STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, April 1, 2014

Magaidi wailipua tena Kenya, sita wafa

 

MILIPUKO mitatu katika mji mkuu wa Kenya wa Nairobi imesababisha vifo vya watu 6 na karibu darzeni mbili kujeruhiwa jumatatu usiku katika mtaa mkubwa wenye wakazi wengi wa asili ya Kisomali wa Eastleigh.     

Mkuu wa polisi wa County ya Nairobi Benson Kibue anasema milipuko hiyo ilitokea takriban saa moja na nusu usiku  na kwa karibu wakati mmoja katika migahawa ya Sheraton Café na The New Kwa muzairua Grill.


Kufuatana na mmiliki wa Sheraton Café Bw. Patrick Gakuyu watu walikuwa wanatizama taarifa ya habari ya saa moja kwenye televisheni wakati aliposikia milipuko miwili na umeme kuzimika na kuwa katika kiza. Anasema anadhani ni grunetti mbili zilizorushwa ndani ya mgahawa wake.


Jumapili usiku karibu na mtaa huo mtu anayedhaniwa ni gaidi aliuwawa alipokuwa anatengeneza milipuko yake pamoja na wenzake watatu. Na gruneti moja ilipatikana siku hiyo hiyo ya jumapili katika mji wa pwani wa Lamu ndani ya kanisa moja.


Usalama umeimarishwa katika miji mikuu ya Kenya na hadi hivi sasa haijulikani aliyehusika na mashambulio ya jumatatu.
Voa

Ulaya ni vita leo Man Utt vs Bavarians, Barca vs A. Madrid

Lionel Messi kufanya nini leo kwa Atletico Madrid>
Watetezi Bayern Munic watavuna nini Old Trafford

Mashetani Wekundu watawamudu Bavarians leo nyumbani kwao>
KIVUMBI cha Ligi ya Mabingwa kinatarajiwa kuendelea tena leo kwa michezo ya hatua ya Roibo Fainali kuanza ambapo mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Bayern Munich ya Ujerumani itakuwa ugenini kuvaana na Manchester United.
Wakichechemea kwenye nafasi ya saba ya msimamo wa Ligi Kuu ya England kufuatia msimu mbaya wa kwanza chini ya kocha David Moyes, Man U hawapewi nafasi katika mechi zao mbili za robo fainali dhidi ya miamba hao wa Ujerumani ambao tayari wameshatwaa ubingwa wa msimu huu wa Bundesliga.
Moyes atakuwa na matumaini kidogo kufuatia matokeo ya wikiendi wakati mwendo wa Bayern wa kushinda mechi 19 uliposimamishwa na sare ya 3-3 nyumbani dhidi ya Hoffenheim baada ya kupoteza uongozi wao wa magoli 3-1 huku Man U ikiisambaratisha Aston Villa 4-1 kwenye Ligi Kuu.
Man U haifanani kabisa na timu ambayo ilikuwa ikitisha Ulaya chini ya utawala wa Alex Ferguson lakini kiwango chao cha nyumbani katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu huu kimekuwa cha kuvutia, tofauti na rekodi yao mbaya Old Trafford kwenye ligi kuu ya England.
Mabingwa hao wa England wameshinda mechi zao nne za kwanza katika michuano hiyo ya Ulaya msimu huu, jambo ambalo walilifanya mara ya mwisho katika msimu wa 2007-08 wakati waliposhinda mechi nne kati ya sita na kwenda kutwaa kombe hilo mjini Moscow.
Lakini Bayern, inayofundishwa na Pep Guardiola ambaye aliisambaratisha Man U katika mechi za fainali mwaka 2009 na 2011 akiwa kocha wa Barcelona, imeshinda mechi zao saba zilizopita za ugenini katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya. Pia waliwang'oa Man U kwa sheria ya magoli ya ugenini katika hatua kama hiyo 2010.
"Hatuwezi kuruhusu hali waliyonayo Manchester United kwenye ligi kuu kwa sasa iathiri mtazamo wetu kwenye mechi hii," nahodha Bayern, Philipp Lahm aliiambia uefa.com.
"Tutaenda Manchester ili kucheza mpira wa kushambulia na kufunga magoli. Sidhani kama inajalisha kwamba umecheza kwanza mechi ya ugenini. Mwaka jana tulicheza mechi zetu nyingi za kwanza nyumbani na bado tukatwaa kombe.
"Jambo la muhimu zaidi kwetu ni kufunga magoli katika mechi ya ugenini," aliongeza Lahm, ambaye kikosi chake iliwang'oa Arsenal kwa kutumia magoli ya ugenini katika hatua ya 16-Bora msimu huu.
Moyes anaweza kubeba ushujaa waliouonyesha katika hatua iliyotangulia ya 16-Bora wakati walipolala 2-0 ugenini dhidi ya Olympiakos Piraeus kabla ya kushinda 3-0 nyumbani Old Trafford, shukrani kwa 'hat-trick' ya Robin van Persie.
Van Persie atakosa mechi zote mbili dhidi ya Bayern kutokana na kuwa majeruhi lakini Wayne Rooney amekuwa katika kiwango kizuri, kilichomshuhudia mshambuliaji huyo Muingereza akifunga magoli mawili dhidi ya Villa na kufikisha jumla ya mabao matano mwezi uliopita na 15 katika ligi msimu huu.
Moyes haoni kama kucheza mechi ya kwanza nyumbani kama ni faida kwa wapinzani.
"Kwa mechi zinavyokwenda sasa kwa soka la mashambulizi ya kustukiza na mbinu tofauti za kukabili mchezo zinazotumiwa na timu zinazocheza ugenini (inamaanisha hamna umuhimu)," alisema.
Mechi hiyo inazikutanisha timu mbili ambazo zimetwaa ubingwa wa Ulaya mara nane jumla na walikutana katika fainali ya 1999 mjini Barcelona ambako Man U walipata ushindi wa kukumbukwa wa 2-1 kwa magoli ya dakika za lala-salama.
Kipigo hicho kiliwatafuna Bayern kwa miaka mingi lakini wamekuwa wakiwafunga Man U kila walipokutana nao tangu wakati huo na itakuwa ni miujiza kama Wajerumani hao watashindwa kutinga nusu fainali.

BARCA v ATLETICO MADRID
Mechi nyingine ya robo fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya leo itakuwa ni baina ya Barcelona na Atletico Madrid, itakayokumbushia upinzani wa kocha Gerardo Martino na Diego Simeone waliokuwa nao wakati wote wakicheza soka kwao Argentina.
Simeone alikuwa hajafikisha umri wa miaka 18 wakati alipokabiliana na Martino, ambaye amemzidi umri kwa takriban miaka 10, katika mechi ya ligi baina ya timu ya Velez Sarsfield na Newell's Old Boys Januari 1988, na kumshuhudia Martino akitolewa kwa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu kiungo mwenzake Simeone, ambaye naye pia alitolewa kwa kadi nyekundu dakika 10 baadaye.
Simeone ambaye si mgeni katika matukio ya utata wakati akicheza soka -- kumbuka alivyohusika katika kumfanya kiungo wa timu ya taifa ya England, David Beckham atolewe kwa kadi nyekundu katika mechi ya Kombe la Dunia 1998 -- alikiri mwaka jana kwamba alidanganya kaumia ili kumsababishia kadi nyekundu Martino.
Takriban miongo mitatu baadaye, Martino na Simeone wanaziongoza timu mbili za Hispania zenye nafasi adimu ya kutwaa mataji mawili ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya na La Liga.
Atletico wako pointi moja juu ya Barca kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Hispania huku mechi saba zikiwa zimesalia ligi kumalizika na mechi yao mwisho msimu huu ni safari nyingine ya kwenda kuwakabili Barca kwenye Uwanja wa Nou Camp mwezi Mei.
Tayari timu hizo zimeshakutana mara tatu msimu huu, huku matokeo yote yakiwa ni sare.
Barca waliwashinda Atletico katika mechi ya ufunguzi wa msimu ya Kombe la Super Cup wakati goli la Neymar katika sare ya 1-1 katika mechi ya kwanza mjini Madrid lilipotosha kuwapa taji Barca baada ya timu hizo kutoka sare ya 0-0 katika mechi ya marudiano Nou Camp. Mechi yao ya La Liga kwenye Uwanja wa Calderon mwezi Januari pia ilimalizika kwa sare ya bila magoli.
Wakati Diego Costa yuko katika kiwango cha juu, kikosi cha Diego Simeone kitalazimika kumchunga vyema Lione Messi ambaye amewafunga magoli 20 katika mechi 19 dhidi Atletico, zikiwamo 'hat-trick' tatu.
Washindi wa raundi hii baada ya mechi za marudiano zitakazopigwa wiki ijayo, wataingia katika 'droo' ya nusu fainali itakayopangwa Aprili 11.
Kesho, Real Madrid watawavaa Borussia Dortmund, wakati PSG watawakaribisha Chelsea.

Wema Sepetu, Batuli kupamba tamasha la Kanumba Foundation

Yobnesh Yusuf 'Batuli'
Wema Sepetu 'Madam'
WASANII maarufu wa filamu nchini, Wema Sepetu na Yobnesh Yusuf 'Batuli, ni miongoni mwa wasanii watakaonogesha tamasha la mfuko maalum, utakajulikana kama Kanumba The Great Foundation, litakalofanyika Aprili 7, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Dar Live.
Akizungumza Dar es Salaam jana, mratibu wa tamasha hilo kutoka kampuni ya Vannedrick, George Wakuganda, alisema kuwa
Wema na Batuli wamekubali kushiriki tamasha hilo.
Wakuganda alisema kuwa tamasha hilo litafanyika siku kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Steven Kanumba.
"Wema na Batuli wamekubali kuungana na wasanii wenzao katika tamasha hilo kubwa ambalo litakuwa ni mara ya kwanza kufanyika tangu kifo cha Kanumba," alisema Wakuganda.
Alisema kuwa maandalizi ya tamasha hilo yanaendelea vizuri kama yalivyopangwa na kwamba kabla ya siku hiyo kutakuwa na mambo mbalimbali ya kijamii.
Alisema kuwa Jumamosi Aprili 5 wasanii mbalimbali watatembelea hospitali, magereza, vituo vya watoto yatima na kaburi la marehemu Kanumba.
Wakuganda alisema siku ya Jumapili kutakuwa na bonanza maalum ambalo litafanyika kwenye viwanja vya Leaders Club likishirikisha timu 12 za soka.
Alizitaja baadhi ya timu kuwa ni Bandari Veterani, Multi Choice, Boko Veterani, Bongo Movie, Bongo Fleva, NMB, Tanzania Stars, Taswa, Tanzania Stars, CXC Africa na NSSF.
Wakuganda alisema pia kuwa siku ya Aprili 7, kwenye Ukumbi wa Dar Live, patakuwa hapatoshi pale bendi ya muziki wa dansi The African Stars 'wana Twanga Pepeta', pamoja na kundi la muziki wa taarab, Jahazi Morden yatakapotumbuiza.
Alisema kwa upande muziki kipya ni watakaosindikiza watakuwa Snura, TMK Family, Juma Nature, Afande Sele, Babu Ayoub, Tunda Man, Dogo Janja na Linah, huku wasanii wa filamu watakaokuwapo Elizabeth Michael 'Lulu', Patcho Mwamba, Benny Kinyaiya, Aunt Ezekiel, Dude, Wema na Batuli.

Jahazi la Sundrland lazidi kuzama England

Andy Carroll akishangilia bao lake jana
JAHAZI la timu ya Sunderland limezidi kuzama kwenye Ligi Kuu ya England baada ya usiku wa kuamkia leo kubamizwa nyumbani kwao kwa mabao 2-1 na West Ham United katika mechi pekee ya ligi hiyo iliyochezwa Jumatatu.
Mabao ya Andy Carroll la dakika ya 9 na jingine la Mohammefd Diame la dakika ya 50 yalitosha kuwapa wakati mgumu Sunderland katika janga la kujinasua kushuka daraja kwani imezidi kuwaweka pabaya.
 Bao la kiufutia machozi la wengine lilifungwa dakika ya 65 na Adma Johnson, ambalo hata hivyo halikuweza kuwanasua kutokana nafasi ya pili toka mkiani mwa ligi hiyo inayoelekea ukingoni.

Katiba ya Simba yakwaa kisiki TFF

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage
KAMATI ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imekutana Machi 30 mwaka huu kujadili utekelezaji wa maagizo ya TFF kwa wanachama wake kurekebisha Katiba zao ili ziendane na Katiba ya TFF pamoja na ile ya FIFA kabla ya Machi 30 mwaka huu.
Vyama vya mikoa Lindi na Dar es Salaam na Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake (TWFA) viliomba kuongezewa muda wakati vingine vimeomba Katiba mama kama angalizo lao la mabadiliko hayo.
Wanachama wa SImba SC, klabu yao ndiyo pekee kati ya wanachama wa TFF waliowasilisha mabadiliko ya Katiba

Klabu ya Simba Sports ndiye mwanachama pekee aliyewasilisha mabadiliko ya Katiba.  TFF inawapongeza viongozi na wanachama wa klabu hiyo kwa kufanya mkutano wao kwa utulivu.
Kamati itatangaza nyongeza ya muda wa kufanya mabadiliko hayo baada ya kuviandalia vyama vya mikoa na vyama shiriki katiba mfano kwa ajili ya kurahisisha shughuli hiyo.
Baada ya kupitia uamuzi wa wanachama  wa Simba S.C. Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imeamua ifuatavyo:

(i)           Kwa kuwa pendekezo la wanachama wa Simba kubadili kipengele na 26 kuhusu sifa za mgombea kinapingana na kipengele na 29 (4)  cha Katiba ya TFF, hivyo basi Kamati imeagiza kipengele cha Katiba ya Simba kibaki vilevile bila kubadilishwa.
(ii)         Vipengele vingine vyote vimepitishwa na vitapelekwa kwa Msajili wa Klabu na  Vyama vya Michezo kwa ajili ya kusajiliwa.
(iii)       Mchakato wa uchaguzi wa Klabu ya Simba uendelee kama ulivyopangwa wakizingatia uamuzi huu wa Kamati.  TFF inaitakia Klabu ya Simba uchaguzi mwema.
Pia Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imeshauri TFF kuwasiliana na FIFA kupata mwongozo kuhusu katazo la watu wenye rekodi ya kifungo kugombea.
TFF imepokea ushauri huo na itaufanyia kazi na kama kuna mabadiliko yoyote kiutaratibu yataanzia katika Katiba ya TFF kupitia Mkutano Mkuu.

Ajali nyingine yachukua uhai wa watu Rufiji


WATU nane wamefariki katika ajali ya majini iliyotokea Mto Rufiji baada ya Mtumbwi kugonga Pantoni na kuzama, ambapo maiti moja kati ya watu hao nane imepatikana.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Rufiji, zinasema kuwa tukio hilo lilitokea Utete majira ya saa 12 jana baada ya nahodha wa mtumbwi huo, Abdallah Yusuf kuzidiwa nguvu na chombo hicho na kulivaa Panton i lililokuwa limeegeshwa kutokana na mto Rufiji kufurika maji.
Taarifa zaidi zinasema watu kadhaa walizama majini na saba kati yao waliokolewa ma wengine nane kutoonekana na kuhisiwa wamekufa majini.
Miongoni mwa waliookolewa ni Ramadhan Mkono, Pili Hungwa, Nasra Magimbi, Shaaban Mbonde, Ramadhani Gido, Karim Salim na Khalid Mbonde. Ikielezwa kuwa watu hao walikuwa wakitoka katika shughuli zao za kila siku.
Wanaodaiwa kufa katika ajali ni ni pamoja na Husna Rwambo, Rubia Rwando, Latifa Mkono, Prisca Kulwa, Diana Kulwa, Uwesu Mbonde, Zaria Mbonde na Mwashamba Chinga.
Ajali hiyo imetokea siku moja baada ya watu 22 kufariki katika ajali ya barabarani wilayani humo iliyohusisha magari matatu, likiwemo basi lililowaparamia waokoaji.