 |
| Askofu Pengo |
 |
| Baadhi ya Majeruhi wa tukio hilo akihudumiwa |
WATANZANIA wametakiwa kuwa watulivu na kuachana na hisia za kunyoosheana
kidole kwamba wahusika wa shambulizi la kigaidi dhidi Kanisa Katoliki
la Mtakatifu Josefu Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti, jijini Arusha
Jumapili iliyopita kuwa ni Waislamu kwa kuwa watuhumiwa waliokwisha
kukamatwa pia kuna Wakristo.
Kauli hiyo ilitolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es
Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, alipokuwa akizungumza kupitia
kituo cha televisheni cha Tumaini.
Askofu Pengo aliwataka wananchi kuacha hisia badala yake waache
uchunguzi wa kubaini waliohusika uendelee ili kupata matokeo mazuri.
“Siamini kama waliofanya tukio hili baya ni Waislamu kwa kuwa watuhumiwa
wanaoshikiliwa mpaka sasa wamo Wakristo, ni bora kuacha kuhisi,”
alisema Askofu Pengo.
Hii ni mara ya kwanza kwa Kardinali Pengo kuzungumzia shambulizi hilo
baya la bomu ambalo limeibua hisia kali miongoni mwa jamii kwani ni kwa
mara ya kwanza kanisa linapigwa bomu kwa mbinu zinazodhihirisha kuwa ni
harakati za kigaidi.
WASAUDI WALIINGIA NCHINI MEI 4
Pengo akiweka msimamo huo, NIPASHE imefahamishwa kuwa raia wanne wa
Saudi Arabia waliokamatwa kwa tuhuma za kuhusika ugaidi dhidi ya Parokia
ya Olasiti, walilala katika hoteli moja iliyopo jirani na stendi kuu ya
mabasi ya kwenda na kutoka mikoani.
Uchunguzi wa NIPASHE umebaini kuwa watuhumiwa hao waliingia nchini
kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) Mei 4, mwaka
huu, na baada ya tukio la mlipuko wa bomu hilo walianza safari ya
kutoroka nchini kupitia mpaka wa Tanzania na Kenya wa Namanga.
Habari zinasema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa na vyombo vya usalama
karibu na maeneo ya mzunguko wa Forida katika barabara itokayo Mianzini
kwenda katikati ya jiji.
VIFO VYAFIKA WATU WANNE
Katika hatua nyingine, majeruhi mwingine wa mlipuko huo, Isabela Michael
(19), amefariki dunia katika Hospitali ya Mtakatifu Elizabeth, maarufu
kama ‘kwa babu’ jana.
Taarifa hizo zilizotolewa na Mganga Mkuu wa Hospitali ya St. Elizabeth,
Goodluck Kwayu mbele ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu jana.
Kifo cha Isabela ambaye mama yake mzazi naye yupo mahututi hospitalini
hapo, kinafanya idadi ya watu waliokufa kutokana na shambulizi kufikia
wanne.
Juzi waliotajwa kufariki dunia ni Regina Longino Kurusei (45) na James
Gabriel (16) pamoja na majeruhi mwingine ambaye jina lake halikutajwa.
Katika tukio hilo, zaidi ya watu 66 walijeruhiwa na kulazwa katika
Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, Hospitali binafsi ya Selian
na St. Elizabeth.
Akizungumza katika Hospitali ya Mount Meru baada ya kuwatembelea
majeruhi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd,
alilaani tukio hilo na akawataka Watanzania kuwa tukio hilo lisiwagawe
Wakristo na Waislamu.
Alisema Wakristo na Waislamu kwa miaka mingi wamekuwa wakishirikiana kama ndugu, hivyo ni vyema ushirikiano huo ukaendelea.
“Tukio hili lisitugawe Wakristo na Waislamu, tuna historia ya muda mrefu ya kushirikiana vizuri,” alisema.
Balozi Idd aliwataka Watanzani kuwa watulivu wakati vyombo vya ulinzi na
usalama vikifanya kazi ya uchunguzi wa tukio hilo na kuwanasa wahusika.
MAALIM SEIF: TUMESIKITISHWA
Naye Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharrif Hamad, ambaye
aliwatembelea majeruhi hao, alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
(SMZ) na Chama cha Wananchi (CUF) wanalaani vikali tukio hilo.
“SMZ na CUF tumesikitishwa na kulaani tukio hilo la uhalifu na ugaidi wa hali ya juu kufanyika hapa nchini,” alisema.
Aliwaomba Watanzania kuwa watulivu na akawaomba wananchi ambao wana
taarifa kuhusiana na watu waliohusika kwenye tukio hilo kutoa taarifa
hizo kwa vyombo vya dola.
TAARIFA YA PINDA BUNGENI
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amesema tukio hilo si jambo la kushabikiwa kisiasa.
Alitoa kauli hiyo jana bungeni mara baada ya kurejea kutoka Arusha
alikokwenda kutembelea eneo la tukio, baada ya Spika wa Bunge, Anne
Makinda, kumpa nafasi ya kutoa taarifa fupi ya safari yake.
Alisema kwa bahati mbaya wapo baadhi ya viongozi wachache wanapitapita
eneo la tukio na badala ya kutumia wananchi kuzungumza nao wanaingiza
visiasaisa. “Naomba sana jambo hili tusilitumie kwa namna hiyo.”
Pinda alisema uchunguzi bado unaendelea, wamekamatwa watu wanane, wanne
ni watu wenye asili ya kutoka Uarabuni, watatu ni Watanzania ambao
wameanza kuhojiwa katika vuguvugu la jambo hilo.
Alisema raia wanne wa Kenya ambao walikamatwa ni kwa sababu tu ya kutaka
kujiridhisha kwa kuwa wako Arusha siku moja kabla na siku ya tukio
ndipo walipoanza safari ya kwenda Nairobi.
“Kwa sababu barabara zile zilikuwa zimeshafungwa, isingewezekana wao
kupita kiurahisi bila kuhojiwa kwa maana ya kujiridhisha. Ni matumaini
yetu kuwa pengine taarifa itatoka mapema leo (jana) au kesho (leo) kwa
sababu wameanza tangu jana kuzungumza nao kama wanahusika kwa namna moja
au nyingine.
Wengine bado uchunguzi na mahojiano yanaendelea.” Alisema alipofika
Arusha alikuta wananchi wameshatulia na eneo la tukio palikuwa na
utulivu, ingawa watu walihamaki, lakini wamefarijika na hatua za
serikali za kufanya uchunguzi mara moja.
Alisema hospitalini katika majeruhi 66, walioruhusiwa ni 24 waliobaki
wanaendelea kuuguzwa katika hospitali mbalimbali, wengi wao wapo Mount
Meru.
Alisema sehemu kubwa ya wale walioathirika wameshafanyiwa upasuaji kwa
ajili ya kutoa vipande vya vyuma vilivyokuwa vimewaathiri.
“Wengi tumewakuta wako katika hali nzuri, wengine leo (jana) watapelekwa
katika chumba cha upasuaji na wengine inawezekana kesho (leo).”
Alisema wamewaomba madaktari vile vipande vya vyuma vikipatikana
wasivitupe wakabidhi kwa vyombo vya dola ili waweze kubaini kama bomu
lile la mkono limetengenezwa kienyeji au lililotengenezwa viwandani na
kwa hiyo ni bomu linalotokana na jeshi. “Tutaweza kubaini chimbuko la
bomu hilo ni nini.”
Wakati uchunguzi ukiendelea, Waziri Mkuu alisema wamewaomba wakazi wa
Arusha yeyote mwenye taarifa ambazo zinaweza kusaidia za kubaini kwa
uhakika juu ya nani kafanya jambo hilo na kwanini ajitokeze.
WABUNGE: AMANI KWA GHARAMA YOYOTE
Baadhi ya wabunge wamewataka Watanzania kuungana, kuepuka tofauti zao za
kiitikadi, dini na viongozi kunyoosheana vidole ili amani ilindwe kwa
gharama yoyote.
Wakichangia mjadala wa hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi jana, wabunge wengi waliochangia mjadala huo walisema tukio la
Arusha limeishtua nchi na dunia na kilichotokea huko si utamaduni,
desturi na jambo lililozoeleka kwa Watanzania.
Waliwaomba Watanzania wajikumbushe yaliyotokea Rwanda kwani mgogoro ule
kwa kiasi kikubwa ulisababishwa na kauli. Mbunge wa Kuteuliwa, James
Mbatia (NCCR-Mageuzi), alisema ni mambo ya kusikitisha kwa kuwa taifa ni
la Watanzania.
Alisema janga likitokea inabidi Watanzania wote bila kujali imani, dini wala itikadi wawe wamoja.
“Amani inabidi ilindwe kwa gharama yoyote ile. Chochoko zilizozama
miongoni mwa Watanzania kwa kauli za baadhi ya viongozi na Watanzania,”
alisema.
Alisema Serikali haina dini na kila mtu ana imani yake ya dini, lakini
leo unaweza kumpigia kiongozi wa serikali, hata askari simu mlio wake ni
wa nyimbo za dini.
“Ningeomba kuanzia leo milio ya simu ya dini tuiondoe inasambaratisha
Watanzania. Tuko wapi na tunaipeleka wapi. Naomba kwa moyo wa dhati
mihadhara ya kidini iliyodumu kwa zaidi ya miaka 20 tuseme basi
imetosha,” alisema.
Alihoji serikali inashindwaje kufanya maamuzi huku akinukuu maneno ya
falsafa yanayosema ukiona maovu yanatokea, kemea, zuia. Alisema ukumbi
wa Bunge ni baraza, lakini limefanywa la matusi.
Alishauri Watanzania wawe na utulivu na watafakari pamoja.
“Watanzania, viongozi wa dini tusiwe wepesi kuonyesheana vidole, mauaji
ya padre, viongozi wamekata tamaa, wamesema sasa tumechoka.
Tusiwaruhusu viongozi wetu watupeleke huko,” alisema na kuongeza: “Ndimi
zetu kauli zetu zitaliangamiza taifa la Tanzania. Tumefika mahali
Tanzania tuseme basi.”
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsa Vuai Nahodha,
akichangia mjadala huo alisema, ni kawaida kwa viongozi kulaumiana na
kumtafuta mchawi.
Alisema viongozi wenye busara kama hawa hawapaswi kulaumu watu
linapotokea tatizo kama hilo. Alisema ajenda iliyopo mbele ni tatizo la
kuvurugika kwa amani.
“Huu si wakati wa kulaumiana ni wakati kujenga mshikamano wa kuwatafuta waliohusika na tukio hili.”
Alisema sifa ya uongozi ni kukubali ukweli hata kwa mambo ambayo
hawayapendi. “Kuna mahali sisi viongozi tumekosea. Unaposikiliza
mijadala ya wabunge, wakati mwingine kauli zetu haziashirii mema. Na
hatuwezi kushangaa haya yanayotokea,” alisema.
Aliongeza kuwa kiongozi anaposema jambo ni lazima apime kwani Tanzania
ni nchi changa ina miaka 50 tu na kutokana na kiwango cha elimu na uwezo
wa kuchanganua mambo ni mdogo.
“Tujikumbushe yaliyotokea Rwanda. Mgogoro ule kwa kiasi kikubwa ulisababishwa na kauli.
Waswahili husema watu makini na wenye busara hujifunza. Najua ni ngumu
sana mwanadamu kubadilika na kuacha mambo ambayo ameyazoea,” alisema.
Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema), alisema tukio la Arusha
limeishtua nchi na kilichotokea Arusha siyo utamaduni, desturi na
halijazoeleka kwa Watanzania.
“Nitoe wito kwa wabunge na Watanzania wote kuwa huu si wakati wa kutupiana lawama.
Katika jambo hili lazima tuhakikishe kwamba tunashirikiana kurejesha
utulivu katika jiji la Arusha. Lazima tuchunge ndimi zetu, viongozi
pamoja na sisi wananchi.
Tuanzie hapa bungeni. Hakuna sababu ya kuanza kunyoosheana vidole,
kwamba jambo hili ni la kisiasa au la kidini. Mwenye kuhisi hivyo
ashirikiane na tume ya uchunguzi kuwabaini,” alisema.
Alisema sheria zimetungwa na zipo, lakini kuna woga wa kuzitumia. Mtu
mwenye uhakika kwamba ni la kidini au la kisiasa kwa nini asitoe
ushahidi?”
Aliongeza kuwa jambo hili linafundisha kuwa nchi haiko salama,
Watanzania wamegawanyika kwa sababu hiyo ni rahisi kutumiwa na maadui.
“Baadhi yetu tunasema jambo hilo limesababishwa na kundi fulani. Hatuko
salama. Hakuna mashehe au maaskofu wanaotengeneza makundi kutukana
wenzao.
Lakini naamini kuna kundi la wahuni wanaofanya hivyo. Sababu gani
hawakamatwi, tunawaogopa nini. Nyinyi polisi ndiyo mnatoa vibali vya
mikutano ya kutukana watu. Kwa nini watu hawa hawakamatwi?” alihoji.
Alisema watu wamefikia hatua ya kusimama hadharani na kushambulia kuwa
chama hiki ni cha Waislamu, chama hichi ni cha Wakristo. Serikali
ionyeshe ipo na weledi wake.
Aidha, alitaka Serikali itunge sheria ya kudhibiti lugha za uchochezi kwenye mikutano na majukwaa.
Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa, alisema kutokana na matukio
yanayotokea hivi sasa kuna haja ya kuimarisha ulinzi kwenye eneo la
jengo la Bunge.
Alimwambia Spika wa Bunge kuwa asije kushangaa siku moja Bunge lake tukufu linavamiwa na wahuni.
“Arusha kusingekuwa na ulinzi wa kutosha hata wale waliohusika wasingekamatwa.
Kuanzia sasa huku nyuma (bungeni) mtu akirusha kitu kitafika ndani.
Watu kule nje wanatuona tunavyozungumza na tunavyosigana humu ndani.
Lazima ulinzi uimarishwe,” alisema na kuongeza: “Tuzime moto kabla moto
haujalipuka, anayechokozwa, huchokozeka.”
Aidha, alipendekeza makomandoo wa Jeshi la Polisi, waongezewe muda wa kustaafu ili kutoa uzoefu kwa vijana.
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Chiku Abwao , alihoji kuhusu uchunguzi
wa kutekwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen
Ulimboka na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom
Kibanda, na kwamba serikali imefikia wapi kuhusiana na suala hilo.
Hamad Ali Hamad (CUF-Magogoni), alisema chama chake kimewagharimu muda
mwingi kuwaambia Watanzania kuwa si chama cha kidini, lakini ilikuwa
ikitumiwa kama propaganda ya kukiua.
Naibu Waziri wa Serikali za Mitaa, Tawala za Mikoa (Tamisemi), Aggrey Mwanry, alisema adui anaigawa Tanzania.
Alisema Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliposema nchi hii haina dini watu hawakumuelewa.
“Taifa hili likienda likateketea, sisi hatutaacha kulaumiwa. Hapa
imezungumzwa habari za dola, hiki ni chombo cha kundi ni chombo
kinachoangalia tabaka. Dola ni chombo cha mabavu, akifika anabamiza.
Kiwango cha mabavu kinategemea na kiwango kitakachokutwa sehemu ya
tukio,” alisema.
Alisema ikifika mahali kwamba nchi haitawaliki maana yake unafika kwenye
shamba la mtu unavuna mahindi unaondoka, unaenda sokoni unachukua
samaki wa watu unaondoka bila kulipa, hapo ndipo utasema nchi
haitawaliki.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Samia Hassan Suluhu,
alisema vitabu vyote vya dini havina maamrisho ya kuvuruga imani ya
mwenzie. “Kinachozungumzwa ndani ya ukumbi wa Bunge ni kizuri, lakini
kinachotokea nje kinasababishwa na sisi wenyewe,” alisema.
Alisema amani ni kama uzi wa hariri, hivyo Watanzania wasiukate, ukikatika vinginevyo watashindwa kuunga.
Waziri Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika, alitaka
polisi kuchapa kazi yao kwani hata nje ya nchi wanasifiwa. Alisema
baadhi ya wanasiasa wanafanya kazi ya polisi kuwa ngumu.
“Kauli zetu wanasiasa tuchunge maslahi ya nchi hii, anayesema mtu huyu
ni mhalifu tunamtia hatiani ni kazi ya mahakama,” alisisitiza.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William
Lukuvi, alisema Jeshi la Polisi litatimiza wajibu wake pamoja na
kufanyakazi katika mazingira magumu.
Alisema ukiona mtu anaichukia polisi, lazima ujiulize ana nini.
CHANZO:NIPASHE