STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, June 4, 2012

Kitale: 'Teja' la kwenye runinga lisiloujua 'unga'

KWA jinsi anavyoigiza na muonekano wake kama 'teja' katika baadhi ya kazi zake za filamu za kawaida na vichekesho, ni vigumu kuamini kuwa msanii Mussa Yusuph 'Kitale Rais wa Mateja' sio mtumiaji wa dawa za kulevya. Mwenyewe anadai hatumii kilevi cha aina yoyote zaidi ya kuigiza tu kama muathirika wa dawa hizo haramu za kulevya. Msanii huyo aliyewahi kutamba na makundi ya Kaole Sanaa na Fukuro Arts Professional, alisema watu wachache wanaoamini kama kweli hatumii kilevi. "Situmii kilevi chochote, sio pombe wala bangi, naigiza tu we mwenyewe unaniona bonge la HB au vipi?" Kitale alisema kwa utani alipohojiawa. Kitale alidokeza chanzo cha yeye kupenda kuigiza kama 'teja' aliyeathiriwa na 'unga' kiasi cha kuwa kibaka ni uzoefu alioupata kwa kuishi karibu na 'mateja'. Kitale, alisema jirani na kwao na sehemu kubwa ya Mwananyamala wapo vijana walioathiriwa na dawa hizo za kulevya, hivyo alikuwa akiwachunguza jinsi wanavyoongea, kutembea na maisha yao kwa ujumla na kujifunza mengi. "We unajua Mwananyamala na maeneo mengi ya uswazi kuna mateja wengi na bahati nzuri karibu na home kuna maskani yao ndio walionisaidia kunifanya niigize kama teja la kutupwa," alisema. Alisema mbali na uigizaji huo kuwa kama 'nembo' yake, lengo lake ni kuishtua jamii jinsi ya kuthibiti tatizo la dawa za kulevya, linaloteketeza kizazi na nguvu kazi ya taifa. "Naigiza hivyo, ili kuizindua jamii na kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya, dawa hizi zimekuwa zikiharibu na kupoteza nguvu kazi kwa jinsi zinavyoathiri na kuwa na madhara makubwa kwa taifa letu," alisema. Alisema japo wanaibuka wasanii wanaoigiza kama yeye (Kitale), msanii huyo alidai hana hofu kwa kutambua ataendelea kubaki kuwa Kitale na kamwe hajishughulishi na wasanii hao wanaoiga 'nembo' yake. "Kwa kweli wapo baadhi ya wasanii wameanza kuiga uigizaji wangu, ila sina hofu na wala muda wa kuwajadili, mie naendelea kupiga kazi kwani naamini nitaendelea kubaki kuwa Kitale aliye mmoja tu yaani Rais wa Mateja," alisema. Kitale, aliyeanzia sanaa tangu akiwa kinda wakati akisoma Shule ya Msingi, alisema licha ya umaarufu mkubwa alioupata kwa namna ya uigizaji huo wa kama 'teja' hasa alipong'ara katika tamthilia ya 'Jumba la Dhahabu', alidai wakati mwingine hupata usumbufu. "Ukiacha watu kunishangaa, wapo wengine hudhani uigizaji wangu ni uhalisia wa maisha yangu hivyo huniogopa wakidhani ni teja na kibaka, ingawa huwa naamini ujumbe nilioukusidia umefika kwa jamii," alisema. VIPAJI KIBAO Kitale, mchumba wa Fatuma Salum na baba wa mtoto mwenye umri wa miaka karibu miwili aitwae Ahmed, licha ya kuigiza pia ni mahiri kwa utunzi na utayarishaji wa filamu sambamba na akiimba muziki wa kizazi kipya. Kwa sasa mkali huyo anatamba na wimbo uitwao 'Hili Dude Noma' alioimba na kaka yake Mide Zo na Corner, kikiwa ni kibao cha pili kwake baada ya 'Chuma cha Reli' alichokitoa mwaka jana akiimba na mchekeshaji wenzake, Gondo Msambaa. Msanii huyo alisema kwa sasa anaendelea kumalizia kazi yake ya mwisho kabla ya kuhitimisha albamu itakayokuwa na nyimbo nane akizitaja zilizokamilisha kuwa ni 'Anajifanya Msela' alioimba na Juma Nature, 'Hili Toto' ft. Sharo Milionea na Mide Zo, 'Tulianzishe' na 'Kinaunau'. "Nimebakisha wimbo mmoja tu ambao nimeshautunga na kuufanyia mazoezi ila nasubiri kuafikiana na mmoja wa wasanii nyota nchini ili niurekodi," alisema. Hata hivyo Kitale alikiri kuwa, licha ya umaarufu mkubwa aliopata katika uigizaji, bado haridhiki na masilhai anayopata katika fani hiyo akidai hailipi kama ilivyo kwa muziki. Alisema, uigizaji haulipi kama muziki, lakini bado hana mpango wa kuachana na fani hiyo. "Kwenye uigizaji tunaambulia sifa tu, ila masilahi ni madogo mno tofauti na muziki, hata hivyo siwezi kuachana na fani hii kwani nimeshaizoea, na kwa sasa najiandaa kutoa kazi mpya nikishirikiana na Sharo Milionea," alisema. Alizitaja kazi hizo mpya ni; 'Sharo Madimpoz', 'Sharo Crazy', 'Sharo Taxi Driver' na 'Drug Dealer' wanazoziandaa na msanii mwenzake. Kitale alisema hizo ni baadhi ya filamu walizopanga kuzitoa ndani ya mwaka huu, sambamba na kuendelea na masuala ya muziki akidai kila mmoja imekuwa ikimpa mafanikio makubwa. FILAMU Kitale aliyezaliwa miaka kadhaa iliyopita mjini Morogoro ni shabiki mkubwa wa soka, mchezo aliowahi kucheza utotoni kabla ya kutumbukia kwenye uigizaji, akizitaka timu anazoshabikia kuwa ni Yanga na Manchester City. "Aisee katika soka huniambii kitu, licha ya kulicheza pia ni mnazi mkubwa wa Yanga na naipenda mno Manchester City," alisema. Kitale anayependa kula ugali kwa dagaa na kunywa vinywaji laini, alisema mbali na kucheza 'Jumba la Dhahabu' iliyompa umaarufu mkubwa, ameigiza pia filamu kama 30 na kushiriki kipindi cha vichekesho cha 'Vituko Show'. Alizitaja baadhi ya kazi hizo kuwa ni 'Back from Prisons', 'Mtoto wa Mama', 'Alosto', Mbwembwe', 'More than Lion' aliomshirikisha msanii wa muziki wa kizazi kipya wa kundi la Tip Top Connection, Abdulaziz Chende 'Dogo Janja'. Kitale, anayemzimia King Majuto aliyeigiza naye baadhi ya kazi, alisema fani ya sanaa nchini imepiga hatua kubwa, isipokuwa inakwamishwa na wajanja wachache wanaowanyonya wasanii na kuwafanya wasinufaike na fani hiyo. Alisema ni vema juhudi za kupambana na maharamia ikaongezwa, ili wasanii wa Bongo wanufaike na jasho lao na kuishi kama wasanii wa mataifa mengine ambao ni matajiri kuliko hata watu wa kada zingine. Kitale, anayefurahishwa na tukio la kuzaliwa kwa mwanae, akihuzunishwa na kifo cha mjomba wake aliyekufa kwa ajali ya gari, alisema matarajio yake ni kumuomba Mungu ampe umri mrefu na afya njema afike mbali kisanii. Alisema angependa kujikita zaidi katika muziki na kutoa kazi zake binafsi za filamu ili kunufaika na jasho lake baada ya kutumikia watu wengine bila kunufaika zaidi ya kuambulia sifa tu.

Drogba aimwagia sifa Taifa Stars, achekelea kuwatungua

NAHODHA wa timu ya taifa ya Ivory Coast, Didier Drogba, ameisifu timu ya Tanzania kwamba iliwapa wakati mgumu sana katika mechi yao ya raundi ya awali ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2014 kwenye Uwanja wa Felix Houphouet Boigny mjini Abidjan Jumamosi. "Ilikuwa ni mechi ngumu sana, lakini jambo la muhimu ni kwamba tumepata pointi tatu," alisema Drogba baada ya mechi hiyo ambayo wenyeji walishinda 2-0. "Kocha alikuwa na siku tatu za kuwa pamoja nasi, lakini tumeshinda mechi hivyo ni kazi nzuri kwake. Sasa tuna muda wa kufanya kazi pamoja naye na kujaribu kuboresha tulichofanya. Tutajiandaa na mechi ijayo dhidi ya Morocco kisha tuone nini kitatokea." Ivory Coast ilimfukuza kocha wake, Francois Zahoui na kumpa nafasi hiyo nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa, Sabri Lamouchi, siku tatu kabla ya mechi dhidi ya Stars. Ushindi unaifanya Ivory Coast kuongoza Kundi C la kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za Brazil 2014 ikiwa na pointi tatu baada ya Gambia na Morocco kutoka sare ya 1-1 katika mechi nyingine ya kundi hilo na kuzifanya kuwa na pointi moja kila moja baada ya mechi hiyo moja. Tanzania imeanza kwa kushika mkia ikiwa haina pointi. Baada ya kuanza vibaya, Stars imedhamiria kumalizia hasira zao kwa ushindi katika mechi yao ya pili dhidi ya Gambia Jumapili 10 jijini Dar es Salaam. Stars haijaonekana kurudishwa nyuma na kipigo kutoka kwa miamba hao wa Afrika na badala yake kikosi kilianza mazoezi jana asubuhi kwenye uwanja wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Ivory Coast (FIF) ambao uko pembezoni mwa jiji la Abidjan. Timu hiyo ilitarajia pia kutafanya tena mazoezi leo asubuhi asubuhi kabla ya kuanza safari ya kurejea nyumbani saa 1:30 usiku kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi ambapo itawasili Dar es Salaam kesho saa 1:40 asubuhi. Kocha Kim ambaye amekuja na wachezaji wote hapa ukiondoa wanne ambao ni majeruhi (Thomas Ulimwengu, Nurdin Bakari, Haruna Moshi na Nassoro Masoud Cholo) amesema hivi sasa wameelekeza akili yao kwenye mechi ijayo dhidi ya Gambia. “Safari ya kujenga timu ndiyo imeanza. Mechi dhidi ya Ivory Coast imepita na ninawashukuru wachezaji kwa kucheza kwa mujibu wa maelekezo na kujituma. Mpira ni mchezo wa makosa, tumefanya makosa yaliyosababisha tuwape Ivory Coast mabao mepesi," alisema kocha wa Stars, Kim Poulsen. “Lakini kama nilivyosema mechi hiyo imepita, hivi sasa tunaangalia mechi ijayo dhidi ya Gambia. Hatuna muda mwingine wa kujipanga na ndio maana niliamua kuja na wachezaji wote Abidjan,” amesema Kim. Mechi dhidi ya Gambia itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni. Gambia ilitoka sare ya bao 1-1 na Morocco katika mechi iliyochezwa juzi jijini Banjul. Stars itamkosa nahodha msaidizi Aggrey Morris ambaye alitolewa kwa kadi ya pili ya njano dakika ya 65 baada ya baada ya kumkwatua mchezaji wa Ivory Coast, Gosso Gosso. Morris alipewa njano ya kwanza katika dakika ya 12 baada ya kumkwatua Didier Drogba. Vikosi katika mechi hiyo vilikuwa; Ivory Coast: Boubacary Barry, Kolo Toure, Siaka Tiene, I. Lolo, Emmanuel Eboue, Cheik Tiote/Ya Konan, K. Coulibaly, Jean Gosso Gosso, Didier Drogba, Salomon Kalou/Max Gardel na Gervinho/Kader Keita. Tanzania; Juma Kaseja, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Mrisho Ngassa, Shaban Nditi, Mwinyi Kazimoto, Salum Abubakar/ John Bocco, Mbwana Samatta na Frank Domayo. CHANZO:NIPASHE

Wazee wa Ngwasuma kutumbuiza Miss Kigamboni

BENDI ya muziki wa dansi ya FM Academia maarufu kama 'Wazee wa Ngwasuma' na msanii wa vichekesho, Mpoki, wataburudisha wakati wa shindano la kumsaka mrembo kitongoji cha Kigamboni City 2012 litakalofanyika Juni 15 katika ukumbi wa Navy Beach, Kigamboni jijini Dar es Salaam. Mratibu wa shindano hilo, Somoe Ng'itu alisema kutakuwa na ushindani mkubwa katika shindano hilo kutokana na vimwana wakali waliopo kambini na bendi ya FM inafahamika kwa kutoa burudani nzuri kwa mashabiki wa muziki wa dansi nchini. Somoe alisema kuwa burudani nyingine kali itatoka kwa Mpoki ambaye mbali ya kuwa ni mkazi wa Kigamboni, lakini ukubwa wa kazi yake unafahamika na kwamba mashabiki watapaswa kuandaa mbavu za ziada kutokana na vichekesho vyake. Mratibu huyo kutoka kampuni ya K& L, alisema kuwa jumla ya warembo 15 wanaendelea kujifua katika kambi ya mazoezi chini ya mwalimu wao Miss Temeke, Hawa Ismail, ambaye anashirikiana na mshiriki wa Miss Tanzania mwaka jana Blessing Ngowi. Aliwataja warembo hao kuwa ni pamoja na Carolyne Dandu, Fatina Francis, Edda Slyvester, Aisha Mussa, Rosemary Peter, Doreen Kweka, Caroline Peter, Agnes Goodluck, Sophia Martine, Rosemary Deogratius, Beatrice Boniface, Julieth Philip na Khadija Kombo. "Kigamboni ni zaidi ya kitongoji, tunaamini shindano letu litakuwa na mvuto na hadhi ya kipekee kama eneo lake lilivyo," aliongeza. Somoe alisema kuwa warembo watakaofanya vizuri watapata nafasi ya kuwakilisha kitongoji hicho katika mashindano ya kanda ambayo yatafanyika baadaye mwaka huu. Aliwataja wadhamini ambao tayari wamethibitisha kuwezesha shindano hilo kuwa ni pamoja na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Redd's, Dodoma Wine na NSSF, Hope Country Motel, Norbro’s Collections, Screen Masters, Global Publishers. Salha Israel kutoka Kanda ya Ilala ndiye mrembo anayeshikilia taji la taifa ambapo mwaka huu ratiba ya mashindano hayo imebadilika. CHANZO:NIPASHE Warembo watakaochuana kwenye shindano la Miss Kigamboni 2012

Masai Nyota Mbofu aachia Rungu na Mukuki

MCHEKESHAJI maarufu nchini, Gilliad Severine 'Masai Nyota Mbofu', ameachia wimbo mpya uitwao 'Rungu na Mukuki' sambamba na video yake akishirikiana na wasanii wa kundi la Vichwa la Zambia, Simple K na G4. Tayari wimbo na video hiyo imeshaanza kurushwa hewani wakati mwenyewe akijiandaa kupakua kazi nyingine mpya. Akizungumza na MICHARAZO, Masai Nyota Mbofu, alisema wimbo huo ameurekodia nchini Zambia katika studio za Hez Sound chini ya Prodyuza, Acknex na video yake amefyatulia nchini humo na kuja kuimalizia Tanzania. Msanii huyo, alisema kazi hiyo mpya ni salamu kwa mashabiki wake waliomzoea kumuona katika filamu na komedi tu, kwamba kwenye muziki naye yumo. Masai Nyota Mbofu, alisema wakati wimbo na video hiyo ikiendelea kutamba ameanza kuandaa wimbo mipango ya kutoa kazi nyingine kwa lengo la kuja kufyatua albamu hapo baadae. "Wakati Rungu na Mukuki, ikiendelea kukimbiza kwa fideo na radio, tayari nimenza kuandaa kazi nyingine nataka onyesha mashabiki angu kwamba mi nawesa," alisema Masai kwa kiswahili kibovu cha kikomedi. Mkali huyo aliyeanza kutamba kwenye michezo ya runinga akiwa na kikundi cha Jakaya Theatre kabla ya kuibukia kwenye filamu chini ya kampuni ya Al Riyamy Production. Baadhi ya kazi zilizowahi kumpa ujiko msanii huyo ni Iny'e Plus, 'Iny'e Gwedegwede', 'Vumba Vimejaa', 'Pedeshee' na sasa anatamba na kipindi cha Vituko Show.

Mosha awachomolea wazee Yanga, fomu zachangamkiwa

HUKU zoezi la uchukuaji fomu za kuwania uongozi kwa ajili ya Uchaguzi wa klabu ya Yanga ukizidi kupambamoto, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo Davis Mosha amewachomolea wazee wa Yanga waliomtaka awanie tena uongozi akidai hana mpango huo. Aidha, kamati ya uchaguzi imekanusha taarifa kwamba Mfadhili Mkuu wa klabu huyo, Yusuf Manji amejityosa kuchukua fomu za kuwania Uenyekiti, ingawa kamati hiyo imesema milango i wazi kwake kama ana dhamira hiyo ya kuwania uongozi Yanga katika uchaguzi utakaofanyika Julai 15. Mosha, aliyefuatwa na wazee hadi nyumbani kwake Mikocheni juzi jijini Dar es Salaam, akijibu maombi ya baraza wazee lililomuomba kugombea moja ya nafasi katika uchaguzi huo na kusema hana mpango wa kuwania uongozi. Alisema kwa sasa hayuko tayari kugombea uongozi katika klabu lakini yupo tayari kusaidia kitu chochote kinachohitajika kwa maendeleo ya klabu. “NAwashukuru wazee kwa kuja kuniaona na kunipa pole, pia nashukuru kwa kuona umuhimu wa mimi kuwepo Yanga, ila napenda niwaeleze sintoweza kuwania uongozi kwa sasa, bali nipo tayari kuisaidia Yanga kwa lolote litakalokuwa ndani ya uwezo wangu,”alisema. “Mimi ni mpiganaji kweli, naiopenda Yanga na napenda iwe na maendeleo…nitashirikiana na viongozi watakaochaguliwa lakini mimi siwezi kuongoza Yanga kwa sasa nina mambo mengi ya kufganya,”alisema Mosha ambaye alijitoa madarakani miezi michache kabla iongeza kuwa wanachama wa Yanga hawana budi kuchagua viongozi ambao wapo tayari kuisaidia klabu hiyo na si kupata chochote. “Napenda kuwahadharisha wanachama wenzangu nkwamba tusikurupuke, tutafute watu wenye mapenzi ya kweli na si maslahi kwani Yanga ni kwa ajili ya kutumika si kuvuna,”alisema. Awali Katibu wa baraza hilo Ibrahim Akilimali ‘Abramovich’ kwa niaba ya wazee wengine wa Yanga ambao walikwenda nyumbani kwa Mosha kwa ajili ya kumpa pole kutokana na kufiwa na Mkwewe, aliwasilisha ombi la kumtaka Mosha kurejea kundini. Mzee Akilimali alisema kuwa wameamua kumuomba Mosha arejee kuongoza Yanga kutokana na umahiri mkubwa aliouonesha kipindi alichoongoza ambapo alikuwa mstari wa mbele kuisaidia timu hiyo na hatimaye kwa kipindi kifupi iliweza kupata mafanikio. “Mwanetu sisi wazee wako tumekuja kukupa pole lakini pamoja na hilo tunakuomba urejee kuongoza kwani bado tunakumbuka ushupavu wako katika kuongoza…kuna kombe la Kagame linakuja ambalo wewe ulichangia kwa kiasi kikubwa kupatikana, sasa uje ulibakize tena kombe hilo,”alisema Mzee Akilimali. Aidha , Mzee Akilimali aliongeza kuwa wanataka Yanga iingie kwenye mashindano na kushiriki hivyo mchango wa Mosha katika hilo ni muhimu sana. Uuchaguzi huo utajaza nafasi za viongozi waliojiuzulu na ile ya mjumbe mmoja aliyefariki dunia, ambapo viongozi watakaochaguliwa watakaa madarakani kwa muda uliosalia kama katiba inavyoelekeza na kwa mantiki hiyo viongozi hao watamaliza muda wao wa miaka minne mwaka 2014. Uchaguzi huo unafuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti Lloyd Nchunga baada ya kushinikizwa na baadhi ya wanachama wakiongozwa na baraza la wazee wa klabu hiyo kutokana na kushindwa kuiletea mafanikio klabu hiyo chini ya uongozi wake. Pia nafasi ya Makamu mwenyekiti iliyokuwa inashikiliwa na Davis Mosha ambaye alijitoa miezi michache baada ya kuchaguliwa kutokana na kutoelewana na Nchunga, huku mjumbe Theonest Rutashoborwa akitangulia mbele ya haki. Uchaguzi huo pia utajaza nafasi za Wajumbe walioachia ngazi ambao ni pamoja na Mzee Yusuf, Charles Mgondo na Ally Mayay. Kwa sasa Yanga imebaki na wajumbe wanne, Mohammed Bhinda, Sarah Ramadhan, Tito Osoro na Salum Rupia ambao baada ya uchaguzi wataungana na viongozi wapya na kuteua wajumbe wengine watatu kwa mujibu wa katiba, hiyo inatokana na wajumbe hao wa kuteuliwa Seif Ahmed, Mbaraka Igangula na Pascal Kihanga kujiuzulu. Katika hatua nyingine, wagombea watatu walijitokeza kuchukua fomu za kuwanmia nafasi ya ujumbe katika, wanachama hao ni pamoja na Jumanne Mwamamwenye na Salehe Hassan na Ayoub Nyenzi anayewania nafasi ya Makamu Mwenyekiti. Huku kamati ya uchaguzi ikikanusha taarifa kwamba Manji naye amejitosa kuchukua fomu kuwania Uenyekiti wa klabu hiyo, ingawa umesema milango i wazi kwake na kwa yeyote mwenye sifa kabla ya zoezi la kuchukua na kurudisha fomu kufungwa rasmi Jumatano jioni.

Simba noma, yabebe mzigo wa matibabu ya akina Boban

UONGOZI wa klabu ya Simba umesema kuwa umechukua jukumu la kuwatibu wachezaji wake Haruna Moshi 'Boban' na Nasoro Masoud 'Cholo' walioumia wakiwa na kikosi cha timu ya taifa 'Taifa Stars' baada ya kukatishwa tamaa na kusuasua kwa shirikisho la soka (TFF) kubeba gharama hizo. Akizungumza jijini Dar, Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala alisema kuwa klabu yake haina muda wa kusubiri matibabu ya TFF kwa wachezaji hao kwasababu ya kuzongwa na kalenda ya mashindano. Simba imeanza maandalizi kwa ajili ya mashindano ya klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati hivyo haiwezi kusubiri mpaka TFF liwatibie 'Boban' na 'Cholo'. Kauli hiyo ya Mtawala imekuja siku moja baada ya katibu mkuu wa TFF, Angetile Osiah, kusema bila kutaja tareeh rasmi kuwa shirikisho litafanya jitihada za kuwatibu wachezaji hao walioumia wakiwa ndani ya kikosi cha Stars. "Sisi ndio tunawalipa mshahara wachezaji hawa, na mtu akigundulika ameumia anatakiwa kutibiwa haraka na hakuna kusubiri," alisema. "Tumeanza kuwatibu ili kocha wetu atakaporudi awakute wachezaji katika hali nzuri na kuendelea na programu zake za mazoezi." Kocha wa timu hiyo Mserbia Milovan Cirkovic atarejea nchini Juni 15, alisema. Kocha huyo ametuma programu ya mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya Kombe la Kagame ambayo kwa sasa yanasimamiwa na kocha wa makipa wa timu hiyo James Kisaka. "Timu imeanza maandalizi chini ya Kisaka (James) kwa sababu kocha msaidizi naye ameenda mapumzikoni nchini kwao," alisema zaidi Mtawala. Alisema kocha msaidizi Richard Amatre ataungana na timu Alhamisi baada ya kuwasili nchini Jumatano. Mtawala alisema klabu hiyo imeweka malengo ya kutwaa ubingwa wa Kagame ambao unashikiliwa na watani zao Yanga walioutwaa kwenye mashindano ya mwaka jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuifunga Simba goli 1-0.

Noela ndiye Miss Tabata 2012

MREMBO Noela Michael, 19, usiku wa kuamkia juzi alifanikiwa kutwaa taji la Tabata 'Miss Tabata 2012' katika shindano lililofanyika kwenye ukumbi wa Da’ West Park jijini Dar es Salaam. Noela ambaye awali alibwagwa katika kuwania taji la talent aliweza kuwafunika warembo wengine 18 waliokuwa wanawania taji hilo lililokuwa linashikiwa na Faiza Ally. Noela alizawadiwa shilingi 500,000 na king’amuzi iliyolipiwa miezi sita iliyotolewa na Multichoice. Nafasi ya pili katika shindano hilo ilishikwa na Diana Simon, 20, aliyeshinda Sh 500,000 watatu ni Wilhemina Mvungi, 21, (Sh 350,000), wanne ni Phillos Lemi, 19, na Suzzane Deodatus, 20, alishika nafasi ya tano. Wote wawili walizawadiwa Sh 200,000 kila moja. Warembo hao watano watakiwakilisha Tabata katika mashindano ya Kanda ya Ilala yatakayofanyika baadaye mwaka huu. Warembo wengine waliofanikiwa kuingia hatua ya 10 walikuwa ni Angel Kisanga, Khadija Nurdin, Haika Joseph, Queen Issa na Neema Saleh. Wote walizawadiwa Sh 100,000 kila moja. Queen Issa alifanikiwa kutwaa taji la mrembo mwenye kipaji cha kucheza huku Mercy Mlay akiteuliwa kuwa mrembo aliyekuwa na nidhamu ya juu tangu kuanza kwa shindano hilo. Queen na Mercy kila moja alizawadiwa Sh 100,000. Warembo waliosalia walipata kifuta jasho cha Sh 50,000 kila moja. Shindano hilo lilipambwa na burudani kutoka kwa bendi ya Mashujaa, Mashauzi Classic iliyoko chini ya Isha Ramadhani Mfalme na Costa Sibuka. PICHA Tofauti za matukio ya Miss Tabata 2012, ambapo Noela Michael aliibuka kidedea.

Saturday, June 2, 2012

Mr Blue, Malaki wachanganywa na Msichana Mzuri

Malaki MSANII anayekuja kwa kasi nchini, Sela Myovela 'Malaki' ameachia ngoma mpya iitwayo 'Msichana Mzuri' aliyoimba akishirikiana na mkali wa R&B, Khery Sameer Rajab maarufu kama Mr Blue au 'Kabaysa'. Akizungumza na MICHARAZO, Malaki aliyewahi kufyatua ngoma nyingine kali iitwao 'Maisha' aliyoimba na mkali wa Bongofleva nchini, Juma Kassim Kiroboto 'Sir Juma Nature' alisema wimbo huo mpya ameurekodia katika studio za Fishcrab chini ya prodyuza matata, Lamar. Malaki alisema wimbo huo uliopo katika miondoko ya R&B ni maalum ya ujio wake mpya chini ya usimamizi wa kaka yake, Mfaiswa Myovela 'Mzee wa FilamuCentral'. "Baada ya kimya kirefu cha miaka kama mitano, nimekuja na ngoma mpya kabisa iitwayo 'Msichana Mzuri' niliyopigwa tafu na Mr Blue, ikifanywa chini ya Lamar wa Fishcrabs Studio," alisema. Alisema, tayari wimbo huo ameshausambaza katika vituo vya redio na kuanza kurushwa hewani, huku mwenyewe nakijipanga kwa ajili ya kuitolea video yake. Aliongeza, lengo lake ni kufyatua albamu hapo baadae ingawa alisema kwa sasa ataendelea kudondosha wimbo mmoja mmoja kwa ajili ya kuweza kujitangaza na kupata shoo zitakazomwezesha kupata fedha za kukamilishia albamu hiyo. Malaki alitumbukia kwenye muziki wa kizazi kipya tangu mwaka 2005 na kutoa kazi yake ya kwanza kabisa akiwa na Juma Nature mwaka 2007 kabla ya kuwa kimya hadi mwaka huu alipotoka na 'ngoma' hiyo mpya.
Mr Blue katika pozi zake.

'Maafande' wamnyemelea Ngassa

KLABU nne tofauti zimekuwa zikimnyatia mshambuliaji mahiri wa timu ya Moro United, Benedict Ngassa, kwa ajili ya kutaka kumnasa ili wazichezee timu zao katika msimu moya wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Akizungumza na MICHARAZO, Ngassa alizitaja klabu hizo zinazomnyemelea kuwa ni JKT Ruvu, Ruvu Shooting, African Lyon na timu iliyopanda daraja ya Prisons ya Mbeya. Ngassa alisema viongozi wa klabu hizo kwa nyakati tofauti wamekuwa wa kiwasiliana nae na kufanya mazungumzo ingawa alikiri bado hajaafikiana nao mpaka sasa. "Licha ya kufuatwa na viongozi wa klabu hizo, bado sijaamua niende wapi, nitaangalia kwanza masilahi," alisema. Aliongeza kuwa, ingawa anafurahia kunyatiwa na timu hizo, lakini roho yake inamuuma kwa timu yake ya Moro United kushuka daraja akielekeza lawama zake kwa wachezaji walioichezea timu hiyo kwa mkopo. Ngassa, alisema wachezaji waliotua katika timu hiyo kwa mkopo toka klabu mbalimbali nyingine za ligi kuu walikuwa wakiihujumu timu yao ambapo licha ya wachezaji halisi wa Moro kujituma na kuifungia mabao, magoli hayo yalikuwa yakirejeshwa kitatanishi. "sio siri tumeshushwa daraja na wachezaji waliokuja Moro kwa mkopo, inauma sana," alisema. Moro United iliyokuwa imerejea tena Ligi Kuu imejikuta ikishuka daraja ikiungana na timu za Villa Squad na Polisi Dodoma kutokana na kujikusanyia pointi chache katika mechi 26 ilizocheza msimu huu ambapo Simba waliibuka mabingwa.

Bondia Magoma Shaaban afariki, azikwa kwao Tanga

ALIYEKUWA Bingwa wa Dunia wa WBU uzani wa Super Fly, Magoma Shaaban amefariki dunia na kuzikwa kwao mkoani Tanga. Kwa mujibu wa mdau mkubwa wa mchezo wa ngumi ambaye pia ni promota, Ibrahim Kamwe, Magoma alikumbwa na umauti juzi kwenye hospitali ya Bombo mkoani Tanga. Magoma alikuwa amelazwa katika hospitali hiyo siku nne zilizopita kutokana na kuzidiwa na maradhi aliyokuwa nayo siku nyingi na kufariki majira ya jioni na alizikwa jana nyumbani kwao Mabovu Mwembesamaki, mjini Tanga. Marehemu aliyeacha mjane na watoto wawili Sudi,10 na Almasi,7 alizaliwa Oktoba 21, 1980 mjini Tanga na alianza kucheza ngumi tangu akiwa kinda akipitia klabu mbalimbali za ngumi za ridhaa kabla ya kuingia za kulipwa mwaka 1996 alipopanda ulingoni kuzipiga na Athumani Omari na kushinda kwa pointi. Hadi mauti yanamkuta bondia huyo aliyekuwa mfupi lakini machachari, alikuwa amepigana mapambano 16 na kushinda 13 kati ya hayo mapambano manne akishinda kwa KnockOut (KO) na kupigwa matatu pia kwa KO. Mara ya mwisho kupanda ulingoni ilikuwa Julai 21 mwaka 2006 na Eugen Sorin Tanasie mjini Timisoara, Romania katika pambano ambalo alipigwa kwa Technical Knockout (TKO) raundi ya pili. Taji lake la kwanza kutwaa lilikuwa ni la IBF Afrika, Septemba 12, mwaka 1998 akimpiga Mkenya Joseph Waweru kwa KO raundi ya kwanza, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Mei 11, mwaka 2000 alimpiga bondia ‘matata sana’ Totin Lukunim wa Thailand na kutwaa taji la IBF Intercontinental, uzito wa Super Fly kwenye ukumbi wa PTA, Temeke, Dar es Salaam. Agosti 3, mwaka 2001 ndipo alitwaa ubingwa wa dunia wa WBU baada ya kumpiga Ferid Ben Jeddou wa Tunisia kwa TKO raundi ya sita mjini Avezzano, Abruzzo, Italia, kabla ya kupoteza taji hilo kwa kupigwa na Gabula Vabaza Julai 26, mwaka 2002 katika ukumbi wa Hemingways Casino, East London, Eastern Cape, Afrika Kusini kwa KO raundi ya kwanza. Mei 25, mwaka 2003 alipigwa na Mtanzania mwenzake, Mbwana Matumla kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam kwa TKO raundi ya nne. Wadau mbalimbali wa ngumi wameelezwa kusikitishwa na kifo cha Magoma, wakiitaka familia, ndugu, jamaa na rafiki zake kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu wakiwakumbusha kuwa kazi ya Mola huwa haina makosa.

Friday, June 1, 2012

Costa, Jabu, Kago watupiwa virago Simba, wanne wajaza nafasi zao

NYOTA watano wa kikosi cha Simba ambao kwa kiasi kikubwa waliisaidia timu hiyo kung'ara msimu huu wamedaiwa kutupiwa virago, huku nafasi zao zikichukuliwa na wakali wanne waliosajiliwa mpaka sasa ndani ya kikosi hicho. Habari za kuaminika ambazo zimenaswa jijini ni kwamba wachezaji walitupiwa virago ni nyota wa kimataifa toka Jamhuri wa Kati, Gervais Kago, mabeki wa kati Victor Costa na Juma Nyosso, Juma Jabu na Ulimboka Mwakingwe aliyekuwa majeruhi kwa muda mrefu. Aidha kuna taarifa nyingine kwamba naye Uhuru Seleman yupo katika mchakato pia wa kutemwa katika kikosi hicho iwapo atafanikiwa kupata timu, ikidaiwa ananyemelewa na Yanga. Kwa mujibu wa chanzo cha habari toka ndani ya Simba, ni kwamba Costa, Jabu na Kago wametemwa kwa kushuka viwango, huku Nyosso anaysakwa na Yanga pia, ametemwa kutokana na utovu wa nidhamu wa mara kwa mara anaoufanya dimbani na kuigharimu timu, huku Mwakingwe kwa umri na kuwa majeruhi wa muda mrefu. Nafasi za wachezaji hao mpaka sasa zimechukuliwa na wakali wanne walionaswa Msimbazi ambao ni Juma Abdallah, Mussa Mudde Mbongo aliyekuwa akicheza SOFAPAKA, Patrick Nkanu toka Congo na Ibrahim Rajab 'Jebba'. Viongozi wa Simba walinukuliwa jana kwamba, zoezi zima la usajili wa timu yao utaanikwa baada ya kamati zao za ufundi na mashindano kuendesha zoezi hilo kwa maelekezo ya kocha wao, Cirkovic Milovan. Zoezi la usajili nchini kwa timu za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2012-2013 umefunguliwa rasmi leo Juni Mosi na unatarajiwa kumalizika mwanzoni mwa Julai kabla ya Ligi kuanza Agosti ambapo miongoni mwa timu zitakazoshiriki ni Polisi Moro, Mgambo Shooting ya Tanga na Prisons ya Mbeya zilizopanda daraja toka la Kwanza.

Wema Sepetu afafanua pete aliyovishwa Maisha Club

MSANII nyota wa filamu nchini, Wema Sepetu amefafanua uvumi ulioenea jijini Dar kwamba ameangukia kwenye penzi na mwanamuziki wa bendi ya Machozi, Mwinyi kiasi cha kuvishwa pete ya uchumba kama alivyofanyiwa na aliyekuwa boifrend wake, Naseeb Abdul 'Diamond' kabla ya kumwagana hivi karibuni. Wema alisema pete aliyovishwa mwishoni mwa mwezi uliopita ilikuwa ni igizo la filamu aliyokuwa akiishoot iitwayo 'Super Star' kazi binafsi anayokuja nayo ambayo sehemu kubwa inahusu maisha yake halisi. Mrembo huyo alisema wengi walishindwa kuelewa walipomuona akivishwa pete na Mwinyi na kukumbatiwa huku wakipigana mabusu kwa kuwa kamera zilizokuwa zikitumika kutengenezea filamu hiyo zilikuwa juu na hivyo hazikuonwa na watu. "Sio kweli kama nimechumbiwa na Mwinyi wa Machozi, ila tulikuwa tukiigiza filamu yangu ya kwanza binafsi iitwayo 'SUPER STAR' ambayo ni kama inazungumzia maisha yangu," alisema. Mwinyi amecheza kama Diamond katika filamu hiyo ambapo aliwahi kumvisha pete na kutamka maneno ya kusisimua kabla ya kuja kugeukana. Wema alisema filamu hiyo anatarajia kuizindua Juni 23 baada ya kukamilika na imemgharimu karibu Sh Milioni 30 mpaka sasa. Miss Tanzania huyo wa 2006 amesema filamu hiyo imewashirikisha wasanii kadhaa nyota, na anatarajia itakuwa filamu ya kusisimua kutokana na kuigiza sehemu kubwa katika uhalisi wa maisha yake kama WEMA SEPETU.

YANGA MPO? RATIBA YA UCHAGUZI WENU HII HAPA

Stars yafika salama Abidjan, kuwavaa Tembo wa Ivory Coast kesho

Kikosi cha Taifa Stars kimewasili salama mjini Abidjan mchana wa jana huku Kocha Mkuu wa timu hiyo Kim Poulsen akisema mechi dhidi ya Ivory Coast itakuwa ngumu. Kwa mujibu wa ofisa habari wa TFF Boniface WAmbura ambaye ameambatana na timu, Stars yenye wachezaji 21 ilikuwa iwasili hapa asubuhi, lakini ndege iliyobadilisha Nairobi ilichelewa kuondoka kwa saa tatu. Mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Taifa Stars na wenyeji Ivory Coast (Tembo) itachezwa Juni 2 mwaka huu Uwanja wa Felix Houphouet-Boigny kuanzia saa 11 kamili jioni ambapo Tanzania itakuwa saa 2 kamili usiku. Licha ya kwanza, Stars ililazimika kuacha wachezaji wawili dakika za mwisho (Haruna Moshi na Nassoro Cholo), Kim amesema kikosi chake ambacho kimefikia hoteli ya Ibis bado kimejipanga vizuri kwa ajili ya mechi hiyo. “Tunaiheshimu Ivory Coast kwa vile ni timu ambayo inaundwa na baadhi ya wachezaji nyota wa dunia kama akina Drogba (Didier) na Yaya (Toure), lakini wajiandaa kupata wakati mgumu kutoka kwetu,” amesema Kim ambayo kikosi chake baada ya kuwasili hapa kilipata fursa ya kufanya mazoezi jioni. Kikosi cha Stars kinaongozwa na nahodha wake Juma Kaseja akisaidiwa na Aggrey Morris. Wachezaji wengine waliopo hapa na kikosi hicho ni Mwadini Ally, Deogratius Munishi, Amir Maftah, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Waziri Salum, Shomari Kapombe na Juma Nyoso. Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Salum Abubakar, Shabani Nditi, Edward Christopher, Mrisho Ngasa, Frank Domayo, Mbwana Samata, Ramadhan Singano, Simon Msuva na John Bocco. Mbali ya Kim, Benchi la Ufundi lina Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold Mukebezi (Meneja wa timu), Juma Mwankemwa (Daktari wa timu), Frank Mhonda (Physiotherapist) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).
Msafara wa Stars hapa unaongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Crescentius Magori lakini pia yupo Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi ambaye amekuja kushuhudia mechi hiyo.

Kipa Lyon akiri udhaifu, ajipanga

MLINDA mlango wa kutumainiwa wa timu ya African Lyon, Noel Lucas, amekiri kuwa msimu uliopita timu yao haikuwa katika ubora wake, huku mwenyewe akishuka kiwango jambo lililosababisha timu yao kunusurika kushuka daraja. Hata hivyo, alisema yeye binafsi amekuwa akitumia muda wake wa mapumziko kwao Kigoma kujifua ili kurejesha kiwango chake na akiamini pia usukwaji upya wa kikosi chao unaweza kutoa ushindani mkubwa katika msimu ujao. Akizungumza na MICHARAZO
kwa njia ya simu kutoka Kigoma, Lucas alisema Lyon kwa msimu uliopita ilicheza chini ya kiwango na kusababisha kuwa na wakati mgumu kabla ya kunusurika kushuka daraja dakika za mwisho. Kipa huyo aliyepoteza namba kwa kipa mwenzake Abdul Seif, alisema hata hivyo anashukuru timu yao kupona kurudi Ligi Daraja la Kwanza, akiamini msimu ujao itakuwa timu tishio huku mwenyewe akidai anajipanga upya. "Najipanga kurejesha makali yangu, sio siri msimu uliopita sikuwa katika kiwango kabisa na ndio maana nilipoteza namba," alisema Lucas. Kipa huyo ambaye kabla ya kutua Lyon alitamba timu za Small Boys ya Singida, FC Congo ya Kigoma na Toto Afrika ya Mwanza na mwaka jana kuipa Kombe la Taifa mkoa wa Singida 'Kindai Shooting' kwa mara ya kwanza mkoa huo kufanya hivyo.

Coastal yamng'ang'ania Nsa Job

UONGOZI wa klabu ya Coastal Union ya Tanga, umesisitiza kuwa umeshamalizana na mshambuliaji wa Villa Squad, Nsa Job, aliyedai bado hajasaini kwao. Aidha, uongozi huo umetangaza kuwanasa nyota wengine wawili, Selemain Kassim 'Selembi' aliyekuwa akiichezea African Lyon kwa mkopo akitokea Azam na Mohammed Soud wa Toto Afrika ya Mwanza. Afisa Habari wa Coastal Union, Eddo Kumwembe, aliiambia MICHARAZO kuwa, Nsa aliyenukuliwa hajasaini kokote, ameshamwaga wino kwao tangu wiki iliyopita hivyo ni mali yao kwa ajili ya msimu ujao. Kumwembe alisema, Nsa ni mmoja kati ya wachezaji watatu ambao wameshamalizana nao mpaka sasa kwa ajili ya kusuka kikosi chao kwa msimu ujao, wengine wakiwa ni Selembi. "Nsa ni mmoja wa wachezaji wetu wapya ameshasaini fomu za usajili tangu karibu wiki sasa, tunashangaa akituruka, ila huenda hakupenda watu wajue mapema, lakini ukweli ndio huo msimu ujao ni wetu," alisema. Msemaji huyo aliongeza kuwa mbali na wachezaji hao watatu, pia wanakaribia kumnasa kinda wa timu ya taifa, (Taifa Stars), Simon Msuva aliyekuwa katika timu iliyoshuka daraja ya Moro United akitokea kikosi cha U-20. "Kwa sasa tunamfukuzia Msuva ambapo tunakaribia kumnasa," alisema Kumwembe. Coastal Union iliyorejea Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu na kumaliza katika nafasi ya tano, tayari imetangaza kuwatema wachezaji wake tisa akiwemo Ally Ahmed Shiboli aliyemwaga wino Polisi Moro iliyopanda daraja msimu huu. Wengine waliotemwa sambamba na Shiboli ni Ramadhani Wasso, Ben Mwalala, Samuel Temi, Enock John, Laurent Mugia, Bakari Mohamed, Daudi Changula na Francis Busungu.

Malipo kiduchu yamkimbiza bondia ulingoni

BONDIA machachari wa ngumi za kulipwa nchini, Saleh Mkalekwa, amesema malipo madogo wanayolipwa mabondia wengi akiwemo yeye yamefanya wengi wao kufa maskini, jambo linalomfanya afikirie kuachana na mchezo huo kabla ya kutimiza ndoto zake. Akizungumza na MICHARAZO
, Mkalekwa mwenye rekodi ya kucheza mara saba, akishinda sita na kupoteza moja, alisema alipotumbukia katika ngumi alikuwa na ndoto nyingi ikiwemo kutamba kimataifa, ila amekatishwa tamaa na malipo kiduchu anayolipwa. Alisema hali ya kulipwa kidogo haipo kwake tu, bali karibu mabondia wote ambao licha ya kuhatarisha maisha yao wamekuwa hawathaminiwi zaidi ya kuwanufaisha wasimamizi wa mchezo huo wakiwemo mapromota. Mkalekwa alisema kutokana na hali hiyo anafikiria kuachana na mchezo huo kwani haoni faida anayopata zaidi ya kuhatarisha maisha yake na kuwanufaisha waandaaji ambao wamekuwa wakiweka mbele masilahi yao kuliko ya mabondia na ngumi kwa ujumla. "Kwa kweli nilitamani mno kufika mbali kama walivyofika wakali wengine, lakini kwa jinsi tunavyonyonywa na kutumiwa kuwaneemesha wengine, ngumi zimenitumbukia nyongo," alisema. Alisema tangu alipoanza kupanda ulingoni mwaka 2008 hajawahi kulipwa pigano lolote malipo yanayozidi Sh 100,000, licha ya gharama kubwa za kuajiandaa na michezo hiyo kitu ambacho akihoji anaambiwa acheze kwanza ili akuze jina lake. "Wenzetu katika soka, hata kama ni chipukizi, wanalipwa fedha ambazo zinawatia nguvu kuendelea kuufurahia mchezo huo sio sisi, ndio maana unaona nimejiweka kando nikijifanyia mazoezi mwenyewe nikishughulisha na biashara ya spea za magari," alisema. Hata hivyo bondia huyo alisema iwapo atafanikiwa kupata mtu wa kumsaidia kumtafutia michezo yenye malipo ya kuridhisha na hasa ile ya kimataifa atakuwa tayari kuendelea na ngumi.

Hili Dude la Kitale videoni

VIDEO ya wimbo mpya wa mchekeshaji maarufu nchini, Mussa Yusuf 'Kitale' uitwao 'Hili Dude' inatarajiwa kuanza kurekodiwa wiki hii. Kitale, alisema atarekodi video hiyo baada ya kuona wapenzi wa muziki wameupokea vizuri wimbo wake huo ulioanza kushika chati katika vituo mbalimbali vya redio. Wakati msanii huyo akimalizia wimbo wa mwisho kuhitimisha albamu yake ya kwanza, alisema, wakati akianza kurekodi video hiyo, pia anajipanga kumalizia wimbo wa mwisho kwa ajili ya albamu yake itakayokuwa na jumla ya nyimbo nane. "Najiandaa kurekodi video ya wimbo wangu mpya wa 'Hili Dude' wakati pia nikijipanga kumalizia wimbo wa mwisho kwa ajili ya albamu yangu ya kwanza," alisema. Alisema mpaka sasa amekamilikisha nyimbo saba alizoshirikiana na wasanii mbalimbali akiwemo Sir Juma Nature na kuzitaja baadhi yake kuwa ni 'Chuma cha Reli', 'Kama Vipi Tulianzishe', 'Anajifanya Msela', 'Kinaunau' na 'Hili Dude'. Kitale, alisema amepanga hadi Julai awe ameikamilisha albamu yake itakayofahamika kwa jina la 'Kama Vipi Tulianzishe' sambamba na video ya nyimbo zote za albamu hiyo.

Loveness apika nyingine mpya

MSANII na mtayarishaji wa filamu anayekuja juu nchini, Loveness Watson 'Love' yupo jikoni akipika kazi nyingine mpya baada ya filamu yake ya 'Impossible Promise' kufanya vema sokoni. Akizungumza na MICHARAZO, Loveness alisema kama ilivyokuwa kwa kazi ya awali ya 'Impossible Promise, filamu hiyo nyingine ameitunga kuiandika na atatayarisha yeye mwenyewe. Loveness alisema, kazi hiyo mpya itakuwa na simulizi la mapenzi ambapo atashirikiana na wakali kadhaa nchini kuicheza filamu hiyo. "Baada ya kuitoa filamu yangu ya 'Impossible Promise' inayofanya vema sokoni kwa sasa nipo jikoni napika kazi hiyo ambayo natarajia kuiachia kabla ya Agosti," alisema. Aidha msanii huyo alisema pia yupo katika maandalizi ya kutumbukia kwenye muziki, akidai fani hiyo aliifanya siku za nyuma kabla ya kuingia kwenye uigizaji wa filamu kwa ushawishi wa kaka yake aliyemtaja kwa jina la Yokania Watson. Alisema tofauti na wasanii wenzake kuimba miondoko mchanganyiko, yeye atajikita zaidi katika mirindimo ya R&B.

Miss Tabata kufanyika leo, Mashauzi na Mashujaa Band kunogesha uhondo

Shindano la kusaka Miss Tabata 2012 linafanyika leo (Ijumaa) katika ukumbi wa Da’ West Park, Tabata. Mratibu wa shindano hilo Joseph Kapinga alisema jana kuwa bendi za Mashauzi Classic na Mashujaa zitawasindikiza warembo 19 watakaopanda jukwaani kuwania taji hilo. Mratibu wa shindano hilo lililoandaliwa na Bob Entertainment na Keen Arts alisema kuwa mshindi wa kwanza atazawadiwa Sh 500,000/- na king’amuzi ambayo imelipia miezi sita yenye thamani ya sh 800,000 iliyotolewa na Multichoice. Mshindi wa pili atapata sh 500,000, mshindi wa tatu sh 350,000 wakati washindi wa nne na watano kila moja atapata sh 200,000. Kapinga alisema warembo watano watawakilisha Tabata kwenye shindano la Miss Ilala. Warembo wengine watakaoingia 10 bora kila moja atapata sh 100,000 wakati waliyosalia watapata Sh 50,000 kila moja. Kapinga alisema shindano hilo pia litatumika kwa ajili ya kusherehekea miaka 10 tangu kuasisiwa kwa shindano la Miss Tabata. “Shindano la mwaka huu sio la kukosa kwani litakuwa ni la aina yake ukizingatia kuwa litatumika kusherekea miaka 10 tangua kuanza kuandaa Miss Tabata,” alisema Kapinga. Alisema warembo waliyowahi kushinda mataji mbalimbali ya shindano hilo, pia wamealikwa kusherehekea miaka 10 ya Miss Tabata. Shindano hili limedhaminiwa na Dodoma Wine, Redds, Integrated Communications, Fredito Entertainment, Multichoice Tanzania, Screen Masters, Kitwe General Traders, Step In Electronics, Brake Point, Atriums Hotel na Lady Pepeta. Mrembo anayeshikilia taji la Tabata kwa sasa ni Faiza Ally. Warembo wa Tabata wamekuwa wakifanya vizuri katika mashindano ya Miss Tanzania ambapo mwaka juzi Consolata Lukosi alishinda nafasi ya tatu kabla ya kutangazwa kuwa balozi wa kinywaji cha Redds. Katika shindano la mwaka juzi Juliet William pia alishinda nafasi ya tatu katika ngazi hiyo ya taifa. Juliet ndiye anayeshikilia taji la dunia la Miss Progressive International.
Washiriki wa Miss Tabata

Monday, May 28, 2012

Uigizaji haulipi kama muziki-Kitale

MSANII KITALE AKTIKA KATIKA POZI TOFAUTI
MSANII nyota wa filamu cha vichekesho nchini, Mussa Yusuf 'Kitale' amedai licha ya fani ya uchekeshaji kutolipa kama muziki, lakini katu hawezi kuachana na fani hiyo. Akizungumza na MICHARAZO, Kitale alisema ndio maana kwa sasa akishirikiana na Husseni Mkiety 'Sharo Milionea' wameandaa filamu zao binafsi zaidi ya tano. Alisema katika muziki msanii ananufaika kwa vile huwa ni kazi yake binafsi tofauti na filamu ambapo mabosi ndio wanaoneemeka na msanii hutumika tu kama kibarua. "Kwenye filamu na uchekeshaji tunaambulia sifa tu, lakini kimasilahi ni kidogo tofauti na muzikio, hata hivyo siwezi kuachana na fani hii kwani nimeshaizoea na kwa sasa kuna kazi mpya ninazoandaa na Sharo Milionea," alisema. Alizitaja kazi hizo kuwa, "Sharo Madimpoz', 'Sharo Crazy', 'Sharo Taxi Driver' na 'Drug Dealer' ambazo anaziandaa kwa kushirikiana na Sharo Milionea ambaye wamekuwa wakiendana katika uigizaji wao. "Hizi ni baadhi ya filamu tutakazotoa ndani ya mwaka huu, sambamba na kazi zetu za muziki ambazo kila mmoja anaifanya na kumpa mafanikio makubwa," alisema. Kitale anayeigiza kama 'teja', alisema amepanga kabla ya kumalizika kwa mwaka huu albamu yake binafsi iwe imeshaingia sokoni.

Manyika avunja ukimya na Wololowololo

NYOTA wa zamani wa Yanga aliyetumbukia kwenye muziki, Manyika Peter, ameachia wimbo mpya uitwao 'Wolowolo', akijiandaa kutolea video yake. Akizungumza na MICHARAZO, kipa huyo aliywahi kung'ara na timu za Mtibwa Sugar, Sigara, Yanga na klabu kadhaa za kimataifa alisema kazi hiyo ni ya pili tangu alipotoa albamu yake mwaka 2004. Manyika, alisema 'Wololowololo' umetoka ikiwa ni miaka minne tangu atoe wimbo wake wake wa mwisho mwaka 2007 uitwao 'Manabii'. "Baada ya kimya kirefu nimetoka na wimbo wa 'Wololowololo' ninaouandalia video yake, hiki ni kibao cha pili baada ya albamu yangu ya 'Unanipeleka Puta' ilitoka mwaka 2004," alisema. Manyika, alisema tofauti na alipotumbukia kwenye fani hiyo mwaka 2001 wakati akiwa anaichezea Yanga, kwa kutoa albamu, safari hii hana mpango huo kwa madai utoaji wa albamu haulipi kama kutoa 'singo'. "Sina mpango wa kutoa albamu, nitaendelea kutoa wimbo mmoja mmoja kwa lengo la kupata shoo ambazo ndizo zinazolipa vema," alisema. Alisema wakati akihangaikia kuitolea video wimbo huo wa 'Wololowololo', tayari kuna nyimbo nyingine mbili ameshaziandika ambazo atazirekodi baadae ili kudhihirisha nia yake ya kujikita jumla kwenye muziki.
MANYIKA PETER KATIKA POZI TOFAUTI KAMA MSANII WA MUZIKI WA KIZAZI KIPYA

Mpeni muda Kim atufikishe mbali kimataifa-Manyika

NYOTA wa zamani wa kimataifa aliyewahi kuzichezea timu za Mtibwa, Sigara na Yanga, Manyika Peter, amewataka wadau wa soka nchini kumpa muda kocha Kim Poulsen, ili afanye kazi zake kwa manufaa ya soka la Tanzania. Pia, aliwataka wadau hao kutoweka matumaini makubwa ya timu yao ya taifa, Taifa Stars kufuzu fainali za Afrika 2013 au Kombe la Dunia 2014, ila nguvu ziwekezwe kwa fainali za mbele zaidi akiamini timu itakuwa imewiva. Manyika, alisema Tanzania imekuwa ikikwama kufika mbali kwa vile makocha wanaozifundisha timu za taifa na hata klabu hawapewi muda mrefu wa kukaa na timu husika, kitu alichotaka kisitokee tena kwa kocha wa sasa wa Stars. "Tumpeni nafasi Kim aweze kufanya kazi zake na naamini kwa uwezo alionao tunaweza kufika mbali zaidi na hapa tulipo, ila kama tutaendelea na tabia ya kulaumu kisha aondolewe tutadumaa hapa hapa kisoka," alisema. Alisema Kim, ni mmoja wa makocha wazuri kutokana na kufanya nae kazi akiwa kama Mkufunzi wa FIFA wa makipa wa timu za taifa za vijana, hivyo aliwataka wadau wa soka wasimbughudhi ili afanye kazi zake kwa ufanisi. Aliongeza, licha ya kuwataka wadau wawe na subira pia wasiweke tumaini kubwa la Tanzania kufuzu fainali zijazo za Afrika zitakazofanyika Afrika Kusini au Kumbe la Dunia la Brazil, ingawa alikiri lolote linaweza kutokea. "Tukifuzu itakuwa ni bahati, lakini nadhani tunapaswa kuweka nguvu kwa ajili ya fainali za mbele, tumechelewa mno kujipanga hivyo lolote litakalotokea tulichukulie poa na kujipanga zaidi ili tufuzu michuano ijayo," alisema. Tanzania ipo kwenye mbio za kuwania kufuzu fainali za Afrika ikitarajiwa kuvaana na Msumbiji katika mechi ya marudiano Juni 15 baada ya awali kutoka sare. Pia ipo kundi C na timu za Ivory Coast, Morocco na Gambia katika mbio za kuwania kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014 zitakazofanyika nchini Brazil, ikianza kibarua Juni 2 kwa kuumana na Ivory Coast.

Sijasaini kokote-Nsa Job

MSHAMBULIAJI nyota wa timu ya Villa Squad, Nsa Job, amesema licha ya kuzungumza na watu wa Coastal Union ya Tanga, bado hajasaini fomu yoyote ya kujiunga kuichezea timu hiyo kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Kutokana na kutosaini, Nsa alisema milango i wazi kwa klabu yoyote ambayo imevutiwa naye, mradi aridhishwe na dau watakalokubaliana. Akizungumza na MICHARAZO, Nsa alisema ni kweli amefanya mazungumzo na Coastal Union, ila hawaafikiana na ndio maana hajasaini fomu na hivyo kutoa ruksa kwa timu nyingine kuweza kuzungumza nae. "Sijasaini kokote ndugu yangu, ingawa ni kweli nilishafuatwa na kuzungumza na watu wa Coastal Union," alisema. Nsa, alisema yeye kama mchezaji anaangalia masilahi hivyo timu yenye dau kubwa la kuvutia ndio atakayoichezea kwa msimu huo ujao. Nyota huyo aliyewahi kuzichezea timu za Moro United, Simba, Yanga na Azam, alisema hawezi kukurupuka kusaini timu bila kuangalia masilahi yake ikizingatiwa soka kwake ndio ajira inayomuingizia kipato. "Soka la sasa sio la kuchezea sifa, naangalia masilahi kwanza timu baadae," alisema.

Boxer Johnny Tapia has died at the age of 45

Tapia, whose career was marked by cocaine addiction, alcohol, depression and run-ins with the law, was found dead on Sunday in his hometown of Albuquerque, New Mexico. He won the WBO super-flyweight title in 1994, two belts at bantamweight and the IBF featherweight belt in 2002. Police spokesman Robert Gibbs said the death "did not appear to be suspicious". His tragic start in life - both parents were murdered, several stints in jail and numerous rivalries, garnered him a cult following in the sport. Tapia was orphaned at eight when his mother was murdered in brutal circumstances and, despite his successes in the ring, trouble stalked him for the rest of his life. Having been banned from boxing for three and a half years in the early 1990s because of his cocaine addiction, he beat Henry Martinez to become a world champion for the first time. Tapia went 11 years unbeaten as a professional before Paulie Ayala defeated him in 1999 in The Ring magazine's Fight of the Year, taking his WBA bantamweight title. Tapia lost a rematch with Ayala in 2000. In 2002 he beat Manuel Medina to secure the IBF featherweight crown and was good enough to take Mexican great Marco Antonio Barrera the distance later that same year. In 2007, he was hospitalised after an apparent cocaine overdose. Several days later, his brother-in-law and his nephew were killed in car accident on their way to Albuquerque to see the ailing boxer. In his 2006 autobiography, Tapia described how he had been declared clinically dead five times, each time due to a drug overdose. He also survived shootings, a bus crash and a near-drowning. Tapia last fought in June, outpointing Mauricio Pastrana. He finished with a 59-5-2 record.