STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, June 11, 2014

Mapacha kupamba Miss Ubungo Ijumaa


BENDI ya Mapacha Watatu inatarajiwa kupamba shindano la kumsaka mrembo wa Ubungo 'Redd's Miss Ubungo 2014' litakalofanyika siku ya Ijumaa kwenye ukumbi wa Landmark Hotel, Ubungo Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa waandaaji wa shiondano hilo Mapacha Watatu chini ya uongozi wa Khaleed Chuma 'Chokoraa' watafganya makamuzi kunogesha shindano hilo litakalowashirikisha warembo 18 kuwania taji hilo.

Shilole: Tuombe na kufunga sana hali tete

NYOTA wa muziki na filamu nchini, Zuwena Mohammed 'Shilole' amewataka wasanii wenzake na Watanzania kwa ujumla kufunga na kuomba Mungu ili awanusuru na majanga ambayo yamekuwa yakiongezeka kila uchao kiasi cha kuwapa hofu ya maisha.
Aidha ameendelea kuomboleza vifo vya wasanii na wadau wa filamu vilivyotokea akisisitiza kuwa hiyo ni kazi ya Mungu na asisakwe mchawi kwani ni sawa na kukufuru.
Akizungumza na MICHARAZO alisema kwa hali ya mambo yanayozidi kuwaandama wasanii na taifa kwa ujumla ni muda mwafaka kwa kila mtu kwa imani yake kufunga na kumuomba Mungu afanye wepesi katika mitihani anayowapa.
Shilole anayetamba na wimbo wa 'Chuna Buzi' alisema kumekuwa na matukio ya kuhuzunisha na kuogopesha kama ya watu kuchinjana, watoto kufanyiwa vitendo vya ukatili mbali na vifo vya kushtukiza vya wasanii na wanamichezo, kitu alichosema ni vyema kila mtu kwa imani yake kufunga na kuomba Mungu awanusuru.
Kauli ya Shilole imekuja siku chache baada ya vifo mfululizo vya wasanii na wanamichezo ambavyo vimewafanya wadau wake wasipumue.
Kwa wiki mbili vimeshuhudiwa vifo vya watu saba, akiwamo Amina Ngaluma, Adam Kuambiana, Rachel Haule, George Tyson, Gebo Peter, Mzee Small na Kanali Ally Mwanakatwe waliofariki mwishoni mwa wiki.

Wambura arejeshwa uchaguzi wa Simba?!

Michael Wambura
HATMA ya Michael Wambura kurudishwa au kutoswa kwenye kugombea urais Simba inatarajiwa kufahamika leo wakati Kamati ya Rufaa ya TFF itakapotoa taarifa yake kwa wanahabari.
Hata hivyo habari za chini ya kapeti zinadai kuwa Wambura amepeta baada ya maamuzi ya rufaa yake kuamuliwa kwa kura.
Wambura alikata rufaa kupinga kuenguliwa kwenye kinyang'anyiro hicho kitakachofanyika Juni 29 na kwamba Kamati ya rufaa ya TFF, kupitia mwenyekiti wake, Julius Lugaziya imemrudisha, ila tarifa rasmi zitatolewa leo saa 5 asubuhi.
Kama tetesi hizo zitakuwa sahihi basi ni kwamba  Wambura atapambana na Avens Aveva kwenye kinyang’anyiro cha kuwania urais wa klabu maarufu ya Simba.
Awali, Wambura aling’olewa kuwania urais baada ya kubainika uanachama wake una walakini.
Kamati ya uchaguzi ya Simba chini ya mwanasheria maarufu, Dokta Damas Daniel Ndumbaro ilibaini kuwa uanachama wake una walakini na mkutano mkuu wa Simba pekee ndiyo wenye uwezo wa kurekebisha jambo hilo.

Msiba mwingine soka la Bongo, beki wa zamani atunaye

Na Salum Vuai, ZANZIBAR
WAKATI Nahodha wa zamani wa KMKM, Ali Issa Simai 'Kapteni' aliyefariki juzi na kuzikwa jana visiwani Zanzibar, jahazi la michezo limeendelea kupata majonzi mengine kufuatia kifo cha nyota wa zamani wa Pilsner, Abdallah Sumbwa.
Sumbwa alikumbwa na mauti hayo mchana wa jana kutokana na tatizo la Saratani ya Tumbo na anatarajiwa kuagwa leo kabla ya kusafrishwa kwenda kuzikwa kwao Kilosa, Morogoro.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo MICHARAZO imezipata usiku wa jana zilisema kuwa mchezaji huyo alikuwa amelazwa hospitali ya Ocean Road na kukumbwa na mauti saa 8 mchana.
Msiba wa mchezaji huyo upo nyumbani kwake Buguruni na inaelezwa atasafirishwa leo kwenda kuzikwa kijijini wao mijini Kilosa, Morogoro.
Msiba huo umekuja wakati visiwani Zanzibar jana ulishuhudia ukimzika Kapteni aliyeugua ghafla,
Marehemu, alikutwa na mauti nyumbani kwake Fuoni baada ya kurudi kutoka katika shughuli zake za kawaida nyakati za Magharibi na alizikwa jana. Chukwani.
Jeneza lililobeba mwili wa marehemu Ali Issa Simai (katika picha ndogo) likipelekwa mazikoni leo

Mmoja wa wanasoka waliocheza pamoja naye Abdalla Maulid, amenukuliwa na Bin Zubeiry kuwa, marehemu alikuwemo kwenye kikosi cha washika magendo hao kilichoshiriki michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati mwaka 1974 yaliyofanyika mjini Dar es Salaam, yakiwa katika mwaka wake wa kwanza.

Maulid alifahamisha kuwa, mwaka 1975, kepteni huyo aliitwa katika timu ya taifa ya Zanzibar iliyoshiriki mashindano ya Chalenji kwa vijana, yaliyofanyika uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, na ubingwa kuchukuliwa na Kenya.

Aidha mwaka huo wa 1975, marehemu aliyesifika kwa umahiri wake wa kumiliki mpira na mbinu za kufumania nyavu, aliteuliwa katika timu kubwa ya taifa iliyokuwa chini ya kocha Muingereza George Dunga.

Pamoja na kuibeba vyema klabu yake katika ligi kuu ya muungano kuanzia mwaka 1976 na kufanikiwa kutwaa ubingwa mwaka 1984, marehemu Ali Issa pia aliisaidia Navy (sasa KMKM) kucheza klabu bingwa Afrika mwaka 1978, ambapo walifika hatua ya nne bora.

Nahodha huyo alidumu na KMKM hadi mwaka 1990 alipoamua kutundika madaluga, na kuendelea kuchezea timu ya maveterani, Wazee Sports.

Mazishi ya marehemu huyo aliyeacha watoto kumi, yalihudhuriwa na mamia ya wananchi na wanamichezo mbalimbali, ambapo mwili wake ulisaliwa katika msikiti uliopo karibu na uwanja wa Amani, na baadae kupelekwa malazoni Chukwani. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu pahala pema Peponi. Amin.

Ureno yainyuka Ireland, Ronaldo akirejea dimbani

URENO jana iliendelea kudhihirisha dhamira yao ya kufanya kweli kwenye Kombe la Dunia baada ya kuikanyaga timu ya Jamhuri ya Ireland kwa mabao 5-1 katika mechi ya mwisho ya kujiandaa na michuanio hiyo ya Brazil inayoanza kesho.
Ureno waliopangwa kundi G na timu za Ujerumani watakaoanza nao vita Juni 16, Ghana na Marekani huo ni ushindi wake wa pili mfululizo bnaada ya wiki iliyopita kuinyoa Mexico bao 1-0 katike mechi kama hiyo ya maandalizi.
Katika mchezo huo wa jana nyota wa timu hiyo na klabu ya Real Madrid, Cristiano Ronaldo alicheza kwa dakika 65 na kudhihirishia mashabiki wa Ureno kuwa yupo fiti tayari kulipaisha taifa hilo.
Ureno ilianza kuhesabu bao la kwanza dakika ya pili ya mchezo huo kupitia Hugo Almeida kwa pasi ya Silvestre Varela kabla ya Keogh kujifunga dakika ya 20 na kuipa Ureno uongozi wa 2-0 na kwenye dakika ya 37 Hugo Almeida alirejea tena nyavuni , mabao yaliyodumu hadi wakati wa mapumziko.
Kipindi cha pili kilianza kwa wenyeji kujipatia bao lao pekee la kufutia machozi dakika ya 52 kupitia McClean kabla ya Vieirinha kufunga bao la nne dakika ya 77 kwa pande la Nani ambaye pia alimtengenezea mpira Fabio Coentrao kufunga bao la tano kuhitimisha ushindi huo mnono kabla ya kuwakabili Ujerumani wiki ijayo kwenye Fainali za Kombe la Dunia.