STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, December 19, 2012

Pacha wa Dotnata aja na mpya

Dometria Alphonce 'DD' katika pozi


MUIGIZAJI wa filamu ambaye ni pacha wa nyota wa fani hiyo na muziki, Husna Posh 'Dotnata', Dometria Alphonce 'DD', amepakua filamu mpya iitwayo 'Kua Uyaone' ambayo inasimulia mkasa wa kweli uliowahi kumpata katika maisha yake ya ndoa.
DD, aliiambia MICHARAZO juzi kuwa filamu hiyo imeshakamilika na wakati wowote itaachiwa hadharani, ikiwa imemshirikisha yeye mwenyewe na wasanii wengine waliopo katika kikundi chake cha sanaa cha DD Films kilichopo Ukonga.
Msanii huyo ambaye pia anajihusisha na nyimbo za Injili akishirikiana na pacha wake wakiandaa albamu kwa sasa, alisema hiyo itakuwa filamu yake ya kwanza kuitunga na kuiandaa mwenyewe baada ya kushirikishwa kazi kadhaa siku za nyuma.
'Nimekamilisha filamu yangu mpya iliyojikita kwenye simulizi la kweli ambao limewahi kunitokea katika maisha yangu ya ndoa, nimecheza na wasanii mbalimbali baadhi wakiwa ni askari waliopo katika kikundi changu cha sanaa cha DD Films," alisema.
Alisema filamu hiyo ni maalum kwa wanawake wote waliowahi kukutwa na misukosuko katika maisha ya ndoa zao, kwani mbali na mikasa ya kusisimua, lakini pia inatoa suluhu ya nini kifanyike mtu anapokumbwa na misukosuko kama hiyo.
Msanii huyo ambaye kama pacha wake naye ni mjasiriamali, alisema filamu hiyo ni yenye kuwatia nguvu na ujasiri wanawake wote wanaoteseka katika ndoa zao.
Aliongeza kuwa, wakati filamu hiyo ikiwa katika harakati ya kutolewa hadharani pia tayari anaendelea kuandaa kazi nyingine ambayo hakupenda kuitaja, ingawa alidai imeshaanza kufanyiwa 'shutingi'.

Mwisho

After Death sasa Kanumba Day

Jacklyne Wolper na 'watoto wa Kanumba'
Leah Richard 'Lamata'



FILAMU mpya ya kumuenzi aliyekuwa nyota wa zamani wa filamu nchini, marehemu Steven Kanumba iitwayo 'After Death', inatarajiwa kuzinduliwa rasmi siku ya kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu msanii huyo alipofariki dunia Aprili 7.
Mmoja wa waratibu wa filamu hiyo, Leah Richard 'Lamata' alisema wameamua kuupeleka uzinduzi huo Aprili 7 mwakani, ili kuleta maana halisi ya kumuenzi nyota huyo aliyefariki ghafla nyumbani baada ya kutokea mzozo na mpenziwe.
Lamata, ambaye ndiye muongozaji wa filamu hiyo iliyotungwa na Jacklyne Wolper, alisema awali walipanga wafanye uzinduzi huo Februari, lakini wakaona isingeleta maana ilihali Kanumba alifariki mwezi Aprili na hivyo wamepeleka hadi tarehe hiyo.
"Uzinduzi wa filamu maalum ya kumuenzi Kanumba, iitwayo 'After Death' ambayo tulipanga kuizindua Februari sasa itazinduliwa Aprili 7, ambayo itakuwa siku ya kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu msanii huyo alipofariki," alisema Lamata.
Lamata mmoja wa waongozaji mahiri wa filamu nchini, alisema anaamini siku hiyo itawapa fursa nzuri mashabiki wa filamu hasa waliomzimia Kanumba kumuenzi na kushuhudia baadhi ya kazi za mkali huyo.
Alisema After Death, iliyoigizwa na karibu wasanii wote waliowahi kufanya kazi na Kanumba, itawarejeshea kumbukumbu mashabiki wa filamu kutokana na msanii Philemon Lutwaza 'Uncle D' kucheza nafasi ya nyota huyo aliyefanana naye.
Wengine walioshiriki filamu hiyo ni Mayasa Mrisho, Jacklyne Wolper, Patcho Mwamba, Ben Blanco, Irene Paul, Ruth Suka 'Mainda' na watoto walioibuliwa na marehemu Kanumba kupitia 'This is It' na 'Uncle JJ' Patrick na Jennifa.

Mabingwa wa Afrika, Zambia kutua ncnhini leo




Kikosi cha timu ya taifa ya Zambia
MABINGWA wa kandanda barani Afrika, Zambia ‘Chipolopolo’ wakiwa na msafara wa watu 32 wanatarajiwa kuwasili nchini leo tayari kwa pambano lao la kujipima nguvu dhidi ya Tanzania, Taifa Stars.
Timu hiyo itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 11 kamili jioni kwa ndege ya PrecisionAir ikitokea Lusaka.
Mbali ya wachezaji 24, msafara wa Zambia ambayo inakuja nchini kwa ajili ya mechi dhidi ya Taifa Stars utakuwa na maofisa wengine wanane wakiwemo wa benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Herve Renard aliyeipa timu hiyo ubingwa wa Afrika mwaka jana nchini Gabon.
Wachezaji kwenye msafara huo ni Chintu Kampamba, Chisamba Lungu, Christopher Katongo, Danny Munyau, Davy Kaumbwa, Derrick Mwansa, Evans Kangwa, Felix Katongo na Francis Kasonde.
Given Singuluma, Hichani Himonde, Isaac Chansa, James Chamanga, Jimmy Chisenga, Jonas Sakuwaha, Joshua Titima, Kalililo Kakonje, Moses Phiri, Mukuka Mulenga, Rainford Kalaba, Rodrick Kabwe, Salulani Phiri, Shadrack Malambo na Stoppila Sunzu.
Mechi dhidi ya Taifa Stars itafanyika Jumamosi (Desemba 22 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni. Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iko kambini jijini Dar es Salaam tangu Desemba 12 mwaka huu chini ya Kocha Kim Poulsen kujiandaa kwa mechi hiyo.
Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, sh. 7,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C, sh. 20,000 kwa VIP B wakati VIP A itakuwa sh. 30,000.
Tiketi zinatarajiwa kuanza kuuzwa siku moja kabla ya mechi katika vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Uwanja wa Uhuru, Mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa Ohio na Samora, Sokoni Kariakoo, kituo cha mafuta cha Ubungo OilCom na Dar Live Mbagala.
Pia tiketi zitauzwa Ijumaa (Desemba 21 mwaka huu) kwenye tamasha la Kilimanjaro Premium Lager kuhamasisha washabiki wa Taifa Stars litakalofanyika kwenye viwanja vya Sigara, Chang’ombe.

Kikosi cha Zambia kilipokuwa kikishiriki michuano ya AFCON 2012

Maugo, Mbwana wawapania waganda


Kocha wa ngumi Pascal Mhagama kushoto anaemfua bondia Mbwana Matumla kwa ajili ya mpambano wake na David Chalanga wa kenya mpambano utakaochezwa Desemba 25 katika ukumbi wa Dar Live picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com
Bondia Mbwana Matumla kushoto akionesha ufundi wa kutupa masumbwi mbele ya kocha wake Pascal Mhagama kwa ajili ya mpambano wake na David Chalanga wa kenya mpambano utakaochezwa Desemba 25 katika ukumbi wa Dar Live picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com
Bondia Mada MAUGO AKILUKA KAMBA KWA AJILI YA MAANDALIZI YA MPAMBANO WAKE NAbondia Yiga Juma wa Uganda mpambano utakaofanyika Desemba 25 katika ukumbi wa Dar Live jijini Dar es salaam picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com
Kocha wa Mchezo wa Masumbwi Said Chaku kushoto akimwelekeza bondia Mada Maugo jinsi ya kutupa Ngumi wakati wa mazoezi yake ya mwisho kwa ajili ya kumkabili bondia Yiga Juma wa Uganda mpambano utakaofanyika Desemba 25 katika ukumbi wa Dar Live jijini Dar es salaam picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com
Bondia Mada Maugo kushoto akionesha umaili wa kutupa makonde na kocha wake Said Chaku wakati wa mazoezi yake ya mwisho kabla ya kupambana na bondia Yiga Juma wa Uganda Desemba 25 katika ukumbi wa Dar Live jijini Dar es salaam Picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com

Kamote kurudiana na Mmalawi Des 29

Kamote akiwa na mataji anayoyashikilia kwa sasa

BONDIA mtanzania ambaye ni bingwa wa Dunia anayetambuliwa na World Boxing Forum, Allan Kamote anatarajiwa kwenda nchini Malawi ili kuzichapa na mwenyeji wake, Osgood Kayuni katika pambano litakalofanyika wiki ijayo.
Kamote aliyetwaa taji hilo la WBF Septemba 28 mwaka huu kwa kumpiga kwa TKO, Mmalawi Wellington Balakasi, atazichapa na Kayuni katika pambano la uzani wa Light raundi 10 litakalofanyika mjini Blantyre siku ya Desemba 29.
Hilo litakuwa pambano la marudiano baina ya mabondia hao kwani Februari mwaka huu walizichapa nchini huo na Kamote kupigwa kwa pointi, kitu "Natarajia kuondoka nchini siku ya Alhamisi kwenda Malawi kupigana na bondia aitwae Osgood Kayuni, ambayo nilipigana naye Februari mwaka huu na kunishinda kwa pointi, sidhani kama nitarudia tena makosa," alisema.
Kamote anayetokea mkoa wa Tanga, alisema anaendelea vema kujiandaa na pambano hilo na ana imani kubwa kurudia kile alichokifanya kwa Balakasi aliyempiga kwa TKO ya raundi ya nne na kutwaa ubingwa huo wa WBF.

Mwisho

Nusu fainali Kawambwa Cup kuanza kesho


NUSU fainali za michuano ya Kombe la Kawambwa inayoshirikisha timu za soka za Jimbo la Bagamoyo, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi keshokuwa ambao timu nne zilizotiunga hatua hiyo zitachuana kuwania kucheza fainali.
Kwa mujibu wa msemaji wa michuano hiyo inayodhaminia na Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo ambaye pia ni Waziri wa Elimu na Ufundi Stadi, Dk Shukuru Kawambwa, Masau Bwire, timu zilizofuzu hatua hiyo ni pamoja na Beach Boys, Mataya Fc, Chaulu na Matimbwa.
Masau alisema timu hizo zilizofua hatua ya roboi fainali iliyochezwa katika vituo viwili, zitaanza kupepetana katika  nusu fainali zitakazoanza kesho Alhamis kwa pambamo kati ya Chaulu Fc dhidi ya Mataya Fc.
"Nusu fainali ya pili itachezwa siku inayofuata yaani Ijumaa Desemba 21 kwa kuzikutanisha Beach Boys dhidi ya Matimbwa Fc, mechi zote zitachezwa katika uwanja wa Mwanakalenge na fainali itakuwa Jumapili," alisema Bwire.
Bwire alisema katika fainali hiyo, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Dk. Kawambwa ambaye atakabidhi kombe na zawadi nyingine kwea bingwa na washindi wengine wa michuano hiyo.
Msemaji huyo alisema michuano hiyo iliyoanza Septemba 25 mwaka huu ikishirikisha jumla ya timu 84 kutoka kata saba zilizopo jimbo la Bagamyoto za Dunda, Magomeni, Kiromo, Zinga, Kerege, Yombo na Vigwaza iliandaliwa na Waziri huyo kwa lengo la kuibua na kuendeleza vipaji vya soka ndani ya jimbo hilo na mkoa mzima wa Pwani.

Mwisho

Cheka, Mmalawi kuzipiga Boxing Day

Bondia Francis Cheka 'SMG'


BONDIA Francis Cheka 'SMG' ametamba kuwa yupo fiti tayari kwa pambano lake la kimataifa dhidi ya Mmalawi, Chiotcha Chimwemwe watakaovaana naye siku ya Boxing Day kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
Cheka atakayevaana na Chimwemwe katika pambano hilo la raundi 12 uzani wa Super Middle, alisema maandalizi aliyofanya kwa ajili ya mchezo huo yanampa imani ya kufanya vema kwa kumnyuka mpinzani wake.
"Nimejiandaa vya kutosha kuweza kufanya vema katika pambano lao dhidi ya Mmalawi litakalochezwa jijini Arusha, nawaahidi mashabiki wangu sintawangusha kwani kocha wangu Abdallah Saleh 'Komando' amenifua vya kutosha," alisema Cheka.
Naye mraribu wa pambano hilo litakalokuwa la kwanza kufanyika Arusha tangu mji uwe uwe jiji, Andrew George, alisema maandalizi ya mchezo huo utakaosindikizwa na mapambano ya mabondia wa miji ya Arusha na Moshi yamekamilika.
"Maandalizi yote ya pambano hilo yamekamilia kwa asilimia zote ikiwa ni pamoja na kumtumia tiketi bondia huyo wa Malawi," alisema George.
George alisema aliamua kulipeleka pambano hilo jijini humo kwa lengo la kuwapa burudani mashabiki wa mchezo wa ngumi wa mji huo sambamba na kuwapa fursa wakazi wa Arusha kuisherehekea vema sikukuu ya Krismasi.
Mratibu huyo alisema Cheka na Chimwemwe pamoja na mabondia watakaosindikiza pambano hilo watapimwa uzitoi na afya zao siku ya Krismasi tayari kupanda ulingoni Desemba 26.

Mwisho

Msondo, Sikinde kupambana Krismasi Equator Grill

Waimbaji wa Msondo Ngoma Eddo Sanga na Juma Katundu wakiwajibika jukwaani

Baadhi ya wanamuziki wa Mlimani Park 'Sikinde'
 
BAADA ya kila moja kupewa vyombo vipya na Konyagi, bendi pinzani za Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki'  na  Mlimani Park Orchestra 'Sikinde Ngoma ya Ukae' zitapambana siku ya Krismasi katika ukumbi wa Equator Grill, Temeke.
Mpambano huo umeandaliwa na kampuni za Bob Entertainment na Keen Arts na kudhaminiwa na kinywaji cha Konyagi.
Mratibu wa mchuano huo Joseph Kapinga amesema pambano hilo litakuwa la kusherekea sikukuu ya Krismasi na kufunga mwaka 2012.
Kapinga alisema kuwa pia pambano hilo litaamua ni bendi gani bora kati ya magwiji hao wawili wa muziki wa dansi nchini kwa mwaka 2012.
Mratibu huyo alisema bendi hizo zitapiga jukuwaa moja lakini kila moja atatumia vyombo vyake ili kuondoa malamiko ya kuhujumiwa. Kila bendi itatumia muda wa saa moja kabla ya nyingine kupanda jukwani.
“Litakuwa pambano la aina yake ukizingatia kuwa hii itakuwa ni mara ya pili kwa bendi hizo kupambana siku ya Krismasi tangu zianzishwe. Mwaka jana zilipambana katika TCC Club Chang’ombe,” alisema Kapinga.
Alisema mchuano huo itaanza saa tisa alasiri hadi liamba.
 
 

Tuesday, December 11, 2012

Linah: 'Napenda kubambiwa na mashabiki'







Linah Sanga katika mwonekano wa picha tofauti.
 
Na Kambi Mbwana, Handeni
MWIMBAJI wa  muziki wa kizazi kipya hapa nchini, Linah Sanga, maarufu kama Lina, amesema huwa haogopi kubambiwa na mashabiki wake, ndio maana amekuwa mwepesi kuwahitaji kila anavyofanya shoo zake.

Linah aliyeibukia katika taasisi ya kukuza na kulea vipaji ya Tanzania House of Talents (THT), ni miongoni mwa  wasanii wanaofanya vyema mno katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya nchini.
 

Akizungumza na Handeni Kwetu, Linah alisema kwamba anapenda kucheza na mashabiki wake kila anavyoona inafaa, hivyo anaamini aina hiyo itaendelea kwa ajili ya kujipa amani na kuwapa fursa mashabiki wake kucheza nae jukwaani.

Alisema katika maeneo mengi, hasa kwa kuangalia amani, amekuwa akihitaji mmoja wao kwa ajili ya kuacha amani na heshima kwa mashabiki wake, hivyo lengo lake haliwezi kusitishwa na woga wa kucheza, au kubambiwa na mashabiki wake.

"Huwa napenda sana kucheza na shabiki wangu katika shoo ninazofanya, hivyo siogopi kubambiwa, ingawa najua watu ukiwapa nafasi hiyo wanakuja jukwaani na kucheza kwa fujo hasa wale wanaowakamia wasanii.

"Nafanya hivyo kwakuwa sina woga na ndio maana mashabiki wangu nawaacha katika furaha kwa kushangilia, hivyo kwakweli hili ni lengo langu zaidi, ili mradi tu kuwe na amani kwa kuimarishwa ulinzi, hasa katika shoo kubwa.

Linah amewahi kutamba na nyimbo mbalimbali, ukiwamo ule wa ‘Atatamani’, uliomuweka juu na kumpatia mashabiki lukuki.

NMB YAKABIDHI MADAWATI SHULE YA MSINGI VICTORIA


Meneja wa benki ya NMB tawi la NMB House Bi. Benedictor Byabyato (kulia) akikabidhi madawati 25 yenye thamani ya shilingi milioni 5 kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Victoria Bw. Sufini Mbwambo iliyopo Dar es Salaam wiki iliyopita.Aanayeshuhudia tukio hilo ni Afisa wa tawi la NMB House Jane Mubezina pamoja na mmoja wa maafisa wa Elimu.
 
Meneja wa tawi la NMB House  Bi. Benedictor Byabyato (kulia) akiwa pamoja na baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Victoria pamoja na Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bw. Sufini Mbwambo (kulia) wakati wa makabidhiano ya madati yenye thamani ya shilingi milioni 5, jijini Dar es Salaam.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Victoria wakiimba nyimbo kushukuru benki ya NMB kwa msaada wa madawati waliyotoa shuleni hapo

NMB YAKABIDHI MADAWATI SHULE YA MSINGI VICTORIA


Meneja wa benki ya NMB tawi la NMB House Bi. Benedictor Byabyato (kulia) akikabidhi madawati 25 yenye thamani ya shilingi milioni 5 kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Victoria Bw. Sufini Mbwambo iliyopo Dar es Salaam wiki iliyopita.Aanayeshuhudia tukio hilo ni Afisa wa tawi la NMB House Jane Mubezina pamoja na mmoja wa maafisa wa Elimu.
 
Meneja wa tawi la NMB House  Bi. Benedictor Byabyato (kulia) akiwa pamoja na baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Victoria pamoja na Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bw. Sufini Mbwambo (kulia) wakati wa makabidhiano ya madati yenye thamani ya shilingi milioni 5, jijini Dar es Salaam.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Victoria wakiimba nyimbo kushukuru benki ya NMB kwa msaada wa madawati waliyotoa shuleni hapo

JOKHA KASSIM Mwimbaji wa taarabu anayetamba na T-Moto


Jokha Kassim
 
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UKIPATA bahati ya kuusikia wimbo wa Riziki Mafungu Saba, hakika utaanza kuupenda muziki wa taarabu, hata kama awali hujaupenda.
 
Ni wimbo mzuri. Wenye mashairi mazito na yenye ujumbe murua, unaoelezea jinsi riziki zinavyopangwa na Mungu na wala sio binadamu, wakiwamo wenye roho mbaya.
 
Wimbo huo umeimbwa na mwanamama Jokha Kassim, alipokuwa na kundi zima la Zanzibar Stars Modern Taarab.
 
Kwa sasa Jokha anafanya kazi katika kundi zima la Tanzania Moto Modern Taarab, maarufu kama T-Moto, lenye wakali wengine kibao.
 
Tayari Jokha amerekodi wimbo unaokwenda kwa jina la ‘Domo la Udaku’, ukiwa ni ujio mpya wa kundi hilo la taarabu nchini.
 
Mwimbaji huyo juzi alifanya mazungumzo na Fiesta Magazine na kusema kuwa muziki ni kipaji chake, alichobarikiwa na Mungu.
 
Cheche zake zilianza kuonekana tangu zamani, alipokuwa hodari sana wa kuimba nyimbo mbalimbali za taarabu.
 
“Muziki huu ni kipaji changu, tangu zamani niliweza kuimba kwa ufanisi na kushangaza wengi waliokuwa wakiona mahala popote.
 
“Nashukuru, leo hii nimeweza kufanya juhudi na kufika T-Moto, ikiwa ni baada ya kujulikana nilipofanya kazi na Zanzibar Stars kwa mafanikio makubwa,” alisema.
 
Licha ya kuanza zamani kuimba, lakini alianza kuingia kwenye kundi la muziki mwaka 2002, alipohitajiwa na uongozi wa Zanzibar Stars na kumtambulisha kimuziki.
 
Kilichomkwamisha kuingia mapema kwenye sanaa ni kukatazwa na wazazi wake, hivyo kusubiri hadi mwaka huo alipoanza kushika kipaza sauti na kurindimisha sauti yake.
 
Jokha alikuwa mke wa kwanza wa Mfalme, Mzee Yusuph, ila kwa sasa wameachana na kila mmoja anaishi kivyake.
 
Siku chache baada ya kuachana na mzee Yusuph, hamu ya kuimba ilimtesa, hivyo kuamua kufanya harakati za kuibua kipaji chake.
 
Jokha na Mzee Yusuph wamezaa mtoto mmoja, ambaye pia ni mwimbaji na Mkurugenzi wa kundi la Jahazi Modern Taarab.
 
“Nilifanya kazi ya ziada kuingia kwenye muziki, maana baba yangu hakupenda suala hilo, hivyo kunipa wakati mgumu.
 
“Hata hivyo Mungu akipanga lake hakuna wa kuweza kutengua, ndio maana nimeweza kufika hatua hii na kujulikana sehemu kubwa kupitia soko la muziki wa taarabu,” alisema.
 
Mwimbaji huyo mwenye mvuto wa aina yake, anashindwa kubainisha chanzo cha kuvunjika kwa ndoa yake na mume wake Mzee Yusuph.
 
Anasema riziki imekwisha kwa ndoa yao, huku akisema bado wanaheshimiana kwasababu wameachana bila kuwa na ugomvi, huku wakifanikiwa kupata mtoto mmoja, aliyepewa jina la Yusuph Mzee Yusuph.
 
Muziki wa taarabu unazidi kufanya vizuri kutokana na waimbaji wake wengi kuwa wabunifu.
 
Katika hilo anaamini kuwa mambo yatazidi kuwa mazuri, huku mashabiki wakipata vitu adimu kutoka kwao.
 
Mwimbaji huyo anavutiwa na mkali wa muziki huo nchini, Zuhura Shaaban.
 
Katika kundi lake la T-Moto, Jokha ameimba nyimbo zaidi ya tatu, ukiwamo wa ‘Unavyojidhani Haufanani’ ‘Mimi ni Star’ na ‘Aliyeniumba Hajanikosea’, ambao ulibeba jina la albamu ya kwanza.
 
Kwa albamu hii mpya inayoandaliwa, Jokha amesharekodi wimbo mmoja unaokwenda kwa jina la Domo la Udaku.
 
Katika hilo, ni wazi kuwa wao watakuwa juu zaidi, maana bendi nyingi zimekosa ubunifu na mikakati ya kimuziki.
 
“Kwenye muziki kumekuwa na ushindani, hivyo nadhani kinachotakiwa ni mipango, mikakati pamoja na nyimbo nzuri.
 
“Sisi tunavyo vitu hivyo, nadhani ni wakati wetu kuwa kileleni maana mashabiki wana kiu ya kuona mambo yetu yanakuwa mazuri,” alisema.
 
Jokha alizaliwa miaka kadhaa iliyopita, Zanzibar, katika Hospitali ya Mnazi Mmoja.
 
Elimu ya Msingi aliipata katika shule ya Darajani na kuhitimu mwaka 1995 ile ya Sekondari aliipata kwenye shule ya Haile Selasi.
 
Mbali na Jokha, wengine wanaopatikana kwenye kundi hilo ni pamoja na Nyawana Fundikira, Aisha Masanja, Shimuna Kassim, Amina Rashid, Hanifa Juma, Shaban Ramadhan, Mrisho Rajabu, Rahma Omari, Silver Mwandilee, Kasikile Msukule na wengineo.
You might also like:

Azam hatimaye yaiangukia Simba kuhusu Ngassa wakubali kugawa mgao wa usajili kwa wana Msimbazi


KLABU ya soka ya Azam imeuangukia uongozi wa klabu ya Simba wakiwaomba walimalize suala la nyota wao Mrisho Ngassa kwa njia ya amani mradi winga huyo awahi kwenda kufanyia vipimo kwa lengo la kutua rasmi katika klabu ya El Merreikh ya Sudan.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jana jioni na kuthibitishwa na Katibu Msaidizi wa Azam, Twalim Suleiman 'Chuma' ni kwamba Azam imeuandikia barua uongozi wa Simba ukisema wapo tayari kuwapa sehemu ya fedha za usajili za Ngassa, mradi waondoe pingamizi lao lililopo TFF kabla ya saa 5 asubuhi ya leo.
Barua hiyo iliyosainiwa na Makamu Mwenyekiti wa Azam, Shani Cristom, imesema kuwa kwa vile muda wa usajili wa wachezaji kwa El Merreikh ni mfupi wangeomba Simba kutumia uungwana ili kumruhusu Ngassa aende Sudan kufanyiwa vipimo vya afya baada ya awali kusaini mkataba wa miaka miwili kuichezea timu hiyo.
Pia barua hiyo inasema Azam wapo tayari kuwapa Simba Dola za Kimarekani 25,000 na wapo (Azam) kusaliwa na Dola 50,000 katika Dola 75,000 za kumuuzia Ngassa, na kuutaka uongozi huo wa Simba kuhakikisha suala la mchezaji huyo ikiwemo kuondoa pingamizi lao TFF linafanyika kabla ya saa 5 asubuhi.
Katibu Msaidizi wa Azam, Twalib Chuma alikiri kuandikwa kwa barua hiyo na kutumwa kwa uongozi wa Simba na nakala kupelekwa TFF akisema lengo ni kuhakikisha Ngassa anapata fursa ya kujiunga na timu ya El Merreikh inayoshiriki Ligi ya Mabingwa wa Afrika mwakani.
"NI keli tumewaandikia barua Simba na kutuma nakala TFF kwa sababu ya kutaka kulimaliza suala la Ngassa kiungwana ili kumpa nafasi mchezaji huyo kwenda kucheza soka la kulipwa Sudan kwa manufaa ya taifa," alisema.
Twalib alisema anadhani jambo hilo la Ngassa litaisha kwa amani na kila upande kuridhia, japo walisema hawakuona sababu ya kulumbana na Simba ilihali klabu zote zipo kwa maendeleo ya soka la Tanzania.
Habari nyingine zilizotufikia asubuhi hii zinasema kuwa, pande mbili za klabu hizo wanatarajia kukutana kwa ajili ya kusaini makubaliano mapya juu ya uhamisho wa nyota huyo alioyeng'ara katika michuano ya Kombe la Chalenji iliyomalizika nchini Uganda hivi karibuni.





KIM POULSEN AWATAJA ASKARI WA KUWAVAA WAZAMBIA 

KOCHA wa Taifa Stars, Kim Poulsen ametangaza kikosi cha wachezaji 24 kitakachoingia kambini jioni ya Desemba 12 mwaka huu kuajianda kwa mechi ya kirafiki dhidi ya mabingwa wa Afrika, Zambia.

Katika kikosi hicho, wachezaji walioitwa kwa mara ya kwanza ni kipa Aishi Manula anachezea kikosi cha U20 cha Azam na timu ya Taifa kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes), beki wa kushoto wa Azam, Samih Nuhu, beki wa kushoto wa Mtibwa Sugar, Issa Rashid na mshambuliaji wa Azam, Mcha Khamis.

Pia kati ya wachezaji walioitwa, sita walikuwa kwenye kikosi cha Zanzibar (Zanzibar Heroes) kilichokamata nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Chalenji iliyomalizika Jumamosi jijini Kamapala, Uganda. Wachezaji hao ni Mwadini Ally, Nassoro Masoud Cholo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Samih Nuhu, Aggrey Morris na Mcha Khamis.

Kikosi kamili kilichoitwa ni makipa; Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ally na Aishi Manula (Azam U20). Mabeki ni Shomari Kapombe (Simba), Erasto Nyoni (Azam), Nassoro Masoud Cholo (Simba), Aggrey Morris (Azam), Samih Nuhu (Azam), Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (Yanga), Amir Maftah (Simba), Issa Rashid (Mtibwa Sugar) na Kevin Yondani (Simba).

Viungo ni Frank Domayo (Yanga), Athuman Idd Chuji (Yanga), Mrisho Ngasa (Simba), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Mcha Khamis (Azam), Salum Abubakar (Azam), Amri Kiemba (Simba) na Mbwana Samata (TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo- DRC).

Washambuliaji ni John Bocco (Azam), Simon Msuva (Yanga), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC) na Mwinyi Kazimoto (Simba).

Monday, December 10, 2012

Peter Manyika: 'Straika' wa zamani anayefuata nyayo za baba yake









HANA muda mrefu tangu alipotumbukia katika soka, lakini kipaji kikubwa cha alichonacho cha soka kimeanza kumtabiria kuja kuwa nyota kama baba yake aliyewahi kung'ara na timu za Mtibwa Sugar, Yanga na Taifa Stars.
Peter Manyika, ndiye kipa namba moja kwa sasa wa timu ya taifa ya vijana ya U17 'Serengeti Boys' iliyozikosa kiduchu fainali za Afrika zitakazochezwa mwakani nchini Morocco baada ya kujikwaa kwa vijana wenzao wa Kongo.
Manyika, mtoto wa kwanza wa nyota wa zamani, Manyika Peter ndiye aliyekaa langoni katika mechi zote dhidi ya Kondo ikiwemo ile ya ushindi wa bao 1-0 nyumbani na kipigo cha mabao 2-0 ugenini wiki iliyopita.
Kipa huyo anasema mechi ya pili dhidi ya Kongo ndiyo mechi itakayobaki kichwani mwake kama tukio la huzuni kwa kushindwa kuisaidia Serengeti Boys kurejea tukio la mwaka 2004 kufuzu fainali za Afrika kabla ya kutolewa.
Manyika aliyeanzia kucheza kama mshambuliaji wa kati kabla ya kubadilishwa namba akiwa Shule ya Msingi, baada ya kipa wao kuumia na yeye kuhamishiwa langoni na kung'ara, anasema vurugu walizofanyiwa Kongo hatazisahau.
"Kwa kweli fujo na vitimbi tulivyofanyiwa Kongo ni mambo yanayonifanya nishindwe kuisahau mechi hiyo kwani hatukutarajia kama tungerudi salama kwa namna walivyotufanyia 'unyama' ndani na nje ya uwanja," anasema.
Manyika, anayetarajiwa kuibukia timu ya U20 ya Mgambo Shooting katika michuano ya Kombe la Uhai baada ya kuachana na  JKT Ruvu, anasema kwa tukio la furaha hakuna kama alipoitwa timu ya taifa na kuwa kipa namba moja.
"Sio siri kuitwa kwangu Serengeti Boys kulikuwa kwa kushtukiza sikutarajia na furaha zaidi ni kuwa kipa namba moja wa timu hiyo," anasema.
Manyika anasema japo anajiamini ana kipaji cha soka cha kuzaliwa na kurithi toka kwa baba yake, lakini hakutarajia mafanikio hayo ya mapema.

CASILLAS
Manyika anayemtaja mjomba wake, David 'Mzee wa Yeah' na Method kama walioibua na kukiendeleza kipaji chake kabla ya baba yake kutia nguvu, anasema alivutiwa kisoka na nyota wa zamani wa Brazil, Ronaldo de Lima na kujikuta akicheza kama mshambuliaji wa kati.
Anadai hata hivyo alipohamia kwenye ukipa amehamisha mapenzi kwa kipa Joe Hart na Ike Casillas aliyedai ndiyo kiigizo chake huku akimzimia pia Yew Berko wa Yanga.
Manyika anayependa kula ugali kwa dagaa na mlenda na kunywa Fanta, anadai japo Ronaldo kastaafu soka bado anaendelea kuwa mchezaji bora kwake kuwahi kumuona kutokana na umahiri wake wa kufumania nyavu.
Akiwa na ndoto za kucheza soka la kulipwa, Manyika anayesoma kidato cha tatu kwa sasa katika Shule ya Sekondari Kizuka iliyopo Morogoro, anasema kipindi kifupi alichokuepo katika soka amenufaika kwa mambo mengi.
Anadai kutumainiwa na taifa, kumudu maisha kwa kujinunulia vitu bila kutegemea wazazi na kusafiri sehemu mbalimbali ni baadhi ya mafanikio hayo.
Manyika anasema donge nono kulipata ni Sh 540,000 alizopata hivi karibuni na kutumia kununua godoro, runinga na deki yake na matumizi mengine.
"Nashukuru fedha hizo zimenifanya niwe kila kitu cha kuanzia maisha kwani mama yangu alinichongea pia kitanda. Huwezi amini awali hakupenda kabisa nicheze soka ila kwa sasa ananiunga mkono," anasema.

NDOTO
Manyika anayezishabikia Yanga, Barcelona na Real Madrid akiwazimia Dimitar Babatov na Ronaldo, anasema japo Serengeti Boys imeshindwa  kufuzu fainali za Afrika anadhani itafanya hivyo baadaye.
Pia anasema anaamini Taifa Stars chini ya Kim Poulsen ikijipanga vema inaweza kufuzu fainali za Kombe la Dunia na za Afrika kwa vile kocha huyo ni mjanja, mjuzi na mwenye malengo mazuri.
"Kim nimefanya naye kazi ni bonge la kocha na watanzania tunapaswa kumuunga mkono na kumkumbatia kwani anaweza kutupeleka mbali, hata fainali za Dunia, muhimu tujipange, japo watu wanaona ni ngumu."
Manyika anayemtaja John Bocco kama nyota anayemzimia Bongo, anadai wakati anaibukia katika soka hakutaka kabisa kutumia mgongo wa baba yake mpaka alipogundua kama amejitosa kwenye mchezo huo.
"Huwezi amini aliyenisaidia kufika hapa ni mjomba wangu Mzee Yeah, baba alikuja kuwa msaada wa kuninunulia vifaa baada ya kutambua nimejitosa kurithi kipaji chake."
Anaongeza kwa kuwashukuru wawili hao, pia mama yake kipenzi, Method na, ndugu, jamaa na rafiki wote wanaomuunga mkono.

KIPAJI
Peter Manyika 'Casillas' alizaliwa Agosti 13, 1996 jijini Dar es Salaam akiwa mtoto wa kwanza kati ya wawili wa familia yao, elimu yake ya Msingi aliisoma Shule ya Rutihinda kabla ya kujiunga na Kizuka Sekondari.
Kisoka, alianza makeke yake tangu shule ya msingi akicheza kama 'straika'  kabla ya kuhamia kwenye ukipa, timu yake ya kwanza ya kueleweka ikiwa ni Zaragoza ya Magomeni kabla ya kutua kituo cha soka cha Twalipo.
Anasema akiwa na kituoni hapo mwaka jana aling'ara katika michuano ya Airtel akiichezea Shule ya Jitegemee kisha kutua JKT Ruvu U20 na kuichezea katika Kombe la Uhai.
Baadaye Juni mwaka jana aliitwa Serengeti Boys na kumudu nayo mpaka sasa na hivi karibuni ameelekea Mgambo Shooting U20 atakaoicheza katika michuano ya Uhai 2012.
Akiowa na ndoto za kuja kuwa mfanyabiashara mkubwa, Manyika hutumia muda wake wa ziada kusikilia muziki, kuangalia muvi na anadai soka la Bongo  lipo juu hasa baada ya vijana kupewa nafasi ya kuonyesha vipaji vyao.
Anasema kama hali hiyo ikiendelea Tanzania itafika mbali, japo ametaka wadau wa soka kuwekeza zaidi na kudhamini klabu zote bila ubaguzi pia akitaka kuongezeka kwa michuano mingi zaidi ya ile ya ligi.
Juu ya Simba na Yanga, kinda hilo linalowasihi wachezaji wenzake kuzingatia mazoezi na kulitumaini soka kama ajira zao zinazoweza kuwatoa kimaisha anasema hana papara za kuzikimbilia kwa vile anataka kwanza kujenga jina.
"Simba na Yanga kwa sasa ni kubwa mno kwangu, labda baadaye tena kwa kuridhishwa na masilahi, napenda zaidi kucheza nje ya nchi au klabu isiyo na presha kubwa kama vigogo hao," anasema.

MESSI AVUNJA REKODI YA GERD MULLER, FALCAO NOMA

Asante Mungu nimempita Gerd Muller... mshambuliaji wa Barcelona, Lionel Messi akishangilia goli lake la 86 msimu huu jana usiku dhidi ya Real Betis.
Messi akishangilia kuvunja rekodi ya mabao 85 iliyowekwa na Mjerumani Gerd Muller mwaka 1972. Messi alifunga mabao mawili dhidi ya Real Betis jana na kufikisha jumla ya mabao 86 mwaka huu 2012. Ana mechi tatu kabla ya kuumaliza mwaka huu.
Falcao wa Atletico Madrid akishangilia moja ya mabao yake matano dhidi ya Deportivo Coruna jana usiku. Atletico walishinda 6-0.
Shujaa wa mabao MATANO, Radamel Falcao wa Atletico Madrid akishangilia moja ya mabao yake dhidi ya Deportivo Coruna jana usiku. Atletico walishinda 6-0.

MADRID, Hispania
LIONEL Messi asiyezuilika ameweka rekodi mpya ya kufunga mabao mengi zaidi kwa mwaka mmoja wa kalenda katika historia ya soka duniani na kuwasaidia vinara ambao hawajapoteza mechi katika La Liga, Barcelona, kuendelea kuongoza kwa tofauti ya pointi sita juu ya Atletico Madrid kufuatia ushindi mgumu 2-1 ugenini dhidi ya Real Betis jana.

Mwanasoka Bora wa Dunia Messi alifunga goli lake la 85 na la 86 kwa mwaka 2012 katika mechi iliyojaa ushindani kwenye uwanja wa Benito Villamarin mjini Seville na kuipiku rekodi ya mabao 85 iliyowekwa na Mjerumani Gerd Mueller mwaka 1972.

Tukio hilo la kihistoria la Messi lilifunika mambo makubwa yaliyofanywa jana usiku na mshambuliaji Atletico, Radamel Falcao, ambaye mapema alifunga magoli matano peke yake wakati walipoisambaratisha timu inayoburuta mkia ya Deportivo Coruna kwa mabao 6-0 nyumbani.

Mshambuliaji huyo wa Colombia, anayefahamika kama 'the tiger' na ambaye anagombewa na klabu tajiri zaidi za Ulaya, alifikisha jumla ya mabao yake msimu huu kuwa 16 katika mechi 15 wakati Atletico ikidumisha tofauti ya pointi tano juu ya mahasimu wao wa mji mmoja Real Madrid.

Kikosi cha Jose Mourinho cha Real kililazimika kuzinduka kutoka nyuma mara mbili na kupata ushindi mgumu wa 3-2 ugenini dhidi ya Real Valladolid Jumamosi ambao uliwasaidia kupunguza pengo la pointi dhidi ya Atletico, ambao waliwafunga 2-0 wikiendi iliyopita, kuwa pointi mbili kwa usiku huo.

Hata hivyo, Atletico walijibu kwa kushinda mechi yao ya 12 katika 15 za ligi msimu huu dhidi ya timu iliyopanda daraja ya Depor ambayo iko hatarini kurejea moja kwa moja daraja la pili.

Barca wameshinda mechi zao zote msimu huu ukiacha sare ya 2-2 nyumbani dhidi ya Real Madrid Oktoba na magoli mawili ya Messi yaliwafanya wafikishe pointi 43, huku Atletico wakiwa na pointi 37 na Real wana pointi 32. Betis ni wa tano wakiwa na pointi 25, sawa na wanaoshikilia nafasi ya nne Malaga, ambao waliwasambaratisha Granada 4-0 Jumamosi.

"Inaonekana kama jambo lisilowezekana kwamba yeye (Messi) anaweza kufunga magoli mengi kiasi hiki ndani ya mwaka mmoja lakini kuna mechi tatu zimebaki na tunatumai kwamba ataendelea kuongeza jumla ya mabao yake," kocha wa Barca, Tito Vilanova, aliuambia mkutano na waandishi wa habari.

"Tunatumai kwamba atakwenda mbali sana katika maisha yake ya soka kwa sababu bado ni mdogo sana," aliongeza. "Sidhani kama tutaona mchezaji mwingine kama yeye."

BETIS WASIO NA BAHATI
Kikosi cha Vilanova kiliwatawala Betis kama ilivyotarajiwa katika kipindi lakini wakapoteza umiliki baada ya mapumziko na mwamba wa lango uliinyima timu hiyo goli mara tatu.

Messi aliifikia rekodi ya Mueller wakati alipochukua mpira katika eneo la katikati katika dakika ya 16 na akaiacha safu ya ulinzi ya Betis ikiwa imesimama kabla ya kufunga kwa shuti la pembeni chini kulia.

Pasi ya 'akili' ya kisigino ya Andres Iniesta ilimpikia Messi goli la pili dakika tisa baadaye kwa shuti kali kutokea katika eneo lile lile la kwanza ndani kidogo ya boksi na mpira ukatumbukia kwenye kona ile ile ya lango.

Ruben Castro alirudisha goli moja kwa wenyeji katika dakika ya 39 na kufanya kipindi cha pili kuwa kigumu zaidi kwa wageni.

Messi alikaribia kufunga 'hat-trick' dakika tano kabla ya mechi kumalizika wakati alipopiga 'tikitaka' ya jirani na lango lakini kipa wa Beti, Adrian alipangua mpira huo ambao ulimrudia Jordi Alba ambaye shuti lake liligonga 'besela' na mpira kutoka nje.

Kipigo kilikuwa kigumu kwa Betis, ambao waliwachapa Real 1-0 nyumbani mwezi uliopita na kuwapa Barca moja ya mitihani migumu zaidi kufikia sasa msimu huu ambao ulistahili japo pointi moja.

Mshambuliaji wa Atletico, Diego Costa alirekebisha makosa ya kadi nyekundu aliyopewa Alhamisi kwenye Ligi ya Europa wakati alipofunga goli la kuongeza kwenye Uwanja wa Calderon kwa kichwa kutokana na kona iliyopigwa na Koke katika dakika ya 23.

Kiungo wa Depor, Juan Valeron alipiga kichwa kilichogonga nguzo dakika nne baadaye lakini Atletico waliongeza la pili wakati Falcao alipoikimbilia vyema pasi ya Koke na kufumua shuti la chini lililotinga kwenye kona ya wavu.

Mpira uliorushwa haraka kutokea kushoto dakika tatu kabla ya mapumziko ulimpikia goli la pili mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26 na akafumua shuti kali lililomshinda kipa Daniel Aranzubia kutokea kwenye kona ya eneo la penalti.

Falcao kisha akaangushwa ndani ya boksi na akafunga penalti hiyo katika dakika ya 64 na kukamilisha 'hat-trick' yake, akafunga kwa kichwa la nne na akakamilisha lake la tano katika dakika ya 71.

Yeye ni mchezaji wa kwanza kufunga magoli matano katika mechi ya La Liga tangu Fernando Morientes alipofanya hivyo kwa Real Madrid dhidi ya Las Palmas mwaka 2002.

MALLORCA AIBU
Real Mallorca waliendelea kuporomoka kuelekea kushuka daraja wakati walipofungwa 4-0 ugenini Levante, kikiwa ni kipigo cha nane katika mechi 10 walizocheza bila ya ushindi.

Obafemi Martins aliwafungia Levante goli la kuongoza kabla ya mapumziko na David Navarro, Ruben Garcia na Vicente Iborra walifunga katika kipindi cha dakika 10 katika kipindi cha pili.

Levante, ambao wamefuzu hatua ya 32-Bora ya Ligi ya Europa, wako katika nafasi ya sita wakiwa na pointi 24, huku Mallorca wakiwa katika nafasi ya 17 kwa pointi 13.

Timu inayochechemea ya Athletic Bilbao ilipata ushindi wa tano tu msimu huu wakati waliposhinda 1-0 nyumbani dhidi ya Celta Vigo.

Goli la kichwa la Aritz Aduriz katika dakika ya 33 liliamua mechi kwenye uwanja wa San Mames na kuiinua Bilbao hadi nafasi ya  13 wakiwa na pointi 18 points. Celta wako katika nafasi ya 15 kwa pointi 15.

Manyika Jr bado aliota pambano la Kongo



KIPA namba moja wa timu ya taifa ya vijana U17 'Serengeti Boys', Peter Manyika 'Casillas' amesema itamchukua muda mrefu kusahau matukio waliyofanyiwa na wenyeji wao Kongo katika pambano lao la marudiano la kuwania kucheza fainali za Afrika.
Manyika, alisema vitisho na fujo walizofanyiwa na wenyeji wao kabla na baada ya kuanza kwa pambano hilo, kwa kiasi kikubwa vilichangia timu yake kupokea kipigo cha mabao 2-0 na kung'olewa mashindano na kuzima ndoto za kufuzu fainali hizo za 2013.
Akizungumza na MICHARAZO katika mahojiano maalum nyumbani kwao, Kigogo jijini Dar es Salaam juzi, Manyika alisema ingawa hilo ndilo pambano lake la kwanza la kimataifa nje ya nchi, lakini hakuwaza kama angekutana na vitimbi kama hivyo ikizingatiwa michuano yenyewe ni ya vijana, pia wenzetu walipokewa vema hapa nchini.
"Kwa kweli niliingiwa na woga na hofu kubwa kwa namna wenyeji wetu walivyotufanyia vituko na fujo ambazo kwa kiasi fulani zilitupotezea umakini uwanjani, licha ya makocha kututia moyo kulipigania taifa," alisema.
Manyika, alisema anadhani kuna haja ya shirikisho la soka Afrika kuyaangalia matukio hayo waliyofanyiwa ikiwemo kupigwa kwa kocha wao msaidizi, Jamhuri Kihwelu 'Julio' ili kuyakemea yasiweze kurudia tena kwani yanaweza kujenga uhasama usio na maana.
Serengeti Boys, walishindwa kurejea rekodi iliyowekwa na wenzao mwaka 2004 walipofuzu fainali hizo za Afrika za U17 kabla ya kuenguliwa kwa kosa la kuchezesha 'kijeba' Nurdin Bakar na nafasi yao kupewa Zimbabwe waliokuwa wamewatoa.

Mwisho

Miyeyusho, mtwanga Nassib na kutwa taji la WBF






Bondia Fransic Miyeyusho akionesha ufundi wake kwa kumtupia masumbwi Nassibu Ramadhani wakati wa Mpambano wao wa kugombania ubingwa wa WBF uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita Miyeyusho alishinda kwa T.K.O ya raundi ya kumi picha nawww.superdboxingcoach.blogspot.com
Bondia Mohamed Matumla  kulia  akimuhadhibi Doi Miyeyusho wakati wa mpambano huo usiku wa kuamkia  leo Matumla alishinda kwa K,O raundi ya pili Picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com
Bondia Juma Fundi kushoto na Fadhili Majia wakioneshana umwamba wa kutupiana masumbwi wakati wa mpambano wao uliofanyika mwishoni mwa wiki Majia alishinda kwa pointiPicha na www.superdboxingcoach.blogspot.com
Bondia Fransic Miyeyusho kushoto akimwazibu mpinzani wake Nassibu Ramadhani kwa kumtupia makonde mazito wakati wa Mpambano wao wa kugombania ubingwa wa WBF uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita Miyeyusho alishinda kwa T.K.O ya raundi ya kumi picha nawww.superdboxingcoach.blogspot.com
Bondia Fransic Miyeyusho akionesha ufundi wake kwa kumtupia masumbwi Nassibu Ramadhani wakati wa Mpambano wao wa kugombania ubingwa wa WBF uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita Miyeyusho alishinda kwa T.K.O ya raundi ya kumi picha nawww.superdboxingcoach.blogspot.com
Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mkangara kulia akimvisha mkanda wa ubingwa wa WBF bondia Fransic Miyeyusho baada ya kumtwanga Nassibu Ramadhani  kwa T.K.O raundi ya kumi kushoto ni promota wa mpambano huo Mohamed Bawaziri www.superdboxingcoach.blogspot.com
Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mkangara kulia akimpongeza Bingwa wa ubingwa wa WBF bondia Fransic Miyeyusho baada ya kumtwanga Nassibu Ramadhani  kwa T.K.O raundi ya kumi kushoto ni promota wa mpambano huo Mohamed Bawaziri www.superdboxingcoach.blogspot.com
bondia Fransic Miyeyusho akiwa amebebwa juu akiwa na mikanda miwili alioshinda baada ya kumtwanga Nassibu Ramadhani picha nwww.superdboxingcoach.blogspot.coma
Kocha wa Kimataifa wa Mchezo wa Masumbwi Rajabu Mhamila  'Super D' kushoto akiwa na wadau waliojitokeza kuangalia mpambano huo
BONDIA machachari wa ngumi za kulipwa nchini, Francis Miyeyusho juzi alifanikiwa kutetea taji lake la Mabara la UBO na kunyakua taji jipya pia la Mabara la WBF baada ya kumtwanga kwa TKO 10 mpinzani wake Nassib Ramadhani.
Miyeyusho alimtwanga Nassib TKO hiyo katika raundi ya 10 katika pambano kali lililofanyika kwenye ukumbi wa PTA, jijini Dar es Salaam na ikuhudhuriwa na viongozi na wanamasumbwi mbalimbali nyota nchini.
Pambano hilo lililoandaliwa na mratibu Mohammed Bawazir na lililokuwa la kwanza kwa mabondia hao lilikuwa na jumla ya raundi 12 uzito wa bantam na lilianza kwa Nassib kumpeleka puta mpinzani wake kwa makonde makali.
Hata hivyo kadri raundi zilivyokuwa zikisonga mbele Nassib alianza kuonekana kuishiwa pumzi hasa kuanzia raundi ya nane na kumpa nafasi mpinzani wake nafasi ya kusimama imara kabla ya kusalimu amri katika raundi ya 10.
Mara baada ya Miyeyusho kutangazwa kuwa mshindi alikabidhiwa mataji yake mawili na aliyekuwa mgeni ramsi, Waziri wa Habari Utamaduni, Vijana na Michezo Dk Funella Mukangara na kuamsha hoi hoi ukumbini hapo.
Kabla ya pambao hilo, kulikuwa na mapambano mengine ya utangulizi ambapo Mohammed Matumla ' Snake Boy Jr' alimpiga kwa KO Doi Miyeyusho, Deo Samuel alitoka sare na Freddy Sayuni ,Fadhil Majiha alimpiga kwa pointi Juma Fundi na Ibrahim Classic alimpiga kwa pointi Said Mungi.
Baadhi ya mashabiki waliofurika kwenye ukumbi huo waliwapongeza waratibu wa pambano hilo sawia na kuwasifu mabondia wote waliopigana siku hiyo husuisani kumwagia sifa Nassib wakidai ni 'bonge' la bondia licha ya kupoteza mchezo huo.

Mwisho

Wednesday, December 5, 2012

YANGA YAZINDUA KALENDA YAKE KWA MBWEMBWE



YANGA walitumia burudani ya muziki na wanenguaji kujaza watu kwenye makao makuu ya klabu yao jijini Dar es Salaam wakati wakizindua Kalenda yao ya mwaka 2013.
Mabingwa hao wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) wameingia ubia wa mwaka mmoja na kampuni ya ‘Pecha Media & Health Promotion’ kutengeneza kalenda za klabu yao.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Nasib Limira alisema kuwa kampuni yake imeamua kutengeneza kalenda za Yanga ili kuisaidia klabu hiyo kukuza uchumi wake.
Alisema klabu hiyo inayojiandaa kwenda Uturuki kuweka kambi kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu, ina vyanzo vingi vya mapato, lakini inakosa fedha nyingi kutokana na kuwapo kwa ‘wajanja’ wanaotengenezaa bidhaa kwa jina la klabu hiyo na kuziuza kwa faida yao binafsi.
“Yanga ni klabu kubwa, lakini inakosa pesa nyingi kutokana na kuwapo kwa watu ambao wanajinufaisha kwa kutengeneza kalenda na bidhaa nyingine wakitumia jina la klabu hii. Tumeamua kuwasaidia kutengeneza kalenda hizi ikiwa ni sehemu ya mchango wetu katika kuwasaidia kuinua kipato chao,” alisema Limira.
Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema kuwa kutengenewa kwa kalenda hizo ni mwanzo mzuri kuonesha kwamba wamedhamiria kuinua kipato cha klabu hiyo na kudhibiti mianya ya watu kutengeneza bidhaa kwa jina la klabu hiyo huku pesa za mauzo zikiishia kwenye mifuko yao bila klabu hiyo kunufaika chochote.
“Huu ni mwanzo tu, tunataka kuwadhihirishia wapenzi wa Yanga kwamba tuko makini na mali za klabu. Tumeanza na Kalenda, zitafuata bidhaa nyingine kama jezi maana watu wengui wamekuwa wakituhujumu katika hili,” alisema Mwalusako.
Alisema kalenda hizo zinauzwa kwa Sh. 5,000 na katika kila kalenda Yanga itapata Sh.1,500 na kwamba kampuni hiyo imeanza kwa kuitengeneza nakala 100,000.
Hiyo ni mara ya kwanza kwa Yanga, ambao wamemaliza mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo wakiwa katika nafasi ya kwanza, kutengeneza kalenda maalum za klabu yao tangu ianzishe mwaka 1935.