STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, November 26, 2013

Uhai Cup yahami Chamazi, Usajili wafafanuliwa

Michuano ya Kombe la Uhai imeingia hatua ya robo fainali ambapo sasa mechi zinachezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Uamuzi wa kuhamisha mechi hizo kutoka viwanja vya Karume na DUCE ni kuziwezesha zote kuoneshwa moja kwa moja (live) na Azam Tv.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tunaomba radhi kwa washabiki ambao watakuwa wameathirika kutokana na uamuzi huo.
USAJILI DIRISHA DOGO KUFUNGWA DESEMBA 15
Wakati dirisha dogo la usajili linafungwa Desemba 15 mwaka huu, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tunazikumbusha klabu zote kuheshimu kanuni na kuzingatia muda uliowekwa.
Pia tunakumbusha kuwa kupeleka mchezaji kwa mkopo katika klabu nyingine hakutoi nafasi ya kusajili mchezaji mpya. Kama klabu ilisaji wachezaji 30 maana yake ni kuwa haina nafasi ya kuongeza wachezaji.
Kwa upande wa wachezaji wa kigeni (foreign players), tunakumbusha kuwa kuanzia msimu ujao 2014/2015 watakuwa watatu tu badala ya watano wa sasa.
Kuhusu usajili wa wachezaji kutoka nje mpaka sasa hakuna hata klabu moja imeshaingia kwenye TMS kuomba uhamisho. Itakapofika Desemba 15, system ya TMS itafunga.
RAMBIRAMBI MSIMBA WA ANDREW KILOYI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mwamuzi wa zamani wa FIFA, Andrew Kiloyi kilichotokea mjini Iringa.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa, Ramadhan Mahano, Kiloyi alifariki dunia juzi (Novemba 24 mwaka huu) kutoka na ugonjwa wa fangasi ya ubongo, na marehemu amesafirishwa kwenda kwao Kigoma ambapo atazikwa.
Kiloyi alizaliwa Mei 5, 1968. Alijiunga na uamuzi wa mpira wa miguu mwaka 1988 ambapo alipata beji ya FIFA mwaka 2001 akiwa mwamuzi msaidizi. Alistaafu uamuzi mwaka 2009, na hadi anafariki akiwa mjumbe wa Kamati ya Waamuzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa (IREFA).
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pole kwa familia ya marehemu, IREFA, ndugu, jamaa na marafiki kutokana na msiba huo na kuwataka kuwa na moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hicho cha majonzi. Mungu aiweka mahali pema roho ya marehemu Kiloyi.

Wanne washinda Uchaguzi CECAFA

Tanzania FA President Leodegar Tenga: I do not intend to run for re-election on February 24
Rais wa CECAFA, Leodger Tenga
BARAZA la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limepata wajumbe wapya wa wanne wa Kamati ya Utendaji katika uchaguzi uliofanya leo (Novemba 26 mwaka huu) hoteli ya Hillpark jijini Nairobi.
Uchaguzi huo ulifuatiwa na Mkutano Mkuu wa CECAFA ulioongozwa na Mwenyekiti wake Leodegar Tenga na kuhudhuriwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Kalusha Bwalya na ofisa wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Emmanuel Maradas.
Rais wa zamani wa Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Uganda (FUFA), Lawrence Mulindwa ndiye aliyeongoza katika uchaguzi huo ambapo wasimamizi walikuwa Bwalya na Maradas.
Mulindwa alipata kura zote 12 na kufuatiwa na Tariq Atta wa Sudan (10), Abdigaani Saeb Arab wa Somalia (9) na Raoul Gisanura wa Rwanda (8). Atta, Arab na Gisanura walikuwa wakitetea nafasi zao.
Walioshindwa ni Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Sudan Kusini (SSFA), Alei Chabor aliyepata kura tano na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF), Sam Nyamweya aliyepata kura nne.

Kili Stars yatua salama Nai, Znz Heroes kuanza kibarua kesho

Timu ya Kilimajaro Stars

TIMU ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) imewasili salama Nairobi, Kenya tayari kwa mashindano ya Kombe la Chalenji yanayoanza kesho (Novemba 27 mwaka huu) katika Uwanja wa Nyayo.
Kilimanjaro Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iliwasili saa 3 usiku kwa ndege ya RwandAir, na imefikia katika hoteli ya Sandton iliyoko katikati ya Jiji la Nairobi.
Kwa mujibu wa programu ya Kocha Mkuu Kim Poulsen, Kilimanjaro Stars leo (Novemba 26 mwaka huu) ni mapumziko ambapo kesho itafanya mazoezi kujiandaa kwa mechi yake ya kwanza dhidi ya Zambia itakayochezwa Novemba 28 mwaka huu Uwanja wa Machakos.

Mechi ya Tanzanite sasa kuchezwa Dar

Mashujaa wa Tanzania, Tanzanite
MECHI ya kwanza ya raundi ya michuano ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika kwa wanawake chini ya miaka 20 kati ya Tanzania (Tanzanite) na Afrika Kusini iliyokuwa ichezwe Mwanza sasa itafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Baada ya ukaguzi uliofanywa na maofisa wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imebainika uwanja huo unatakiwa ufanyiwe marekebisho ambayo hayawezi kuwahi Desemba 7 mwaka huu, siku ambayo ndiyo mechi hiyo inatakiwa kuchezwa.
Vyumba vya wachezaji vya uwanja huo ndilo eneo ambalo linatakiwa  kufanyiwa marekebisho makubwa.

Zitto Kabwe, Dk Kitila wana mashtaka 11 ya kujibu CHADEMA

Zitto Kabwe
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo kimesema kimewaandikia barua aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Zitto Kabwe na Mjumbe wa kamati Kuu Dk Kitila Mkumbo ambazo wanapaswa kujieleza kwa siku kumi na moja, kisha watapata fursa kujieleza mbele ya kamati kuu maalumu kwanini wasifukuzwe Chama.
Akizungumza katika makao makuu ya chama hicho, Mkurugenzi wa habari na Uenezi John Mnyika, alisema barua hizo zipo tayari na wahusika watapatiwa wakati wowote kuanzia leo Novemba 26.

Mnyika alikuwa akitoa taarifa ya kikao cha Utekelezaji cha sekretarieti ya chama hicho iliyoketi baada ya mkutano wa kamati kuu iliyoketi tarehe 20 – 22 Novemba mwaka huu.

Ni katika Mkutano huo, Mwanasheria Mkuu wa Chama hicho, Tundu Lissu alisema kuwa mkutano uliofanywa na Zitto na Dk Kitila mbele ya waandishi hawajazungumzia tuhuma zinazowakabili, badala yake walichofanya ni  kujitungia tuhuma ambazo kimsingi sizo zilizo wavua nafasi zao.

Lissu alisema, Zitto na Dk Kitila hawakusimamishwa nyadhifa zao kwa masuala ya PAC, Uchaguzi wa mwaka 2010, wala kutoshiriki kwenye operesheni za chama au sababu zingine, na walitaja  hizo sababu ili kupotosha tuhuma zinazowakabili kwa jamii.

“Walichokifanya kina Zitto na Kitilla ni "Diversion" (kubadili mwelekeo) wa  mashtaka yao yanatokana na waraka wa kihaini wa mabadiliko ambao ni kinyume na katiba, kanuni na maadili na itifaki ya Chama.  anawaambia waandishi, "wamevuliwa nafasi zao na kamati kuu kwa sababu ya waraka wenye nia ovu" alisema Lissu.

Aliongeza kuwa Chadema kina mwongozo wa uchaguzi uliopitishwa na kamati kuu, Zitto na Kitila wanaufahamu ingawa haijulikani ni kwanini wao walienda kinyume na mambo yanayojadiliwa katika kamati kuuu

Aidha Lissu alieleza kuwa Dk Kitilla anapotosha umma na wanachaka kwa kauli yake kuwa kamati kuu haina mamlaka ya kumvua yeye nafasi yake ya ujumbe wa kamati kuu maana amechaguliwa na baraza kuu, alimtaka Kitila na Zitto waangalie vema katiba ya chama hasa majukumu ya kamati kuu, pale yanaporuhusu Mwanachama yeyote kusimamishwa au kufutiwa uanachama haraka kama kamati kuu itaona kuna umuhimu wa kufanya vile.

Kigaila alisema, Kamati kuu iliyoketi Novemba 20-22/2013 ilipitisha ratiba ya uchaguzi wa ndani ya chama kama ifuatavyo.

22/11/2013-14/12/2013 ni kukamilisha zoezi la usajili wa  wanachama, 15 Desemba hadi 15 Januari uchaguzi ngazi za vitongoji, 16 januari 30 Januari 2014 Rufaa naukaguzi, ambapo tarehe 01 Februari hadi 15 Februari ni uchaguzi wa matawi.

Chadema pia ilisema 16 Februari hadi 29 mwezi huo huo ni kusikiliza rufaa na ukaguzi, ambapo uchaguzi wa majimbo utaanza rasmi 1 Aprili hadi Aprili 10, huku uchaguzi ngazi ya Wilaya ukitarajiwa kufanyika 25 Aprili hadi mei 5 mwaka 2014, na ngazi ya Mikoa ni 20 Mei hadi 25 Mei.

Huku uchaguzi wa kanda ukitarajiwa kufanyika Julai 9, na haada ya hapo Julai 23 hadi Julai 30 utakuwa ndio muda wa uchaguzi ngazi ya Taifa, utakaoanza na baraza la Wazee, Baraza la Vijana, Baraza la Wanawake kisha uchaguzi wa ndaniya chama.

Bw' Misosi sasa avuta raha

Joseph Rushahu 'Bwana Misosi
NYOTA wa zamani wa muziki wa kizazi kipya nchini, Joseph Rushahu a.k.a 'Bwana Misosi', ameamua kuvunja ukimya kwa kupakua wimbo mpya uitwao 'Vuta Raha'.
Akizungumza na MICHARAZO, Misosi alisema wimbo huo ameurekodia katika studio za Plexity Records chini ya maprodyuza Zest ba Fide Touch.
Misosi alisema tayari wimbo huo ameuachia mwishoni mwa wiki na tayari umeanza kurushwa hewani kupitia vituo vya redio, mitandao ya kijamii na kupigwa katika kumbi za disko.
Msanii huyo aliyewahi kutamba nchini kwa vibao vikali kama 'Nitoke Vipi', 'Mabinti wa Kitanga' na 'Mungu Yupo Bize', alisema wimbo huo mpya ni kati ya kazi zake mpya alizopanga kuzitoa kabla ya kufungia mwaka 2013.
Misosi ambaye mapema mwaka huu alijitosa kwenye masuala ya filamu, alisema kwa sasa anajipanga ili kutengeneza video ya wimbo huo kabla ya kuachia kazi nyingine za kufungia mwaka na kuukaribisha mwaka mpya.
"Baada ya kimya kirefu nimeachia wimbo mpya uitwao 'Vuta Raha' nilioimba na mwanadada aitwaye Namcy na tayari umeshaanza kuwa gumzo katika vituo vya redio na kumbi za disko, nafurahi ulivyopokelewa," alisema Misosi.

Kijogoo wa Jakaya agtaka wasanii wenzake kubadilika wathaminike


MUIGIZAJI anayetamba na kundi la kundi la Jakaya Arts, Boniface Gilliard 'Kijogoo', amewataka wasanii wenzake kutambua nafasi zao ndani ya jamii na kuepuka kujihusisha na mambo ya hovyo kwa madai yanachangia hata kuwanyima tenda za matangazo ya biashara.
Kijogoo anayefahamika pia kama 'Kikoti', alisema kujihisha na skendo mara kwa mara mbali na kuonyesha ujinga walionao baadhi ya wasanii, lakini pia inawanyima nafasi ya kulamba 'tenda' za matangazo ya biashara kama wanavyoneemeka wasanii wenzao wa kimataifa.
"Wasanii lazima wabadilike, watambue nafasi zao mbele ya jamii. Skendo zimekuwa zikichafua sifa ya tasnia na wasanii kwa ujumla na hii inatufanya tuendelee kudharauliwa na kupuuzwa kwa sababu ya wachache wasiojitambua na wanaoendekeza ujinga," alisema Kijogoo.
Kijogoo alijipatia umaarufu mkubwa kwa uigizaji wake kupitia michezo kama 'Riziki', 'Barafu la Moyo', 'Mapito', 'Donda la Kichwa', 'Ulimbo' na 'Chekecheo', alisema ni lazima wasanii wajue wao ni kioo cha jamii hivyo wanapaswa kuwa mfano bora katika maneno na matendo yao.
Alisema ni jambo gumu jamii kuwaelewa wasanii katika kile wanachokifikisha kwao kupitia kazi zao iwapo wenyewe wanafanya mambo ya ovyo na yasiyo ya mfano bora ambayo pia huharibu baada ya vijana na watoto wakiwa miongoni mwa mashabiki wao wanaowafuatilia kwa karibu.
Msanii huyo anayeshiriki pia filamu kadhaa kama 'Mahaba Niue', ' Like Father Like Son', 'XXL' na Best Palyer', alisema wasanii wanapaswa kuthamini fani hiyo kwa vile ni ajira yao na tegemeo la kuwainua kiuchumi kama watajikita kwenye kazi kuliko skendo chafu.

K-Guitar wa Bana Marquis wala hajutii


Kelvin Nyoni 'K Guitar' kaika pozi
MUIMBAJI wa bendi ya muziki wa dansi ya Bana Marquiz, Kelvin Nyoni 'K Guitar', amefyatua wimbo wake binafsi uitwao 'Sintojutia' uliopo katika miondoko ya Zouk.
Tayari wimbo huo umeanza kurushwa hewani na baadhi ya vituo vya redio nchini na kwa sasa anajipanga kwa ajili ya kufyatua video yake ili mashabiki wapoate uhondo kamili.
Akizungumza na MICHARAZO, mwanamuziki huyo anayecharaza pia gitaa la rythm alisema wimbo huo ameurekodia katika studio za Swadt Records chini ya prodyuza T-Tach kwa msaada mkubwa wa mameneja wake watatu  akiwamo mchora katuni wa gazeti hili, Abdul King'O.
Kelvin alisema wimbo huo ni mwanzo wa safari ndefu ya kuwapa burudani mashabiki wa muziki kupitia albamu yake binafsi itakayokuwa na nyimbo zaidi ya sita katikka miondoko tofauti za Zouk, Bongofleva na Rhumba.
"Baada ya kukamilisha kutoa video ndipo nitaanza kurekodi nyimbo nyingine ambapo mpaka sasa tayari ninazo kama tatu zilizokamilisha mashairi yake," alisema Kelvin.
Kelvin kabla ya kuingia kwenye muziki wa dansi akijiunga na bendi ya Bana Marquiz inayoongozwa na mwanamuziki nyota wa kimataifa, Tshimanga Assosa Kalala 'Mtoto Mzuri', alishawahi kutoa wimbo wa Bongofleva wa 'Mapenzi Siyo Pesa' kabla ya kuurudia tena katika bendi hiyo.

Hapatoshi Ligi ya Mabingwa Ulaya

Arsenal watakaokuwa nyumbani Ligi ya Mabingwa Ulaya
KIVUMBI cha Ligi ya Mabingwa Ulaya kinatrajiwa kuendelea tena leo, huku kivumbi kikiwa katika pambano kati ya Borussia Dortmund itakapoikaribisha Napoli ya Italia, hiyo ikiwa ni nafasi pekee kwao kujua kama itakuwa na nafasi ya kusonga hatua ya mtoano ama la.
Kwanza inakabiliwa na majeruhi kutokana na kipigo cha 3-0 ilichokipata Jumamosi kwenye Bundesliga dhidi ya wapinzani wao wakubwa Bayern Munich, timu hiyo ya Kocha Juergen Klopp inahitaji kushinda mechi zake mbili za mwisho katika Kundi F, dhidi ya Napoli na Olympique Marseille ili kutinga hatua ya mtoano.
Matokeo yoyote kinyume na ushindi, yatamaanisha timu hiyo ambayo ilitinga fainali msimu uliopita, itakuwa imeshindwa kufikia malengo hayo.
"Tunakosa umakini na malengo," alisema kipa wa Dortmund, Roman Weidenfeller. "Tunachukua muda mrefu kumalizia gonga zetu. Tunapasiana badala ya kwenda moja kwa moja langoni."
"Bado hakuna lolote ambalo limefanyika, iwe kwenye ligi ya nyumbani ama Ulaya. Lakini mechi ya Jumanne (leo) ni muhimu sana kuliko hii dhidi ya Bayern. Tunahitaji kushinda mechi hii ya nyumbani na tunahitaji kutumia nafasi zetu kwa sababu mchezo ni kushinda kwa kufunga mabao."
Dortmund inashika nafasi ya tatu katika kundi lao ikiwa na pointi sita, tatu nyuma ya kinara Arsenal na  Napoli ambazo zina pointi tisa zikitofautiana kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa. Marseille haina pointi yoyote baada ya kupoteza mecho zote. Napoli iliichapa timu hiyo ya Ujerumani kwa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza iliyopigwa Septemba mwaka huu.
"Niliiambia timu yangu baada ya mechi ya Bayern kuwa ina dakika tano za kusahau machungu na kisha kujipanga upya," alisema Klopp, ambaye timu yake ipo pointi saba nyuma ya vinara Bayern katika Bundesliga.
"Tunapaswa kufikiri kuhusu mechi ijayo, kutoa maamuzi sahihi na kuwa na utayari kimichezo. Tunahitaji kujua mustakabali wa yote katika mechi na Marseille (katika mechi yetu ya mwisho)."

Majeruhi
Klopp atahitaji kufanya mabadiliko katika safu yake ya ulinzi kwa mara nyingine tena baada ya Manuel Friedrich kuwa mbadala pekee wiki iliyopita kutokana na Mats Hummels, Neven Subotic na Marcel Schmelzer, kuwa majeruhi na kuenguliwa katika michuano hiyo ya Ulaya.
Hata hivyo, kuna habari njema kutokana na beki wa kulia Lukasz Piszczek Jumamosi kurejea uwanjani baada ya kupona majeraha yaliyokuwa yakimkabili majira ya joto.

Napoli nayo yashikwa
Napoli nayo kimatokeo haikufanya vizuri baada ya kupoteza mechi zao mbili zilizopita za Serie A tena bila kufunga, awali ilikubali kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Juventus wiki mbili zilizopita na kisha Jumamosi ikanyukwa nyumbani bao 1-0 dhidi ya Parma.
Kocha Rafael Benitez alibadili kikosi chake dhidi ya Parma, sera ambazo zilizua maswali mengi katika vyombo vya habari, hivyo kushuhudia timu yake ikilala kwa bao la usiku la Antonio Cassano.
Hofu kubwa ni mshambuliaji Marek Hamsik, ambaye aliingia dakika 10 za mwisho na kuumia unyayo, hivyo ataikosa Dortmund leo.
Benitez alilalamikia mapumziko ya mechi za kimataifa. "Tumefanya makosa mengi, lakini ni vigumu kufanya vizuri kwa muda mfupi kama huo," alisema.
"Tunapoteza mipira kirahisi, tunaruhusu nafasi nyingi za kuchezewa mashambulizi ya kushtukiza na kupoteza nafasi chache za kusonga mbele kwa  Gonzalo Higuain na Goran Pandev.
"Sishangai kwa Borussia kufungwa na Bayern. Ninayaangalia zaidi matokeo yetu kuliko Borussia. Tayari tunaelekeza akili zetu katika mechi inayofuata."

Cazorla aionya Arsenal kwa Marseille
Licha ya Arsenal leo kuwa nyumbani kwenye dimba lao la Emirates ikicheza dhidi ya vibonde Olympique Marseille, haitahitaji kulala kwenye mchezo huo.
Miamba hiyo inayoongoza Kundi F ikiwa juu ya Napoli kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa huku ikiizidi Borussia Dortmund kwa pointi sita, kama itafanikiwa kuifunga Marseille na Wajerumani hao wakashindwa kuifunga Napoli, kikosi hicho cha Arsene Wenger kitakuwa kimejihakikishia nafasi ya kucheza hatua ya mtoano.
Kiungo Santi Cazorla ameonya kutobweteka katika mechi hiyo wakati huu wakiwa bado wana safari ya kwenda Napoli, kuhitimisha safari yao ya hatua ya makundi.
"Tatizo kubwa ni kwamba, kila mmoja anafikiri itakuwa mechi rahisi kwetu kushinda," Mhispania huyo aliiambia tovuti ya Arsenal (www.arsenal.com) baada ya ushindi wa 2-0 walioupata Jumamosi dhidi ya Southampton, uliowafanya kuendelea kukaa kileleni mwa Ligi Kuu England.
"Hakuna wanalolitarajia Marseille kwa sababu hawana pointi yoyote, lakini watafanya mambo kuwa magumu kwetu. Itakuwa mechi ngumu na kama hatutakuwa makini tutashindwa kupata nafasi ya kusonga mbele.
"Tunapaswa kutambua kwamba ni mechi muhimu," alisema Cazorla. "Kama hatutapata matokeo mazuri, yatafanya mambo kuwa magumu kwetu kwani tutakapokwenda Napoli tutalazimika kushinda."
Marseille ililazimisha suluhu dhidi ya Arsenal zilipokutana Emirates miaka miwili iliyopita, lakini Klabu hiyo ya Ufaransa ina rekodi mbaya ikiwa England.
Ushindi pekee iliyopata katika mechi 11 za mashindano ilizocheza England, ulikuwa wa bao 1-0 dhidi ya Liverpool msimu wa 2007-08 katika mechi ya Ligi ya Mabingwam Ulaya hatua ya makundi na imepoteza mara sita.
Hata hivyo, Marseille itamtegemea Andre-Pierre Gignac baada ya mshambuliaji Dimitri Payet kuwa majeruhi wa goti. Mabingwa hao wa Ulaya wa 1993, pia watamkosa mshambuliaji Mghana Andre Ayew anayesumbuliwa na goti.

Basel v Chelsea, Barca na Ajax
Katika mechi nyingine itakayopigwa leo, Kundi E, Basel  itakuwa mwenyeji wa Chelsea wakati huo Steaua Bucharest ikiialika Schalke 04. Kundi G, Zenit St Petersburg itaialika Atletico Madrid  huku
FC Porto ikiwa nyumbani kuisubiri Austria Vienna.
Kundi H, Ajax Amsterdam itaisubiri  Barcelona wakati  Celtic ikiwa mwenyeji wa  AC Milan.

NIPASHE

Monday, November 25, 2013

Watano wamwaga wino Yanga, Yondani apongezwa


https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhNMyVKtqT3WPzKt5HLtbq8FHl6g9BGflumehITr8kvDY9vjdr_1M9tLapAVbNgQxWu6qwyoAPojN0fECt7CByEWUPeieZRpMl6r1ghkJ9IrBOdwR1nTYSsecyuKluImHFy2BgGWm6pKMU/s1600/Kelvin-Yondani-akiwa-katika-mazoezi-yna-timu-yake-mpya-ya-Yanga-baada-ya-kusajiwa-kwa-ajili-ya-msimu-ujao-wa-Ligi-Kuu-2012-131.jpg
Kelvin Yondani mmoja wa waliomwaga wino, akiwa pia ameula Kili Stars kwa kuteuliwa nahodha
WACHEZAJI watano wa timu ya Young Africans wameongeza mikataba ya muda mrefu ambapo sasa wataendelea kuitumikia klabu yenye maskani yake mitaa ya Twiga/Jangwani mpaka mwaka 2016, hili limefanywa na uongozi kwa mapendekezo ya benchi la ufundi.
Wachezaji ambao mpaka sasa wameshaongeza mikataba ya kuitumikia klabu ya Young Africans ni walinzi Kelvin Yondani (2014-2016), Nadir Haroub "Cannavaro" (2014-2016), kiungo Athuman Idd (2014-2016), mshambuliaji Saimon Msuva (2014-2016) na Jerson Tegete (2014-2016). 
Mwenyekiti wa kamati ya usajili wa klabu ya Young Africans Abdallah Bin Kleb amesema hao ni baadhi tu ya wachezaji ambao wameshamaliza taratibu zote na kusaini mikataba mipya itakayowafanya waitumikie Yanga mpaka mwaka 2016.
"Tupo katika mazungumzo ya mwisho na wachezaji wetu wengine, mazungumzo yanaendelea vizuri na tunaamini muda si mrefu nao tutakua tumeshamalizana nao ili waweze kuendelea kuitumika Yanga tena kwa muda mrefu "alisema Bin Kleb.
Wakati huo huo kikosi cha Young Africans leo kimeanza mazoezi asubuhi katika uwanja wa Bora - Mabatini Kijitonyama kujiandaa na mchezo wa hisani dhidi ya Simba SC Disemba 14, 2013, mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom pamoja na mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika.
Aidha Uongozi wa klabu ya Young Africans unampa pongezi beki wake wa kati Kelvin Patrick Yondani mchezaji bora wa mwaka 2012/2013 kwa kuteuliwa kuwa nahodha mpya wa timu ya Taifa Tanzania bara (Kilimanjaro stars) inayokwenda kushiriki mashindano ya Chalenji jijini Nairobi.
Kelvin Yondani ametambulishwa rasmi leo na kocha mkuu wa timu ya Taifa Kim Poulsen kwa waandishi wa habari  katika hafla ya kuwaaga wachezaji wa timu ya Taifa wanaokwenda nchini Kenya katika hoteli ya Accomondia eneo la gerezani jijini Dar es salaam.
Tunapenda kumpa pongezi kijana wetu, mchezaji wetu Yondani kwa kupewa nafasi hiyo kubwa katika timu ya Taifa, tunamtakia kila la kheri na awe kiongozi bora kwa wachezaji wenzake na kuiwakilisha vizuri nchi yetu na timu yake ya Young Africans.

Young Africans Official Website

Unyama! Mwanamke achomwa kisu na kuuwawa na mumewe wodini, kisa....!

Gervas Kadaga(25) anayetuhumiwa kumuua mkewe akiwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya.

MAMA mkubwa wa Gervas aliyejitambulisha kwa jina la Martha Lugenge alisema kuwa vijana hawa walikutana Madibila kila mmoja akiwa katika shughuli zake ndipo walipoamua kuishi pamoja.


MWANAMKE mkazi wa kijiji cha Mahango kata ya Madibila wilayani Mbarali mkoani Mbeya aliyefahamika kwa jina la Jitihada Mamga(20) ameuawa kwa kuchomwa kisu na mumewe aliyefahamika kwa jina Gervas Kadaga(25) ambaye pia ni mkazi wa kijijini hapo.


Tukio hilo limetokea Novemba 21 majira ya saa 1:00 jioni baada ya kutokea ugomvi baina ya wapenzi hao ambapo marehemu alikutwa na majeraha tisa ya kisu katika sehemu mbalimbali za mwili wake.


Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Bw. Diwani Athumani alisema kuwa marehemu alifia nyumbani kwake ambapo mtuhumiwa ambaye amelazwa katika hospitali ya Rufaa Mbeya naye amejeruhiwa kwa kuchomwa na kisu tumboni.


Hata hivyo Kamanda Athumani alisema kuwa hadi sasa hakijafahamika chanzo halisi cha ugomvi huo ambapo Jeshi la Polisi linaendelea kufanya uchunguzi wa tukio hilo huku mtuhumiwa akiwa amewekwa chini ya ulinzi wa polisi katika hospitali ya rufaa ya Mbeya alikolazwa.


Akizungumza katika hospitali ya rufaa alikolazwa mama mkubwa wa Gervas aliyejitambulisha kwa jina la Martha Lugenge alisema kuwa vijana hawa walikutana Madibila kila mmoja akiwa katika shughuli zake ndipo walipoamua kuishi pamoja.


Alisema yeye alipewa taarifa za tukio hilo siku inayofuata na kwamba alipofika alikuta ndugu wa marehemu wameuchukua mwili wa mtoto wao kwa ajili ya taratibu za mazishi na kwamba hajui chanzo cha ugomvi uliosababisha wapigane visu.


Mama huyo alisema kuwa vijana hao hawajawahi kupata mtoto na kwamba hawajaanza kuishi pamoja muda mrefu; 

''Wote ni watoto, kwani wameanza kuishi muda mrefu? wamekutana kila mmoja akiwa katika kazi zake, ndipo walipoanza kuishi kama mke na mume,''alisema.

Mbeya yetu

Wahitimu kidato cha nne waaswa kuepuka dawa za kulevya

Meza Kuu ikifuatilia maonyesho ya wahitimu wa kidato cha nne Mwandege Boys (hawapo pichani)
DC Mercy Sillah akihutubia
DC Mkuranga akiendelea kutoa nasaha zake kwa wahitimu na wazazi na walezi waliohudhuria mahafali ya tano ya Kidato cha nne Shule ya Mwandege Boys.

MKUU wa Wilaya ya Mkuranga, Mercy Sillah, amewaasa wahitimu ya Kidato cha Nne wa mwaka 2013 wasishawishike kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya kwa lengo la kupata utajiri wa haraka.
Aidha Mkuu huyo wa wilaya, aliwataka wazazi na walezi kusaidia kuwalea watoto wao kwa maadili ya kidini ili kulisaidia taifa kuwa na vijana waadilifu ambao watalisaidia taifa.
Akizungumza kwenye Mahafali ya Tano ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari ya Mwandege Wavulana, DC Mercy, alisema kumekuwa na wimbi kubwa la vijana wengi kuingia tamaa ya kutajirika na kujihusisha na dawa za kulevya kitu alichodai ni hatari kwa taifa.
Alisema kutokana na hilo wahitimu wa shule hiyo na wengine nchini wanapaswa kuepuka vishawishi na tamaa za njia ya mkato ya maisha na badala yake wajikite katika kujiendeleza kielimu na kudumisha nidhamu walizokuwa nazo shuleni ili wafanikiwe maishani.
"Dawa za Kulevya zimekuwa ni kishawishi kibaya kwa sasa kwa vijana wetu, msijiingize huko mkaharibu maisha yenu, jiendelezeni na tumieni nidhamu mliyojengewa kujitengenezea maisha mazuri, mkikaa bure ni rahisi shetani kuwaingiza majaribuni," alisema.
DC Mercy aliwakumbusha kuwa pia kuzingatia sheria za nchi sambamba na kutambua kuwa kuhitimu kidato cha nne siyo kumaliza kila kitu, kwani wana fursa ya kujiendeleza kwa masomo ya juu ya sekondari au ufundi ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kujiajiri.
Mkuu huyo wa wilaya aliwakumbusha wazazi na walezi kuvitambua na kuviendelezxa vipaji vya watoto wao, sambamba na kuwalea kwa malezi bora na mazuri yanayozingatia maadili na mafunzo ya kidini ili kuwajenga kimaadili na uchaji Mungu kwa vijana hao.
Naye Mkuu wa Shule ya Mwandege Wavulana, Mwl Enock Walter, kupitia risala aliyosoma aliomba serikali kuacha kufanya majaribio katika elimu kwa kila anayeingia madarakani kujaribu mambo yake na kuacha mengine aliyoyakuta kwani yanayumbisha elimu nchini.
"Kufanya majaribio katika elimu ni kuliua taifa, utashi na maamuzi ya wanaoingia madarakani kama ilivyotokea siku za nyuma kwa kufutwa kwa baadhi ya masomo na kisha kurejeshwa kunatuyumbisha watu wa chini hasa walimu kuzalisha wasomi wazuri wa kulisaidia taifa," alisema.
Katika mahafali hayo wahitimu 105 walitunukukiwa vyeti na kuzawadiwa kwa waliofanya vyema katika masomo yake shuleni hapo na mwanafunzi Marijani Karanda, aliibuka kidedea kwa kuongoza katika masomo sita kiasi cha kumfanya DC Mercy kumzawadia fedha taslimu.

Shule ya Mwandege Boys yatoa msaada wa vitabu vya Sh Mil 3 Mwandege SM


Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Mercy Sillah (kushoto) alianza kwa kusalimiana na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwandege., Joseph Awino kabla uya makabidhiano ya vitabu hivyo. Picha ni hatua kwa hatua mpaka vitabu hivyo vyenye thamani ya Sh. Milioni Tatu vilipokabidhiwa.










UONGOZI wa Shule ya Sekondari ya Mwandege Wavulana iliyopo Mkurunga, Pwani imetoa msaada wa vitabu mbalimbali vyenye thamani ya Sh. Milioni Tatu kwa Shule ya Msingi ya Mwandege ili kusaidia na kukuza kiwango cha taaluma kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Vitabu hivyo vinavyohusisha kamusi na vile vya masomo mbalimbali kwa Shule ya Msingi vilikabidhiwa juzi kwa shule hiyo katika sherehe za mahafali ya tano  ya kidato cha nne ya Shule ya Mwandede Wavulana yaliyofanyika jana katika shule yao wilayani humo.
Mkuu wa Shule wa Mwandede Wavulana, Enock Walter, alisema uongozi wa Shule yao chini ya Bodi ya Wakurugenzi wametoa vitabu hivyo kwa lengo la kusaidia kuinua kiwango cha elimu kwa wanafunzi wa shule ya Mwandege ambayo ipo jirani nayo.
Mwl Walter, alisema kwa kuwa wao ni wadau wakubwa wa elimu na wanatambua kufanya vyema kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi ni kuzisaidia Shule za Sekondari kupata wanafunzi bora ndiyo maana wamejitolea kutoa zawadi hiyo aliyoamini itasaidia japo ni ndogo.
Mkuu wa wilaya ya Mkuranga, Mercy Sillah, aliyevikabidhi vitabu hivyo kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwandege, Joseph Awino, alisema kilichofanya na uongozi wa Shule ya Mwandege Wavulana ni mfano wa kuigwa na wadau wengine wa elimu nchini.
DC huyo, alisema lau wadau wengine wa elimu wangekuwa wakifanya kama ilivyofanya Shule ya Mwandege Wavulana ni wazi kiwango cha elimu ya Tanzania kingepaa, huku akifichua miongoni mwa shule za msingi wilayani humo zinazofanya vyema ni Mwandege.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwandege, Joseph Awino aliishukuru shule ya Mwandege Wavulana kwa msaada huo na kuahidi kuvitumia kwa lengo la kuongeza kiwango cha elimu na ufaulu kwa wanafunzi wake zaidi na ilivyo sasa.
"Tunashukuru kwa msaada huu na Mungu awazidishie Mwandege Boy's na tunaahidi kutumia vitabu hivyo kama vilivyokusudiwa kwa lengo la kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wetu ambao baadhi wanaweza kusoma hapa, ahsanteni sana," alisema Mwl Awino.

Kili Stars yaagwa, wachezaji waahidi makubwa Chalenji 2013

Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa Henry Lihaya,(kulia) akipeana mkono na kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen kwenye hafla kukabimkabidhi bendera kwa Kilimanjaro Stars inayokwenda kushiriki mashindano ya Chalenji yanayotarajiwa kuanza kesho nchini Kenya. Katikati ni nahodha wa Kilimanjaro Stars Kelvin Yondani. 

Wachezaji wa Kilimanjaro stars
Nahodha mpya wa Kili Stars, Kelvin Yondani 'Vidic' akizungumza huku kocha wake, Kim Poulsen akisikiliza kwa makini
Hiki ndicho kikosi cha Kili Stars
Kikosi cha Kilimanjaro Stars imeagwa leo tayari kwa safari ya Nairobi, Kenya kushiriki michuano ya Kombe la Chalenji inayoanza kutimua vumbi Novemba 27 mwaka huu.
Hafla ya kuiaga timu hiyo imefanyika saa 5 asubuhi kambini kwao katika hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam. Msafara wa Kilimanjaro Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager unaongozwa na Ahmed Idd Mgoyi. Timu itaondoka saa 10 alasiri kwa ndege ya RwandAir.
Wachezaji waliomo katika msafara huo ni makipa Deogratius Munishi (Yanga), Ivo Mapunda (Gor Mahia, Kenya) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Erasto Nyoni (Azam), Himid Mao (Azam), Ismail Gambo (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Michael Pius (Ruvu Shooting) na Said Moradi (Azam).
Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Ramadhan Singano (Simba) na Salum Abubakar (Azam).
Safu ya ushambuliaji inaundwa na Elias Maguli (Ruvu Shooting), Faridi Musa (Azam), Joseph Kimwaga (Azam), Juma Liuzio (Mtibwa Sugar), Mbwana Samata (TP Mazembe, DRC), Mrisho Ngasa (Yanga) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC).
Hata hivyo, washambuliaji Samata na Ulimwengu watajiunga na timu hiyo jijini Nairobi, Desemba Mosi mwaka huu wakitokea Lubumbashi ambapo Novemba 30 mwaka huu TP Mazembe itacheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Benchi la Ufundi la timu hiyo linawajumuisha Kim Poulsen (Kocha Mkuu), Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa Makipa), Leopold Tasso (Meneja wa Timu), Dk Mwanandi Mwankemwa (Daktari wa Timu), Frank Mhonda (mtaalamu wa tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza Vifaa).
Kilimanjaro Stars ambayo ipo kundi B katika michuano hiyo itacheza mechi yake ya kwanza Novemba 28 mwaka dhidi ya Zambia kwenye Uwanja wa Machakos.

Sunday, November 24, 2013

Real Madrid yaijibu Barca, Atletico Madrid ikifanya kufuru La Liga

Fabregas akifunga mkwaju wake wa penati jana
Ronaldo akielekea kufunga bao la kwanza la Real Madrid kabla ya kutolewa kwa maumivu
Teamwork: Neymar and Marc Batra celebrate with the former Arsenal midfielder
Barca wakipongezana
RAUL GARCIA KOKE ATLETICO MADRID GETAFE LIGA BBVA 11232013
Villa na Garcia wa Atletico Madrid wakishangilia mabao yao ya jana. Kila mmoja kati ya wawili hao alifunga mabao mawili
WAKATI Real Madrid ikijibu mapigo kwa mahasimu wao Barcelona waliotangulia kushinda mabao 4-0 kwa kuichakaza Almeria kwa magoli 5-0, Atletico Madrid ilifanya kufuru zaidi kwa kutoa kisago cha mabao 7-0 katika Ligi ya Hispania.
Madrid ilipata ushindi huo ugenini kupitia kwa mabao ya Cristiano Ronaldo aliyefunga bao la mapema la dakika ya tatu tu ya mchezo kabla ya kutolewa uwanjani kwa kuumia.
Mabao mengine yalifungwa na Karim Benzema dakika ya 61 pasi ya Jese Rodriguez kabla ya Gareth Bale kufunga bao la tatu dakika ya 71,  Isco akaongeza la nne na Alvaro Morata akahitimisha karamu ya mabao dakika ya 81.
Mapema Barcelona waliifumua timu ya Grenada kwa mabao 4-0 bila ya kuwa na nyota wake, Lionel Messi aliye majeruhi.
Magoli ya penati ya Andres Iniesta na nahodha wa zamani wa Arsenal, Cesc Fabregas yaliipa uongozi Barcelona kabla ya kuongeza mengine mawili kupitia kwa Alex Sanchez na Pedro kuifanya Barca iendeleze rekodi ya kushinda mechi mfululizo.
Hata hivyo ni Atletico Madrid walifanya kufuru usiku wa manane wa leo baada ya kuifumua Getafe kwa mabao 7-0 na kuzidi kung'ang'ania katika nafasi ya pili ya msimamo wa La Liga ikifikisha pointi 37,
Raul Garcia na David Villa walifunga mara mbili, huku Diego Costa, Adrian na lile la kujifunga la Lopo lilitosha kuifanya Atletico kuifukizia Barca inayoongoza kwa pointi 40, tatu pungufu na ilizonazo klabu hiyo.

Saturday, November 23, 2013

TFF yaunda kamati zake ndogondogo, Zitto Kabwe, Wilfred Kidao waula

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametangaza wajumbe wa kamati ndogongo (standing committees) wakati zile za haki (judicial organs) na uchaguzi zitaundwa baadaye.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika leo (Novemba 23 mwaka huu) jijini Dar es Salaam, Rais Malinzi alisema kamati hizo zimeundwa kwa mujibu wa katiba ili kuisaidia Kamati ya Utendaji.

Pia ametangaza wajumbe wanne wa Kamati ya Utendaji aliowateua. Wajumbe hao ni Richard Sinamtwa na Ramadhan Nassib, wakati wengine wanaoingia moja kwa moja kwenye Kamati ya Utendaji kutokana na kamati wanazoziongoza ni Dk. Paul Marealle na Saloum Umande Chama.

Kamati ya Fedha na Mipango inaongozwa na Makamu wa Rais wa TFF, Wallace Karia wakati wajumbe ni Francis Ndulane (Makamu Mwenyekiti), Omari Walii, Eliud Mvella, Said Muhammed, Geofrey Nyange, Kidao Wilfred, Ayoub Nyenzi, Lina Kessy na Cyprian Kuhyava.

Geofrey Nyange anaongoza Kamati ya Mashindano wakati wajumbe ni Clement Sanga (Makamu Mwenyekiti), Msafiri Mgoyi, James Mhagama, Mohamed Nassoro, Moses Katabaro, Seif Ahmed, Gerald ambi, Davis Mosha, Said George na Nassoro Idrissa.

Kinara wa Kamati ya Ufundi ni Kidao Wilfred wakati wajumbe ni Athumani Kambi (Makamu Mwenyekiti), Vedstus Lufano, Blassy Kiondo, Rahim Kangezi, Patrick Kahemele, Daud Yassin, Nicholas Mihayo na Dk. Cyprian Maro.

Kamati ya Mpira wa Miguu wa Vijana inaongozwa na Ayoub Nyenzi, Khalid Abdallah (Makamu Mwenyekiti), Ali Mayay, Mulamu Ng’hambi, Apollo Kayungi, Said Tully, Luteni Kanali Charles Mbuge, Lameck Nyambaya na Ibrahim Masoud.

Lina Kessy anaongoza Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake wakati wajumbe ni Shyrose Bhanji (Makamu Mwenyekiti), Zena Chande, Amina Karuma, Dk. Cecilia Makafu, Zafarani Damoder, Beatrice Mgaya, Sofia Tigalyoma, Martin Mung’ong’o na Engrid Kimaro.

Kamati ya Waamuzi inaongozwa na Saloum Umande Chama, Nassoro Said (Makamu Mwenyekiti), Charles Ndagala (Katibu), Riziki Majala, Kanali Isaro Chacha, Paschal Chiganga, Victor Mwandike, Soud Abdi na Zahra Mohamed.

Hamad Yahya Juma ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi anaongoza Kamati ya Habari na Masoko wakati wajumbe ni Naibu Waziri January Makamba (Makamu Mwenyekiti), Tido Mhando, Yusuf Manji, Yusuf Bakhresa, Samwel Nyalla, Jack Gotham, Fredrick Mwakalebela na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA).

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji inaongozwa na Richard Sinaitwa, Moses Karuwa (Makamu Mwenyekiti), Zacharia Hanspoppe, Hussein Mwamba, Philemon Ntahilaja, Abdul Sauko na Imani Madega.

Kiongozi wa Kamati ya Ukaguzi wa Fedha ni Ramadhan Nassib wakati wajumbe ni Zitto Kabwe (Makamu Mwenyekiti), Nicholas Magarinza, Jackson Songora, Epaphra Swai, Kalilo Samson, Goodluck Moshi, Golden Sanga na Elias Mwanjala.

Dk. Paul Marealle anaongoza Kamati ya Tiba wakati wajumbe ni Dk. Fred Limbanga (Makamu Mwenyekiti), Dk. Mwanandi Mwankemwa, Dk. Nassoro Matuzya, Dk. Eliezer Ndelema na Asha Sadick.

TFF yamrejesha Rage madarakani yamtaka aitishe mkutano wa dharura

Rais wa TFF, Jamal Malinzi aliyetoa taarifa za Mwenyekiti wa Simba Ismail Aden Rage aitishe mkutano haraka baada ya awali kupiunduliwa na wajumbe wa kamati ya utendaji ya klabu yake akiwa nje ya nchi
MWENYEKITI  wa Simba, Ismail Aden Rage ameagizwa kuitisha Mkutano Mkuu wa Dharura wa klabu ndani ya siku 14 kuanzia sasa.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa agizo hilo baada ya kubaini kuwa mgogoro katika klabu baada ya kupokea barua mbili; moja kutoka Kamati ya Utendaji ikielezea kumsimamisha uongozi Rage, na nyingine kutoka kwa Mwenyekiti huyo ikielezea kutotambua kusimamishwa huko.

Uamuzi wa TFF umefanywa kwa kuzingatia Ibara ya 1(6) ya Katiba ya Simba inayosema: 
 
“Simba Sports Club ni mwanachama wa TFF, itaheshimu Katiba, kanuni, maagizo na uamuzi wa TFF na FIFA, na kuhakikisha kuwa zinaheshimiwa na wanachama wake.”

TFF itatuma wawakilishi wake katika mkutano huo, na kumuagiza Mwenyekiti wa Simba kuhakikisha wanachama wote wenye hoja wanapata fursa ya kusikilizwa.

Mahafali ya Tano ya Kidato cha Nne Mwandege Boy's yalivyofana leo Mkuranga

Wanafunzi waliosalia shuleni wakisimama kumpokea mgeni rasmi
Hata wazazi na walezi nao walisimama wima
Pre Form One nao walikuwapo katika mahafali hayo
Wanafunzi wa kidato wa tatu wakionyesha onyesho la lugha ya Kiswahili kusherehesha mahafali hayo ya leo
Baadhi ya wahitimu wa Kidato cha nne wakiwa wametulia vitini
Mwandege Boys kuna vipaji vya uigizaji usipime!
Yaani ni Full Kidigitali Mwandege Boys
Igizo likiendelea kuhusiana na umuhimu wa kuzingatia masomo shuleni
Hata Bongo Movie hawaoni ndani kwa madogo hawa, vipaji vitupu
Wahitimu wa kidato cha Nne Jesse na Godwin wakisoma taarifa ya habari hawa jamaa nouma

Hashim Abdallah (kulia) akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wa kidato cha nne

Wanafunzi wa kidato cha nne wakitumbuiza
Leo tunawaaga kwaherini tuliwazoea kaka zetu, ndivyo wanavyoimbiwa wahitimu waliokaa na wanafunzi wenzao wa kidato cha tatu
Yaani ni full burudani


Mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Mhe. Mercy Silla (wa pili kulia) akiwasili eneo la tukio akisindikizwa na Mkuu wa Shule, Mwl Enock Walter (kulia)


Meza kuu ikishuhudia vipaji vya wanafunzi wa Mwandege Boys Sec
Mashairi nayo yalisomwa kuwaaga wahitimu
Mmoja wa wazazi akitoa nasaha zake

Mzazi wa kiume naye alitoa nasaha zake.
Mkuu wa Shule ya Mwandege Boys, Mwl Enock Walter akisoma risala

Mgeni Rasmi Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Mercy Sillah akisoma risala yake ambapo aliwataka wahitimu kutojiingiza kwenye kishawishi cha biashara za dawa za kulevya kwa nia ya kutaka utajiri wa haraka badala yake wakomalie kujiendeleza kimasomo na kutumia vipaji walivyonayo kujiletea mafanikio maishani mwao.
Mgeni rasmi (kushoto) akimkabidhi Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwandege, Joseph Awino sehemu ya vitabu vilivyotolea na uongozi wa Shule ya Mwandege Boys kwa shule hiyo ya msingi ili kusaidia kukuza taalum

Mwanafunzi wa Pre Form One, Benard Deogratius aliyefanya vizuri katika masomo yake hayo akikabidhiwa zawadi na Mgeni rasmi

Mhitimu akikadhiwa cheti chake
 

Hata walimu nao walitunukiwa vyeti kwa kufanya vyema shuleni MwandegeBoys Sec

Mmoja ya wahitimu akikabidhiwa cheti na DC Mercy Sillah