STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, October 8, 2013

Cannavaro atamba Yanga kwenda kupata ushindi Kaitaba

Cannavaro (kushoto) akichuana na mchezaji wa Kagera Sugar ligi ya marudiano msimu uliopita
NAHODHA wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara ,Yanga Nadir  Haroub 'Cannavaro', amesema licha ya kutambua ugumu wa pambano lao lijalo dhidi ya Kagera Sugar, bado anaamini timu yake itaibuka na ushindi ugenini.
Yanga itasafiri hadi mjini Bukoba, mkoani Kagera kuvaana na Kagera Sugar siku ya Jumamosi kwenye uwanja wa Kaitaba katika moja ya mfululizo wa mechi za Ligi Kuu mwishoni mwa wiki hii.
Mabingwa hao watetezi wanaokamata nafasi ya pili kwa sasa katika msimamo huo, walichezea kichapo cha bao 1-0 katika mechi kama hiyo kwa msimu uliopita iliyochezwa Oktoba 8 na kuwa pambano pekee kupoteza kipindi chote hadi hivi karibuni walipolazwa na Azam katika ligi ya msimu huu.
Cannavaro, beki wa kati wa kutumianiwa wa Yanga anafahamu usumbufu wa wapinzani wao wanapokuwa uwanja wao wa Kaitaba, lakini alisema kwa namna kikosi chao kilichojipanga anaamini wanaenda Kagera kuvuna pointi tatu.
"Tunajua litakuwa pambano gumu na lenye upinzani mkali, lakini Yanga tutapigana kiume ili kushinda kuendeleza wimbi la ushindi tulilolianza," alisema.
Cannavaro anayeichezea pia timu ya taifa, alisema wachezaji wote wa Yanga wana ari kubwa ya kuisaidia timu yao kuendeleza ushindi baada ya awali kuchechemea kwa sare na kupoteza mchezo wao na Azam.
Yanga imepata ushindi mara mbili mfululizo dhidi ya timu za Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar na kuwafanya wawasogelee watani zao, Simba wanaoongoza wakiwa na pointi 15, tatu pungufu na ilizonazo Yanga na JKT Ruvu.
Kivumbi cha ligi hiyo kinatarajiwa kuendelea tena kesho kwa michezo minne katika viwanja vinne tofauti ambapo Rhino Rangers itakuwa nyumbani mjini Tabora kuikaribisha Mbeya City kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, huku Oljoro JKT itaialika Ruvu Shooting kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid , Arusha.
Pambano jingine litazikutanisha Azam na Mgambo JKT zitakazoumana kwenye uwanja wa Chamazi na Mtibwa Sugar itakuwa nyumbani Manungu kuikaribisha JKT Ruvu.

Mtuhumiwa muhimu mauaji wa Bilionea wa Madini anaswa akitoroka


JESHI la  Polisi nchini limefanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa muhimu wa mauaji ya mfanyabiashara bilionea wa Arusha Erasto Msuya wakati akijaribu kutoroka kwenda Burundi.
Habari za uhakika zilizopatikana jana, zilisema mtuhumiwa huyo (jina tunalo), alikamatwa juzi asubuhi mkoani Kigoma akiwa katika harakati za kutoroka kuelekea nchi jirani ya Burundi.
Mtuhumiwa huyo ndiye anadaiwa kumshawishi marehemu kwenda kukutana na wauaji wake eneo la Mijohoroni wilayani Hai Agosti 7, mwaka huu na alikwenda pamoja na marehemu hadi eneo la tukio.
Habari zinadai mara baada ya marehemu kuuawa kwa kumiminiwa risasi zaidi ya 20, mtuhumiwa huyo alitoroka kutoka eneo la tukio akitumia moja kati ya pikipiki mbili zilizotumika katika mauaji hayo. 

Tangu kutokea kwa mauaji hayo, polisi ambao wameonyesha weledi wa hali ya juu katika upelelezi wa mauaji hayo, walikuwa wakimfuatilia mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa akijificha katika mikoa tofauti.
Habari nyingine zinadai kuwa watuhumiwa waliokodishwa kumuua mfanyabiashara huyo waliahidiwa kulipwa kitita cha Sh4 milioni kila mmoja na kila mmoja akalipwa malipo ya awali ya Sh1 milioni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo aliyesema ni 'muhimu' na kwamba mipango ya kumrejesha Moshi inaendelea kufanyika.
Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kunafanya idadi ya watuhumiwa ambao wamekwishakamatwa hadi sasa kufikia wanane wakiwamo wafanyabiashara wawili wenye ukwasi ambao tayari wamefikishwa mahakamani.



Monday, October 7, 2013

King Majuto naye atangaza kuwania Ubunge 2015

http://www.bongocinema.com/images/casts/king_majuto.jpg
King Majuto



Yekonia
MCHEKESHAJI mkongwe nchini, Amri Athuman 'King Majuto' ametangaza nia yake ya kujitosa kwenye siasa akitaka kuwania Ubunge katika Jimbo la Tanga Mjini katika uchaguzi mkuu ujao wa 2015.
Akihojiwa na kituo cha Clouds FM, Mzee Majuto mwenye umri zaidi ya miaka 60, alisema Mungu akimjalia atajitosa kwenye ubunge jimboni humo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), akidai kiu hiyo imechochewa na mafanikio ya wasanii waliojitosa kwenye siasa na kufanya vyema.
Mzee Majuto alisema, uzoefu alionao katika kuishi kwake mjini Tanga itamwezesha kuwatatulia kero na kuwaletea maendeleo ya kweli wananchi wenzake iwapo Mungu atamjalia katika kusudio lake.
Kadhalika Muigizaji, ambaye pia ni mtayarishaji na muongozaji wa filamu nchini, Yekonia Watson 'Amani' amesema matarajio yake miaka michache ijayo ni kujitosa kwenye siasa akitaka kuwania Ubunge kabla ya kuangalia nafasi ya juu zaidi kwa maana Rais.
Akizungumza na MICHARAZO jioni hii, Watson alisema anaamini ana uwezo na kipawa cha uongozi hivyo anaweka mambo sawa kabla ya kujitosa jumla kwenye duru hilo, japo yeye hakuweka bayana atajitosa kupitia chama gani.
"Kwa sasa ni mapema mno, ila nitaanzia Ubunge kisha kuangalia nafasi ya juu, ila muhimu Mungu anipe uhai na umri wa kufanikisha hilo," alisema mkali huyo anayejiandaa kuachia filamu yake mpya iitwayo 'Uwanja wa Vita' aliyoigiza na wasanii kadhaa nyota akiwamo Irene Uwoya.

Wakuvanga kuwasha moto Fun City

TO make your Eid holiday plans a little easier to decide, Comedian Wakuvanga is performing at FUNCITY! With the option to stay over night in one of our quaint cottages! Experience the best of enjoyment, entertainment and relaxation, with a new menu, new shisha bar, late evening open air movies, prizes to be won, a chance to be on TV and so much more it will entertain the whole family for hours! Book now to avoid disappointment.
Pre-Bookings and Enquiries: call 0712/0785 786 000, reply to this mail or email info@funcity.co.tz

Polisi wanasa vijana msituni wakijifunza mbinu za kigaidi



PictureKamanda Zellothe Stephen akionesha CD za mafunzo ya kijeshi zilizokuwa zinatumiwa na kundi hilo.
 

Na Abdallah Bakari, Mtwara
JESHI la Polisi mkoani Mtwara inawashikilia watu 11 kwa tuhuma za kupata mafunzo ya kijeshi msituni kwa kutumia CDs za al-Shabaab.

Tukio hilo la aina yake limetokea katika mlima Makolionga wilaya ya Nanyumbu mkoani hapa ambapo pia CDs zenye mafunzo mbalimbali ya kijeshi 25 zimekamatwa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen ameuambia “mtandao wa Kusini Leo” kuwa watuhumiwa hao
walikamatwa wiki moja iliyopita baada ya jeshi lake kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema: “CD hizo zilikuwa zinatoa mafunzo ya Al-Shabaab ya kuchinja watu, Mauaji wa Osama Bin Laden, Zindukeni Zanzibar, Kuandaa Majeshi, Mauaji wa Idd Amin na Mogadishu Sniper,” alisema Stephen.

Alisema watuhumiwa wote ni wakazi wa wilaya ya Nanyumbu mkoani hapa na kwamba walikuwa wakiongoza na Mohamed Makande 39, mkazi wa kijiji cha Sengenya ambaye pia anashikiliwa na jeshi hilo.

Aliwataja wengine waliokamatwa kuwani Hassan Omary (39) mkazi wa kijiji cha Nanyulu, Rashid Ismail (27). Abdallah Y. Hamisi (32), Salum Wadi (38), Fadhili Rajabu (20), Abbas Muhidini (32), Ismail Chande (18), Said Mawazo, Issa Abeid (21), na Ramadhani Issa (26) wote wakazi wa kijiji cha Likokona.

Kuhusu vitu watuhumiwa walivyokamatwa navyo, Kamanda Zelothe alisema, “Tumekamata mapanga mawili, Deki ya DVD, Solar, Visu, Tochi, Betri, Simu za kiganjani 5, Vyombo mbalimbali vya kulia chakula, Baiskeli tatu, Vitabu mbalimbali wa dini ya Kiislam, Unga wa mahindi kilo 50, Mahidi kilo 150 na virago vya kulalia. Vingine ni mfuko wa kijani unaosadikiwa ni wa kijeshi wenye nembo ya nanga ya meli yenye mistari kulia na kushoto na nyoka katikati.”

Alisema jeshi lake licha ya kuwafikisha watuhumiwa mahakamani, linaendelea na uchunguzi wa kina kwa kushirikiana na Polisi Makao Makuu kwa lengo la kufanikisha kuunasa mtandao mzima.

Kamati ya Wanawake, TWFA zapongezwa

Rais Leodger Tenga
Na Boniface Wambura
Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) wamepongezwa kwa kuhakikisha akina mama wanacheza mashindano mbalimbali.

Pongezi hizo zimetolewa na Rais wa TFF, Leodegar Tenga ambapo amesema timu za wanawake zimekuwa zikishiriki katika mashindano mbalimbali licha ya ukweli kuwa hadi sasa hakuna udhamini kwenye mchezo huo.

Amesema mpira wa miguu unaendeshwa na udhamini na kuchangia, jambo ambalo linafanikishwa kwa kiasi kikubwa na uwazi katika matumizi ya fedha, jambo ambalo hivi sasa lipo ndani ya TFF.

Rais Tenga amesema baada ya kuanzisha Kamati ya Ligi, hivi sasa TFF inapata asilimia 4.5 tu ya mapato ya mechi za ligi kutoka asilimia 33 iliyokuwa ikipata wakati anaingia madarakani mwaka 2004.

Amesema asilimia hiyo 4.5 haiwezi kuendesha mpira na ndiyo maana nguvu zinaelekezwa katika kutafuta wadhamini na kuchangia. Pia TFF inatoa zaidi ya asilimia 15 ya Fedha za Msaada wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FAP) kutoka FIFA kwenye mpira wa miguu wa wanawake ambapo ni nchi chache zinazofikia kiwango hicho.

Hivyo, ametoa mwito kwa kampuni kujitokeza kudhamini au kuchangia timu za Taifa za mpira wa miguu za wanawake ambazo zinashiriki mashindano mbalimbali mwaka huu, kwani gharama za kuziendesha ni kubwa.

Timu ya wakubwa (Twiga Stars) inacheza mashindano ya mchujo ya Fainali za Afrika (AWC) zitakazofanyika mwakani nchini Namibia wakati ile ya chini ya miaka 20 inacheza mashindano ya Dunia ambayo fainali pia zitachezwa mwakani nchini Canada.

Mradi wa Football 4 Hope kufunguliwa Okt 13 mjini Iringa



Na Boniface Wambura 
MRADI wa Football for Hope kusaidia watoto na wasiojiweza kupitia mpira wa miguu uliofadhiliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) mkoani Iringa utafunguliwa rasmi Oktoba 13 mwaka huu.

FIFA hutoa mradi huo kwa baadhi ya nchi kwa kuzingatia mambo mbalimbali ikiwemo utawala bora, lakini kwa kupitia taasisi zisizo za kiserikali (NGOs) ambapo kwa Tanzania umepatikana kupitia taasisi ya Iringa Development of Youth, Disabled and Child Care (IDYDCC).

Rais wa TFF, Leodegar Tenga ameishukuru FIFA kwa msaada huo, kwani ni mkubwa na kuongeza kuwa ni matumaini yake utatumika kwa lengo lililopangwa.

Amesema mradi huo wa FIFA ambao ni wa kusaidia watoto kielimu na wasiojiweza kwa kupitia mpira wa miguu haukupita moja kwa moja TFF ni mzuri kwani moja ya mambo uliofanikisha ni kuwepo jengo na sehemu ya watoto kucheza.

Ni wastani wa nchi kumi tu duniani kwa mwaka zinapata mradi huo kutoka FIFA, jambo ambalo Rais Tenga amesema linachangiwa pia na uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na shirikisho hilo.

Yanga, Mtibwa Sugar wavuna Mil 97/-



PAMBANO la Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) iliyochezwa jana (Oktoba 6 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya Yanga na Mtibwa Sugar limeingiza sh. 97,557,000.

Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo namba 46 lililochezeshwa na Isihaka Shirikisho kutoka Tanga walikuwa 17,313. Yanga ilishinda mabao 2-0.

Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 23,453,748.95 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 14,881,576.27.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 11,925,635.06, gharama ya kuchapa tiketi ni sh. 3,171,190 wakati gharama za mchezo ni sh. 7,155,381.04.

Kamati ya Ligi sh. 7,155,381.04, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 3,577,690.52 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 2,782,648.18.

Rais Tenga asisitiza kuwa Uchaguzi Mkuu upo pale pale Okt 27

Rais wa TFF, Leodger Tenga
 Na Boniface Wambura
RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amewahakikishia Watanzania kuwa uchaguzi wa kupata Kamati mpya ya Utendaji ya shirikisho utafanyika Oktoba 27 mwaka huu kama ilivyopangwa.

“Wazungu wanasema ije mvua au jua, uchaguzi utafanyika. Isipokuwa tunachotaka kuhakikisha ni kuwa unakuwa uchaguzi huru na wa haki,” amesema Rais Tenga wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF leo mchana (Oktoba 7 mwaka huu).

Amesema mchakato unakwenda vizuri kilichobaki ni revision (mapitio) na rufani, masuala ambayo yako mbele ya Kamati ya Rufani ya Maadili na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi.

Rais Tenga amesema lengo la hatua hizo si kuzuia watu wasigombee kwani ni lazima mambo ya msingi ikiwemo sifa za wagombea yaangaliwe, lakini kwenye haki ni lazima kuhakikisha inatendeka hata kama ni kwa mtu mmoja.

Mchakato wa uchaguzi ulivutia waombaji 58 ambapo watatu wamekata rufani Kamati ya Rufani ya Uchaguzi kupinga kuondolewa na Kamati ya Uchaguzi wakati wengine wanane masuala yao yamepelekwa Kamati ya Rufani ya Maadili kwa njia ya mapitio (revision) ili kupata mwongozo wa utekelezaji.

Mwongozo huo umeombwa na Sekretarieti ya TFF kwa Kamati ya Rufani ya Maadili kwa vile Kamati ya Maadili iliwaona waombaji wanane wa uongozi waliofikishwa mbele yake kwa makosa ya kimaadili kutokuwa na hatia, lakini wakati huo huo ikitambua kuondolewa kwao kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi kulikofanywa na Kamati ya Uchaguzi.

Sunday, October 6, 2013

Tottenham Hotspur yakiona cha moto nyumbani, Arsenal yapunguzwa kasi

 Ravel Morrison
TIMU ya Tottenham Hotspur wakiwa nyumbani kwao White Hart Lane, London ya Kaskazini wamekiona cha moto baada ya kukanidkwa mabao 3-0 na wageni wao, West Ham United katika mechi ya Ligi Kuu ya England iliyomalizika hivi punde, huku Arsenal ikipunguzwa kasi kwa kulazimishwa sare ya 1-1 ugenini.
Vijana hao wa Andre Villa Boas walishindwa kabisa kufurukuta katika pambano hilo ambalo lilishuhudiwa hadi mapumziko kukiwa hakuna mbabe.
Kipindi cha pili kilipoanza, wenyeji walianza kusulubiwa kwa kutanguliwa kufungwa bao la kwanza kupitia kwa Winston Reid dakika ya 66 na dakika sita baadaye Ricardo Tav Te akaongeza la pili kabla ya Ravel Morrison kuongeza la tatu dakika ya 79 lililowanyong'onyesha Spurs.
Nayo Arsenal baada ya ushindi wa mechi tano mfululizo katika ligi hiyo ilirejea kileleni mwa msimamo jioni hii baada ya kulazimisha sare ya 1-1 na West Bromwich Albion uwanja wa ugenini na kuiengua Liverpool iliyokuwa imekalia nafasi ya kwanza kwa tofauti ya uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Wenyeji walitangulia kubata bao dakika ya 42 lililofungwa na Claudio Yacob, bao lililodumu hadi mapumziko.
Jack Welshire aliisawazishia vijana wa Arsene Wenger katika dakika ya  63 na kuifanya Arsenal kuambulia pointi moja na kufikisha pointi 16 sawa na Liverpool lakini ikiwa na mabao mengi ya kufunga kuliko vijogoo hao wa Anfield.

Chemsha Bongo! Kama unawakumbuka ebu wataje majina yao

Wawili kati ya hao bado wapo wapo ndani ya klabu hii ni akina nani na ukiweza taja nafasi zao

Didier Kavumbagu, Peter Michael wamfukuza Amisi Tambwe kimya kimya


Tambwe aliyenyoosha kidole anayeoongoza kwa mabao Ligi Kuu
Didier Kavumbagu (kushoto) akishangilia mabao yake na wachezaji wenzke wa Yanga
WASHAMBULIAJI Didier Kavumbagu wa Yanga na Peter Michael wa Prisons-Mbeya wanamfukuza kimya kimya mshambuliaji wa Simba, Amisi Tambwe baada ya kila mmoja leo kutupia bao moja moja na kufikisha idadi ya mabao manne.
Kavumbagu aliyekuwa mfuingaji namba mbili msimu uliopiota alifunga bao lake jioni hii wakati Yanga wakiilaza Mtibwa mabao 2-0 na Michael akifunga bao pekee lililoizamisha Mgambo JKT mjini Tanga na kufikisha nusu ya mabao aliyonayo Tambwe anaongoza akiwa na mabao nane mpaka sasa.
Naye kiungo mshambuliaji nyota wa Yanga na Taifa Stars, Mrisho Ngassa ameanza kufungua akaunti yake ya mabao baada ya leo kufunga bao likiwa ni goli la kwanza kwa msimu huu ambapo alikosa mechi sita za ligi hiyo kutokana na adhabu aliyokuwa akiitumikia kwa kusaini mikataba katika klabu mbili za Simba na Yanga.
Mpaka sasa jumla ya mabao 101 yameshatinga wavuni wakati ligi ikiwa kwenye raundi ya saba, huku Simba ikiendelea kuongoza kwa kufunga mabao mengi ikiwa na mabao 16 ikifuatiwa na Yanga yenye 13.
Timu yenye safu butu ya ushambuliaji ni Mgambo JKT ikiwa na mabao mawili tu, huku kwa kipigo cha leo imeporomoka hadi nafasi ya 13 ikiipokea Prisons iliyopata ushindi wake wa kwanza na kuipeleka hadi nafasi ya 11.
Kwsa matokeo ya mwishoni mwa wiki ni kwamba Simba imeendelea kukaa kileleni ikiwa na pointi 15 ikifuatiwa na Yanga kisha JKT Ruvu zenye pointi 12 kila moja, kisha timu nne za Azam, Mbeya City, Coastal Union na Kagera zikifuatia zikiwa na pointi 11, huku Ashanti ikiendelea kuzibeba timu zote kwa kuwa na pointi mbili mpaka sasa licha ya kucheza mechi saba.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea Jumatano kwa mechi itakazozikutanisha timu za Rhino Rangers vs Mbeya City, mjini Tabora, huku Oljoro JKT itawalika Ruvu Shooting jijini Arusha, huku Azam itaikaribisha Mgambo JKT uwanja wa Chamazi na Mtibwa Sugar itaonyeshana kazi na JKT Ruvu Manungu, Morogoro.

Msimamo wa Ligi hiyo baada ya mechi za wikiendi hii ni kama ifuatavyo;
                                   P   W  D  L  F  A  GD  PTS
1. Simba                      7    4   3   0 16  5  11   15
2. Yanga                      7    3   3   1  13  7   6   12
3. JKT Ruvu                7    4   0   3   8   5   3    12
4. Kagera Sugar          7    3   2   2   8   5    3   11
5. Azam                      7    2   5   0   9   6   3   11
6. Mbeya City             7    2   5   0   8   6   2    11
7. Coastal Union         7    2   5   0   6   3   3   11
8. Ruvu Shooting         7   3   1   3   7   5   2    10
9.  Rhino Rangers        7   1   4   2   7   8   -1   7
10.Mtibwa Sugar         7   1  4   2   5   8    -3   7
11.Prisons                    7   1  4   2   4   9   -5   7
12. Oljoro                   7   1   2   4   4   8   -4   5
13.Mgambo                7   1   2   4   2  11  -9   5
14.Ashanti                 7    0   2   5   4  15 -11  2

Wafungaji:
8- Tambwe Amisi (Simba)
4- Didier Kavumbagu (Yanga)
3- Jerry Tegete (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Kipre Tchetche (Azam), Peter Michael (Prisons), Bakar Kondo (JKT Ruvu), Paul Nonga (Mbeya City), Themi Felix (Kagera Sugar)
2- Jonas Mkude (Simba), Jerry Santo, Haruna Moshi (Coastal Union), Elias Maguri (Ruvu Shooting), Saady Kipanga (Rhino Rangers), Mwagani Yeya (Mbeya City), Hamis Kiiza (Yanga), Machaku Salum (JKT Ruvu)
1- Abdi Banda, Crispian Odulla,(Coastal Union), Henry Joseph, Betram Mombeki, Ramadhani Singano (Simba), Haruna Niyonzima, Nizar Khalfan, Simon Msuva, Mrisho Ngassa (Yanga), Iman Joel, Salum Majid, Mwalimu Musuku, Kamana Salum, Hussein Abdallah (Rhino Rangers), Gaudence Mwaikimba, Seif Abdallah, Khamis Mcha, Aggrey Morris,  John Bocco, Joseph Kimwaga (Azam), Steven Mazanda, Richard Peter (Mbeya City), Laurian Mpalile (Prisons-OG), Shaaban Susan, Jerome Lembeli, Cosmas Ader, Said Dilunga (Ruvu Shooting), Juma Luzio, Masoud Ally, Shaaban Nditti, Shaaban Kisiga (Mtibwa Sugar), Shaaban Juma, Anthony Matangalu, Tumba Swedi, Paul Maono,            (OG) (Ashanti Utd), Abdallah Bunu, Emmanuel Switta, Amos Mgisa (JKT Ruvu), Fully Maganga, Hamis Msafiri (Mgambo JKT), Seleman Kibuta, Daud Jumanne, Maregesi Marwa, Godfrey Wambura, Clement Douglas (Kagera Sugar), Shaibu Nayopa, Amir Omary, Paul Malipesa, Expedito Kiduko (Oljoro JKT)

Mauaji ya Sheikh Rogo na wenzake yaiweka Mombasa roho juu

Sheikh Abou Rogo enzi za uhai wake. Mwanaharakati huyu wa Kiislama aliuwawa mwaka jana na juzi mrithi wake Ibrahim Rogo na wenzake waliuwawa kama alivyouwawa yeye kwa kupigwa risasi
HALI ya amani katika mji wa Mombasa imezidi kuwa tete, kutokana na makundi ya vijana wenye hasira kali kuendeleza machafuko katika viunga mbalimbali vya mji huo. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na BBC, jumla ya watu wanne wamepoteza maisha katika machafuko hayo, baada ya makundi ya vijana hao kupambana na askari wa kutuliza ghasia.


Habari kutoka nchini humo zinaeleza kuwa machafuko hayo yametokea siku moja baada ya kifo cha Sheikh Ibrahim Omar ‘Rogo’, aliyeuawa kwa kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana.

Katika shambulizi hilo, pia washirika watatu wa Sheikh Rogo nao wamepoteza maisha papo hapo, huku Salim Adbi akinusurika katika shambulizi hilo.

Kwa mujibu wa taarifa zaidi kutoka mjini Mombasa, vijana wenye hasira kali wameteketeza kanisa moja katika ghasia za juzi. 

Sheikh Ibrahim Rogo alikuwa mhubiri katika msikiti ambao ulikuwa unatumiwa kwa mahubiri na marehemu Sheikh Aboud Rogo, ambaye pia aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana mwaka jana.

Sheikh Aboud Rogo alishutumiwa kutoa mafunzo yenye itikadi kali yaliyowashawishi vijana kujiunga na kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab.

Kabla ya kifo chake, marehemu Aboud Rogo alidaiwa kuwa na uhusiano na kundi la kigaidi la Al Shabaab.

Tukio la kifo cha Sheikh Ibrahim Omar ‘Rogo’ limetokea ndani ya kipindi cha wiki mbili baada ya shambulizi la kigaidi la Westgate Mall, ambapo jumla ya watu 67 walipoteza maisha.

Ibrahim Rogo alionekana kama mrithi wa marehemu Aboud Rogo, alipohutubu katika msikiti huo.

Chelsea yaifumua Norwich City, Swansea wakifa ugenini


Mshikemshike wa pambano la Chelsea na Norwich City

Chelsea
Chelsea wakipogezana baada ya kuwatungua Norwich

VIJANA wa Jose Mourinho, Chelsea jioni hii wameifumua bila huruma Norwich City baada ya kuitandika mabao 3-1, huku Swansea City ikifa ugenini kwa kulazwa na Southampton ambayo imeendeleza rekodi ya nzuri ya katika Ligi Kuu ya England.
Bao la mapema la Oscar katika dakika ya 5 na mengine ya dakika za lala salama kupitia kwa Hazard na  William yalimpa faraja Mourinho kwa kuvuna pointi muhimu tatu.
Wenyeji walipata bao lao lililokuwa la kusawazisha katika dakika ya 68  kupitia kwa Pilkington ambalo lilionekana kama lingefanya matokeo kusaliwa bao 1-1 kabla ya Chelsea kucharuka na kupata mabao mawili dakika chache kabla ya pambano hilo kumalizika.
Katika mechi nyingine Southampton imeendeleza libeneke kwa kuizamisha Swansea waliowafuata kwa mabao 2-0 na kuinga kwenye Nne Bora ya msimamo wa Ligi hiyo ingawa kuna mechi mbili kwa sasa zinaendelea kuchezwa zinazoweza kubadilisha msimamo ulivyo.

Yanga yalipa kisasi kwa Mtibwa, yaipumulia Simba, Mgambo yalala nyumbani

Ngassa akipongezwa na wachezaji wenzake baada ya kufunga bao la kwanza
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga jioni imefanikiwa kulipa kisasi kwa Mtibwa Sugar kwa kuinyuka mabao 2-0 na kuwapumulia watani Simba wanaoongoza ligi wakiwa na pointi 15.
Ushindi huoi ambao ni wa pili mfulilizo kwa Yanga baada ya awali kuwa na matokeo mabaya, ulipatikana kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kufanikiwa kukata ngebe za Mtibwa waliotamba awali kuwa wangerejea ilichokifanya msimu uliopita walipoitungua Yanga 3-0 na kutimua kocha na baadhi ya viongozi.
Bao la mapema la dakika ya tano kwa winga mahiri nchini, Mrisho Ngassa na jingine dakika 19 baadaye kupitia kwa Didier Kavumbagu ambalo ni la nne kwake tangu msimu huu uanze, yalitosha kuwazima wapinzani wao ambao walilazimika kufanya mabadiliko ya wachezaji baada ya safu ya nyuma kupwaya.
Kocha Mecky Mexime alimtoa Salvatory Nteba na kumuungiza Dickson Daud kabla ya kumtoa tena Vincent Barnabas na nafasi yake kuchukuliwa na Masoud Mohammed.
Mabadiliko hayo yaliweza kuifanya Yanga ishindwe kufurukuta zaidi hadi walipomaliza dakika 45 za kwanza wakiwa na ushindi huo wa mabao 2-0, matokeo yaliyoendelea kuwepo hata katika kipindi cha pili na kuifanya Yanga ijikusanyie jumla ya pointi 12 sawa na JKT Ruvu ambayo jana iliilaza Kagera Sugar mabao 2-1, lakini mabingwa watetezi wakiwa na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Katika mchezo nwingine uliochezwa uwanja wa Mkwakwani Tanga, Mgmabo JKT ilikumbana na kipigo cha kushtukiza kutoka kwa  Prisons ya Mbeya kwa bao lililotupiwa na mfungaji mahiri wa timu hiyo ya maafande wa Magereza Peter Michael likiwa bao lake la nne msimu huu.
Ligi hiyo itaendelea tena siku ya Jumatano kwa miuchzero kadhaa wakati huo Yanga itakuwa ikianza safari ya kuifuata Kagera Sugar katika pambano lao litakalochezwa Jumamosi kwenye uwanja wa Kaitaba mjini Kagera.

Hivi ndivyo dada wa Mhe Freeman Mbowe alivyozikwa mjini Moshi jana


MWENYEKITI wa Chadema Freeman Mbowe akiweka shada la maua kwenye kaburi la marehemu dada yake,Grace Mbowe, huko Moshi jana.
 Mwenyekiti mtendaji wa makampuni ya IPP Reginald Mengi akiweka shada la maua kwenye kaburi la dada wa Freeman Mbowe.
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge,William Lukuvi akiweka shada la maua kwenye kaburi la dada wa Freeman Mbowe.
 Mbunge wa jimbo la Arusha mjini Godbless Lema akiweka shada la maua kwenye kaburi la dada wa Freeman Mbowe. 
 
Picha na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii

Hussein Gobossi hoi kwa Adam Ngange

Bondia Adamu Ngange kushoto akipambana na Hussein Gobossy wakati wa mpambano wao wa masumbwi uliofanyika katika ukumbi wa Sonata uliopo Chanika Dar es salaam jana Ngange alishinda kwa K.O ya raundi ya nne.
Bondia Adamu Ngange kushoto akipambana na Hussein Gobossy wakati wa mpambano wao wa masumbwi uliofanyika katika ukumbi wa Sonata uliopo Chanika, Dar es salaam jana Ngange alishinda kwa K.O ya Raundi ya Nne.
Adamu Ngange katikati akiwa na kocha wake
Bondia Hussein Gobossy  kushoto akipambana na Adamu Ngange wakati wa mpambano wao wa masumbwi uliofanyika katika ukumbi wa Sonata uliopo Chanika Dar es salaam jana Ngange alishinda kwa K.O ya raundi ya nne.
Bondia Adamu Ngange akisubili kupigana na mpinzani wake
Bondia Adamu Ngange kulia akimwangalia bondia HUSSEIN GOBOSSY ambaye alikimbia ulingoni kwa kipigo kikali ambapo mvua ya makonde ilikuwa ikimwelemea.
Bondia Adamu Ngange akinyosha mikono juu baada ya mpinzani wake kuingia mitini kwa kukimbia mchezo huo

PAMBANO LA RUVU, SIMBA LAINGIZA MIL 75/-

 
Na Boniface Wambura
PAMBANO la Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya wenyeji Ruvu Shooting na Simba lililochezwa jana (Oktoba 5 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 75,692,000.

Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo namba 43 la VPL msimu wa 2013/2014 lililomalizika kwa timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 walikuwa 13,395.

Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 17,983,902.31 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 11,546,237.29.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 9,144,357.11, tiketi sh. 3,183,382, gharama za mechi sh. 5,486,614.26, Kamati ya Ligi sh. 5,486,614.26, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,743,307.13, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) sh. 1,066,841.66 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,066,841.66.