STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, May 8, 2014

Real Madrid yajiweka pabaya Hispania, Ronaldo shakani

KLABU ya Real Madrid imejiweka katika nafasi finyu ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Hispania baada ya usiku wa kuamkia leo kulazimishwa sare ya 1-1 na timu ya Real Vallodolid.
Sare hiyo imeifanya timu hiyo kucheza mechi 36 na kufikisha pointi 84, nne zaidi ya vinara wa ligi hiyo Atletico Madrid ambao watakutana nao kwenye mechi ya Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya itakayochezwa mjini Lisbon Ureno, Mei 24.
Atletico wana pointi 88 tatu zaidi na ilizonazo watetezi Barcelona huku ligi ikisaliwa na raundi tatu kabla ya kukamilishwa kwa msimu huu.
Wageni, Real Madrid walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa beki wake, Sergio Ramos katika dakika ya 35 kabla ya Humberto Osorio kusawazisha dakika tano kabla ya pambano hilo kumalizika na kuzifanya timu hizo kugawana pointi moja moja.
Katika pambano hilo nyota wa Real, Cristiano Ronaldo alitolewa uwanjani huku ikielezwa kuwa alichezeshwa akiwa na maumivu ya nyama ya paja  na kuifanya klabu hiyo kuingiwa na hofu ya kumkosa kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa.

Newz Alert! Gari la magazeti ya Mwananchi lapata ajali na kuua mkoa wa Mara


"Gari la kusambaza Magazeti ya Kampuni ya Mwananchi limegonga na kuua katika daraja la Kirumi mpakani mwa wilaya ya Rorya na Butiama Mkoani Mara leo asubuhi.(Picha zote na mdau wetu Augustine Mgendi)

Said Ndemla awatuliza Simba, adai yupo sana Msimbazi

KIUNGO nyota chipukizi wa Simba, Said Ndemla amezitahadharisha klabu ambazo zinamnyemelea kutopoteza muda wao kwa vile hana mpango wa kutimka klabuni hapo.
Akizungumza na MICHARAZO, Ndemla alisema bado yupo sana Msimbazi, klabu iliyosaidia kukuza kipaji chake.
Ndemla anayemudu nafasi zote za kati, alisema kwa sasa akili yake ni kujipanga kwa msimu ujao kuhakikisha Simba inakuwa na mafanikio makubwa baada ya msimu huu kupepesuka na kumaliza kwenye nafasi ya nne baada ya kipindi kirefu.
"Bado nipo sana Msimbazi, wanaonimezea mate wasipoteze muda wao kwani sina mpango wowote wa kiondoka kwa sasa Simba, nafikiria jinsi ya kuisaidia kwa msimu ujao ili turejeshe heshima mjini," alisema.
Kiungo huyo aliyejijengea jina kubwa hasa katika pambano la watani wa jadi la duru la kwanza lililoisha kwa sare ya 3-3 baada ya kuingia dimbani na kufanikiwa kubadilisha matokeo ya timu yake kulala mabao 3-0 na kumaliza kwa sare.
Ndemla na William Lucian 'Gallas' waliingizwa dimbani kipindi cha pili kuchukua nafasi za Abdulhalim Humud 'Gaucho' na Haruna Chanongo na kufanikiwa kuwadhibiti Yanga na kurudisha maabao matatu kupitia kwa Joseph Owino, Gilbert Kaze na Betram Mombeki.
Kauli ya Ndemla ya kudai ataendelea kusalia Simba imekuwa kukiwa na tetesi kwamba kiungo huyo anatolewa macho na baadhi ya klabu za Ligi Kuu kwa ajili ya kunasa saini yake ili kuzichezea msimu ujao.

Jerry Santo ndiyo basi tena Coastal Union

NAHODHA wa zamani wa klabu ya Coastal Union. Mkenya  Jerry Santo amewaaga mashabiki wa timu hiyo kwa kuweka bayana kuwa, hatakuwa na kikosi hicho kwa msimu ujao.
Kiungo mkabaji huyo aliyewahi kung'ara Simba kabla ya kutua Coastal, aliiambia MICHARAZO kuwa, ameachana na klabu hiyo baada ya kumalizika kwa mkataba wake.
Santo alisema kwa sasa amerejea nchini kwao Kenya akifanya mipango ya kujiunga na klabu nyingine kwa msimu ujao iwe ndani au nje ya nchi yao.
Mkenya huyo, aliyekuwa mmoja wa wafungaji wa mabao ya Coastal katika misimu miwili ya timu hiyo kwenye Ligi Kuu, alisema ni mapema mno kusema kama atarejea Tanzania.
"Sintakuwa na Coastal kwa msimu ujao, naendelea kutafuta timu ya kuichezea iwe hapa Kenya au nje ya nchi, sidhani kama nitarejea Tanzania, ngoja tuone," alisema.
Nyota huyo aliyekuwa akiichezea Tusker ya Kenya kabla ya kuja nchini kuichezea Simba, alipoteza cheo chake cha unahodha katika duru la pili kwa beki Juma Said 'Nyosso.
Badiliko hilo lilifanywa na kocha Mkenya, Yusuph Chipo aliyeichukua timu hiyo mikononi mwa Hemed Morocco.

Rose Ndauka, Wastara Juma, Lulu kuchuana kwenye tuzo

Riyama
Rose Ndauka

WAIGIZAJI wa kike nyota wa filamu nchini, Rose Ndauka, Wastara Juma, Elizabeth Michael 'Lulu' na Irene Paul ni kati ya waigizaji wanaowania Tuzo za Filamu za ACVC-2014.
Wasanii hao wanachuana kwenye kipengele cha Msanii Bora wa Kike wakiwa sambamba na waigizaji, Jacklyne Wolper, Irene Uwoya na Riyama Ally.
Kwa mujibu wa waratibu wa tuzo hizo, Ndauka kaingia kwenye kipengele hicho kupitia filamu ya Waiting Soul, Irene Paul (Love& Power), Irene Uwoya (Questions Mark), Lulu (Foolish Age), Wolper (Mahaba Niue), huku Wastara (Mr Mres Sajuki) na Riyama ( The Dream).
Kwa upande wa Msanii Bora wa Kiume tuzo hiyo inawaniwa na Jacob Stephen 'JB', Mohammed Mwikongi 'Frank', Simon Mwampagata 'Rado',Hemed Suleiman 'PHD', Steve Mengere 'Nyerere' na
Salim Ahmed 'Gabo'.
Upande wa vunja mbavu (Comedian) wapo King Majuto, Mboto, Dk Cheni, Kitale na Marehemu Sharo Milionea huku wachekeshaji wa kike tuzo hiyo inawaniwa na Salma Jabu 'Nisha'
Rehema Abdallah 'Bi Rehema' na Chuma Suleiman 'Bi Chau'.
Tuzo nyingine zinazowaniwa na  Wasanii Bora Chipukizi wa Kiume na Kike ambazo zitawaniwa na
Rammy Gallis, Mohammed Mussa, Gerry wa Rhymes, Lukeye Lukamo, Mteme Baga, Wellu Sengo, Janeth Lameck, Najma Dattan, Gertrude Mwita na Khadija Kopa.
Vincent Kigosi 'Ray', Issa Mussa 'Claud 112', John Lister, Jackson Kabirigi, Leah Richard 'Lamata' na Kulwa Kikumba 'Dude' wanawania tuzo ya Muongozaji Bora, huku Filamu Bora inawania na filamu za
Twisted ya RJ Production, Nguvu ya Imani-Timamu Effects, Shikamoo Mzee-Jerusalem Film Production, Tikisa-Nisha Production na Mr & Mrs Sajuki ya Wajey Film Production.
Tuzo nyingine zinazowaniwa ni ya Mhariri Bora wa Filamu, Muigizaji Msaidizi Bora wa Kike na Kiume, Filamu Bora ya Maadili, Filamu Bora ya Kuitangaza Tanzania, Wasambazaji Bora na zoezi la upigaji kura kwa washiriki hao litahusishwa 'code' za kila kipengele na kutumwa katika namba 15678.

PSG yatetea taji Ufaransa licha ya kipigo nyubani

Wanafurahia ubingwa kinyonge
LICHA ya kipigo cha mabao 2-1 ilichopewa nyumbani kwake na Rennes, klabu ya Paris Saint-Germain (PSG) imefanikiwa kutangazwa kuwa mabingwa tena nchini Ufaransa, baada ya wapinzani wao wa karibu Monaco kulazimishwa sare ya 1-1 na timu inayopigana kushuka daraja la Guingamp.
Kipigo hicho kimeifanya PSG kusaliwa na pointi zao 83 ambazo haziwezi kufikiwa na Monaco kwani kwa sare hiyo imewafanya wafikishe pointi 76 na kusaliwa na mechi mbili ambazo wakishinda zote watafikisha pointi 82 tu.
PSG imetetea taji hilo iliyokuwa ikilishikilia na ni ubingwa wake wa pili msimu huu baada ya hivi karibuni kunyakua Kombe la Ligi kwa kuicharaza Olympique Lyon kwa mabao Edinson Cavani waliposhinda mabao 2-1.
Wenyeji PSG walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Ezequiel Lavezzi katika dakika ya tatu akimalizia kazi nzuri ya Cavani, kabla ya wageni kucharuka na kurejesha bao hilo dakika ya 23 kupitia kwa Foued Kadir na  Paul Ntep kufunga la ushindi dakika nne baadaye.

Brazili yaanika kikosi chake, Kaka, Robinho, Coutinho watemwa

KOCHA wa timu ya taifa ya Brazil, Luis Felipe Scolari amebainisha kuwa ilikuwa kazi rahisi kuchagua kikosi chake kwa ajili ya Kombe la Dunia baada ya kutangaza majina ya wachezaji 23.
Kocha huyo amewatema mastaa kibao wa taifa hilo katika kikosi alichotangaza baadhi yao wakiwa ni Kaka, Robinho na Lucas Moura.
Pia nyota wa Atletico Madrid Filipe Luis na Miranda pia hawapo, sambamba na mchezaji wa Bayern Munich Rafinha na kiungo wa Liverpool Philippe Coutinho. 
Scolari ambaye aliiongoza Brazil kushinda Kombe la Dunia mwaka 2002 amesema ilikuwa vigumu kufanya kazi kama hiyo miaka 12 iliyopita kuliko ilivyo sasa, na kudai kuwa kutakuwa na baadhi ya wachezaji hawatafurahishwa kwa majina yao kukatwa. 
Kocha huyo amesema ilikuwa kazi ngumu mwaka 2002 kutangaza kikosi kwasababu kulikuwa na kelele nyingi sana mpaka ikabidi abadilishe hoteli ambayo hakuna mtu aliyekuwa akifahamu lakini safari haikuwa hivyo. 
Brazil inatarajia kuanza kampeni zake kwa kucheza mchezo wa fungua dimba dhidi ya Croatia Juni 12 mwaka huu kabla ya kuzivaa Mexico na Cameroon zilizopo katika kundi A.

Kikosi kamili cha Brazil ni hiki hapa:

Makipa: Jefferson (Botafogo), Julio Cesar (Toronto FC), Victor (Atletico MG).

Mabeki: Dante (Bayern Munich) David Luiz (Chelsea), Henrique (Napoli), Thiago Silva (PSG) Dani Alves (Barcelona), Maicon (Roma) Marcelo (Real Madrid), Maxwell (PSG).

Viungo: Fernandinho (Manchester City) Hernanes (Inter) Luiz Gustavo (Wolfsburg) Oscar (Chelsea) Paulinho (Tottenham Hotspur), Ramires (Chelsea), Willian (Chelsea).

Washambuliaji: Bernard (Shakhtar Donetsk), Fred (Fluminense) Hulk (Zenit) Jo (Atletico MG), Neymar (Barcelona).