STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, October 4, 2014

Simba majaribuni tena leo Taifa, Yanga kujiuliza kwa JKT Ruvu kesho

Simba wanaoingia tena majaribuni kusaka ushindi wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu
Azam wapo ugenini Mjini Mbeya kuvaana na Prisons wataendeleza ubabe au...!
Mbeya City wanatoka kwa mara ya kwanza kuvaana na Ruvu Shooting-Mbatini
Mtibwa wenyewe watashuka dimbani kesho kuvaana na Mgambo JKT

Ndanda Kuchele watakuwa Mkwakwani kujiuliza kwa Coastal Union
Baada ya kushindwa kuhimili vishindo vya Yanga, Prosns kuvuna nini kwa Azam leo?
Yanga wataendeleza ubabe wao kwa JKT Ruvu au watazamishwa Taifa kesho

BAADA ya kushindwa kupata ushindi katika mechi mbili mfululizo kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Taifa, Simba leo itashuka tena kwenye dimba hilo kujaribu bahatai yake kwa timu iliyopanda daraja ya Stand United wakati watani zao wakijiandaa kuivaa JKT Ruvu kesho katika uwanja huo huo wa Taifa.
Simba iliambulia sare mbili kwa Coastal Union na Polisi Moro na kuibua taharuki kwa mashabiki wao ambao hawaamini kama timu yao ndiyo inayochechemea katika ligi hiyo baada ya kufanya mabdiliko ya benchi ya ufundi na kikosi chao toka kile cha msimu uliopita kiliochowanyima raha na kuambulia nafasi ya nne.
Kocha wa Simba, Patrick Phiri ameahidi kufanya mabadiliko makubwa katika kikosi chake ili kupata ushindi baada ya kuchoshwa na sare mfululizo, huku wakitangulia kufunga mabao na kurejeshwa na wapinzani wao.
Ushindi pekee ndiyo utakaoisaidia Simba kuwatuliza mashabiki wao ambao tayari wameanza kumsaka mchawi wakiamini mgawanyiko wa makundi ya wanachama ni sababu ya 'kuhujumuiana'.
Wakati Simba ikipania kupata ushindi wake wa kwanza wapinzani wao walionja ushindi katika mechi yao iliyopita dhidi ya Mgambo JKT imeapa kuendelea kuwatonesha Msimbazi kwa kuwagiwa dozi ili waendelee kula tamu ya ligi hiyo wanayoicheza kwa mara ya kwanza msimu huu.
Kikosi hicho kupitia kocha msaidizi, Athuman Bilal 'Bilo' kimetamba kuwa kinatambua Simba kama timu kubwa na kongwe, lakini soka halitegemei vigezo hivyo zaidi ya timu kujituma na kupata uishindi uwanjani kitu ambacho wamekipania kufanya hivyo jioni ya leo.
Mbali na pambano hilo leo kuna mechi nyingine nne katika viwanja tofauti ambao mabingwa watetezi na vinara wa msimamo huo kwa sasa, Azam watakuwa ugenini kuwakabili wenyeji wao Prisons ya Mbeya inayouguza kichapo cha amabao 2-1 ilichopewa na Yanga wiki iliyopita.
Pambano hilo linasubiriwa kwa hamu kubwa kutokana na ukweli hiyo ni mechi ya kwanza ya nyumbani kwa Prisons na ya kwanza ya ugenini pia kwa Azam walioshinda mechi mbili za awali nyumbani uwanja wa Chamazi dhdidi ya Polisi Moro na Ruvu Shooting.
Ruvu wanaoburuza mkia katika msimamo wa ligi hiyo watakuwa uwanja wa nyumbani kuwaalika Mbeya City wakiwa na machungu ya kupoteza mechi zao mbili za awali huku wakiwa hawana bao hata moja kuonyesha kwamba pengo la Elias Maguri, bado halijapata mbadala wake.
Kocha Tom Oloba amesema kuwa anaamini timu yake leo itashinda nyumbani baada ya kurekebisha tatizo lililokuwa likiikabili Ruvu hasa eneo la kiungo na ushambuliaji waliokuwa wakipoteza mipira kizembe.
Pambano jingine ni lile litakalochezwa mjini Morogoro wakati Polisi watakapowakaribisha kwenye uwanja wa Jamhuri, Kagera Sugar ambao mechi yao ya tatu sasa wapo ugenini, huku Ndanda Fc walioanza kwa mbwembwe ligi hiyo kwa kuicharaza Stand mabao 4-1 itakuwa wageni wa Wagosi wa Kaya, Coastal Union.
Siku ya kesho Yanga watavaana na maafande wa JKT Ruvu wanaonolewa na nyota wao wa zamani na aliyekuwa kocha msaidizi wa vijana wa Jangwani, Fred Felix Minziro.
Katika mechi ya mwisho kukutana kwa tyimu hizo msimu uliopita, Minziro na vijana wake waliaibika kwa kukandikwa mabao 5-1, jambo ambalo hata hivyo halitegemewi litokee leo hasa baada ya JKT Ruvu kusuka upya kikosi chake na kikiwa na usongo wa kutaka kupata ushindi wa kwanza katika ligi hiyo.
Maafande hao walianza kwa suluhu mjini Mbeya kabla ya kutolewa nishai wiki iliyopita na Kagera Sugar hali inayowafanya Yanga wajiandae kukabiliana na upinzani mkubwa toka kwa vijana hao wa Minziro.
Pambano jingine litakalochezwa kesho litakuwa ni kati ya Mtibwa Sugar watakaoialika Mgambo JKT wakiwa na kumbukumbu ya kushinda mechi zao mbili za awali na kuongoza msimamo sambamba na Azam.
Mtibwa inayonolewa na Nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Mecky Mexime ilianza kwa kuinyuka Yanga mabao 2-0 kabla ya kuwazima Ndanda kwa mabao 3-1, huku wenzao walianza kwa kuilaza Kagera Sugar bao 1-0 na kulala kwa idadi kama hiyo mbele ya Stand United kitu kinachofanya pambano hilo kushindwa kutabirika mapema.
Je ni timu zipi zitakazocheka au kulia kwa leo na kesho? Bila shaka ni suala la kusubiri baada ya dakika 90 kumalizika katika viwanja vitakavyotumiwa kwa mipambano hiyo ya kusisimua ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

No comments:

Post a Comment