STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, April 15, 2011

Cloud aibuka na Basilisa



MSANII nyota na mkongwe wa fani ya uigizaji nchini, Issa Mussa 'Cloud' ameibuka na kazi mpya iitwayo 'Basilisa', akitamba kuwa ni moja ya kazi itakayoziba midomo wote wanaoziponda filamu za Kitanzania.
Cloud, aliyeanza kufahamika kupitia michezo ya kuigiza iliyokuwa ikirushwa na kituo cha ITV alipokuwa na kundi la Splended, alisema filamu hiyo iliyowashirikisha wasanii kadhaa nyota nchini imeshakamilika na kwa sasa ipo foleni kabla ya kuanza kuwa mitaani.
Filamu hiyo ambayo Cloud kaigiza katika nafasi tatu tofauti imekuja wiki kadhaa tangu mkali huyo kutamba na kazi kama Ukiwa, Pigo na Suria.
Cloud alisema ndani ya filamu hiyo amefanya mambo makubwa akishirikiana na wakali wenzake kama Adam Kuambiana, Wema Sepetu, Single Mtambalike 'Richie', Ummy Weslaunce 'Dokii', Suleiman Said 'Barafu', Kajala Masanja na wengineo.
"Sitaki kujisifu, lakini naamini Basilisa ni moja ya kazi makini itakayoleta mapinduzi katika sanaa ya filamu nchini, hii inatokana na vichwa vilivyoshirikishwa ndani yake na jinsi kazi yenyewe ilivyo na ubora wake kuanzia hadithi, upigaji picha, mandhari na mengineyo," alisema Cloud.
Alisema kitu cha muhimu ni mashabiki wa filamu kukaa mkao wa kula kuishuhudia kazi hiyo mpya itakayosambazwa na kampuni ya Steps Entertainment ambayo ilivutiwa na filamu hiyo.
"Kazi yangu inatarajiwa kusambazwa na Steps na itakuwa mitaani kabla ya mwisho wa mwezi huu, hivyo wadau wa filamu wakae mkao wa kula kupata kitu roho inapenda," alisema Cloud.
Ndani ya filamu hiyo, Cloud, ameshiriki baadhi ya vipande akiwa kama kichaa, jitu la kutisha na muonekano wake wa kawaida, huku simulizi kuu la kazi hiyo mpya ni kuiasa jamii juu ya kutodharau viumbe wengine kwa jinsi ya muonekano wao.

No comments:

Post a Comment