STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, May 8, 2014

Man City yanusa ubingwa England, Sunderland yaendeleza maajabu yake

Dzeko akifunga bao
Dzeko akishangilia moja ya mabao yake na wachezaji wenzake wa Man City
Fabio Borini akishangilia bao lake lililoisaidia Sunderland kunusurika kushuka daraja
WAKATI Sunderland ikijihakikisha kusalia kwenye Ligi Kuu ya England baada ya kuitwanga West Bromwich kwa mabao 2-0, Manchester City imejiweka katika nafasi nzuri ya kunyakua taji la ligi hiyo baada ya kupata ushindi mnono nyumbani dhidi ya Aston Villa.
Manchester City iliyorejea kileleni ikiitoa Liverpool ilipata ushindi wa mabao 4-0 na kuwafanya wafikishe jumla ya pointi 83, mbili zaidi ya Liverpool huku ligi ikitarajiwa kumalizika mwishoni mwa wiki ambapo itahitaji ushindi kurejesha taji hilo kwenye himaya yao toka kwa wapinzani wao Manchester United waliolitema taji hilo walilowapokonya msimu uliopita.
Ikicheza kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Etihad, Manchester City ilipata mabao yake kupitia kwa  Edin Dzeko aliyefunga mabao mawili katika dakika za 64 na 72, Stevan Jovetic na Yaya Toure.
Katika mechi nyingine iliyochezwa pia jana, Sunderland ikiwa nyumbani iliweza kupata ushindi wake wanne mfululizo kwa kuilaza West Brom kwa mabao 2-0 na kujinasua kwenye janga la kushuka daraja ikiwaachgia kasheshe wapinzani wao, West Brom, Norwich City na Hull City.
Mabao yaliyoivusha salama Sunderland katika msimu huu baada ya kusota mkiani kwa muda mrefu yalifungwa na Jack Colback katika dakika ya 13 na Fabio Borini dakika ya 31 na kuifanya timu hiyo kufikisha jumla ya pointi 38 ambazo haziwezi kufikiwa na timu ya Norwich iliyopo nafasi ya 18 ikiwa na pointi 33 ligi ikiwa imesaliwa na mzungumzo mmoja tu siku ya Jumamosi.
Msimu wa Ligi Kuu ya England utakamilishwa siku hiyo ya Mei 11 kwa mechi kati ya Cardiff City vs Chelsea, Fulham vs Crystal Palace, Hull City vs Everton, Liverpool vs Newcastle United, Manchester City vs West Ham United, Norwich City vs Arsenal, Southampton vs Manchester United, Sunderland vs Swansea City, Tottenham Hotspur vs Aston Villa na West Bromwich vs Stoke City.
Timu za Fulham na Cardiff City zenyewe tayari zimeshaaga ligi hiyo na inasubiri timu moja ya mwisho za kurudi nao Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao.

Tuesday, May 6, 2014

Pep Guardiaol apata mtetezi Bayern Munich

WINGA wa Bayern Munich, Arjen Robben anaona kwamba mambo yamekuzwa mno tangu walipotolewa katika nusu fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid.
Mabingwa hao waliokuwa watetezi walitolewa kwa jumla ya mabao 5-0, na kusababisha mbinu za ufundishaji za kocha Pep Guardiola kupingwa kufuatia kipigo cha 4-0 nyumbani katika mechi yao ya marudiano.
Wakiwa wameshatwaa ubingwa wa Bundesliga mapema zaidi katika historia msimu huu, kikosi cha Guardiola kinawania taji la pili la Kombe la 'FA' (DFB-Pokal), dhidi ya Borussia Dortmund katika fainali na Robben anaona kwamba hawastahili kusakamwa kama vile hamna walichofanya.

Uchaguzi Mkuu Simba Waiva, Hanspope ndiyo basi tena!

Zakaria Hanspope
MSAJILI wa Klabu na Vyama vya Michezo Nchini jana aliipitisha katiba ya klabu ya Simba lakini ikiwa imeondolewa kipengele cha 26 (4) kilichokuwa kimefanyiwa marekebisho na wanachama wa klabu hiyo ambao walifanya mkutano mkuu wao Machi 16 mwaka huu kwenye ukumbi wa Bwalo la Maafisa wa Polisi, Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Kugonga mwamba kwa kipengele hicho kunamaanisha kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba wa kuteuliwa, Zacharia Hanspoppe, hataweza kuwania uongozi ndani ya klabu hiyo.
Kipengele hicho kinachoelezea sifa ya mgombea kwamba ni lazima asiwe mtu aliyewahi kufungwa/ kutiwa hatiani kwa kosa la jinai, ndiyo kilimuondoa Hanspoppe aliyekuwa anawania uenyekiti katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2010 ambao ulimuweka madarakani Mwenyekiti, Ismail Aden Rage na wenzake.
Akizungumza jana jijini, Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kwamba kipengele hicho hakikufika kwa msajili na kiliondolewa na Kamati ya Katiba ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa sababu inapingana na katiba ya shirikisho hilo linalosimamia mchezo huo nchini.
Kamwaga alisema kuwa kukamilika kwa katiba hiyo ni fursa kwa klabu yao kutangaza tarehe mpya ya kufanya uchaguzi utakaowaweka madarakani viongozi wapya.
Kamwaga alisema kuwa marekebisho mengine ambayo yalifanyiwa marekebisho na wanachama wa Simba yamepitishwa mojawapo ni kiongozi wa juu sasa atajulikana kwa jina la Rais badala ya Mwenyekiti na kutakuwa na Makamu wa Rais.
Alisema kuwa mabadiliko yaliyopitishwa ni pamoja na kuundwa kwa Kamati ya Rufaa, Kamati ya Maadili na pia ndani ya kata moja sasa inaruhusiwa kuwa na tawi zaidi ya moja lakini liwe na wanachama kuanzia 50 na wasiozidi 250.
Pia Kamwaga alisema kwamba kati ya wajumbe watano wa watakaochaguliwa, nafasi moja itakuwa ni kwa mjumbe mwanamke na hiyo wamelenga kuleta mawazo ya jinsi hiyo ndani ya uongozi.
"Kuundwa kwa kamati hizi kunaashiria kwamba matatizo yetu ndani ya Simba yanaweza kumalizwa na kamati hizi kabla ya kuvuka ngazi nyingine," alisema Kamwaga.
Alieleza kwamba kufuatia katiba hiyo kusajiliwa, Kamati ya Uchaguzi ambayo iko chini ya Mwenyekiti wake, Damas Ndumbaro, inatarajia kukutana leo jioni kwa ajili ya kupanga tarehe ya uchaguzi na mchakato mzima utakaohusisha zoezi hilo.

Tanki la mafuta lateketea na kuleta hopfu Singida

BAADHI ya  wananchi wakipiga picha wakati tanki la mafuta la kampuni ya B. Clarke Haulege Construction, Tanki hilo ni mali ya Bw. Bundala Kapela wa Igunga ni namba T634 BCZ lenye vyumba vinne na uwezo wa kubeba lita 40.000 za mafuta ya Petroli lililipuka majira ya Saa 11:00 katika barabara kuu ya Dodoma Mwanza eneo la Shelui mkoani Singida wakati breki za tanki hilo upande wa kushoto zilipojam na kusababisha moto.
Jambo lililomfanya dereva wa roli lenye namba za usajiri T 164 CGF aina ya Scania lililokuwa likivuta tanki hilo kusimamisha na kukata haraka tanki hilo huku akiondoa haraka injini ili kuepusha madhara zaidi ambayo yangeweza kutokea.
Katika tukio hilo lililosababisha usumbufu mkubwa kwa abiria na msururu wa magari kushindwa kupita katika eneo hilo kutokana na moto mkubwa uliochanganyika na moshi kutishia usalama wa watumiaji wengine.
Hata hivyo baada ya moto kupungua kiasi askari wa usalama barabarani waliamuru magari yaanze kupitia pembeni mwa barabara hiyo ili kuendelea na safari. Hakuna mtu aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa katika tukio hilo.
 Angalia matukio zaidi ya picha hapo chini. 
(PICHA FULLSHANGWE-SHELUI-SINGIDA) 5 4 3 2 111 
Msururu wa magari ukiwa mkubwa katika eneo hilo baada ya kushindwa kupita kutokana na moto mkubwa uliokuwa ukiwaka. 10 
Wananchi na wasafiri mbalimbali wakitoka kuangalia tukio hilo. 8 
Askari wa usalama barabarani akihakikisha mambo yanakwenda sawana usalama unaimarishwa katika eneo hilo.

Liverpool yaduwazwa ugenini, ubingwa kwao ni majaliwa sasa!

Hekaheka uwanjani kati ya Crystal Palace na Liverpool jana
Liverpool wakipongezana baada ya kufunga moja ya mabao yao matatu

Suarez akioyesha makali yake kabla ya kufuga bao la tatu la Liverpool
MBIO za kuelekea kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England baada ya miaka 24 kupita kwa Liverpool imekutana na vikwazo baada ya usiku wa jana kung'ang'aniwa na timu ya Crystal Palace na kutoka sare ya mabao 3-3, huku Suarez akizidi kutikisa nyavu akifikisha bao la 31.
Liverpool waliokuwa ugenini walifanikiwa kuongoza zaidi ya nusu ya mchezo huo wakiwa mbele kwa mabao 3-0, lakini cha ajabu mabao yote yalikuja kurejeshwa na wenyeji na kufanya wagane pointi moja moja, ambazo zinawarejesha Liverpool kileleni lakini wakiweka rehani matumaini yao ya ubingwa msimu huu.
Wageni walianza kuandika bao la kuongoza lililofungwa na Joe Allen katika dakika ya 18 kwa kumalizia kazi nzuri ya nahodha wake, Steven Gerrard na kudumu hadi wakati wa mapumziko.
Dakika nane baada ya kuanza kwa kipindi cha pili Daniel Sturridge aliifungia Liverpool bao la pili kabla ya dakika mbili baadaye Suarez kufunga bao lake la 31 katika msimu huu na kuifanya timu yake iongoze kwa mabao 3-0.
Hata hjivyo wenyeji walicharuka na kurejesha mabao hayo kupitia kwa Delaney aliyefunga dakika ya 79 na Gayle aliyefunga mabao mawili katiika dakika ya 81 na 88 na kuiduwaza Liverpool ambao wamesaliwa na mchezo mmoja,huku wapinzani wao,Manchester City waliowaoindoa kileleni kwa sare hiyo ya jana wamesaliwa na mechi mbili wakiwa na pointi 80.
Ligi hiyo itaendelea tena leo kwa pambano moja kati ya Manchestert United iliyotoka kupokea kipigo cha baoa 1-0 toka kwa Sunderland itakapoumana na Hull City.

Network Love ya Ruvu Stars videoni

Kiongozi wa Ruvu Stars, Khamis Amigolas
BENDI ya muziki wa dansi ya Ruvu Stars keshokutwa inatarajia kuanza kurekodi video za nyimbo zao tatu ambazo zinaendelea kutamba kwenye vituo mbalimbali vya redio nchini.
Akizungumza na MICHARAZO mmoja wa viongozi wa bendi hiyo ya maafande wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Rogart Hegga 'Katapila' alisema kuwa video hiyo itahusisha nyimbo zao za 'Network Love', 'Spirit' na 'Jua Kali' ambazo ndizo zilizolitambulisha kundi hilo kwa mashabiki wa muziki baada ya kusukwa upya likiwahusisha wanamuziki mahiri nchini.
Baadhi ya wanamuziki walionyakuliwa na kundi hilo ili kulisuka upya ni pamoja na Hegga, Khamis Kayumbu 'Amigolas', Khadija Mnoga 'Kimobitel', Jojo Jumanne, Victor Nkambi na rapa Msafiri Diouf.
Hegga alisema kazi hiyo ya kurekodi video hizo itaanza wiki hii na zoezi hilo litakapomalizika wataingia studio kumalizia nyimbo zao tatu za mwisho za kukamilisha albamu yao ya kwanza waliyopanga kuizindua baadaye mwaka huu.
"Tumesitisha zoezi la kumalizia nyimbo zetu tatu za kuhitimisha albamu ili kurekodi video za nyimbo za awali na kazi hiyo itafanywa katikati ya wiki chini ya kampuni moja ya jijini Dar es Salaam," alisema Hegga.
Alisema nyimbo za mwisho walizokuwa wameanza kurekodi ni 'Kioo' utunzi wake kiongozi mkuu wa bendi hiyo, Khamis Amigolas, 'Chewa Original' wa Seleman Muhumba na 'Facebook' wa Mkuu wa Jukwaa, Victor Nkambi ambaye pia ni 'mpapasa' kinanda mahiri nchini.

Matumla, Miyeyusho kuyeyushana Jumamosi PTA

Miyeyusho na Matumla wakiwa katika pozi. Wawili haowatapigana siku ya Jumamosi pale PTA
MABONDIA Francis Miyeyusho 'Chichi Mawe' na mtoto wa bingwa wa zamani wa dunia, Rashid Matumla, Mohammed Matumla 'Snake Boy Jr' watapanda ulingoni siku ya Jumamosi kuchapana katika pambano lisilo la ubingwa.
Aidha, mabondia hao wanatarajiwa kupima uzito na afya zao siku ya Ijumaa kwenye ukumbi wa Mango Garden, Kinondoni kabla ya kuvaana siku inayofuata kwenye ukumbi wa PTA, jijini Dar es Salaam.
Mabondia hao awali walipangwa kupigana Aprili 26, lakini likasogezwa mbele ili kupisha pigano la Miyeyusho dhidi ya Mthailand Sukkasem Kietyngyuth ambaye alimchapa Miyeyusho kwa TKO ya raundi ya kwanza.
Akizungumza na MICHARAZO, Rais wa TPBO-Limited inayosimamia pambano hilo, Yasin 'Ustaadh' Abdallah alisema pambano hilo lipo kama lilivyopangwa siku ya Mei 10.
Ustaadh alisema mabondia wote wapo kambini kujiandaa kwa ajili ya pambano hilo la kukata mzizi wa fitina baina yao baada ya kuwapo kwa tambo za muda mrefu. Miyeyusho amejichimbia mjini Bagamoyo na mpinzani wake yuko jijini Dar.
Rais huyo wa TPBO-Limited alisema maandalizi ya pambano hilo lililoandaliwa na promota Ally Mwazoa na litakalokuwa na michezo kadhaa ya utangulizi, yanaendelea vizuri.
Ustaadh alisema mapambano ya utangulizi siku hiyo yatakuwa kama ifuatavyo; Simon Zablon dhidi ya Keis Amary (kg 60), Mane Patrick dhidi ya  Sadiq Abdul (kg 50), Kassim Gamboo dhidi ya Kassim Rajab (Kg55), Azizi Abdallah atapigana na Ide Mnali (kg 60) na mkongwe Rashid Ally dhidi ya Suma Ninja (kg 60).

Monday, May 5, 2014

SIMANZI! Kidume Sheikh Ilunga Hassan Kapungu afariki dunia

Sheikh Ilunga Hassan Kapungu enzi za uhai wake.
MMOJA wa Wanaharakati na viongozi machachari wa Kiislam,  Sheikh Ilunga Hassan Kapungu amefariki dunia usiku wa kuamkia leo kwa ugonjwa wa Kisukari jijini Dar es Salaam. 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Sheikh Mohammed Kassim, Marehemu Sheikh Ilunga ambaye kwa siku za karibuni alikuwa akiandamwa kutokana na DVD zenye hotuba zake za kusisimua za kiharakati zilizokuwa zikiwaamsha waislam kutambua na kutetea haki zao  amezikwa leo majira ya saa 10 jioni baada ya mwili wake kuswaliwa msikiti wa Kichangani. Magomeni.
Inna Lillah Waina Illah Rajiun, Sheikh Ilunga katangulia nasi tu nyuma yake kwa sababu Kila Nafsi ni Lazima Itaonja Mauti.

Juventus mabingwa wapya Italia

http://cdn.bleacherreport.net/images_root/slides/photos/003/467/801/hi-res-454028537-gianluigi-buffon-of-juventus-fc-celebrates-victory-at_crop_650x440.jpg?1386971109MABINGWA watetezi wa Italia, Juventus ambao usiku huu wataingia uwanjani kupepetana na Atalanta wamejihakikishia ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo, Seria A baada ya wapinzani wao Roma kupoteza 4-1.
Kipigo hicho kimeifanya Roma kusaliwa na pointi 85 na michezo miwili ambapo hata kama wakishinda mechi hizo hawataweza kuzifikia pointi ilizonazo Juve ambazo ni 93 na kuwafanya kibibi cha Turin kuingia uwanja wa nyumbani wakiwa tayari mabingwa wa Seria A.
Katika mechi nyingine za jana nchini humo, AC Milan iliwashikika adabu wapinzani wao wa jiji la Milan, Inter Milan kwa kuwalaza bao 1-0, huku Parma wakishinda nyumbani mabao 2-0 dhidi ya Sampdoria, Udenese ikishinda pia nyumbani mabao 5-3 dhidi ya Livorno, Torino ikiiduwaza  Chievo Verona kwa kuwalaza bao 1-0 na Genoa na Bologna zilishindwa kutambiana kwa kutofungana.

Suarez ashinda tena tuzo England

http://thebeastbrief.com/wp-content/uploads/fbl-eng-pr-man_city-liverpool_yat6982_33846537.jpgNYOTA ya neema imeendelea kumuangazia Mshambuliaji mahiri wa klabu ya Liverpool, Luis Suarez baada ya kutajwa tena kuwa Mchezaji bora wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini Uingereza. 
Strika huyo kutoka Uruguay, aliyefunga mabao mabao 30 (kabla ya mechi ya usiku huu)msimu huu katika Ligi Kuu na kuiwezesha timu yake kufukuzia taji la ubingwa toka walipofanya hivyo mwaka 1990. 
Suarez, 27, alipata asilimia 52 ya kura zilizopigwa na waandishi hao akimshinda nahodha wake Steven Gerrard, huku Yaya Toure wa Manchester City akishika nafasi ya tatu. 
Mshambuliaji huyo hiyo ni tuzo ya pili baada ya wiki iliyopita alitajwa kama mchezaji bora na Chama cha wachezaji wa Kulipwa nchini humo (PFA) anatarajiwa kupokea zawadi yake hiyo katika sherehe za chakula cha usiku zitakazofanyika jijini London Mei 15.