa wanawake, mkenya Edna Joseph, alishinda mbio hizo pale alipomaliza kwa dakika 2:39:05 na kufuatiwa na Eunice Muchiri, (Kenya), aliekimbia kwa dakika 2:41:00 na watatu alikuwa ni Fridar Too, aliekimbia kwa dakika 2:44:04.

Akiongea muda mfupi baada ya kuwazawadia washindi, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenela Mukangara, aliahidi ushirikiano wa serikali katika kuendeleza michezo hapa nchini.

 “Nichukue nafasi hii kuwapongeza wadhamini wa mbio hizi, Kilimanjaro Premium Lager pamoja na wadhamini shirikishi mbalimbali wa mashindano haya wakiongozwa na mdhamini mkuu, kwani mbali na kuibua na kukuza vipaji vipya, mashindano haya yametokea kuwa mchango mkubwa katika kuitangaza Tanzania na kukuza uchumi wa Kilimanjaro na nchi kwa ujumla kutokana na kushirikisha watu wengi kutoka ndani na nje ya nchi”, alisema.

Aliwataja wadhamini wengine kuwa ni pamoja na Vodacom Tanzania, GAPCO, Tanga Cement, CFAO Motors, KK Security, Keys Hotel, TPC Sugar, Tanzanite One, New Arusha Hotel, UNFPA, Fastjet na Kilimanjaro Water.

Aidha alitoa changamoto kubwa kwa viongozi wa riadha nchini kuhakikisha wanariadha wa Tanzania wanaandaliwa vyema na mapema ili kuendeleza ushindi, ambapo alisema ushindi wa Sarah na Failuna Makanga na mfano mzuri wa matayarisho mema.

Kwa upande wake Meneja wa  Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe alisema kuwa mbio hizi zimeweza kuleta hamasa kwa watu mbalimbali kushiriki mchezo wa riadha kwani Kilimanjaro Marathon ni tukio pekee la kimichezo ambalo linatoa fursa kwa watu wote kushiriki. “Tutaendelea kuwekeza katika riadha kwa kadri tuwezavyo kwa sababu Kilimanjaro Marathon sio tu kwa sababu imeishakuwa tukio linalosubiriwa na wanariadha wetu kila mwaka lakini pia ni tukio ambalo limeendelea kuitangaza nchi yetu kimataifa”, alisema.

Kavishe alisema tangu mbio hizi zilipofanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2003, Kilimanjaro Premium Lager iliamua kudhamini tukio hili kwa kuzingatia umuhimu wake kwa nchi yetu katika kukuza na kuendeleza mchezo wa riadha na vilevile kuutangaza Mlima Kilimanjaro ambao ni fahari ya Watanzania kama ilivyo bia yao ya Kilimanjaro Premium Lager.