STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, April 15, 2011

Katundu ana Nadhiri ya Mapenzi Msondo






MTUNZI na muimbaji mahiri wa bendi ya Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki', Juma Katundu ameibuka na kibao kipya kiitwacho 'Nadhiri ya Mapenzi', ambacho kimekamilisha idadi ya nyimbo sita za albamu mpya ya bendi hiyo inayoandaliwa kwa sasa.
Akizungumza na MICHARAZO, Shaaban Dede 'Mzee wa Loliondo', alisema Msondo imeongeza nyimbo mbili mpya ambazo zinakamilisha idadi ya nyimbo za albamu yao ijayo, kikiwemo kibao chake kiitwacho 'Suluhu' na hicho cha Katundu ambacho kinaendelea kufanyiwa mazoezi.
Dede, alisema kibao chake kingine kinachokemea Dawa za Kulevya, nacho kipo tayari isipokuwa hana hakika kama kitakuwa kwenye albamu hiyo ijayo ya Msondo Ngoma, moja ya bendi kongwe ya muziki wa dansi nchini.
"Kwa kifupi ni kwamba Msondo imekamilisha nyimbo nyingine mbili mpya, moja ukiwa ni wangu uitwao 'Suluhu' na kingine kimetungwa na Juma Katundu, kinaitwa 'Nadhiri ya Mapenzi'," alisema.
Dede, aliyetua hivi karibuni katika bendi hiyo akitokea Mlimani Park 'Sikinde' alisema pamoja na kukamilika kwa nyimbo hizo sita za albamu yao ijayo, bado wanamuziki wa bendi hiyo wanaendelea kutunga vibao vingine vinavyoendelea kufanyiwa mazoezi ili vipigwe ukumbini.
"Wanamuziki tunaendelea kutunga nyimbo nyingine kwa ajili ya kudhihirisha kuwa Msondo ni Baba ya Muziki kutokana na kuundwa na wanamuziki wanaojua majukumu yao, vibao hivyo vitakuwa vikipigwa kwenye maonyesho yetu ya ndani na nje ya jijini la Dar," alisema Dede.
Msondo, iliyokuwa na desturi ya kufyatua albamu mpya kila mwaka, kwa mwaka uliopita ilishindwa kufanya hivyo kwa kile kilichoelezwa na meneja wake, Said Kibiriti, maelekezo ya wasambazaji wa kazi zao waliotaka watoe nafasi kwa albamu yao ya 'Huna Shukrani' ifanye vema sokoni.
Albamu zilizofuatana pamoja kwa miaka karibu 10 mfululizo ni 'Cheusi Mangala', 'Demokrasi ya Mapenzi', 'Ndoa Ndoana', 'Kilio cha Mtu Mzima', 'Piga Ua Talaka Utatoa', 'Kaza Moyo', 'Ajali', 'Kicheko kwa Jirani' na 'Huna Shukrani' inayoendelea kutamba iliyoachiwa mwaka juzi.

No comments:

Post a Comment