STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, September 27, 2014

NCCR-Mageuzi yalia na Wabunge wa BMK

Faustin Sungura (kulia) katika moja ya mikutano yake na wanahabari
Na Kipimo Abdallah
CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimesikitishwa na kitendo cha Bunge Maalum la Katiba kuhitaji wajumbe ambao hawapo nchini au ndani ya Bunge kuruhusiwa kupiga kura wakati ukweli ni kwamba ushiriki wao katika utengenezaji wa rasimu hiyo ulikuwa mdogo.
Kaimu Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi Faustin Sungura, aliyasema hayo juzi alipozungumza na mwandishi wa habari hii kwa njia ya simu.
Alisema utaratibu huo wa kuruhusu wajumbe walioko nje kupiga kura haujawahi kutokea katika Bunge lolote duniani jambo ambalo linatia aibu kwa Taifa.
Kaimu Katibu huyo alisema iwapo wajumbe hao ambao hawakushiriki katika mchakato kwa kiwango cha kuridhisha wataruhusiwa kupiga kura hali hiyo ingekuwa hata kwa wale wa UKAWA kwani uwepo wao nje una sababu kama hao wengine.
“Jamani Watanzania tuamke hii sasa aibu tunapopelekwa pabaya haiwezekani watu wapo nje ya Bunge alafu wapewe nafasi ya  kupiga kura jambo ambalo haliwezi kuvumiliwa kwani linatia aibu nchi”, alisema.
Alisema katika Bunge hilo linaloendelea mkoani Dodoma mambo mengi yamekiukwa ila hapo walipofikia ni vema jamii ya Kitanzania ikafungua macho na kuamua kufanya maamuzi mazito kwani kinachoonekana ni watu kuhitaji kwa maslahi yao.
Sungura alisema ni vema Wabunge waliopo Dodoma wakatambua kuwa mambo megine hayalazimishwi kwani yanahusu jamii kubwa na sio kama wanavyofikiria kuwa wao ndio wanahusika pekee.
Alisema NCCR-Mageuzi imejipanga kuhakikisha kuwa katiba hiyo inakataliwa kutokana na ukweli kuwa kilichopo ndani sio yaliyokuwa mapendekezo ya wananchi ambayo yaliwakilishwa na iliyokuwa Tume ya Katiba.
Sungura alisema ukweli dhidi ya UKAWA kutoka Bungeni umedhihirika hivyo juhudi zao ni kuhakikisha kuwa rasimu hiyo haipitishwi na wananchi kutokana na kudharauliwa kwa maoni yao ambayo walipendekeza katika rasimu ya Jaji Joseph Warioba.
Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema nguvu yao pia inaongezwa na maamuzi ya Mahakama Kuu hivi karibuni ambapo imeweka bayana kuwa kitendo kilichofanywa na Mwenyekiti wa Bunge hilo kupokea maoni mapya ni ukiukwaji wa sheria.
Sungura alisema mabadiliko na maingizo mapya yaliyofanywa na Bunge hilo ambalo alilitaja kuwa ni la upande mmoja yamekiuka sheria kwa kiwango kikubwa na cha kusikitisha.
Alisema kwa sasa NCCR- Mageuzi ipo katika mikakati ya kuhakikisha wananchi wanapata elimu sahihi juu ya mchezo mchafu unaofanywa na Bunge hilo jambo ambalo litawajengea uwezo wa kufanya maamuzi sahihi katika upigaji kura.

Mwisho

No comments:

Post a Comment