STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, August 17, 2013

Pambano laMada Maugo, Thomas Mashali utata mtupu

Bondia Thomas Mashali
Bondia Mada Maugo
PAMBANO la kimataifa la kuwania ubingwa wa WBF-Afrika kati ya mabondia Mada Maugo na Thomas Mashali ni utata mtupu baada ya Mashali kutangaza kutolitambua na kusema hayupo tayari kupanda ulingoni kama inavyotangazwa na waandaaji wake.
Akizungumza na MICHARAZO  Mashali alisema anashangaa waratibu wanaotangaza kuwa atapigana na Maugo wakati hawajamalizana naye kwa lolote, huku akitishia kuwaburuza katika vyombo vya sheria kama wataendelea kumtangaza.
Mashali alisema ni kweli kulikuwa na mipango ya kupambanishwa na Maugo, lakini hakuna muafaka wowote uliofikiwa na hivyo anashangaa kutangazwa atapanda ulingoni Agosti 30 kupigana katika pambano la uzani wa kati la raundi 12.
"Sijasaini kokte hivyo silitambui pambano hilo, kwani hata Maugo anayetajwa ndiye mpinzani wangu anatarajiwa kuondoka Agosti 24 kwenda Ghana, ndiyo maana wala sifanyi mazoezi kwa sasa kwa ajili ya shindano lolote, " alisema na kuongeza;
"Nawasiliana na mwanasheria wangu kuchukua hatua dhidi ya watu hao kwani inaweza kuja kuniharibia pambano lisipofanyika kwa kuonekana nimeingia mtini," alisema Mashali alipozungumza kwa njia ya simu na gazeti hili.
Hata hivyo Maugo aliyepo Musoma kwa sasa, alisema anajua pambano lake la Mashali lipo kwa vile alisaini mkataba wa kupigana Agosti 30 kuwania mkanda wa WBF-Afrika na kushangaa kusikia taarifa za mpinzani wake kuukana mchezo huo.
"Japo siwezi kumsemea, lakini mimi nalitambua pambano hilo na nitaanza rasmi mazoezi yangu kwa ajili ya kumtwanga Mashali Jumatatu ijayo. Ni kweli nilikuwa niende Ghana kucheza pambano la kimataifa ila nimeahirisha kwa vile nilishasaini mkataba na waratibu wa pambano la Francis Cheka dhidi ya Mmarekani Phil Williams," alisema.
Maugo alisema yeye hawezi kubweteka na maneno ya Mashali akiamini huenda ni janja yake ya kumfanya aridhike na kutojiandaa na mchezo huo.
Naye Rais wa TPBO-Limited wanaolisimamia pambano hilo, Yasin Abdallah 'Ustaadh' alisema anashangazwa na kauli ya Mashali kuukana mchezo huo wakati alishasaini na kupewa sehemu ya malipo ya awali ya mchezo huo toka kwa waratibu wake.
Ustaadh alisema kama Mashali anamuogopa Maugo na kutaka kulikwepa kijanja pambano hilo anaandike barua na kuiwasilisha TPBO aliposaini mkataba wa awali pia arejeshe kiasi cha fedha alizopewa akitaja Sh. Mil. 2 kati ya 5 walizokubaliana.
"Asitake kutuyumbisha kama anafanya hivyo kwa kumhofia Maugo aseme kwa kuandika barua, ila anachokifanya kinakatisha tamaa mapromota," alisema Ustaadh.
Aliongeza kwa hali kama hii ya Mashali kusaini mkataba na kuchukua malipo ya awali akipendekeza mwenyewe pambano hilo lichezwe raundi 12 badala ya 8 zilizokuwa zimepangwa kisha kuja kulikana ni kuonyesha namna gani mabondia wa Tanzania wasivyojitambua.
"Hii ndiyo inatufanya sisi TPBO kupendekeza kila mara mabondia wetu wapimwe ulevi ili kuepusha usumbufu kama huu, inasikitisha," alisema.
Rais huyo alisisitiza kuwa TPBO na waratibu wa pambano hilo wanatambua kuwa mchezo huo wa Maugo na Mashali upo kama ulivyopangwa licha ya mkwara huo wa Mashali aliyesisitiza hakuna chochote alichokubaliana na waratibu au TPBO Limited.

Kocha Mpya JKT Ruvu hana mchecheto

Kocha Mbwana Makatta

KOCHA Mkuu mpya wa JKT Ruvu, Mbwana Makatta ameapa kurekebisha makosa yaliyoigharimu timu hiyo katika msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku akiionya Mgambo JKT ya Tanga isitarajie mteremko wiki ijayo katika pambano lao la fungua dimba la Ligi Kuu litakalochezwa Mkwakwani jijini Tanga.
Makatta aliyetua katuika kikosi hicho kuchukua nafasi ya Charles Kilinda aliyejiuzulu katikati ya msimu uliopita baada ya JKT Ruvu kufanya vibaya na kupokewa kwa muda na kocha Kennedy Mwaisabula, alisema kitu anachoomba kwa wana JKT ni ushirikiano na nguvu ya pamoja kuweza kuiwezesha timu yao ifanye vyema.
Kocha huyo alisema mara baada ya kutua katika timu hiyo amejaribu kuweka mambo sawa kati ya yale yaliyoigharimu JKT Ruvu na kuyumba msimu uliopita na kwa muda wa maandalizi waliyofanya kwa kiasi fulani mambo yametengemaa na wapo tayari kwa 'vita'.
"Tunaamini hatuwezi kurejea makosa ya msimu uliopita, pia itambuliwe kila kocha na falsafa yake na mimi nimetua JKT nikiwa na malengo yangu na hasa kuhakikisha naifikisha mahali pazuri timu hii, ila naomba kupewa ushirikiano wa kutosha kufanikisha hayo," alisema.
Aliongeza kwa maandalizi waliyofanya wakati wa kujiandaa na ligi hiyo wanaamini kikosi chake kimewiva kuikabili Mgambo JKT katika mechi ya ufunguzi Agosti 24 na nyingine za ligi hiyo na wamepania kuhakikisha wanapata ushindi kwa kila mechi ili angalau duru la kwanza litakapoisha wawe katika nafasi nzuri.
"Tutaanzia  ugenini katika mechi yetu ya kwanza, lakini hilo halitutishi tutaenda kwa dhamira moja ya kusaka ushindi dhidi ya Mgambo JKT," alisema Makatta kipa wa zamani wa Tukuyu Stars na Yanga.
Baada ya mechi hiyo vijana hao wa JKT Ruvu watarejea nyumbani uwanja wa Mabatini-Mlandizi Pwani kuikaribisha Prisons ya Mbeya katika mchezo wake wa pili.

Azam, Yanga hatumwi mtoto dukani! Zawania Ngao ya Hisani

Mashabiki wa Yanga watashangilia kama hivi leo mbele ya Azam

Mashabiki wa Azam watapuliza kwa mbwembwe 'kidedea' chao leo kwa Yanga?
WAKATI Yanga ikitamba itawatia adabu Azam katika pambano lao la Ngao ya Hisani linalochezwa leo kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wapinzani wao hao wamesema watautumia mchezo huo kama dira na muelekeo ya timu yao kwa msimu mpya wa 2013-2014 wakipania kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza.
Meneja wa Azam, Jemedari Said alisema watashuka dimbani leo kwa tahadhari kubwa kwa kutambua kuwa huo ndiyo mchezo wao wa mwisho kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo wamepania kutwaa taji lake na wanataka kuonyesha matunda ya ziara ya kambi yao ya mazoezi nchini Afrika Kusini.
Said, alisema wanafahamu Yanga ni timu kubwa na imekuwa na upinzani mkubwa kila ikikutana na timu yao, lakini bado hawana hofu kwa sababu malengo yao makuu yapo kwenye Ligi Kuu, hivyo wanataka kuutumia mchezo huo kujua muelekeo wao kwa msimu huu.
Meneja huyo aliongeza kitu cha kufurahisha ni kwamba kikosi chao chote kilichoenda Afrika Kusini kipo fiti kikiwa hakina majeruhi wala mgonjwa, huku nyota wa wawili wa kimataifa, Brian Umony na Humphrey Mieno wameanza kufanya mazoezi mepesi ya gym kuonyesha wanaendelea vyema na majeraha waliyokuwa nayo.
"Mechi ya Ngao ya Hisani kwetu ni kipimo cha kujua tutakuwa na msimu gani safari hii, tutashuka dimbani kwa tahadhari kubwa lengo likiwa kutaka kuwoanyesha mashabiki kile tulichovuna Afrika Kusini na katika mechi zetu nane za maandalizi ya ligi zikiwemo nne za nchini humo," alisema Said.
Alisema akili yao kwa dhati kabisa ipo kwenue ligi na hasa pambano lao la ufunguzi dhidi ya Mtibwa Sugar ambalo litachezwa ugenini na mechi nyingine zijazo wakikusudia kufanya kweli na kuweka rekodi ya kutwaa ubingwa huo kwa mara ya kwanza baada ya kuhiodhiwa mfululizo kwa kupokezana kati ya Simba na Yanga.
Upande wa Yanga inayonolewa na Mholanzi, Ernie Brands, imesema haina mchecheto na pambano hilo la leo kwa vile vijana wao wapo kamili kuendeleza rekodi ya ushindi mfululizo kwa siku za karuibuni.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Fred Felix Minziro, alisema kikosi chao kipo tayari kwa 'vita' na kwamba wangependa kutoa dozi kwa Azam kabla ya kuanza kuzishughulikia timu nyingine katika Ligi Kuu inayoanza wiki ijayo.
Yanga imepata matokeo ya ushindi katika mechi tatu mfululizo, ikizilaza Mtibwa Sugar kwa mabao 3-1 kabla ya kuinyoa 3 Pillars ya Nigeria kwa bao 1-0 na kuisulubu SC Villa ya Uganda kwa mabao 4-1 katika mechi za kirafiki za kimataifa zilizochezwa uwanja wa Taifa siku chache iliponusurika kipigo na kupata sare ya 2-2 na URA-Uganda.

Friday, August 16, 2013

Waislam waitana Dar kuhusiana kupigwa risasi, kukimbizwa Segerea akiwa mgonjwa kwa Sheikh Ponda


SIKU moja tu baada ya jeshi la Polisi 'kumtorosha' kininja Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania akiwa bado akiuguza jehara la kupigwa risasi alipokuwa amelazwa Hospitali ya Muhimbili (MOI), Waislam wameitana kwa ajili ya kutoa tamko na kuamua la kufanya kutokana na kadhia hiyo.
Sheikh Ponda anadaiwa kupigwa risasi na Polisi mkoani Morogoro mara baada ya kumaliza kuzungumza na Waislam katika Kongamano la Wahadhiri wa Kiislam mkoani humo kwa kilichoelezwa kwamba anasakwa kwa kauli za kichochezi visiwani Zanzibar, ambapo awali Polisi waliruka kuwepo kwa tukio hilo kabla ya baada ya kudai ililazimika kupiga mabomu ya machozi na risasi baridi baada ya kuzuiwa na wafuasi wa Ponda wasimkamate Sheikh wao.
Sheikh huyo alipata huduma ya kwanza mjini humo kabla ya kuletwa Muhimbili, ambapo Polisi walitangaza kumtia mbaroni kisha juzi kusomewa mashtaka akiwa kitandani kabla ya jana kuondolewa kinyemela akiwa bado mgonjwa na kuifanya familia kuiachia Jumuiya ya Kiislam kuamua la kufanya.
Hivyo Waislam kupitia Jumuiya hiyo wameitisha kongamano kubwa litakalofanyika siku ya Jumapili kwenye viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke jijini Dar es Salaam ambapo kutakuwa na ajenda moja tu isemayo 'KWANINI SERIKALI YA CCM IMEMPIGA RISASI SHEIKH PONDA?'
Kongamano hilo pia linatarajiwa kufichua mambo mengine kadhaa dhidi ya dhuluma wanazofanyiwa Waislam wa Tanzania kabla ya kufanyika maandamano makubwa jijini Dar es Salaam na mikoani kupigwa udhalili wanaodaiwa kufanyiwa na serikali ya CCM.
Kwa mujibu wa vipeperushi vilivyosambazwa karibu msikiti yote mikubwa jijini Dar na hasa ile ya harakati imesema kongamano hilo litafanyika kuanzia saa 8 mchana na kuwahimiza waislam popote walipo kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kutoa maamuzi mazito yasiyotarajiwa kwa kilichoelezwa kuchoshwa na unyonge.
Kipeperushi hicho kinasema kuwa Waislam watajitahidi kupambana na hali hiyo ya unyonge kwa gharama yoyote ili amani ya kweli iweze kupatikana.
"Polisi waliotaka kumuua Sheikh Ponda, sasa wanamteka toka Muhimbili hadi Segerea akiwa bado mgonjwa, ili mfumo wa kuwakandamiza Waislam na kuwapendelea Wakristo (Mfumo Kristo) uweze kudumu na waweze kuikalia Zanzibar kinyume na matakwa ya Wazanzibar" Sehemu ya Kipeperushi hicho kinasomeka hivyo.
"Kwamba Wakristo waendelee kupoewa fedha na serikali chini ya Mkataba (MoU), wanedelee kupendelewa Baraza la Mitihani, Waendelee kupata nafasi nyingi za ajira na utawala serikalini, waendelee kuwafanya wasilam kuwa Raia wa daraja la pili, waendelee kuwazuia Waislam kutekeleza dini yao na kuwabana wasijiendeleze, ili waendelee kuwaweka Masheikh magerezani bila ya Haki. Shime Waislam"
Kipeperushi hicho kinaongeza kikionyesha kimetolewa na Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania ambalo Sheikh Ponda Issa Ponda ndiye kiongozi wake.
Katika Wahubiri wa Kiislam wametahadharisha serikali kwa kudai kuwa hata kama itaamua kumdhuru Sheikh Ponda na 'kutowesha' kabisa bado haiwezi kuwarudisha nyuma Waislam kudai haki zao kna kudai njia ya kufanya waislam watulie ni kupewa haki zao na kutendewa usawa kama wenzao wa dini nyingine.
Khatibu aliyehutubia swala ya Ijumaa msikiti Mwenge mchana wa leo, alisema waislam hawawezi kunyamaza kwa kukamatiwa au kudhuriwa kwa viongozi wao kwa madai kuwa Uislam ni dini iliyokamilika na inayoongozwa kwa mujibu wa Qur'an na mafgundisho ya Mtume Muhammad (SAW).
"Yu wapi Mtume na kipenzi cha Mwenyezi Mungu (SW), kuondoka kwake kumeuzima uislam> Hapana, makhalifa na maulamaa wangapi wamepita na uislam umebaki hivyo hivyo na nguvu zake, hivyo hata Ponda akiuwawa na masheikh wengine watafutiliwa mbali bado haiwezi kuuzima Uislam na kuwanyamzisha waislam kulilia na kutetea haki zao," alisema Khatibu huyo.
"Jambo la muhimu kwa serikali itambue na tunajua mpo vibaraka wake humu ndani nendeni mkawaambie mabosi wenu kuwa waislam HATUTANYAMAZA KUDAI HAKI ZETU mpaka iache DHULUMA kwa WAISLAM na UPENDELEO kwa WAKRISTO," alisisitiza.
Kipeperushi cha kongamano hilo la Jumapili litakalofanyika Viwanja vya Mwemba Yanga ni hiki hapa:

Maajabu! Mama ajifungua kichanga na 'chura' huko Chunya

Mtoto aliyezaliwa pamoja na kiumbe cha ajabu kinachofanana na chura
Mtoto akiwa na afya tele
Hiki ndicho kiumbe kilchotoka tumboni pamoja na mtoto mchanga kwa mama Matrida picha hii mara baada ya kutenganishwa na mtoto huyo
Kushoto ni Matrida Erick (20) aliyejifungua mtoto pamoja na kiumbe hicho cha ajabu akiwa na mkunga Agripina Sikanyika aliyembeba mtoto wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kujifungua kwa mkunga huyo
Hapa ndipo  kwa mkunga Agripina Sikanyika Matrida alipojifungulia watoto hao
Mkunga huyo akionyesha mkeka unaotumika kuwatandikia wajawazito wanaokuja kujifungulia katika  kliniki yake

Mkunga akionyesha vibali vinavyothibitisha ruhusa aliopewa na Serikali kwa ajili ya kutoa huduma ya kuwazalisha akina mama wajawazito.

Mwanamke mmoja anayejulikana kwa jina la MATRIDA ERICK  mwenye umri  wa miaka ishirini mkazi wa magamba ,wilaya ya chunya ,amejifungua mtoto jinsi ya kiume na wakati huohuo na chura.

Mkunga aliyemzalisha bi AGGRIPINA SIKANYIKA mkazi wa MBUYUNI wilaya ya chunya amesema tukio hilo limetokea majira ya saa tisa alasiri agosti 13 mwaka huu,mara  mwanamke huyo kufikishwa kwa mkunga huyo na mumewe aitwaye BUNDALA JOSEPHAT ISANDU mwenye umri wa miaka thelathini na tano

MATRIDA amesema huo ni uzao wake wanne  na kwamba alishangazwa na kiumbe hicho ingawa wakati anajifungua hakupata tatizo  lolote na pia alifurahia kupata mtoto wa kiume mwenye afya na alisikitishwa kupata hicho kiumbe ambacho kilikuwa na miguu ya mbele yenye vidole vinne na miguu ya nyuma vidole vitano vya binadamu.

Kwa upande wake AGGRIPINA amesema mtoto alikuwa katika kondo lake na chura alikuwa katika kondo lake la nyuma la uzazi wa mwanamke huyo na pia ameeleza kuwa hilo ni tukio la tatu ambapo la kwanza  mwanamke alijifungua kichwa cha ng’ombe mwaka jana na la pili mwaka huu mwezi wa tano ambapo mwanamke alijifungua chura badala ya binadamu kwa hiyo hili ni tukio la tatu  hivyo hakushangazwa na tukio hilo.

Hata hivyo mume wa Matrida amesema katika familia yao hilo ni tukio la kwanza na kwamba limewashangaza.
Baada ya tukio hilo mkunga alimtafuta mwenyekiti wa kijiji cha MBUYUNI bwana CONRAD WAMBOKA ambaye alimtaarifu mtendaji wa kijiji MICHAEL SANZIMWA ambao walishuhudia tukio hilo na walimwamuru mkunga huyo kuondoa kiumbe hicho ‘’CHURA’’ kwenye kondo la uzazi.

Aidha chura hicho kilikufa na ndugu siku moja baadae ambapo ndugu walikabidhiwa na taratibu za mila zilifuatwa.
Baadhi ya ndugu wamehusisha kitendo hicho na imani za kishirikina zilizokithiri huko wilayani chunya.  

Na Ezekiel Kamanga  Mbeya yetu

Tiketi za Yanga, Azam kuuzwa kesho asubuhi lengo kukwepa 'vishoka'


Na Boniface Wambura
TIKETI  kwa ajili ya mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Yanga na Azam itakayochezwa kesho (Agosti 17 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zitaanza kuuzwa saa 3 asubuhi.

Vituo vitakavyouza tiketi hizo Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala na BMM Barber Shop iliyoko Sinza Madukani.

Katika vituo hivyo tiketi zitauzwa katika magari maalumu. Magari yote yanayouza tiketi yatahamia uwanjani saa 7 kamili mchana.

Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 7,000 kwa viti vya rangi ya kijani na bluu wakati viti vya rangi ya chungwa ni sh. 10,000. Watakaiongia viti vya VIP C watalipa sh. 15,000, viti vya VIP B ni sh. 20,000 wakati VIP A watalipa sh. 30,000.

Ajali tena! Watatu wafa baada ya magari mawili kugongana na Trekta



TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KWA VYOMBO VYA HABARI -AJALI
MNAMO TAREHE 15.08.2013 MAJIRA YA  SAA 20:30HRS HUKO KATIKA KIJIJI CHA CHIMBUYA BARABARA YA  MBEYA/TUNDUMA WILAYA YA  MBOZI MKOA WA MBEYA. GARI T.765 BBA AINA YA  SCANIA LILILOKUWA LIKITOKEA MBEYA MJINI KUELEKEA TUNDUMA LILIENDESHWA NA DEREVA AMBAYE BADO HAJAFAHAMIKA JINA WALA MAKAZI YAKE LILIGONGA  TREKTA AMBALO HALIJAFAHAMIKA NAMBA ZA USAJILI KISHA KULIGONGA GARI ACP 8839 AINA YA  SCANIA  MALI YA  KAMPUNI YA  USAFIRISHAJI YA  DHANDHO LILILOKUWA LIKITOKEA TUNDUMA KUELEKEA MBEYA MJINI DEREVA WA GARI HILO BADO KUFAHAMIKA. KATIKA AJALI HIYO WATU WATATU  WAWILI KATI YAO WALIKUWA KATIKA GARI T.765 BBA NA MMOJA NI DEREVA WA TREKTA  AMBAO HAWAJATAMBULIKA MAJINA WALA MAKAZI YAO,  WOTE WANAUME WALIFARIKI DUNIA PAPO HAPO.  AIDHA WATU WAWILI  WALIOKUWA KATIKA GARI ACP 8839 AMBAO PIA HAWAJATAMBULIKA WALIJERUHIWA NA WAMELAZWA  KATIKA HOSPITALI YA  RUFAA MBEYA.  MIILI YA  MAREHEMU IMEHIFADHIWA KATIKA HOSPITALI YA  SERIKALI VWAWA WILAYA YA  MBOZI. CHANZO CHA AJALI KINACHUNGUZWA. KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA KAMISHNA MSAIDIZI WA POLISI DIWANI ATHUMANI  ANATOA WITO KWA MADEREVA KUWA MAKINI WANAPOTUMIA VYOMBO VYA MOTO KWA KUZINGATIA SHERIA ZA USALAMA BARABARANI ILI KUEPUSHA AJALI ZINAZOWEZA KUEPUKIKA.
 
Mkuu wa wilaya ya Mbozi Dk. Michael Kadeghe akiwa na Mkuu wa Polisi wilaya ya Mbozi Ally Wendo katika eneo la ajali leo asubuhi



Mabaki ya lori
 



Mabaki ya trekta






TFF yamlilia Mtangazaji Radi ABM- Dodoma

Na Boniface Wambura
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha aliyekuwa mwandishi wa habari za michezo wa Radio ABM ya Dodoma, Gracemo Bambaza kilichotokea Agosti 14 mwaka huu katika Hospitali ya Ocean Road, Dar es Salaam.

Msiba huo ni mkubwa katika sekta ya habari na mpira wa miguu kwani Bambaza kwa kipindi chote akiwa mwandishi alikuwa akifanya kazi nasi, hivyo mchango wake katika mpira wa miguu tutaukumbuka daima.

Bambaza aliyezaliwa mwaka 1973 na ambaye pia aliwahi kufanya kazi katika vituo vya redio vya Wapo cha Dar es Salaam na Pride cha Mtwara amesafirishwa jana (Agosti 15 mwaka huu) kwenda Karagwe mkoani Kagera kwa ajili ya mazishi.

TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Bambaza, ABM Radio na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Mungu aiweke roho ya marehemu Bambaza mahali pema peponi. Amina

Dk Mwakyembe azidi kuwasha moto sakata dawa za kulevya, atimua mtandao uliopo JNIA



SOURCE-MTAA KWA MTAA BLOG

Kumekucha Copa Coca Cola, mipira fulana zamwaga kama njugu kwa timu shiriki


SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa shukrani kwa kampuni ya Coca Cola kwa kukabidhi fulana 800 na mipira 100 kwa ajili ya ngazi ya mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 15 ngazi ya mikoa yanayoanza Septemba Mosi mwaka huu.

Coca Cola ndiyo inayodhamini mashindano hayo yaliyoanzia ngazi ya wilaya ambapo mwaka huu yatachezwa kwa kanda na baadaye fainali itakayochezwa kuanzia Septemba 7-14 mwaka huu jijini Dar es Salaam ikishirikisha mikoa 16 itakayokuwa imefanya vizuri katika ngazi ya kanda.
Kila mkoa utapata fulana 25 na mipira mitatu ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya timu zao kwa ajili ya michuano hiyo ngazi ya kanda itakayomazika Septemba 6 mwaka huu.

Kanda hizo ni Mwanza itakayokuwa na timu za mikoa ya Geita, Kagera, Kigoma, Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Tabora. Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Singida inaunda Kanda ya Arusha.

Zanzibar itakuwa na Kaskazini Pemba, Kusini Pemba na mikoa miwili ya Unguja wakati Kanda ya Dar es Salaam ina Ilala, Kinondoni, Lindi, Mtwara, Temeke na mkoa mmoja wa Unguja.

Kanda ya Mbeya inaundwa na Iringa, Katavi, Mbeya, Njombe, Rukwa na Ruvuma wakati Dodoma, Morogoro, Pwani na Tanga zinaunda Kanda ya Morogoro.

Mwanza itatoa timu nne kucheza hatua ya fainali wakati kanda nyingine za Arusha timu mbili, Zanzibar (2), Mbeya (3) na Kanda ya Morogoro itaingiza timu mbili.

Wakati huo huo, semina ya makocha 32 wa timu za mikoa zitakazoshiriki michuano ya U15 FIFA Copa Coca-Cola iliyokuwa ikiendeshwa na mkufunzi Govinder Thondoo kutoka Mauritius inafungwa leo (Agosti 16 mwaka huu) saa 9 alasiri kwenye ukumbi wa Msimbazi Center, Dar es Salaam.

Uchaguzi wa TFF wapigwa 'dochi' sasa kufanyika Okt 27

Na Boniface Wambura
UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF uliokuwa umepangwa siku moja na pambano la watani wa jadi Simba na Yanga, sasa umesogezwa mbele kwa wiki moja na sasa utafanyika Oktoba 26 na 27 mwa huu.
Maamuzi ya kusogezwa mbele kwa uchaguzi huo ambao tangu Desemba mwaka jana umekuwa ukipigwa danadana yaliyotolewa naKamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kuzingatia mamlaka iliyonayo katika kifungu cha 10(6) cha Kanuni za Uchaguzi za TFF na kuusogeza mbele hadi tarehe hiyo mpya.
Sababu za kusogeza mbele uchaguzi ni kutokana na ukweli kuwa Oktoba 20 mwaka huu uongozi wa TFF utakuwa na shughuli nyingi za maandalizi ya mechi ya Simba na Yanga, na hivyo haitawezekana kusimamia shughuli za Mkutano Mkuu wa Uchaguzi kwa wakati mmoja na mchezo huo.
Siku ya mwisho ya kampeni itakuwa Oktoba 25 mwaka huu. Ukiondoa  mabadiliko hayo ya tarehe ya uchaguzi wa viongozi wa TFF, ratiba ya mchakato wa uchaguzi na itabaki kama ilivyotangazwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF katika mkutano wake na waandishi wa habari Agosti 24 mwaka huu.
Pia Kamati imeamua kuwa uchaguzi wa Bodi ya Ligi utabakia kuwa Oktoba 18 mwaka huu kama ilivyopangwa awali.
Kamati imesema inaamini wahusika wote watapokea vizuri mabadiliko hayo na inasikitika kwa usumbufu utakaosababishwa na mabadiliko hayo.

Yanga yaibwaga Simba, TFF yawapa Ngassa lakini yamfungia mechi 6


Mrisho Ngassa aliyeidhinishwa Yanga, lakini atupwa 'kifungoni'
Na Boniface Wambura
KAMATI ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imepitia usajili wa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom na kumuidhinisha Mrisho Ngassa kuchezea timu ya Yanga baada ya kukamilisha usajili wake.

Hata hivyo, Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa imebaini kuwa Ngassa alisaini mkataba mwingine Simba (katika kipindi ambacho alikuwa na mkataba na Azam) ambapo anatakiwa kurejesha fedha alizopokea (sh. milioni 30) pamoja na fidia ya asilimia 50 (sh. milioni 15) ya fedha hizo kwa Simba.

Kamati pia imemfungia mechi sita za mashindano (kuanzia mechi ya Ngao ya Jamii), na anatakiwa awe amelipa fedha hizo ndani ya kipindi hicho cha kukosa mechi hizo. Akishindwa, hataruhusiwa kucheza hadi atakapolipa fedha hizo.

Vilevile Kamati imepitia pingamizi zote zilizowasilishwa kuhusu usajili wa wachezaji, kukatiza mikataba ya wachezaji na kuzitaka klabu husika ziwe zimetatua masuala hayo hadi Alhamisi (Agosti 22 mwaka huu).

Kwa upande wa wachezaji wa kigeni, Kamati imeagiza wasiruhusiwe kucheza hadi watakapopata Hati za Uhamisho wa Kimataifa (ITC) pamoja na vibali vya kufanya kazi nchini (work permits).

Kamati hiyo itakutana tena Ijumaa (Agosti 23 mwaka huu) ili kupata ripoti za pingamizi ilizoagiza ziwe zimefanyiwa kazi hadi Agosti 22 mwaka huu na kutoa uamuzi kwa pande ambazo hazikuafikiana.

Thursday, August 15, 2013

Familia ya Sheikh Ponda yalaani kutolewa kwa sheikh huyoi hospitalini akiendelea na matibabu kupelekwa Segerea

Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda (wa pili kulia), ambaye kwa sasa anakabiliwa na tuhuma za uchochezi,  akitolewa katika taasisi ya mifupa MOI, kuelekea katika gereza la Segerea jijini Dar es Salaam majira ya asubuhi leo. (Na Mpiga Picha Wetu)

DAR ES SALAAM, Tanzania

Kwa upande wao familia ya Sheikh Ponda wamesema wanalaani kitendo kilichofanywa na serikali cha kumuondoa ndugu yao hospitalini huku akiwa anaendelea kupata matibabu.

Msemaji wa familia hiyo Is-haq Rashid, alisema kutokana na hali hiyo kama familia wanalirudisha suala la Sheikh Ponda kwa uongozi wa jumuiya na Taasisi za kiislamu kwa ajili ya hatua zaidi ya kuhakikisha kiongozi mwenzao anakuwa salama.

“Uporaji huu wa mgonjwa unazidi kutupa mashaka juu ya dhamira ya serikali hasa ikiwa tunalituhumu jeshi la polisi katika kumdhuru Sheikh,hatujui kwanini kila wakati wanafanya mambo yao kwa kuvizia kama mwanzonui tuliwaomba viongozi wenzie wawe na subira juu ya yaliyotokea sasa tunaachia hili walizungumzie wao.”alisema Is-haq.


Wakati huo huo taarifa zilizopatikana zinaeleza kuwa viongozi wa jumuiya na taasisi za kiislamu jana walikuwa katika kikao kizito cha kujadili hatua hiyo ya kuporwa kwa Sheikh Ponda akiwa katika matibabu na kwamba leo watakutana na waandishi wa habari kuelezea msimamo wao.

Dk Mwakyembe aanza mambo, Rasta anaswa na dawa za kulevya JNIA




Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe akionesha picha ya kijana Leonard Jeremiah Monyo ( Edwin Jeremiah Monyo) ambaye amekamatwa na kete 86 za madawa ya kulevya aina ya heroine.


Kijana Leonard Jeremiah Monyo ( Edwin Jeremiah Monyo) ambaye amekamatwa na kete 86 za madawa ya kulevya aina ya heroine.


Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe akizungumza na vyombo vya habari leo.
JUHUDI za Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe za kupambana na dawa za kulevya nchini Tanzana zimeanza kuzaa matunda baada ya jana akiwa katika ukaguzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Julius Nyerere kunaswa kijana akijaribu kupita na dawa za kulevya katika uwanja huo.
Kwa kile kuoneshwa kukerwa na tabia hizo, Dk. Mwakyembe amempiga picha kijana huyo ambaye ni rasta na pita yake itasambazwa maeneo tofauti, huku kesi yake ikiendelea ya kupatikana na madawa hayo ya kulevya.
Akizungumza na vyombo vya habari leo ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Dk. Mwakyembe alimtaja kijana aliyekamatwa jana kuwa ni Leonard Jeremia Monyo (Edwin Jeremiah Monyo) ambaye amekamatwa na kete 86 za madawa ya kulevya aina ya heroin akitaka kusafiri nazo kuelekea misokoto ya bangi 34 akiwa ameficha kwenye begi lake.
Alisema kijana huyo rasta alinaswa na mtambo wa kukagua mzigo baada ya wakaguzi kuushuku mzigo wake hivyo kuamuru ukaguliwe ndipo alipokutwa na madawa hayo haramu akijaribu kusafiri nayo kwa ndege.


Baadhi ya wanahabari wakimsikiliza Dk. Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe
Alisema kijana huyo kwa sasa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa uchunguzi zaidi kabla ya kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kukutwa na dawa hizo haramu. Alisema kwa kile kuoneshwa kukerwa na vitendo hivyo na kuamua kwa dhati kupambana navyo wamempiga picha kijana huyo na picha zake zitasambazwa maeneo mbalimbali ili aonekane na umma kujua watua ambao wamekuwa wakilichafua taifa nje na ndani kutokana na biashara hizo haramu.
Dk. Mwakyembe amesema atahakikisha anafuatilia kesi ya kijana huyo hadi itakapoishia ili uona hatua za kisheria zinachukuliwa kwa wahusika na vitendo hivyo kukomeshwa. Alisema maofisa wakaguzi wa mizigo wawili (wote wasichana) ambao walimnasa kijana huyo watazawadiwa na kupandishwa daraja kutokana na kazi nzuri waliyoifanya.
“Jana tu baada ya ukaguzi wenzetu ambao wanaona kama tunafanya mzaha jana tena wakapitisha mzigo wa madawa ya kulevya kiwanja cha ndege cha Dar es Salaam, kwa sababu vijana wetu sasa wameamka na hawataki mchezo wakamkamata kijana huyo…,” alisema.
“Picha yake itasambazwa kila sehemu…sidhani kama tunahitaji upelelezi kwa sababu tumekukamata na dawa za kulevya. Mimi na viongozi wangu kupitisha dawa za kulevya akikisha kuuhakikisha.
Alisema kijana huyo alikamatwa majira ya saa mbili na nusu usiku akiwa anasafiri kwenda nchini Italia kwa kutumia ndege ya kampuni ya Swissair. Alisema kwa sasa kila atakayekamatwa na dawa za kulevya picha yake itasambazwa maeneo mbalimbali ya nchi ili watu hao wajulikane.
Alisema kwa sasa taratibu zinafanywa ili kuhakikisha mizigo ya abiria wanaowasili kutoka nje ya nchi kuingia Tanzania nao mizigo ikaguliwe ili kuwabaini wanaoingiza bidhaa hiyo haramu ichini pia. Aliongeza zoezi hilo litafanyika katika viwanja vya ndege na bandarini kwa kila mizigo inapowasili.
Alisema lengo ni kuhakikisha viwanja vya ndege vinakuwa salama na kuacha kutumika vibaya na baadhi ya watu, jambo ambalo limeendelea kulichafua taifa. Alisem kiwanja cha Dar es Salaam ni kizuri na kina vifaa vya usalama vya kutosha ila mapungufu yaliyopo ni kwa baadhi ya wafanyakazi ambao wanatumia vibaya madaraka yao.
Dk. Mwakyembe ameahidi kuwataja na kuweka picha zao hadharani watu ambao wanajihusisha na madawa hayo ya kulevya. Amesema wanatarajia kutaja majina ya Watanzania ambao hivi karibuni walinaswa na dawa za kulevya nchini Afrika Kusini katika uwanja wa ndege wa Oliver Tambo. Alisema Watanzania wengine wamekamatwa Hong Kong wakihusishwa na dawa hizo na wanafuatilia pia picha na majina yao yatawekwa hadharani muda wowote.

thehabari.com

Wakili Nassoro asikitishwa na kitendo cha Sheikh Ponda kupelekwa Segerea


Picture
Wakili Nassor Jumaa
WAKILI Nassor Jumaa anayesimamia Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda (54) ambaye kwa sasa anakabiliwa na kesi mpya ya kufanya uchochezi katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo hii majira ya saa 7 mchana nje ya viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar  es Salaam amesema kuwa amesikitishwa na hatua  ya vyombo vya dola kumuondoa Sheikh Ponda aliyekuwa amelazwa katika wodi ya Kitengo  cha Taasisi ya Tiba  ya Mifupa  na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (MOI) alikokuwa akipatiwa matibabu na kisha kumhamishia katika gereza la Segerea.

Wakili Jumaa alisema amesikitisha na kitendo hicho kwani muda mfupi baada ya wakili mwandamizi wa serikali Tumaini Kweka kumaliza kumsomea Sheikh Ponda shitaka linalomkabili, Hakimu Hellen Riwa alitoa amri kuwa Sheikh Ponda aendelee kukaa chini ya ulinzi.

Jumaa akasema ameshangazwa kuona leo, wanausalama wamemtoa Sheikh Ponda wodini na kumpeleka katika gereza la Segerea na kwamba atalazimika kurudishwa tena mahakamani siku kesi yake itakapojatwa Agosti 28 mwaka huu, ambapo upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika: “Kwa kweli kitendo hicho kime nisikitisha na kunishitua sana… ila tunatafakari ni hatua gani za kisheria tutazichukua huko siku za usoni,”alisema Jumaa. 
 
(via Habari Mseto)

Hivi ndivyo alivyozikwa Bilionea Erasto Msuya





MAZISHI ya kufuru ya yule bilionea mfanyabiashara wa madini ya tanzanite mkoani hapa, marehemu Erasto Saimon Msuya, yameacha gumzo kubwa.
Mfanyabiashara huyo aliuawa kwa kumiminiwa risasi zaidi ya 20 na watu wawili wasiojulikana Agosti 7, mwaka huu maeneo ya Kia wilayani Hai, Kilimanjaro kabla ya kupumzishwa Jumanne wiki hii kijijini kwao Kairo huko Simanjiro mkoani Manyara
Baada ya kutokea kwa mauaji hayo, iliundwa kamati ya mazishi ikihusisha  wafanyabiashara wa madini ya tanzanite pekee ambayo ilitengeneza bajeti ya maziko ya takribani shilingi milioni 100.
Habari kutoka ndani ya kamati hiyo zilieleza kuwa gari maalum la kifahari na jeneza lililobeba mwili vilinunuliwa Nairobi nchini Kenya
KUHUSU JENEZA
Ilisemekana kuwa jeneza hilo liliagizwa na kampuni inayojishughulisha na shughuli za maziko ya Montezuma & Monalisa Funeral Home.
Ilielezwa kuwa jeneza hilo lilinunuliwa shilingi milioni nane ikidaiwa kuwa lilikuwa lina uwezo wa kufunga na kufunguliwa kwa kutumia ‘rimoti’.
Ilidaiwa kuwa jeneza hilo lilikuwa na vishikio maalum vilivyokuwa viking’aa kama dhahabu au tanzanite na kulifanya kuonekana la aina yake
MSHANGAO
Hali hiyo iliwaacha na mshangao maelfu ya waombolezaji waliofika kuaga mwili wakati wa ibada iliyofanyika nyumbani kwa marehemu, maeneo ya Kwaiddi, barabara inayoelekea Ngaramtoni wilayani Arumeru kabla ya kusafirishwa kwenda Simanjiro kwa maziko.

MAGARI
Pamoja na lile lililobeba mwili wa marehemu, msafara wa magari ya kifahari kuelekea kijijini huko ulisababisha Jiji la Arusha kuzizima kwa majonzi huku wengi wakishindwa kuamini kama jamaa huyo amefariki dunia na kuacha utajiri wa kutisha.
“Hebu ona, hakuna gari la ovyo, yote ni makali. Ingekuwa utajiri unaweza kumfufua mtu, basi Erasto angefufuliwa,” alisema mmoja wa waombolezaji akimwelezea jamaa huyo kuwa alikuwa mtu ‘smati’.

SUTI KUTOKA KWA MALKIA ELIZABETH
Habari za ndani zilidai kuwa hata suti aliyozikwa nayo ilitoka nje ya nchi, London, Uingereza kwa Malkia Elizabeth.
Pia ilidaiwa kuwa jamaa huyo alizikwa na cheni ya dhahabu (gold) shingoni yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 10.

VYAKULA, VINYWAJI
Habari zilinyetisha kuwa huduma kama vyakula, vinywaji, mapambo na magari ya kukodishwa kutoka Arusha kwenda kijijini na kurudi viligharimu zaidi ya shilingi milioni 80
MC NI JB
Ili kuthibitisha kuwa msiba huo haukuwa wa kitoto, Msema Chochote ‘MC’ alikuwa ni staa mkubwa wa filamu za Kibongo, Jacob Steven ‘JB’.

KAIRO, SIMANJIRO
Habari zilidai kuwa waombolezaji walipofika kijijini kwa ajili ya maziko Jumanne mchana, watu walikanyagana makaburini huku vijana wakitaka azikwe na mtu hai wa kumlinda.

KABURI
Walipofika walikuta kaburi la kifahari limeshajengwa ambapo kulikuwa na zulia maalum la kufuta miguu kabla ya kukanyaga marumaru za madini ya tanzanite zilizolizunguka.
Kuthibitisha kuwa ilikuwa ni kufuru, baadhi ya wachimbaji wadogo ‘nyoka’ walikuwa wakiwataka matajiri kulifungia kaburi hilo umeme na kiyoyozi.

MNARA WA KUMBUKUMBU
Baada ya mazishi hayo, inaelezwa kuwa familia ilikubaliana kufanya juu chini kulinunua shamba alilouliwa katika Mji wa Bomang’ombe, Mtaa wa Wasomali eneo la Mjohoroni wilayani Hai, Kilimanjaro ili kujenga mnara wa kumbukumbu.
Ilidaiwa kuwa baada ya kujenga mnara huo, familia itakuwa inatembelea eneo hilo Agosti 7, kila mwaka kwa ajili ya tambiko.

KAKA WA MAREHEMU
Kaka wa marehemu, Israel Msuya, alisema kuwa walifikia uamuzi wa kufanya mazishi hayo kwenye makaburi ya familia ya mzee Elisaria Msuya ‘Kikaango’ ambaye ni baba wa marehemu Erasto.
KUNA KULIPIZA KISASI?
Kwa mujibu wa kaka huyo wa marehemu, familia haitalipiza kisasi kwa watu waliomuua Erasto bali wao wanamwachia yote Mungu.

VIPI KUHUSU KESI?
Katika hatua nyingine, polisi mkoani hapa wanaendelea kuwahoji wafanyabiashara maarufu wa madini ya tanzanite wa mji mdogo wa Mererani wanaodaiwa kuhusika na kifo hicho.
Habari za kipolisi zilieleza kuwa mfanyabiashara mmoja wa madini, kijana ambaye aliibuka ghafla kuwa tajiri mkubwa kutokana na biashara ya madini ya tanzanite, anashikiliwa kwa mahojiano.
               
Chanzo:GlobalPublishers

Timu ya Taifa ya Ngumi yakumbukwa kumwagiwa vifaa, fedha kesho Dar



TIMU ya taifa ya mchezo wa Ngumi iliyopo kambini ikijiandaa na ushiriki wa michuano ya kimataifa inatarajiwa kukabidhiwa vifaa vya michezo na nauli kwa wachezaji tuko litakalofanyika mchana wa leo jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT) vifaa na fedha hizo zinatolewa na Mkurugenzi wa  Shule za St Mary na Hoteli ya Kitalii iliyopo Bagamoyo, Rutta Rwakatare na ifanyika kwenye ofisi za BFT, jijini Dar.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga, inasema hafla hiyo itafanyika saa 6;30 ikiw na lengo la kuisaidia kamb ya mazoezi ya timu hiyo ambao inajiandaa na michuano ya Afrika itakayofanyika mezi ujao nchini Mauritius.
Uongozi wa BFT umedai umefurahishwa na kitendo hicho kinachotarajiwa kufanyika leo ukiwa umekuja wakati muafaka wakati timu hiyo ikihitaji msaada kwa sasa kwa maandalizi ya michuano hiyo na le ya mwakani ya Jumuiya ya Madola.
BFT ikatoa wito kwa wadau wengine wa michezo kujiokeza kuisaidia timu hiyo kwa madai ina hali mbaya kifedha.
"BFT tumefurahishwa mno na mwitikio wa Mkurugenzi huyo kwa kusikia na kuguswa kuhusu timu ya taifa ya ngumi na BFT, tunawaomba watanzania wengine wajitokeze zaidi kusaidia timu yetu ya taifa ili uwakilishi katika mashindano ya kimataifa uwe na tija," taarifa hiyo ya BFT inasomeka hivyo.
Pia BFT imeviomba vyombo mbalimbali vya habari kujitokeza kuhamasisha ili watanzania wengine kujitokeza kuendelea kusaida zaidi kwa madai msaada unahitajika wa vifaa vya mazoezi, matibabu, chakula, maji,nauli, nguo za mazoezi na posho za wachezaji.