STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, February 25, 2013

TIMBULO KAKAMATWA BURUNDI NA MADAWA YA KULEVYA?


Kuna tetesi kuwa msanii wa Bongo flava maarufu kwa jina la Timbulo, ambaye amepata umaarufu mkubwa kutokana na umahiri wa kuimba katika nyimbo zake kadhaa kama  Domo Langu, Waleo Wakesho, Samson na Delilah, amekamatwa mjini Bujumbura kwa tuhuma za kukutwa na madawa ya kulevya. Timbulo alikuwa huko katika kufanya mipango ya kufanya maonyesho kadhaa nchini Burundi mwezi April mwaka huu.
CHANZO:SANAA NA WASANII TANZANIA

BREAKING NEWS: WAZIRI WA MICHEZO AFUTA KATIBA YA TFF, KISA

 

Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk Funella Mukangara
SERIKALI imeingilia kati sakata la uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuamuru kufutwa kwa katiba ya sasa ya shirikisho hilo na badala yake kuamuru itumike katiba ya zamani (mwaka 2006) baada ya kubaini kuwa iliyopo ina kasoro nyingi.

Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari leo, Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo imeeleza kuwa katiba ya sasa ya TFF si halali. Imeelezwa vilevile kuwa msajili wa vyama vya michezo aliyedaiwa kuipitisha katiba hiyo ameondolewa.

Mchakato wa uchaguzi mkuu wa TFF umesimamishwa kutokana na mgogoro mzito uliotokana na kuenguliwa kiutata kwa wagombea kadhaa, wakiwamo Jamal Malinzi anayewania urais na Michael Wambura anayetaka kugombea nafasi ya makamu wa rais.

Kamati ya rufani ya TFF inayoongozwa na Iddi Mtiginjola ndiyo iliyozua balaa lote la sasa baada ya kuwaengua kina Malinzi na mwishowe kumuacha makamu wa sasa wa rais, Athumani Nyamlani abaki kuwa mgombea pekee.


Hata hivyo, tayari mchakato wa uchaguzi huo uliozua mabishano makali umeshasimamishwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na maafisa wa chombo hicho cha juu cha mchezo wa soka duniani wameshaanza kuwasili kufuatilia kinachotokea nchini.

Uamuzi wa serikali wa kufuta katiba ya sasa na kutaka itumike ya 2006 unampa ahueni kubwa Wambura ambaye alishasema hadharani kuwa  ataiburuza TFF mahakamani kama isipoachana na katiba mpya na kufuata ya zamani; huku akitoa sababu kadhaa za kupinga matumizi ya katiba mpya, mojawapo ikiwa ni kupitishwa kwake kwa njia ya waraka wa barua pepe (e-mail) kwenda kwa wajumbe badala ya kufuata maelekezo ya katiba yanayotaka mabadiliko kufanywa na wajumbe kupitia mkutano mkuu.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taratibu za FIFA, ni marufuku kwa shughuli za soka kuingiliwa na serikali au mahakama na nchi yoyote inayokwenda kinyume na taratibu hizo hujikuta ikifungiwa kama ilivyowahi kutokea enzi za FAT au ilivyoikumba nchi ya Kenya.

PAMBANO LA GOLDEN BUSH VETERANI VS CLOUDS KATIKA PICHA


Kikosi cha Clouds The Dream Team

Wachezaji wa timu za Golden Bush na Clouds wakiwa katika picha ya pamoja

Kikosi cha Golden Bush kilichoipa kichapo cha mabao 4-1 Clouds The Dream Team

Kivumbi uwanjani

Shija Katina (8) Nahodha wa Golden Bush katika harakati zake uwanjani na vijana wa Clouds

Mchezaji wa Clouds akitafuta wapi pa kupeleka pasi kwa wenzake

Shija Katina na wachezaji wa Cl;ouds wakiusaka mpira


Said Swedi 'Panucci' aliyefunga mabao mawili kati ya manne ya Golden Bush akiambaa na mpita, huku akinyemelewa na Shafii Dauda (kulia)

Baadhi ya mashabiki wa Clouds wakiwa hawaamini kama wamelala kwa Golden Bush

Mkali Shafii Dauda


Shafii Dauda akionyesha kiwango chake katika soka, sio kutangaza tu!

MAN II MAN: Majaliwa (14) beki wa Golden Bush akimchunga Ben KInyaiya, mfungaji wa bao la kufutia machozi la Clouds katika mechi iliyochezwa juzi jijini Dar es Salaam. (PICHA ZOTE ZIMEHAMISHWA SHAFII DAUDA)

YANGA, AZAM KITANZINI, KISA VURUGU

Polisi wakidhibiti vurugu zilizotokea mara baada ya pambano la Yanga na Azam juzi

KLABU ya Yanga inayoongoza katika msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara na Azam inayoifuata huenda zikakumbana na adhabu kali kufuatia makosa mbalimbali yakiwamo ya vitendo vya vurugu vilivyojitokeza katika mechi yao ya ligi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam juzi.
Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda kwa bao 1-0 lililowekwa wavuni na kiungo wake wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Niyonzima 'Fabregas' ambapo baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa, vurugu zilizidi na watu kadhaa walijeruhiwa.
Akizungumza jana, Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa Kamati ya Ligi itakutana mara tu baada ya kupokea ripoti ya waamuzi na kamishna wa mechi mechi hiyo kabla ya kutoa maelekezo juu ya nini kitakachofuata.
Akieleza zaidi, Wambura alisema kuwa watu kibao waliokuwapo uwanjani walishuhudia kila kilichotokea, baadhi yao wakiwa ni maafisa wa TFF (akiwamo yeye) na kwamba, kinachosubiriwa ni ripoti rasmi tu kutoka kwa waamuzi na kamishna ambao hawapaswi kuingiliwa majukumu yao.
"Ripoti ikishakuwa tayari na kuonekana kuwa kuna makosa,  yale ya kinidhamu yatapelekwa kwenye kamati ya nidhamu," alisema Wambura.
Miongoni mwa matukio yaliyoonekana juzi baada ya kumalizika kwa mechi, ni baadhi ya mashabiki waliodhaniwa kuwa wa Azam kutaka kumvamia refa aliyechezesha mechi hiyo na hata baada ya polisi kuingilia kwa nia ya kumlinda (refa), baadhi ya mashabiki hao wakataka kutwangana na askari pia. Watu hao walikuwa wakimtuhumu refa kuwa ameipendelea Yanga, hasa kwa kukataa goli lililofungwa na John Bocco katika dakika ya mwisho ya kipindi cha kwanza kwavile halikuwa halali.
Katika mechi mojawapo ya msimu uliopita baina ya timu hizo, kuliibuka vurugu pia ambapo refa alidaiwa kuibeba Yanga wakati 'wanajangwani' wakipata kipigo kikali cha mabao 3-1. Yanga walioonekana wazi wakitaka kumpiga refa Israel Nkongo walikumbana na adhabu kali ikiwa ni pamoja na kulimwa faini kwa wachezaji wake kadhaa na baadhi yao kufungiwa kwa vipindi tofauti.


CHANZO:NIPASHE

SIMBA HATARINI KUPOROMOSHWA ZAIDI

Kikosi cha Coastal Union

WAKATI wakijiandaa na safari yao ya Angola kwa ajili ya pambano la marudiano la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Libolo, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba ipo hatarini kuporomoka zaidi kwenye msimamo wa ligi iwapo Coastal Union itashinda pambano lake dhidi ya Ruvu Shooting keshokutwa.
Coastal inatarajiwa kuvaana na Shooting Jumatano kwenye uwanja wa Mkwakwani Tanga, ambapo ushindi wowote itakaopata utaifanya ifikishe poiinti 33 na hivyo kuiengua Simba yenye piointi 31 ambayo haitakuwa dimbani nchini katika ligi hiyo.
Japo Coastal iliyorekebisha makosa kwa kuinyuka Oljoro katika mechi yake iliyopita, isitarajie mteremko kwa Ruvu kwani maafande hao katika mechi zao za duru la pili wameonekana kuimarika zaidi, hivyo huenda ikapata upinzani mkali iwapo watataka kukalia nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi hiyo.
Mechi nyingine zitakazochezwa siku hiyo ni pamoja na pambano la kukata na mundu kati ya Yanga na Kagera Sugar ambayo jana ililazimishwa sare ya bao 1-1 na wageni wao African Lyon katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Kaitaba.
Katika mechi yao ya awali Yanga ilicharazwa bao 1-0 na Kagera na kuibua hisia kali kwamba kuna baadhi ya wanahabari walitumika kuihujumu timu na kupelekea kutolewa vitisho na kuwapiga marufuku waandishi hao walioambatana na timu hiyo toka Dar kukaa mbali na kambi yao.
Yanga itahitaji ushindi ili kuimarisha nafasi yake ya kukaa kileleni kutokana na kwamba timu inazowafukuza kwa karibu Azam na Simba watakuwa kwenye mechi za kimataifa ugenini mwishoni mwa wiki.
Iwapo Yanga itashinda itafikisha pointi 41 ikiwa michezo sawa na Azam wenye pointi 36 na kuiacha Simba kwa pointi 10 kitu kitakachoiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa msimu huu.
Michezo mingine kwa siku ya Jumatano kwa mujibu wa ratiba ya ligi hiyo ni Polisi Moro itakayoikaribisha Mgambo JKT uwanja wa Jamhuri Morogoro, JKT RUvu dhidi ya Toto African mechi itakayochezwa uwanja wa Chamazi na 'wababe wa Simba' Mtibwa Sugar watakuwa viwanja vyao vya Manungu Complex kuikaribisha Prisons ya Mbeya.

Msimami kamili wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya mechi za mwishoni mwa wiki ni kama ifuatavyo:



          P W D L GF GA GD Pts
1 Young Africans FC Young Africans 17  12  3 2 33 12 21 39
2 Azam FC Azam 18  11 3 4 31 15 16 36
3 Simba SC Simba 18 8 7 3 26 15 11 31
4 Coastal Union  18 8 6 4 21 16 5 30
5 Kagera Sugar FC Kagera Sugar 18 7 7 4 19 16 3 28
6 Mtibwa Sugar FC Mtibwa Sugar 18 7 6 5 21 18 3 27
7 Ruvu Shooting Stars Ruvu Shooting  16 7 4 5 20 17 3 25
8 JKT Mgambo 17 6 3 8 13 16 -3 21
9 JKT Oljoro 18 5 6 7 19 22 -3 21
10 Prisons-Mbeya 16 4 6 6 10 13 -3 18
11 JKT Ruvu Stars JKT Ruvu Stars 16 4 4 8 14 26 -12 16
12 Toto African Toto African 19 2 8 9 15 28 -13 14
13 African Lyon FC African Lyon 19 3 4 12 13 31 -18 13
14 Polisi Moro 16 2 5 9 8 18 -10 11


FIFA KUCHUNGUZA KWA KINA MCHAKATO WA UCHAGUZI TFF


OFISA Maendeleo wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) Kusini mwa Afrika, Ashford Mamelodi amewahakikishia Watanzania kuwa ujumbe wa Shirikisho hilo utakaokuja nchini mwezi ujao, utafanya uchunguzi wa kina kuhusu mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (FIFA) na kutoa uamuzi kwa maslahi ya mchezo huo.

“Ninafurahi kwamba hali ya utulivu imefikia kiwango hiki na nina uhakika FIFA itafanya uchunguzi wa kina na kufanya uamuzi kwa maslahi ya mpira wa miguu,” amesema Mamelodi alipokuwa akizungumzia uchaguzi mkuu wa TFF ambao ulikuwa ufanyike Februari 24 mwaka huu lakini ukasimamishwa kutokana na matatizo kadhaa baada ya baadhi ya wagombea kuenguliwa.

Mbali na kuhudhuria Mkutano Mkuu wa TFF na uchaguzi, safari ya Mamelodi nchini pia ilihusisha kumtambulisha msaidizi wake, Patrick Onyango ambaye amejiunga na ofisi hiyo ya FIFA kuanzia mwishoni mwa mwaka jana, kufuatilia miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na GOAL Project 4 ambayo ni uwekaji wa nyasi bandia kwenye Uwanja wa Nyamagana na maendeleo ya Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba, mikakati ya mwaka 2013 na kozi mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Mikutano wa TFF jana, Mamelodi alisema uamuzi wa Shirikisho hilo kutuma wajumbe katikati ya mwezi ujao unatokana na mawasiliano baina ya Rais wa TFF, Leodegar Tenga na FIFA ambayo ilitaarifiwa hali halisi ilivyo na kama inaweza kusaidia kutatua matatizo yaliyopo.

“FIFA haitakuja kuingilia mchakato wa uchaguzi, itakuja kutatua matatizo,” amesema Mamelodi. “Masuala ya uchaguzi ni ya ndani ya nchi. FIFA haiji kuichagulia Tanzania rais. Wajumbe wanaweza kumchagua mtu yeyote wanayeona kuwa anafaa kuwa rais,” amesema Mamelodi.

“Lakini katiba ya FIFA iko wazi kwamba mwanachama wake ni lazima akubaliane na sheria za Shirikisho kuwa wanachama ni lazima wabanwe na Katiba ya FIFA. Kwa hiyo mara tu unapopata uanachama wa FIFA, ni lazima ujue kuwa utabanwa na katiba ya FIFA na mojawapo ya mambo haya.

“Lakini kuna tofauti na kitendo cha Serikali kusimamisha uchaguzi kwa kuwa hiyo inakuwa ni Serikali kuingilia moja kwa moja masuala ya mpira wa miguu, kitu ambacho katiba ya FIFA inakataza.”

Mamelodi, ambaye alitumia muda mwingi kuelezea umuhimu wa hali ya utulivu iliyotawala kwa muda mrefu nchini, amesema anajua kuwa uongozi wa Rais wa sasa wa TFF, Leodegar Tenga umefanya mengi katika kuhakikisha unajenga mazingira mazuri ya maendeleo ya mpira wa miguu, lakini kuna wakati ni lazima uheshimu uamuzi wa mtu.

“Tenga amesema imetosha anaondoka na hatuna budi kuheshimu uamuzi wake. Hiyo ni kauli inayotoka kwa kiongozi wa kweli, kiongozi anayewajibika. Lakini kwa kuangalia misingi ambayo uongozi wake umeijenga, ni wazi kuwa kiongozi mpya ataendeleza taasisi bila ya matatizo.

“Tanzania haikufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika, lakini kuna miradi mingi ya maendeleo ambayo ilifanyika, mingine ambayo ilijaribiwa kwa mara ya kwanza nchini Tanzania na ikafanikiwa. Kuna Azimio la Bagamoyo, Semina ya Mawasiliano ya Jamii (Comm-Unity) ya Wanawake, Futuro III na mingine. Yote hii ilifanyika kwa sababu kulikuwa na utulivu.

“Hivi sasa TFF ina sekretarieti ina Mkurugenzi wa Ufundi; ina programu za maendeleo na kuna utulivu. Cha msingi ni kuendeleza haya. Kama mambo haya yataendelezwa baada ya uchaguzi, ni dhahiri kuwa mpira utazidi kuendelea. Hakuna njia ya mkato katika maendeleo.”

Uchaguzi wa TFF ulihusisha nafasi za rais, makamu wa rais na wajumbe wa Kamati ya Utendaji kutoka Kanda 13 za Shirikisho.

Angetile Osiah
Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Sunday, February 24, 2013

BREAKING NEWS:RAGE KUACHIA NGAZI SIMBA

Mwenyekiti wa Simba ismail Aden Rage


HABARI zilizotufikia hivi punde kutoka ndani ya klabu ya soka ya Simba zinasema kuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage anatarajiwa kujiuzulu nafasi yake kutokana na kipigo ilichopewa timu yake jioni ya leo na Mtibwa Sugar.
Taarifa hizo zimedokeza kuwa, Rage atatangaza msimamo huo wa kuachia ngazi Msimbazi kesho atakapokutana na waandishi wa habari.
MICHARAZO imekuwa ikimsaka Rage mwenyewe kusikia kauli yake, lakini simu yake imekuwa haipatikani, hivyo juhudi zinaendelea ili kuthibitisha taarifa hizo na tutawajuvya mara tukibahatika kumpata.

CHELSEA HOI KWA MAN CITY, NEWCASTLE YATAKATA



Lampard (8) akikosa penati iliyopanguliwa na kipa Joe Hart


WAKATI Newcastle United ikitakata nyumbani kwake kwa kuigagadua Southampton kwa mabao 4-2, vijana wa Rafa Benitez wamejikuta wakiangukia pua ugenini kwa kunyukwa na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya England, Manchester City mabao 2-0 katika pambano kali lililochezwa jioni hii.
Chelsea walionyesha kuhimili vishindo vya wenyeji wao na kulazimisha kwenda mapumziko wakiwa nguvu sawa kwa kutofunga bao lolote.
Hata katika kipindi cha pili, Chelsea walionyesha uhai kwa kuwakimbiza wapinzani wao na kufanikiwa kupata penati iliyoshindwa kufungwa na mkongwe Frank Lampard kabla ya Yaya Toure kuifungia wenyeji bao dakika ya 63.
Dakika tano kabla ya pambano hilo kumalizika shuti kali la kushtukiza la Carlos Tevez liliwanyong'onyesha Chelsea kwani liliwavunja nguvu za kuweza kusawisha bao na kuambulia sare.
Katika pambano jingine lililochezwa leo, Newcastle United wakiwa nyumbani waliishindilia wageni wao Southampton kwa mabao 4-2.
Wageni waliwashtua wenyeji wao wa kuandika bao la kuongoza dakika tatu tu ya mchezo kupitiaMorgan Schneiderlin kabla ya Mousa Sissoko kusawazisha dakika ya 33 na na nyota wa Senegal, Papiss Demba Cisse kuongeza la pili dakika ya 42 naa kufanya hadi mapumziko Newcastle kuongeza bao 2-1.
Kipindi cha pili kilianza kwa wageni kusawazisha bao kupitia Rickie Lambert  kabla ya Yohan Cabaye kufunga bao la tatu la Newcastle dakika ya 67 na dakika ya 79 beki wa Southampton, Jos Hooiveld kujifunga na kuihakikishia wenyeji ushindi huo mnon0.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena kwa mchezo mmoja tu, West Ham United kuikaribisha Tottenham Hotspur ambayo itakuwa inafukuzia kukalia nafasi ya tatu baada ya leo Chelsea kudorora mbele ya Manchester City.

SIMBA YAVUTWA SHARUBU, YALALA TENA NA MTIBWA

KIkosi cha Simba kilicholala leo kwa Mtibwa Sugar


Mtibwa Sugar walioendeleza ubabe kwa Simba leo uwanja wa Taifa (Picha Zote:Francis Dande)

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba jioni ya leo imeendelea kuwa mteja wa Mtibwa Sugar baada ya kufungwa bao 1-0 katika pambano kali lililochezwa kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mtibwa ilijipatia bao hilo la pekee katika dakika ya 19 ya mchezo kupitia kwa beki wake mahiri, Salvatory Ntebe bao lililoihakikishia timu yake kuvuna pointi zote sita kwa msimu mbele ya Simba.
Kwani katika pambano lao la duru la kwanza Simba ilikubali pia kichapo cha mabao 2-0 na kupelekea kuibuka kwa mtafaruku toka kwa wanachama wa klabu hiyo waliokuwa wakishinikiza nahodha na kipa tegemeo wa timu hiyo Juma Kaseja na baadhi ya viongozi kujiuzulu kwa madai waliifanyia hujuma.
Katika pambano hilo, beki kisiki wa Simba Juma Nyosso alijikuta akitolewa nje na mwamuzi Kidiwa dakikia za lala salama, wakati tayari jahazi la timu yake likielekea kuzama mbele ya Mtibwa ambayo katika mechi yake ya mwisho ilikumbana na kipigo cha mabo 4-1 toka kwa Azam.
Kipigo hicho kimeiacha Simba kuendelea kusalia kwenye nafasi yake ya tatu nyuma ya Azam waliolala bao 1-0 jana kwa vinara wa ligi hiyo Yanga wanaoongoza msimamo kwa sasa wakiwa na pointi 39.
Mabingwa hao watetezi wa ligi kuu wanatarajiwa kuondoka nchini katikati ya wiki hii kuelekea Angola kwa ajili ya pambano lake la marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji wao Libolo ambao walishinda meechi ya wali kwa bao 1-0.
Kocha Msaidizi wa Simba alizungumza baada ya pambano hilo akidai wanakubali matokeo kwanu kufungwa ni sehemu ya matokeo matatu ya soka, huku akiahidi kujipanga kwa ajili ya mechi zao nyinginee za ligi mara watakaporejea toka Angola.

Sheikh auwawa Zenji, ni muendelezo wa mauaji wa viongozi wa kidini


IGP Said Mwema wakati wa mkutano na waandishi wa habari kufuatia tukio la kuuwawa kwa Padri wa Kikatoliki
SIKU chache baada ya kutokea kifo cha Padri Evarist Gabriel Mushi kupigwa risasi na watu wasiojulikana kichwani eneo la Beit el Raas, Jana Imamu wa Msikiti wa Mwakaje ameuawa baada ya kupigwa mapanga hadi kufa.
Kwa mujibu wa maelezo ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ahmada Khamis amethibitisha kutokea kwa tukio hilo hapo jana mchana majira ya saa 8 na kumtaja aliyefariki kuwa ni Sheikh Ali Khamis ambaye ameuawa na watu wasiojulikana.
Kamanda Ahmada alisema Sheikh Khamis mbali ya kuwa ni Imamu wa Msikiti lakini pia ni mkulima na ameuliwa wakati akiwa katika mazingira ya kazi zake ndani ya shamba lake huko Kidoti Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Akielezea mazingira ya tukio hilo Kamanda Ahmada alisema tukio hilo limetokea baada ya Sheikh Khamis kwenda shambani kwake katika shmba la minazi Kidoti ambapo wakati akiwa shambani hapo ndipo walipotokea watu kadhaa na kumpiga mapanga sehemu za shingoni mwake na kusababisha kifo chake muda mfupi baada ya kipigo hicho.
Alisema baada ya tukio hilo, watu walimchukua na kumkimbiza hospitali lakini kutokana na kupoteza damu nyingi alifariki dunia wakati akiwa njiani na hivyo harakati za mazishi zinafanyika baada ya kuchukuliwa vipimo na wataalamu wa afya.
Kamanda Ahmada ametoa wito kwa wananchi kutopuuzia taarifa za watu ambao wanawashuku na wenye kuleta maafa yakiwemo mauaji hapa nchini, kwani kuwaficha wahalifu ni kuendeleza utamaduni usiofaa katika jamii ambayo imeanza kuharibika kutokana na mauaji hayo yanayoendelea kila kukicha.
Hili ni tukio la nne kwa viongozi wa dini kuhujumiwa ambapo tukio la kwanza Sheikh Fadhil Suleiman Soraga kumwagiwa tindi kali na watu wasiojulikana na kujeruhiwa vibaya wakati akifanya mazoezi nyakati za asubuhi karibu na nyumbani kwake Magomeni, tukio la pili ni lile la Padri Ambrose Mkenda aliyepigwa mapanga shingoni na kurejuhiwa vibaya na watu wasiojulikana wakati akitaka kuingia nyumbani kwake huko Tomondo Mjini Unguja. matukio hayo mawili yalitokea mwaka jana.
Katika mwaka huu nako kumetokea matukio mawili kwa kuuawa kwa Pardi Evarist Mushi huko Beit El Raas wakati akitaka kuingia Kanisani na pia kuuawa kwa Sheikh Ali Khamis huko Kidoti shambani kwake Mkoa wa Kaskanizini Unguja.  Inna lillahi wainna ilayhi rajiiun.

MECHI YA YANGA, AZAM YAINGIZA MIL 240

Mshambuliaji wa Azam Kipre Tchetche akichuana na beki wa Yanga Nadir Haroub 'Cannavaro' katika mechi yao iliyochezwa jana na Yanga kuibuka mshindi wa bao 1-0
Na Boniface Wambura
MECHI namba 120 ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa jana (Februari 23 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa Yanga kuibuka ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam imeingiza sh. 239,686,000.

Watazamaji 39,315 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 58,794,927.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 36,562,271.19.

Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata tiketi hizo walikuwa 33,315 na kuingiza sh. 165,655,000 wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa ya kiingilio cha sh. 20,000 kilichovutia washabiki 485 na kuingiza sh. 9,700,000.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 29,895,725.82, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 17,937,435.49, Kamati ya Ligi sh. 17,937,435.49, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 8,968,717.75 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 6,975,669.36.


Saturday, February 23, 2013

NIYONZIMA AZIMA NGEBE ZA AZAM, AWATIA SIMANZI TAIFA



BAO pekee lililotumbukiwa kimiani na kiungo nyota wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Niyonzima limeweza kuzima ngebe za Azam kwa kuiwezesha timu yake kuibuka na ushindi wa bao 1-0 na kuzidi kujikita kileleni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Pambano hilo lililojaa upinzani na wenye kukamiana ulichezwa jioni ya leo kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuifanya Yanga kuitambia Azam kwa kuzoa pointi zote sita za msimu huu katika ligi hiyo, baada ya duru la kwanza kuwalaza mabao 2-0.
Ushindi huo, umeifanya Yanga kufikisha jumla ya pointi 39 tatu zaidi ya Azam na ikiwa bado ina mchezo mmoja mkononi kwani vinara hao wamecheza mechi 17 wakati Azam wanaendelea kushika nafasi ya pili wamecheza mechi 18.
Mnyarwanda huyo anayefahamika kwa jina la Fabregas alifunga bao hilo la pekee lililowafanya mashabiki wa Yanga kupagawa kwa furaha na kuwazomea wale wa Azama mabo walikuwa wakiiungwa mkono na Simba, kwa shuti la nje ya 18 katika dk ya 32 baada ya kugongeana vema na Jerry Tegete kabla hya kufumua kombora kali.
Azam ilishangilia bao la kusawazisha lililofungwa kwa kichwa na John Bocco 'Adebayor' lililokataliwa na mwamuzi kwa madai alimchezea vibaya kipa Ally Mustafa kabla ya kuutumbukiza kimiani, hali iliyowakumba pia Yanga katika kipindi cha pili kwa bao la Didier Kavumbagu nalo kukataliwa na mwamuzi.
Ligi hioyo inatarajiwa kuendelea tena kesho kwa pambano litakalowakutanisha mabingwa watetezi Simba dhidi ya Mtibwa Sugar.
Pambano hilo litachezwa kwenye uwanja wa Taifa, huku Simba wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi ya awali dhidi ya Mtibwa kwa mabao 2-0.
Vikosi vya pambano la leo;
Yanga:
Ali Mustapha 'Barthez', Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub, 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Athumani Idd 'Chuji', Simon Msuva, Frank Domayo, Jerryson Tegete, Hamis Kiiza 'Diego'/ Said Bahanunzi, Haruna Niyonzima.
Azam:
Mwadini Ali, Michael Bolou, Waziri Salum, Joackins Atudo, David Mwantika, Ibrahim Mwaipopo, Salum Abubakar 'Salum Aboubakar 'Sure Boy', John Bocco 'Adebayor', Kipre Tchetche, Humphrey Mieno na Khamis Mcha 'Vialli'.

MAJANGILI MATATU YAUAWA MKOANI DODOMA

Mwili wa Mtu anayedhani wa kuwa ni Jangili ukiwa umehalibika baada ya kuuawa kuchinjwa na kuchomwa moto katika chumba cha kuhifadhia maiti mvumi Dodoma.

Kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma David Misime akiwaonyesha waandishi wa Habari meno 73 ya tembo yenye thamani ya zaidi 225 mil ambayo ni sawa na tembo 36 pamoja na Gari aina ya Noah NO T 983 BZJ waliokamata juzi katika kijiji cha Miganga mvimi wilayani Chamwino Dodoma.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Dodoma David Misime akifafanua jambo mbele ya waandishi wa Habri kuhusu tukio la vifo vya watu watatu wanaodhaniwa kuwa ni majangili waliouawa na wananchi katika kiji cha miganga Mvumi Dodoma pembeni ni Gari aina ya Noah No T 983 BZJ walilokuwa wakilitumia na kuku meno 73 ya Tembo.
Na John Banda, Dodoma
MAJANGILI watatu wa nyara za serekali wameuawa kwa mishale yenye sumu na kisha miili yao kuchomwa moto na wananchi katika purukushani na polisi walipokuwa wakijaribu kukimbia ili kutorosha meno ya tembo.
Tukio hilo lilitokea jioni ya alhamis wiki hii katika kijiji cha Miganga kata ya mvumi wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma ambapo miili yao ilikutwa ikiwa imehalibika kutokana na kuchomwa moto.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma David Misime alisema majangili hayo yaliuawa na wanachi wenye hasira kali kwa zana mbalimbali za kijadi walipokuwa wanakimbilia polini ili kujiokoa na mkono wa polisi.
Misime alisema jeshi hilo lipokea taarifa kutoka kwa wananchi wema kuwa kulikuwa na Gali likitokea Manda likiwa na Meno ya Tembo na kisha kuweka mtego katika kijiji cha mwitikila ambapo waliona gali aina ya NOAH T 983 BZJ na kulisimamisha na Dereva wa Gali hilo alifanya kama anapunguza mwendo na kisha kuondoka kwa mwendo wa kasi.
‘’Polisi wakishirikiana na wananchi walianza kulifukuza walipofika kijiji cha Miganga Mvumi polisi walifanikiwa kupiga Risasi tairi moja ya kushoto na hivyo watu watatu waliokuwemo ndani gari hilo waliruka na kutawanyika, wananchi waliojichukulia sheria mkononi waliwashambulia kuasi cha kupoteza maisha yao’’, alisema
Aidha kamanda Misime alisema baada ya kulipekua Gari hilo walikutaMeno 73 ya Tembo yenye uzito wa kilo 255.9 yakiwa na thamani ya zaidi ya TSH 225 mil pamoja na hati ya mashitaka [CHARGE SHEET] ambayo ni kesi ya kuhujumu uchumi namba 4/2012 iliyokuwa imefunguliwa katika mahama yam panda mkoa wa katavi na Leseni ya Udereva na 4000692535 Aboubakar Peter huku wakihisi ni mmoja ya waliouawa.
Alisema walikuwa wameshitakiwa kwa kosa la kupatikana na Meno 3 ya Tembo Tarehe 17.06.2012 na maafisa wanyama poli katika eneo la Msaginya Wilaya ya Mlele mkoa wa katavi majina ya walikuwa wameshatakiwa ni Joseph Marius [NGONDO] 59 mkazi wa maili mbili Dodoma, Aboubakar Mhina 25 mkazi wa Mkuhungu Dodoma, Msafiri Milawa 36 mkazi wa Nkuhungu Dodoma na Petro Mtipula 55 mkazi wa mpanda.
Kamanda alitoa wito kwa wananchi wasijichukulie Sheria mikononi kwani kwa kufanya hivyo ni kupoteza ushahidi na inawawia vigumu polisi kupata mtandao inayohusika na matukio kama hayo. 
 
CHANZO:BOSS NGASA 

GOLDEN BUSH YAIZIMA CLOUDS MARA NNE



WAKALI wa soka jijini Dar es Salaam, Golden Bush Veterani jana ilitimiza tambo zake kwa kuifumua timu ya Clouds Fc kwa mabao 4-1 katika mechi kali iliyochezwa kwenye uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam.
Golden Bush iliahidi kutoa kipigo kwa wapinzani wao kabla ya mchezo huo uliochezwa jioni ya jana kupitia kwa mlezi wake na mmoja wa wachezaji tegemeo, Onesmo Waziri 'Ticotico'.
Tambo hizo zilihitimishwa baada ya mechi hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi, Othman Kazi kwa mabao mawili ya Said Swedi 'Panucci', Nico Nyagawa na De Natale, huku bao la kufutia machozi la Clouds iliyokuwa ikiongozwa na Mbwiga Mbwiguke lilifungwa na Ben Kinyaiya.
Ticotico alisema ushindi huo umekiuwa faraja kwao baada ya wiki iliyopita kuchezea kichapo toka Survet, pia kuzima ngebe za wapinzani wao waliokuwa wakichonga kabla ya pambano hilo.

Aliongeza kwa sasa timu yake imevunja kambi yake iliyokuwa imewekwa hoteli ya Star Light na kufanya mazoezi ya kawaida kujiandaa na mechi za kirafiki zitakazochezwa hivi karibuni pamoja na mipambano ya kusherehekea sikukuu ya Pasaka.

MWANARIADHA OSCAR PISTORIUS AACHIWA KWA DHAMANA

  Oscar Pistorius
 Oscar Pistorius akiwa na mpenzi wake Reeva Steenkamp wakati wa uhai wake.
 Reeva Steenkamp


Kesi kamili inayomkabili nyota huyo inaweza kuanza kusikilizwa miezi kadhaa ijayo, na Pistorius nyota wa Olimpiki na Paralimpiki, ambaye hana miguu yote miwili, anakabiliwa na hatari ya kifungo cha maisha kama akikutwa na hatia ya mauaji


JOHNNESBURG, South Africa

MWANARIADHA nyota wa mbio za walemavu Oscar Pistorius, hatimaye leo Ijumaa mchana ameachiwa kwa dhamana, kutokana na kesi ya mauaji ya mpenzi wake inayomkabili.

Umauzi wa Pistorius kupewa dhamana ulitolewa na Jaji Desmond Nair, na kuamsha furaha miongoni mwa wanafamilia wa Pistorius na mashabiki wake ndani na nje ya Mahakama ya jijini Pretoria, huku mwenyewe akiwa amesimama imara kama aliyenyimwa dhamana hiyo.

Kuachiwa kwa Pistorius kunafuatia wiki nzima ya usikilizaji wa maelezo ya namna mwanariadha huyo alivyompiga risasi na kumuua mpenzi wake Reeva Steenkamp wakiwa katika jumba lao la kifahari, asubuhi ya Siku ya Wapendao Februari 14.

Waendesha mashtaka wamesema Pistorius, 26, anakabiliwa na kesi ya kujibu kutokana na kupiga risasi nne kwenye mlango wa bafu ukiwa umefungwa, huku mpenzi wake akiwa ndani. Steenkamp, 29, alikutwa na majeraha ya risasi katika kichwa chake, mkononi na kwenye nyonga.

Upande unaomtetea Pistorius umeendelea kusisitiza kuwa mkali huyo alimuua mkewe kimakosa, wakisema alifanya hivyo kutokana na kuhisi kuwa amevamia na jambazi, wakataka apewe dhamana kuweza kujiandaa, kuikabili kesi hiyo iliyoteka hisia za wengi duniani.

Kesi kamili inayomkabili nyota huyo inaweza kuanza kusikilizwa miezi kadhaa ijayo, na Pistorius nyota wa Olimpiki na Paralimpiki, ambaye hana miguu yote miwili, anakabiliwa na hatari ya kifungo cha maisha kama akikutwa na hatia ya mauaji.

Dhamana hii imefungua milango ya matumaini miongoni mwa wanafamilia na mashabiki wake, kuwa anaweza kushinda vita ya kuepuka kifungo cha maisha.