Mwina Kaduguda (kushoto) akiwa na aliyekuwa mwenyekiti wake, Hassan Dalali walipokuwa wakiukabidhi uongozi wa sasa wa Simba, chini ya mwenyekiti wake Ismail Rage |
Aidha amewakumbusha wanachama wa klabu hiyo kuhakikisha wanachagua viongozi ambao wataiwezesha Simba kuwa moja na itakayokuwa na uwezo wa kunyakua ubingwa wa Afrika.
Akizungumza kwenye kituo cha radio Clouds Fm leo mchana, Kaduguda alisema uzoefu alionayo katika kuongoza soka ndani ya klabu hiyo na kwingine umemfanya kuitambua kinachokwaza soka la Tanzania kusonga mbele mojawapo ikiwa ni mifarakano ya kuendekeza makundi.
Kaduguda aliyewahi kuwa Katibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kipindi ikiitwa FAT, alisema ndani ya Simba kuna makundi ambayo yamekuwa yakiwagawa wanachama kila upande ukitaka kundi lao litoe kiongozi kitu alichodhani kinapaswa kudhibitiwa mapema.
Alisema ni vyema makundi yaliyopo kukaa meza moja kwa nia ya kuijenga Simba kuelekea kwenye uchaguzi kwa kuiwezesha klabu hiyo kupata viongozi bora watakaoivusha mahali ilipo na kuja kutamba Afrika, la sivyo inaweza kukutwa na yaliyozikuta Gor Mahia au AFC Leopard za nchini Kenya, zilizopotea kwenye umaarufu wao wa soka kabla ya kuibuka tena.
"Hakuna siri ndani ya Simba kuna makundi kama ya Simba Taleban, Friend's of Simba na Banyamulenge ambalo hata hivyo limelegalega, nashauri wanayounga mkono makundi hayo yakae pamoja na kumaliza tofauti na kujadiliana kiongozi gani anayewafaa kuwaongoza."
Kaduguda alisema na kuongeza, pia makundi hayo yanapaswa kutowapuuza au kuwabeba watu kwa sababu ya haiba yao au uwezo wa kiuchumi, akieleza hata wasio na uwezo wa kifedha wana haki na nafasi kubwa ndani ya klabu hiyo.
Pia aliwakumbusha wanachama wa klabu hiyo kuwa makini katika uchaguzi huo ili kuipa Simba viongozi makini na bora watakaoiwezesha klabu yao kutamba kimataifa badala ya kuwabeba watu ambao watakuja kuwanyima raha kwa miaka minne ijayo.
Klabu ya Simba inaelekea kufanya uchaguzi mkuu baada ya uongozi wa sasa chini ya Mwenyekiti wao, Ismail Aden Rage kumaliza muda wao mwezi ujao.
Hata hivyo uchaguzi huo bado haujatangazwa rasmi na Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo kwa sababu ya kusubiri kupitishwa kwanza kwa Katiba yao mpya na ofisi ya Msajili ili kuweka hadharani mchakato kamili ya kinyang'anyiro hicho.
No comments:
Post a Comment