STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, April 27, 2014

Bao moja lamliza Amissi Tambwe

Tambwe akiwa na Mombeki
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Simba na Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, Amissi Tambwe amesema pamoja na kunyakua kiatu cha dhahabu, lakini hajafurahishwa na kushindwa kutimiza lengo lake la kufunga jumla ya mabao 20.
Tambwe aliyesajiliwa na Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Vital'O ya Burundi, aliwaahidi mashabiki kwamba angefunga jumla ya mabao 20 kama lengo lake la kuendeleza rekodi yake ya kufumania nyavu iliyompa kiatu cha dhahabu pia katika michuano ya Kombe la Kagame ya mwaka jana iliyofanyika nchini Sudan.
Mrundi huyo alisema kitendo cha kushindwa kupata bao moja la kukamilisha idadi ya mabao aliyopania msimu huu, inamuuma ingawa hakuwa na jinsi kwa jinsi alivyokuwa akikamiwa uwanjani na wakati mwingine kuumizwa na kushindwa kucheza mechi zilizofuata.
"Nasikitika kushindwa kukamilisha idadi ya mabao niliyokuwa nimepania msimu wangu wa kwanza ndani ya Simba, nilipanga nifunge 20, lakini moja nimeshindwa kulipata mpaka ligi ilipomalizika," alisema Tambwe.
Hata hivyo mchezaji huyo ambaye amekuwa gumzo na aliyeweka rekodi ya kufunga hat trick mara mbili baada ya ukame wa muda mrefu wa kufungwa idadi hiyo ya mabao katika ligi ya Tanzania tangu alipokuwa amefanya hivyo Juma Semsue wa Polisi Dodoma mwaka 2010, alisema anajipanga kwa msimu ujao panapo majaliwa.
Tambwe alisema anaamini tayari amepata uzoefu wa kutosha wa ligi ya Tanzania hivyo atajua namna ya kujipanga kuendelea kuwaliza makipa na timu pinzani kama alivyofanya katika msimu huu akifikia rekodi ya ufungaji wa mabao mengi iliyowahi kuwekwa na John Bocco misimu miwili iliyopita.
Katika msimu uliopita Mfungaji Bora alikuwa Kipre Tchetche wa Azam aliyefunga mabao 17 ambaye msimu huu aliungana na wachezaji Elias Maguli wa Ruvu Shooting na Mrisho Ngassa kufunga mabao 13 kila mmoja na kushika nafasi ya pili nyuma ya Tambwe.
Tambwe jana aliiongoza timu yake ya taifa ya Intamba Murugamba kuitoa nishai timu ya taifa, Taifa Stars kwa kuwacharaza mabao 3-0 katika mchezo maalum wa sherehe za Muungano, akisaidiana na mkali mwingine anaycheza Yanga, Didier Kavumbagu kila mmoja akifunga bao moja.
Kwa kunyakua kiatu hicho cha dhahabu, Tambwe amejihakikishia kuzoa kitita cha Sh. Mil 5.2 toka kwa wadhamini wa Ligi Kuu kampuni ya Vodacom.

No comments:

Post a Comment