STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, June 22, 2014

Tanzia: Onesmo Waziri 'Ticotico' hatunaye, afa ajalini mjini Mafinga

Onesmo Waziri 'Ticotico akihiojiwa
Ticotico (kushoto) akiwa na wachezaji wenzake wa Golden Bush Veterani
Ticotico akimiliki mpira enzi za uhai wake
Jamaa alipenda soka nyie acheni
TAARIFA zilizotufikia muda huu zinasema kuwa, aliyekuwa Mkurugenzi wa timu ya Golden Bush na mwanachama maarufu wa Simba Onesmo Waziri 'Ticotico' amefariki kwa ajali ya gari mjini Mafinga wakati akielekea kwenye michezo ya kirafiki uliokuwa uchezwe Makambako.
Mmoja wa viongozi wa Golden Bush, Geofrey Chambua alilidokeza gazeti hili kuwa marehemu alikumbana na mauti baada ya gari walilokuwa wakisafiria mjini humo kukumbwa na ajali na Ticotico kupoteza uhai wake.
Chambuia hata hivyo hakufafanua kama kuna wachezaji wengine waliokuwa kwenye msafara wao wapo katika hali gani iwapo nao walikuwa kwenye gari alilokuwa marehemu Ticotico.
Ila alisema kuwa mwili wa marehemu, aliyekuwa akifanya kazi katika kampuni ya SMEC inayohusika na Ujenzi wa Mradi wa Magari ya Mwendo Kasi jijini Dar umehifadhiwa katika Hospitali ya Mafinga kwa ajili ya taratibu za mazishi yake.
Enzi za uhai wake Ticotico aliwahi kuwa Katibu wa Kamati ya Fedha na Uchumi ya klabu ya Simba chini ya uongozi wa Ismail Aden Rage.
Ticotico aliyekuwa shabiki mkubwa wa klabu za Arsenal na Barcelona alikuwa akimiliki klabu ya Golden Bush inayoshiriki Ligi Daraja la Tatu wilaya ya Kinondoni na ile ya maveterani.

Kabla ya kuamua kuanzisha klabu yake, Ticotico alikuwa akijitolea kwa hali na mali katika kufanikisha baadhi ya usajili wa wachezaji wa Simba, ikiwamo ya George Owino aliyewahi kuichezea pia Yanga na uongozi wa Rage ulipoingia madarakani mwaka 2010 ulimteua kuwa Katibu wa Kamati ya Fedha kabla ya kujiuzulu kutokana na kutingwa na majukumu binafsi.
Taarifa zaidi zitawajia, ila kwa hakika ni msiba unaumiza kwa wadau wa soka na hasa wale wa Golden Bush Veterani, Simba pamoja na rafiki zake wote akiwamo mmiliki wa blogu hii.
Kwa hakika Ticotico atakumbukwa kwa ucheshi wake na mapenzi yake katika soka na moyo wa kujitolea na ukarimu mkubwa ulioanikizwa na mwingi wa utani.
MICHARAZO Inawapa pole familia, ndugu, jamaa na rafiki pamoja na wadau wote wa soka kutokana na msiba huu. Mungu awape subira kwa kutambua kuwa kila Nafsi Itaonja Mauti na kwamba sisi sote ni wa Mola na Kwake Tutarejea Hakika. Innalillah Waina Illah Rajiun

Huu ni ujumbe wake wake wa mwisho kuhusiana na ziara yao hiyo ya michezo mjini Makambako;

Kwa niaba ya uongozi wa Golden bush veterans ambao ni mabingwa wa Tanzania Bara na visiswani yaani Mabingwa wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, napenda kuwapa taarifa kwamba timu kamili ikijumuisha kikosi cha kwanza kama kinavyoonekana katika picha hapo chini, itaondoka siku ya jumamosi alfajiri kuelekea Makambako kwa ajili ya mechi mbili yaani Makambako Veterans VS Golden Bush na Mafinga Veterans vs Golden Bush. Games zote zitapigwa uwanja Makambako Veterans siku ya tarehe 22/06/2014. Kwakutambua umuhimu na ugumu wa game hizo, Golden Bush ametanguliza watu wafuatao kwenda kuweka mambo sawa, Godfrey Chambua a k a Hans Poppe (mwanasheria na mwenyekiti kamati ya ufundi na mambo ya kale), Awilly Mshanga mchezaji mwandamizi kutoka Mbeya na Nico Nyagawa  ambaye ndiye Nahodha msaidizi wa timu yetu.


Aidha masafara wa wachezaji 28 ni viongozi watu utaondoka siku ya jumamosi. Mkuu wetu wa msafara bwana Waziri Mahadhi “Mandieta” ambaye ndie Mhazini wetu amekamilisha mambo yote ya kiutawala tayari kabisa kwasafari.


Kwa siku chache zilizobaki tutaweka camp ya muda na kufanya mazoezi ufukweni mwa bahari tayari kabisa kutoa kipigo kwa timu hizo mbili.


Tunasikitika wapenzi wetu wa Dar es salaam kwamba weekend hii hatutakuwepo kuwapa burudani hadi weekend inayofuata. Nawatakieni maandalizi mema ya mfungo mtukufu wa mwezi wa Ramadhan.


Asanteni kwa kunisikiliza.


Onesmo Waziri

Msamaji wa timu.

Ureno, Algeria kusuka au kunyoa leo Brazil

Ronaldo kuibeba Ureno leo kwa Wamerekani?
BAADA ya kupokea kipigo cha 'Paka mwizi' cha mabao 4-0 toka kwa Wajerumani timu ya taifa ya Ureno itakuwa na kibarua kingine kigumu usiku wa leo watakapoikabili Marekani katika mechi ya Kundi G.
Ureno ikiongozwa na nahodha wake, Cristiano Ronaldo itahitaji ushindi mbele ya Marekani ambayo iliitambia Ghana kwa mabao 2-1 katika mechi yao ya kwanza ili kufufua matumaini ya kusalia Brazili.
Kipigo cha aina yoyote itakuwa na maana kwamba Ureno itaungana na nchi za Cameroon, Australia, waliokuwa mabingwa watetezi, Hispania na Uingereza kufungasha virago kurudi kwao kujipanga kwa fainali za mwaka 2018.
Pambano hilo Ureno na Marekani zitachezwa usiku wa manane na mashabiki wa Ureno watakuwa wakiomba Mungu nyota wao wapigane kiume kuendelea kuwapa raha kufuatilia fainali hizo.
Hata hivyo kwa namna Marekani iliyoonyesha kandanda tamu siku walipoumana na Ghana na kupata ushindi wa kushtukiza wa 2-1 ni wazi Ureno itakuwa katika kazi kubwa kuliko ilivyokuwa kwa Ujerumani.
Katika mfululizo wa mechi za makundi leo pia itashuhudiwa Ubelgiji ikikabiliana na Russia katika mechi ya saa 1 usiku ya kundi H kabla ya wawakilishi wa Afrika Algeria kupimana ubavu na Korea Kusini.
Katika mechi ya kwanza, Algeria ilijikuta ikipoteza uongozi kwa kulazwa mabao 2-1 na Ubelgiji, hali inayoifanya katika mchezo wao wa leo kuhitaji ushindi iwapo haitaki kufungashwa virago mapema.
Wapinzani wao Korea Kusini nayo siyo timu ya kubeza kwani katika mechi yao ya kwanza dhidi ya Russia ililazimishwa sare na kuwapa tumaini la kuweza kutinga 16 Bora iwapo itashinda mechi ya leo.
Vinara wa kundi hilo Ubelgiji watakuwa wakisaka ushindi mwingine mbele ya Russia ili kujiandikishia nafasi ya kucheza 16 Bora, ingawa wafuatilia wa soka wanashindwa kutabiri matokeo ya mchezo huo.
Mpaka sasa timu zikiwa zimeshacheza mechi mbili mbili za makundi imeshuhudiwa matokeo yasiyotegemewa ikiwamo ya watetezi Hispania kufurushwa michuano ikiwa haijapata hata pointi moja.
Hispania iliyotwaa taji hilo katika fainali zilizopita nchini Afrika Kusini ilianza kwa kipigo cha aibu cha mabao 5-1 toka kwa wanafainali wenzao wa 2010 Uholanzi kabla ya kulala tena mabao 2-0 kwa Chile.
Kuondoshwa kwa watetezi wao kumelifanya taji hilo kukosa mwenyewe hivyo kuzipa urahisi nchi nyingine kupigana kiume ili kutawazwa kuwa mabingwa wapya kwa fainali hizo za Brazili.
Kundi G
                    P  W  D  L  F  A PTS
Ujerumani    2    1   1  0  6  2   4  
Marekani     1    1   0  0  2   1   3
Ghana          2    0   2  1  3   4   1
Ureno          1    0   0  1   0  4   0
Kundi H:
                    P  W  D  L  F  A  PTS
Ubelgiji       1    1   0  0  2  1   3
Korea         1    0   1  0  1  1   1
Russia         1    0   1  0  1  1   1
Algeria        1    0   0   1  1  2  0
===========

TFF yaridhia uchaguzi wa Simba kuendelea

malinzi
Rais wa TFF, Jamal Malinzi

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeridhia Uchaguzi Mkuu wa Simba uendelee kufanyika Juni 29 baada ya awali Rais wa shirikishiko hilo, Jamal Malinzi kunukuliwa akiupiga 'stop'.
Katika taarifa yake kwa wanahabari, TFF imesema baada ya kupokea na kuzingatia maombi ya Simba na kwa kuzingatia Ibara ya 26 ya Kanuni za Uchaguzi za TFF toleo la 2013 limeiruhusu klabu hiyo kuendelea na mchakato wa uchaguzi wao uliopangwa kufanyika Juni 29 mwaka huu.
 TFF inawahimiza wanachama wa klabu ya Simba kuwa watulivu na wafanye uchaguzi wao kwa amani.

Manji awapa mtihani mgumu wanaompinga Yanga

bejo
Mwenyekiti wa Klabu ya Young Africans Bw Yusuf Manji amesema wanachama wanaopinga maamuzi ya mkutano mkuu uliofanyika Juni Mosi 2014 katika Bwalo la Polisi Osyterbay ya kuwaongezea muda wa mwaka mmoja, wafike makao makuu ya klabu na kujiorodhesha majina yao kwa Katibu Mkuu.
 
Akiongea na waandishi wa habari makao makuu ya klabu, Manji amesema sisi sote tunajenga nyumba  hatuna haja ya kugombania fito, wanaopinga maamuzi yale ni vyema wakajiorodhesha majina yao ili kuweza kupata idadi yao na kama itafikia idadi ya waliohudhuria mkutano ule watu 1522 basi tutaitisha mkutano mwingine.
 
Vyombo vya Habari vimekua vikiripoti kuwa baadhi ya wanachama hawakubaliani na maamuzi ya mkutano mkuu, na mie ni mfuata Demokrasia namuagiza Katibu Mkuu kuweka reja hapa makao makuu kwa siku 5 kuanzia jumatatu mpaka ijumaa saa 11 jioni hivyo wale wote wanaosema/wanaopingana na maamuzi ya mkutano mkuu wapate kujioorodhesha.
 
Pili kwa yoyote ambaye anaona anaweza kuiongoza Yanga kwa sasa milango iko wazi, anaweza kufika makao makuu na kuongea na katibu mkuu kisha anaweza kunadi sera zake/kuongea na waandishi wa habari na baadae tutapeleka jina lake kwa Bodi ya Wadhamini wakiridhika nitaitisha mkutano mkuu wa Uchaguzi.
 
Zoezi la kujiorodhesha wanachama makao makuu litakua na usalama wa kutosha kutoka kwa jeshi la Polisi ambapo patakua na askari wa usalama watakao kuwa wakilinda usalama wa wanachama wanaofika kujiorodhesha kwenye reja hiyo.
 
Jumamosi ijayo Katibu Mkuu atatoa ripoti ya idadi ya wanachama walijiorodhesha kwenye reja na kama idadi ifikia 1522 kama ya waliohudhuria mkutano mkuu basi uongozi utaitisha upya mkutano mkuu, na kama idadi yao haitafikia baadhi demokrasia itatawala kwa kufuata maamuzi ya watu wengi.
Chanzo: Tovuti ya Yanga

Nigeria yaua, Ghana yaibana Ujerumani, Klose akiweka rekodi



GERMANY: Neuer 6;  Boateng 6 (Mustafi 45mins 5.4), Mertesacker 6, Hummels  6, Howedes 6;  Lahm 7; Khedira 6.5 (Schweinsteiger 69mins 7),  Kroos 7; Mueller 6), Ozil 7, Goetze 7 (Klose 69mins 7.5).
GOALS: Gotze 51, Klose 71

GHANA: Dauda 7; Afful 6.5, Mensah 6.5, Asamoah 6, Boye 6; Boateng (J Ayew 51mins 6.5 ), Muntari 6, A Ayew 7.5, Atsu 7 (Wakaso 71mins 6); Rabiu 6 (Badu 77mins 6); Gyan 8 
GOALS: Ayew 54, Gyan 63
REFEREE: Sandro Ricci.













WAAFRIKA wameendelea kupumua katika Fainali za Kombe la Dunia timu za Nigeria na Ghana kufufua matumaini yao ya kucheza hatua ya 16 Bora kwa kupata matokeo ya kuridhisha mbele ya timu za Bosnia % Hezergonina na Ujerumani katika mechi zao zilizochezwa jana usiku.
Ghana ikiwa katika kiwango bora kabisa ilikaribia kuiadhiri Ujerumani baada ya kuongoza mabao 2-1 kabla ya mabingwa hao wa zamani wa Dunia kuchomoa bao 'jioni' kupitia mkongwe Miroslav Klose aliyeweka rekodi katika michuano hiyo kwa kufikisha bao 15 akilingana na Ronaldo de Lima.
Klose, 36 alifunga bao la kuisawazisha na kufanya matokeo kuwa 2-2 katika dakika ya 71 na kuiepushia Ujerumani kipigo chake cha kwanza baada ya muda mrefu kutokana na kufunikwa vilivyo na Black Stars.
Mechi hiyo ya kundi G ilichezwa mjini Fortaleza, Brazil ilishuhudia Waghana wakitanguliwa kufungwa bao dakika chache baada ya kutoka mapumziko kupitia kwa Mario Gotze aliyefunga dakika ya 51 kabla ya Ghana kuchomoa dakika tatu badaye kupitia kwa Andre Ayew 'Dede' .
Nyota wa Black Stars, Asamoah Gyan kuifungia timu yake bao la pili dakika ya 63 na kuonekana wazi Ujerumani walioifumua Ureno mabao 4-0 'itakufa' kwa Waafrika ikiwa ni mara ya kwanza tangu ilipofungwa mara ya kwanza na mwisho na timu za Afrika baada ya Algeria kuwatoa nishai 1982.
Hata hivyo Klose akaisawazishia Ujerumani bao hilo dakika ya 71 na kumfanya kumfikia Ronaldo wa Brazil ambaye ameshaachana na soka muda mrefu, huku pambano hilo likishuhudia pia beki wa Arsenal, Per Mertesacker ametimzia mechi 100 za kuichezea Ujerumani.
Katika mechi nyingine ya kusisimua Nigeria iliondoa 'gundu' la kutowahi kushinda katika fainali hizo tangu mwaka 1998 nchini Ufaransa baada ya kuilaza Bosnia kwa bao 1-0 na kufufua matumaini ya kuingia 16 Bora ikifikisha pointi 4 katika kundi lake.
Bao pekee la Peter Odemwingie la dakika ya 29 ya pambano hilo liliifanya waafrika kupumua kutokana na matokeo mabaya iliyopata timu zao Cameroon ikiondoshwa na Ivory Coast na Ghana zikipumulia mashine katika makundi yao katika kuwania kutinga raundi ya pili ya fainali hizo za Brazil.
Katika mechi ya mapema jana usiku, Argentina ikiwa na 'mchawi' wake, Lionel Messi ilijihakikishia kucheza 16 Bora baada ya kuilaza Iran bao 1-0 katika pambano la kundi F.
Argentina imefuzu kutokana na kupata ushindi wa pili mfululizo katika mechi ambayo ilioneikana kama ingeisha kwa suluhu kabla ya Messi kufunga bao la 'miujiza' dakika ya 90 na kuibeba Argentina ambayo sasa itamalizana na Nigeria wiki inayoanza kesho.