MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya England, Manchester City wamekumbana na kipigo cha kushtukiza ugenini baada ya kuzamishwa mabao 2-1 na West Ham United katika mchezo wa mapema wa ligi hiyo maarufu kama EPL.
Hicho kilikuwa ni kipigo cha pili kwa Machester City kwa msimu huu baada ya awali kushindw akuhimili vishindo vya Stoke City waliowatambia kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Etihad kwa bao 1-0 mnamo Agosti 30.
Wenyeji waliochupa hadi nafasi ya nne kwa ushindi huo walianza kuandika bao la kuongoza dakika ya 21 kupitia kwa Morgan Amalfitano akimalizia kazi nzuri ya Valencia, bao lililodumu hadi mapumziko.
Kipindi cha pili timu zote zilizoendelea kushambuliana na kufanya kosa kosa nyingi kabla ya wenyeji kujiandikia bao la pili dakika ya 75 kupitia kwa Diafra Sakho kabla ya David Silva kuipatia Manchester City bao la kufutia machozi dakika mbili baadaye akimaliza kazi ya Jesús Navas.
Kipigo hicho kimeiacha Manchester City ikisaliwa na pointi 17 na kushindwa kupunguza pengo la pointi dhidi ya Chelsea yenye 22 ambayo itashuka kesho ugenini kuvaana na Manchester United. Watetezi hao wanaweza kuporomoka nafasi ya chini toka nafasi ya pili wanaoishikilia kwa sasa kwa sababu michezo mingine ya ligi inaendelea kuchezwa hivi sasa.
No comments:
Post a Comment