Kijiko |
Wachezaji hao beki Ibrahim Susan 'Chogo' kiungo Juma Seid 'Kijiko' na mshambuliaji Cosmas Lewis walisimamishwa na viongozi kwa tuhuma za utovu wa nidhamu baada ya kutoweka kambini bila taarifa zozote wakielekea kwenye mechi hiyo na Azam iliisha kwa mabingwa wapya wa msimu huu, Azam kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 na kuvunja mwiko wa Ruvu kufungwa Mabatini.
Afisa Habari wa Ruvu, Masau Bwire alisema licha ya awali uongozi kupanga kuwaita wachezaji hao ili wajieleze, suala hilo lilishindikana kutokana na kubanwa na ratiba ya mechi za kufungia msimu, hivyo watakutana Jumatatu kuamua hatma yao.
Bwire alisema wataamua hatma ya wachezaji hao kutegemeana na ripoti ya benchi la ufundi la timu hiyo iliyowasilishwa kwao na kocha wao Tom Olaba ambayo ina mapendekezo kwa ajili ya msimu ujao.
"Hatma ya wachezaji watatu na wengine ambao wataachwa au kubakishwa kwenye kikosi cha Ruvu kwa ajili ya msimu ujao itafahamika Jumatatu (kesho) wakati viongozi watakapokutana ili kuipitia na kuijadili kwa kina ripoti ya kocha iliyowasilishwa kwetu siku ya Ijumaa," alisema.
Aliongeza, uongozi huo pia utafanya tathimini ya msimu mzima wa ligi kwao kama wamefanikiwa katika malengo yao na kujipanga kwa msimu ujao ili kuhakikisha yale yaliyowaangusha msimu huu yasijirudie na Ruvu Shooting iendelee kuwa timu ya upinzani na siyo shiriki katika ligi hiyo ambayo iliyoshuhudia ushindani ya hali ya juu.
Ruvu Shooting imekuwa na msimu mzuri mwaka huu baada ya kufanikiwa kumaliza nafasi ya sita ikiwa na pointi 38 ikilingana na klabu ya Simba na Kagera Sugar waliotofautiana nao mabao ya kufunga na kufungwa.
No comments:
Post a Comment