STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, September 27, 2014

Barua ya wazi kwa Wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka Zanzibar

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhOkLsciXf-74G8GIdbS_htvzslWBy8miIPYzTL96vqTVCU_0Tg1cOReOW6eT0QjqSONTsFX3mfXtU9sxZ6p14UIXghJu9H5CZcjNo-wlAeSz-A8BWvps1Lmj_8MrM-CgwAe0rLJ8Kl2LPx/s1600/WABUNGE+WAKIPITIA+RASIMU+YA+MAPENDEKEZO+YATAKAYO+TUMIWA+NA+KIKAO+CHA+BUNGE+LA++KUJADILI++RASIMU+YA+KATIBA.JPG
Assalam alaykum
Natumai hamjambo ndugu, kaka na dada zangu. Inshallah Mwenyenzi Mungu akupeni afya na uzima kuelekea kipindi hiki muhimu cha kupiga kura kuamua Katiba Inayopendezwa na pia Mola akupeni busara na maamuzi mema.
Nakuandikieni barua hii kama Mzanzibari mwenzenu sina zaidi ya hilo. Ni kutokana na Uzanzibari wangu nimeona kuwa nijaribu kukuaidhini, kunasihini, kukushawishini, kukusemeshini, kukuombeni kuwa msiikubali Katiba Inayopendekezwa na muipigie kura ya HAPANA.
Tafadhalini wekeni mbali ushindani, itikadi na mitazamo ambayo inatutenganisha Wazanzibari na muamue kwa maslahi makubwa, mapana na ya muda mrefu ya Zanzibar. Msitizame tulipojikwaa bali tizameni tulipoanguka. Msitizame nyuma mkahesabu visa na mikasa ila nyinyi hapo mlipo ndio wenye fursa ya kuikoa, kuinusuru na kuihuisha Zanzibar.

Naam, ni kura ya HAPANA ndio ambayo itaibakisha, itaiokoa, itaisimamisha Zanzibar. Mjue mkipigia kura ya NDIYO maana yake ni kuwa Zanzibar tuipendayo inazidi kupungua, kuchukuliwa na kumezwa kama ambavyo imekuwa khofu yetu kwa miaka kadhaa ya Muungano huu.
Nataka muamini ndani ya dhati yangu mimi ni muumini wa Muungano. Nataka Muungano wa haki na hadhi sawa baina ya Washirika wa Muungano – Tanganyika na Zanzibar- ili kila nchi ipate fursa sawa za kuhudumia watu wake.
Wengi wenu kwa kauli zenu mara kadhaa mmekuwa mkisema Muungano hauakisi hali ya usawa, haki na hadhi sawa lakini mkawa mnatumia neno KERO kuwasilisha fikra zenu hizo, na wengi tukawa na matumaini kwamba fursa hiiya kuunda upya Katiba yetu itapunguza kama si kuondosha kabisa KERO hizo.
Ila baada ya kuiona Katiba inayopendekezwa nimeona kuwa andiko hilo halina msaada, halina muelekeo na halina wema na Zanzibar. Kulikubali andiko hilo ni kujitia kitanzi wenyewe na sasa imekuwa ni kusokotwa, kubanwa na kudhibitiwa Zanzibar lakini mara hii itakuwa kwa kujitakia wenyewe.

Huko nyuma tumekuwa tukisema kuwa kumekuwa na hadaa, sijui ujanja, sijui ghalat,sijui unyemela wa kuongeza Mambo ya Muungano ambayo yamekuwa yakipunguza madaraka ya Zanzibar, lakini mara hii tunajichinja wenyewe kwa mikono yetu.
Hii ilikuwa ni fursa kubwa kwetu kusimama kama Zanzibar. Zanzibar ilipaswa kusimama kama kundi zima ndani ya Bunge na kukaa na kundi zima la upande wa pili yaani Tanganyika, na watu wa pande mbili hizi kuamua umbo, hadhi na sifa gani tunataka Tanzania iwe.
Hili la pande mbili lilikuwa lisionewe aibu kwa sababu ndio ukweli na uhalisia kwamba tuko pande mbili. Haiwezekani kuwa na Muungano, ambapo upande mmoja una kila sifa za kuwa nchi, halafu upande mwengine uwe na sifa za kuwa dola na nchi ifichwe ndani yake.

Ilikuwa ni nafasi nzuri kwa Zanzibar kudai haki zake, stahiki zake, fursa zake ili iweze kukidhi mahitaji ya watu wake, maana hata kama tumo ndani ya Muungano basi bado tuna chumi mbili zinazoshindana na kwa kweli zinazopigania na kunyang’anyiana rasilmali karibu zile zile.
Ilikuwa ni wakati wa kufanya kila njia ili Zanzibar ijitengenezee fursa ya kuwa na mafanikio kama ya Visiwa vya Seychelles au Mauritius ambavyo wastani wa kipato cha mwananchi wa nchi hizo mbili ni zaidi ya dola 14,000 na dola 15,000 mtawalia.
Najua hoja itakuja basi haya yangefanywa kwa umoja, na mbona umoja huo haukuwepo, nakiri kuwa hilo kweli limetokea, lakini ni kama katika mchezo iwapo mchezaji mmoja ametolewa ama kwa kuonewa na mwamuzi au kwa kitendo chake cha makusudi, haina maana kuwa waliobakia uwanjani wakubali kupoteza mchezo, badala yake hujibidiisha kushinda ili iwe njia moja ya kumsuta mwenzao aliyetolewa na sifa kwa kweli inakuja kwa waliobakia uwanjani.
Kwa kuendelea kujigandisha katika ubavu, kuendelea kuamini kuwa hatuwezi kujitegemea na kwa hivyo mambo kadhaa kuyabakisha katika Muungano ni kujiviza akili, ni kujidhalilisha kimkakati na kujidogosha kihadhi.
Si kweli na si kweli kabisa kuwa Katiba Inayopendekezwa ina maslahi na Zanzibar. Haina, haina katu, haina Abadan, kamwe haina. Ni katiba ambayo inatuweka pabaya na pagumu zaidi na imeendelea kuyachukua mamlaka ya Zanzibar na kuyatia katika Muungano.

Vipi Katiba hii itakuwa na maslahi na sisi? Hebu tutizame mambo machache:
1. Kundosha au kuukataa mfumo wa Shirikisho ina maana
a) Zanzibar haiwezi kuwa na hadhi na haki sawa na Serikali ya Muungano.
b) Tumejibakisha pale pale Zanzibar haina mshirikia mwenziwe kwenye Muungano
c) Tumerudi pale pale mshirika wa Zanzibar ni Tanzania na kwa hivyo hakuna usawa
d) Tumeganda pale pale kuwa Tanganyika inasimamiwa na Serikali ya Muungano
e) Tumesalia papo kuwa Bunge la Muungano linatunga sheria za Tanganyika na tunajua kuwa sheria kama hizo hazina nguvu Zanzibar
f) Tumejizuga vile vile kumwita Waziri wa Muungano hata asiesimamia jambo la Muungano kama kilimo bila ya kuwa na hadhi kama hiyo.
g) Tumekwama pale pale Mahakama Kuu ya Tanganyika inaitwa ya Muungano
h) Tumejidanganya vile vile wafanyakazi wote wa Tanganyika wanabaki ni wa Muungano na wale wa Zanzibar mwisho wao Chumbe.

Fikiria hii ndio Zanzibar tuitakayo?
2. Tunajipa moyo kuwa kumfanya Rais wa Zanzibar kuwa ni Makamo wa Rais wa Muungano kuna manufaa kwa Zanzibar ilhali hakutakuwa na msaada wowote.
Tumewapa watu matumaini kuwa hilo litawezesha Rais wa Zanzibar akitoka nje atakuwa na hadhi ya kimuungano wakati tunajua hilo litaleta utata mkubwa zaidi huko mbele. Kwanza kwa suala la gharama pili kutakuwa na mgongano wa maslahi na majukumu yake kama Rais wa Zanzibar vs Umakamo wa Muungano

3. Haiwezekani Rasimu Inayopendekezwa iwe imenyofoa mamlaka zaidi yaliokuwa yameanza kuikaribia Zanzibar kutokana na Rasimu ya Warioba, halafu isemwe kuwa kuna maslahi kwa Zanzibar.
a) Kuondoa uwezo wa Zanzibar kuunda Benki yake
b) Kurudisha nguvu za kuigawa Zanzibar kwa Rais wa Muungano
c) Kukubali ardhi kurembwa
d) Tumerudisha suala la Tume ya Pamoja ya Fedha ambayo imeshindikana kwa miaka kadhaa toka nia hiyo ilipotiwa kwenye Katiba ya 1977.
4. Uamuzi wa kuyatia madaraka ya Serikali ya Zanzibar ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ilhali hakuna sehemu yoyote ya Katiba Inayopendekezwa ambapo madaraka ya Serikali ya Tanzania Bara kama inavyoitwa yameainishwa ni kuendelea kujidanganya.

Pili, kwa kufanya hivyo tunarudi tena pale pale ambapo Zanzibar inaonekana inakiuka Katiba ya Jamhuri pale inapotaka kufanya mabadiliko yenye maslahi yake, ilhali jambo kama hilo halionekani na wala halipo kwa upande wa mshirika mwenziwe, maana mshirika ni huyo huyo Serikali ya Jamhuri na Serikali ya Tanzania Bara.
Ndugu, kaka na dada zangu ujue wazi kuwa maamuzi unayotaka kuyafanya ni makubwa na yana athari ya muda mrefu kwa vizazi vingi vya Zanzibar, ambayo pamoja na tofauti zetu, lakini naamini tunakubaliana kuwa Zanzibar tuipendayo iwepo. Na kuwepo kwake lazima iwe na nguvu na matao yake.
Na kwa dalili zote Rasimu Inayopendekezwa inapopotoa nguvu na matao ya Zanzibar. Inaondosha uzuri na haiba yake kwa kuifanya kuwa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano badala ya kuwa ni nchi moja kamili ndani ya Muungano huu.

Fikirini, pimeni na muvuke nje ya itikadi na mitizamo. Fanya uamuzi ili nafsi yake iwe na amani kwa sababu umefanya uamuzi wako bila ya shindikizo, maelekezo au utashi wa kisiasa, maana wewe kwanza ni Mzanzibari kisha mengine ndio yanafuata.
Nawaomba radhi kwa uamuzi huu wa kuandika barua ya wazi maana isingewezekana kumfika kila mmoja wenu, lakini nataka muamini kuwa barua hii nimeiandika kwa sababu nimeona kuna wajibu kwangu kufanya hivyo.
Unapotaka kupiga kura fikiria, wazia na pimia juu ya uzito wa mchoro wako mmoja tu wa kalamu utavyokuwa na athari kwa nchi yako, watu wako na watoto na wajukuu wako. Fumba macho, rudisha nyuma fikra zako,
kumbubuka wema na ihsani za waliokuzunguka, uliokuwa nao pamoja katika maisha yako na uwafikirie khatma njema ya muda mrefu.

Kumbubuka jukumu lako kwa Mwenyenzi Mungu na fikiria kama hicho ni kitendo cha mwisho cha maisha yako ili ukitie katika mizania nzuri ya maamuzi yako.
Piga HAPANA kwa faida ya Zanzibar na usinitizame mimi kama Ally Saleh, la. 

Mimi ni mtu mmoja tu tena tunaweza kuwa tuna mzigo wa tofauti zetu, lakini pamoja na yote mimi na wewe ndio Zanzibar.
Kwa maslahi ya Zanzibar piga HAPANA.

Ally Saleh
Zanzibar

No comments:

Post a Comment