STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, September 28, 2012

KOCHA MPYA YANGA AWASILI KIMYAKIMYA

Brandts

Na Mahmoud Zubeiry
KOCHA mpya wa Yanga, Ernstus ‘Ernie’ Wilhelmus Johannes Brandts, beki wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi na klabu ya PSV Eindhoven ya Holanzi, atawasili wakati wowote kuanzia leo kusaini mkataba na kuanza kazi katika klabu hiyo.
Hata hivyo, Yanga imeamua kufanya siri ujio wa kocha huyo, kwa sababu haitaki mapokezi ya mbwembwe, kutokana na rekodi yake ya kutodumu na makocha.
Yanga, imetimiza malengo yake ya kuwa kocha mpya, kabla ya kucheza na wapinzani wao wa jadi, Simba SC, Oktoba 3, mwaka huu baada ya kumfukuza Mbelgiji, Tom Saintfiet, kutokana na kufikia makubaliano na Brandts.
Mholanzi huyo aliyefukuzwa APR ya Rwanda baada ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Agosti mwaka huu amepewa ukocha wa Yanga, baada ya Mbrazil Marcio Maximo kukataa nafasi hiyo kwa mara ya pili.
Mtaalamu huyo, alizaliwa Februari 3, mwaka 1956 mjini Nieuw-Dijk, Gelderland, mbali na PSV Eindhoven, alichezea pia Roda JC Kerkrade, MVV Maastricht na De Graafschap.
Brandts aliichezea mechi 28 timu ya taifa ya Uholanzi na kuifungia mabao matano na pia alicheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1978.
Katika fainali hizo, Raundi ya pili kwenye mechi na Italia, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyezifungia mabao timu zote katika mechi moja kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Alianza kujifunga dakika ya 18, kisha akaisawazishia Uholanzi dakika ya 50 katika mechi ambayo, mchezaji mwenzake Arie Haan baadaye aliifungia timu yake bao la ushindi na kutoka kifua mbele kwa mabao 2–1.
Alipostaafu soka akawa kocha na katikati ya msimu wa 2007–2008, Brandts aliambiwa hataongezewa mkataba NAC-Breda, licha ya matokeo mazuri ya kushika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Uholanzi (Eredivisie), ingawa uamuzi huo haukuwafurahisha mashabiki wa timu hiyo na nafasi yake akapewa Robert Maaskant kuanzia msimu wa 2008–2009.
Akateuliwa kuwa Kocha wa Rah Ahan mwaka 2009, kabla ya kufukuzwa Desemba 2009 na kuibukia APR ya Rwanda mwaka 2010, ambako ‘riziki’ yake imeisha miezi miwili iliyopita na sasa amepata maisha mapya Yanga.
Akiwa APR, Brandts alifungwa mechi zote mbili na Yanga iliyokuwa ikifundishwa na Mbelgiji Tom Saintfiet katika Kombe la Kagame, moja ya makundi 2-0 na nyingine ya Nusu Fainali 1-0. Yanga iliibuka bingwa, ikiifunga Azam FC 2-0 kwenye fainali.
Brandts atakutana na wachezaji wake wa zamani wawili Yanga, beki Mbuyu Twite anayeanza msimu wa kwanza katika klabu hiyo na kiungo Haruna Niyonzima anayeingia katika msimu wa pili, ambao alifanya nao kazi APR.
 
CHANZO:BIN ZUBEIRY

Chelsea uso kwa uso na Man Utd Kombe la Ligi

 

 

BAADA ya kufanikiwa kupenya katika michuano ya Kombe la Ligi, mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Chelsea na Manchester United zinatarajiwa kuvaana katika hatua ya 16 Bora ya michuano ya Kombe la Ligi.

Timu hizo vigogo vimepangwa kuumana katika droo ya michuano hiyo iliyotolewa juzi baada ya timu hizo kupata ushindi katika mechi zao za hatua iliyopita ambayo ilishuhudia mabingwa watetezi wa Ligi ya England ikitupwa nje na Aston Villa.

Ratiba hiyo inaonyesha pia timu za Liverpool na Swansea City zilizobadilishana makocha zitavaana, huku Sunderland itaumana na Middlesbrough kuwania nafasi ya kutinga robo fainali hapo baadae.

Mechi hizo za kuwania kutinga robo fainali zinatarajiwa kuchezwa Oktoba 29 mwaka huu ambapo timu zilizopangwa kung'oa hatua hiyo ya 16 Bora ni kama ifuatavyo hapo chini:

 

Sunderland v Middlesbrough
Swindon Town v Aston Villa
Wigan Athletic v Bradford City
Leeds United v Southampton
Norwich City v Tottenham Hotspur 
Liverpool v Swansea City
Chelsea v Manchester United

Reading v Arsenal

FAINALI ZA STR8 MUZIKI ZAFANA MWANZA



Izzo Bizness akishusha michano
 






FAINALI za tamasha la muziki la STR8 zilimalizika jana mjini hapa kwa kishindo cha aina yake huku tuzo ya DJ Bora yenye thamani ya thamani ya Sh. milioni 7 ikimuangukia DJ Juma Ramadhani.

Ilikuwa ni patashika nguo kuchanika wakati ma-DJ na ma-MC walipokuwa wakipambana vikali kuwania moja ya vifaa vya kisasa kabisa katika masuala ya kuchezesha muziki, DJ Pioneer.


Ruyobya Johaness a.k.a DJ YT alikamata nafasi ya pili katika kategori ya ma-MC akiondoka zawadi kadhaa zikiwamo fedha taslimu Sh.100,000.


Mshindi katika kategori ya MC alikuwa ni Joash Magadula ambaye pamoja na tuzo pia alipata nafasi ya kurekodi albamu katika moja ya studio tatu bora za muziki nchini.


Nchana Anthony alishika nafasi ya pili katika kategori hiyo ya ma-MC na aliondoka na zawadi kadhaa na fedha taslimu Sh.100,000.


Fainali hizo ambazo ni za tatu tangu zianzishwe nchini zinaratibiwa na kampuni ya Sigara nchini (TCC) kwa lengo la kukuza vipaji miongoni mwa vijana na kutengeneza nafasi ya ajira.


Michuano hiyo ambayo ilihusisha ma-Mc 85 na ma-DJ 25 zilichuja washindani wake hadi 16 kwa MC na 10 kwa ma-DJ katika raundi ya kwanza kabla ya raundi ya pili kutoa washiriki wa fainali.


Ma-DJ hao walipewa maksi kwa kuangaliwa na majaji kuhusu uwezo wao wa kuchanganya muziki, uwezo wa kiufundi, wanavyomudu vifaa wanavyofanyia kazi na jinsi wanavyoburudisha.


Ma-DJ sita waliofika fainali walikuwa Bernard Fabian, DJ Yt, Robert Rowan, DJ Megastar, Tony Wyclif na Juma Ramadhani.


Kategori ya MC ilihusisha mshiriki kupewa mada ya kuielezea kwa mtindo wa kufokafoka kwa dakika tatu kiushairi kimpangilio.


Matukio hayo ya fainali yalinogeshwa na burudani mbalimbali zikiwamo zilizotolewa na wakali wa Bongofleva kama rapa Izzo Bizness ambaye ni maarufu kupitia wimbo wake wa 'Riz-One (Ongea na Mshua)’ .


Walikuwapo pia vijana wa kundi la kudansi la BFB la Mwanza, ambao walipagawisha mashabiki kwa staili zao mbalimbali za kucheza ikiwamo kwa sarakasi.


Aliyetingisha zaidi katika vionjo alikuwa ni mshindi mwaka 2010 katika kategori ya MC, DJ Simba, ambaye alionesha ubabe wake katika kucheza na biti kiasi cha kufanya ukumbi mzima kurindima kwa shangwe.


“Vipaji hivi vinatakiwa kulelewa na kuendelezwa,” alisema Deogratius Kamugisha, mwenyeji wa mashindano hayo ambaye pia ni Meneja wa TCC Mwanza.


Alisema kwamba michuano hiyo ilikuwa si tu burudani bali pia ilitoa mwanya wa mafanikio mengine kama ajira.


Alisema washindi wa michuano iliyopita kwa sasa wako katika ajira mbalimbali zikiwemo vilabu vya usiku na vituo vya radio.


"Hii ni namna ya kutengeneza ajira," alisema na kuongeza kwamba mashine ya kuchezea muziki kama aliyopewa Juma Ramadhani ni chanzo cha ajira kwani anaweza kuitumia yeye au kuikodisha kwa wengine anapokuwa hana kazi nayo.


Mchuano mingine miwili itafanyika mjini Dar es Salaam na Mbeya kukamilisha tamasha la mwaka huu.

UDOM YAKARIBIA KUINGIZA FILAMU YA MY MAN 2 SOKONI.


Filamu Mpya Ya My Man Sehemu ya 2 inatarajiwa kuingia Sokoni muda si mrefu kutokana na kumalizika kwa kazi nzima ya utengenezaji wake.

Filamu hii ya kitanzania ambayo story yake imeandikwa na Kijana Geric Kimaro anayesomea Shahada ya Kwanza ya Filamu katika Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM) akiwa mwanafunzi wa Mwaka wa 2 Chuo Hapo.

Akiongea na Mtandao  wa LUKAZA BLOG amesema " Mashabiki wa filamu za kitanzania wakae Mkao wa Kula kwasababu kwanza hawataboreka kutokana na waigizaji wake ni Vijana wanaosomea fani ya Filamu katika ngazi ya Shahada ya Kwanza ambao wana vipaji na ujuzi pia katika tasnia ya filamu nchini lakini pia Katika filamu hiyo ambayo imetengenezwa na kampuni ya BORNAGAIN na kumshirikisha Nguli wa filamu za Bongo Mwenye Swaga za Uchungaji, Pastor Myamba." 

Mbali na Kumshirikisha Pastor Myamba amesema kuwa katika filamu hiyo kuna sura mpya nyingi ambazo ni vipaji na zao kutoka Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM) ambapo wengi wao ni wanafunzi wanaosomea Shahada ya Kwanza ya Filamu,Na amefanya hivi kuonyesha na Kutambulisha vipaji ambavyo badi vipo Shuleni.

Alimalizia kwa Kusema kuwa Filamu hii sio ya Kukosa kwasababu humo ndani ni kuna vitu vipya ambavyo havijawahi kuonekana katika filamu za bongo, Kwahiyo Usikose nakala Yako

RICK ROSS KUCHANA SERENGETI FIESTA DAR OKT 6



Na Mwandishi Wetu, Dar
Msanii nyota kutoka nchini Marekani, mzaliwa wa nchini  Marekani, anayetambulika kwa jina la kisanii kama Rick Ross, ambaye kwa jina halisi anajulikana kama William Leonard Roberts II, anatarajia kutua nchini Tanzania hivi karibuni kwa ajili ya kushiriki kikamilifu kushambulia jukwaa la Serengeti Fiesta 2012, litakalofanyika Oktoba 6 ndani ya viwanja vya Lidaz Club,Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Katika kuhakikisha mambo yanakwenda sawa bin sawia kwa kila idara kuhusiana na tamasha hilo, waandaaji ambao ni Prime Time Promotions Ltd wakishirikiana na Clouds Media Group huku mdhamini wao mkubwa ikiwa ni kampuni ya bia ya Serengeti,wameandaa shamara shamra mbalimbali za kuhakikisha tamasha hilo mpaka linafika kileleni,linaamsha na kuacha gumzo la kipekee kabisa miongoni mwa wakazi wa jiji la Dar na vitongoji vyake, ikibidi mpaka Kigoma mwisho wa reli kwa namna moja ama nyingine.

Msanii huyo mwenye umahiri mkubwa wa kufloo awapo jukwaani mpaka sasa anatamba na nyimbo/albamu kadhaa kama vile  Hold Me Back 2012 God Forgives, I Don't, Hustlin' 2006 Port of Miami Diced Pineapples 2012 God Forgives, I Don't So Sophisticated 2012 God Forgives, I Don't 911 2012 God Forgives, I Don't Stay Schemin 2012 Rich Forever Aston Martin Music. 

Nyinginezo ni  2010 Teflon Don DJ Khaled 2008 Trilla Lemme See 2012 So Sophisticated Amsterdam 2012 God Forgives, I Don't Black Magic 2012 Maybach Music Group Presents Self Made, Vol. 2: The Untouchable Empire The Boss 2008 Trilla You the Boss 2011 You the Boss Touch'n You 2012 Touch'N You Bag of Money 2012 Maybach Music Group Presents Self Made, Vol. 2: The Untouchable

AZAM, JKT RUVU KUANZA KUONEKANA SUPER SPORT WEEKEND 


Mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kesho inaingia raundi ya nne, ambapo kwa mechi za Super Weekend ambazo zitakuwa zikionyeshwa moja kwa moja (live) na kituo cha televisheni cha SuperSport cha Afrika Kusini. 
Miongoni mwa mechi zitakazoonyeshwa na kituo hicho, mechi ya kwanza itakuwa ni kati ya Azam na JKT Ruvu Stars, itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ambayo itaanza saa 1 kamili usiku kwa viingilio vya sh. 3,000 mzunguko, sh. 5,000 kwa VIP C na VIP B wakati VIP A kiingilio kitakuwa ni sh. 10,000.
 
Jumamosi pia kutakuwa na mechi kati ya Simba na Tanzania Prisons, ambayo pia itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 11 kamili jioni na siku ya jumapili, Yanga na African Lyon zote za jijini Dar es Salaam, zitakutana katika uwanja huo huo kuanzia saa 11 kamili jioni.

Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam wenyewe utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar, mchezo utakaochezwa Oktoba 1, mwaka huu kuanza saa 10.30 jioni.
Na mechi ya mwisho ya Super Weekend itachezwa Oktoba 3 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikizikutanisha Yanga na Simba kuanzia saa 1 kamili usiku.

SHY-ROSE BHANJI APITISHWA CCM KUWANIA NEC- TZ BARA



Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Mh. Shy-Rose Bhanji amefanikiwa kuwa mmoja wa wagombea 10 waliopitishwa kati ya 31 na Kamati ya Halmashauri Kuu ya CCM-NEC kugombea Ujumbe wa Halmashauri kuu ya CCM NEC Tanzania bara. Katika kinyang'anyiro hicho Mh. Shy-Rose Bhanji anapambana na baadhi ya mawaziri na viongozi wa juu wa chama hicho.

MAMA AFRIKA SARAKASI YAFANA


... ilikuwa ni maajabu na kweli.
 
Kijana mwingine alionyesha umahili wake ni huyu kama vile unavyomuona.
Michezo ya kamba nayo ilikuwa ya kuvutia.
 Mchezo mwingine ulikuwa niwa kurushiana vikapu ya kutimia miguu.
 Vijana wakionyesha uhodari wao wa kupaa juu.
 
Vijana wakiaga mara baada ya onyesho kumalizika.

FAINALI ZA MICHUANO YA SAFARI POOL MWANZA YAFUNGULIWA 


Waamuzi wa mchezo wa Pool wakiongoza maandamano ya kuingia ukumbini wakati wa ufunguzi wa mashindano ya Safari Pool Taifa yaliyofunguliwa rasmi jana katika Hoteli ya Monarch jijini Mwanza na Mkuu wa Wilya ya Ilemela, Amina Masenza.

 Meneja wa Bia ya Safari Lager, Oscar Shelukindo akizungumza na wachezaji wa Pool (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa mashindano ya Safari Pool Taifa yaliyofunguliwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amina Masenza katika Hoteli ya Monarch jijini Mwanza
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amina Masenza (wapili kulia) akifungua rasmi mashindano ya Safari Pool Taifa .Kulia ni Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ilemela(OCD),Debora Magiligimba.Wengine kutoka kushoto ni Katibu wa chama cha Pool Mkoa wa Ilala, Mohamed Mwarabu, Mwenyekiti wa kamati ya mashindano, Haji Kapulila na Makamu mwenyekiti wa TAPA, Fred Mushi


Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amina Masenza akizungumza na wachezaji (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa mashindano ya Safari Pool Taifa katika Hoteli ya Monarch jijini Mwanza.Kushoto ni Meneja wa Bia ya Safari Lager, Oscar Shelukindo na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Pool Taifa, Fred Mushi.

BONDIA RAJABU MAOJA AELEKEA NAMIBIA


. Ataiwakilisha Tanzania kwenye programu ya “IBF Utalii wa Michezo” (IBF Sports Tourism)

. Anakutana na bingwa wa Namibia kwenye mpambano wa IBF Africa.


Mtanzania Rajabu mtoto wa Jumanne Maoja mkazi wa jiji la Tanga anaondoka na Shirika la Ndege la Afrika ya Kusini (South African Airways) kuelekea jijini Windhoek, Namibia ambako ana kibarua kikali kuiwakilisha Tanzania kwenye IBF Utalii wa Michezo (IBF Sports Tourism).

Maoja atakutana na bingwa wa nchi ya Namibia, Goettlieb Ndokosho kwenye mpambano uliopewa jina la “Vita Vya Jangwa la Kalahari” (The Battle for the Kalahari Desert) na waandaaji wa mpambano huo wa raundi 12 kumpata bingwa wa IBF Afrika katika uzito wa unyoya. Kinda Boxing Promotions inayoongozwa na bwana Simon Nangolo ambaye ni mkaguzi mwandamizi wa ndani wa mahesabu (Senior Internal Auditor) nchini Namibia ndio waandaaji wa mpambano huo wakukata na shoka.

Mshindi wa mpambano huo atakutana na bingwa wa IBF Afrika, Mashariki ya Kati, Ghuba ya Uarabu na Uajemi, Mtanzania Ramadhani Shauri ambaye hivi karibuni alimkung’uta bondia Sande Kizito wa Uganda katika mpambano ulioishia raundi ya 8 baada ya Kizito kushindwa kuendelea.

Huu unakuwa mpambano wa tatu kwa Watanzania mwaka huu kuwania ubingwa wa IBF katika bara la Afrika, Mashariki ya Kati ya Ghuba ya Uajemi ambako tayari mikanda miwili ya IBF iko Tanzania.

Mpambano wa Mtanzania Rajabu Jumanne Maoja na Goettlieb Ndokosho wa Namibia utafanyika katika jiji la Windhoek, mji mkuu wa nchi ya Namibia tarehe 29 Septemba siku ya Jumamosi.

Mtanzania Rajabu Jumanne Maoja atafuatana na Kocha wake Ibrahim Raphael Jorum ambaye naye anatoka katika jiji la Tanga.

Msimamizi mkuu wa mpambano huo ni Mtanzania Onesmo Alfred McBride Ngowi ambaye atalisimamia pambano hilo lililo na upinzania mkubwa!

Mungu mbariki Rajabu Jumanne Maoja, Mungu ibariki nchi nzuri ya Tanzania.

Imetolewa na:
Utawala
KAMISHENI YA NGUMI ZA KULIPWA NCHINI (TPBC)

ESTHER BULAYA AKIKABIDHI JEZI ZA MPIRA KWA VIJANA



 Mbunge wa viti maalumu kundi la vijana mkoa wa Mara, Ester Bulaya akikabidhi jezi na mpira kwa wenyeviti na makatibu wa vijana wa CCM wilaya ya Butiama kwenye hafra fupi iliyofanyika kwenye ukumbi wa Chama cha Mapinduzi mjini Musoma. (Picha na Berensi Alikadi)

Jeshi Stars yaivua Magereza ubingwa wa Wavu


MABINGWA mara tatu mfululizo wa michuano ya wavu ya wanawake, Magereza, wamevuliwa ubingwa huo na maafande wenzao wa Jeshi Stars baada ya kubwagwa kwa seti 3-1 katika mechi ya fainali iliyopigwa kwenye viwanja vya Bwalo la Umwema mjini Morogoro.
Kwa upande wa wanaume, timu ya Magereza ilitetea vyema taji lao baada ya kuwachapa Jeshi Stars kwa seti 3-0 katika mechi nyingine ya fainali iliyochezwa jana.
Nahodha wa Jeshi Stars (Wanawake), Zainab Thabit alisema timu yake imetwaa ubingwa huo kutokana na ujasiri wa kupambana hadi mwisho waliouonyesha dhidi ya mabingwa hao wa muda mrefu huku Ester Noel wa Magereza akiahidi kwamba mwakani watajifua zaidi kuhakikisha wanarejesha taji walilopoteza.
Mgeni rasmi katika fainali hizo, Katibu Mkuu Msaidizi wa Baraza la Michezo Taifa (BMT), Mohamed Kiganja, alisema mwamko wa baadhi ya michezo kama wavu umeendelea kuwa ni mdogo kwa kukosa ufadhili na ndio sababu mikoa mingi imeshindwa kuleta timu.
Aidha, Kiganja alilaumu baadhi ya viongozi kuua michezo kwa kugombea nyadhifa kwenye vyama vya michezo kwa matarajio fulani ambayo wakiyakosa huvitelekeza.
Alishauri zifanyike juhudi za kuibua vipaji vipya kwa kuweka nguvu kwenye ngazi ya shule badala ya kuendelea kutumia wachezaji walioibuliwa zamani kwenye michuano ya Umoja wa Michezo kwa Shule za Msingi (UMISHUMTA), ambao wameendelea kuliwakilisha taifa.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Wavu Tanzania, Muarami Msumi, alitaka serikali kupitia kitengo chake cha uwekezaji kuhakikisha wawekezaji wanapewa masharti ya kujenga viwanja vya michezo kama sehemu ya uwekezaji, sambamba na kuendelea kujenga na kuimarisha viwanja vya michezo kuanzia ngazi za shule za awali.
Timu 11 zikiwamo tatu za wanawake zilishiriki michuano hiyo.

AZAM KUIENGUA SIMBA KILELENI LEO?

Kikosi cha Azam kitakachopambana na JKT Ruvu leo usiku

TATIZO la majeruhi limeendelea kuikumba timu ngumu ya JKT Ruvu baada ya nyota wake Credo Mwaipopo, Damas Makwaya na George Minja kuondolewa katika kikosi kitakachoshuka dimbani leo kuivaa Azam katika mechi yao ya Ligi Kuu ya Bara itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 1:00 usiku na kuonyeshwa ‘live’ kupitia kituo cha televbisheni cha Super Sport.
Azam inasaka pointi tatu zaidi leo kuwapiku vinara Simba na kukwea kileleni mwa msimamo wa Ligi kuu ya Bara.
Akizungumza na NIPASHE jana, kocha wa JKT Ruvu, Charles Kilinda, alisema kuwa Makwaya ataikosa mechi ya leo kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya misuli, Minja jeraha la goti na mwaipopo atakuwa nje akiuguza maumivu ya jeraha paja.
Kilinda amesema kuwa anasikitika kuwakosa wachezaji hao, lakini hana hofu kwa vile ana wachezaji wengine wazuri wa kuziba nafasi zao, wakiwamo Ramadhan Kauogo na Dumba Ramadhan.
"Pamoja na kuwakosa majeruhi hao, bado kikosi changu kina ari kubwa ya kuibuka na ushindi," alisema Kilinda.
Hata hivyo, Kilinda alilalamikia ratiba ya ligi kwa kusema kwamba imewabana mno kwani  wamejikuta wakicheza mechi tatu mfululizo dhidi ya timu tatu zilizokamata nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi msimu uliopita,  ambazo ni Simba, Azam na Yanga.
Katika mechi mbili zilizopita kabla ya leo, JKT Ruvu walicheza dhidi ya Simba na kuchapwa 2-0 na kasha wakafungwa tena 4-1 katika mechi iliyopita dhidi ya Yanga.
Endapo Azam itashinda, itakwea kileleni kwenye msimamo wa ligi kwani itafikisha pointi 10, moja zaidi ya vinara wa sasa, Simba.
Coastal Union ya jijini Tanga iliyoshinda nyumbani 3-2 katika mechi yao ya juzi dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani ilikwea hadi katika nafasi ya pili baada ya kufikisha pointi nane.
Ligi hiyo inayoshirikisha timu 14, itaendelea pia kesho wakati Simba itakapocheza dhidi ya Prisons ya Mbeya kwenye uwanja huo huo wa Taifa kuanzia saa 11:00 jioni huku Yanga na African Lyon wakivaana keshokutwa Jumapili, pia kwenye Uwanja wa Taifa.
Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam utachezewa mechi kati ya Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar itakayochezwa Oktoba 1 kuanza saa 10.30 jioni na mechi ya mwisho ya 'Super Weekend' itachezwa Oktoba 3 kwenye Uwanja wa Taifa na kuwakutanisha mahasimu wa jadi, Yanga na Simba kuanzia saa 1:00 usiku.
Wakati huo huo, Shirikisho la Soka Nchini (TFF) limesikitishwa na taarifa za kifo cha Katibu Mkuu mstaafu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Erasto Zambi kilichotokea Septemba 26 jijini Dar es Salaam kutokana na maradhi.
Zambi ambaye anatarajiwa kuzikwa keshokutwa Jumapili, kabla ya kuwa kiongozi TOC, kwa muda mrefu alikuwa mwalimu wa michezo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambapo wanamichezo wengi hasa waliokuwa wanafunzi katika chuo hicho wamepita mikononi mwake.

Kikosi cha JKT Ruvu kikiwa mazoezini


CHANZO:NIPASHE

RAIS TFF AFAANUA SUALA LA UDHAMINI WA LIGI KUU TANZANIA BARA


RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodgar Tenga ameingilia kati msuguano unaoendelea kati ya klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara na mdhamini mkuu wa ligi hiyo, kampuni ya huduma za simu ya Vodacom kuhusiana na kuwapo kwa kipengele cha upekee katika mkataba wa udhamini wa ligi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya TFF jijini Dar es Salaam jana, rais huyo alizionya klabu zinazokiuka makubaliano yaliyomo kwenye mkataba huo na kwamba klabu zitakazoendelea kufanya hivyo zitachukuliwa hatua.
“Tunashukuru kupata mkataba ambao ni mara mbili ya ilivyokuwa awali. Mkataba huu lazima ulindwe na uheshimiwe. Yeyote atayekiuka, atachukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu,” alisema Tenga.
Tenga aliyasema hayo wakati mazungumzo kati ya klabu na mdhamini yakiendelea pia jijini Dar es Salaam jana.
Klabu zinalamikia kuwapo kwa vipengele kadhaa katika mkataba huo, vikiwamo vya posho za wachezaji, usafiri na kipengele cha upekee ambacho kinazuia timu kuvaa jezi au kubandika nembo za wapinzani wa kampuni hiyo kibiashara (makampuni ya huduma za simu).
Tenga alisema kuwa kuwapo kwa kipengele cha upekee lazima kiheshimiwe si wakati wa mechi tu, bali hata wakati wa mazoezi ya timu zote 14 zinazoshiriki ligi hiyo kwa kuwa kampuni hiyo ina haki ya matangazo hadi kwenye viwanja vya mazoezi vya timu hizo.
“Klabu zote zinazoshiri Ligi Kuu lazima zielewe hilo. Hata kwenye viwanja vyao vya mazoezi hawaruhusiwi kuvaa jezi au kubandika mabango ya wapinzani wa Vodacom, maana tulikubaliana hivyo na kampuni hiyo kabla ya kusaini mkataba huu,” alisema.
“African Lyon hawakuelewa vizuri vipengele vilivyomo kwenye mkataba huo ndiyo maana tulizungumza nao baada ya kutokea kwa tukio la timu yao kuingia na jezi zenye nembo ya Zantel wakati wa mechi ya Ligi Kuu.
Alidai kuwa mdhamini mkuu wa Ligi ya England ni benki ya Barclays, lakini Liverpool wanavaa jezi zenye nembo ya wadhamini wao ambao ni benki ya Standard Chartered kwa vile benki hizo mbili si wapinzani kibiashara maana kila moja ina aina yake ya wateja.
Alisema kuwa shirikisho hilo liliamua kuondoa kipengele cha upekee katika udhamini kama ilivyokuwa kwenye mkataba wa miaka mitano wa kampuni hiyo uliomalizika mwishoni mwa mwezi uliopita, lakini kipengele hicho kimebaki kwenye bidhaa miongoni mwa wadhamini.
Aidha, Tenga alisema kuwa baadhi ya klabu zinazoshiriki ligi hiyo zinadaiwa kiasi kikubwa cha pesa na shirikisho hilo na kwamba pesa zote zitakazotolewa na wadhamini zitaingizwa kwenye akaunti maalum itakayokuwa chini ya Kamati ya Ligi ya TFF kabla ya kusambazwa kwa klabu husika.
“Klabu zimechelewa kupata fedha kutoka kwa mdhamini mkuu kwa sababu mkataba ulichelewa kusainiwa. Ni kweli kwamba baadhi ya klabu zinadai pesa ya msimu uliopita, lakini klabu nyingi hasa zile kubwa tunazidai kiasi kikubwa sana cha pesa. Safari hii tumefungua akaunti maalum ambapo pesa za wadhamini zitawekwa kabla ya kupelekwa kwa wahusika. Wale wanaodai watalipwa na wale tunaowadai tutakata pesa yetu kwanza kabla ya kuwapatia fungu lao,” alisema.
Alizitaja klabu zinazodaiwa na shirikisho hilo kuwa ni pamoja na Simba, Yanga na Tanzania Prisons na kwamba madeni hayo yalitokana na TFF kuzilipia faini katika nyakati tofauti kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), lakini alikataa kutaja kiasi hicho wanachozidai klabu.
Klabu zimekuwa katika mgongano na wadhamini kwa kudai kwamba kiasi wanachotoa cha Sh. bilioni 1.7 kwa mwaka ni kidogo mno kulinganisha na gharama za uendeshaji na kwamba, ili kipengele cha upekee kiendelee kuwapo, ni lazima waongeze fedha hizo na baadhi wamekaririwa wakitaka walau udhamini huo uwe wa Sh. bilioni 4 kwa mwaka.
Wakati ligi kuu ya Bara yenye timu 14 na kuhusisha mechi zaidi ya 180 kwa msimu ikidhaminiwa kwa Sh. bilioni 1.7, timu ya taifa pekee (Taifa Stars) hudhaminiwa na Kampuni ya Bia (TBL) kwa dau la zaidi ya Sh. bilioni 3.5 kwa msimu, bila kujali kwamba mechi zake huwa hazizidi 20 kwa mwaka.

TWIGA STARS
Katika hatua nyingine, Tenga pia aliomba wadhamini wajitokeze kuzisaidia timu za taifa za vijana na timu ya taifa ya wanawake (Twiga Stars) kwa kuwa zina hali mbaya kifedha.
“Tunatumia fedha nyingi sana kuiendesha timu ya Twiga Stars. Kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu, tumetumia Sh. milioni 222 kuihudumi timu hiyo wakati wa kambi na mechi ndani na nje ya nchi,” alisema Tenga.
Tenga, ambaye pia ni Rais wa Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), aliushukuru uongozi wa kituo cha televisheni cha Super Sport cha Afrika Kusini kwa kuamua kuonesha baadhi ya mechi za Ligi Kuu msimu huu.

FA YAMFUNGIA NA KUMPIGA FAINI JOHN TERRY KWA UBAGUZI



John Terry na Anton Ferdinand wakigombana katika tukio linalodaiwa Terry kumbagua Ferdinand
Terry akiwasili mahakamani kutoa ushahidi wa tuhuma hizo na kisha kukutwa hana hatia
LONDON, England
Katika sakata hilo ambalo lilifikishwa mahakamani na Terry kukutwa hana hatia, nahodha huyo wa zamani wa England anadaiwa kumbagua beki wa klabu ya QPR, Anton Ferdinand
HATIMAYE Chama cha Soka cha England (FA), leo kimefikisha tamati sakata la ubaguzi wa rangi lililokuwa likimkabili beki na nahodha wa Chelsea, John Terry na kutoa huku iliyotabiriwa na mtuhumiwa huyo mapema wiki hii.
Katika hukumu yake iliyotoka jana, iliyokuja baada ya mfululizo wa siku nne za kuhojiwa kwa nyota huyo na wakili wake kutoa ushahidi wa kumtetea, FA imemfungia nyota huyo mechi nne na faini ya pauni 220,000.
Katika sakata hilo ambalo lilifikishwa mahakamani na Terry kukutwa hana hatia, nahodha huyo wa zamani wa England anadaiwa kumtolea lugha za kibaguzi beki wa kimataifa wa England anayechezea klabu ya Queens Park Rangers, Anton Ferdinand.
Terry tayari alishakana kuhusika na tuhuma hizo anazodaiwa kuzitoa Oktoba mwaka jana wakati wa mechi baina ya Chelsea na QPR na kusema kuwa, FA inajaribu kukwepa ukweli uliomuacha huru kwenye Mahakama ya Westminster Magistrates.
Kutokana na kuhisi kuonewa na kutambua kama FA ilipanga kumhukumu isivyo, Terry mapema wiki hii alitangaza kustaafu kuichezea timu ya taifa ya England, kama sehemu ya kutoa hisia zake kuwa FA kwamba haimtendei haki katika sakata hilo.
Akitangaza uamuzi wa kustaafu soka la kimataifa, Terry, 31, alisema: “Natangaza rasmi leo kuwa nastaafu soka la kimataifa. Napenda kutoa shukrani kwa makocha wote wa England walionichagua mimi kuwamo dimbani na timu hiyo mara 78.
“Nimefanya maamuzi haya mapema kabla hata ya kusikia nini kitaamuliwa juu yangu kwa tuhuma zinazonikabili kwa sababu nahisi FA, imepanga hukumu isiyo ya haki dhidi yangu, licha uamuzi mzuri wa mahakama ulionisafisha na tuhuma hizo.”

Thursday, September 27, 2012

Cheka, Nyilawila kupimwa afya uzito kesho, kuvaana PTA J'mosi

Karama Nyilawila (kushoto) na Francis Cheka wanaotarajia kupima uzito na afya kesho kabla ya kuvaana katika pambano lao lwa kuwania ubingwa wa Mabara wa UBO litakalofanyika siku ya Jumamosi ukumbi wa PTA.

BINGWA wa ngumi za kulipwa anayetambuliwa na  ICB na IBF-Afrika, Francis Cheka na aliyekuwa bingwa wa Dunia wa WBF, Karama Nyilawila wanatarajia kupima uzito na afya zao kesho tayari kwa pambano lao la Jumamosi kuwania ubingwa wa UBO-Mabara.
Mabondia hao wanatarajiwa kupambana katika pambano la uzani wa Super Middle la raundi 12 kwenye ukumbi wa PTA, jijini Dar es Salaam siku ya Jumamosi.
Mratibu wa pambano hilo, Robert Ekerege wa Afrika Kabisa Entertainment, alisema Cheka na Nyilawila watapimwa uzito na afya zao sambamba na mabondia wengine watakaowasindikiza kwenye pambano lao kwenye ukumbi wa Mawela jijini Dar.
Ekerege, alisema kupimwa kwa afya na uzito wa mabondia hao ni kuashiria kuiva kwa pambano hilo la kimataifa litakalochezewa na mwamuzi toka Malawi.
"Tunatarajia kuwapima afya na uzito wao mabondia wote watakaopigana Jumamosi, karibu mabondia wote wameshatua Dar tayari kwa zoezi hilo litakaloanza kufanyika saa 5 asubuhi ili kujiweka tayari kwa mchezo huo utakaofanyika PTA," alisema.
Aliongeza kuwa, maandalizi ya ujumla wa pambano hilo la Cheka na Nyilawila ambalo ni la tatu kwao kukutana na yale ya utangulizi yamekamilika ikiwemo kubadilisha mgeni rasmi wa siku hiyo kutoka Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo , Amos Makalla hadi kuwa Kamanda wa Kanda Maalum Dar, Afande Suleiman Kova.
Ekerege alisema wamemkosa Waziri Makalla waliokuwa wamempanga awali kwa vile atakuwa safarini na hivyo kumpa jukumu la kumvika mshindi wa pambano hilo la kesho Mlezi wa mchezo wa ngumi nchini, Kamanda Kova aliyethibitisha kushiriki.
Aliongeza kuwa katika mapambano hayo bendi maarufu ya Mashukaa Band 'Wana Kibega' ndio watakaotoa burudani ukumbini.

Mwisho

Arsenal, Man Utd, Liverpool zang'ara Kombe la Ligi

Mchezaji Ignasi Miquel akishangilia bao lake dhidi ya Coventry City
VIGOGO vya Ligi Kuu wa England, Arsenal, Manchester United, Liverpool na Tottenham Hotspurs usiku wa kuamkia zimefanya vema katika michuano ya Kombe la Ligi baada ya kutoa vipigo kwa wapinzani wao na kuvuka raundi nyingine.
Arsenal iliisasambua  Coventry City kwa mabao 6-1 kwenye pambano lililochezwa uwanja wa Emirates mjini London, wakati mahasimu wao Tottenham walipata ushindi wa magoli 3-0 dhidi ya Carlisle United ikiwa ugenini.
Manchester United wenyewe walipata ushindi wa mabao 2-1 wakiwa uwanja wa Old Trafford dhidi ya Newcastle United, wakati Liverpool ilitoka kupokea kichapo katika Ligi Kuu toka kwa wapinzani wao wa jadi Man United iliitafuna West Bromwich Albion kwa idadi kama hiyo ya mabao 2-1.
Mechi nyingine zilizochezwa jana WPR ilijikuta ikinyukwa nyumbani na Readind kwa mabao 3-2 na Norwich City iliilaza kwa bao 1-0 timu ya Doncaster Rovers.
Matokeo kamili ya mechi za michuano hiyo kwa siku ya jana ni kama ifuatavyo:
Norwich City 1-0 Doncaster Rovers
QPR 2-3 Reading
Arsenal 6-1 Coventry City
Celtic 2-1 Benfica
Manchester United 2-2 Newcastle
Carlisle United 0-3 Tottenham
West Brom 1-2 Liverpool
More: Scores | Fixtures | League Cup
 

Coastal yatakata Mkwakwani, Toto ikiendeleza mdudu wa sare

 MABAO mawili toka kwa mshambuliaji nyota na mzoefu, Nsa Job na jingine la Daniel Lyanga jana yaliipaisha timu ya Coastal Union hadi nafasi ya pili mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuilaza Kagera Sugar goli 3-2.
Coastal  ilipata ushindi huo katika pambano lililochezwa kwenye uwanja wa Mkwakwani Tanga ikiwa chini ya kocha wao wa makipa, Juma Pondamali na kulingana kila kitu na Azam waliokuwa wakiishikilia nafasi hiyo.
Huo ni ushindi wa pili kw atimu hiyo baada ya awali kufanya hivyo katika mechi ya fungua dimba la Ligi Kuu dhidi ya 'majirani' Mgambo Shooting kabla ya kutoka sare mbechi nyingine mbili.
Katika mfululizo wa ligi hiyo timu ya Toto Africans ya Mwanza imeendelea na mdudu wake wa sare baada ya jana kutoka suluhu ya bila kufungana na wenyeji wao Polisi Morogoro.
Hiyo ni sare ya nne kwa Toto Africans baada ya awali kufanya hivyo dhidi ya JKT Oljoro ilitoka sare ya 1-1, Azam 2-2 na kisha Mgambo Shooting mechi yao iliyopita.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea mwishoni mwa wiki kwa michezo kadhaa itakazozihusisha timu za Azam, Yanga na Simba ambazo kwa sasa zinawindana kwa ajili ya pambano lao litakalofanyika Jumatano ijayo jijini Dar. 

Wednesday, September 26, 2012

SHINDALO LA UCHORAJI KWA TAASISI ZA KIELIMU


Shindalo la Uchoraji Kwa Taasisi za Kielimu
Image Profession ikishirikiana na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) kwa mara nyingine inatangaza kuanza kwa muhula mpya wa pili wa Shindano ya Uchoraji maalumu kwa Taasisi za elimu.
Shindano ambalo pia linajulikana Kama: Educational Drawing Competition au Image Profession Educational Drawing Competition, lina malengo ya kuibua vipaji katika fani ya uchoraji kwa kuzingatia uwekezaji kwa watoto na vijana.
Theme/Wazo kuu la mwaka huu: ART IMITATES LIFE au SANAA HUFUATISHA MAISHA
Makundi ya ushiriki
´ Chekechea,
´ Elimu ya Msingi,
´ Elimu ya Sekondari na  
´ Elimu  ya Juu
Kwa maelezo na taratibu za Shindano tembelea Facebook Page/Group “Tanzania Drawing Competition” au wasiliana na BASATA au
DRAWING COMPETITION – IMAGE PROFESSION,
P O BOX 92 DAR ES SALAAM.
SIMU: +255 222 664 740 / +255 713 484 040
/ +255 714 676 217 / +255 716 430 084
EMAIL: info@imageprofession.com

Kamanda Kova ambadili Waziri Makalla pambano la Cheka, Nyilawila

Kamanda Kova
KAMANDA wa Polisi Kanda Maalum ya Mkoa wa Dar es Salaam, Suleiman Kova, amembadili Naibu waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Amos Makalla katika kuwa mgeni rasmi wa pambano la kimataifa la kuwania ubingwa wa UBO, kati ya Francis Cheka na Karama Nyilawila.
Mratibu wa pambano hilo litakalofanyika siku ya Jumamosi kwenye ukumbi wa PTA, jijini Dar es Salaam, Robert Ekerege aliiambia MICHARAZO kuwa, kumekuwa na mabadiliko ya mgeni rasmi badala ya Waziri Makalla sasa atakuwa Kova ambaye ni mlezi wa ngumi Tanzania.
Ekerege alisema Kova amechukua nafasi ya Makalla kutokana na waziri huyo kupangiwa safari nje ya nchi ambayo itafanyika wakati pambano la Cheka na Nyilawila likifanyika PTA.
Mratibu huyo alisema kutokana na udhuru huo wameona ni vema nafasi hiyo achukue mlezi wao wa ngumi, Kamanda KOva ambaye ameshaitikia wito huo wa kuwa mgeni rasmi ambapo ndiye atakayemvisha mkanda mshindi wa pambano hilo la uzani wa Supermiddle la raundi 12 litakalochezwa na mwamuzi toka Malawi.
"Kwa sababu zilizo nje ya uwezo wetu, tumeamua kubadili mgeni rasmi wa pambano la jumamosi badala ya kuwa Waziri Makalla sasa ni Kamanda wa Kanda Maalum ya Mkoa wa Dar es Salaam, Suleiman Kova, Waziri atakuwa safarini na hivyo hataweza kuhudhuria kama tulivyotangaza awali," alisema Ekerege.
Aliongeza, ugeni wa Kova katika pambano lao limewaongezea uhakika wa ulinzi wa kutosha siku ya mchezo huo ambao unawakutanisha Cheka na Nyilawila kwa mara ya tatu katika safari yao ya ngumi baina yao.
Ekerege alisema maandalizi mengine yanaendelea kama kawaida ambapo mabondia wote watakaopanda ulingoni wanatarajiwa kupima afya na uzito wao kesho kwenye ukumbi huo tayari kwa pambano la Jumamosi ambalo linadhaminiwa na kinywaji cha Coca Cola na kondomu za Dume na litapambwa na burudani toka kwa Mashujaa Band waliopania kuwachezesha wapenzi wa ngumi mtindo wao wa 'Kibega'.


Manchester City hoi Kombe la Ligi, Chelsea yaua

Wachezaji wa Man City wakiwa hoi baada ya kujifunga moja ya mabao yaliyoizamisha jana mbele ya Aston Villa

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya England, Manchester City, imeanza vibaya msimu kwa kung'olewa   mapema kwenye michuano ya Kombe la Ligi baada ya kulazwa mabao 4-2 na Aston Villa, huku vinara wa ligi hiyo ya England, Chelsea ikitoa kichapo cha  mabao 6-0 kwa 'Mbweha'.
Kipigo hicho toka kwa Aston Villa, kimempa wakati mgumu kocha wa Man City, Roberto Mancini, kwani ni dalili za kushindwa kurejea mafanikio iliyopata msimu uliopita ilipotwaa taji la Ligi Kuu baada ya miaka 50.
Matokeo mengine ya mechi za jana za michuano hiyo ya Kombe la Ligi ni kama ifuatavyo;
Bradford iliinyuka Burton Abilion mabao 3-2 katika muda wa nyongeza, Chelsea  ilivuna ushindi wa mabao 6-0 kw Wolves, Crawley ilinyukwa mabao 3-2 na Swansea, Leeds United ikainyoa Everton magoli 2-1.


Wachezaji wa Chelsea wakishangilia moja ya mabao yao katika mechi ya Kombe la Ligi jana usiku
Mechi nyingine Manchester City vs Aston Villa baada ya muda wa nyongeza 2-4,MK Dons ikalala mabao 2-0 kwa Sunderland, Preston iliangukia pua mbele ya Middlesbrough kwa kichapo cha mabao 3-1 na Southmpton ilivuna ushindi wa mabao 2-0 kwa Sheffied Wed, Swindon iliinyuka Burnley 3-1 na wagonga nyundo wa West Ham wakalala mabao 4-1 kwa Wigan.

Mgunda afuata nyayo za Saintfiet atimuliwa Coastal Union

Hemed Suleiman 'Morocco' (kushoto) aliyetua Coastal Union
SIKU chake tangu klabu ya Yanga kumtimua kazi aliyekuwa kocha wake mkuu, Tom Saintfiet kutoka Ubelgoji, uongozi wa Coastal Union ya jijini Tanga umemtangaza, Hemed Suleiman 'Morocco' kuwa kocha mpya akichukua nafasi ya aliyekuwa kocha wao, Juma Mgunda.
Morocco, aliyekuwa akiinoa timu ya taifa ya Zanzibar, anatarajiwa kuiangalia Coastal ikicheza pambano  lao dhidi ya Kagera Sugar litakalofanyika kwenye uwanja wa Mkwakwani, chini ya kocha wa makipa, Juma Pondamali aliyekuwa ameachiwa timu baada ya Mgunda na msaidizi wake, Habib Kondo kutimuliwa.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jijini, uongozi wa Coastal ulifikia maamuzi hayo katika kikao kilichofanyika jana asubuhi na kwamba wamewatimua kufuatia kutoridhishwa na kiwango cha wachezaji wa timu hiyo licha ya kutofungwa mechi.
"Tayari wameshajulishwa maamuzi haya na Morocco atakuwa jukwaani kesho na ndiye atakayeongoza jahazi," alisema kiongozi mmoja wa juu wa timu hiyo.
Chanzo hicho kilisema kuwa katika mchezo wa leo, kocha wa makipa, Juma Pondamali ndiye atakayeiongoza timu hiyo na wanaamini mabadiliko yatazaa matunda.
Mgunda mwenyewe alinukuliwa jana akidai kuwa ameamua kujiondoa Coastal kwa nia njema na mapenzi mkubwa aliyonayo kwa timu hiyo aliyowahi kuichezea kwa mafanikio enzi zake za uchezaji.
Mgunda alisema aliona ni bora ajiondoe kutokana na shinikizo kubwa lililopo ndani ya Coastal ambayo imejiwekea malengo makubwa katika msimu huu wa ligi na kuwataka mashabiki na viongozi wa timu hiyo kumheshimu na kuyaheshimu maamuzi yake yaliyokuja wakati Coastal ikiwa nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi kutokana na kushinda mechi moja na kupata sare mechi mbili.

Simba yaenda Zenji kuiwinda Yanga, Jangwani wakimbilia Bagamoyo








MABINGWA watetezi wa soka nchini Simba imeondoka jijini jana kuelekea Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi ya kujiwinda na pambano lao na watani zao Yanga litakalochezwa Jumatano ijayo.
Timu hizo mbili zinatarajiwa kukutana katika pambano la kwanza kwa msimu huu litakalochezwa kwenye uwanja wa Taifa na kurushwa 'live' na kituo cha Super Sport, huku Yanga ikiwa na deni kubwa la kipigo cha mabao 5-0 iliyopata katika pambano baiona yao lililofungia msimu uliopita.
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu', alinukuliwa jana kuwa wachezaji wote 29 wa timu hiyo wameondoka na wanatarajia kurejea keshokutwa kwa ajili ya kuvaana na Prisons ya Mbeya kabla ya kurejea tena visiwani humo kuweka kambi hadi siku ya mchezo wao na Yanga.
Alisema kuwa wakiwa Zanzibar wataendelea kufanya mazoezi ya ufukweni na ya uwanjani na wanaamini kambi yao itazaa mafanikio kwa kushinda mechi hizo zinazowakabili.


Wakati Simba ikienda kujichimbia Zenji, watani zao walikuwa katika mchakato wa kuelekea mjii Bagamoyo kwa ajili ya kujiandaa na pambano hilo la watani zao na lile la Jumamosi ijayo itakapoumana na African Lyon.


Yanga imepania kulipa kisasi cha mabao hayo 5-0 iliyofungwa na Simba Mei 6, lakini pia wakiwa na deni la miaka zaidi ya 30 ya kipigo cha mabao 6-0 ilichopewa na Simba mwaka 1977.



YANGA HATARINI KUSHUSHWA DARAJA - MADENI YA PAPIC NA NJOROGE YAWAPONZA FIFA

Kikosi cha Yanga kilichopo hatarini kiushushwa daraja
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Oseah


Tumepokea barua kutoka Kitengo cha Sheria cha Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpirawa Miguu (FIFA) likitutaka tuitaarifu Yanga kuhusu mashtaka yaliyowasilishwa na kocha wazamani wa klabu ya Yanga, Kostadin Papic. Katika malalamiko yake, Papic anadai kuwa hajalipwa malimbikizo ya mshahara wake yanayofikia kiasi cha Dola 12,300 za Kimarekani. Katika barua yake, kocha huyo anadai kuwa alikuwa akiwasiliana na maofisa na viongozi wa Yanga, lakini hakupata ushirikiano na hivyo kuamua kwenda FIFA. TFF ilifanya juhudi za kuwasiliana na Yanga kuhusu malalamiko hayo ili kujaribu kumzuia kocha huyo asishtaki FIFA, lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda.
Kama chombo kinachosimamia uendeshaji wa mpira wa miguu nchini, TFF imesikitishwa na habari hizo na inaiomba klabu ya Yanga kufanya kila jitihada kuhakikisha kuwa inawasilisha taarifa zote muhimu na nyaraka zinazohusiana na stahiki za kocha huyo ili kama ilishamalizana naye, sifa ya klabu ya Yanga isafishwe. Tayari barua imeshaandikwa kwa klabu ya Yanga kuitaka itekeleze utashi huo mapema iwezekanavyo.
Tukio hilo, si tu linachafua sifa ya klabu ya Yanga, bali soka ya Tanzania kwa ujumla kutokana na ukweli kwamba ikishadhihirika kuwa kuna tatizo la malipo ya makocha nchini, ni dhahiri kuwa itakuwa ni vigumu kwa klabu zetu na hata timu za taifa kupata makocha wazuri kutoka nje kwa kuwa watakuwa wamejengeka hofu ya kufanya kazi nchini.
Hili ni tukio la pili kwa Yanga baada ya mchezaji wake mwingine, John Njoroge kuishtaki klabu hiyo FIFA na kushinda kesi yake iliyoamuliwa mwezi Januari na Kitengo cha Usuluhishi wa Migogoro cha FIFA (DRC). Ushindi wa Njoroge unamaanisha kuwa iwapo Yanga itashindwa kutekeleza kumlipa mchezaji huyo kasi cha Sh milioni 17, inaweza kujikuta katika adhabu ambayo itatulazimisha tuishushe daraja; kuinyang’anya pointi kwa kiwango kitakachotajwa na FIFA; kuipiga faini au adhabu zote kwenda kwa pamoja. Tunaiomba Yanga itekeleze hukumu hiyo kwa wakati uliotajwa kwenye barua ya FIFA ili kuepuka hatua hizo.
Suala la Njoroge ni moja kati ya matukio mengi yanayohusu ukiukwaji wa taratibu za kuvunja mikataba yanayofanywa na klabu zetu. Kuna malalamiko ya wachezaji wengi dhidi ya klabu zao za zamani kuhusu kutolipwa stahiki zao. Hivyo TFF inatoa wito kwa klabu kujiepusha na vitendo hivyo kwa kuwa vinawanyima haki wachezaji, lakini pia vinachafua sifa ya nchi iwapo wachezaji wanachukua hatua za kwenda kwenye vyombo vya juu.
Tumekuwa tukisoma kwenye vyombo vya habari kuhusu kutimuliwa kwa sekretarieti nzima ya Yanga kutokana na kuonekana kuwa ina udhaifu. Taarifa hizo hazijaifikia rasmi TFF. Kiutaratibu, Yanga inatakiwa iwsasilishe majina ya maofisa watakaofanya kazi na TFF kwa sasa na itakapoajiri sekretarieti ya kudumu, basi itume barua nyingine ya kuwatambulisha watendaji wake.
Kama itakuwa imeitimua sekretarieti nzima, basi TFF inapokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa. Si nia ya TFF kutetea watendaji wazembe, lakini klabu hazina budi kufuatilia kwa karibu utendaji wa sekretarieti zao ili isije ikafikia wakati sekretarieti nzima inaondolewa kwa makosa ambayo yangeweza kusahihishwa kama kungekuwa na ufuatiliaji wa karibu. TFF imekuwa ikitoa mafunzo kwa watendaji wa klabu ili waweze kufanya kazi zao vizuri na kwa mintaarafu ya mpira wa miguu na hivyo kuondolewa kwa timu nzima kama hiyo kunamaanisha kuwa ni upotevu wa rasilimali ambayo imetumika kuwapa elimu ya kutenda kazi zao vizuri. TFF ilishafanya kozi ya Event Management kwa ajili ya watendaji wa klabu; semina ya kuangalia upya maazimio ya Bagamoyo kwa watendaji na viongozi na pia kozi ya utawala hivyo haipendi juhudi hizi zipotee kirahisi.
Angetile Osiah
KATIBU MKUU