STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, January 9, 2013

Chipolopolo aanza kusuka kundi lake

Chipolopolo katika pozi

MUIMBAJI wa zamani wa kundi la King's Modern Taarab, Mwanahawa Ally 'Mwanahawa Chipolopolo', ameanza kulisuka kundi lake la miondoko hiyo aliloliunda hivi karibuni baada ya kupata mfadhili aliyempa vyombo vya muziki.
Pia msanii huyo amekanusha kumnyakua wasanii waliodaiwa kujiengua katika kundi lake la zamani wa King's Modern, kwa kile alichodai hataki ugomvi na 'bosi' wake wa zamani wala kutaka wasanii wenye majina makubwa.
Akizungumza na MICHARAZO jana, alisema kundi lake linaloendelea kujifua kabla ya kutoa burudani, linaundwa na wasanii kadhaa wasio na majina makubwa lakini wenye vipaji vya hali ya juu katika muziki.
Msanii huyo aliwataja baadhi ya wasanii wanaounda kundi lake hilo lenye maskani yake Keko kuwa ni Haruna Hassani 'Bonge la Bwana', Kuruthumu Akida, Mwajuma Abdalla na Rehema 'Mtu Mzima Dawa ambao ni waimbaji.
Msanii huyo aliongeza hata taarifa kwamba wamewanyakua baadhi ya wasanii wenzake wa zamani wa Kings Modern waliodaiwa kulihama kundi hilo, sio za kweli kwa sababu hana mpango wa kunyakua msanii yeyote mwenye jina kubwa.
"Hakuna msanii hata mmoja mwenye jina aliyetua kwangu, wala sijamnyakua msanii aliyetoka Kings Modern au kokote kule kunakotajwa kuna wasanii wakali," alisema.






Dogo Muu ‘Siwezi Kushukuru’

Dogo Muu (kulia) akiwa na Dogo Aslay


MSANII chipukizi kutoka kituo cha Mkubwa na Wanae, Muharami Kajonjo 'Dogo Muu' anatarajiwa kuachia kazi mbili tofauti, moja ikiwa 'audio' ya wimbo wake mpya wa 'Nashukuru' na video ya kibao chake kiitwacho 'Siwezi'.
Meneja wa msanii huyo, Said Fella, aliiambia MICHARAZO kuwa wameamua kutoa 'audio' na video kwa lengo la kuwapa burudani mashabiki wa msanii huyo ambaye wanajiopanga ili kumtambulisha rasmi katika ulimwengu wa muziki.
Fella, alisema katika wimbo wa 'Nashukuru'. Dogo Muu ameimba pamoja na msanii nyota aliyetoka kuwania tuzo za Kora Africa, Dogo Aslay.
"Tupo katika maandalizi ya kutoa kazi za msanii wetu mpya, Dogo Muu, tutatoa nyimbo zake mbili katika mfumo wa 'audio' na video, lakini zikiwa tofauti," alisema Fella.
Aliongeza wakati Dogo Muu akijiandaa kujitambulisha kwa mashabiki wa muziki na kazi hizo, kundi la TMK Wanaume Family, nalo limefyatua vibao viwili vipya kimoja kiifahamika kwa jina la 'Tutaonekanaje?
Katika hatua nyingine, alisema pamoja na Dogo Aslay kushindwa katika tuzo za muziki za Kora, lakini fursa ya kuteuliwa kuwania tuzo hiyo kama Msanii Bora Chipukizi, imeonyesha ni namna gani kijana huyo alivyo na kipaji.
"Tunajivunia uteuzi wake, hata kama hatafanikiwa kushinda ikizangatiwa ndio kwanza ameingia kwenye sanaa hii baada ya kukitambua kipaji chake," alisema Fella.

Simba, Azam hapatoshi Mapinduzi Cup Z’bar leo

Simba na Azam katika mechi yao ya Ligi Kuu duru lililopita

Na Mwinyi Sadallah, Zanzibar
MABINGWA  watetezi wa Kombe la Mapinduzi, klabu ya Azam wanashuka dimbani kucheza dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba katika mechi yao ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi 2012 kwenye Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar leo.
Mechi hiyo itaanza saa 2:00 usiku, ikitanguliwa na nusu fainali nyingine itakayochezwa jioni kati ya mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya, Tusker na Miembeni ya mjini visiwani hapa.
Tusker wamefanikiwa kuingia fainali wakiwa na pointi 7 na kuongoza katika kundi lao la A baada ya kushinda pia katika mechi yao ya mwisho kwa bao 1-0 dhidi ya Jamhuri ya Pemba.
 Simba ambao wamekuwa wakionyesha kiwango kizuri kadri mashindano hayo yanavyosonga mbele, walitinga nusu fainali wakiwa pointi tano baada ya kutoka sare ya 1-1 katika mechi yao ya mwisho ya hatua ya makundi dhidi ya Bandari.
Azam pia waliingia hatua ya leo wakiwa na pointi tano baada ya juzi kutoka sare na Mtibwa Sugar na hivyo kuongoza katika kundi lao la B, huku Miembeni wakiingia nusu fainali wakiwa na pointi nne baada ya kutoka sare ya 0-0 na Coastal Union ya Tanga.
Kocha wa Simba, Jamhuri Kihwelu alisema kwamba lengo la timu yake ni kutwaa ubingwa baada ya wachezaji wake kuonyesha kiwango kizuri tangu kuanza kwa mashindano hayo.
“Nia tunayo na uwezo wa kutwaa Kombe la Mapinduzi mwaka huu tunao…  wachezaji wetu wameonyesha kiwango kizuri na hivyo naamini kesho (leo) tutashinda tu,” alisema Kihwelu.
Kocha wa Tusker, Robert Matano, alisema kwamba pamoja na timu yake kushiriki kwa mara ya kwanza mashindano hayo, wachezaji wake wameonyesha kiwango kizuri na kufanikiwa kuongoza katika kundi A, hivyo ni imani yake kwamba watashinda pia leo na kutinga fainali.
Hata hivyo, alisema kwamba timu zote zilizofanikiwa kuingia nusu fainali ni nzuri na mafanikio yao yatatokana na juhudi na maarifa ya wachezaji watakocheza leo.
Katibu wa Kamati ya Kombe la Mapinduzi, Abdallah Said, alisema bingwa wa mashindano ya mwaka huu atazawadiwa Sh. milioni 10, mshindi wa pili Sh. milioni tano na mfungaji bora atazawadiwa Sh. 300,000.
Aliongeza kuwa mwamuzi bora wa mashindano hayo na mwanahabari bora pia watapata zawadi ya Sh. 200,000 kila mmoja.
Fainali ya mashindano hayo zitafanyika Jumamosi ambayo ni siku ya kilele cha maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar na utachezwa pia kwenye Uwanja wa Amaan na kuhudhuriwa na mgeni rasmi,  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.


CHANZO:NIPASHE

SUGU AFUNGUA INTERNET CAFE YA IZZO B MJINI MBEYA


Mbunge wa Mbeya mjini Mh Joseph Mbilinyi (Sugu) ndiye aliye fanya ufunguzi wa biashara mpya ya msanii Izzo B "INTERNETE CAFE" iliyoko katika chuo cha Teku jijini Mbeya.
Huu utakua ni uwekezaji wa pili wa msanii Izzo B baada ya kufungua duka la nguo hapo mjini mbeya ambapo ndipo anapotoka.

NJEMBA APEWA KIPONDO BAADA YA KUIBA 'KITIMOTO' NA BIA



 Kijana mmojaambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja akilia kwa uchungu mara baada ya kupokea kichapo kutoka kwa wananchi wenye hasira kali mara baada ya kudaiwa ameiba nyama ya Nguruwe (Kitimoto) pamoja na Bia katika glosali jijini Dar es Salaam.
Mmoja ya wasamalia wema akimtetea kijana huyo ambaye alipokea kichapo.
Akijitetea.
Akisaidiwa na wasamalia wema.

Mrisho Ngassa, John Bocco wainogesha Stars

Ngassa na Bocco wakipongezana


 
WASHAMBULIAJI Mrisho Ngassa wa Simba na John Bocco ‘Adebayor’ wa Azam ni miongoni mwa nyota zaidi walioripoti katika kambi ya timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itakayosafiri leo jioni  kwenda jijini Addis Ababa, Ethiopia kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya wenyeji keshokutwa Ijumaa.
Awali, Bocco, Ngassa, kipa Juma Kaseja na wachezaji wengine kadhaa walioitwa Stars kutoka katika klabu za Simba na Azam walishindwa kuripoti katika kambi ya timu hiyo kwavile walikuwa na klabu zao kwenye michuano inayoendelea visiwani Zanzibar ya Kombe la Mapinduzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa nyota kutoka Simba, Azam na Mtibwa wameungana na wenzao na kwamba sasa Stars itasafiri leo ikiwa na kikosi chenye wachezaji wengi zaidi miongoni mwa wale walioutwa na kocha wao Mdenmark, Kim Poulsen.
Mbali na Bocco, Ngassa na Kaseja, wachezaji wengine walioitwa Stars kutoka Simba, Azam na Mtibwa ni Shomari Kapombe, Amri Kiemba, Amir Maftaha, Mwinyi Kazimoto, Salum Aboubakar 'Sure Boy', Mwadini Ali, Mcha Khamis, Aggrey Morris,  Erasto Nyoni, Aishi Manula na nyota Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ na Shabani Nditi kutoka Mtibwa Sugar,
"Stars inaondoka leo huku ikiwa kamili baada ya nyota wengi kuripoti kambini," alisema Wambura.
Alisema timu hiyo itarejea jijini Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa mechi dhidi ya Ethiopia na kuendelea na kambi yao kujiandaa kwa mechi nyingine mbili za kirafiki, zote zikiwa ni sehemu ya maandalizi kabla ya mechi ya kuwania kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia dhidi ya Morocco itakayochezwa Machi.

MTANGAZAJI ALIYEPOTEA AKUTWA PORINI AMEKUFA HANA SEHEMU NYETI

Bw. Issa Ngumba.

Mwandishi wa habari wa Radio Kwizera anayefanyia kazi wilayani Kakonko mkoani Kigoma,Bw. Issa Ngumba aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha amekutwa amekufa huku akiwa kanyofolewa  sehemu zake za  siri.
 

Taarifa  kutoka Kigoma ambazo mtandao huu  MICHARAZO umezipata jana kuwa, mwili wa mwanahabari  huyo umekutwa nje  kidogo na mkoa  wa Kigoma.
Kamanda  wa  polisi  wa mkoa wa Kigoma Frasser Kishai, amethibitisha  juu ya kutokea kwa  tukio  hilo na kwamba  bado jeshi la polisi linaendelea kufanya uchunguzi.
Mbunge wa  jimbo la Kigoma Zitto Kabwe amenukuliwa kusikitishwa na kifo cha mwandishi huyo na kulitaka jeshi hilo kufanya uchunguzi wa kina juu ya kifo chake.
Kabwe  ameeleza  jinsi  mwanahabari  huyo  alivyokuwa akiifanya kazi yake kwa jamii ya Kigoma kwa ufanisi zaidi na kuwa wakati mwingine yeye kama mbunge alikuwa akizunguka na mwanahabari huyo katika jimbo lake.
" Kweli  nimeguswa   sana na kifo  cha kusikitisha cha mwanahabari huyo nilimfahamu  vema kwa  utendaji kazi wake  ila nawapa  pole sana  waandishi  wote nchini kwa  msiba huu mkubwa .....na zaidi nitapata  kueleza mengi mara baada ya  uchunguzi"
Taarifa za awali  zilizotolewa na  Jeshi la Polisi wilayani Kakonko baada ya  kupotea kwa mwanahabari huyo zilisema kuwa Bw Ngumba alipotea  tangu January 05 mwaka huu majira ya saa 11 jioni ambapo alimuaga mke wake Bi. Rukia Yunus kuwa anakwenda Muhange senta wilayani Kakonko na kwamba hajarudi nyumbani hadi sasa.
Kufuatia tukio hilo jeshi la polisi kwa kushirikiana na wananchi wa Kijiji cha Muhange wanaendelea kumtafuta katika mapori ya kijiji hicho baada ya rafiki zake kueleza kuwa aliwaanga kuwa anakwenda kutafuta dawa msituni.
Bw. Issa Ngumba.
Aidha jeshi la polisi Wilayani Kibondo liliomba kampuni za mitandao ya simu anayotumia Bw Ngumba kusaidia kutambua simu zake zilipotumika kwa mara ya mwisho ili kurahisisha upatikanaji wake.
Akizungumza kwa njia ya simu, Mke wa Bw Issa Ngumba, Bi Rukia Yunus amesema kuwa wananchi walio wengi ambao walikuwa wakimtafuta maporini wamerudi kijiji hapo baada ya kumkosa.

CHANZO:FRANCIS Godwin

OMARI OMARI KUZIKWA LEO TEMEKE


MSANII nyota wa miondoko ya Mchiriku, Omari Omari, aliyefariki jana alfajiri anatarajiwa kuzikwa leo saa 7 mchana kwenye makaburi yaliyopo eneo la Temeke Mikoroshini, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa rafiki ya karibu wa marehemu huyo aliyekuwa akitajwa kama mfalme wa Mnanda King Sapeto, alisema mipango ya mazishi yanaendelea vema na kwamba Omar Omar atazikwa leo mchana.
Sapeto, alisema ndugu na jamaa wa marehemu wanategemea kupata ujumbe mzito kutoka kwa viongozi wa Serikali watakaopishana kwenda kutoa mkono wa faraja kwenye nyumba ya msiba.
Kwa siku za hivi karibuni viongozi wa serikali na vyama mbali mbali vya siasa wamekuwa mstari wa mbele kwa kushiriki bega kwa bega kwenye misiba ya wasanii, hivyo watu wa karibu na Omari Omari wanategemea hali hiyo pia itatokea kwa ndugu yao kipenzi. 
"Hatutegemi ubaguzi wa misiba" anaeleza mmoja wa ndugu wa marehemu.
Omari Omari aliyetamba na wimbo “Kupata Majaaliwa”, alifariki katika hospitali kuu ya Temeke baada ya kuugua ugonjwa wa kifua kikuu.
Msiba wake umekuja siku chache baada ya watanzania kumzika nyota wa filamu, Juma Kilowoko 'Sajuki' aliyefarikia Januari 2, katika hospitali ya Muhimbili alipokuwa amelazwa kwa matatizo ya kiafya.
 
Mwisho

Tuesday, January 8, 2013

Omar Omar mkali wa Mchiriku afariki dunia Dar

MSANII  nyota wa miondoko ya Mnanda a.k.a Mchiriku, Omari Omar amefariki dunia usiku wa kuamkia leo baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Habari zilizoifikia MICHARAZO, asubuhii zinasema kuwa, Omar Omar aliyetamba na nyimbo mbalimbali ukiwemo ule maarufu wa 'Kupata ni Majaliwa' alifariki nyumbani kwao Temeke, saa chache baada ya kurejeshwa toka hospitali ya temeke alipokuwa amelazwa kwa siku kadhaa.
Taarifa hizo zinasema kuwa mara baada ya kurejea nyumbani, msanii huyo alizidiwa na hatimaye kufariki na kwamba msiba wake upo nyumbani kwao Temeke Mikoroshini kwa ajili ya mipango ya mazishi.
Msiba wa msanii huo umekuja siku chache baada ya tasnia ya sanaa na burudani kumpoteza Juma Kilowoko 'Sajuki' msanii nyota wa filamu aliyefariki pia kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya muda mrefu.
MICHARAZO inawamuombea kila la heri Omar Omar na wengine waliotangulia mbele ya haki mapumziko mema katika safari yao ya Ahera. Innallillah Waina Illah Rajiun.
Taarifa zaidi tutakuwa tunawaletea kujua mkali huyo wa mduara aliyewafanya wasanii wengine kufuata mkondo wake akiwemo Dogo Mfaume, Ferouz, Easy Man na wengine.

Mayweather Jr, kuvaana na Guerrero Mei 4

BONDIA Floyd Mayweather Jr anatarajia kupanda jukwaani katika ukumbi wa MGM Grand, Las Vegas, Nevada, USA kuwania taji la WBC welterweight title May 4 ,2013 kuzipiga na Robert Guerrero bondia huyo ambaye ajawai kupigwa tangia angie katika uwanja wa masumbwi ya kulipwa tarehe 11-10-1996 bondia huyo alichezo mpambano wake wa mwisho May 5 mwaka jana na kutumikia kifungo cha Miezi mitatu kwa kosa la kumshambulia aliyekuwa mpenzi wake mama watoto wake kwa sasa yupo katika maandalizi ya mpambano huo wa tarehe hiyo katika mchezo wake wa mwisho aliocheza na Miguel Cotto alipata ushindi mwembamba kwa kuibuka kumtwanga kwa point
www.superdboxingcoach.blogspot.com    BONDIA Floyd Mayweather Jr  anatarajia kupanda jukwaani katika ukumbi wa MGM Grand, Las Vegas, Nevada, USA kuwania taji la    WBC welterweight title May 4 ,2013 kuzipiga na Robert     Guerrero bondia huyo ambaye ajawai kupigwa tangia angie katika uwanja wa masumbwi ya kulipwa  tarehe 11-10-1996 bondia huyo alichezo mpambano wake wa mwisho May 5 mwaka jana na kutumikia kifungo cha Miezi mitatu kwa kosa la kumshambulia aliyekuwa mpenzi wake mama watoto wake kwa sasa yupo katika maandalizi ya mpambano huo wa tarehe hiyo katika mchezo wake wa mwisho aliocheza na Miguel Cotto alipata ushindi mwembamba kwa kuibuka kumtwanga kwa point

LIONEL MESSI TENA MWANASOKA BORA WA DUNIA

Lionel Messi akifurahi baada ya kupokea tuzo yake ya nne mfululizo ya Ballon d'Or ya kwenye Ukumbi wa Convention Centre mjini Zurich Uswisi jana.
Lionel Messi akiwa kwenye tuzo za FIFA jana
Ronaldo, Iniesta na Messi wakiwa kwenye tuzo.
Kikosi XI cha FIFA kilichotangazwa jana. Kutoka kushoto mstari wa nyuma Cristiano Ronaldo, Marcelo, Sergio Ramos, Gerard Pique, Dani Alves, Iker Casillas. Mstari wa mbele kutoka kushoto: Radamel Falcao, Lionel Messi, Andres Iniesta, Xavi Hernandez na Xabi Alonso
Winga wa Fenerbahce, raia wa Slovakia, Miroslav Stoch akishukuru kwa tuzo ya Puskas ya Goli Bora la Mwaka wakati wa sherehe za tuzo za FIFA Ballon d'Or.
Vicente del Bosque akishukuru baada ya kupokea tuzo ya Kocha Bora wa Dunia wa Mwaka 2012
Mwanasoka Bora wa Dunia wa zamani, Fabio Cannavaro wa Italia akionyesha jina la mshindi wa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia wa Mwaka 2012, Lione Messi
Straika wa timu ya taifa ya Marekani, Abby Wambach akishukuru baada ya kutangazwa mshindi wa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Kike wa Dunia

Mwanasoka wa zamani wa Colombia, Carlos Valderrama (kushoto) na mchezaji wa zamani wa Uholanzi, Ruud Gullit wakati wa kukabidhi tuzo ya Puskas ya Goli Bora la Mwaka.

Mwanasoka wa zamani wa Colombia, Carlos Valderrama akisoma jina la mshindi wa tuzo ya Puskas ya Goli Bora la Mwaka.

Fuleco, kikatuni cha fainali za Kombe la Dunia 2014 za nchini Brazil kikimkumbatia mwanasoka bora wa zamani Ronaldo stejini wakati wa sherehe za tuzo za FIFA Ballon d'Or.

Kocha wa timu ya taifa ya Brazi, Luiz Felipe Scolari na mwanasoka wa zamani wa Colombia, Carlos Valderrama wakipozi kwa picha

Straika wa Real Madrid, Mreno Cristiano Ronaldo na rafikiye wa kike Irina Shayk wakiingia kwenye sherehe za tuzo za FIFA Ballon d'Or.

Rais wa FIFA, Joseph Blatter akiambatana na muigizaji wa Kirafansa, Gerard Depardieu wakati akiwasili kabla ya kuanza kwa kwenye sherehe za tuzo za FIFA Ballon d'Or.
Waongozaji wa sherehe ya tuzo za FIFA Ballon d'Or, Ruud Gullit (kushoto) na Kay Murray wakiwa mzigoni

NYOTA wa Barcelona, Lionel Messi (25) jana aliweka rekodi ya kipekee ya kuwa mwanasoka wa kwanza duniani kutwaa tuzo ya Ballon d'Or ya Mwanasoka Bora wa Dunia kwa miaka minne mfululizo baada ya kuwashinda wapinzani wake Cristiano Ronaldo wa Real Madrid na Andres Iniesta wa Barcelona.
Muargentina huyo amekuwa mtu wa kwanza katika historia ya miaka 61 ya tuzo hiyo kuibeba mara nne mfululizo.
Johan Cruyff (1971, 1973, 1974) na Marco Van Basten (1988, 1989, 1992) wa Uholanzi, na Michel Platini wa Ufaransa walishinda tuzo ya Ballon d'Or mara tatu.
Mwanadada Abby Wambach wa Marekani alishinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Kike, wakati tuzo ya kocha bora wa kiume ilienda kwa Vicente Del Bosque wa timu ya taifa ya Hispania baada ya kuwashinda, Jose Mourinho wa Real Madrid ambaye alishasema mapema kwamba hatahudhuria sherehe hizo nchini Uswisi na Pep Guardiola.
Tuzo ya Puskas ya Goli Bora la Mwaka
ilienda kwa winga wa Fenerbahce, raia wa Slovakia, Miroslav Stoch ambaye alifunga goli lake kwa kuunganisha moja kwa moja bila ya kutua chini mpira wa kona uliomfikia akiwa nje ya boksi. Stoch aliwaangusha Radamel Falcao aliyefunga goli la 'tik-taka' na Neymar aliyefunga goli katika mazingira magumu.
Kikosi cha wachezaji bora "First Eleven" wa dunia chote kimeundwa na nyota wanaocheza katika Ligi Kuu ya Hispania, huku Radamel Falcao pekee akitokea nje ya Barcelona na Real Madrid.
Real Madrid na Barcelona zimetoa wachezaji watano kila moja.

Kikosi Bora cha Dunia XI cha FIFA kilichotangazwa jana ni:

Kipa

Iker Casillas
Mabeki
Dani Alves, Marcelo, Sergio Ramos na Gerard Pique
Viungo
Xabi Alonso, Xavi Hernandez na Andres Iniesta
Washambuliaji
Cristiano Ronaldo, Radamel Falcao na Lionel Messi

Monday, January 7, 2013

SIMBA YATINGA NUSU FAINALI MAPINDUZI CUP, 'YAJITOA'

Kikosi cha Simba kilichotinga Nusu Fainali jana

Na Mahmoud Zubeiry, Zanzibar
PAMOJA na kufuzu hatua ya Nusu Fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi jana, Simba SC italazimika kuiachia timu yao ya pili, maarufu kama Simba B iendelee na michuano hiyo hata kama ikiingia fainali, ili kikosi cha kwanza kiende Oman keshokutwa.
Kocha Mkuu wa Simba SC, Mfaransa Patrick Liewig aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, anataka kwenda Oman na kikosi kamili ili aweze kuwajua wachezaji wote na kuweza kuipanga vyema timu yake.
Kuhusu wachezaji wa timu ya taifa, ambayo Januari 11 itacheza mchezo wa kirafiki na Ethiopia, Liewig alisema suala hilo linashughulikiwa na viongozi wa klabu hiyo. “Najua viongozi walikuwa wana kikao na viongozi wa shirikisho (TFF).
Sijui wamekubaliana vipi, lakini naweza kuwavumilia wachezaji hao wajiunge na timu Oman baada ya mechi na Ethiopia,”alisema.
Simba jana ilifuzu Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi, licha ya kutoka sare ya 1-1 na Bandari ya hapa katika mchezo wa mwisho wa Kundi A, kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Hadi mapumziko, timu hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1, Bandari wakitangulia kupata bao kwa penalti, mfungaji Haitham Juma dakika ya sita kabla ya Kiggi Makassy kuisawazishia Simba SC dakika ya 16.
Refa aliwapa penalti Bandari baada ya Haruna Shamte kumchezea rafu Fauzi Ally katika eneo la hatari na Haitham akaenda kupiga penalti, ambayo ilipanguliwa na kipa Dhaira na mpira kumkuta tena mpigaji, aliyeukwamisha nyavuni.
Kiggi alifunga kwa mpira wa adhabu kutoka upande wa kulia wa Uwanja, umbali wa mita 20, baada ya Abdallah Seseme kuangushwa.    
Kipindi cha pili, Simba walianza kwa kuimarisha kwa kikosi chao wakiwaingiza kwa mpigo, Mwinyi Kazimoto, Haruna Chanongo na Jonas Mkude kuchukua nafasi za Mussa Mude, Salim Kinje na Ramadhani Singano ‘Messi’, wakati Bandari walimtoa kipa wao Hassan Hajji na kumuingiza Ahmad Suleiman.
Kwa matokeo hayo, Simba SC imeungana na Tusker ya Kenya kufuzu Nusu Fainali ya michuano hiyo. Tusker ni kinara wa kundi kwa pointi zake saba na Simba imeingia kama mshindi wa pili kwa pointi zake tano.
Wachezaji wa Simba SC walioitwa Stars ni kipa Juma Kaseja, mabeki Amir Maftah na Shomari Kapombe, viungo Amri Kiemba na Mwinyi Kazimoto na mshambuliaji Mrisho Ngasa.
Katika wachezaji wote hao walioitwa Stars, walio kwenye kikosi cha Simba kinachocheza Kombe la Mapinduzi ni Kapombe na Mwinyi Kazimoto pekee. Kaseja, Ngassa, Kiemba ni majeruhi, wakati Amir Maftah imeelezwa ana madai yake anayosubiri alipwe ndipo ajiunge na timu.  

Imehamishwa Bin Zubeiry

Sepp Blatter apinga kitendo kilichofanywa na Boateng, AC Milan

Rais wa FIFA, Sepp Blatter

RAIS wa Shirikisho wa Soka Duniani, FIFA, Sepp Blatter ameponda kitendo cha nyota wa AC Milan, Kevin Prince Boateng kuamua kususa pambano lao la kirafiki la wiki iliyopita dhidi ya timu ya daraja la chini ya Pro Patria, akidai haiwezi kuvumiliwa.
Blatter alinukuliwa jana akiwa Dubai kwenye zira ndefu ya Mashariki na Kati, akisema kuwa kilichofanywa na Boateng na timu yake ya Milan haiwezi kusaidia kumaliza ubaguzi zaidi ya kuongeza tatizo, iwapo kila timu au kila mchezaji watakuwa wakiamua kususa mechi kwa kufanyiwa vitendo kama hivyo.
"Sidhani kama kuondoka uwanjani ndio suluhisho la tatizo, inaweza kutumiwa vibaya na timu nyingine hasa kama timu imefungwa katika pambano hilo," alinukuliwa Bletter.
Alisema wanasubiri taarifa toka Shirikisho la Soka la Italia kujua kitu gani kilichotokea, ingawa alisisitiza kuwa pamoja na kwamba FIFA inapinga vitendo vya ubaguzi, lakini pia haiungi mkono tabia ya kususia mechi vinapotokea vitendo kama hivyo wakati wa mechi.
Kevin Prince Boateng kiungo wa AC Milan

Boateng nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Ghana, Black Stars, aliamua kutoka uwanjani baada ya kufanyiwa vitendo vya kibaguzi na mashabiki wa Pro Patria katika mechi ya kirafiki iliyochezwa Alhamis iliyopita ambapo licha ya kubembelezwa aligoma kufuta msimamo wake na kusababisha mechi hiyo kuvunjika.
Jana Jumapili wachezaaji wa timu hiyo ya Milan, walitinga uwanjani katika pambano lao la Seria A wakiwa na jezi zenye maandishi ya kupinga ubaguzi wa rangi ambapo timu hiyo ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Siena.
Vitendo vya kibaguzi dhidi ya wachezaji wenye asili ya Afrika kwa mataifa ya Ulaya vimekuwa vikizidi kushamiri kwa siku za karibuni, baadhi vikifanywa na wachezaji wenyewe kwa wenyewe na wakati mwingine vikifanywa na mashabiki kama ilivyotokea kwa Boateng.


Wachezaji wa AC Milan wakiwa wamevaa jezi zinazopinga ubaguzi wa rangi kabla ya mechi yao ya Seria A dhidi ya Siena jana
Hata hivyo pamoja na FIFA na FA za nchi mbalimbali kuvipinga vitendo hivyo na kutoa adhabu kwa wahusika bado havijaleta tija hasa kutokana na adhabu zake kuonekana nyepesi kuliko ukubwa wa jambo hilo.

TAFF YAWAONYA WASANII WALIOHARIBU MSIBA WA SAJUKI


Rais wa TAFF, Simon Mwakifwamba


SHIRIKISHO la Filamu Tanzania (TAFF) limekemea baadhi ya wasanii walioonyesha utovu wa nidhamu katika msiba wa  aliyekuwa msanii wa filamu nchini, Juma Kilowoko ‘Sajuki’.

Pia limesisitiza kuwa msanii atakaeripotiwa katika vyombo vya habari kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu atafungiwa kuigiza.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Rais wa TAFF, Simon Mwakifwamba alisema amesikitishwa na kitendo cha wasanii kuacha msiba na kwenda kunywa pombe wakati msiba huo ni wa dini.

Alisema baadhi ya wasanii kuonyesha utovu wa nidhamu katika msiba wa marehemu Kanumba na wengine katika msiba wa Sajuki.

“Nasikitika kuona msanii hajitambui hata kidogo, yani anaacha msiba anakwenda kunywa pombe tena jirani na mahala pa msiba, jamani huu msiba ni wa dini, hivyo atakayeripotiwa vibaya katika misiba TAFF tutamfungia” alisema Mwakifwamba.

Katika hatua nyingine alisema msiba huo ulitawaliwa na utani hali ya kwamba umewakutanisha watani wa makabila.

Msiba huo ulitawaliwa na utani baada ya kuwepo kwa wasanii wachekeshaji kama vile, Steven Mengele ‘Steve Nyerere’ ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya fedha, Lucas  Mhuvile ‘Joti’ na wengineo wengi.

Tuzo za wakali wa filamu 2012 kutolewa Februari



MBIVU na mbichi ya nani mkali katika fani ya filamu kwa mwaka 2012 zinatarajiwa kufahamika mwezi ujao wakati wa hafla ya kutangaza washindi itakapofanyika jijini Dar es Salaam.
Tuzo hizo za Wasanii Bora wa Filamu 2012 zilizoandaliwa na Mtandao wa filamucentral zinatarajiwa kutolewa kwa washindi mwezi Februari katika tarehe na ukumbi utakaotajwa na waratibu wake.
Mratibu wa tuzo hizo, Myovela Mfaiswa, aliiambia MICHARAZO kuwa maandalizi kwa ujumla ya hafla hiyo inaendelea vema huku wadau wa filamu wakiendelea kuwapigia kura washiriki wanaochuana katika kinyang'anyiro hicho.
Mfaiswa alisema vipengele vinavyowaniwa katika tuzo hizo zinazofanyika kwa mara ya pili baada ya kufanyika mara ya mwisho mapema mwaka jana kwa wasanii bora wa 2010 ni pamoja na cha Muigizaji Bora wa Kike inayowaniwa na Yvonne Cherry 'Monalisa', Jacklyne Wolper, Wema Sepetu, Jennifer Kyaka 'Odama' na Elizabeth Michael 'Lulu'.
Tuzo nyingine ni ya Mchekeshaji Bora inayowaniwa na wasanii Haji Salum 'Mboto', King Majuto, Sharo Milionea, Kitale na Kinyapi, huku Muigizaji Bora Chipukizi ikiwaniwa na Mariam Ismail 'Mammy', Abdallah Ambua 'Dulla', Slim Omary 'Mdudu Kiu', Jose Mteme 'Baga' na Halima Ali.
Tuzo ya Muigizaji Bora wa Kiume inawaniwa na Jacob Stephen 'JB', Vincent Kigosi 'Ray', Steven Kanumba, Hisani Muya 'Tino' na Single Mtambalike 'Richie', wakati tuzo za Mwandishi Bora wa Mswada inawaniwa na Octavian Natalis, Ali Yakuti, F Kanuti, Elizabeth Chijumba na Kimela Bila.
------

KUMEKUCHA MISS UTALII TANZANIA


KAMBI ya warembo watakaoshiriki fainali za shindano la urembo la Utalii, Miss Utalii Tanzania, inatarajiwa kuanza rasmi Jumamosi ijayo ikishirikisha warembo walioshika nafasi mbili za juu ya mashindano ya ngazi ya mkoa.
Rais wa Miss Utalii Tanzania, Gideon Chipungahelo 'Chipps' aliiambia MICHARAZO kambi hiyo itakuwa ya siku 21 kabla ya kufanyika kwa kinyang'anyiro hicho mwishoni mwa mwezi huu jijini Dar es Salaam.
Chipps aliwataja warembo watakaoingia kambini tayari kuwania taji hilo la Tanzania na tuzo nyingine 28 zitakazowaniwa kuwa ni pamoja na Rose Godwin (Arusha), Irene Thomas, Sophia Yusuph na Ivon Stephen wote wa Dar.
Wengine ni Erica Elibariki (Dodoma), Jamia Abdul (Geita), Debora J. Mwansepeta (Iringa), Anna Pogaly (Kilimanjaro), Zena Sultan (Kigoma), Asha Ramadhani (Katavi), Joan John (Lindi), Doreen Bukoli (Mara), Dayana Joachim (Mbeya) na Jessica Rugalabamu wa Mwanza.
Warembo wengine ni Halima Suleman (Mtwara), Hadija Saidi (Morogoro), Mary Rutta (Manyara), Paulina Mgeni (Njombe), Anganile Rogers (Rukwa), Furaha Kinyunyu (Ruvuma), Neema Julius (Singida), Flora Msangi (Simiyu), Lightness Kitua (Shinyanga), Magreth Malale (Tabora) na Sarafina Jackson wa Tanga.
Wawakilishi wa vyuo wakaoshiriki kinyang'anyiro hicho ni Irene Richard Makoye na Hawa Nyange.
Tuzo zitakazowaniwa na warembo hao mbali na taji litakalompa mshindi uwakilishi wa nchi katika shindano la kimataifa ni pamoja na tuzo za heshima za Jamii, Elimu ya Jamii, Afya ya Jamii, Utalii, Utamaduni, Uchumi, Miundo Mbinu ya Utalii, Uwekezaji, Madini na maliasili mbalimbali za taifa.

Suarez afunga bao la utata na kuivusha Liverpool Kombe la FA

HATUA KWA HATUA YA BAO LA UTATA LA SUAREZ JANA
Suarez akijitengenezea vizuri mzuri kwa mkono
Amefanikiwa na sasa anaelekea kufunga bao

Akimtoka kipa aliyejaribu kumzuia
Kazi imekuwa nyepesi anafunga kilainii..huku Mansfield wakiinua mikono wakilalamikia bao hilo

Anashangilia na wenzake

Anaubusu mkono wake kwa kazi nzuri uliofanya

 

NYOTA wa timu ya Liverpool, Luis Suarez, jana akitokea benchi alitengeneza bao kwa mkono kisha kufunga na kuivusha timu yake kwenye michuano ya Kombe la FA nchini England.

Bao hilo ambalo tukio la kutengenezwa na mkono halikuonwa na mwamuzi wa pambano hilo la raundi ya tatu ya michuano hiyo iliisaidia kuipa Liverpool ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya

Mansfield Town.
Raia huyo wa Uruguay ambaye anakumbukwa na Waafrika kwa kulizuia bao la Ghana katika Fainali za Kombe la Dunia 2010, alifunga bao hilo katika dakika ya 59 dakika tano tangu aingie dimbani kuchukua nafasi ya Daniel Sturridge, aliyetangulia kufunga bao la mapema.
Wenyeji Mansfield waliolalamikia tukio hilo, walipata bao la kufutia machozi dakika ya 80 kupitia Matt Green, ambalo halikuwasaidia kutong'oka kwenye michuano hiyo ambayo pia jana ilishuhudiwa Arsenal wakilazimishwa sare ya 2-2 ugenini na Swansea City.
Arsenal ilielekea kushinda pambano hilo baada ya kutoka nyuma ya bao 1-0 mara kipindi cha pili kilipoanza baada ya dakika 45 za kwanza kwenda mapumziko bila kufungana na kufunga mabao mawili dakika 10 za mwisho wa mchezo huo kabla ya kujisahau na Swansea kusawazisha zikiwa zimesalia dakika tatu.
Michu alianza kuiandikia Swansea bao dakika ya 51 kabla ya Lucas Podolski kusawazisha dakika ya 81 na Kieran Gibbs kufunga bao la pili dakika mbili baadae na wakati wengi wakiamini Arsenal imepita kwa raundi ya nne,  Danny Graham kusawazisha bao hilo na kuzifanya timu zao sasa kurudiana tena ili kufuzu hatua ijayo itakayoanza Januria 26.

Amefanikiwa na sasa anaelekea kufunga bao

TUZO BALLON D'OR LEO, AGUERO ATAKA MESSI APEWE

Aguero  akiwa na Lionel Messi

NYOTA wa timu ya Mamchester City ya England ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Argentina, Sergio 'kun' Aguero, amesema kwamba tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia ya Ballon d'Or inapaswa kwenda kwa Lionel Messi. 
Sherehe za kumtangaza mwanasoka bora wa dunia wa mwaka 2012 zitafanyika leo kwenye Ukumbi wa Zurich Convention Centre nchini Uswisi.

Aguero akihojiwa na gazeti la Argentina la 'Ole', alisema Muargentina mwenzake huyo anayeichezea Barcelona ya Hispania anastahili kupewa tuzo hiyo.
"Anastahili tuzo hiyo kwa yote aliyoyafanya akiwa na Barcelona na timu ya taifa ya Argentina," alisema Muargentina huyo, ambaye pia ana ndoto za kuja kuwa mchezaji bora wa dunia siku moja.
 "Si jambo rahisi, lakini kama utafanya mambo yako vizuri huwezi kujua (unaweza kushinda tuzo). Unajua daima unapaswa kuota kuwa mchezaji bora duniani," aliongeza.
Aguero pia alizungumzia kiwango cha timu yake cha sasa. "Hatujacheza kama ambavyo tulikuwa tukicheza msimu uliopita, lakini tuko katika nafasi nzuri. Tunaongezeka ubora na katika mechi mbili zilizopita tulicheza vizuri sana. Tuna kikosi kizuri na tuna uwezo wa kurejea katika kiwango kama cha msimu uliopita. Kutolewa kwenye Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya ilikuwa pigo kubwa kwa sababu tulikuwa na matumaini makubwa katika michuno ile. Tulikuwa katika kundi gumu. Taji la Ligi ya Klabu Bingwa ni jambo tunaloliota pia. Tutafanya vyema siku zijazo," alisema.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina pia alijumuisha mwaka wake 2012 akisema: "Ulikuwa ni mwaka mzuri katika maisha yangu ya soka. Ulikuwa muhimu katika kujijenga kwenye klabu ya Man City na kutwaa ubingwa wa England. Na kikubwa ni kufunga goli lile lililoamua bingwa katika dakika za lala salama. Ilikuwa ni ndoto iliyogeuka kwa kweli," aliongeza Aguero.
Mshambuliaji huyo pia alizungumzia timu ya taifa ya Argentina, akisema: "Jambo muhimu zaidi ni kwamba tufuzu kwa Kombe la Dunia 2014 mapema iwezekanavyo. Kama ukipoteza mechi mbili katika michuano hii migumu ya kuwania kufuzu timu nyingine zinakufikia. Ulikuwa ni mwaka mzuri kwa timu ya taifa. Tumeanza kuzoeana na kufanya mambo sahihi uwanjani," alisema.

Saturday, January 5, 2013

Machini aibuka kumtetea Balotelli, adai hawatamfukuza

Kocha Mancini na Balotelli
MANCHESTER, England
KOCHA wa Manchester City, Roberto Mancini amesema atampa Mario Balotelli "nafasi nyingine 100 zaidi" za kujirekebisha baada ya kusisitiza kuwa malumbano yake na mshambuliaji huyo hayakuwa ni ngumi.
Picha zinaonyesha wawili hao wakitenganishwa wakati wa mazoezi yao ya jana.
Lakini Mancini alisema kuhusu tukio hilo kwamba kilichotokea na Muitalia mwenzake huyo: "Si ngumi, siyo kweli. Picha zinaelezea vibaya tukio.
"Nitampa nafasi nyingine 100 kama nadhani inawezekana akabadilika. Nampa nafasi nyingine, hakika, kwa sababu ana umri wa miaka 22 na anaweza kufanya makosa."
Tukio hilo jipya zaidi katika mfululizo wa matukio ya utata yanayomhusisha mshambuliaji huyo, limemuonyesha Balotelli katika picha akikunjana na kocha wake.
Picha zinaonyesha Mancini akimbwatukia mchezaji wake huyo, ambaye amefunga magoli matatu katika mechi 21 msimu huu.
Picha moja inawaonyesha wawili hao wakiangaliana uso kwa uso, nyingine Mancini akivuta jezi ya Balotelli, wakati katika picha nyingine mshambuliaji huyo anaonekana akivutwa pembeni na wafanyakazi wa uwanjani hapo.
Lakini Mancini amedai kwamba tukio hilo limekuzwa mno na kusisitiza kwamba Balotelli anahitaji klabuni hapo.
"Haikuwa mbaya," alifafanua. "Tulikuwa tunacheza mechi, Mario akampiga teke mwenzake nikamwambia 'nenda ndani (kwenye vyumba vya kuvalia), ondoka uwanjani'.
"Alisema 'hapana' hivyo nikamvuta shati lake na kumsukuma nje ya uwanja. Hicho ndicho kilichotokea. Hakuna cha zaidi."
"Mario yuko hivi lakini mtazamo wangu (kuhusu hatma yake) hautabadilika, hii siyo muhimu. Tatizo litakuwa yeye mwenyewe. Kama hatabadilika, kwake itakuwa ngumu sana huko baadaye, Kwake, si kwangu.
"Mario anaweza kubaki nami siku moja, mwezi mmoja, miaka mitano. Ana miaka 22. Anahitaji kubadilika. Tatizo lake ni yeye mwenyewe."
Alipoulizwa kama ni yeye ndiye aliyepandisha hasira katika tukio hilo, Mancini alijibu: "Hapana. Kwa sekunde mbili za kwanza, ndiyo, lakini baada ya sekunde tatu ama nne hakutaka kuondoka uwanjani. Kwangu alipaswa kuondoka."