STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, April 15, 2014

Azam yawekwa rekodi saba Tanzania Bara

Mabingwa wa Tanzania Bara, Azam Fc
TIMU ya Azam ambayo juzi ilitwaa ubingwa wa Tanzania Bara kwa msimu wa 2013/14, imeweka rekodi saba kwenye medani ya soka nchini.
Azam iliifunga Mbeya City mabao 2-1 kwenye uwanja wa Sokoine na kuweka rekodi ya kuwa timu pekee iliyoifunga timu hiyo kwenye uwanja wake wa nyumbani.
Awali, Mbeya City ilikuwa haijawahi kufungwa kwenye uwanja wake wa nyumbani kabla ya rekodi yake kuvunjwa na Azam.
Mabingwa hao wameifikia pia rekodi ya Simba ya kutwaa ubingwa bila ya kupoteza mechi ya msimu wa 2009/10 na sasa wanafukuzia rekodi nyingine ya 'Wekundu wa Msimbazi' ya kumaliza msimu bila ya kupoteza mechi wakati watakapowakabili JKT Ruvu katika mechi yao ya mwisho ya msimu.
Mbali na hilo, pia wameweka rekodi ya kuwa timu ya tisa kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara tangu ligi hiyo ilipoanza.
Azam pia imekuwa ni timu ya saba kutwaa ubingwa huo nje ya miamba wawili wa soka nchini ambao wamekuwa wakipokezana ubingwa huo, Simba na Yanga.
Timu nyingine ambazo zimeshawahi kufanya hivyo, nazo ni Cosmopolitan ya Dar es salaam mwaka 1967, Mseto Sports ya Morogoro (1975), Pan African (1982), Tukuyu Stars (1986), Coastal Union (1988) na Mtibwa Sugar mwaka 1999 na 2000.
Rekodi nyingine ni kuwa timu ya tano kutoka jijini Dar es Salaam kutwaa ubingwa wa Bara, ikizifuata timu za Simba, Yanga, Cosmopolitan na Pan African.
Lakini vile vile Azam imekuwa ni timu ya kwanza kutoka nje ya Manispaa ya Ilala kutwaa ubingwa kwani timu za Simba, Yanga, Cosmopolitan na Pan African zinatoka Ilala, huku yenyewe ikitokea Temeke.
Vile vile imekuwa ni timu ya pili ya kampuni kutwaa ubingwa nchini baada ya Mtibwa Sugar kufanya hivyo mwaka 1999 na 2000.
Timu hiyo imetwaa ubingwa kwa pointi 59 ambazo hazitafikiwa na timu yoyote kwenye mechi ya kuhitimisha Ligi Kuu Jumamosi.
Wakati huo huo, Sanula Athanas, anaripoti kuwa wadhamini wakuu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania, wameipongeza Azam FC kwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo msimu huu msimu ikiwa ni mara ya kwanza tangu ipande miaka saba iliyopita.
Azam inayonolewa na Mcameroon Joseph Omog ilitwaa ubingwa huo juzi baada ya kuifunga Mbeya City 2-1 katika raundi ya 25 ya ligi hiyo na kufikisha pointi 59 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote msimu huu.
Mara tu baada ya kumalizika kwa mechi hiyo kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini Mbeya juzi, Meneja Uhusiano wa Nje wa kampumi hiyo, Salum Mwalim alisema wameridhishwa na kiwango cha Azam FC pamoja na timu zote zinazoshiriki katika ligi na hivyo wanawapongeza kwa dhati timu hiyo kutwaa taji.
"Tunawapongeza Azam kwa kuwa bingwa mpya wa VPL kwa sababu wamekabiliana vema na mikikimikiki ya ligi, hivyo ubingwa wao haukuwa mwepesi kuupata kutokana na ushindani uliokuwapo kwa timu zote shiriki," alisema Mwalim.
"Tunaamini ubingwa huu wa Azam utaifanya ligi msimu ujao kuwa ngumu zaidi kwani timu za Yanga na Simba ambazo zimekuwa zikipokezana ubingwa tangu 2001 zitataka kurudisha heshima yao na nyingine zikipata nguvu kwa kuwa yoyote inaweza kuwa bingwa, na hilo likitokea ubora wa ligi yetu utazidi kupaa," alisema zaidi Mwalim.
Alisema Azam watakabidhiwa kombe lao la ubingwa Jumamosi kwenye uwanja wao wa nyumbani, Chamazi jijini Dar es Salaam wakati wa mechi yao ya mwisho dhidi ya JKT Ruvu.
Aidha Mwalim amezipongeza timu zote 14 zilizoshiriki ligi hiyo kwa kujituma na kutoa changamoto katika kila mechi jambo lililofanya bingwa kutopatikana kwa urahisi na mapema.

Taswira katika msiba wa Gurumo













Monday, April 14, 2014

Idadi ya waliokufa kwa mafuriko yaongezeka

Baadhi ya nyumba zilizozungukwa na maji


IDADI ya waliokufa kutokana na mafuriko jijini Dar es Salaam imefikia watu 13 kufikia Jumatatu.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Sadiq Meck Sadiq amesema idadi hiyo huenda ikaongezeka baada ya kupata taarifa za matukio ya mafuriko kutoka maeneo yote ya mkoa wa Dar es Salaam.
Kwa siku tatu mfululizo tangu Ijumaa iliyopita, mvua kubwa ziliendelea kunyesha na kusababisha madhara makubwa vikiwemo vifo, uharibifu wa miundombinu ya barabara na madaraja, hivyo kukata mawasiliano na mikoa ya jirani ya Pwani na Morogoro na hata ndani ya mkoa wenyewe. Karibu maeneo yote ya mkoa wa Dar es Salaam yameathirika kutokana na mvua kubwa zilizonyesha na kusababisha mafuriko, huku wakaazi wa maeneo ya mabondeni wakiathirika zaidi baada ya nyumba zao kujaa maji. Miundombinu ya barabara na madaraja mbalimbali yanayounganisha jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake pia imeharibiwa.
Picha ya Anga ya mafuriko jijini Dar
Mradi mwingine muhimu wa mabasi yaendayo kasi, DART unaolenga kutatua tatizo la usafiri jijini Dar es Salaam, nao umeathiriwa na mafuriko hayo ambapo magari, mashine na mifuko ya saruji imechukuliwa na maji hivyo kusitisha shughuli zake za ujenzi zilizo katika hatua za mwisho za kukamilisha mradi huo.
Shughuli za urejeshaji wa miundombinu zimekuwa zikiendelea ikiwa ni pamoja na matengenezo katika daraja la Mpiji linaloiunganisha mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Hata hivyo Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania, TMA, yametahadharisha kuhusu kuendelea kunyesha kwa mvua na kuwataka watu wanaoishi katika maeneo hatarishi kuhama ili kusalimisha maisha na mali yao.
BBC

Kocha Azam kicheko kitupu baada ya ubingwa

Kocha Joseph Omog (kushoto) toka Cameroon akiwa na msaidizi wake
KOCHA Mcameroon, Joseph Marius Omog amefurahia ushindi wa jana wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji Mbeya City Uwanja wa Sokoine ulioihakikishia ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara timu yake, Azam FC, lakini amewaambia wachezaji wake, pati ni baada ya mechi ya mwisho Aprili 19, mwaka huu.

“Ni furaha sana, tumepambana sana, haikuwa kazi nyepesi, tumepitia mechi ngumu tangu naanza kazi hapa, lakini tulibaki kwenye dhamira yetu na tukaendelea kupambana hatimaye tumetimiza malengo. Sote tuna furaha sasa, kila mtu ana sababu ya kufurahia kazi yake kati yetu,”alisema Omog.

Omog amewataka wachezaji wake kutobweteka na matokeo ya jana, na badala yake waelekeze nguvu zao katika mchezo wa Aprili 19, ili washinde na kukabidhiwa Kombe kwa furaha. 

“Nasikia Yanga walikata rufaa, hata kama haina maana, lakini lazima tushinde mechi ya mwisho, wachezaji wangu wanajua hilo, nimewaambia,”alisema.

Mabao ya Gaudence Mwaikimba na John Bocco ‘Adebayor’ kila kipindi jana yalitosha kuihakikishia Azam FC ubingwa wa Ligi Kuu Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya dhidi ya bao la Mwagane Yeya.

Ushindi huo, umeifanya Azam ifikishe pointi 59 ikiwa na mchezo mmoja mkononi ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote baada ya mechi za mwisho Aprili 19, mwaka huu.

Nafasi ya pili tayari ni Yanga SC yenye pointi 55 sasa baada ya jana kuifunga JKT Oljoro 2-1 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha ambayo kama itawafunga pia na Simba SC wiki ijayo itafikisha pointi 58, ambazo haziwezi pia kufikiwa na timu za chini
yake.

Azam FC itacheza mechi ya mwisho nyumbani, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam Jumamosi wiki hii, dhidi ya JKT Ruvu ikiwa na dhamira ya kushinda ili kuweka rekodi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu bila kupoteza mechi.

Kikosi cha Azam kinaondoka leo Saa 10:00 mjini Mbeya kwa ndege kurejea Dar es Salaam na wachezaji watapewa mapumziko ya siku moja kabla ya kukutana kwa maandalizi ya mchezo wa kufungia pazia la msimu. 

LIWAZO ZITO

Rais JK naye amlilia Mzee Gurumo

Rais Jakaya Kikwete akimpongeza Mzee Gurumo enzi za uhai wake baada ya kumkabidhi tuzo maalum ya mchango wake kwa taifa kupitimia muziki
RAIS Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kutokana na kifo cha mwanamuziki maarufu na wa siku nyingi, Muhidini Gurumo kilichotokea juzi mjini Dar es Salaam.

Gurumo alifariki dunia jana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya ugonjwa wa moyo uliomsumbua kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Rais Kikwete alisema mchango wa marehemu Gurumo kwa Taifa ni mkubwa na wa kupigiwa mfano kupitia kipaji alichojaaliwa na Mwenyezi Mungu ambacho alikitumia kikamilifu kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla.

“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa na taarifa za kifo cha Gurumo ambaye alikuwa mmoja wa wasanii wa muziki wa dansi nchini waliolitumikia Taifa hili kwa bidii tangu miaka ya sitini kupitia sanaa ya muziki,

Katika bendi mbalimbali za muziki wa dansi kuanzia Bendi ya NUTA Jazz, Mlimani Park Orchestra, Orchestra Safari Sound (OSS) na Msondo Ngoma ambayo ameitumikia hadi alipostaafu mwaka 2013,”alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alimuomba Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kumfikishia salamu zake za rambirambi na pole nyingi kwa familia ya marehemu Gurumo kwa kumpoteza kiongozi na mhimili wa familia yao.

Alisema anaungana na familia ya marehemu kuomboleza msiba huo mkubwa kwa kutambua kuwa msiba wao ni wa wote, na anamuomba Mwenyezi Mungu.

Aliwaomba wanafamilia ya marehemu kuwa na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha kuomboleza msiba wa mpendwa wao kwa kutambua kwamba yote ni mapenzi ya mola.

Man City yapata pigo kwa Yaya Toure

KLABU ya Manchester City imepata pigo baada ya kufahamika kuwa huenda kiungo wake mahiri Yaya Toure asicheze tena msimu huu baada ya kuumia katika mchezo dhidi ya Liverpool uliochezwa mwishoni mwa wiki katika Uwanja wa Anfield. 
Nyota huyo wa kimataifa wa Ivory Coast alitolewa nje wakati wa kipindi kwanza na kusababisha hali kuwa mbaya kwa kikosi chake na kupelekea kufungwa mabao 3-2 na mahasimu wao hao katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu. 
Akihojiwa kuhusiana na hali ya nyota huyo, kocha wa City Manuel Pellegrini amesema itakuwa ngumu kwa mchezaji huyo kumaliza msimu huu. 
Toure alijiumiza mwenyewe baada ya kupiga shuti lililopaa katika mchezo huo wakati City wakijaribu kurejea baada ya kufungwa bao la kuongoza na Raheem Sterling.

Lyon yaidonyoa PSG kimoja Ufaransa

Mfungaji wa bao pekee la Lyon, Ferri (12) akipambana uwanjani dhidi ya PSG jana
MABINGWA watetezi wa Ligi ya Ufaransa, PSG jana ilionja kipigo chake cha kwanza baada ya mfululizo wa ushindi katika ligi hiyo kwa kudonyolewa goli 1-0 dhidi ya Olympique Lyon.
Ikicheza ugenini, PSG ilishindwa kufuruka kwa Lyon waliopata bao lao katika dakika ya 31 kupitia kwa Jordan Ferri.
Pamoja na kwamba kipigo hicho hakijaiteteresha matajiri hao wa Paris, lakini imefanya pengo la pointi baina ya wapinzani wanaowafukuzia kileleni, Monaco kuwa pointi 10 badala ya 13 ya awali baada ya Monaco kupata ushindi ugenini siku ya Jumamosi dhidi ya Rennes.
PSG imeendelea kusaliwa na pointi zake 79, huku Monaco wakiwa nafasi ya pili na pointi zao 69 huku timu zote zikiwa zimecheza michezo 33 na kusaliwa na mechi tano kabla ya kufungia msimu wa 2013-2014.

BASATA waomboleza kifo cha Gurumo


Mzee Gurumo enzi za uhai wake
BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa msanii nguli wa tasnia ya muziki wa Dansi nchini Muhidini Mwalimu Gurumo


“ Baraza limestushwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa ya kifo hiki cha Muhidini Maalimu Ngurumo ambaye mchango wake katika muziki wa dansi ni mkubwa mno na  unahitajika sana, pengo aliloliacha ni kubwa kwani ubunifu wake bado unahitajika katika tasnia hii.” 
Baraza linatoa pole kwa familia ya marehemu na wasanii wote nchini, aidha tunawatakia moyo wa subira katika wakati huu wa majonzi ya kuondokewa na mpendwa wetu.
Mwenyezi Mungu aipumzishe mahala pema peponi roho ya marehemu. Baraza liko pamoja na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Imetolewa na
Godfrey Mngereza
Kaimu Katibu Mtendaji

Baraza la Sanaa la taifa

Katibu Mkuu wa FIFA kutua Dar Mei 1

KATIBU MKUU WA FIFA KUFUNGUA SEMINA DAR
Katibu Mkuu wa FIFA

KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Jerome Valcke atawasili nchini Mei 1 mwaka huu ambapo atafungua semina ya mawasiliano itakayoshirikisha viongozi wa vyama wanachama wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
 
Akizungumza Dar es Salaam leo (Aprili 14 mwaka huu), Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema Valcke ambaye hii ni mara yake ya kwanza kuja Tanzania atafuatana na maofisa wengine wa saba wa FIFA.

Amesema semina hiyo iliyoandaliwa na FIFA itafanyika kwa siku mbili (Mei 1 na 2 mwaka huu) ambapo vilevile Valcke atapata fursa ya kuzungumza na waandishi wa habari wa ndani na wa kimataifa.

Rais Malinzi amesema washiriki wa semina hiyo ni marais, makatibu wakuu na wakuu wa mawasiliano wa wanachama 12 wa CECAFA ambao ni Burundi, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somali, Sudan, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda.

Naye Mwenyekiti wa CECAFA, Leodegar Tenga ambaye alifuatana na Katibu Mkuu wake Nicholas Musonye amemshukuru Rais wa TFF kwa kukubali kuwa mwenyeji wa semina hiyo kwani itasaidia katika maendeleo ya mpira wa miguu katika ukanda huu

Bomu jingine lalipuka jijini Arusha

Kijana ambaye hakufahamika jina lake baada ya kupata majeraha makubwa mguuni.

Hali ya sintofahamu iliyowakumba wakazi wa jiji la Arusha baada ya bomu kulipuka jana.
Majeruhi baada ya bomu kulipuka.
Mmoja wa majeruhi akiwa hoi baada ya mlipuko.
Taarifa kutoka mjini Arusha zinasema bomu la kutengenezwa kwa mkono lililipuliwa jana usiku April 13 kwenye Baada iitwayo Arusha Night Park, iliyopo eneo la Mianzini jijin i Arusha na kusababisha watu kadhaa kujeruhiwa, huku taarifa zingine zikisema watu wawili wamepoteza maisha katika mlipuko huo kwamba ni watu 15 wamejeruhiwa kwenye mlipuko huo.
Inaelezwa watu 15 walithibitishwa kuumia katika mlipuko huo wa tatu kutokea mkoani humo kwa kipindi cha mwaka mmoja baada ya tukio la mlipuko kanisani na kwenye mkutano wa CHADEMA na kupelekea vifo vya watu kadhaa.
Inaelezwa wengi wa majeruhi katika mlipuko huo wa jana ni wahudumu wa baa hiyo pamoja na waliojitokeza kuangalia mpira kqwenye truninga na kwamba walikimbizwa hospitali za Mount Meru, Seliani na St. Elizabeth kwa ajili ya matibabu zaidi.

Mzee Gurumo kuagwa na kuzikwa kesho

Mzee Gurumo enzi za uhai wake akiwa na mkewe kipenzi, Pili bint Said Kitwana

Waombolezaji wakiwa wamekusanyika nyumbani kwa marehemu Muhidin Gurumo maeneo ya Mabibo Makuburi, Dar es Salaam.
Mke wa marehemu Gurumo (kulia) akifarijiwa na baadhi ya jamaa zake kwenye msiba wa mumewe nyumbani kwake Makuburi.
MWILI wa gwiji wa muziki wa dansi nchini, marehemu Muhidin Gurumo 'Mjomba' unatarajiwa kuagwa rasmi kesho kuanzia saa 2 asubuhi kabla ya kusafirishwa kijijini kwao Masaki kwa ajili ya maziko yatakayofanyika mchana.
Awali ilipangwa marehemu Gurumo aliyefariki jana katika hospitali ya Muhimbili azikwe leo, ila kwa kuzingatia wosia ulioachwa na kusisitizwa na gwiji huyo enzi za uhai kuwa,  asiharakishwe kuzikwa mapema familia imeamua kutii wosia huo.
Akizungumza na MICHARAZO nyumbani kwa marehemu Gurumo, Mabibo External, Msemaji wa familia, Yahya Mikole alisema mara kadha Mzee Gurumo alikuwa akiwasisitiza kuwa atakapokufa asizikwe kwa haraka.
Mikole ambaye ni mdogo binamu wa marehemu alisema, Mzee Gurumo alikuwa akimwambia kwa kuwa yeye ni mwanamuziki mkubwa na maarufu kuharakishwa kuzikwa kwake kunaweza kuwanyima wengine kumuaga au kuhudhuria maziko yake.
"Kwa kuzingatia hilo na ombo toka serikali, tumeamua kusogeza shughuli za mazishi ya merehemu kutoka leo mpaka kesho kwa utaratibu wa kuagwa kuanzia saa 2-4 asubuhi kabla ya kuondoka kwenda kumpumzisha kijijini kwao majira ya saa 7 mchana," alisema Mikole.
Msemaji huyo alieleza marehemu alikuwa akisumbuliwa na tatizo la mapafu na uigonjwa wa moyo na juzi kabla ya kifo chake alipatwa na tatizo la ukosefu wa damu ambapo alipofikishwa Muhimbili aliwekewa chupa tatu za damu.
"Tatizo la ukosefu wa damu lilijitokeza juzi na aliwekewa chupa tatu zilizoisha asubuhi ya jana kabla ya alasiri kupoteza maisha, huku akionekana mwenye afya yake ya kawaida kabisa," alisema Mikole.
Mikole alisema taratibu za mazishi ya marehemu zinaendelea kama kawaida nyumbani kwa marehemu.
Kwenye msiba huo watu mbalimbali wakiwamo wanamuziki wa zamani na walio wahi kufanya kazi na marehemu walihudhuria kama akina Juma Ubao, Mjusi Shemboza, Karama Regesu na wengine.
Marehemu Gurumo aliyezaliwa mwaka 1940 ameacha mjane mmoja na watoto sita, watatu wa kiume ambao ni Abdallah, Omar na Mwalimu na wa kike pia wakiwa watatu ambao ni Mariam, ambaye ndiye mtoto mkubwa wa marehemu, Mwazani na Kibibi aliye wa mwisho kuzaliwa.
Hata hivyo wakati wa uhai wake alipozungumza na Mmiliki wa blogu hii alisema ana watoto wanne, lakini Msemaji huyo wa familia alifafanua mzee Gurumo 'alichepuka' ila hakupenda kuzungumzia suala la watoto wake hao wengine japo wanafamilia wanawatambua na wameshajulishwa msiba huo.

Julio amlilia Mzee Gurumo

Jamhuri Kihwelu 'Julio'
KOCHA maarufu wa soka na mdau mkubwa wa bendi ya Msondo Ngoma, Jamhuri Kihwelu 'Julio' amemlilia nguli wa bendi hiyo, Muhidini Gurumo akidai kifo chake ni pigo kwa familia, wadau wa muziki na michezo nchini.
Julio aliyewahi kuichezea na kuinoa Simba kabla ya kutua Mwadui-Shinyanga na kukaribia kuipandisha Ligi Kuu, alisema kifo cha Gurumo kwake ni pigo kubwa kwani alikuwa ni mjomba wake mbali na unazi wao wa Simba na Msondo.
Alisema yeye binafsi ameumia sana kwa msiba wa mwanamuziki na mwanachama huyo wa Simba kama ambavyo wadau wa fani za muziki na michezo walivyoumizwa na kudai ni vigumu kupatikana wa kuziba pengo lake.
"Kwa hakika nimeumia kama walivyoumia wadau wa michezo na muziki kwani enzi za uhai wake, Gurumo alikuwa mwanachama wa Simba na pia ni gwiji wa muziki ambaye hakuwa na mfano wake katika kizazi chake," alisema Julio.
Julio, alisema marehemu Gurumo alikuwa mmoja wa watu wa mfano kwa kule kuipenda fani yake na kujali masilahi ya wanamuziki, mbali na kufanya kazi kwa umri mkubwa mpaka miezi michache alipotangaza kustaafu.
Alisema kustaafu na mwisho kufa kwake, kumeifanya krimu na safu ya mbele ya Msongo imetoweka baada ya kuondoka kwa Tx Moshi, Joseph Maina, Athuman Momba na Suleiman Mbwembwe.
"Itatuchukua muda mrefu kumsahau Mzee Gurumo, nakumbuka wakati anaumwa mara kwa mara nilikuwa namtembelea kumjulia hali na kutaniana naye sijui nitamtania nani tena, kwa kweli naumia..Mungu Amrehemu," alisema Julio.
Enzi za uhai wake Mzee Gurumo alikuwa mwanachama wa Simba na shabiki mkubwa wa Mabingwa watetezi wa England, Manchester United.
Chini ya uongozi wa akina Hassan Dalali, Mzee Gurumo aliwahi kuwapelekea wachezaji wa Simba wakiwa mazoezi matunda mbalimbali kutoka shambani mwake kwa nia ya kuboresha siha na afya zao kuonyesha unazi wake wa Simba.
Mzee Gurumo (74) alifariki Alasiri ya jana Muhimbili baada ya kuugua kwa muda mrefu maradhi ya Mapafu na ugonjwa wa Moyo na anatarajiwa kuzika leo kijijini kwao, Masaki wilaya ya Kisarawe, Pwani.

TFF yamlilia Josephat Magazi

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu (FRAT) Mkoa wa Singida, Josephat Magazi kilichotokea jana mkoani Kilimanjaro.
Magazi ambaye pia aliwahi kuwa mwamuzi na kamishna wa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) alikuwa amelazwa katika Hospitali ya KCMC. Mazishi yatafanyika kesho (Aprili 15 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwao Ushirombo mkoani Shinyanga.
Msiba huo ni mkubwa katika fani ya mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Magazi alishirikiana na TFF na wadau wengine wa mpira wa miguu katika masuala ya uamuzi na uongozi, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Magazi, FRAT na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida (SHIREFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
 
Bwana alitoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Amina

Sunday, April 13, 2014

Demba Ba aibeba tena Chelsea, yashinda ugenini

Demba Ba of Chelsea celebrates after scoring against Swansea.
Demba Ba akimshukuru Mungu baada ya kuifungia Chelsea bao dhidi ya Swansea muda mfupi uliopita

Chelsea's Eden Hazard and Swansea's Jose Canas
BAO pekee lililofungwa na Demba Ba limeiwezesha Chelsea kuzidi kuisogelea Liverpool katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya England baada ya kuifunga Swansea City ikiwa kwao bao 1-0.
Msenegal huyo aliyeivusha Chelsea kwenye Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya PSG aliyeanzishwa katika pambano hilo alitumbukiza wavuni bao hilo dhidi ya Swansea katika dakika ya 68 akimalizia kazi nzuri ya Nemanja Matic na kuwachambua mabeki wa Swansea kabla ya kufumua shuti kali lililoenda kimiani.
Wenyeji wa mchezo huowalijikuta wakicheza pungufu kwa muda mrefu baada ya beki wao Chico kutolewa mapema kwa kuonyeshwa kati ya pili ya njano dakika ya 16 ikiwa ni dakika mbili tangu aonyeshwe ya kwanza na kuifanya timu yake ipate pengo lililotumiwa vyema na vijana wa Jose Mourinho kuibuka na ushindi.
Ushindi huo wa Chelsea umeifanya ifikishe pointi 75, mbili pungufu na ilizonazo vinara wa ligi hiyo, Liverpool iliyoitia adabu Manchester City mapema leo katika pambano lililochezwa katika uwanja wa Anfield.

Buriani Mzee Muhidini Mwalimu Gurumo

Mkurugenzi wa ASET, Asha Baraka akimkabidhi Muhidi Gurumo fedha alizochangiwa kwa ajili ya matibabu wakati akiugua
MUHIDINI Mwalimu Gurumo (sio Maalim kama ilivyozoeleka kwa wengi) hatunaye baada ya kufariki dunia mchana wa leo baada ya kuteseka kwa muda mrefu na maradhi mchanganyiko.
Mkongwe huyo ambaye alitangaza kustaafu muziki Septemba mwaka jana baada ya kuitumikia fani hiyo kwa miaka karibu 55, amefariki akiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Mzee huyo ameondoka huku akiwa bado anahitajika katika medani ya muziki kutokana na uzoefu wake katika fani hiyo aliyoianza akiwa na miaka 21 tu.
Mmiliki wa Blogu hii aliwahi kufanya mazungumzo na gwiji huyo wakati akijiuguza nyumbani kwake na kupata historia kamili ya fani yake ya muziki alipoanzia mpaka alipotangaza kustaafu ambapo nyota wa muziki wa kizazi kipya Naseeb Abdul 'Diamond' aliamua kumzawadia zawadi wa gari kufuatia kulalama kwamba kwa miaka yote 55 ya kufanya muziki hana cha kujivunia.
Hapo chini nimeamua kuiweka makala hiyo kama ilivyo ili umjue kwa undani mwanamuziki huyo ambaye ni vigumu kusahaulika kwa kipaji alichokuwa amejaliwa na namna alivyokuwa mstari wa mbele kutetea wanamuziki pamoja na kukumbatia utamaduni wa Kitanzania.
Taarifa ziliztufikia muda mfupi uliopita zinasema kuwa Mzee Gurumo atazikwa kesho majira ya saa 7 mchana kijijini kwake Masaki, Kisarawe mkoani Pwani na msiba kwa sasa upo Mabibo External.
***
Mzee Gurumo alikuwa mtu wa kujichanganya hapa akiwa na Nyosi El Saadat wa FM Academia
HUWEZI kuuzungumzia muziki wa Tanzania hasa miondoko ya dansi, bila kulitaja jina la Muhidin Mwalimu Gurumo (sio Maalim kama baadhi walivyozoea kumuita).
Hii ni kwa sababu mwanamuziki huyo mkongwe, maarufu kama 'Kamanda' au 'Mjomba', aliyewahi kutamba na kuziasisi bendi mbalimbali nchini ameutumia zaidi ya nusu ya umri wake katika mambo ya muziki, hivyo kuwa na mchango mkubwa katika fani hiyo.
Gurumo alianza fani ya muziki katika bendi za mitaani miaka ya 1950 akipitia bendi moja baada ya nyingine hadi Msondo Ngoma, ingawa kwa siku za karibuni amekuwa hapandi jukwaani mara kwa mara kutokana na afya yake kutetereka kwa maradhi, hata hivyo aliendelea kuwa mhimili wa bendi hiyo.
Mzee Gurumo akitunukiwa tuzo maalum na Rais Jakaya Kikwete wakati wa uzinduzi wa TBC1 ya Tido Mhando

Gurumo (wa tatu toka kushoto) akiwa na wanamuziki wenzake wakongwe
Mzee Gurumo akionyesha ukali wake enzi za uhai wake
Gurumo akiwa nyumbani kwake kipindi akichanganya kwente maradhi yake
Mzee Gurumo akiwa uwani mwa nyumba yake iliyopo Mabibo mmiliki wa blogu alipomtembea nyumbani kwake mwaka 2012 na kutengeneza makala hii.
Mzee Gurumo akiwa na tuzo zake
Mzee Gurumo akiwa sebeleni kwake
Mzee Gurumo akiwa na mkewe kipenzi.
Mzee Gurumo akiwa na wanamuziki wenzake wa Msondo wakati maradhi yakichanganya mwilini mwake, lakini damu ya muziki haikumzuia kupanda jukwaani.
Mbali na mchango wake binafsi kama mwanamuziki, Gurumo mwenye umri wa miaka 71 amekuwa msaada mkubwa kwa wanamuziki waliowahi kuibuliwa naye au kufanya naye kazi kutokana na misimamo yake thabiti ya kulinda na kutetea haki za wanamuziki.
Baadhi ya wanamuziki waliowahi kufanya naye kazi na Gurumo ni Shaaban Dede 'Super Motisha', Bennovilla Anthony, Hassan Rehani ‘Bitchuka’ na wengine kadhaa wakiwemo waliotangulia mbele ya haki kama Suleiman Mbwembwe na Tx Moshi William, wamewahi kukiri jambo hilo.
"Kama viongozi wa bendi wangekuwa kama Gurumo katika kupigania na kutetea haki za wasanii, naamini tungekuwa mbali mno, mjomba (jina jingine la utani la Gurumo) huwa hataki mchezo," aliwahi kusema Dede.
Wakati wa mahojiano maalum na yeye yaliyofanyika hivi karibuni nyumbani kwake Mabibo jijini Dar es Salaam, Gurumo alisema kwamba kilichokuwa kikimsukuma kuwapigania wanamuziki wenzake na yeye mwenyewe ni dhamana ya uongozi na hali ya umaskini aliozaliwa nao.
"Unajua mimi nimezaliwa katika familia ya kimaskini na kimekulia kwenye umaskini, hivyo nafsi yangu huwa ngumu kumkandamiza maskini mwenzangu kwani naamini sio haki na dhambi kubwa kwa Mungu," alisema.
"Japo nilikuwa katika nafasi ya kufanya hila kwa kuegemea upande wa wamiliki wa bendi, ila kule kutambua kuwa uongozi niliopewa na wenzagu umetokana na imani  yao kwangu, ndio maana nilikuwa mkali kama pilipili kuwapigania wenzangu," aliongeza.
Gurumo, alisema hata alipokuwa akishawishiwa na baadhi ya wamiliki wa bendi ili kuwageuka wenzake ilimradi yeye aongezwe dau lolote analotaka, hakukubali kirahisi na  wakati mwingine kufikia kuamua kuhama iwapo dai lake halisikilizwi.
"Karibu bendi zote nilizopitia misimamo yangu ilikuwa hivyo na ikitokea uongozi ukawa mbishi  kukaidi madai ninayowasilisha kwao, huwa radhi kuondoka kama nilivyofanya OSS na kwingine," aliongeza.
Gurumo, alisema kutokana na misimamo hiyo mikali, alijikuta kila bendi aliyojiunga nayo wanamuziki wenzake humchangua kuwa kiongozi hadi sasa akielekea kustaafu fani hiyo kutokana na umri kumtupa mkono na maradhi yanayomsumbua kwa hivi sasa.
Alisema, tabia yake ya kutanguliza masilahi ya wanamuziki wenzake mbele kwa kiasi fulani yamechangia kushindwa kujijenga kimaisha kulinganisha na umaarufu wa jina lake na umri alioutumia katika fani hiyo ya muziki.
Gurumo, alisema katika umri wa zaidi ya miaka 40 aliyotumia katika muziki hana cha  kujivunia zaidi ya kujenga nyumba yenye vyumba 17 eneo la Mabibo, kujenga nyumba nyingine katika shamba lake lililopo kijijini kwao Masaki, Kisarawe, mkoani Pwani.
"Nyumba hii kama unavyoiona ambayo nimewapangisha watu na ninaendelea kuikarabati ndio pekee ya kujivunia, pia nina shamba nililojenga kibanda kingine huko Masaki, lakini kwa hadhi yangu nilipaswa kuwa mbali na hapa au vipi?" alisema Gurumo kwa kuhoji.
Alisema, kwa hadhi yake wala asingekuwa akipigana vikumbo na mashabiki wake kwenye daladala aendapo kwenye shughuli zake na hata kwenye kliniki ya matatizo yake kiafya, lakini hana jinsi kwa vile hana uwezo wa kumiliki hata gari ndogo ya kutembelea.
"Naamini wengine wanaweza wasiamini, lakini ukweli ni kwamba sijahi na wala sijui ni lini nitakuwa na usafari wangu binafsi, natamani lakini tatizo uwezo wa kifedha ndio tatizo, kama sio kujenga banda hili hapa Mabibo, sijui ingekuwaje," alisema.
Alisema, kinachomfanya awe katika maisha hayo licha ya umaarufu wake kimuziki,  Gurumo alisema mbali na kuthamini na kujali wengine, lakini ukweli ni kwamba enzi  akiutumikia muziki hakukuwa na masilahi ya kutosha kama wapatavyo vijana wa sasa.
"Huwa natamani miaka irudi nyuma na zama zile ziwe hivi sasa, ili nami niweze kunufaika na jasho langu katika muziki," alisema huku tabasamu la uchungu likimtoka usoni mwake.

MJOMBA
Mkongwe huyo aliyejifunza muziki tangu akiwa Shule ya Msingi Sungwi, iliyopo Kisarawe akiimba na kupiga dramu katika bendi ya shule, alisema safari yake ya muziki kwa kiasi kikubwa ilichangiwa na mjomba wake aitwaye Seleman Sultan Wamikole.
Alisema mjomba wake aliyemchukua tangu akiwa mdogo baada ya baba yake mzazi  Mwalimu Mohammed Gurumo, kufariki na kumuacha katika maisha magumu na ndugu zake wakiwa na mama yao Mwazani Sultan aliyefariki mwaka 1981.
Alisema kutokana na hali ilivyokuwa nyumbani kwao, mjomba wake huyo alimchukua na kuja kuishi nae Dar es Salaam maeneo ya Ilala ambapo moja kwa moja alimwandikisha katika madrasa ambako alipata fursa ya kuimba kaswida.
Alisema kuwa baadaye alipata hamu ya muziki hasa kutokana na kuvutiwa na kazi za nyota wa wakati huo, Salum Abdallah 'SAY' na Luambo Luanzo Makiadi 'Franco'.
Alisema mjomba wake huyo akishirikiana na mama yake walitambua kiu kubwa aliyokuwa nayo katika sanaa ya muziki na hivyo wakamruhusu kujiunga jumla ambako alizidi kuiva na baadaye kufuatwa na bendi mbalimbali.
"Kwa kitendo nilichofanyiwa na mjomba kwa kunitunza, kunilea na kunisaidia katika harakati zangu za muziki, ilinifanya nimtungie wimbo maalum nilikuwa OSS miaka ya  1980, wimbo uliitwa 'Shukrani kwa Mjomba'," alisema Gurumo.
Alisema anaamini kama sio mjomba na mama yake ambaye hadi leo anamliza akikumbuka alivyofariki, huenda asingefikia mahala alipo sasa kimuziki.
Mtunzi na muimbaji huyo mahiri nchini, alisema licha ya kipaji cha kuzaliwa, lakini Salum Abdallah na Franco ni watu waliochangia kufika kwake hapo alipo kwani enzi zao walimvutia mno.
"Ni kweli kipaji cha muziki nimezaliwa nacho na kukirithi kutoka kwa mama yangu Mwazani aliyekuwa kiongozi wa kundi la ngoma, ila kuvutiwa na Salum Abdallah na Franco ni sababu ya mimi kufika hapa nilipo, niliwapenda mno wanamuziki hawa," alisema.

SAFARI
Gurumo alisema baada ya kujifunza muziki kwenye makundi mbalimbali ya mitaani,  mwaka 1959 ndipo alipoanza kutambulika rasmi baada ya kuchukuliwa na bendi ya  Kilimanjaro Chacha.
Alisema alijiunga na bendi hiyo kama muimbaji ingawa pia alikuwa anamudu kupiga  dramu chombo alichokuwa akikipiga katika bendi ya shule na ndani ya bendi hiyo ndipo alipotunga kibao chake cha kwamba kilichoitwa 'Wakati Nikiingia Bar'.
Hata hivyo Gurumo alisema hakukaa sana Kilimanjaro Chacha kwani mwaka 1962  alihama na kwenda kujiunga bendi ya Rufiji Jazz alipokutana na wakali kama Salum  Nonde, Mbarouk Khalfan na wengine.
Alisema alijiunga na bendi hiyo kutokana na kushawishiwa na safari ambayo Rufiji Jazz ilikuwa ikitarajia kufanya mkoani Arusha na pia maslahi, hata hivyo miezi michache baadaye aliiacha bendi hiyo na kuhamia Kilwa Jazz B mwaka 1963.
"Masiahi na ujana ndio ulionifanya niikache bendi ile na kutua Kilwa Jazz B, ambapo  kutokana na kipaji kikubwa cha uimbaji nilichokuwa nacho, uongozi wa Chama cha Wafanyakazi (NUTA) uliamua  kunichukua na kutua NUTA Jazz mwaka 1964," alisema.
Alisema kuwa alipotua NUTA alitunga kibao kilichokuja kumpa umaarufu cha kilichoitwa 'Mwangele', kikiwa na maana 'Mchumba' kwa lugha ya Kingoni na kisha kufuatiwa na nyimbo nyingine kadhaa.
"Kwa kweli idadi ya nyimbo nilizotunga nikiwa NUTA sizikumbuki kwa wingi wake, ila baadhi ni kama "Nimuokoe Nani', 'Kaka Seleman', 'Amina', Msondo Ngoma Na.1-4 na 'Maneno ya Nyerere'," alisema.
Gurumo alisema baada ya kuipandisha NUTA  iliyokuwa ikifahamika baadaye kwa jina la JUWATA, hasa alipowachukua wanamuziki nyota kama Bitchuka 'Stereo' na Said Mabera aliyekuwa akipuliza 'trumpet' katika bendi moja ya Arusha, Shirika la Teksi (TTTS) lilimfuata ili kuasisi bendi yao.
"TTTS walinifuata na kunieleza nia yao ya kutaka kuanzisha bendi na nikakubaliana nao ambapo walinilipa Sh 50,000, nikaondoka Juwata Jazz mwaka 1978 na kuasisi bendi ya Mlimani Park 'Sikinde' nikiwa na wanamuziki wenzangu wa Juwata na wengine kutoka Dar International," alisema.
Aliwataja baadhi ya waasisi wa bendi hiyo iliyokuja kufahamika kama DDC Mlimani Park kabla ya miaka mitatu iliyopita kurejea jina lake la awali baada ya kutemwa na mwajiri wao,  Shirika la Maendeleo mkoa wa Dar es Salaam, ni Hassani Bitchuka na marehemu Abel Baltazar aliotoka nao Juwata.
Wengine ni Joseph Mulenga 'Spoiler', Salum Machaku, Cosmas Chidumule, Hamis Juma  'Maalim Kinyasi', Ibrahim Mwinchande, Abdallah Gama na George Kessy kabla ya kuongezwa nguvu na akina Michael Enoch 'Teacher', Joseph Benard na Habib Jeff.

‘KASSIM WA KUTUMIA’
Alisema ndani ya Sikinde, kama kawaida aliendelea kutamba na utunzi wa nyimbo zilizotwaa umaarufu mkubwa ukiwemo wa 'Kassim' uliokuwa na sehemu mbili.
Gurumo alisema kibao hicho ni tukio la kweli lililomhusu rafiki yake aitwaye Kassim aliyekuwa akifanya kazi katika kampuni ya mizigo uwanja wa ndege (DAHACO), ambaye alikuwa akisifika enzi hizo kwa ulevi na kusahau familia yake.
"Huu wimbo nilimtungia rafiki yangu ambaye alikuwa akiendekeza starehe kupita kiasi na kila nilipokuwa nikimsihi apunguze,  alikuwa akinitaka nimuimbe ndipo ataacha ulevi," alisema.
Alisema kuwa baada ya hapo, ndipo alipoamua kutunga 'Kassim namba 1', ambapo mwenyewe (Kassim) alikuwa akijisikia fahari, ingawa hakuacha ulevi hadi alipopatwa matatizo kazini na kuchacha ambapo kidogo aliacha pombe na yeye kumtungia Kassim Na.2'.
Gurumo alisema mpaka sasa hajui kama jamaa yake huyo aliacha pombe na pia hajui kama yu hai au la kwa vile ni miaka mingi imepita bila kuonana naYe.
"Sijui kama yu hai au la, ila nyimbo zile zilimhusu yeye katika kumkataza anasa ingawa pia nilikuwa natoa ujumbe kwa jamii," alisema.
Mkali huyo ambaye ni shabiki wa kutupwa wa Simba, akiwa ni mmoja wa wanachama wake tangu mwaka 1972 na pia anayeishabikia Manchester United ya Uingereza, alisema alikaa na Mlimani Park hadi mwaka 1985 alipojiunga na safari Sound (OSS) akiwa na Bitchuka.
Alisema alipotua OSS aliwakuta baadhi ya wanamuziki wake ambao wengi wao walitokea Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo) wakilala chini na kuushinikiza kuwanunulia vitanda kama anataka aifanyie kazi bendi hiyo.
Alisema kuwa kwa bahati nzuri, uongozi ulimsikiliza  na kuwanunulia wanamuziki wote vitanda kama alivyotaka na kuanza kufanya kazi ikiwemo kubadili mtindo wa bendi hiyo wa 'Dukuduku Yee' na kuwa 'Ndekule'.
Gurumo alifichua kuwa mitindo yote aliyoasisi katika bendi za NUTA Jazz, Mlimani Park na OSS ya 'Msondo Ngoma', 'Sikinde Ngoma ya Ukae na 'Ndekule' ni ngoma ya asili ya kabila lake la Kizaramo ambazo mama yake alikuwa akiimba na kuzicheza enzi zake.
Alisema jambo hilo la kutumia ngoma za makabila ya kabila lake, ndilo ambalo hata wanamuziki nyota wa nchi za Kongo na mataifa mengine ya Afrika Magharibi wamekuwa wakifanya na kuutangaza muziki wao kimataifa tofauti na ilivyo nchini.
"Hata Wakongo na wanamuziki wa kimataifa kutoka nchi kama Senegal, Cameroon, Nigeria na Chad wamekuwa wakibuni muziki wao kwa kutumia ngoma za makabila yao, bahati mbaya vijana wengi wameshindwa kuumiza vichwa nao kubuni kazi zao na kuishia kunakili kazi za wenzao bila kujua wanawasaidia kuwatangazia, kwa kulikwepa hilo ndio maana nilikuwa nakubuni miondoko ya kabila langu la Kizaramo," alisema.
Gurumo, alisema sio jambo baya wanamuziki wa Tanzania kuiga kazi za wenzao, kitu alichodai ni vigumu kukikwepa, lakini alidai ni vema kama wangekuwa wakibuni vionjo vitakavyowatofautisha na wanamuziki hao wanaowaiga.
Alisema kwa muono wake ukiondoa Msondo na Sikinde zinazopiga muziki unaotambulika kama dansi la Tanzania, karibu bendi zote zinapiga muziki kwa kuwaiga wakongo, hata kwa zile bendi ambazo zilikuwa zikiaminika kuwa ni kilelezo rahisi kuitambulisha Tanzania kimataifa.

ULEVI
Gurumo hafichi kitu juu ya ujana wake kwa kueleza mbali na 'ubitozi' aliokuwa nao, pia alikuwa 'gangwe' enzi zake na pia aligeuzwa mtumwa wa pombe kutokana na kuwa mlevi aliyepitiliza.
Alisema, alikuwa anakata kilaji isivyo kawaida jambo ambalo lilikuwa likimfanya akorofishane na mama yake mzazi aliyetishia kumuachia 'laana' kama angeendelea kuendekeza ulevi.
"Kwa wanaonijua sidhani kama hili ni jipya, nilikuwa mlevi haswaa, kiasi mama alishindwa kunivumilia na kutishia kuniachia laana kama nisingesikilia wito wake wa kuachana na pombe," alisema.
Alisema, baada ya kushindana na 'shetani' kwa muda mrefu akikorofishana hata na mkewe, Pili bint Said Kitwana, hatimaye aliachana na ulevi mwaka 1982, miezi michache tangu mama yake mzazi kufariki.
"Ilikuwa ni kazi ngumu kuachana na pombe, lakini kwa heshima ya mama niliacha, pia shinikizo la mke wangu kipenzi ambaye ninampenda na kumsifia kwa uvumilivu wake, niliacha miezi michache baada ya mama kufariki na hadi leo situmii hiyo kitu," alisema.
Gurumo, alisema binafsi anajutia masuala ya ulevi akidai ni kati ya mambo yaliyochangia kumkosesha kufanya mambo ya maendeleo pamoja na kuihatarisha ndoa yake, kama mkewe asingekumvumilia kwa miaka 20 tangu walipooana mwaka 1962.
"Naamini ulevi uliopitiliza kwa hakika ni mbaya kama vijana wa sasa mnavyosema kwamba 'ulevi ni noma', nusura ndoa yangu ivunjike kwa ajili ya kuendekeza hii kitu, hata nilipotangaza kuachana na pombe si mke wangu wala marafiki zangu waliokuwa wakiamini hadi walipoona siku zikienda bila kupiga kilaji," alisema Gurumo.
Gurumo alisema hakuna kitu anachofurahia maishani mwake kama siku alipooana na mkewe, aliyezaa nae watoto wanne, Mariam aliyemzaa mwaka 1981,  Mwalimu, 28, Omar na Mwazani pamoja na alipoachana na pombe.
"Hivyo ndivyo vinavyonifurahisha hadi leo, nilipomuoa mke wangu na nilipoacha pombe, ila kwa huzuni ni kifo cha mama yangu, huwezi kuamini hadi leo huwa nikikumbuka natokwa machozi kwa namna mama alivyokuwa anikipenda na tulivyokuwa tunapendana na kuishi kwa upendo na furaha," alisema.
Gurumo, alisema maisha yake yamekuwa mikononi mwa mama yake kutokana na baba yake kufariki mwaka 1948 wakati akiwa na miaka nane tu, ndio maana amekuwa akimkumbuka kila mara marehemu mama yake.

BITCHUKA
Gurumo anayekula vyakula vyote halali na vyenye manufaa kwa afya yake na kunywa juisi na soda, alisema hakuna tukio lisilofutika kichwani mwake kama siku alipoamua kumsimamisha kazi 'swahiba' wake, Hassani Rehani Bitchuka.
Alisema, alifanya uamuzi huo aliouita kuwa mgumu kuwahi kukutana nao maishani kama mwanamuziki mwaka 2005, baada ya Bitchuka kugoma kushiriki kwenye onyesho la pamoja kati ya Msondo Ngoma na African Stars 'Twanga Pepeta'.
"Bitchuka aligoma kushiriki onyesho hilo kwa madai asingeweza kufanya onyesho na watoto, kitu ambacho kiliwaudhi wanamuziki wenzake na wote waliniangalia mimi kama kiongozi wao nitafanya nini kwa kosa alilofanya 'swahiba' wangu ambaye tumekuwa katika 'udugu' tangu nilipomchukua toka Arusha mwaka 1973," alisema.
Alisema, hata hivyo alilazimika kusimama kidete kama kiongozi kwa kuweka kando 'uswahiba' wake kwa Bitchuka, ili kuinusuru Msondo na kuitisha kikao nilichotangaza kumtimua kundini, jambo ambalo anadai hadi leo humpa tabu kubwa kutokana na uhusiano aliokuwa nao na Bitchuka kwa mjda mrefu.
"Kwa kweli jinamizi la tukio lile hadi leo huniwewesesha, lakini tayari nilishazungumza na Bitchuka na kunielewa, pia unajua wakati mwingine ukiwa kiongozi unapaswa kufanya maamuzi magumu bila kutarajiwa," alisema.
Alipoulizwa juu ya msanii gani kwa sasa anayemuona kama ndiye mrithi atakayeendeleza gurudumu la muziki wa dansi nchini, Gurumo bila kificho alimtaja Husseni Jumbe mmiliki wa bendi ya Talent.
"Kwangu namuona Jumbe kama ndiye tumaini pekee la maendeleo ya muziki wa dansi kutokana na kipaji kikubwa alichonacho akitunga, kuimba, kupanga muziki na kujaliwa sauti ya kipekee," alisema.
Kuhusu muziki wa kizazi kipya, alisema upo juu kwa vile unatangazwa mno na vyombo vya habari, ila haoni kama ni muziki wenye nguvu unaoweza kuufunika muziki wa dansi.
"Promo ndio inayoubeba muziki huu, kitu kinachowalemaza wasanii wake kushindwa kuwa wabunifu na kujiona wamefika mbali, wakati wana kazi kubwa hususani ya kujifunza kupiga ala mbalimbali ili wapige muziki wao utakaokubalika kimataifa tofauti na sasa wakitegemea kila kitu kifanywe studio," alisema.
Hata hivyo alikiri wanaoufanya muziki huo na taarabu wamekuwa na mafanikio makubwa kimaisha kwa vile soko limewapokea vema, jambo ambalo hata yeye hupata wivu akifikiria anapowaona vijana wakiendesha magari wakati yeye akitembea kwa miguu licha ya muda mrefu aliotumia kwenye fani hiyo ya muziki.

SWAHIBA WA JK
Gurumo, alisema fani yake ya muziki imemsaidia kufahamiana na wengi wakiwemo viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, huku akimtaja Rais Jakaya Kikwete kwamba ni mmoja wa viongozi 'rafiki' zake.
Alisema, urafiki huo ndio anaoamini ulimfanya Rais Kikwete kuvunja shughuli zake na kumtembelea hospitalini kumjulia hali alipolazwa kwa mara ya kwanza kutokana na maradhi yanayomsumbua.
Gurumo, alisema kitendo cha Rais Kikwete kuacha kazi zake kwendsa kumjulia hali na kumsaidia katika matibabu yake kumemfariji mno, kwa vile katika kulazwa kwake na hata sasa akiendelea kujiuguza nyumbani hakuna kiongozi yeyote wa serikali wakiwemo wa Wizara wa Habari na Utamaduni, kuwahi kwenda kumjulia hali.
"Huwezi amini ni yeye na mkewe, Mama Salma ndio waliokuja kunijulia hali hospitalini, akianza mwenyewe kisha mkewe kitu ambacho kinanifariji hadi leo nikiamini Rais Kikwete anatujali na kututhamini wasanii," alisema.
Aliongeza kuwa, ukiondoa kufarijika kwake kutembelewa hospitalini na Rais Kikwete na mkewe, Mama Salma, pia kitendo kilichofanya na Mkurugenzi wa ASET, Asha Baraka cha kuandaa onyesho maalum kwa ajili ya kumchangia ni kitu ambacho kitabaki kichwani mwake na kumpongeza mwanamama huyo maaraufu kama 'Iron Lady'.
"Kwa kweli sikutarajia kama Asha Baraka angeweza kufanya kitendo kile ambacho ni wazi ninaonyesha ni jinsi gani anavyothamini na kujali mchango katika muziki. Nadhani watu wengine wanapaswa kuiga mfano wake, ni mtu ambaye ameonyesha mapenzi kwangu na kujali mchango wangu katika muziki, namshukuru na kumpongeza," alisema.
Gurumo, anayechizishwa na rangi nyekundu na nyeupe na ambaye anapenda kutumia muda wake za ziada kujishughulisha na mambo ya Kilimo kwenye shamba lake lililopo Masaki, alisema katika maisha yake kisanii amewahi kupata tuzo mbili tu zote za mwaka 2008.
Alisema tuzo hizo ni ile ya Kili Music Award kama Mwanamuiki Mkongwe na ile ya Hall of Fame, huku aliyekuwa mdau mkubwa wa muziki nchini aliyekuwa akifanya shughuli zake Umangani, Is'haka Kibene alimtengenezea na kumpa tuzo maalum kumtambua kama 'Kamanda wa Muziki wa Tanzania.

UBUNIFU
Gurumo, aliyeanza kuonekana tena kwenye jukwaa la bendi yake ya  Msondo baada ya kuwa nje kwa wiki kadhaa kutokana na kulazwa hospitalini, alisema muziki wa Tanzania umepiga hatua kubwa kimaendeleo, ingawa alikiri kwamba kukosekana kwa ubunifu miongoni mwa wananamuziki na wasanii wake ni tatizo linaloukwaza usitambe nje.
Alisema, hata muziki wa kizazi kipya (bongofleva) ambao umekuwa ukitajwa kama wenye maendeleo makubwa kwa wasanii wake, alisema unashindwa kutamba kimataifa kwa sababu wasanii hao hawaumizi vichwa kubuni vitu vipya.
Mkongwe huyo alisema tatizo la wasanii kupenda kuiga kazi za wenzao wa nje na kuzifanya zao kwa kuziimba kiswahili, ndilo linalowafanya wasitambe kimataifa na kutaka kuwepo kwa mabadiliko kuanzia sasa.
Alisema suala la kuiga kazi za nje halijaanza sasa, bali kitamboi kirefu akikiri hata wao (wakongwe) walikuwa wakifanya hivyo, ila alisema ubunifu wa ziada ndio uliowafanya waonekane mahiri katika soko la kimataifa.
"Kuiga ni jambo lisilokwepeka, lakini ni wajibu wa wasanii wa sasa kuumiza vichwa na kubuni vitu vipya ambavyo vitawatofautisha na wanaowaiga. Sio Bongofleva wala dansi kote wamelemaa kwa kuiga kazi za wenzao," alisema.
Alisema cha ajabu hata bendi za zamani ukiondoa Msondo Ngoma na Mlimani Park, zote hushindana kupiga muziki wa kikongo bila kujua wanasaidia kuutangaza muziki wa nchi hiyo na kuzidumaza bendi zao tofauti na Msondo na Sikinde.
Aliongeza anahisi bendi hizo zimeamua kuingia kwenye mkumbo huo kutokana na upepo wa soko ulivyo, japo alisema kimezifanya bendi husika zisiwasisimue mashabiki wake kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

KUSTAAFU
Gurumo, alisema hana muda mrefu kabla ya kutangaza kustaafu fani ya muziki kutokana na hali yake ya kiafya na umri mkubwa alionao akitaka kuwapisha wanamuziki wenye damnu changa kuendelea gurudumu la fani hiyo.
Alisema, ingawa hajajua ni lini atafanya hivyo ila hadhani kama utamalizika mwaka huu wa 2012 kabla ya kutimiza azma hiyo na kudai atakapostaafu atajikita kwenye kuwasaidia vijana chipukizi.
Gurumo, alisema mipango yake ni kuanzisha chuo cha muziki anachotaka kukijenga Masaki, Kisarawe iwapo atapata mtu wa kumsaidia kufanikisha hilo kwa lengo la kutaka kuendeleza vipaji na kuudumisha muziki wa Tanzania.
"Sina muda mrefu kabla ya kustaafu rasmi muziki, sitajiweka kando kabisa na ndoto zangu ni kutaka kujenga chuo cha muziki katika shamba langu lililopo Masaki, lakini natatizwa na hali ya kiuchumi, hivyo kama serikali au mtu yeyote mwenye uwezo kifedha akinisaidia nitafurahi kwa vile nataka kuendeleza muziki wetu," alisema.
Alisema, anaamini vijana wanapaswa kujifunza mengi kutoka kwake na kwa wakongwe wengine ili kuufanya muziki wa Tanzania uendelea kudumu hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya kidunia.

FAMILIA
Muhidini Mwalimu Gurumo, alizaliwa mnamo mwaka 1940 katika kijiji cha Masaki, Kisarawe akiwa ni mtoto wa pili kati ya watatu wa mzee Mwalimu Mohammed Gurumo.
Baba yake alifariki wakati Gurumo akiwa na miaka nane tu na hivyo maisha yake ya utotoni kuwa chini ya mama yake mzazi kabla ya kuchukuliwa na mjomba wake aliyemsaidia kuingia kwennye muziki.
Gurumo, alifanikiwa kufunga ndoa na mkewe, Pili bint Said Kitwana na kubahatika kuzaa nae watoto wanne, ambapo ni mmoja tu aitwae Mariam ndiye aliyerithi kipaji chake cha muziki akiimba kundi moja la taarabu lililopo Temeke.
Mkongwe huyo anayemtaja Said Mabera 'Dokta' kama mmoja wa wanamuziki viongozi anayemzimia, alisema katika maisha yake ya ndoa hakuna anachokifurahia kama kudumu kwa ndoa yake na mkewe ambayo imetimiza miaka 50 mwaka huu.
Alisema, kama sio uvumilivu wa mkewe, huenda ndoa hiyo ingevunjika kitambo kutokana na ukweli ukiondoa ulevi na kazi yake ya sanaa, pia ukorofi aliokuwa nao uliochangiwa na ujana ni kati ya mambo yaliyotaka kuivunja ndoa yake.
"Sio siri najivunia kuwa na mke mvumilivu kama huyu, kuna mambo niliyomfanyia kwa muda mrefu ndani ya ndoa yetu, lakini alinivumilia hadi leo tukiingia mwaka wa 50 tangu tuoane mwaka 1962," alisema.
Aliongeza, kuwa anaamini ndoa yao ilikuwa mipango ya Mungu ndio maana wamedumu na kuzeeka pamoja wakiwa ndio kwanza wanapendana kama wameoana jana, jambo ambalo linamfanya kila mara kumshukuru Mungu.

MKEWE
Pili Bint Said Kitwana, alikiri kwamba ndani ya uhusiano wa kimapenzi hadi kuja kuoana na Gurumo alipitia katika misukosuko mingi, lakini anashukuru Mungu alijaliwa uvumilivu na kuidumisha hadi leo.
Mama huyo alisema ugomvi wake mkubwa na mumewe ilikuwa ni tabia yake ya ulevi, hali iliyomfanya mara kwa mara kukwaruzana nae akimsihi aache.
Alisema, kuna wakati mumewe alikuwa akiondoka nyumbani Ijumaa kwenda kwenye maonyesho na asionekane hadi Jumatatu akiletwa na rafiki zake akiwa 'bwii', kitu kilichokuwa kikimuuma.
"Tatizo kubwa baina yangu na Gurumo ilikuwa suala la ulevi, hata alipokuja kuacha sikuamini," alisema.
Aliongeza, jingine ni tabia ya kuwa na 'kuchakachua nje', na kumfanya aumie roho hasa wanawake zake wa nje kumfuata na kumtukana na hata wakati mwingine kutaka kupigana nao hasa anapoamua kuambatana nae kwenye maonyesho.
Alisema, ukiondoa matatizo hayo, Gurumo ni mume bora, mpole, mkarimu  na baba anayejali familia mwenye mapenzi ya dhati, ndio maana aliamua kumvumilia hadi leo na kutoa wito kwa wanandoa wengine kuvumiliana katika ndoa zao ili kuzifanya zidumu kama ilivyo kwao.
Pia, alisema kitu kinachomfurahisha kwa Gurumo ni tabia ya kutochagua chakula cha kula, akidai hula chakula chochote isipokuwa 'kitimoto'.
Mama huyo alisema kwa namna mumewe alivyojitolea ndani ya taifa hili kupitia fani yake ya muziki ni vema serikali ikamkumbuka kwa kumsaidia angali akiwa hai, badala ya kusubiri aje afe ndipo wajitokeze kumwagia sifa lukuki.
"Naiomba serikali imsaidie mzee huyu, huwa naumia roho tunapokuwa tukipelekana klinini jinsi abiria ndani ya daladala wanavyotushangaa, najua ni kutokana na jina kubwa la Gurumo na hali aliyonayo kimaisha," alisema.
Aliongeza, ingelikuwa ni amri yake angependa kuona Gurumo akipumzika masuala ya muziki baada ya kuutumikia kwa zaidi ya miaka 50.

Mwisho

Vita ya kushuka daraja nouma


Mgambo JKT
Ashanti United
BAADA ya Azam kupata ushindi wa mabao 2-1 na kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara bila kupoteza mchezo wowote, huku Yanga ikishinda mjini Arusha kwa idadi kama hiyo, vita kwa sasa ipo kwa timu zilizopo mkiani, baada ya Mgambo JKT leo kulazimishwa suluhu kwenye uwanja wa Mkwakwani na Kagera Sugar na kuwafanya wasipumue vyema.
Sare hiyo imeifanya timu hiyo kufikisha pointi 26 moja zaidi ya timu za Ashanti United iliyoinyoa Simba jijini Dar es Salaam na Prisons iliyoishusha daraja Rhino Rangers mjini Mbeya jana kwa kuilaza mabao 4-3 ambazo kila moja ina pointi 25 baada ya mechi 25 kwa kila timu.
Timu mojawapo kati ya hizo zitaungana na Rhino Rangers na Oljoro JKT iliteremsha leo kurudi Ligi Daraja la Kwanza na Mabingwa watetezi Yanga kwa kufungwa 2-1 kuzipisha timu za Polisi Moro, Ndanda Fc ya Mtwara na Stand United ya Shinyanga zilizopanda Ligi Kuu kwa msimu ujao.
Mechi za Jumamosi hasa inayozikutanisha AShanti United na Prisons mjini Morogoro ndiyo inayosubiriwa kwa hamu kuona inakuwaje kwa timu hizo zilizorejea ligi kuu kwa misimu miwili tofauti.
Pia kama Simba itaendelea kutoa takrima kwa wapinzani wake kuna uwezekano ikajikuta ikitolewa kwenye nafasi ya nne iliyoikalia kwa muda mrefu kutokana na Kagera Sugar na Ruvu Shooting kuonekana kuinyemelea nafasi hiyo nyuma yao.
Hapa chini ni msimamo kamili baada ya mechi za leo za ligi hiyo;

                            P     W      D     L     F      A         D      Pts
1.Azam              25     17     8     0     50     15     +35     59    
2.Yanga              25     16     7     2     60     18     +42     55    
3.Mbeya City    25     12     10   3     32     20     +12     46    
4.Simba             25      9      10    6     40     26     +16     37    
5.Kagera Sugar 25      8      11    6     22     20     +2       35    
6.Ruvu Shooting25     9      8      8     26     32      -6       35    
7.Ruvu Stars     25     10     1     14     23     39     -16     31
8.Mtibwa Sugar25      7      9       9      29     30     -1      30
9.Coastal Union25     6      11     8      16     19     -3      29
10.JKT Mgambo25    6       8     11     18     34     -16    26    
11.Prisons          25     5     10    10     25     33     -8      25    
12.Ashanti Utd   25     6     7      12     20     38     -18    25    
13.JKT Oljoro    25     3     9     13     18     36     -18     18    
14.Rhino Rangers25    3     7     15     18     37     -19     16