STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, April 15, 2011

KASEBA, MAUGO WAPIMA UZITO KUZIPIGA KESHO PTA






MABONDIA Japhet Kaseba na Mada Maugo pamoja na watakaowasindikiza kwenye pambano lao litakalofanyika Jumamosi, wanatarajiwa kupima uzito wao leo jijini Dar es Salaam.
Upimaji huo wa uzito utafanyika kwenye ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO saa 5 asubuhi, ukihusisha pia upimaji wa afya kama moja ya kampeni ya kupambana na ukimwi michezoni.
Akizungumza na MICHARAZO asubuhi ya leo, Mratibu wa pambano hilo, Kaike Siraju, alisema mabondia wote watakaopigana Jumamosi watapimwa leo tayari kwa michezo hiyo itakayofanyika kwenye ukumbi wa PTA, jijini Dar es salaam.
Siraju, alisema mbali na Kaseba na Maugo watakaopogana kwenye pambano la kusaka mkali kati yao ili kupata tiketi ya kwenda kupigana na Francis Cheka, mabondia wengine watakaopimwa ni wale watakaosindikiza pambano hilo.
"Mabondia wanaotarajiwa kucheza siku ya Jumamosi kwenye pambano la kusaka mkali kati ya Kaseba na Maugo, watapimwa uzito na afya yao siku ya Ijumaa majira ya saa 5 asubuhi kwenye ukumbi wa Idara ya Habari-Maelezo," alisema Siraju.
Siraju, alisema maandalizi ya michezo yote ikihusisha pambano hilo la Nani Mkali la uzani wa Middle raundi 10, yamekamilika na kinachosubiriwa ni mashabiki kwenda ukumbini kupata burudani.
Michezo itakayosindikiza pambano hilo la Kaseba na Maugo, ni lile la Bingwa wa Kick Boxing wa Afrika, Kanda Kabondo atakayezipiga na Maneno Osward 'Mtambo wa Gongo', nahodha wa zamani wa ngumi za ridhaa, Joseph Martin dhidi ya George Dimoso.
Mapambano mengine ni la Yohana Robert dhidi ya Saidi Zungu, Deo Njiku atakayepigana na Issa Sewa, Fadhili Awadh atapigana na Bakari Dunda na Hassan Mandula atatwangana na Uwesu Said, Mohammed Matumla 'Snake Boy Junior' atakayeonyeshana kazi na Sadiki Momba.

Mwisho

No comments:

Post a Comment