STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, April 15, 2011

KITABU CHA ASSOSA CHATOKA HADHARANI




Na Badru Kimwaga
MWANAMUZIKI mkongwe wa muziki wa dansi, Tshimanga Kalala Assosa, amekamilisha kitabu chake cha tafsiri ya Lugha ya Kilingala na Kiswahili kiitwacho 'Jifunze Lingala', ambapo licha ya kufunza lugha hizo mbili pia ina nyimbo kadhaa za wanamuziki wa zamani wa DR Congo (Zaire).
Kitabu hicho kilichoanza kuandaliwa tangu mwishoni mwa mwaka jana, tayari kimeshachapishwa na mwanamuziki huyo anayemiliki bendi ya Bana Marquiz anafanya mipango ya kuanza kuvisambaza ili wadau wa muziki wa lingala na wengineo waanze kukipata.
Akizungumza na MICHARAZO, Assosa, aliyewahi kutamba na bendi mbalimbali kama 'Negro Succes', 'Le Kamalee', 'Lipualipua' na 'Fukafuka', alisema kitabu hicho ni mwanzo wa kujitosa kwenye kazi ya uandikaji vitabu wenye lengo la kufundisha lugha ya Kilingala, moja ya lugha maarufu ya Congo.
Assosa, alisema msukumo wa kuandika kitabu hicho alichochapisha nakala 50,000 za awali kama majaribio ni kutokana na simu na maombi ya mashabiki wa muziki wanaofuatilia fasiri zake katika kituo cha TBC! kinachohusu miziki ya Kavasha.
"Nilikuwa napokea simu nyingi za kuwatafsiria watu baadhi ya nyimbo za nyota wa zamani wa Zaire (sasa DR Congo) na kupata wazo la kuandaa kitabu kwa mfumo wa kamusi ambao pia una nyimbo za wakali hao na tafsiri mbalimbali za maneno ya lugha hiyo," alisema Assosa.
Mtunzi na muimbaji huyo aliyefanyia kazi bendi nyingine za 'Mambo Bado', 'Legho Stars', 'DDC Mlimani Park', 'Marquiz du Zaire' na ile ya Original, alisema mafanikio ya mauzo ya kitabu hicho kitamfanya aweze kutoa muendelezo wake siku za baadae.
Assosa, alisema shukrani pekee katika maandalizi ya kitabu hicho 'toleo la kwanza' ni kwa wanachama wa klabu ya Dar Family Kavasha na Mhariri, Joseph Kulangwa aliyekihariri hadi kuweza kuchapishwa na kuandaliwa kuachiwa mtaani wakati wowote kuanzia sasa.
Mwanamuziki huyo aliyetamba kwa utunzi wa nyimbo kama 'Minou', 'Salama', 'Huba', 'Promotion' 'Masua' na 'Abisina' alizoimba kwa kushirikiana na Nyboma Mwandido, alisema pamoja na kutaka kujitosa jumla kwenye utunzi wa vitabu, bado hajaachana na kazi ya muziki akiwa na bendi yake ya Bana Marquiz ambayo inaendeela kutumbuiza kuanzia Alhamis hadi Jumapili kila wiki.

Mwisho

No comments:

Post a Comment