STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, December 2, 2014

TPBO-Limited yafichua siri ya mabondia wa Tz kupigwa ughaibuni

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEix_ikFUVQYo2XFuYXtUqvjRzHYr5VnfbR27zD1v1mQO9vDKcyGTWjAyDe3E9fbTST0rnQCVDupyg8mHUY0b4E6Sd-_s4zemsQTsSDaMD7Fz_DjHVmpMzcqxBTIkpxN200Ne6-sNZjJDms7/s1600/IMG_0009.JPG
Rais wa TPBO-Ltd, Yasin 'Ustaadh' Abdallah
RAIS wa Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO-Ltd) Yasin Abdallah 'Ustaadh' amefichua siri za mabondia wengi wa Tanzania kushindwa kufanya vema kwenye mapambano yao ya kimataifa nje ya Tanzania, akidai inachangiwa na maandalizi duni na pia kutohimili kucheza mbele ya umati mkubwa wa watazamaji.
Ustaadh, alisema siyo kweli kama mabondia wa Tanzania wanapigwa na kupoteza michezo yao nje ya nchi kwa sababu ya hujuma, bali ni kutokana na kutojiandaa vema kwa utamaduni uliipo miongoni mwa mabondia wengi nchini kutotambua kama ngumi za kulipwa ni biashara zinazohitaji wahusika kuzingatia miiko, maadili na nidhamu ya hali ya juu kufikia mafanikio ya wenzao wanaotamba duniani.
"Siyo kama wanapigwa kwa hila, wengi huwa hawafanyi maandalizi mazuri, hukurupuka tu kwenda nje kupigana na mwishowe kutia aibu imefika wakati sasa mabondia wakazinduka na kujitambua," alisema Ustaadh.
Alitoa maoni yake kufuatia bondia Fadhili Majiha kupigwa kwa KO ya raundi ya 3 kwenye pambano la utangulizi wakati Manny Pacquiao akitetea taji lake la WBO mbele ya Chris Algieri, ambapo Ustaadh alisema inawezekana kucheza mbele ya umati mkubwa na kukosa kwake maandalizi yamechangia kupata matokeo mabaya kulinganisha na yale aliyopata Russia alipoenda kupigwa kwa pointi.
Kwa muda mrefu mabondia wa Tanzania wamekuwa wakipata matokeo mabaya kwenye mapambano yao nje ya Tanzania, kiasi cha kuzushiwa kuwa huenda ni 'dili' zinazofanywa na baadhi ya mawakala wa mabondia wanaotoa ofa ya Watanzania kwenda kupigana katika nchi zao ili kulinda na kuboresha rekodi  za mabondia wanaowasimamia, wakishirikiana na viongozi wa mchezo huo nchini.
Hata hivyo mara kadhaa viongozi wa vyama vya ngumi za kulipwa wamekuwa wakikanusha kuwepo kwa suala hilo na kusisitiza kuwa mabondia wa Tanzania wanapigwa kwa sababu ya maandalizi ya zima moto na kutokuwa na mameneja wa kuwasimamia.

No comments:

Post a Comment