STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, April 15, 2011

Tshimanga Kalala Assosa: Mkongwe wa muziki asiyechuja *Ajitosa kwenye utuzi wa vitabu







SI kila wakati mipango yetu inaweza kutimia kama yalivo matarajio. Unaweza kupanga kufanya jambo fulani lakini lisitimie, na badala yake likaja lingine ambalo hukulipanga, lakini likawa na faida pengine kuliko hata lile la awali.
Hivi ndivyo ilivyotokea kwa msanii wa muziki Tshimanga Kalala Assosa, ambaye hakuwahi kufikiria katika maisha yake kama ingetokea siku akawa mwanamuziki.
Malezi kutoka kwa wazazi wake wakati akiwa mdogo, yalimpa mwanga wa siku moja kuja kuwa mtumishi wa kiroho-padri.
Lakini baba yake aliyemlea kwa kipindi chote akiwa mdogo, naye alikuwa na mtazamo tofauti juu nini atakachokuja kukifanya mwanae.
Yeye (mzazi) alipenda sana mtoto wake aje kuwa daktari wa binadamu, lakini kumbe yote hayo hakuna lililotimia. Assosa ametua kwenye sanaa ya muziki.
Assosa ni mmoja wa wakongwe wa muziki wa dansi aliyeng'ara barani Afrika kupitia bendi kadhaa za Kongo (zamani Zaire) kama Negro Succes, Lipualipua, Fukafuka na Marquis du Zaire.
"Nilipokuwa mdogo mjini Kamana, Jimbo la Katanga, nilifanya kazi kanisani na kutamani kuwa Padri, wakati baba mzazi yeye alitaka nisome zaidi ili niwe daktari," alisema.
Assosa, maarufu kama 'Mtoto Mzuri', alisema alivutwa kwenye muziki kwa nyimbo za wakali wa zamani wa Kongo kama Franco, Vicky Longomba na Kabasela Joseph.
Ladha na utamu wa muziki wao ulimfanya asitishe mipango ya kusomea zaidi taaluma na kujiingiza kwenye elimu ya muziki akiwa darasa la 5.
Alianza kuimba kanisani, shuleni na baadaye mitaani akipigia bendi ndogo ndogo za mjini Kamana, kabla ya kuhamia Kinshasa katikati ya 1960 alipokutana na Bavon Marie Marie aliyemchukua katika bendi yake ya Negro Succes.
"Nilipata taabu sana kupata mafanikio ndani ya Negro Success kwa vile sikujua vema lugha ya Lingala. Nashukuru Bavon aliyenisaidia mpaka alipofariki kwa ajali ya gari mwaka 1970, na mimi kuhamia Lipualipua nikiwa na Nyboma Mwandido," alisema.
Makundi mengine aliyopitia mkali huyo aliyejitosa kwenye Uandishi wa Vitabu kwa sasa, akiwa ameachia kitabu kiitwacho 'Jifunze Lingala', ni Le Kamalee, Fukafuka, Marquiz du Zaire kabla ya kuja nchini na kupigia bendi mbalimbali.
Baadhi ya bendi alizopigia nchini ni DDC Mlimani Park, Makassy Band, Mambo Bado, Marquiz Original, Legho Stars kabla ya kuanzisha bendi ya Bana Marquiz inayotamba hadi sasa jijini Dar es Salaam.
Assosa alisema japo anasikitika kushindwa kuwa Padri, bado anashukuru fani ya muziki imemsaidia kwa mengi, ikiwemo kumudu maisha, akisomesha watoto na kuitunza familia yake, mbali na kufahamika na kumiliki mali ambazo hakupendwa zitajwe.
"Sio siri muziki umenisaidia kwa mengi na siwezi kuacha mpaka mwisho wa maisha yangu. Nimejikita kwenye uandishi wa vitabu, lakini haina maana ndio mwisho wangu wa muziki."
Mkali huyo, alizaliwa miaka 60 iliyopita akiwa mtoto wa pili kati ya nane, ameoana na Evangeline Paul Kimiti na kupata naye watoto.
Mkali huyo, alisema ameingia kwenye uandishi wa vitabu baada ya kuona Watanzania wengi wanapenda kujifunza Kilingala kwa kuzipenda nyimbo za Kongo.
"Nimeanza na 'Jifunze Lingala' ili kukidhi maombi ya mashabiki wa nyimbo za Lingala waliotaka tafsiri ya mashairi yake, ila nipo mbioni kutoa vingine ili niwasaidie wale wanaotaka kujifunza lugha hiyo," aliongeza.
Assosa anayependa kula Ugali kwa Kisamvu na Uyoga, aliwahi kucheza soka kama kiungo alipokuwa St Luhanga Seminary.
Assosa ni shabiki wa Manchester United, na mpenzi mkubwa wa mavazi ya rangi nyeupe na nyeusi. Hatumii kilevi.
Assosa, aliyetikisa Afrika na vibao kama Masua, Abisina, alichokitunga na kuimba na Nyboma, kabla ya mwenzake kumuomba akimiliki, alisema tukio la furaha kwake ni siku alipoanza kuwa na familia, huku akihuzunishwa na vifo vya wanamuziki wenzake.
Mtunzi na muimbaji huyo, alisema licha ya kutunga vibao vingi, kibao cha Bomoa Tutajenga Kesho alichotunga akiwa Mambo Bado, ndicho anachokikumbuka zaidi kwa jinsi kilivyomtia misukosuko na serikali ya awamu ya kwanza miaka ya 1980.
Assosa alisema japo alitunga kibao hicho bila ya maana yoyote zaidi ya kutoa burudani mashabiki wao, ulitafsiriwa vibaya na serikali ya Julius Nyerere kiasi cha kufikia kupigwa marufuku kwa kuonekana unachochea 'ufisadi'.
Kibao hicho alichotunga mwaka 1983, kina mistari isemayo 'Bomoa ee Bomoa ee Bomoa aa mamaa tutajenga kesho ooh i maee Oo Beti mayaiee ooh maax2'
Assosa, alisema kama angekutana na Rais angemuomba awe mkali kwa wanaoichezea amani na kutaka kuleta vurugu nchini.
"Rais awe mkali kwa wanaoichezea amani na utulivu wa nchi, machafuko na vita ni mambo mabaya, wanaovishabikia hawajui madhara yake," alisema.
Assosa aliyeitungia DDC Mlimani Park kibao cha 'Gama Nihurumie', alisema muziki wa Tanzania hautambi kama zamani kwa sababu ya uvivu wa wasanii wa sasa na bendi zote kupiga muziki unaofanana wakiiga toka Kongo.
"Zamani ilikuwa rahisi kujua miondoko ya Msondo, Sikinde, Marquiz au OSS, kwa vile zilikuwa zikipiga mirindimo yao, kwa sasa bendi zote zinapiga muziki wa aina moja wakiiga nje, ndio maana muziki wetu hautambi kimataifa," alisema.
Alisema jambo hilo lipo hata Kongo, kwa JB Mpiana, Koffi Olomide, Werrason, Ferre Gora na Fally Ipupa kutojitofautisha kama ilivyokuwa kwa akina Tabu Ley au Franco na African Jazz waliowapagawisha wazungu.

Mwisho

No comments:

Post a Comment