STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, October 2, 2013

Beki Yanga akiri Ligi Kuu msimu huu kiboko!

Oscar Joshua
BEKI wa pembeni wa klabu ya Yanga, Oscar Joshua Nkululo, amesema kwa jinsi Ligi Kuu Tanzania Bara ilivyo ngumu msimu huu imekuwa vigumu kutabiri mapema timu ipi itakayoibuka kidedea kutwaa ubingwa.
Joshua, aliyetwaa taji la ligi kuu mara mbili sawa na idadi ya Kombe la Kagame akiwa na Yanga, alisema ugumu wa ligi hiyo unaweza kuonekana katika matokeo ya kushangaza katika mechi zilizochezwa mpaka sasa.
Akizungumza na MICHARAZO katika mahojiano maalum, beki huyo alisema kwa mfano Yanga iliweza kuitungua Ashanti United magoli 5-1, lakini timu hiyo hiyo iliweza kuisimamisha Azam ambayo waliicharaza Yanga mabao 3-2.
"Kwa ligi ya msimu huu ni ngumu sijawahi kuona, inasisimua na inafanya iwe vigumu mtu kutabiri nani atakayeibuka na ubingwa kwa sababu hakuna timu nyonge kama ilivyokuwa misimu kadhaa iliyopita," alisema Joshua.
Beki huyo mwenye 'mwili jumba', alisema anadhani kuwepo kwa udhamini wa uhakika na vijana wengi kupewa nafasi katika timu shiriki zimesaidia kuifanya ligi iwe na ushindani na upinzani mkubwa.
Alisema kuwepo kwa ligi ngumu kama hiyo itasaidia kuliweka soka la Tanzania katika kiwango kizuri na hatiamye kupatikana kwa timu nzuri ya taifa itakayoipeperusha vyema bendera katika anga la kimataifa.
Joshua aliizungumzia timu yake ya Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu kuwa, pamoja na kwamba imeonekana kuyumba, lakini bado anaamini italitetea taji lake mwisho wa msimu.
"Kwa sasa tupo nafasi ya nne, lakini hii haitukatishi tamaa kwa sababu tumejipanga kupigana mpaka mwisho kuhakikisha tunalitetea taji kwa mara ya pili, licha ya kutambua kuna upinzani mkali toka kwa wengine," alisema.

Tuesday, October 1, 2013

Simba kuivaa Yanga bila First Eleven

Wachezaji wa Simba wakijifua asubuhi ya leo
Mombeki

Lazima tuwe fiti kwa mechi zijazo
Chollo, Adeyum saleh na wenzao wakijifua
Kwa tizi hizi Ruvu Shooting atoke salama Jumamosi...Mawe....!
Fundi a.k.a Gaucho
Ramadhani Singano 'Messi' naye alikuwepo
Dua ni muhimu iwe kabla au baada ya mazoezi, vijana wa Simba wakiwa na benchi lao la ufundi likimshukuru Mungu kwa kumaliza salama mazoezi yao ya leo asubuhi
KOCHA Mkuu wa timu ya Simba, Abdallah Kibadeni 'King Mputa' amesema bado hajapata kikosi chake cha kwanza (First Eleven) cha timu yake, japo anaridhishwa na baadhi ya wachezaji kwa namna wanavyojituma mazoezi na uwanjani na kuisaidia timu.
Hata hivyo alisema anatumaini baada ya mechi nne zijazo atakuwa ameshafanikiwa kukipata kikosi hicho kwani alijiwekea lengo hilo ndani ya mechi 10 za Ligi Kuu Tanzania Bara inayozidi kushika kasi.
Kwa maana ni kwamba Simba itaikabili Yanga Oktoba 20 ikiwa bado haijapata kikosi chake cha kwanza.
Akizungumza kwenye mazoezi ya timu hiyo leo asubuhi, Kibadeni alisema bado hajafanikiwa kupata kikosi chake cha kwanza cha kukitegemea kwa vile anaendelea kuwaangalia nyota wake, ambapo alikiri wapo wanaomkuna kwa umahiri wao.
Kibadeni alisema kwa kuwa alijiwekea lengo la kukipata kikosi hicho katika mechi 10 anatarajia baada ya mechi nne kuanzia ile ya Jumamosi dhidi ya Ruvu Shooting, Prisons-Mbeya, Yanga na Coastal Union.
"Bado sijapata kikosi cha kwanza kwa sababu nilishatangaza tangu awali nitatumia mechi 10 kupata kikosi hicho na ndiyo kwanza tupo mechi ya sita, nadhani baada ya mechi nne zijazo ndipo nitakuwa na uhakika wa kikosi hicho, ila vijana wanajitahidi," alisema.
Kocha huyo mwenye rekodi nzuri nzuri kwa Simba na Tanzania kwa ujumla, aliizungumzia mechi yao ijayo dhidi ya Ruvu Shooting na kukiri itakuwa ngumu kama ilivyokuwa kwa JKT Ruvu kwa vile karibu timu zote za majeshi zinafanana, ila anashukuru baadhi ya nyota wake waliokuwa majeruhi wameanza kurejea uwanjani na kutumaini huenda akawatumia katika mchezo huo.
Wachezaji hao waliokuwa miongoni mwa majeruhi na jana walishiriki mazoezi ni kiungo Henry Joseph na beki wa pembeni Issa Rashid 'Baba Ubaya'.
"Nashukuru baadhi ya nyota wangu waliokuwa majeruhi wamerejea uwanjani na nina tumaini kuwatumia katika mechi ijayo dhidi ya Ruvu Shooting, japo nitaendelea kuwakosa Miraji Adam na Abdallah Seseme bado wanaendelea kujiuguza," alisema.
Kuhusu ushindani katika Ligi Kuu ya msimu huu, Kibadeni alisema ni mkubwa na ndiyo maana hata kwenye msimamo timu zimepishana kwa idadi ndogo ya pointi kitu alichosema kinafanya ligi isisimue na kutabiri siyo rahisi bingwa kutangazwa mapema kama ilivyokuwa mwaka jana.
"Ligi ni ngumu na ina ushindani mkubwa na karibu timu zote zimejizatiti  kunipa raha na hasa ikizingatiwa kuwa ligi ni ngumu na ina ushindani mkali kama ilivyokuwa msimu uliopita," alisema Kibadeni.

Tambwe atamba, 'Yanga kitu gani bwana, nitawatungua tu Okto 20'


Amisi Tambwe (kulia) akishangilia mabao yake na Betram Mombeki
MSHAMBULIAJI nyota wa Simba, Amissi Tambwe ameitumia salamu Yanga akiiambia kwamba ikae chonjo kwa ajili ya pambano la watani wa jadi wa soka nchini litakalofanyika Okotba 20, akiahidi kuwatungua ili kuendeleza rekodi yake ya mabao.
Mrundi huyo aliyesajiliwa Simba akitokea Vital'O ya Burundi alisema kwa vile lengo lake ni kufikisha idadi ya mabao 20 mwishoni mwa msimu kitu yoyote itakayokutana na Simba bila kujali kama ni Yanga au Ashanti United akili yake itakuwa kwenye kufumania nyavu tu.
Akizungumza na MICHARAZO leo mara baada ya mazoezi ya klabu yake uwanja wa Kinesi, Tambwe alisema licha ya kwamba hajaiona Yanga ikicheza katika msimu huu, bado anaichukulia kama timu nyingine zilizokutana na Simba ambapo hujitahidi kufunga mabao kwa lengo la kuisaidia timu yake kadhalika kutimiza lengo la kufunga jumla ya mabao 20.
"Sijabahatika kuwaona Yanga wakicheza tangu nitue nchini, lakini nafahamu ni timu kubwa na wapinzani wakubwa wa Simba, lakini hilo mimi sijali siku tutakayokutana nitakuwa na kazi moja tu ya kuwafunga kama ninavyozifunga timu nyingine," alisema.
Alisema yeye awapo dimbani akili zake ni namna ya kujipanga ili kufunga mabao kitu ambacho kimemsaidia kutwaa tuzo kadhaa za ufungaji bora katika ligi yao ya nyumbani na ile ya Kombe la Kagame, kitu anachotaka kitokee pia katika Ligi Kuu ya Tanzania.
Mshambuliaji huyo ambaye alishindwa kuendelea kufanya mazoezi na wenzake kwa kile alichoeleza kusumbuliwa na tumbo, alikiri ligi ya Tanzania ni ngumu na yenye ushindani mkali akidai karibu timu zote zilizocheza na Simba zilionekana kuwakamia kitu anachotarajia hata katika mechi ijayo dhidi ya Ruvu Shooting itakayoyochezwa Jumamosi.
"Ligi ni ngumu na ina ushindani mkubwa, siowezi kusema kuna timu iliyoonekana tishio zaidi ya nyingine ila zote zinacheza kwa malengo na kukamia zaidi, tunashukuru tunaoongoza katika msimamo mpaka sasa," alisema.
na karibu timu zote zina upinzani mkali huku akidai mpaka sasa katika mechi tano alizocheza hawezi kusema timu ipi ilikuwa kali zaidi Mchezaji huyo ndiye anayeoingoza orodha ya wafungaji kwa sasa katika ligi akiwa na mabao saba kutokana na mechi tano alizocheza kwa vile mechi ya awali ya fungua dimba kati ya Simba na Rhion Rangers alikuwa bado hajaruhisiwa kucheza nchini..

Michuano ya Chalenji kuanza Nov 27

Na Boniface Wambura
MICHUANO ya Kombe la Chalenji inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) inafanyika Kenya kuanzia Novemba 27 hadi Desemba 12 mwaka huu.

Nchi wanachama ambazo zinataka kushiriki zinatakiwa kuthibitisha ushiriki wao kwa Sekretarieti ya CECAFA kabla ya Oktoba 20 mwaka huu. Wanachama wa CECAFA ni Burundi, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan, Sudan Kusini, Tanzania, Uganda na Zanzibar.

Michuano hiyo itatanguliwa na Mkutano Mkuu wa CECAFA utakaofanyika Novemba 26 mwaka huu ambao pamoja na mambo mengine utakuwa na ajenda ya uchaguzi. Uchaguzi huo ni kwa ajili ya kujaza nafasi nne za wajumbe wa Kamati ya Utendaji.

Wajumbe wanaomaliza muda wao ni Sahilu Gebremarian wa Ethiopia ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CECAFA, Abdigaani Saed Arab (Somalia), Tariq Atta (Sudan) na Raoul Gisanura (Rwanda).

Majina ya wagombea yanatakiwa kuwa yamewasilishwa katika Sekretarieti ya CECAFA kabla ya Oktoba 20 mwaka huu, na yakiwa yamethibitishwa na vyama vyao vya mpira wa miguu.

Simba, Yanga zavuna kiduchu Ligi Kuu


Yanga
Simba
MECHI za Yanga na Simba za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zilizochezwa wikiendi iliyopita jijini Dar es Salaam zimeingiza jumla ya sh. 182,103,000.

Yanga katika mechi yake dhidi ya Ruvu Shooting iliyochezwa Jumamosi (Septemba 28 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 imeingiza sh. 94,202,000.

Watazamaji 16,492 walikata tiketi kushuhudia pambano hilo ambapo kila klabu ilipata mgawo wa sh. 22,630,921.58. Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000, na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 14,369,796.61.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 11,507,248.26, tiketi sh. 3,117,215, gharama za mechi sh. 6,904,348.96, Kamati ya Ligi sh. 6,904,348.96, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 3,452,174.48 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 2,685,024.59.

Nayo Simba ambayo iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Ruvu katika mechi iliyochezwa Jumapili (Septemba 29 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 87,901,000.

Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo namba 41 walikuwa 15,780. Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 21,051,025.92 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 13,408,627.12.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 10,703,911.48, tiketi sh. 3,132,963, gharama za mechi sh. 6,422,346.89, Kamati ya Ligi sh. 6,422,346.89, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 3,211,173.44, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,248,789.67 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) sh. 1,248,789.67.

Wakati huo huo, mechi ya ligi hiyo kati ya Mbeya City na Coastal Union  iliyochezwa Jumamosi (Septemba 28 mwaka huu) Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya imeingiza sh. 16,959,000 huku kila klabu ikipata sh. 4,035,229.

Mgawo wa mechi hiyo ulikuwa ifuatavyo; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 2,586,966, uwanja sh. 2,051,811.57, tiketi sh. 696,290, gharama za mechi sh. 1,231,086, Kamati ya Ligi sh. 1,231,086, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 615,543, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA) sh. 478,756.

Kukata rufaa Kamati ya Maadili mwisho kesho

Na Boniface Wambura
Wakati walalamikiwa waliofikishwa kwenye Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wakiwa wameshapokea uamuzi dhidi yao kwa maandishi, mwisho wa kukata rufani Kamati ya Rufani ya Maadili ni kesho (Oktoba 2 mwaka huu).

Walalamikiwa wote saba waliohudhuriwa mashauli dhidi yao; Kamwanga Tambwe, Nazarius Kilungeja, Omar Abdulkadir, Richard Rukambura, Riziki Majala, Shaffih Dauda na Wilfred Kidao wamepokea uamuzi wa Kamati hiyo inayoongozwa na Jessie Mnguto.

Kwa mujibu wa Kanuni za Maadili, kwa ambao hawakuridhika na uamuzi huo wanatakiwa kukata rufani Kamati ya Rufani ya Maadili inayoongozwa na Jaji Mstaafu Stephen Ihema ndani ya siku tatu zinazomalizika kesho.

Rufani ziwasilishwe kwa Katibu Mkuu wa TFF kabla ya saa 10 kamili jioni. Kwa mujibu wa Kanuni ya 74 (1) na (2) ya Kanuni za Maadili, rufani zikionesha sababu za kufanya hivyo zinatakiwa kuwasilishwa ndani ya siku tatu kwa njia ya posta (registered post or dispatch or courier service) kwa Sekretarieti.

Vilevile inatakiwa rufani inatakiwa kuambatanishwa risiti ya malipo ya ada ya rufani. Ada ya rufani ni sh. milioni moja.

FIFA kuamua hatma ya Papic na Yanga

Kocha Kostadin Papic
SHIRIKISHO la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limewasilisha rasmi suala la madai ya aliyekuwa Kocha wa Yanga, Kostadin Papic dhidi ya klabu hiyo katika Kamati ya Hadhi ya Wachezaji.

FIFA imesema imepeleka rasmi suala hilo katika kamati yake hiyo baada ya kupokea vielelezo vya Papic anayedai kuidai Yanga dola 10,000 za Marekani pamoja na vile vya Yanga inayodai kumlipa kocha huyo fedha zote alizokuwa akiidai klabu hiyo.

Kwa taratibu za FIFA, hivi sasa haitapokea vielelezo vingine kutoka pande hizo mbili, na badala yake Kamati hiyo inayoongozwa na Theo Zwanziger kutoka Ujerumani itafanya uamuzi na kuziarifu pande husika. Zwanziger kitaaluma ni mwanasheria.

Papic aliyeinoa Yanga kwa vipindi viwili tofauti aliwasilisha malalamiko yake FIFA akidai hadi mkataba wake unamalizika klabu hiyo ilikuwa haijamlipa dola 10,000 za Marekani.

Mwenge wa Uhuru wazuia pambano la FDL Iringa

Na Boniface Wambura
PAMBANO la Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kati ya Lipuli ya Iringa na Majimaji ya Songea ambalo lilikuwa lichezwe kesho (Oktoba 2 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Iringa Mjini, sasa utafanyika uwanja wa Wambi Mafinga.

Mabadiliko hayo yamefanyika kutokana na Serikali kuutumia Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora kwa ajili ya shughuli za mbio za Mwenge.

Mechi nyingine ya FDL kesho itakuwa kati ya Tessema FC ya Dar es Salaam na Ndanda FC ya Mtwara, na itafanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam.

Monday, September 30, 2013

Simba yaalika matawi kutoa maoni ya katiba yao


KLABU ya soka ya Simba imefungua milango kwa wanachama wake kuanza kutoa maoni na mapendekezo ya mchakato wa katiba yao ambapo kuanzia kesho wataanza kufanya hivyo kwa kupitia matawi yoao yaliyopo ndani na nje ya jijini la Dar.
Kwa mujibu wa Afisa Habari wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga alisema kuwa zoezi hilo litachukua muda wa usiozidi siku 10 kwa kuwasilisha kwa Katibu Mkuu wao, Evodius Mtawala kabla ya kuja kufanyika kwa mkutano.

Ajali tena! Basi la 5 Alliance laua mmoja Lindi



Basi la 5 Alliance likiwa limeanguka katika ajali iliyopata leo
ABIRIA mmoja ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja amefariki dunia katika ajali ya basi la 5 Alliance na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Ajali hili inaelezwa imetokea eneo ya Nyamwage mkoa wa Lindi wakati bali basi hilo    lililokuwa likitokea Dar Es Salaam kuelekea Lindi limepinduka na kusababisha kifo cha abiria huyo na watu wengine waliokuwa ndani ya gari hilo kujeruhiwa. Taarifa kamili tunafuatilia na kuziweka hapa.

Msiba Tena! Mac 2 B afariki, Watuguru naye katangulia

TASNIA ya sanaa nchini imeendelea kupata pigo baada ya mcharaza gitaa Joseph Watuguru na Mac Maliki Simba 'Mac 2 B wamefariki dunia siku ya leo.

Watuguru alifariki  katika hospitali ya Amana wakati Mac 2 B aliyekuwa msanii wa muziki wa kizazi kipya, mtayarishaji wa muziki huo na Reggae kufariki leo asubuhi nyumbani kwao Yombo kwa Abiola.

Mac 2B aliyekuwa membaz wa kundi la Wateule alikuwa akisumbuliwa na miguu mpaka mauti yalipompata nyumbani kwao Yombo na anatarajiwa kuzikwa kesho asubuhi.

Naye Watuguru aliyewahi kutamba na bendi mbalimbali ikiwemo African Revolution 'Tamtam' na Mchinga Sound alifariki kutokana na kuugua muda mrefu na inaelezwa kuwa huenda naye akazikwa kesho.

MICHARAZO inatoa pole kwa wanafamilia, ndugu, jamaa na wadau wa sanaa kwa ujumla kwa misiba hiyo ambayo imekuja wakati tasnia hiyo ikiendelea kuomboleza vifo vya wasanii wengine waliotangulia mbele ya haki tangu mwaka jana.

Yanga yatoa taarifa juu ya mradi wa ujenzi wa uwanja wao


LEO tungependa kupitia kwenu kutoa taarifa kuhusu maendeleo ya mradi wetu wa Uwanja wa kisasa wa mpira katika Jiji la Jangwani kama itakavyojulikana

Mara ya mwisho tuliongea ama kuonana ilikuwa mwezi wa tatu wakati Ndugu zetu wa BCEG walipokabizi Concept design ama Usanifu wa awali na kuanzia sasa tutakuwa tunatoa taarifa za mara kwa mara kuhusu mradi huu. Wahenga walisema UKICHA KUSEMA HUTATENDA JAMBO lakini pia KUKAA KIMYA SANA kunajenga hisia mbaya na kutoa nafasi ya upotoshwaji wa habari.

Kwa kifupi napenda kuwakumbusha kuwa Makubalino ya Awali (Memorandum of Understanding) yalisainiwa 23 Novemba 2012. Pamoja na mengineyo YANGA inatakiwa:

· Kupata na kuwa na eneo la kutoshereza malengo ya mradi

· Kupata ushauri mzuri, michoro mizuri na mkandarasi mzuri wa mradi

· Kupata na kutenga fedha za kukamilisha usanifu na ujenzi wa mradi

Kwa upande wa BCEG wajibu wao ni kuwa na utaalamu na uzoefu wa kutosha. BCEG wameandaa na kukabidhi michoro ya usanifu wa awali kukidhi matakwa ya YANGA. YANGA tunatakiwa kutoa maoni yetu na na kuingia RASMI mkataba wa ujenzi.

Kutokana na kukua kwa Jiji la Dar es Salaam, na katika hali ya kutaka klabu iwe na vitega uchumi klabu imeonelea ni vyema kama ingekuwa na uwanja wa mpira wa karne ya sasa na baadaye ambao pamoja na mambo mengine utakuwa na mioundombinu ifuatayo:-

1. Uwanja wa mpira wenye viti 40,000

2. Hostel ya wachezaji na football academy ya vijana

3. Viwanja vya mazoezi

4. Uwanja wa kutosha kuegesha magari

5. ­­­­­Hoteli na sehemu ya makazi

6. Ukumbi wa mikutano

7. Sehemu ya maofisi, benki, zahanati (sports clinic)

8. Maduka, supermarket na sinema

9. Sehemu za kubarizi, kupumzikia (Recretional and Open spaces)

Mara baada ya azma yetu kukamilika eneo hili litaitwa “Jangwani City” na kufanya wakazi wa maeneo ya Jangwani na sehemu za jirani wasiende maeneo ya mbali kutafuta huduma muhimu za kijamii. Eneo hili litaboresha mandhari nzima ya Jangwani kwa kukuza mazingira na miundombinu. Hii itahusu pamoja na mambo mengine ujazaji udongo (tuta kubwa), upandaji miti, bustani za kubarizi, kuboresha mifereji ya majitaka na kudhibiti mafuriko ya eneo la Jangwani na hivyo kulipatia sura ya kibiashara na kitalii.

Ili kukamilisha azma ya kuwa na Jangwani City itakayo kuwa na miundombinu yote hiyo, Uongozi ulipeleka maombi ya eneo la nyongeza Manispaa ya Ilala na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa barua zenye kumbukumbu namba YASC/ARDHI/MWK/YM/46/2012 na YASC/ARDHI/MWK/YM/47/2012 za 12 Desemba 2012, na mpaka sasa bado maombi yetu hayajajibiwa.

Mwezi wa saba, Wadhamini/Uongozi wa YANGA walimwandikia Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuomba msaada wake kufanikisha maombi ya nyongeza ya kiwanja yaliyowasilishwa Manispaa ya Ilala na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Klabu ya Yanga ina kiwanja chenye ukubwa wa hekta 3.59 eneo la Jangwani. Kiwanja hiki kina hati miliki kwa miaka 99 toka mwaka 1972 na katika eneo hilo, klabu ilifanikiwa kujenga uwanja wa mpira wa Kaunda na Jengo la klabu la ghorofa tatu. Jengo hili lilijengwa kwa ufadhili mkubwa sana wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume (Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi) na michango ya wanachama na wapenzi wa klabu ambao kila siku wamekuwa wakiamini kuwa haba na haba hujaza kibaba.

Ndugu Wandishi wa habari kwa kifupi tumefikia hapo, zoezi la kutoa maoni yetu kuhusu michoro ya usanifu wa awali na kuingia rasmi mkataba wa ujenzi na BCEG limesimama, likisubiri majibu ya nyongeza la eneo. Ni matumaini yetu zoezi hili litakamilika hivi karibuni na kuendelea na mradi.

YANGA DAIMA MBELE NYUMA MWIKO
Dar es Salaam, 30 September 2013
Francis Mponjoli Kifukwe

Mrembo Miss Utalii Tanzania kupaa kesho kwenda Equatorial Guinea

Miss Utalii Tanzania 2013

MREMBO wa Miss Utalii Tanzania 2013, Khadija Mswaga anatarajiwa kuondoka nchini kesho kuelekea Equatorial Guinea kwa ajili ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kusaka mrembo wa Utalii Duniani 'Miss Tourism World 2013'.
Shindano hilo la urembo la dunia litafanyika katika nchi ya Equatorial Guinea ambapo warembo wa nchi 126 wanatarajiwa kuchuana kuwania taji hilo.
Rais wa Bodi ya Miss Utalii Tanzania, Gideon Chipungahelo 'Chipps' aliiambia MICHARAZO kuwa mrembo huyo wa Tanzania ataondoka kesho Jumanne kwa ndege ya kampuni ya Ethiopia kuelekea nchini humo tayari kwa kinyang'anyiro kitakachofanyika Oktoba 12.
Chipungahelo alisema mwakilishi wao anaenda katika shindano hilo akiwa amebeba ujumbe wa kutangaza hifadhi ya taifa ya Ngorongoro Crater kama moja ya maajabu ya dunia Afrika.
Mrembo huyo alisema ameamua kubeba ujumbe huo kwa sababu ni hifadhi ya kipekee duniani ambayo pia inaelezewa ndiyo chimbuko la binadamu wa kwanza na sehemu pekee binadamu anaishi na wanyama kwa ushirikiano bila kudhuriana.
Mrembo huyo alisema ana imani kubwa ya kufanya vizuri katika shindano hilo ili kuifuta machozi Tanzania ambayo imekuwa na bahati mbaya ya kufanya vibaya katika kila shindano la kimataifa inayoshiriki duniani.