STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, April 17, 2014

'Mzee Gurumo kama alikiona kifo mapema hospitalini

Masheikh wakiendelea na kisomo cha kumuombea Mzee Gurumo katika safari yake ya Ahera

Mwili wa Mzee Gurumo ukitolewa kwenye nyumba yake ya Mabibo tayari kwa safari ya kwenda kuzikwa Masaki

Mzee Jangala na JB wakiteta kwenye msiba wa Mzee Gurumo, Mabibo

Juma Ubao akimuelezea Mzee Gurumo kwa waandishi wa Habari

Umma uliojitokeza Masaki

Kaburi alilozikiwa Mzee Gurumo

Shamsa Ford alikuwapo kumsindikiza Mzee Gurumo

Said Mabela kizungumza na wanahabari

Jeneza la mwili wa Mzee Gurumo likiswaliwa Mabibo
Mwili waq Gurumo ulitoka kuswaliwa msikiti wa kijijini kwao Masaki

HUWEZI kujua ni kitu gani kilimjia, lakini ukweli ni kwamba saa chache kabla ya kufariki, gwiji wa muziki wa dansi nchini, Muhidini Gurumo aliyefia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), alikiona kifo chake na kujaribu 'kukikwepa'.
Inaelezwa Gurumo asubuhi ya Jumapili, alitoroka hospitalini hapo kabla ya kushtukiwa na kurudishwa wodini huku akiieleza familia yake amechoka kukaa hapo na kutaka aende nyumbani.
Kwa mujibu wa mmoja wa wanafamilia, Gurumo alitaka akakae nyumbani japo siku mbili kisha arejee hospitalini kuendelea na matibabu.
"Huwezi kuamini alitoroka wodini na kukamatiwa getini, tulimweleza haoni aibu kama wanahabari wakijua alitaka kutoroka bila ruksa ya daktari, lakini alidai asingejali kwa vile amechoka kukaa hospitalini hapo," alisema mwanafamilia huyo anayedai ameoa nyumba moja na Gurumo.
Aliongeza walimbembeleza na kumuahidi kumuombea ruksa kwa daktari wake ili aende nyumbani kwa siku nne badala ya mbili alizotaka na kutulia.
"Niliachana naye saa 7:30 mchana akiridhika akijua mpango huo utafanyika Jumatatu, ila nilipofika Mbagala nilipigiwa simu amefariki, nahisi huenda alikiona kifo mapema ndiyo maana alitaka kuondoka hospitalini."
Naye mdogo wa marehemu, Yahya Mikole alisema mara kadhaa Gurumo alimsisitizia akifa asizikwe haraka ili kutoa nafasi watu kuhudhuria mazishi yake.
"Alidai asizikwe haraka kama Tx Moshi William, ndiyo maana tumezingatia wosia wake na kumzika Jumanne badala ya Jumatatu," alisema Mikole.

ELIMU
Siyo katika muziki tu, Gurumo japo hakubahatika kusoma sana elimu ya kawaida zaidi ya ile ya dini ya Kiislam, lakini alikuwa mdau mkubwa wa sekta ya elimu.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Fatma Lusindilo alifichua kwenye msiba wa Mzee Gurumo kijijini kwake Masaki wakati akitoa ubani wao wa Sh.400,000 kwa familia ya marehemu, akidai enzi za uhai wake Gurumo alijali na kuthamini elimu kwa kuchangia kila mara Mfuko wa Elimu wa wilaya hiyo.
"Kwa mchango wake kwa jamii, tunatoa mkono wa pole kwa familia kiasi cha Sh.400,000, tunawaomba muwe na subira katika kipindi hiki kigumu," alisema DC Fatma.

CHOKI
Mkurugenzi wa Extra Bongo, Ally Choki, mmoja wa waombolezaji waliojitolea kwa hali na mali katika msiba wa Gurumo kama ilivyokuwa kwa Ruge Mutahaba na Lady Jaydee waliotoa usafiri kusafirisha waombolezaji, alisema itamchukua muda mrefu kusahau msiba wa Gurumo.
Choki alisema yeye ni kati ya wanamuziki wachache na wa pekee kwa kizazi kipya kuimba na Gurumo akirejea albamu yao akiimba vyema wimbo wa Kassim wa Kutumia.
"Ni pigo kwa wadau wa muziki na familia nzima ya gwiji huyo, lakini kwangu ni pigo zaidi kwa vile ndiye pekee wa kizazi cha sasa niliyeimba naye kazi binafsi, ila nadhani ni mipango ya Mungu nami kubakiwa na kumbukumbu yake," alisema Choki ambaye aliurudia wimbo wa Gurumo wa 'Kassim', ambao Choki aliimba sauti ya gwiji huyo.

SIFA
Waombolezaji wakiwamo viongozi na wanamuziki wenzake walimmiminia sifa Gurumo wakidai alikuwa mfano Tanzania, kiasi cha Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Ado Novemba alidiriki kumtaja kama 'Nyerere wa Muziki'.
Said Mabela aliyechukuliwa na Gurumo kutoka Kurugenzi Jazz ya Arusha mwaka 1973, alisema hana cha kusema zaidi ya kumuombea safari njema na atamkumbuka kwa mengi hasa katika kupeleka mbele muziki wa Tanzania.
Shaaban Dede, Juma Ubao, Kassim Mapili, Jamhuri Kihwelu, Shem Ibrahim Kalenga, Mafumu Bilal 'Bombega' na wengine walisema Gurumo ameacha pengo katika fani ya muziki na michezo kwani enzi za uhai wake alikuwa shabiki wa Simba ya Dar es Salaam na Manchester United ya Uingereza bila kificho.
Waliohudhuria msiba wa Gurumo mbali na Makamu wa Rais, Dk Gharib Bilal ni DC wa Kinondoni, Jordan Rugimbana, Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan, Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, Makamu wa Rais wa zamani wa TFF, Nassib Ramadhan, MB Doggy, Dully Sykes, Omar Tamba, Idd Seleman, Chiki Mchoma na wengine.

MAZISHI
Gurumo muasisi wa miondoko na bendi za Msondo Ngoma, Sikinde na Ndekule' aliyezipigia pia Kilimanjaro Chacha, Kilwa Jazz na Orchestra Safari Sound (OSS), alifariki saa 9 ya Jumapili na kuzikwa saa 7:53 ya Jumanne  kijijini kwao.
Alisumbuliwa na maradhi ya mapafu na moyo kwa miaka zaidi ya miwili na kusababisha kustaafu muziki Septemba mwaka jana.
Safari ya maziko yake ilianza saa 2 asubuhi mwili wake kutolewa Muhimbili na kuletwa nyumbani kwake saa 2:45 na kupokewa na umati wa waombolezaji kabla ya kuswaliwa saa 4:38 na saa 4:57 kusafirishwa kwenda Kisarawe.
Msafara kuelekea kijijini uliongozwa na gari la kubebea wagonjwa la Hospitali ya Mwananyamala na kuwasili saa 7:09 kisha kuswaliwa tena msikiti wa kijiji hicho na kuzikwa saa 7:53 kuhitimisha safari yake ya miaka 74 duniani.
Marehemu Gurumo aliyezaliwa 1940 ameacha mjane Pili bint Said na watoto sita na enzi za uhai wake alitamba na nyimbo mbalimbali ukiwamo wa 'Kassim Na.1' na Na.2.

Wednesday, April 16, 2014

Everton yafa nyumbani, Man City chupuchupu kwa Sunderland

Fernandinho
Fernandinho akiifungia City bao la kuongoza dhidi ya Sunderland
Jason Puncheon
Wachezaji wa Crystal Palace wakishangilia moja ya mabao yao wakati wakiizamisha Everton kwao
Manchester City's Samir Nasri scores his side's equaliser
Samir Nasir akiisawazishia Manchester City bao la pili dhidi ya Sunderland
Kevin Mirallas of Everton goes past Julian Speroni to score his side's second goal
Everton walipokuwa wakifurukuta kwa Crystal Palace na kuangukia pua usiku huu
Connor Wickham of Sunderland scores their first goal past Joe Hart of Manchester City
Sunderland wakiandika moja ya mabao yao langoni mw Manchester City usiku huu
TIMU ya Everton imeshindwa kurejea kwenye nafasi ya nne ya Ligi Kuu ya England baada ya kujikuta ikipokea kipigo cha mabao 3-2 kwenye uwanja wake wa nyumbani, huku Manchester City wakiponea chupuchupu kwa Sunderland na kulazimisha sare ya 2-2 nyumbani bila kutarajiwa.
Everton iliyoipisha Arsenal katika nafasi ya nne baada ya The Gunners kupata ushindi mnono jana wa mabao 3-1, ilishuktukizwa na Crystal Palace waliowafuata uwanja wa Godson Park kwa kufungwa bao  dakika ya 23 kupitia Jason Puncheon goli lililodumu hadi mapumziko.
Kipindi cha pili kilianza kwa wageni kuandikisha bao la pili kupitia kwa Scott Dann dakika nne baada ya kuanza kwa kipindi hicho kabla ya Steven Naismith kuifungia Everton bao la kwanza la kufutia machozi dakika ya 61.
Wageni waliongeza bao la tatu dakika ya 73 kupitia kwa Cameron Jerome kabla ya Kevin Mirallas akaifungia wenyeji bao la pili la kufutia machozi dakika nne kabla ya mchezo huo kuisha.
Kwa matokeo hayo Everton amesaliwa nafasi ya tano na pointi 66, moja zaidi ya ilizonazo Arsenal huku wakiwa wamecheza mechi 33 kila mmoja, Crystal Palace wamechupa hadi nafasi ya 11 wakiwa na pointi 40.
Katika pambano jingine la mfululizo wa ligi hiyo, Manchestwer City ikiwa uwanja wa nyumbani ilishtukizwa na vibonde, Sunderland kwa kulazimishwa sare ya mabao 2-2.
Wenyeji walianza kuandika bao dakika ya pili lililofungwa na Fernandinho akimalizia kazi nzuri ya Kun Aguero.
Hata hivyo Sunderland wanaopigana kuepuka kushuka daraja ilirejesha bao hilo kupitia kwa Cannor Wickham katika dakika ya 73 kabla ya mchezaji huyo huyo kuongeza bao la pili lililowakata maini Manchester City katika harakati za kupunguza pengo la pointi dhidi yake na vinara Liverpool na waliopo nafasi ya pili Chelsea watakaoumana nao hivi karibuni.
Bao hilo la pili Wickham alilifunga katika dakika ya 83 kabla ya Samir Nasir kusawazisha bao hilo dakika mbili kabla ya mchezo huo kumalizika na kuifanya City kuambulia pointi moja na kufikisha 71, nne pungufu na za Chelsea yenye 75 na sita na ilizonazo Livewrpool yenye pointi 77, huku Sunderland ikisalia mkiani na pointi 26.

Bayern yaua sasa uso kwa uso na Dortmund Kombe la Ujerumani

http://images.sportinglife.com/12/02/800x600/Bayern-Munich-celeb-v-Kaiserslautern_2717058.jpgBAYERN Munich imezinduka toka kwenye vipigo mfululizo vya Ligi Kuu ya Ujerumani kwa kuifumua Kaiserslautern kwa mabao 5-1 na kutinga fainali ya Kombe la FA (DFB-Pokal).
Ushindi huo iliypopata nyumbani imeifanya Bavarians hao kukutana na mahasimu wao Borussia Dortmund iliyotangulia hatua hiyo ya fainali tangu jana kwa kuilaza Wolfsburg kwa mabao 2-0.
Bayern ilipata ushindi wake huo kwa mabao ya Schweinsteiger aliyefunga dakika ya 23,Tom Kroos dk ya 32, Thomas  Müller kwa penati dakika ya 50 kabla ya wageni wao kufunga dakika ya 60 kupitia Zoller.
Mabao mengine ya washindi yalifungwa na Mandžukić dakika ya 78 na Mario Götze dakika za lala salama.

Tuesday, April 15, 2014

Azam yawekwa rekodi saba Tanzania Bara

Mabingwa wa Tanzania Bara, Azam Fc
TIMU ya Azam ambayo juzi ilitwaa ubingwa wa Tanzania Bara kwa msimu wa 2013/14, imeweka rekodi saba kwenye medani ya soka nchini.
Azam iliifunga Mbeya City mabao 2-1 kwenye uwanja wa Sokoine na kuweka rekodi ya kuwa timu pekee iliyoifunga timu hiyo kwenye uwanja wake wa nyumbani.
Awali, Mbeya City ilikuwa haijawahi kufungwa kwenye uwanja wake wa nyumbani kabla ya rekodi yake kuvunjwa na Azam.
Mabingwa hao wameifikia pia rekodi ya Simba ya kutwaa ubingwa bila ya kupoteza mechi ya msimu wa 2009/10 na sasa wanafukuzia rekodi nyingine ya 'Wekundu wa Msimbazi' ya kumaliza msimu bila ya kupoteza mechi wakati watakapowakabili JKT Ruvu katika mechi yao ya mwisho ya msimu.
Mbali na hilo, pia wameweka rekodi ya kuwa timu ya tisa kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara tangu ligi hiyo ilipoanza.
Azam pia imekuwa ni timu ya saba kutwaa ubingwa huo nje ya miamba wawili wa soka nchini ambao wamekuwa wakipokezana ubingwa huo, Simba na Yanga.
Timu nyingine ambazo zimeshawahi kufanya hivyo, nazo ni Cosmopolitan ya Dar es salaam mwaka 1967, Mseto Sports ya Morogoro (1975), Pan African (1982), Tukuyu Stars (1986), Coastal Union (1988) na Mtibwa Sugar mwaka 1999 na 2000.
Rekodi nyingine ni kuwa timu ya tano kutoka jijini Dar es Salaam kutwaa ubingwa wa Bara, ikizifuata timu za Simba, Yanga, Cosmopolitan na Pan African.
Lakini vile vile Azam imekuwa ni timu ya kwanza kutoka nje ya Manispaa ya Ilala kutwaa ubingwa kwani timu za Simba, Yanga, Cosmopolitan na Pan African zinatoka Ilala, huku yenyewe ikitokea Temeke.
Vile vile imekuwa ni timu ya pili ya kampuni kutwaa ubingwa nchini baada ya Mtibwa Sugar kufanya hivyo mwaka 1999 na 2000.
Timu hiyo imetwaa ubingwa kwa pointi 59 ambazo hazitafikiwa na timu yoyote kwenye mechi ya kuhitimisha Ligi Kuu Jumamosi.
Wakati huo huo, Sanula Athanas, anaripoti kuwa wadhamini wakuu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania, wameipongeza Azam FC kwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo msimu huu msimu ikiwa ni mara ya kwanza tangu ipande miaka saba iliyopita.
Azam inayonolewa na Mcameroon Joseph Omog ilitwaa ubingwa huo juzi baada ya kuifunga Mbeya City 2-1 katika raundi ya 25 ya ligi hiyo na kufikisha pointi 59 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote msimu huu.
Mara tu baada ya kumalizika kwa mechi hiyo kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini Mbeya juzi, Meneja Uhusiano wa Nje wa kampumi hiyo, Salum Mwalim alisema wameridhishwa na kiwango cha Azam FC pamoja na timu zote zinazoshiriki katika ligi na hivyo wanawapongeza kwa dhati timu hiyo kutwaa taji.
"Tunawapongeza Azam kwa kuwa bingwa mpya wa VPL kwa sababu wamekabiliana vema na mikikimikiki ya ligi, hivyo ubingwa wao haukuwa mwepesi kuupata kutokana na ushindani uliokuwapo kwa timu zote shiriki," alisema Mwalim.
"Tunaamini ubingwa huu wa Azam utaifanya ligi msimu ujao kuwa ngumu zaidi kwani timu za Yanga na Simba ambazo zimekuwa zikipokezana ubingwa tangu 2001 zitataka kurudisha heshima yao na nyingine zikipata nguvu kwa kuwa yoyote inaweza kuwa bingwa, na hilo likitokea ubora wa ligi yetu utazidi kupaa," alisema zaidi Mwalim.
Alisema Azam watakabidhiwa kombe lao la ubingwa Jumamosi kwenye uwanja wao wa nyumbani, Chamazi jijini Dar es Salaam wakati wa mechi yao ya mwisho dhidi ya JKT Ruvu.
Aidha Mwalim amezipongeza timu zote 14 zilizoshiriki ligi hiyo kwa kujituma na kutoa changamoto katika kila mechi jambo lililofanya bingwa kutopatikana kwa urahisi na mapema.

Taswira katika msiba wa Gurumo













Monday, April 14, 2014

Idadi ya waliokufa kwa mafuriko yaongezeka

Baadhi ya nyumba zilizozungukwa na maji


IDADI ya waliokufa kutokana na mafuriko jijini Dar es Salaam imefikia watu 13 kufikia Jumatatu.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Sadiq Meck Sadiq amesema idadi hiyo huenda ikaongezeka baada ya kupata taarifa za matukio ya mafuriko kutoka maeneo yote ya mkoa wa Dar es Salaam.
Kwa siku tatu mfululizo tangu Ijumaa iliyopita, mvua kubwa ziliendelea kunyesha na kusababisha madhara makubwa vikiwemo vifo, uharibifu wa miundombinu ya barabara na madaraja, hivyo kukata mawasiliano na mikoa ya jirani ya Pwani na Morogoro na hata ndani ya mkoa wenyewe. Karibu maeneo yote ya mkoa wa Dar es Salaam yameathirika kutokana na mvua kubwa zilizonyesha na kusababisha mafuriko, huku wakaazi wa maeneo ya mabondeni wakiathirika zaidi baada ya nyumba zao kujaa maji. Miundombinu ya barabara na madaraja mbalimbali yanayounganisha jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake pia imeharibiwa.
Picha ya Anga ya mafuriko jijini Dar
Mradi mwingine muhimu wa mabasi yaendayo kasi, DART unaolenga kutatua tatizo la usafiri jijini Dar es Salaam, nao umeathiriwa na mafuriko hayo ambapo magari, mashine na mifuko ya saruji imechukuliwa na maji hivyo kusitisha shughuli zake za ujenzi zilizo katika hatua za mwisho za kukamilisha mradi huo.
Shughuli za urejeshaji wa miundombinu zimekuwa zikiendelea ikiwa ni pamoja na matengenezo katika daraja la Mpiji linaloiunganisha mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Hata hivyo Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania, TMA, yametahadharisha kuhusu kuendelea kunyesha kwa mvua na kuwataka watu wanaoishi katika maeneo hatarishi kuhama ili kusalimisha maisha na mali yao.
BBC

Kocha Azam kicheko kitupu baada ya ubingwa

Kocha Joseph Omog (kushoto) toka Cameroon akiwa na msaidizi wake
KOCHA Mcameroon, Joseph Marius Omog amefurahia ushindi wa jana wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji Mbeya City Uwanja wa Sokoine ulioihakikishia ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara timu yake, Azam FC, lakini amewaambia wachezaji wake, pati ni baada ya mechi ya mwisho Aprili 19, mwaka huu.

“Ni furaha sana, tumepambana sana, haikuwa kazi nyepesi, tumepitia mechi ngumu tangu naanza kazi hapa, lakini tulibaki kwenye dhamira yetu na tukaendelea kupambana hatimaye tumetimiza malengo. Sote tuna furaha sasa, kila mtu ana sababu ya kufurahia kazi yake kati yetu,”alisema Omog.

Omog amewataka wachezaji wake kutobweteka na matokeo ya jana, na badala yake waelekeze nguvu zao katika mchezo wa Aprili 19, ili washinde na kukabidhiwa Kombe kwa furaha. 

“Nasikia Yanga walikata rufaa, hata kama haina maana, lakini lazima tushinde mechi ya mwisho, wachezaji wangu wanajua hilo, nimewaambia,”alisema.

Mabao ya Gaudence Mwaikimba na John Bocco ‘Adebayor’ kila kipindi jana yalitosha kuihakikishia Azam FC ubingwa wa Ligi Kuu Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya dhidi ya bao la Mwagane Yeya.

Ushindi huo, umeifanya Azam ifikishe pointi 59 ikiwa na mchezo mmoja mkononi ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote baada ya mechi za mwisho Aprili 19, mwaka huu.

Nafasi ya pili tayari ni Yanga SC yenye pointi 55 sasa baada ya jana kuifunga JKT Oljoro 2-1 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha ambayo kama itawafunga pia na Simba SC wiki ijayo itafikisha pointi 58, ambazo haziwezi pia kufikiwa na timu za chini
yake.

Azam FC itacheza mechi ya mwisho nyumbani, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam Jumamosi wiki hii, dhidi ya JKT Ruvu ikiwa na dhamira ya kushinda ili kuweka rekodi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu bila kupoteza mechi.

Kikosi cha Azam kinaondoka leo Saa 10:00 mjini Mbeya kwa ndege kurejea Dar es Salaam na wachezaji watapewa mapumziko ya siku moja kabla ya kukutana kwa maandalizi ya mchezo wa kufungia pazia la msimu. 

LIWAZO ZITO

Rais JK naye amlilia Mzee Gurumo

Rais Jakaya Kikwete akimpongeza Mzee Gurumo enzi za uhai wake baada ya kumkabidhi tuzo maalum ya mchango wake kwa taifa kupitimia muziki
RAIS Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kutokana na kifo cha mwanamuziki maarufu na wa siku nyingi, Muhidini Gurumo kilichotokea juzi mjini Dar es Salaam.

Gurumo alifariki dunia jana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya ugonjwa wa moyo uliomsumbua kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Rais Kikwete alisema mchango wa marehemu Gurumo kwa Taifa ni mkubwa na wa kupigiwa mfano kupitia kipaji alichojaaliwa na Mwenyezi Mungu ambacho alikitumia kikamilifu kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla.

“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa na taarifa za kifo cha Gurumo ambaye alikuwa mmoja wa wasanii wa muziki wa dansi nchini waliolitumikia Taifa hili kwa bidii tangu miaka ya sitini kupitia sanaa ya muziki,

Katika bendi mbalimbali za muziki wa dansi kuanzia Bendi ya NUTA Jazz, Mlimani Park Orchestra, Orchestra Safari Sound (OSS) na Msondo Ngoma ambayo ameitumikia hadi alipostaafu mwaka 2013,”alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alimuomba Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kumfikishia salamu zake za rambirambi na pole nyingi kwa familia ya marehemu Gurumo kwa kumpoteza kiongozi na mhimili wa familia yao.

Alisema anaungana na familia ya marehemu kuomboleza msiba huo mkubwa kwa kutambua kuwa msiba wao ni wa wote, na anamuomba Mwenyezi Mungu.

Aliwaomba wanafamilia ya marehemu kuwa na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha kuomboleza msiba wa mpendwa wao kwa kutambua kwamba yote ni mapenzi ya mola.

Man City yapata pigo kwa Yaya Toure

KLABU ya Manchester City imepata pigo baada ya kufahamika kuwa huenda kiungo wake mahiri Yaya Toure asicheze tena msimu huu baada ya kuumia katika mchezo dhidi ya Liverpool uliochezwa mwishoni mwa wiki katika Uwanja wa Anfield. 
Nyota huyo wa kimataifa wa Ivory Coast alitolewa nje wakati wa kipindi kwanza na kusababisha hali kuwa mbaya kwa kikosi chake na kupelekea kufungwa mabao 3-2 na mahasimu wao hao katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu. 
Akihojiwa kuhusiana na hali ya nyota huyo, kocha wa City Manuel Pellegrini amesema itakuwa ngumu kwa mchezaji huyo kumaliza msimu huu. 
Toure alijiumiza mwenyewe baada ya kupiga shuti lililopaa katika mchezo huo wakati City wakijaribu kurejea baada ya kufungwa bao la kuongoza na Raheem Sterling.

Lyon yaidonyoa PSG kimoja Ufaransa

Mfungaji wa bao pekee la Lyon, Ferri (12) akipambana uwanjani dhidi ya PSG jana
MABINGWA watetezi wa Ligi ya Ufaransa, PSG jana ilionja kipigo chake cha kwanza baada ya mfululizo wa ushindi katika ligi hiyo kwa kudonyolewa goli 1-0 dhidi ya Olympique Lyon.
Ikicheza ugenini, PSG ilishindwa kufuruka kwa Lyon waliopata bao lao katika dakika ya 31 kupitia kwa Jordan Ferri.
Pamoja na kwamba kipigo hicho hakijaiteteresha matajiri hao wa Paris, lakini imefanya pengo la pointi baina ya wapinzani wanaowafukuzia kileleni, Monaco kuwa pointi 10 badala ya 13 ya awali baada ya Monaco kupata ushindi ugenini siku ya Jumamosi dhidi ya Rennes.
PSG imeendelea kusaliwa na pointi zake 79, huku Monaco wakiwa nafasi ya pili na pointi zao 69 huku timu zote zikiwa zimecheza michezo 33 na kusaliwa na mechi tano kabla ya kufungia msimu wa 2013-2014.

BASATA waomboleza kifo cha Gurumo


Mzee Gurumo enzi za uhai wake
BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa msanii nguli wa tasnia ya muziki wa Dansi nchini Muhidini Mwalimu Gurumo


“ Baraza limestushwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa ya kifo hiki cha Muhidini Maalimu Ngurumo ambaye mchango wake katika muziki wa dansi ni mkubwa mno na  unahitajika sana, pengo aliloliacha ni kubwa kwani ubunifu wake bado unahitajika katika tasnia hii.” 
Baraza linatoa pole kwa familia ya marehemu na wasanii wote nchini, aidha tunawatakia moyo wa subira katika wakati huu wa majonzi ya kuondokewa na mpendwa wetu.
Mwenyezi Mungu aipumzishe mahala pema peponi roho ya marehemu. Baraza liko pamoja na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Imetolewa na
Godfrey Mngereza
Kaimu Katibu Mtendaji

Baraza la Sanaa la taifa

Katibu Mkuu wa FIFA kutua Dar Mei 1

KATIBU MKUU WA FIFA KUFUNGUA SEMINA DAR
Katibu Mkuu wa FIFA

KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Jerome Valcke atawasili nchini Mei 1 mwaka huu ambapo atafungua semina ya mawasiliano itakayoshirikisha viongozi wa vyama wanachama wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
 
Akizungumza Dar es Salaam leo (Aprili 14 mwaka huu), Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema Valcke ambaye hii ni mara yake ya kwanza kuja Tanzania atafuatana na maofisa wengine wa saba wa FIFA.

Amesema semina hiyo iliyoandaliwa na FIFA itafanyika kwa siku mbili (Mei 1 na 2 mwaka huu) ambapo vilevile Valcke atapata fursa ya kuzungumza na waandishi wa habari wa ndani na wa kimataifa.

Rais Malinzi amesema washiriki wa semina hiyo ni marais, makatibu wakuu na wakuu wa mawasiliano wa wanachama 12 wa CECAFA ambao ni Burundi, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somali, Sudan, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda.

Naye Mwenyekiti wa CECAFA, Leodegar Tenga ambaye alifuatana na Katibu Mkuu wake Nicholas Musonye amemshukuru Rais wa TFF kwa kukubali kuwa mwenyeji wa semina hiyo kwani itasaidia katika maendeleo ya mpira wa miguu katika ukanda huu

Bomu jingine lalipuka jijini Arusha

Kijana ambaye hakufahamika jina lake baada ya kupata majeraha makubwa mguuni.

Hali ya sintofahamu iliyowakumba wakazi wa jiji la Arusha baada ya bomu kulipuka jana.
Majeruhi baada ya bomu kulipuka.
Mmoja wa majeruhi akiwa hoi baada ya mlipuko.
Taarifa kutoka mjini Arusha zinasema bomu la kutengenezwa kwa mkono lililipuliwa jana usiku April 13 kwenye Baada iitwayo Arusha Night Park, iliyopo eneo la Mianzini jijin i Arusha na kusababisha watu kadhaa kujeruhiwa, huku taarifa zingine zikisema watu wawili wamepoteza maisha katika mlipuko huo kwamba ni watu 15 wamejeruhiwa kwenye mlipuko huo.
Inaelezwa watu 15 walithibitishwa kuumia katika mlipuko huo wa tatu kutokea mkoani humo kwa kipindi cha mwaka mmoja baada ya tukio la mlipuko kanisani na kwenye mkutano wa CHADEMA na kupelekea vifo vya watu kadhaa.
Inaelezwa wengi wa majeruhi katika mlipuko huo wa jana ni wahudumu wa baa hiyo pamoja na waliojitokeza kuangalia mpira kqwenye truninga na kwamba walikimbizwa hospitali za Mount Meru, Seliani na St. Elizabeth kwa ajili ya matibabu zaidi.

Mzee Gurumo kuagwa na kuzikwa kesho

Mzee Gurumo enzi za uhai wake akiwa na mkewe kipenzi, Pili bint Said Kitwana

Waombolezaji wakiwa wamekusanyika nyumbani kwa marehemu Muhidin Gurumo maeneo ya Mabibo Makuburi, Dar es Salaam.
Mke wa marehemu Gurumo (kulia) akifarijiwa na baadhi ya jamaa zake kwenye msiba wa mumewe nyumbani kwake Makuburi.
MWILI wa gwiji wa muziki wa dansi nchini, marehemu Muhidin Gurumo 'Mjomba' unatarajiwa kuagwa rasmi kesho kuanzia saa 2 asubuhi kabla ya kusafirishwa kijijini kwao Masaki kwa ajili ya maziko yatakayofanyika mchana.
Awali ilipangwa marehemu Gurumo aliyefariki jana katika hospitali ya Muhimbili azikwe leo, ila kwa kuzingatia wosia ulioachwa na kusisitizwa na gwiji huyo enzi za uhai kuwa,  asiharakishwe kuzikwa mapema familia imeamua kutii wosia huo.
Akizungumza na MICHARAZO nyumbani kwa marehemu Gurumo, Mabibo External, Msemaji wa familia, Yahya Mikole alisema mara kadha Mzee Gurumo alikuwa akiwasisitiza kuwa atakapokufa asizikwe kwa haraka.
Mikole ambaye ni mdogo binamu wa marehemu alisema, Mzee Gurumo alikuwa akimwambia kwa kuwa yeye ni mwanamuziki mkubwa na maarufu kuharakishwa kuzikwa kwake kunaweza kuwanyima wengine kumuaga au kuhudhuria maziko yake.
"Kwa kuzingatia hilo na ombo toka serikali, tumeamua kusogeza shughuli za mazishi ya merehemu kutoka leo mpaka kesho kwa utaratibu wa kuagwa kuanzia saa 2-4 asubuhi kabla ya kuondoka kwenda kumpumzisha kijijini kwao majira ya saa 7 mchana," alisema Mikole.
Msemaji huyo alieleza marehemu alikuwa akisumbuliwa na tatizo la mapafu na uigonjwa wa moyo na juzi kabla ya kifo chake alipatwa na tatizo la ukosefu wa damu ambapo alipofikishwa Muhimbili aliwekewa chupa tatu za damu.
"Tatizo la ukosefu wa damu lilijitokeza juzi na aliwekewa chupa tatu zilizoisha asubuhi ya jana kabla ya alasiri kupoteza maisha, huku akionekana mwenye afya yake ya kawaida kabisa," alisema Mikole.
Mikole alisema taratibu za mazishi ya marehemu zinaendelea kama kawaida nyumbani kwa marehemu.
Kwenye msiba huo watu mbalimbali wakiwamo wanamuziki wa zamani na walio wahi kufanya kazi na marehemu walihudhuria kama akina Juma Ubao, Mjusi Shemboza, Karama Regesu na wengine.
Marehemu Gurumo aliyezaliwa mwaka 1940 ameacha mjane mmoja na watoto sita, watatu wa kiume ambao ni Abdallah, Omar na Mwalimu na wa kike pia wakiwa watatu ambao ni Mariam, ambaye ndiye mtoto mkubwa wa marehemu, Mwazani na Kibibi aliye wa mwisho kuzaliwa.
Hata hivyo wakati wa uhai wake alipozungumza na Mmiliki wa blogu hii alisema ana watoto wanne, lakini Msemaji huyo wa familia alifafanua mzee Gurumo 'alichepuka' ila hakupenda kuzungumzia suala la watoto wake hao wengine japo wanafamilia wanawatambua na wameshajulishwa msiba huo.

Julio amlilia Mzee Gurumo

Jamhuri Kihwelu 'Julio'
KOCHA maarufu wa soka na mdau mkubwa wa bendi ya Msondo Ngoma, Jamhuri Kihwelu 'Julio' amemlilia nguli wa bendi hiyo, Muhidini Gurumo akidai kifo chake ni pigo kwa familia, wadau wa muziki na michezo nchini.
Julio aliyewahi kuichezea na kuinoa Simba kabla ya kutua Mwadui-Shinyanga na kukaribia kuipandisha Ligi Kuu, alisema kifo cha Gurumo kwake ni pigo kubwa kwani alikuwa ni mjomba wake mbali na unazi wao wa Simba na Msondo.
Alisema yeye binafsi ameumia sana kwa msiba wa mwanamuziki na mwanachama huyo wa Simba kama ambavyo wadau wa fani za muziki na michezo walivyoumizwa na kudai ni vigumu kupatikana wa kuziba pengo lake.
"Kwa hakika nimeumia kama walivyoumia wadau wa michezo na muziki kwani enzi za uhai wake, Gurumo alikuwa mwanachama wa Simba na pia ni gwiji wa muziki ambaye hakuwa na mfano wake katika kizazi chake," alisema Julio.
Julio, alisema marehemu Gurumo alikuwa mmoja wa watu wa mfano kwa kule kuipenda fani yake na kujali masilahi ya wanamuziki, mbali na kufanya kazi kwa umri mkubwa mpaka miezi michache alipotangaza kustaafu.
Alisema kustaafu na mwisho kufa kwake, kumeifanya krimu na safu ya mbele ya Msongo imetoweka baada ya kuondoka kwa Tx Moshi, Joseph Maina, Athuman Momba na Suleiman Mbwembwe.
"Itatuchukua muda mrefu kumsahau Mzee Gurumo, nakumbuka wakati anaumwa mara kwa mara nilikuwa namtembelea kumjulia hali na kutaniana naye sijui nitamtania nani tena, kwa kweli naumia..Mungu Amrehemu," alisema Julio.
Enzi za uhai wake Mzee Gurumo alikuwa mwanachama wa Simba na shabiki mkubwa wa Mabingwa watetezi wa England, Manchester United.
Chini ya uongozi wa akina Hassan Dalali, Mzee Gurumo aliwahi kuwapelekea wachezaji wa Simba wakiwa mazoezi matunda mbalimbali kutoka shambani mwake kwa nia ya kuboresha siha na afya zao kuonyesha unazi wake wa Simba.
Mzee Gurumo (74) alifariki Alasiri ya jana Muhimbili baada ya kuugua kwa muda mrefu maradhi ya Mapafu na ugonjwa wa Moyo na anatarajiwa kuzika leo kijijini kwao, Masaki wilaya ya Kisarawe, Pwani.

TFF yamlilia Josephat Magazi

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu (FRAT) Mkoa wa Singida, Josephat Magazi kilichotokea jana mkoani Kilimanjaro.
Magazi ambaye pia aliwahi kuwa mwamuzi na kamishna wa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) alikuwa amelazwa katika Hospitali ya KCMC. Mazishi yatafanyika kesho (Aprili 15 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwao Ushirombo mkoani Shinyanga.
Msiba huo ni mkubwa katika fani ya mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Magazi alishirikiana na TFF na wadau wengine wa mpira wa miguu katika masuala ya uamuzi na uongozi, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Magazi, FRAT na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida (SHIREFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
 
Bwana alitoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Amina