STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, July 21, 2013

Maskini! Papii Kocha alilia tena Rais Kikwete

MUIMBAJI Nyota wa zamani wa bendi ya FM Academia, Papii Kocha amemuandikia ombi jingine maalum Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kumuomba MSAMAHA wa kufutiwa adhabu yake ya kifungo cha maisha jela alichopewa yeye na wanafamilia yake kwa kesi ya kubaka.
Ujumbe huo unaelezwa ni wa mara nyingine tena kwa msanii huyo aliyepo gerezani na baba yake, japo hakujawa na hakika kama barua hizo zinamfikia Mheshimiwa na kuzisoma au la. Ebu isome mwenyewe barua hiyo ya 'Mwana Mfalme' Papii Kocha kwenda kwa Rais Jakaya Kikwete...inaumiza!
MF/NA: 836'04 Johnson Nguza
(Papii Kocha) Gereza Kuu Ukonga
S.L.P 9091
Dar es Salaam
Mh. Rais Jamuhuri ya Muungano Tanzania

YAH: MAOMBI YA KUPEWA MSAADA (MSAMAHA) WA KUFUTIWA ADHABU YA KIFUNGO NILIYOPEWA NA MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI KISUTU.

Husika na somo hilo hapo juu. Mimi ni mfungwa katika gereza kuu Ukonga. Kwa heshma na taadhima na kwa kutambua utu na huruma yako ya kiMUNGU ulionayo dhidi ya binadamu wenzako pamoja na mamlaka uliokabidhiwa na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Naanguka na kushika miguu yako mitukufu muheshimiwa rais....Nakuomba msaada (msamaha) kwako muheshimiwa rais, kwa njia hii ya maandishi kusudi niweze kuondolewa adhabu ya kifungo cha maisha gerezani, niliyohukumiwa na mahakama tajwa hapo juu. Mh.Rais mimi nimefungwa nikiwa bado kijana mwenye umri mdogo, na ukweli kutoka moyoni sikufanya kosa hilo.

Si mimi, baba yangu Nguza wala ndugu yangu yeyote aliyefanya kitendo kile. Lakini wenye mamlaka wakatuona tuna hatia na kuamua kuteketeza kizazi chetu gerezani.

Natamani kiama ifike ili mwenyezi Mungu aweke wazi ukweli wote uliojificha nyuma ya pazia. Mpaka sasa natambua wazi hatima pamoja na dhamana ya maisha yangu ipo katika mikono yako mitukufu Mh. Rais Naomba huruma yako muheshimiwa Rais maana mimi ni mtoto wako ninaehitaji huruma yako wewe mzazi. Lakini pia sisi ni binadamu wenye nafsi na miili kama wengine. Waliotumia mamlaka yao kutuweka gerezani nao ni binadamu pia, wenye miili na nafsi.

Ipo siku nafsi zetu zitapaswa kutoa hesabu ya tuliyoyafanya hapa duniani. wakati huo miili yetu tunayoitumia kunyanyasa wanyonge itakuwa imeoza mavumbini.

Natumaini kauli yako ya mwisho ndio itakayoleta pumzi ya uhai nafsini mwangu. Nakutakia kazi njema, afya njema na maisha marefu. Mungu akubariki. Wako mtiifu

Mfungwa NO:836'04 JOHNSON NGUZA (PAPII KOCHA)
 
Udaku Specially

Kumbe Msajili wa Vyama alibariki CHADEMA kuunda 'jeshi'?!


  Nakala za majibu ya Ofisi ya Tendwa kwa CHADEMA zilipelekwa kwa
  • Waziri wa Mambo ya Ndani wakati huo, Omar Mapuri,
  • Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, aliyekuwa anashughulikia Habari na Siasa, Muhammed    Seif Khatib;
  • Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu;
  • Inspekta Jenerali wa Polisi na
  • Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai

LICHA ya kuwapo kwa shutuma mbalimbali zinazopinga mpango wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuanzisha kikundi cha, kujihami cha Red Brigade kitakachotoa ulinzi kwa viongozi wao, imebainika kuwa msajili wa vyama vya siasa nchini, John Tendwa alitoa baraka za kuanzishwa kwake.

Tanzania Daima imeona nakala ya barua ya mwaka 2005 kutoka katika ofisi ya Tendwa, ikionyesha kubariki jambo hilo ambalo katika siku za hivi karibuni limezua gumzo kubwa na kusababisha Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, kuhojiwa na polisi kuhusiana na kauli zake.

Uchunguzi wa kina uliofanywa na Tanzania Daima umebaini kuwa Desemba 30, 2004 ofisi ya msajili wa vyama siasa ilimwandikia Katibu Mkuu wa CHADEMA barua yenye kumbukumbu Na. RPP/CHADEMA/72/29 ikitaka ufafanuzi baada ya kusikia kupitia vyombo vya habari kuwa chama hicho kinataka kuanzisha kikundi cha kujihami (Red Brigade). “Kulingana na Ibara ya 9 (2) (c) ya Sheria Na. 5 ya Vyama vya Siasa 1992, ibara ya 147 na 148 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria ya Jeshi la Polisi, kuanzishwa kwa kikundi hicho ni kinyume cha sheria hizo,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.

Barua hiyo ambayo Tanzania Daima inayo iliyosainiwa na Hilda Lugembe kwa niaba ya msajili wa vyama vya siasa, inaeleza kuwa kuvunjwa kwa sheria hizo kutasababisha CHADEMA kufutwa. CHADEMA baada ya kupata barua hiyo, Januari 6 mwaka 2005 iliijibu kuwa kikundi kinachozungumziwa ni walinzi wa ndani ya chama, vijana wa kike na wa kiume, wanachama wa CHADEMA, watu wasio na silaha, chini ya usimamizi wa kurugenzi ya ulinzi na usalama ya chama hicho. “Kikundi kinachokusudiwa kuundwa ni kutokana na Katiba ya CHADEMA ambayo inaruhusu uundwaji wa Kurugenzi ya Ulinzi na Usalama chini ya Katiba ya CHADEMA, kifungu cha 7.6.4 (h),” inaeleza barua ya CHADEMA yenye kumbukumbu Na. C/HQ/ADM/64 iliyosainiwa na Suzan Kiwanga kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CHADEMA. Chama hicho kiliilaumu serikali kwa vitisho ilivyotoa vya kutaka kukifuta endapo kingeendelea na kusudio la kuanzisha kikundi hicho.

Barua ya ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa nchini ya kuithinisha uanzishwaji

Hata hivyo, baada ya ufafanuzi huo, Januari 11 mwaka 2005, ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, ilipopata majibu hayo ya CHADEMA, ilieleza kuwa kwa madhumuni yaliyoelezwa na chama hicho inakubaliana na malengo ya kuanzisha kikundi cha ulinzi kwa ajili ya usalama wa ndani ya chama. “Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, kwa madhumuni mliyoyatoa kwenye barua yenu C/HQ/ADM/62 inakubaliana na maelezo yenu ya kuanzishwa kwa kikundi cha ulinzi kwa ajili ya usalama wa ndani ya chama ingawa Katiba ya CHADEMA haijatoa ufafanuzi huo, vinginevyo tunawatakia kila la heri kwenye matayarisho ya uundwaji wa kikundi hicho,” ilisema barua ya msajili wa vyama vya siasa nchini.

Barua hiyo yenye kumbukumbu Na. RPP/CHADEMA/72/32 iliyosainiwa na Hilda Lugembe kwa niaba ya msajili wa vyama vya siasa nchini, pia iliwatakia kila la heri CHADEMA kwenye matayarisho ya uundwaji wa kikundi hicho.

Nakala za majibu ya Ofisi ya Tendwa kwa CHADEMA zilipelekwa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani wakati huo, Omar Mapuri, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, aliyekuwa anashughulikia Habari na Siasa, Muhammed Seif Khatib; Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu; Inspekta Jenerali wa Polisi na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai

TANZANIA DAIMA

Golden Bush Veterani waikwanyua Faru Dume x3

Golden Bush Veterani a.k.a 'Wazee wa Dozi' katika moja ya mechi zao
WAKALI wa soka la maveterani jijini Dar es Salaam, Golden Bush Veterani jana asubuhi wameikwanyua bila huruma, Faru Dume ya Manzese kwa kuicharaza mabao 3-1 katika pambano la kirafiki lililochezwa kwenye uwanja wa Kinesi, Ubungo jijini Dar es Salaam.
Golden Bush ilipata ushindi wake huo mnono kupitia mabao ya Waziri Mahadhi 'Mandieta', Kudra Omar na Ally Chuo yaliyotosha kuizima Faru katika pambano hilo.
Uongozi wa Golden Bush ulisema umeridhishwa na kiwango cha timu yake na kwa sasa wanaendelea kujipanga kwa ajili ya mechi nyingine za kirafiki ili kugawa 'dozi' kwa wapinzani wao watakaoshuka mbele yao.

Mr Bomba kuagwa kesho kuzikwa kwao Mpwapwa

REV. John Makanyagana
Msanii John Makanyaga (Mchungaji) 'Mr Bomba' enzi za uhai wake


http://www.bongocinema.com/images/products/dangerous_deal.jpg
Moja ya kazi za mwisho mwisho za marehemu Mr Bomba

MWILI wa msanii nyota wa zamani wa Kaole Sanaa, John Makanyanga maarufu kama Mr Bomba unatarajiwa kuagwa kesho jijini Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa Mpwapwani, Dodoma kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika siku ya Jumanne.
Kwa mujibu wa mmoja wa wasanii wenzake ambaye hivi karibuni walitoka na filamu mpya iitwayo 'Dangerous Deal', Adam Malele 'Swebe Santana' ni kwamba mwili wa msanii huyo aliyerafiki jana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili utaagwa kesho Jumatatu kabla ya kusafirishwa jioni kuepekwa Mpwapwa.
Swebe, ambaye anayemlilia Mr Bomba na kudai ni mtu aliyekuwa naye karibu tangu wakiwa wote Kaole, alisema mwili huo utaagwa nyumbani kwa marehemu Buguruni Malapa karibu na Kanisa la Anglikana, jijini Dar.
"Kwa taarifa ambazo mpaka muda huu nilizonazo ni kwamba marehemu ataagwa kesho kabla ya kusafirishwa kwao Mpwapwa Dodoma kwa ajili ya mazishi ambayo yatafanyika siku ijayofuata," alisema.
Mr Bomba, ambaye kitaaluma alikuwa ni mwalimu aliyewahi kufundisha Shule ya Sekondari Makongo na nyingine binafsi eneo la Mbezi, alifariki jana baada ya kusumbuliwa kwa muda mrefu na kansa ya uvimbe wa kwenye ini mbali na sanaa na ualimu pia alikuwa Mtumishi wa Mungu akiwa kama Mchungaji wa Kanisa la Anglikana.
Enzi za uhai wake msanii huyo aliyejaliwa mwili mkubwa alitamba na tamthilia mbalimbali akiwa na kundi la Kaole Sanaa iliyokuwa ikirushwa na kituo cha ITV, akimudu zaidi nafasi ya 'kibosile' na wakati mwingine kama 'mafia' anayehusika na biashara ya dawa za kulevya na alicheza filamu kadhaa ikiwamo 'Kidole Tumbo', iliyozuiwa kuingizwa sokoni.
Mbali na uigizaji, pia marewhemu alikuwa mtunzi, mwandishi wa miswada ya filamu na kazi ya karibu kuiandaa ni Dangerous Deal ambayo aliitunga na kuiandikia mswada mwenyewe na kuongoza na Swebe ambapo mbali na kuichezea yeye mwenyewe, pia aliigiza na Swebe, Chuchu Hans, Hashim Kambi, Sebastian Mwanangulo, Mama Sonia na wengine.

Mungu aiweke mahali pema roho ya marehemu Mr Bomba.

Waamuzi wa Madagascar kuzihukumu Stars, The Cranes

Stars na Uganda the Cranes walipoumana wiki iliyopita katika pambano lao la kwanza la CHAN na Stars kulala kwa bao 1-0
Na Boniface Wambura
SHIRKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Madagascar kuchezesha mechi kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Uganda (The Cranes) itakayochezwa Jumamosi (Julai 27 mwaka huu) Uwanja wa Mandela ulioko Namboole nje kidogo ya Jiji la Kampala.

Waamuzi wataongozwa na Kanoso Abdoul Ohabee wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Andirvoavonjy Pierre Jean Eric. Mwamuzi msaidizi namba mbili ni Jinoro Velomanana Ferdinand huku Andriamiharisoa Hubert Marie Bruno akiwa mwamuzi wa mezani (fourth official).

Kamishna wa mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya mwisho kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) ni Ismail Kamal kutoka Ethiopia.

Mechi hiyo namba 38 itachezwa kuanzia saa 10 kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki. Taifa Stars ilipoteza mechi ya kwanza iliyochezwa Julai 13 mwaka huu jijini Dar es Salaam kwa bao 1-0.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iko kambini jijini Mwanza ikijiandaa kwa mechi hiyo itakayoamua ni timu ipi kati ya hizo mbili itacheza Fainali za CHAN mwakani nchini Afrika Kusini.

Mmiliki wa Home Shopping Centre amwagiwa tindikali


Duka moja wapo la Home Shopping Centre lililopo jijini Dar es Salaam 

MTU asiyejulikana juzi usiku alimvamia mmiliki wa maduka ya Home Shopping Centre, Said Mohammed Saad  na kumwagia maji usoni yanayodhaniwa kuwa ni tindikali.
Tukio hilo lililotokea juzi saa 1 usiku karibu na kituo cha Polisi cha Oysterbay, lilithibitishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Ally Mlege kwa kusema kuwa bado polisi wanaendelea na uchunguzi wao ili kuwabaini waliohusika.
“Ni kweli tukio hili limetokea ila polisi wanaendelea na uchunguzi. Tukikamilisha uchunguzi tunatarajia kutoa taarifa kamili za tukio zima,” alisema na kuongeza;
“Hatuna haja ya kuficha ukweli wa tukio hili, uchunguzi wetu ukikamilika na watuhumiwa wakikamatwa kila mtu atajua.”
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zilizolifikia gazeti hili zilieleza kuwa mtu huyo, alimkuta Saad akiwa anazungumza na mmoja wa wafanyakazi wake katika duka lake jipya lililopo karibu na Kituo cha Polisi cha Oysterbay.
“Wakati akizungumza na mfanyakazi wake, huyo mtu alikuwa kama anapita na alichomoa kitu fulani na kummwagia Saad usoni na kisha kukimbia,” zilieleza taarifa hizo na kuongeza;
“Baada ya tukio hilo alipelekwa katika Hospitali ya AMI, sasa hatujui kama bado yupo hapo au ameondoka, ila sisi tulizungumza naye na alitueleza mwonekano wa mtu aliyemwagia tindikali.”
Taarifa hizo zilifafanua kwamba polisi wanazitumia taarifa hizo walizopewa na Saad, ili kuweza kumkamata mhusika.
Taarifa hizo zilifafanua kuwa polisi wanapanga tena siku ya kumhoji kwa mara ya pili Saad, kwamba watataka kufahamu kama mfanyabiashara huyo alikuwa akipewa vitisho au ujumbe wowote, kabla ya kukutwa na tukio hilo.
Hata hivyo, habari nyingine zilizolifikia Mwananchi Jumapili zilieleza kuwa mtu huyo baada ya kummwagia Saad tindikali, alipanda pikipiki na kutokomea eneo hilo.
“Walikuwa wawili, mmoja alikwenda kufanya unyama na mwingine alibakia katika pikipiki, baada tu ya kumwagia tindikali mtu yule alikimbia mpaka pale alipokuwa imesimama pikipiki, alipanda na kuondoka kwa kasi,” zilieleza habari hizo.
Taarifa zilizopatikana jana asubuhi zilieleza kuwa ndugu na marafiki wa mfanyabiashara huyo, walikuwa katika mipango ya kumpeleka nje ya nchi kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.

MWANANCHI

Picha za matukio ya miili ya wanajeshi waliouwawa Darfur


MKUU WA MAJESHI GENERALI DAVIS MWAMUNYANGE AKISUBIRI KUPOKEA MIILI YA VIJANA WAKE WALIOUAWA SUDAN
BAADHI YA VIONGOZI WA SERIKALI WAKIONGOZWA NA MAKAMU WA RAIS DR MOHAMMED GHARIB BILAL

MAMA SALMA KIKWETE NA MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM NAO WALIKUWEPO


NDEGE ILIYOBEBA MIILI YA WANAJESHI MARA BAADA YA KUWASILI KUTOKA SUDAN


MIILI YA WANAJESHI 7 WALIOUAWA SUDAN IKIONEKANA KWENYE NDEGE MARA BAADA YA KUWASILI
WANAJESHI WA JWTZ WAKIBEBA MIILI YA WENZAO WALIOUAWA HUKO SUDAN
NDUGU JAMAA NA MARAFIKI WAKISUBIRI KUWASILI KWA MIILI YA WANAJESHI WALIOUAWA SUDAN
ILIKUWA NI VIGUMU KUVUMILIA HALI HII BAADA YA KUONA MIILI YA WAPENDWA WAO
HALI ILIKUWA YA MACHUNGU KWA NDUGU WA KARIBU
WANAJESHI WA JWTZ WAKIPOKEA MIILI YA WENZAO
MIILI IKITOLEWA KWENYE NDEGE
MMOJA KATI YA MIILI YA MAREHEMU UKIINGIZWA KWENYE GARI
MOJA KATI YA FAMILIA ZA MAREHEM WALIOUAWA SUDAN
FAMILIA ZA MAREHEM WAKISUBIRI KUWAPOKEA WAPENDWA WAO
Miili ya wanajeshi saba mashujaa wa Tanzania waliofariki wakiwa kazini wakitekeleza ulinzi wa amani wa kimataifa katika mkoa wa Darfur nchini Sudan, iliwasilia jana ndege maalumu ya Umoja wa Mataifa.

Kaimu Mkurugenzi wa habari wa JWTZ, Meja Joseph Masanja amesema miili hiyo iliwasili Jumamosi majira ya saa 9.45 alasiri katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa JNIA na imehifadhiwa katika hospitali ya jeshi ya Lugalo hadi Julai 22 ambapo itaagwa rasmi.

Miili iliyowasili ni ya Sajenti Shaibu Othuman, Koplo Oswald Chaula, Koplo Mohamed Juma, Koplo Mohamed Chikilizo, Pte. Rodney Ndunguru, Pte. Peter Werema na Pte. Fortunatus Msofe.

Shughuli za kuagwa miili ya wanajeshi hao zitafanyika katika viwanja vya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga taifa vilivyoko Upanga jijini Dar es salaam.

Kuwapoteza wanajeshi hawa ni la kwanza na kubwa kwa nchi ya Tanzania tangu Tanzania ilipoanza kuchangia walinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa mwaka 2007. Wanajeshi wengine watatu wa Tanzania walifariki dunia mwezi uliopita baada ya chombo chao cha kusafiria kusombwa na maji ya mto uliokuwa umefurika huko nchini Sudan. 

 
BONGOCLAN

TFF YAMLILIA KOCHA WA ZAMANI WA TAIFA STARS

Bert Trautmann
Na Boniface Wambura
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha kocha wa zamani wa Taifa Stars, Bert Trautmann (89) kilichotokea jana (Julai 19 mwaka huu) nchini Hispania.

Kabla ya kuwa kocha, Trautmann aliyezaliwa 1923 mjini Bremen, Ujerumani alikuwa kipa wa timu ya Manchester City ya Uingereza ambapo anakumbukwa kwa kucheza mechi ya fainali ya Kombe la FA dhidi ya Birmingham City akiwa amevunjika shingo.

Manchester City ilishinda fainali hiyo iliyochezwa mwaka 1956 mabao 3-1. Trautmann ambaye aligongana na mshambuliaji wa Birmingham, Peter Murphy zikiwa zimesalia dakika 17 mechi hiyo kumalizika aligundua kuwa amevunjika shingo siku tatu baadaye.

Mbali ya kuwa kocha wa Taifa Stars mwanzoni mwa miaka ya 60, Trautmann pia alikuwa mkufunzi wa makocha ambapo hapa nchini aliendesha kozi mbalimbali zilizotoa makocha waliokuja kutamba baadaye.

TFF itamkumbuka Trautmann kwa mchango wake aliotoa katika maendeleo ya mpira wa miguu nchini ikiwemo wazo lake la kuanzishwa kwa Ligi Kuu (Daraja la Kwanza) ambalo alilitekeleza katikati ya miaka ya 60.

Msiba huo ni pigo kwa familia ya Trautmann, TFF na familia ya mpira wa miguu kwa ujumla nchini kutokana na mchango alioutoa kwa Tanzania hasa wakati akiwa kocha na mkufunzi wa makocha.

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Trautmann, Chama cha Mpira wa Miguu cha Ujerumani (DFB), Chama cha Mpira wa Miguu cha Uingereza (FA) na kuwataka kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki cha msiba huo mzito.

Mungu aiweke roho ya marehemu Bert Trautmann mahali pema peponi. Amina

Friday, July 19, 2013

Mpigania haki za Mashoga auwawa kikatili


MPIGANIA  Haki za mashoga nchini Cameroon amekutwa amekufa nyumbani kwake Yaounde baada ya kuteswa, Wapigania Haki za Binadamu wamesema.
Mwili wa Eric Lembembe ulikutwa kwenye jiji hilo mnamo siku ya Jumatatu huku ukionekana alikuwa ameteswa vibaya sana, kundi hilo lilisema kwenye maelezo yao siku ya Jumanne.
 
Marafiki wa Lembembe waliukuta mwili wake mnamo siku ya Jumatatu jioni. Kwa mujibu wa rafiki zake shingo yake ilivunjwa na uso wake, mikono na miguu viliunguzwa moto kwa kutumia pasi, taarifa ilisema.
 
Shirika hilo limeelezea kitendo hicho kama ni cha “mauaji”na kuzitaka mamlaka husika kuendelea kufanya uchunguzi wa kina.

Denti wa Tegeta Sec ajinyonga hadi kufa kisa...!


Mwanafunzi  wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Tegeta jijini Dar es Salaam, Bertha Amir (14), pichani, amejinyonga hadi kufa akipinga kulazimishwa na mama yake mzazi kusoma.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alisema mwanafunzi huyo alijinyonga juzi  saa 11:00 jioni, maeneo ya Tegeta Namanga, jijini Dar es Salaam.
Alisema marehemu alikutwa amejinyonga chumbani kwa kutumia mtandio ulioning’inizwa juu ya dari.
Kamanda Wambura alisema sababu za mwanafunzi huyo kujinyonga bado hazijafahamika, lakini akasema inasadikika kuwa wakati wa enzi za uhai wake, siku moja kabla ya kifo chake, alikuwa ameongea na mama yake, Angelina Maiko Mshami (30), ambaye alimtaka achukue fedha kwa ajili ya kujiandaa kwenda shule.
Alisema mtoto huyo alimjibu mama yake kuwa hahitaji kusoma, bali anataka kufanya kazi.

Kamanda alisema kuwa mwili wa mwanafunzi huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala kwa uchunguzi na kwamba, polisi wanaendelea na upelelezi kuhusiana na kifo chake.
 Mama wa mtoto huyo, Angelina Mshami, alisema alishangazwa na kitendo cha mtoto wake kuamua kukataa shule ghafla wakati alikuwa ana uwezo mzuri darasani.

Alisema kuwa mtoto wake alikuwa na akili darasani akishika nafasi ya kwanza ama ya pili wakati akisoma shule ya msingi na hivyo kumfanya afaulu kujiunga  kidato cha kwanza.

Hata hivyo, alisema kabla ya kifo chake, binti yake alimweleza kuwa hataki shule bali anataka kufanya kazi.

Alisema alipomuuliza kazi gani anataka kuifanya, hakuitaja bali alisisitiza kuwa anaifahamu mwenyewe.

Betha ambaye ni mtoto wa kwanza kati ya watoto wawili katika familia yao, alizaliwa mwaka 1999, Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga.

Alianza  darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Malindi mkoani Tanga na kufanikiwa kujiunga na Shule ya Sekondari Mtumbi na baadaye kuhamishiwa katika Shule ya Sekondari Tegeta.

Aidha, baadhi ya majirani waliokuwapo msibani hapo, walielezea masikitiko yao na huzuni kuhusiana na kifo cha msichana huyo.

Marehemu anatarajiwa kusafirishwa leo kuelekea mkoani Tanga kwa mazishi yatakayofanyika kesho kijijini Malindi

CREDIT:swahili tz.

Deo Lyatto atoa Shukrani kwa wadau wa soka nchini

Deo Lyatto, alipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF
HAPO chini ni Maelezo ya Shurani ya Mwenyekiti Aliyemaliza muda wake wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Deo Lyatto kwa wadau wa soka nchini.

1. Kama wote tunavyofahamu jana uongozi wangu wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ulifikia tamati kama mlivyotangaziwa na Rais wa TFF. Kwa heshima kubwa naomba kutumia fursa hii kuwashukuru viongozi na wadau wa soka kwa ushirikiano mkubwa nilioupata kutoka kwao wakati nikitekeleza majukumu mbalimbali ya TFF.

2.  Kwa kushirikiana na viongozi wa mpira wa miguu katika TFF na mikoa yote Tanzania Bara, pamoja na wadau wa soka, nimepata fursa kulitumikia soka la nchi yetu kwa nafasi mbalimbali. Kwa pamoja tumetekeleza majukumu ya ujenzi wa misingi ya uongozi bora katika TFF na wanachama wake.

3.  Naishukuru Kamati ya Utendaji ya TFF:

(i)kwa kuniteua kuwa mjumbe wa Kamati ya Nidhamu ya TFF, (Jan 2005 - Jan 2007). Nawashukuru pia wajumbe wa Kamati hiyo chini ya Mhe. Said El-Maamry kwa kunichagua kuwa Katibu wa Kamati hiyo. Ushirikiano mlionipatia ulioniwezesha kulitumikia taifa katika soka na kwa pamoja kurejesha nidhamu kwa kiwango kikubwa.

(ii)kwa kuniteua kuwa mjumbe wa Kamati Maalumu, iliyochunguza mkasa wa timu yetu ya Taifa ya wachezaji wa umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) mwezi Juni 2005. Nawashukuru wajumbe wa kamati  hiyo chini ya Dr. Hamad Ndee Mkuu wa Idara ya Michezo ya Chuo kikuu cha Dar es salaam, kwa kunichagua kuwa Katibu wa kamati hiyo iliyoandaa taratibu za mashindano ya vijana  ambazo ni msingi  wa mashindano ya vijana wa umri chini ya miaka 17  hapa nchini.

(iii)kwa kuniteua kuwa Mjumbe wa Kamati Maalumu iliyotayarisha Programu ya kuendeleza Timu ya Taifa kwa kipindi cha miezi 15 (April 2006 hadi Juni 2007). Progamu iliyochangia Tanzania kiinua kiwango cha ubora wa soka kutoka nafasi ya 165 duniani mwezi Februari 2006 hadi nafasi ya 89 mwezi Desemba 2007.

(iv)kwa kunipa fursa ya kuwa mjumbe wa Kamati Maalumu ya kuboresha mapato ya TFF mwaka 2009. Nikiwa mjumbe na Katibu wa Kamati hiyo nilipata ushurikiano mkubwa kutoka kwa wadau wa soka nchini  na nje ya nchi.  Nina imani kuwa TFF itakamilisha utekelezaji wa mapendekezo ya Kamati na ya wadau wa soka ikiwa ni pamoja na kuanza kutumia tiketi za elektroniki.

(v)kwa kuniteua kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF  kwa  vipindi viwili; Februari 2009 - Machi 2011 na kuniteua tena kuiongoza Kamati hiyo kwa kipindi cha pili Machi 2011 hadi jana tarehe 18 Julai 2013. Naishukuru Kamati ya Utendaji ya TFF kwa imani kubwa iliyoonyesha kwangu na wanakamati wenzangu.
4.  Nawashukuru wajumbe wote wa wa Mkutano Mkuu wa TFF, kwa ushirikiano mkubwa mliotoa kwangu na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kushiriki kwa amani na utulivu na kuzingatia Katiba za vyama vyenu, Katiba ya TFF na Kanuni za Uchaguzi na hivyo kufanikisha zoezi la chaguzi za viongozi katika wilaya zote na Mikoa yote ya Tanzania Bara na hivyo kuwezesha kuwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu, ambao  katika kikao chake cha kwanza baada ya chaguzi hizo kimefanya jambo la kihistoria kuweka nguzo za  Mwenendo, Maadili  na Miiko ya uongozi wa soka la nchi yetu. Nilifarijika kuwa sehemu ya Mkutano Mkuu huo nikiwa mwalikwa.

5. Nawashukuru viongozi na wafanyakazi wote wa Sekretarieti ya TFF, wajumbe wa Kamati zote za TFF, Wajumbe wa Kamati zote za Uchaguzi za wanachama wa TFF na wanachama wao, kwa ushirikiano mkubwa na wa dhati uliowezesha kuwatumikia wadau wa soka kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.

6. Nawashukuru sana wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa ushirikiano niliopata kutoka kwao kwa muda tuliofanya kazi pamoja. Si jambo rahisi kusimamia chaguzi za mikoa yote na klabu zenye wanachama za Ligi Kuu, hata hivyo kwa kushirikiana na wadau mbalimali wa soka ambao nachukua fursa hii kuwashukuru, kwa pamoja tumeweza kutimiza jukumu hilo kikamilifu.  

7. Nawashukuru sana Waandishi na Wahariri wa habari za michezo na pia Wahariri Watendaji wa vyombo vya habari, kwa ushirikiano mzuri nanyi, ushirikiano na uhusiano wa uwazi ambao haukuwa na mikwaruzo ya aina yoyote kwa kipindi chote (Jan 2005-Jul 2013) tulichoshirikiana kwa pamoja kulitumikia soka la nchi yetu.

8. Namshukuru sana Rais wa TFF Ndg. Leodegar Tenga kwa imani kubwa aliyonayo kwangu na kwa wanakamati niliokuwa nao katika kutekeleza majukumu ya umma. Miaka ishirini na tisa (29) iliyopita nilipata fursa ya kufanya kazi ya mpira miguu kwa mara ya kwanza na Ndg. Tenga, nikiwa nahodha wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Chuo kikuu cha Dar es salaam, Desemba 1984, wakati Ndg. Tenga alipojitolea kuifundisha timu ya Chuo Kikuu cha DSM. Tangu wakati huo hadi sasa imani  na  ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya umma niliopata kutoka kwa Ndg. Tenga haujawai kutetereka hata kwa siku moja. Ni faraja kubwa kwangu kufanya kazi hizi za umma chini ya kiongozi anayeheshimika na kuaminika na wadau wa soka hapa nchini, Afrika Mashariki na Kati, Afrika na familia ya soka Duniani kwa ujumla.

9. Mwisho, kwa viongozi na wadau wote wa mpira wa miguu, nawashukuru na nawatakia kheri, baraka  na mafanikio katika Uchaguzi Mkuu wa TFF na  ujenzi wa  soka la nchi yetu..

Asanteni.
 
Deogratias J. Lyatto
19 Julai 2013, Dar es salaam, Tanzania.

Yanga wamegeuzia kibao Kiiza, kisa...!

Na Dina Ismail
BAADA ya kuipiga danadana kwa muda mrefu, hatimaye klabu ya soka ya Yanga imemgeuzia kibao aliyekuwa kiungo mshambuliaji wake wa kimataifa,Hamis Kiiza. 
Hivi karibuni nyota huyo kutoka nchini Uganda, amekuwa katika mvutano na uongozi wa klabu hiyo juu ya kusaini mkataba mpya wa kuendelea kutumikia klabu hiyo. 
Kwamba, Kiiza alitaka kuongezwa ofa ya aliyopewa na uongozi kutoka dola 35,000 hadi dola 50, 000 ambazo amesisitiza kupewa na baadaye kumuongeza hadi dola 40,000. 
Hata hivyo, habari kutoka ndani ya uongozi wa Yanga zinaeleza kwamba wameamua kuachana kwanza na suala la Kiiza kutokana na nafasi yake kutokuwa na umuhimu katika kikosi hicho. 
Kiongozi mmoja aliliambia gazeti hili kwamba kwa sasa Yanga inahitaji mshambuliaji halisi mmoja ambaye atashirikiana na mshambuliaji aliyepo sasa, Didier Kavumbagu. 
“Kwa sasa suala la Kiiza tumeliweka kando kwani nafasi yake haina umuhimu katika kikosi chetu, tunatafuta mshambuliaji halisi, ila tukikosa ndo tutarudi kwake,”alisema 
Akienda mbali zaidi, kiongozi huyo alisema kwamba mshambuliaji huyo anafahamu kila kitu juu ya mustakabali wake ndani ya klabu hiyo na hata hilo suala la kumpa fedha anayoitaka yeye halipo. 
Aliongeza kuwa baada ya kumleta mshambuliaji kutoka Nigeria Ogbu Brendan  kwa ajili ya majaribio, hivi karibuni tena wanataleta washambuliaji wengine kuja kujaribiwa. 
Katika hatua nyingine, kikosi cha Yanga kimeendelea na mazoezi yake ya kujiandaa na ligi kuu soka Tanzania Bara ambapo keshokutwa itacheza mechi ya kirafiki na URA ya Uganda. 

Mchezo huo utakaopigwa kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya kukipima kikosi hicho.

Mtwara kumekucha! Lori lenye shehena ya mabomba lashambuliwa mawe dereva hoi


Habari zilizotufikia kutoka mjini Mtwara zinasema kuwa Gari lililokuwa limebeba Shehena ya Mabomba ya Kusafirishia gesi kutoka Mjini Mtwara kuelekea Dar limeshambuliwa na mawe na kupelekea dereva wa lori hilo Kujeruhiwa Vibaya. 
Lori hilo lilianza kushambuliwa mara baada ya kuingia katika eneo la Mikindani Manispaa ya Mtwara Mjini na sababu ya kushambulia gari hilo ni katika kile kinachodhihirisha kuwa wana Mtwara bado hawajakubaliana na hoja ya Serikali ya kutaka Kusafirisha Gesi hiyo kwa ajili ya Manufaa ya Nchi. Lori hilo kwa sasa lipo kituo kikubwa cha polisi  Mtwara.
Tukio hilo linatokea ikiwa ni wiki moja tu imepita tokea watu kadhaa kukamatwa na jeshi la polisi mkoani Mtwara kwa kile kinachodaiwa kusambaza waraka wa kuhujumu miundombinu yote ya gesi mara tu serikali itakapoanza utekelezaji wake wa ujenzi wa bomba hilo kupeleka Dar.

Source: Jamii Forum

Miili ya wanajeshi waliouwawa Darfur kurejeshwa nchini kesho

http://www.raiamwema.co.tz/sites/default/files/styles/slideshow/public/field/image/307_jwtz.jpg?itok=8L3GOhTM
Miili ya wanajeshi hao ilipokuwa ikiagwa na askari wenzao nchini Sudan

MIILI ya wanajeshi waliouwawa katika mji wa Darfur, nchini Sudan inatarajiwa kuwasili nchini kesho kuanzia majira ya saa 4 asubuhi kwa ajili ya mazishi yake.
Wanajeshi hao waliokuwa kwenye jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa, walishambuliwa asubuhi ya Jumamosi iliyopita na waasi wanaopigana na serikali ya Sudan katika jimbo hilo la Darfur wakati wakisindikiza msafara ambaopo askari wengine akiwemo Polisi wa Tanzania walijeruhiwa.
Taarifa zinasema miili hiyo itapokelewa kesho kwa heshima zote kabla ya kufanyiwa taratibu za kuagwa kitaifa kisha kuzikwa kwa kushirikiana na familia zao.

Wenger amkatia tamaa Fabregas

http://gossip.ladyarse.com/wp-content/uploads/2012/07/wenger-arsene.jpg
Kocha Arsene Wenger

KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema kwamba kuwa hatarajii kumsajili Cesc Fabregas katika kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi kwani kiungo huyo wa timu ya taifa ya Hispania ameamua kubaki kwa "mwaka mmoja zaidi " kwenye klabu yake ya Barcelona.
Arsenal wamesisitiza kuwapo kwa kipengele kinachowaruhusu kumnunua tena Fabregas kwa paundi za England milioni 25 ambacho kiliwekwa wakati wa mkataba wao wa kumuuza Mhispania huyo kwa Barca miaka miwili iliyopita.
Hata hivyo, licha ya Manchester United kujaribu kumtwaa kwa kuwasilisha ofa ya euro milioni 30 Jumatatu iliyopita, Mfaransa Wenger anaamini kwamba wao hawahitaji kutuma ofa yoyote kwa nia ya kumzuia nahodha wao huyo wa zamani kwenda Man U.
Iliripotiwa mwishoni mwa mwezi uliopita kuwa Wenger amekuwa akiwasiliana kila mara na nahodha wake huyo wa zamani, na sasa amedai kuwa anafahamu msimamo wa Mhispania huyo kuhusiana na hatma yake msimu ujao.
"Hivi sasa, Fabregas ameamua kubaki Barcelona kwa mwaka mmoja zaidi," Wenger aliwaambia waandishi wa habari.
Nahodha huyo wa zamani wa Arsenal amekuwa akihaha kupata nafasi ya uhakika katika kikosi cha kwanza tangu arejee katika timu yake ya utotoni lakini kuondoka kwa Thiago Alcantara kwenda Bayern Munich kunamaanisha kuwa sasa ana nafasi kubwa ya kucheza katika kiungo cha kocha Tito Vilanova.
Vilanova alisisitiza mwanzoni mwa wiki hii kwamba kiungo huyo mwenye miaka 26 anataka kubaki Barca na kuigania namba.
Alisema: "Natambua kwamba tumepokea ofa kadhaa kutoka klabu nyingine. Nilizungumza naye na ameniambia anataka kubaki.
"Cesc hafikirii kuhamia katika klabu nyingine. Anajua kwamba ushindani hapa ni mkubwa. Ndoto zake ni kuona anafanikiwa akiwa hapa."
Katika hatua nyingine kocha huyo amesema klabu yake inamudu mshahara wa kumlipa mshambuliaji wa Manchester United, Wayne Rooney anayetajwa kutaka kuhama Old Trafford licha ya klabu kudai HAUZWI.
Wenger alisema kama mchezaji huyo ataamua kukubali kutua kwao hawatakuwa na tabu ya kumlipa mshahara ambao kwa wiki hulipwa pauni 250,000.
"Rooney ana mkataba na amebakisha miaka miwili uishe, hivyo ni Man U wenye maamuzi. Lakini hatutakuwa na shida kulipa mshahara wa Rooney." alinukuliwa kocha huyo kutoka Ufaransa.

Mama atelekeza kichanga kisa wivu wa mapenzi

http://www.varbak.com/images/photos-of-black-babies-nb17527.jpg
Picha hii haihusiani na tukio hilo la kutelekezwa mtoto mjini Tanga
MWANAMKE mmoja mkazi wa eneo la Mtakuja jijini Tanga, aliyetajwa kwa jina la Asha Muhidini, amedaiwa kumtekeleza mtoto wake mchanga wa miezi miwili na kutokomea kusikojulikana kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni wivu wa mapenzi dhidi ya mumewe.
Mtonyaji wa habari hizi, Mariam Victor aliyejitambulisha kama mpwa wa mume wa mwanamke huyo, aliiambia MICHARAZO kuwa, mama huyo amekuwa na mzozo kwa muda mrefu na mumewe aliyetajwa kwa jina la Muhidini Mohammed baada ya mwanaume kuzaa nje ya ndoa mtoto mwenye miaka mitano.
Mariam alisema mwanamke huyo alimtelekeza kichanga hicho kwa kumfungia ndani ya chumba wanachoishi na mumewe tangu saa 1 usiku na walikuja kushtuka saa 5 usiku mtoto akilia na mjomba aliporejea kazini.

Aliongeza kuwa Asha amekuwa akipinga mtoto huyo aliyezaliwa kuja kuishi katia familia yao, lakini mumewe alikuwa akipinga akidai hawezi kuiacha damu yake kwa msimamo wa mkewe huyo.
"Mzozo uliosababisha hili jambo ni mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa na Mjomba ambapo kwa muda mrefu amekuwa akipinga na mkazamjomba (Asha) na jana alikuja kumtembelea baba yake na mke akapinga lakini mjomba alishikilia msimamo wake," alidokeza Mariam.
Alisema hawakujua kinachoendelea mpaka walipobaini kuwa mtoto kaachwa pekee yake na mama wa mtoto katoweka na kuanza kumsaka asubuhi hii bila ya mafanikio na kukimbilia ofisi ya serikali ya mtaa wao kuripoti ambapo wameombwa kuwa na subira kuona kama mwanamke huyo atarudi au la.
"Mwenyekiti katuambia tuvute subira na tumlishe mtoto maziwa na ng'ombe wakati tunasubiri mama yake arejee na kama vipi tuangalie ustaarabu mwingine ikiwemo kuripoti Polisi au kuendelea kumtunza mtoto kwa sababu pia hasumbui zaidi ya anapotaka kunyonya tu," alisema Mariam.
Juu ya mjomba wake na tukio hilo alilofanyiwa na mkewe, Mariam alidai hana la kusema kwa vile ni mpole kupita maelezo na kwamba amekubali kilichotokea kwa sababu kichanga hicho ni mwanae na ana wajibu wa kumtunza hasa ikizingatiwa wanapoishi ni nyuma ya familia hivyo kichanga kitaangaliwa.

Salha atua King's Modern Taarab


MUIMBAJI wa zamani wa kundi la Dar Modern Salha Abdallah 'Salha wa Hammer' aliyetimuliwa katika kundi hilo kwa kutoa wimbo binafsi na mumewe, amejiunga na la King's Modern Taarab na ameanza kuijifua kwa ajili ya maonyesho ya sikukuu ya Idd el Fitri.
Salha aliyetamba na vibao kadhaa akiwa na Dar Modern ukiwamo utunzi wake uliobeba jina la albamu ya 'Nauvua Ushoga' amelamba ajira King's Modern Julai 4 mwaka huu na anaendelea kujifua nao kwa ajili shoo za Idd na maandalizi ya albamu mpya ya kundi hilo.
Akizungumza na MICHARAZO, Salha alisema amesaini mkataba wa kulifanyia kazi kundi hilo linalotamba na kibwagizo cha 'Kijoka chazima taa' na hakuona sababu ya kuvunga huku akiwa ameshatimuliwa katika kundi lake la zamani.
"Baada ya kutemeshwa mzigo Dar Modern hivi karibuni, kundi la King's Modern limenifuata na kuniomba kujiunga nalo na kwa sasa mimi ni muimbaji wa kundi hilo, tunajiandaa kwa shoo za sikukuu ya Idd," alisema Salha.
Alisema hana cha kuahidi kwa mashabiki wa kundi hilo lakini wajiandae kupata burudani kabambe akishirikiana na wanamuziki wenzake ambao wamempokea kwa mikono miwili.
Uongozi wa Dar Modern unadaiwa kumtimua Salha baada ya muimbaji huyo na mumewe kutoa wimbo wa 'Mapenzi Matamu' (Wapendanao) kinyume na utaratibu uliopo ndani ya kundi hilo, japo Salha alilia kwamba hakutendewa haki kwa vile aliyeimba naye katika kazi hiyo ni mumewe na siyo kundi au msanii mwingine wa nje.