STRIKA

USILIKOSE

Thursday, June 7, 2012
Bingwa wa karate aililia serikali
BINGWA wa mchezo wa Karate kwa nchi za Afrika Mashariki ngazi ya klabu, Sensei Mikidadi Kilindo, ameiomba serikali iutupie macho mchezo huo na kuupa sapoti kama ilivyo kwa michezo mingine ili kuuhamasisha nchini.
Aidha, Kilindo amedai kuwa kutopewa kipaumbele kwa mchezo huo ndio kilichomfanya mara zote awe anaenda na kurudi na medali bila hata kutangazwa au kufahamika kwa wananchi kitu kinachomsikitisha.
Akizungumza na MICHARAZO
, Sensei Kilindo alisema licha ya mchezo huo kuwa na manufaa makubwa kwa taifa na jamii kwa ujumla umekuwa haupewi kipaumbele kama michezo mingine.
Alisema kutokana na hali hiyo ni vema serikali na wadau wa michezo kuutupia macho na kuusaidia ili utangazike na kutumiwa kuiletea sifa Tanzania baada ya michezo mingine kushindwa kufanya hivyo.
Bingwa huyo wa miaka minne mfululizo wa Afrika Mashariki tangu 2008 alisema, kutopewa kipaumbele kwa karate ndiko kunakofanya hata wachezaji wanaoenda kuitangaza nchi wasifahamike warudipo na ushindi.
"Mimi nimerudi hivi karibuni na medali ya dhahabu baada ya kuwa mshindi wa kwanza Afrika Mashariki, hii ni mara ya nne mfululizo, ila hakuna anayejua wala kiongozi aliyewahi kunipokea na kunipongeza inauma sana," alisema.
Pia Kilindo alisema ukimya unaofanywa na viongozi wa Chama cha Karate nchini, TASHOKA katika kuutangaza mchezo huo ni tatizo linalofanya usisikike licha ya mafanikio yake kwa ngazi ya klabu.
Alisema ni vema TASHOKA ikafanya utaratibu wa kuandaa michuano ya taifa angalau mara mbili kwa mwaka itakayoshirikisha klabu mbalimbali nchini kwa lengo la kuuhamasisha na kuutangaza mchezo huo.
Zuri Chuchu Anapenda Kuishi bwana!
Yanga, Simba 'jino kwa jino' kisa Kelvin Yondani


Wednesday, June 6, 2012
Mwenyekiti Villa Squad ajiuzulu, kisa...!
MAKAMU Mwenyekiti wa klabu ya Villa Sqaud aliyekuwa pia akikaimu nafasi ya Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ramadhani Uledi ametangaza kujiuzulu kuiongoza klabu hiyo kwa kile alichodai kutaka kulinda heshima yake.
Habari za kuaminika toka katika klabu hiyo iliyoshuka daraja toka Ligi Kuu na yenye maskani yake eneo la Magomeni Mapipa, jijini Dar na kuthibitishwa na Uledi mwenyewe zinasema mwenyekiti huyo ameamua kubwaga manyanga tangu jana.
Sababu zilizomfanya Uledi ajiondoe uongozini ni kutokana na kusakamwa na wanachama na kutengwa na viongozi wenzake baada ya kushindwa kushindwa kuinusuru Villa Squad isishuke daraja.
Chanzo cha habari cha awali kilisema kutokana na shinikizo kubwa la wanachama hao, Uledi aliamua kubwaga manyanga akiandika barua ya kujitoa madarakani.
Hata hivyo MICHARAZO lilipowasiliana na Uledi kutaka kuthibitisha taarifa hizo, alikiri juu ya kujiuzulu kwake, akidai amefanya hivyo ili kulinda heshima yake kutokana na kuona hali si shwari ndani ya klabu yao.
Uledi, alisema tangu alipochaguliwa hakuwahi kupata ushirikiano wa kutosha kwa viongozi na wanachama, ila aliichukulia hali hiyo kama changamoto wake, lakini kwa hali inavyozidi kwenda mrama klabu kwao ameona bora ajiengue ili Villa itulie.
"Ni kweli nimejiuzulu kutokana na hali ya mambo iliyopo klabuni, pia nahofia kuvunjiwa heshima, hivyo nimewaachia wanachama klabu yao, ingawa bado nitaendelea kuwa ndani ya timu hiyo kwa hali na mali kama mwanachama hai," alisema.
Uledi, aliongeza anadhani chokochoko zote zilizopo Villa Squad kwa sasa zimetokana na timu hiyo kushindwa kubaki ligi kuu, japo alidai yapo mambo mengi yaliyochangia timu hiyo kutohimili ushindani hasa kutokana na hali mbaya ya kifedha iliyokuwa nayo.
Mwenyekiti huyo na wenzake walichaguliwa kwenye uchaguzi mkuu uliokuwa umejaa mizengwe Juni 25 mwaka jana, huku nafasi ya Mwenyekiti na wajumbe watatu zikiwa wazi baada ya Kamati ya Uchaguzi wa TFF, kuwaengua waliokuwa wagombea wake kwa kukosa sifa za kuwania nafasi hizo ikiwemo suala la elimu zao.
Muziki wa Dansi walilia nafasi redioni, runingani


Uchaguzi Mkuu Yanga kumekucha, wanawake waitwa Jangwani
WAKATI zoezi la uchukuaji na urudishaji fomu kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa klabu ya Yanga ukitarajiwa kufungwa rasmi leo saa 10:00 jioni, wanachama vibopa wa klabu hiyo wamejitokeza kuwania uongozi na kuonyesha namna gani Jangwani walivyopania kufanya mabadiliko ya kuondokana na viongozi 'ombaomba'.
Miongoni mwa waliojitokeza kwa jana kuchukua fomu za kuwania madarakani katika uchaguzi huo utakaofanyika Julai 15 ni pamoja na Yono Kevella wa Yono Auction Mart, Muzzammil Katunzi na Mussa Katabalo wanaowania nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo.
Wanachama wengine waliochukua fomu jana kuwania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Eliakim Mmaswi, Lameck Nyambaya, Ahmed Gao na wachezaji nyota wa zamani wa klabu hiyo ambao ni Edgar Fongo, Ramadhani Kampira, Ally Mayai na Aaron Nyanda.
Uchaguzi mdogo wa Yanga unatarajiwa kufanyika Julai 15, hatua inayotokana na idadi kubwa ya viongozi waliokuwa madarakani hapo awali kutangaza kujizulu hivi karibuni, akiwemo Lloyd Nchunga aliyekuwa akishikilia nafasi ya uenyekiti.
Tofauti na wagombea wengine, Katunzi na Katabalo wao walichukuliwa fomu na wazee wa klabu hiyo ambao wako chini ya mwenyekiti wao Jabir Katundu na katibu, Ibrahim Akilimali.
Akimkabidhi fomu Katunzi, Akilimali alisema kuwa lengo la kumtaka mwanachama huyo wa Yanga kugombea ni kuimarisha safu yao ya uongozi ambayo itakuja na jukumu moja tu la kuiendeleza Yanga na kuokoa jahazi lao ambalo anaamini kwamba lilikuwa likizama.
Akilimali alisema kuwa Yanga inahitaji wanachama wenye uwezo wa kuisaidia timu wakati wowote ili ifanye vizuri na kurejesha furaha kwa wanachama wao.
"Hatuhitaji waomba dagaa, tunataka kiongozi mwenye uwezo ambapo inapohitajika Sh. 300,000, yeye atatoa Sh. 600,000," alisema Akilimali.
Hadi kufikia jana, waliochukua fomu kuwania kutwaa mikoba ya Nchunga ni pamoja na John Lambele, huku Ayuob Nyenzi ambaye katika uchaguzi uliopita alijitoa kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti, akichukua fomu ya kuomba kuchaguliwa kwenye cheo hicho.
Wengine waliochukua fomu wakiwania nafasi za ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga ni Jumanne Mwamwenya, Peter Haule, Gaudecius Ishengoma, Abdallah Sheria, Saleh Abdallah, Abdallah Binkleb na Muhingo Rweyemamu.
Isack Chanzi amejitokeza kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti ambayo Davis Mosha alijiuzulu mapema mwaka jana baada ya kudai kwamba ameshindwa kutimiza malengo yake kwa kukosa ushirikiano kutoka kwa viongozi wenzake.
Uchaguzi huo unasimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo iliyoko chini ya Jaji Mstaafu John Mkwawa.
Hata hivyo mpaka sasa hakuna mwanachama yeyote wa kike wa klabu hiyo aliyejitokeza kuwania uongozi, hali iliyofanya kamati hiyo kutoa wito kwa wanachama hao kujitokeza kwani milango i wazi kwa wote.

John Kitime ajitosa kwenye utunzi wa vitabu, aja na 'vunja mbavu'
MWANAMUZIKI mkongwe wa muziki wa dansi nchini, John Kitime, amejitosa kwenye utunzi wa vitabu, ambapo kwa sasa yuko hatua za mwisho kukamilisha kitabu chake cha kwanza cha 'vunja mbavu' kiitwacho 'Kucheka ni Muhimu'.
Akizungumza na MICHARAZO
jana, Kitime ambaye ni mwanamuziki wa bendi ya Kilimanjaro 'Wana Njenje na pia ni mmoja wa wanakamati ya kutetea muziki wa dansi nchini, alisema amepata wazo la kuandika kitabu hicho kutokana na kipaji cha uchekeshaji alichonacho.
Kitime ambaye wakati mwingine huwa jaji wa shindano la kusaka vipaji vya kuimba la Bongo Star Search, alisema kitabu hicho kwa sasa kipo katika hatua ya uhariri kabla ya kuanza mipango ya kukichapisha na kukisambaza ili kuwapa burudani wapenzi wa vunja mbavu.
"Nipo katika hatua ya mwisho ya kumalizia kitabu changu cha kwanza kiitwacho 'Kucheka ni Muhimu', nadhani muda si mrefu mhakato wake wa kukitoa utafanyika na kuwapa burudani Watanzania," alisema.
Aliongeza mbali na kitabu hicho pia ameshaandika vitabu vingine viwili kimoja kiitwacho 'Kilimanjaro Band' ambacho kitakuwa maalum kwa ajili ya kuzungumzia historia ya bendi hiyo ilitoka, ilipo na inapoenda pamoja na wasifu wa wanamuziki wake.
"Kitabu kingine cha tatu ni cha 'Haki Miliki'. Nimeamua kuandika hiki kwa nia ya kuwazindua wasanii kufahamu haki zao katika miliki ya kazi zao," alisema mkongwe huo.
Kitime anakuwa mwanamuziki wa pili mkongwe kujitosa kwenye fani ya uandishi vitabu, baada ya Tshimanga Kalala Assosa, aliyetunga kitabu cha 'Jifunze Lingala' ambacho kinaendelea kutamba sokoni kwa sasa huku akiandaa kingine cha wasifu wake.

Nassib, Majia kuwania ubingwa wa TPBO
MABONDIA machachari wa ngumi za kulipwa nchini, Nassib Ramadhani na Fadhili Majia wanatarajiwa kupanda ulingoni Juni 9 kuwania taji la taifa la Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO).
Pambano hilo la uzani wa Super Fly (kilo 52) litafanyika kwenye ukumbi wa Friend's Corner, Manzese na litasindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi.
Rais wa TPBO, Yasin Abdallah 'Ustaadh', aliiambia MICHARAZO jana kuwa pambano hilo limeandaliwa na promota Kaike Siraju na kwamba maandalizi yanaendelea vema.
Ustaadh alisema tayari mabondia wote wanaendelea kujifua tayari kwa pambano hilo litakalokuwa la raundi 10 ambapo siku moja ya kupanda ulingoni watapimwa afya na uzito wao.
"Mabondia wetu mahiri kabisa nchini, Nassib Ramadhani na Fadhili Majia wanatarajiwa kupigana kuwania ubingwa wa TPBO uzani wa Super Fly, litakalofanyika siku ya Jumamosi kwenye ukumbi wa Friend's Corner," alisema.
Katika kuzuia vitendo vyovyote vya kihuni, Ustaadh alisema TPBO imejipanga kuhakikisha ulinzi madhubuti katika pambano hilo kwa kuanza kuwasiliana na mkuu wa polisi kituo cha urafiki ili kuwasaidia siku hiyo.
"Tayari tumeshamuandikia barua mkuu wa kituo cha Polisi cha Urafiki, Afande Paparika, ili kutupa ulinzi wa kutosha siku ya pambano," alisema.
Ustaadh alisema imani yake pambano hilo litawasisimua wengi kutokana na upinzani mkali uliopo baina ya mabondia hao na wale watakapambana katika michezo ya utangulizi siku hiyo na kuwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi.
Bibi Cheka, Dogo Aslay kutambulishwa Kanda ya Ziwa
WASANII wanaokuja juu katika muziki wa kizazi kipya nchini, Asilahi Is'haka 'Dogo Aslay' na Cheka Hija a.k.a 'Bibi Cheka' wanatarajiwa kwenda kutambulishwa rasmi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa wakisindikizwa na wasanii kibao nyota.
Meneja wa wasanii hao, Said Hassani 'Mkubwa Fella' aliiambia MICHARAZO
kwamba wasanii hao wataenda kutambuliwa katika mikoa ya Mwanza na Mara katika maonyesho yatakayofanyika mwishoni mwa wiki hii.
Fella alisema wasanii watakaoenda kuwasindikiza Bibi Cheka anayetamba na wimbo wake wa 'Ni Wewe' alioimba na Mheshimiwa Temba, na Dogo Aslay aliyeachia ngoma mpya ya 'Umbea', ni pamoja na Ferooz, Easy Man, kundi la TMK Wanaume Family na wengine.
"Mkubwa tunatarajia kwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa ajili ya maonyesho maalum ya kuwatambulisha Dogo Aslay na Bibi Cheka, shoo hizo zitakuwa tatu mfululizo zikianza Juni 8 mpaka 10 na watasindikizwa na 'vichwa' kibao," alisema Fella.
Aliongeza kuwa maonyesho yao mawili ya awali yatafanyika jijini Mwanza kabla ya kumalizia burudani yao mkoani Mara na iwapo watapata fursa zaidi wanaweza kuhamishia utambulisho huo mkoani Shinyanga kabla ya kurejea Dar es Salaam.
Alisema mbali na 'Ni Wewe', Bibi Cheka msanii wa muziki wa kizazi kipya mwenye umri mkubwa kuliko wote nchini, atatambulisha wimbo wake mwingine mpya aliouimba kwa kushirikiana tena na Mheshimiwa Temba uitwao 'Mario'.

Warembo Miss Bagamoyo kusaka vipaji J'pili Dar
WAREMBO tisa wanaojiandaa na shindano la urembo la 'Redd's Miss Bagamoyo 2012' wanatarajiwa kuonyeshana kazi katika mchuano wa kusaka kipaji 'Miss Talent' Jumapili ijayo.
Mratibu wa shindano hilo, Awetu Salim, alisema shindano hilo la vipaji litafanyika kwenye ukumbi wa Club Masai, Kinondoni kabla ya warembo hao kuelekea mjini Bagamoyo kuwania taji la urembo la mji huo litakalofanyika Juni 15.
Alisema warembo hao wanaoendelea na mazoezi kwenye ukumbi wa Club Masai chini ya mkufunzi wao, Sadah Salim wameanza kutambiana kila mmoja akidai ana kipaji kitakachompa ushindi kabla ya kwenda kutwaa taji la urembo.
"Warembo wetu wanaendelea vizuri na mazoezi yetu na Jumapili wanatarajia kuchuana kwenye shindano la vipaji, litakalofanyikia kwenye ukumbi wa Club Masai na siku chache baadae wataelekea Bagamoyo kuwania taji la urembo litakalofanyika Juni 15 kwenye ukumbi wa TaSUBA," alisema.
Awetu aliwataja warembo hao kuwa ni Zuhura Abdallah, Veronica James, Rose Lucas, Beatrice Bahaya, Diana Exavery, Nancy, Flora, Yvonne Steven na Celline Wangusu.
Aidha, Awetu alishukuru kuongezeka kwa wadhamini zaidi katika shindano lao ambapo aliitaja kiwanda cha mvinyo cha Dodoma Wines kuwa ni miongoni mwa wadhamini wapya waliojitosa kuwapiga tafu.
Mratibu huyo aliongeza kuwa upande wa burudani katika shindano lao watapambwa na bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' na mshehereshaji wa shughuli hiyo anatarajiwa kuwa Khadija Shaibu 'Dida wa G'.
Aurora afariki, azikwa Dar atakumbukwa kwa mengi

Monday, June 4, 2012
Kitale: 'Teja' la kwenye runinga lisiloujua 'unga'





Drogba aimwagia sifa Taifa Stars, achekelea kuwatungua


Wazee wa Ngwasuma kutumbuiza Miss Kigamboni


Masai Nyota Mbofu aachia Rungu na Mukuki
MCHEKESHAJI maarufu nchini, Gilliad Severine 'Masai Nyota Mbofu', ameachia wimbo mpya uitwao 'Rungu na Mukuki' sambamba na video yake akishirikiana na wasanii wa kundi la Vichwa la Zambia, Simple K na G4.
Tayari wimbo na video hiyo imeshaanza kurushwa hewani wakati mwenyewe akijiandaa kupakua kazi nyingine mpya.
Akizungumza na MICHARAZO, Masai Nyota Mbofu, alisema wimbo huo ameurekodia nchini Zambia katika studio za Hez Sound chini ya Prodyuza, Acknex na video yake amefyatulia nchini humo na kuja kuimalizia Tanzania.
Msanii huyo, alisema kazi hiyo mpya ni salamu kwa mashabiki wake waliomzoea kumuona katika filamu na komedi tu, kwamba kwenye muziki naye yumo.
Masai Nyota Mbofu, alisema wakati wimbo na video hiyo ikiendelea kutamba ameanza kuandaa wimbo mipango ya kutoa kazi nyingine kwa lengo la kuja kufyatua albamu hapo baadae.
"Wakati Rungu na Mukuki, ikiendelea kukimbiza kwa fideo na radio, tayari nimenza kuandaa kazi nyingine nataka onyesha mashabiki angu kwamba mi nawesa," alisema Masai kwa kiswahili kibovu cha kikomedi.
Mkali huyo aliyeanza kutamba kwenye michezo ya runinga akiwa na kikundi cha Jakaya Theatre kabla ya kuibukia kwenye filamu chini ya kampuni ya Al Riyamy Production.
Baadhi ya kazi zilizowahi kumpa ujiko msanii huyo ni Iny'e Plus, 'Iny'e Gwedegwede', 'Vumba Vimejaa', 'Pedeshee' na sasa anatamba na kipindi cha Vituko Show.

Mosha awachomolea wazee Yanga, fomu zachangamkiwa

Simba noma, yabebe mzigo wa matibabu ya akina Boban

Noela ndiye Miss Tabata 2012
Saturday, June 2, 2012
Mr Blue, Malaki wachanganywa na Msichana Mzuri
Malaki
MSANII anayekuja kwa kasi nchini, Sela Myovela 'Malaki' ameachia ngoma mpya iitwayo 'Msichana Mzuri' aliyoimba akishirikiana na mkali wa R&B, Khery Sameer Rajab maarufu kama Mr Blue au 'Kabaysa'.
Akizungumza na MICHARAZO, Malaki aliyewahi kufyatua ngoma nyingine kali iitwao 'Maisha' aliyoimba na mkali wa Bongofleva nchini, Juma Kassim Kiroboto 'Sir Juma Nature' alisema wimbo huo mpya ameurekodia katika studio za Fishcrab chini ya prodyuza matata, Lamar.
Malaki alisema wimbo huo uliopo katika miondoko ya R&B ni maalum ya ujio wake mpya chini ya usimamizi wa kaka yake, Mfaiswa Myovela 'Mzee wa FilamuCentral'.
"Baada ya kimya kirefu cha miaka kama mitano, nimekuja na ngoma mpya kabisa iitwayo 'Msichana Mzuri' niliyopigwa tafu na Mr Blue, ikifanywa chini ya Lamar wa Fishcrabs Studio," alisema.
Alisema, tayari wimbo huo ameshausambaza katika vituo vya redio na kuanza kurushwa hewani, huku mwenyewe nakijipanga kwa ajili ya kuitolea video yake.
Aliongeza, lengo lake ni kufyatua albamu hapo baadae ingawa alisema kwa sasa ataendelea kudondosha wimbo mmoja mmoja kwa ajili ya kuweza kujitangaza na kupata shoo zitakazomwezesha kupata fedha za kukamilishia albamu hiyo.
Malaki alitumbukia kwenye muziki wa kizazi kipya tangu mwaka 2005 na kutoa kazi yake ya kwanza kabisa akiwa na Juma Nature mwaka 2007 kabla ya kuwa kimya hadi mwaka huu alipotoka na 'ngoma' hiyo mpya.
Mr Blue katika pozi zake.
'Maafande' wamnyemelea Ngassa
KLABU nne tofauti zimekuwa zikimnyatia mshambuliaji mahiri wa timu ya Moro United, Benedict Ngassa, kwa ajili ya kutaka kumnasa ili wazichezee timu zao katika msimu moya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza na MICHARAZO, Ngassa alizitaja klabu hizo zinazomnyemelea kuwa ni JKT Ruvu, Ruvu Shooting, African Lyon na timu iliyopanda daraja ya Prisons ya Mbeya.
Ngassa alisema viongozi wa klabu hizo kwa nyakati tofauti wamekuwa wa kiwasiliana nae na kufanya mazungumzo ingawa alikiri bado hajaafikiana nao mpaka sasa.
"Licha ya kufuatwa na viongozi wa klabu hizo, bado sijaamua niende wapi, nitaangalia kwanza masilahi," alisema.
Aliongeza kuwa, ingawa anafurahia kunyatiwa na timu hizo, lakini roho yake inamuuma kwa timu yake ya Moro United kushuka daraja akielekeza lawama zake kwa wachezaji walioichezea timu hiyo kwa mkopo.
Ngassa, alisema wachezaji waliotua katika timu hiyo kwa mkopo toka klabu mbalimbali nyingine za ligi kuu walikuwa wakiihujumu timu yao ambapo licha ya wachezaji halisi wa Moro kujituma na kuifungia mabao, magoli hayo yalikuwa yakirejeshwa kitatanishi.
"sio siri tumeshushwa daraja na wachezaji waliokuja Moro kwa mkopo, inauma sana," alisema.
Moro United iliyokuwa imerejea tena Ligi Kuu imejikuta ikishuka daraja ikiungana na timu za Villa Squad na Polisi Dodoma kutokana na kujikusanyia pointi chache katika mechi 26 ilizocheza msimu huu ambapo Simba waliibuka mabingwa.
Bondia Magoma Shaaban afariki, azikwa kwao Tanga
ALIYEKUWA Bingwa wa Dunia wa WBU uzani wa Super Fly, Magoma Shaaban amefariki dunia na kuzikwa kwao mkoani Tanga.
Kwa mujibu wa mdau mkubwa wa mchezo wa ngumi ambaye pia ni promota, Ibrahim Kamwe, Magoma alikumbwa na umauti juzi kwenye hospitali ya Bombo mkoani Tanga.
Magoma alikuwa amelazwa katika hospitali hiyo siku nne zilizopita kutokana na kuzidiwa na maradhi aliyokuwa nayo siku nyingi na kufariki majira ya jioni na alizikwa jana nyumbani kwao Mabovu Mwembesamaki, mjini Tanga.
Marehemu aliyeacha mjane na watoto wawili Sudi,10 na Almasi,7 alizaliwa Oktoba 21, 1980 mjini Tanga na alianza kucheza ngumi tangu akiwa kinda akipitia klabu mbalimbali za ngumi za ridhaa kabla ya kuingia za kulipwa mwaka 1996 alipopanda ulingoni kuzipiga na Athumani Omari na kushinda kwa pointi.
Hadi mauti yanamkuta bondia huyo aliyekuwa mfupi lakini machachari, alikuwa amepigana mapambano 16 na kushinda 13 kati ya hayo mapambano manne akishinda kwa KnockOut (KO) na kupigwa matatu pia kwa KO.
Mara ya mwisho kupanda ulingoni ilikuwa Julai 21 mwaka 2006 na Eugen Sorin Tanasie mjini Timisoara, Romania katika pambano ambalo alipigwa kwa Technical Knockout (TKO) raundi ya pili.
Taji lake la kwanza kutwaa lilikuwa ni la IBF Afrika, Septemba 12, mwaka 1998 akimpiga Mkenya Joseph Waweru kwa KO raundi ya kwanza, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Mei 11, mwaka 2000 alimpiga bondia ‘matata sana’ Totin Lukunim wa Thailand na kutwaa taji la IBF Intercontinental, uzito wa Super Fly kwenye ukumbi wa PTA, Temeke, Dar es Salaam.
Agosti 3, mwaka 2001 ndipo alitwaa ubingwa wa dunia wa WBU baada ya kumpiga Ferid Ben Jeddou wa Tunisia kwa TKO raundi ya sita mjini Avezzano, Abruzzo, Italia, kabla ya kupoteza taji hilo kwa kupigwa na Gabula Vabaza Julai 26, mwaka 2002 katika ukumbi wa Hemingways Casino, East London, Eastern Cape, Afrika Kusini kwa KO raundi ya kwanza.
Mei 25, mwaka 2003 alipigwa na Mtanzania mwenzake, Mbwana Matumla kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam kwa TKO raundi ya nne.
Wadau mbalimbali wa ngumi wameelezwa kusikitishwa na kifo cha Magoma, wakiitaka familia, ndugu, jamaa na rafiki zake kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu wakiwakumbusha kuwa kazi ya Mola huwa haina makosa.
Friday, June 1, 2012
Costa, Jabu, Kago watupiwa virago Simba, wanne wajaza nafasi zao
NYOTA watano wa kikosi cha Simba ambao kwa kiasi kikubwa waliisaidia timu hiyo kung'ara msimu huu wamedaiwa kutupiwa virago, huku nafasi zao zikichukuliwa na wakali wanne waliosajiliwa mpaka sasa ndani ya kikosi hicho.
Habari za kuaminika ambazo zimenaswa jijini ni kwamba wachezaji walitupiwa virago ni nyota wa kimataifa toka Jamhuri wa Kati, Gervais Kago, mabeki wa kati Victor Costa na Juma Nyosso, Juma Jabu na Ulimboka Mwakingwe aliyekuwa majeruhi kwa muda mrefu.
Aidha kuna taarifa nyingine kwamba naye Uhuru Seleman yupo katika mchakato pia wa kutemwa katika kikosi hicho iwapo atafanikiwa kupata timu, ikidaiwa ananyemelewa na Yanga.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari toka ndani ya Simba, ni kwamba Costa, Jabu na Kago wametemwa kwa kushuka viwango, huku Nyosso anaysakwa na Yanga pia, ametemwa kutokana na utovu wa nidhamu wa mara kwa mara anaoufanya dimbani na kuigharimu timu, huku Mwakingwe kwa umri na kuwa majeruhi wa muda mrefu.
Nafasi za wachezaji hao mpaka sasa zimechukuliwa na wakali wanne walionaswa Msimbazi ambao ni Juma Abdallah, Mussa Mudde Mbongo aliyekuwa akicheza SOFAPAKA, Patrick Nkanu toka Congo na Ibrahim Rajab 'Jebba'.
Viongozi wa Simba walinukuliwa jana kwamba, zoezi zima la usajili wa timu yao utaanikwa baada ya kamati zao za ufundi na mashindano kuendesha zoezi hilo kwa maelekezo ya kocha wao, Cirkovic Milovan.
Zoezi la usajili nchini kwa timu za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2012-2013 umefunguliwa rasmi leo Juni Mosi na unatarajiwa kumalizika mwanzoni mwa Julai kabla ya Ligi kuanza Agosti ambapo miongoni mwa timu zitakazoshiriki ni Polisi Moro, Mgambo Shooting ya Tanga na Prisons ya Mbeya zilizopanda daraja toka la Kwanza.
Wema Sepetu afafanua pete aliyovishwa Maisha Club
MSANII nyota wa filamu nchini, Wema Sepetu amefafanua uvumi ulioenea jijini Dar kwamba ameangukia kwenye penzi na mwanamuziki wa bendi ya Machozi, Mwinyi kiasi cha kuvishwa pete ya uchumba kama alivyofanyiwa na aliyekuwa boifrend wake, Naseeb Abdul 'Diamond' kabla ya kumwagana hivi karibuni.
Wema alisema pete aliyovishwa mwishoni mwa mwezi uliopita ilikuwa ni igizo la filamu aliyokuwa akiishoot iitwayo 'Super Star' kazi binafsi anayokuja nayo ambayo sehemu kubwa inahusu maisha yake halisi.
Mrembo huyo alisema wengi walishindwa kuelewa walipomuona akivishwa pete na Mwinyi na kukumbatiwa huku wakipigana mabusu kwa kuwa kamera zilizokuwa zikitumika kutengenezea filamu hiyo zilikuwa juu na hivyo hazikuonwa na watu.
"Sio kweli kama nimechumbiwa na Mwinyi wa Machozi, ila tulikuwa tukiigiza filamu yangu ya kwanza binafsi iitwayo 'SUPER STAR' ambayo ni kama inazungumzia maisha yangu," alisema.
Mwinyi amecheza kama Diamond katika filamu hiyo ambapo aliwahi kumvisha pete na kutamka maneno ya kusisimua kabla ya kuja kugeukana.
Wema alisema filamu hiyo anatarajia kuizindua Juni 23 baada ya kukamilika na imemgharimu karibu Sh Milioni 30 mpaka sasa.
Miss Tanzania huyo wa 2006 amesema filamu hiyo imewashirikisha wasanii kadhaa nyota, na anatarajia itakuwa filamu ya kusisimua kutokana na kuigiza sehemu kubwa katika uhalisi wa maisha yake kama WEMA SEPETU.
Stars yafika salama Abidjan, kuwavaa Tembo wa Ivory Coast kesho
Kikosi cha Taifa Stars kimewasili salama mjini Abidjan mchana wa jana huku Kocha Mkuu wa timu hiyo Kim Poulsen akisema mechi dhidi ya Ivory Coast itakuwa ngumu.
Kwa mujibu wa ofisa habari wa TFF Boniface WAmbura ambaye ameambatana na timu, Stars yenye wachezaji 21 ilikuwa iwasili hapa asubuhi, lakini ndege iliyobadilisha Nairobi ilichelewa kuondoka kwa saa tatu. Mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Taifa Stars na wenyeji Ivory Coast (Tembo) itachezwa Juni 2 mwaka huu Uwanja wa Felix Houphouet-Boigny kuanzia saa 11 kamili jioni ambapo Tanzania itakuwa saa 2 kamili usiku.
Licha ya kwanza, Stars ililazimika kuacha wachezaji wawili dakika za mwisho (Haruna Moshi na Nassoro Cholo), Kim amesema kikosi chake ambacho kimefikia hoteli ya Ibis bado kimejipanga vizuri kwa ajili ya mechi hiyo.
“Tunaiheshimu Ivory Coast kwa vile ni timu ambayo inaundwa na baadhi ya wachezaji nyota wa dunia kama akina Drogba (Didier) na Yaya (Toure), lakini wajiandaa kupata wakati mgumu kutoka kwetu,” amesema Kim ambayo kikosi chake baada ya kuwasili hapa kilipata fursa ya kufanya mazoezi jioni.
Kikosi cha Stars kinaongozwa na nahodha wake Juma Kaseja akisaidiwa na Aggrey Morris. Wachezaji wengine waliopo hapa na kikosi hicho ni Mwadini Ally, Deogratius Munishi, Amir Maftah, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Waziri Salum, Shomari Kapombe na Juma Nyoso.
Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Salum Abubakar, Shabani Nditi, Edward Christopher, Mrisho Ngasa, Frank Domayo, Mbwana Samata, Ramadhan Singano, Simon Msuva na John Bocco.
Mbali ya Kim, Benchi la Ufundi lina Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold Mukebezi (Meneja wa timu), Juma Mwankemwa (Daktari wa timu), Frank Mhonda (Physiotherapist) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).
Msafara wa Stars hapa unaongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Crescentius Magori lakini pia yupo Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi ambaye amekuja kushuhudia mechi hiyo.
Subscribe to:
Posts (Atom)