STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, June 1, 2013

RIPOTI KAMILI YA KUTEKWA NA KUUMIZWA KWA KIBANDA HII HAPA!!


Absalom Kibanda akiwa mahututi baada ya tukiwa na kujeruhiwa kwake

UTANGULIZI: 
Usiku wa Jumanne ya Machi 5 kuamkia Machi 6, 2013, Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006) Ltd, ambaye pia Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda alivamiwa na kujeruhiwa vibaya akiwa nje ya lango la kuingilia nyumbani kwake Mbezi Juu, Dar es Salaam.
Tukio hilo liliishtua na kutikisa taifa kwa kiwango kikubwa si tu katika tasnia ya habari nchini, bali pia jamii kwa ujumla hasa baada ya aina ya utekaji, utesaji na usiri uliotumika katika kufanikisha uhalifu huu kufanana kwa karibu na tukio lilomkuta Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madkatari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka lililotokea karibu miezi tisa kabla ya tukio la Kibanda yaani, usiku wa Juni 26, 2012.
Ukiacha matukio hayo, miezi sita kabla ya Kibanda kutekwa na kuteswa Mwandishi Daudi Mwangosi, aliuawa akiwa mikononi mwa vyombo vya dola Septemba 2, 2012 huko Nyololo, Iringa akiwa kazini.
Tukio la Kibanda limekuwa na sura ya mwendelezo wa mauaji au utesaji wa wanahabari, hasa ikitiliwa maanani kuwa Mwandishi Issa Ngumba (45) wa Radio Kwizera aliyekuwa anafanyia kazi zake katika Wilaya ya Kakonko, Kigoma, Januari mwaka huu, alipigwa risasi na kuuawa katika mazingira ya kutatanisha.
Kama hiyo haitoshi, tukio la kutekwa na kudhuriwa kwa Kibanda limetokea mwezi mmoja tu baada ya Mwandishi wa Gazeti la Tanzania Daima, Shaaban Matutu kupigwa risasi na polisi akiwa nyumbani kwake Dar es Salaam kwa maelezo kuwa kimakosa polisi walidhani Matutu ni jambazi.
Mazingira ya kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda yalitia wasiwasi kuwa upo uwezekano, na dalili zilionyesha kwamba waliofanya kitendo hicho cha kinyama hawakuwa wezi wala majambazi kutokana na ukweli kwamba licha ya kuwa na fedha zipatazo shilingi milioni tatu taslimu ndani ya gari, laptop, simu tatu za gharama (ipad, iphone na Blackberry), watekaji hawa hawakuchukua chochote baada ya kukamilisha uhalifu wao.
Kibanda aliumizwa kwa kiwango kikubwa. Alitobolewa jicho la kushoto, akaumizwa vibaya kichwani kiasi cha kusababisha kuvunjika kwa baadhi ya mifupa ya kichwa. Aling’olewa meno mawili na kucha mbili, tena bila gazi. 
Watekaji hawa, katika unyama wa ajabu kabisa, walimkata pingiri ya kidole cha pete chini ya kucha na kuondokana nayo.
Hali hiyo iliibua maswali mengi, watu wengi wakajiuliza na kutafuta sababu za kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda kiasi hiki. 
Kutokana na kuwapo kwa maelezo mengi yanayotofautiana kuhusu tukio hilo, ikabidi Jukwaa la Wahariri Tanzania lifanye uamuzi.Katika kikao cha Machi 8, 2013 Jukwaa la Wahariri Tanzania liliunda TIMU ya watu watano na kuipa hadidu rejea za kufanya uchunguzi wa kihabari juu ya shambulio hilo kubaini limetokana na nini.
Timu hiyo iliundwa kufuatia uamuzi wa Jukwaa la Wahariri kufanya uchunguzi huo na baada ya kukubalika kwa ombi la ruzuku ya kufanya uchunguzi huo wa kihabari kutoka Mfuko wa Vyombo Vya Habari Tanzania (TMF). 
Ruzuku ya TMF ililenga kiujumla kutumia tukio la Kibanda kuwa chanzo cha kutengeneza mazingira salama zaidi kwa waandishi na wahariri na kwamba kiwango cha matukio ya kuteswa, kupigwa na kuuawa kwa waandishi yanapungua kila mwaka. 
Timu hii imefanya kazi usiku na mchana kwa kwa zaidi ya mwezi. Timu imezungumza na wadau 26. Kati ya hawa yumo Kibanda mwenyewe, mke wake, ndugu zake, wasaidizi wake, waajiri wake wa zamani na wa sasa, viongozi wa kisiasa na vyombo vya dola kutafuta ukweli wa jambo hili. 
Pia tumesoma matamko na habari zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii na magazeti ya kati ya Machi 5, 2012 na Aprili 5, 2012 kwa nia ya kufanya ulinganishi wa taarifa tulizozipata kutokana na uchunguzi na habari zilizochapishwa baada ya kutekwa kwake.
Vyombo vya dola akiwamo Waziri mwenye dhamana walikataa kuhojiwa wakisema kuna tume ya serikali inayofanya kazi hiyo na kwamba kuhojiwa kungeonyesha kutokuwa na imani na tume hiyo.
Leo tunawasilisha muhtasari wa ripoti hii. Ripoti kubwa pamoja na viambatanisho vyake, itachapishwa na kuwekwa katika kitabu kimoja. 
Utaratibu mwingine wa kuchapisha habari ambazo hazijachapishwa kuhusiana na tukio hili (untold stories) pia utaandaliwa kwa ushirikiano na Jukwaa la Wahariri kwa nia ya kuieleza jamii maajabu juu ya kadhia hii.Tulipewa Hadidu Rejea ziafuatazo:
 
HADIDU REJEA:
1. Kuchunguza mazingira ya kabla na baada ya tukio la kushambuliwa kwake. Kabla ya kushambuliwa kwa maana ya kufahamu kama kulikuwa na viashiria vyovyote vinavyoelekea kuwapo kwa mipango ya mashambulizi dhidi yake.
2. Kuchunguza mazingira ya tukio lenyewe kwa kujikitika katika mwenendo wake hasa siku nzima ya Jumanne Machi 5, 2013.
3. Kuangalia mazingira ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari (2006), Ltd na nje ya kampuni hiyo kwa kumulika sababu za kuhama kwake kutoka Free Media mwishoni mwa mwaka jana na kuhamia New Habari.
4. Kuchunguza jambo jingine lolote linaloweza kutoa mwanga wa sababu za kuvamiwa na kupigwa kwa Kibanda.5. Kuchunguza mazingira ya sasa ya kazi kwa wanahabari na kupendekeza hatua za kuchukua kutokana na kile kitakachobainika
 
YALIYOJIRI KATIKA UCHUNGUZI:
1.0. Kuchunguza mazingira ya kabla na baada ya tukio la kushambuliwa kwake. Kabla ya kushambuliwa kwa maana ya kufahamu kama kulikuwa na viashiria vyovyote vinavyoelekea kuwapo kwa mipango ya mashambulizi dhidi yake.
Timu ya uchunguzi ilitumia muda mwingi katika eneo hili, kubaini iwapo kulikuwapo viashiria, sababu au matukio ya wazi yenye mwelekeo wa kujitokeza kwa shambulio hili. Tuliangalia pia iwapo wapo watu au makundi yaliyokwishapata kuonyesha ishara kwa matendo au kwa kauli juu ya uwapo wa nia hii. 
Uchunguzi umebaini kuwa kuliwapo viashiria vingi, isipokuwa Kibanda au watu wake wa karibu hawakupata kufikiri kuwa huenda vingeweza kuleta madhara makubwa kiasi hiki kama ifuatayo:-
 
1.1. Wiki tatu kabla ya Kibanda kuvamiwa, kutekwa na kuumizwa, gari la polisi aina ya gofu Na PT 180 liliwafuatilia kwa muda mrefu Absalom Kibanda na Ofisa Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Ltd, Hussein Bashe likiwa limeegeshwa nje ya ofisi zao Sinza Kijiweni na baadaye likawafuatilia hadi Sinza Makaburini, ambapo walisimamisha magari yao na kuzungumza na polisi hao waliosema walikuwa wanatilia shaka magari yao. Baada ya kuzungumza kwa muda polisi waliondoka.

1.2. Usiku wa Februari 25, mwaka huu majira ya saa 09:00 usiku, Kibanda walivamiwa na watu walioingia kwenye uzio wa nyumba yao wakavunja kioo cha gari analotumia, lakini kioo kilipovunjwa ‘alarm’ ilipiga kelele, Kibanda akatoka nje na watu hao wakakimbia.

1.3. Kutokana na uvamizi huo, Kibanda na wapangaji wengine katika nyumba zilizopo kwenye uzio mmoja, waliona hatari ya kuvamiwa hivyo wakaanza mazungumzo na kampuni ya Ulinzi ya Kiwango, iliyowataka kufunga kamera za usalama na kuweka walinzi watano. Hadi Kibanda anatekwa, walikuwa hawajahitimisha mazungumzo na kampuni hii ya Kiwango.

1.4. Kuna askari anayefanya kazi Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) miezi minane kabla alipata kumpa Kibanda taarifa za kinteligensia, kuwa kulikuwapo mpango wa kumteka na kumuumiza. 
Taarifa kama hizo pia alipewa na wasamaria wanaofanya kazi katika Jeshi la Polisi. Kwa maneno yake Kibanda alisema:
“Kuna rafiki yangu askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kama miezi minane au tisa hivi aliwahi kuniambia ‘unaandika sana usidhani kama watu wanakupenda. Chukua tahadhari hasa unapofika getini nyumbani kwako’. 
Tangu wakati huo nimekuwa nikichukua tahadhari sana.“Wiki mbili kabla ya tukio, niliwahi kuhisi kitu kama hicho [cha kuvamiwa] nikiwa getini. Nilipiga honi wakachelewa kuja kunifungulia, niliogopa sana. Hata nilipoingia ndani nilikuwa nimekosa raha kabisa.“Pia kuna rafiki zangu polisi waliwahi kuniambia kwamba ninatafutwa na kwamba watu wananifuatilia na ikibidi wanitengenezee ajali au kunifanyia kama Ulimboka au Kubenea.”

1.5. Ndani ya miezi mitatu mbele ya mlango wa ofisi yake Kibanda (Free Media Limited) ilikuwa mara kwa mara muda wa asubuhi anapofika ofisini anakuta damu. Haikufahamika kama damu hiyo ilikuwa ni ya binadamu, kuku, ng’ombe, kunguru au mbuzi, bali waliipuuza wakidhani ni masuala ya ushirikina. 
Mhariri Mtendaji wa sasa, Ansbert Ngurumo, amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo.1.6. Mfanyakazi mwandamizi wa Kampuni ya New Habari anakofanya kazi sasa Kibanda ndani ya wiki mbili kabla ya kutekwa na kuumizwa kwake alipata kumwabia Kibanda maneno mazito mara tatu, na hapa tunamnukuhu Kibanda:
“Aliniambia Danny Mwakiteleko [aliyekuwa Naibu Mhariri Mtendaji wa New Habari] hakufa kwa ajali, bali alikufa kutokana na blood clotting (kuganda kwa damu). Hivyo ikitokea mtu ukapata ajali au ukapigwa na kuumizwa sana sehemu za kichwa hivi au tumbo, ni lazima madaktari wadhibiti sana blood clotting.
“Na kweli, nilivyoletwa hapa Milpark hospitalini, madaktari walikuwa wananidunga sindano sita kila siku kwenye kitovu kuzuia blood clotting. .... (jina linahifadhiwa) aliniambia maneno haya mara tatu, katika mazingira yasiliyotarajiwa na kwa msisitizo ambao sikujua maana yake. Nasema .... (jina linahifadhiwa) naye achunguzwe kwa kina. Inawezekana kuna jambo analijua.”
Ofisa huyu, alipishana dakika chache na Kibanda muda wa kutoka ofisini baada ya kipindi cha kwanza cha mechi kati ya Real Madrid na Manchester United kumaliza nusu ya kwanza (half time). Dakika ishirini baadaye Kibanda alishambuliwa.

2.0. Kuchunguza mazingira ya tukio lenyewe kwa kujikitika katika mwenendo wake hasa siku nzima ya Jumanne Machi 5, 2013.
 
2.1. Familia ya Kibanda na Kibanda Mwenyewe hawakuwa na wasiwasi wowote siku hiyo kwani hawakuwa na hisia wala wazo kuwa ungetokea uvamizi huo.

2.2. Kibanda alipopiga honi, mlinzi alisogea langoni kumfungulia. Ghafla akasikia kishindo kikubwa. Akasikia kelele za Kibanda akiomba msaada. Kijana huyu Baraka Ibrahim mwenye umri wa miaka 27, aliogopa. 
Aliogopa kwa mana hakuwa na silaha yoyote mkononi. Hakuwa na panga, kisu, rungu, wala filimbi. Kwa maneno yake anasema:“Nilivyoona ningefungua geti hata mimi ningekufa, nilikimbia kuwaamsha majirani. Sikuwa hata na namba ya simu ya mtu yeyote kati ya mabosi wangu ninaowalinda. 
Nilikuwa mimi tu, imani yangu na Mungu wangu.... kutokana na maisha naifanya hivyo hivyo tu. Vinginevyo milele nisingefanya kazi hii ya ulinzi.”Mlinzi huyo alikimbilia kwa majirani katika nyumba aliyoamini yumo mwanaume, lakini akaanza kumwamsha House Girl, ili house girl amwamshe baba mwenyenyumba. 
Kitendo cha kuamshana na kuwapa taarifa kilichukua dakika tano hadi saba, na ndani ya muda huo, Mlinzi anasema watekaji wa Kibanda walifanya unyama na uasi huo na kuondoka ndani ya muda mfupi kiasi hicho. “Watu hawa wana mafunzo maalumu,” anahitimisha.

2.3. Mke wake alikwenda kazini asubuhi na kurejea nyumbani jioni, lakini tofauti na utaratibu wake wa kawaida ambapo huwa anaangalia televisheni sebuleni hadi Kibanda anaporejea nyumbani, siku hiyo alikwenda kuangalia televisheni akiwa chumbani na usingizi ukampitia. 
Anasema hakusikia honi wala tukio la Kibanda kutekwa. “Hii inanitesa sana moyoni. Najiuliza kwa nini siku hiyo tu sikukaa sebuleni? Kwa nini siku hiyo tu nimelala mapema kabla Baba Joshua hajarudi (machozi yanamlengalenga). Najiuliza sipati jibu.”
 
2.4. Mmoja kati ya wasaidizi wawili wa nyumbani kwa Kibanda, alisikia kelele za Kibanda akiomba msaada. Alimwamsha mwenzake na kumwambia. 
“Nasikia Baba Joshua anapiga kelele kama amevamiwa hivi.” Mwenzake alimwambia “Unaota maana kuna kelele za mpira.” Siku hiyo kulikuwa na mechi kati ya Real Madrid na Manchester United.
Ni kweli zilikuwapo pia kelele za wanaoshangilia mpira siku hiyo, hivyo Kibanda alipoomba msaada, hata waliosikia walidhani watu wanashangilia mpira. Binti aliwaamsha Angela na mwenzake, wakaenda sebuleni, wakakaa na kuchungulia dirishani, wakaona mwanga wa gari getini, lakini baada ya kutosikia kelele yoyote wakarejea kulala wakidhani siye. 
Lakini binti mmoja alibaki sebuleni. Baada ya muda jirani mmoja akampigia simu Angela kumweleza kuwa mumewe ameshambuliwa.
 
2.5. Kibanda kwa upande wake, anasema alipofika getini, alipiga honi, ghafla akaona watu wawili wamesimama pembeni mwa gari lake na mtu wa tatu akiwa kwa mbali. Kisha akasikia kishindo kikubwa, akidhani wanataka kuiba gari, aliatokea mlango wa abiria na kuanza kukimbia huku akiita. 
“Mama Joshua nisaidieeeeee.”Katika kukimbia, aliteleza akaanguka. Huku watesaji wake wakisema mara tatu “Afande piga risasi.” 
Kibanda alijaribu kupambana, akashika rungu, akawahoji amewakosea nini hadi wampige kiasi hicho, lakini hawakumjibu lolote. Waliendelea kumpiga, hadi akapoteza fahamu. Hakujua jicho limetobolewa saa ngapi, meno yameng’olewaje na wala pingiri ya kidole chake imekatawaje. Ifuatayo ni sauti ya Kibanda mwenyewe. Inasikitisha ila tuwe wavumilivu na tuisikilize.

3.0. Kuangalia mazingira ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd na nje ya kampuni hiyo kwa kumulika sababu za kuhama kwake kutoka Free Media mwishoni mwa mwaka jana na kuhamia New Habari.

3.1. Mazingira ya kazi ndani ya New Habari (2006) Limited na Freemedia Limited, yanaacha maswali kadhaa yenye kustahili majibu. Kama ilivyoelezwa kwenye Hadidu Rejea Na: 1, ndani ya kampuni ya New Habari imekuwapo misuguano isiyo na afya kwa kazi ya Kibanda kama mwandishi na tasnia ya habari kwa ujumla.

3.2.Mazingira ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd ni utata. Uhusiano katika chumba cha habari si mzuri. Ndani ya kampuni hawaaminiani na imefikia hatua wanatuhumiana kuwa huenda baadhi ya viongozi ndani ya New Habari wamehusika kumteka na kumuumiza Kibanda. 
Haya yameandikwa ndani ya mitandao ya kijamii, ikidai kwamba kiongozi mmoja ndani ya kampuni hiyo alihusika na utekaji wa Kibanda. Mkurugenzi wa Uhariri, Prince Bagenda anasema waliohusika kusambaza taarifa chafu dhidi ya kiongozi huyo wa New Habari wanatoka ndani ya kampuni hiyo.
 
3.3. Timu ya uchunguzi ilibaini kuwapo mgawanyiko mkubwa ndani ya New Habari (2006) Ltd kwa kuwapo kundi la ‘Habari Wazawa’ na ‘Habari wa Kuja’. Malalamiko mengi yanajikita katika msingi kuwa ajira hazitangazwi na watu wanaajiriwa bila kuzingatia sifa za kitaaluma.

3.4. Kibanda hakuhama Free Media kwa amani. Uchunguzi unaonyesha kuwa miezi kadhaa kabla ya kuondoka kwake alianza kupoteza mamlaka. Mwenyekiti wa Kampuni ya Free Media Ltd, Freeman Mbowe alianza kumsikiliza zaidi msaidizi wake ambaye alikuwa Naibu Mhariri Mtendaji, Ansbert Ngurumo kuliko yeye Kibanda. 
Kwa maneno yake, anasema:“Nilihofu kuwa Mbowe anaweza kutugombanisha. Nikaona ni bora niondoke nisije nikagombana na Mbowe au Ngurumo.”
Anasema alianza kupoteza mamlaka yake na kutoaminika kwa mwajiri wake baada ya kuandika makala kuhusu Abdulrahman Kinana ambayo kabla ya kuiandika hakuwa na wazo la kuondoka. Yaliyofuata baada ya makala hiyo, yalimshukuma aondoke.
 
4.0. Kuchunguza jambo jingine lolote linaloweza kutoa mwanga wa sababu za kuvamiwa na kupigwa kwa Kibanda.

4.1. Uchunguzi ulifuatilia masuala mbalimbali ikiwamo miendendo ya watu waliotajwa kwa njia moja au nyingine kuhusinaa na tukio hili. 
 
Hata hivyo, karibu watu wote waliohojiwa, akiwamo Kibanda mwenyewe aliyeumizwa walimtaja kwa kutilia shaka mwenendo wa kijana Joseph Ludovick. Hofu yao, iliongezwa nguvu na maandishi aliyoyachapisha Ludovick kwenye mitandano ya kijamii siku ya Machi 6, 2013.

4.2. Usiku aliotekwa na kuumizwa Kibanda, Ludovick naye alidai kuwa ametekwa katika eneo la Shekilango na kupelekwa hadi Kigogo. Baada ya kutekwa aliibiwa kila kitu, ikiwamo begi, laptop, simu mbili, fedha taslimu Sh 35,000, akavuliwa nguo na kubaki na chupi tu. Pia alieleza kuwa alitoa taarifa hizo kituo cha polisi Mabibo.
 
4.3. Maelezo ya Ludovick yalitiliwa shaka na watu wengi hasa baada ya kuleeza kuwa watekaji walitumia muda wa saa mbili kumtoa Shekilango hadi Mabibo, umbali ambao kwa kawaida mwendo wake hauwezi kuzidi dakika 10. 
 
4.4. Daniel Chongolo aliiambia timu kuwa alfajiri ya Machi 6, siku anayodai kutekwa Ludovick yeye alimuona eneo la Mabibo wakati anatoka Muhimbili. Chongolo alikwenda kituo cha polisi Mabibo na kupewa taarifa kuwa Ludovick alitoa taarifa polisi kuwa alikuwa ametekwa ila akarudishiwa mali zake zote. 
“Alipouliza amefuata nini polisi, akawaambia kama raia mwema amefika kuandikisha kumbukumbu kwa nia ya kuonyesha kiwango cha uhalifu kinavyoongezeka nchini,” anasema Chongolo. Timu ya uchunguzi ilikataliwa kupitia leja ya polisi kama itakavyoelezwa hapa chini.

4.5. Pia taarifa za uchunguzi wa timu hii zinathibitisha kuwapo kwa utata juu ya madai ya kuibwa kwa simu za Joseph Ludovick, kwani simu yake ya tigo (inayodaiwa kuibwa) ilitumika saa 01:21 asubuhi siku ya Machi 6, 2013. Muda huu ofisi za Serikali na Kampuni ya Tigo zilikuwa hazijafunguliwa
 
5.0. Kuchunguza mazingira ya sasa ya kazi kwa wanahabari na kupendekeza hatua za kuchukua kutokana na kile kitakachobainika.

5.1. Uchunguzi umebaini kuwa maisha ya wanahabari yapo hatarini. Hatari hii inatokana na makundi mengi yenye masilahi kuwaona wanahabari wanaosimamia ukweli kuwa maadui wa masilahi yao haramu. Kuna hatari kubwa inayowakabili waandishi wakati nchi inapoelekea kwenye uchaguzi wa mwaka 2015.

5.2. Uchunguzi umebaini kuwa usiri umepungua katika vyombo vya habari. Tofauti na zamani ambapo habari nyeti ziliandikwa kwa kuhifadhi majina ya waandishi wakitumia jina la MWANDISHI WETU. Simu hizi hata habari za kutisha waandishi wanaweka majina yao na hata wasipoweka, ndani ya vyumba vya habari vingi waandishi wapo tayari kutaja nani ameandika habari fulani.

5.3. Usaliti miongoni mwa waandishi wenyewe ndani ya vyumba vya habari unazidi kuongezeka na usipodhibitiwa hali itazidi kuwa mbaya zaidi. Mwenyekiti wa MOAT, Dk. Reginald Mengi anasema: “Hili ni jambo muhimu sana. Tuache usaliti vinginevyo wengi wataumia.”

5.4. Pia alishauri waandishi wa habari kurejea katika msingi wa taaluma, ambayo inawataka wao kuwa ndio wenye kuendesha vyombo vya habari badala ya kutegemea matakwa ya wamiliki au makundi yenye masilahi binafsi.


6.0. KILICHOBAINIKA:
6.1. Uchambuzi uliofanywa ni timu hii umebaini kuwa hoja nne zinazungumzwa kuhusiana na kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda. 
 
Hoja hizi ni:-
(i) Kazi yake ya uandishi wa habari
(ii) Uhusiano wa kisiasa na vyama au wanasiasa mbalimbali
(iii)Uhusiano wa kijamii ikiwamo mapenzi
(iv) Vitendo vya rushwa.

6.2. Timu imejiridhisha kutokana na majibu ya wengi kuwa dhana ya mapenzi na rushwa, havina nafasi yoyote katika tukio hili. Wote waliohojiwa walieleza pasi na shaka kwamba suala hili la kushambuliwa na kuumizwa kwa kiwango kikubwa kwa Kibanda, halina uhusiano wowote na rushwa au mapenzi.
 
6.3. Kutokana na yaliyotajwa hapo juu kazi yake na siasa vikiunganishwa vimechangia kwa kiasi kikubwa kuvamiwa kwa Kibanda. Timu imebaini kuwa kuna kutupiana mpira kati ya vyombo vya dola na vyama vya siasa. Mchezo huu mchafu unaweza ukawa mwanzo wa kuumizwa kwa Kibanda na waandishi wengine.

6.4. Baadhi ya waliohojiwa walidai kuwa utekaji huu umefanywa na vyombo vya dola ukiwa sehemu ya mpango mkakati wa vyombo hivi kukihusisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na vitendo vya ugaidi.
 
6.5. Wanayataja matukio ya Uchaguzi Mdogo wa Igunga, maandamano ya Morogoro na Mkanda anaodaiwa kurekodiwa Mkurugenzi wa Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare kuwa vililenga kukifanya CHADEMA kichukiwe na Watanzania kwa kukitaja kama chama cha kigaidi ambacho kinateka watu na kinawaumiza.

6.6. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anadai kwamba mpango kama huo vyombo vya dola viliutumia kwa NCCR Mageuzi vikakisambaratisha, Chama cha Wananchi (CUF) kilisingiziwa udini kikapoteza mwelekeo na sasa vyombo hivyo vililenga kukifanya CHADEMA kionekane cha kigaidi mbele ya macho ya jamii ndiyo maana imerekodiwa mikanda kwa nia ya kuitumia kujenga hoja hiyo.

6.7. Wakati Mbowe akisema hayo, baadhi ya watu waliohojiwa wanadai kuwa CHADEMA kimepewa mafunzo na ushauri kutoka nje ya nchi kuwa kikitumia baadhi ya watumishi wa vyombo vya dola wasiokuwa waaminifu kuteka, kuumiza na hata kuua baadhi ya watu maarufu nchini wakiwamo waandishi na wanasiasa, basi wananchi wataamini kuwa Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake kimeshindwa uongozi na sasa kimeanza kazi ya kuua wanaowapinga.

6.8. Kwa njia hiyo, inaelezwa kuwa hesabu za Chadema ni kuwa wananchi wataichukia CCM na Serikali yake na kukipa nafasi ya kuingia madarakani. Hapa kauli ya Chadema kuwa NCHI HAITATAWALIKA itakuwa imetimia.

6.9. Dhana nyingine iliyojitokeza ni kuwa wapo wafanyabiashara ambao wana vita binafsi, hivyo wanaamua kuumiza watu wasiowaunga mkono katika mipango yao na hilo ndilo limemkumba Kibanda, baada ya kuwa ameepusha mauaji ya mwandishi mmoja na aliyekuwa ameandaa mpango wa kuua mwandishi huyo hakuridhika hivyo akaamua amshughulikie Kibanda.

7.0. MAPENDEKEZO: 
 
Baada ya Timu kupata taarifa hizi na nyingine nyingi, inapendekeza yafuatayo:-

7.1. Taarifa hii ichukuliwe kama chanzo cha uchunguzi zaidi wa vyombo husika.
 
7.2. Yanahitajika marekebisho makubwa na ya haraka katika mifumo ya uendeshaji wa vyumba vya habari kwa nia ya kurejesha misingi ya uandishi wa habari inayokubalika.

7.3. Usalama wa wanahabari unapaswa kupewa kipaumbele na wamiliki, wanahabari wenyewe na jamii kwa ujumla. Hapa Timu inapendekeza yawepo mafunzo ya kuwawezesha wanahabari kutambua viashiria vya hatari na kuchukua hatua mara moja.

7.4. Kwa kiwango alichoumizwa Kibanda iwapo mwajiri wake asingejitolea kugharamia matibabu, hatujui hatima yake ingekuwaje leo hii. 
Tunapendekeza taasisi na mifuko mbalimbali inayojihusisha na masuala ya wanahabari kama Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) , Baraza la Habari Tanzania (MCT), Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kuanzisha mfuko wa pamoja utakaotumika kugharamia matibabu ya waandishi watakaoumia wakiwa kazini.

7.5. Tukio la kutekwa kwa Kibanda limeonyesha mwanga kuwa wahariri tumegawanyika mno. Habari zilizochapishwa katika magazeti mbalimbali na mitandao ya kijamii zimeonyesha haja ya kuwafanya wahariri kuwa kitu kimoja kwa kuondoa tofauti zao zisizo na masilahi kwa tasnia ya habari.

7.6. Kuna viashiria vingi kuwa kuelekea mwaka 2015 matukio ya waandishi kuumizwa au kutekwa yanaweza kuongezeka kutokana na wanasiasa na vyama kuwania madaraka huku wakitumia baadhi ya watumishi katika vyombo vya dola. Kwa mantiki hiyo, vyombo vya habari na waandishi wa habari wachukue tahadhari kuanzia sasa.

7.7. Taasisi za habari zifanye juhudi za makusudi kukutana na vyama viwili vya siasa vya CCM na CHADEMA haraka iwezekanavyo, kuzungumzia viashiria hivi vya hatari vinavyoelekea kuvuruga amani ya Tanzania.

8.0. HITIMISHO: 
 
Ni dhahiri kuwa kupigwa na kuteswa kwa Kibanda kumejiegemeza katika siasa na kazi yake, hali inayofanya makundi muhimu kuchukua wajibu wa msingi. Kwa upande wa Serikali ni muhimu kufuatilia viashiria katika taarifa hii kwa nia ya kupata ukweli zaidi na kuchukua hatua stahiki za kisheria dhidi ya wahusika.
Na kwa upande wa vyombo vya habari na taasisi za kihabari zinapaswa kutambua viashiria vinavyohatarisha usalama wa waandishi wa habari na wahariri na kutengeneza mazingira yatayokuwa salama zaidi kwa waandishi kufanya kazi zao.

9.0. SHUKRANI:

9.1. Tunapenda kulishukuru Jukwaa la Wahariri Tanzania, kwa kufanya uamuzi sahihi wa kuwezesha kufanyika kwa uchunguzi huu ulioanza kuonyesha mwanga wa nini kilitokea.

9.2. Tunapenda kulishukuru Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa kushiriki kikamilifu na kuiwezesha timu hii kwa Rasilimali Watu na Mali kufanikisha kazi hii.

9.3. Tunapenda kuwashukuru Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) kwa uwezeshaji wa ruzuku, uliofanikisha kufanya uchunguzi wa kihabari uliohusisha kwenda nchini Afrika Kusini kufanya mahojiano na Kibanda. Uwezeshaji huo pia unahusisha kutengeneza mwongozo kwa waandishi wenye lengo la kuwaepusha na hatari za kiusalama.

9.4. Tunawashukuru Kibanda, mkewe Angela, wanafamilia, ndugu na jamaa wa Kibanda na wanahabari wote waliohojiwa kwa ushirikiano mkubwa walioutoa kwa Timu hii.

9.5. Tunawashukuru wahariri wote kila mtu kwa nafasi yake, kutokana na ushauri wa mara kwa mara mliotupatia katika kufanikisha uchunguzi huu.


10.0. WAJUMBE WA TIMU:
Timu hii iliundwa na wajumbe watano ambalo ni:1. Deodatus Balile – Mwenyekiti
2. Pili Mtambalike – Mjumbe
3. Jane Mihanji – Mjumbe
4. Tumaini Mwailenge – Mjumbe
5. Rashid Kejo – Katibu

Mwisho
NB:TAARIFA YA UCHUGUZI JUU YA KUTEKWA NA KUUMIZWA KWA ABSALOM KIBANDA IMEWASILISHWA NYUMBANI HOTEL - TANGA MEI 30, 2013

Mkataba Ligi Kuu sasa kushirikisha pande tatu

SHIRIKISHO la soka (TFF) limesema kuwa baada ya kuundwa kwa kamati ya ligi ambayo ina majukumu ya kusimamia ligi kuu ya Bara, mikataba ya udhamini ya michuano hiyo ya klabu sasa itakuwa ikisainiwa na pande tatu.
Hivi karibuni Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema mikataba ya wadhamini wa ligi kuu Ya Bara itakuwa ikisainiwa na Kamati ya ligi, TFF pamoja na wadhamini husika lengo ikiwa ni kuiboresha ligi na kuepuka manung'uniko kutoka kwa klabu.
"Kwa sasa si TFF peke yake wanaoingia mikataba na wadhamini... mikataba yote ya udhamini wa ligi kuu itakuwa ikisainiwa kwa pamoja na Kamati ya ligi, sisi TFF kama wasimamizi wa mpira hapa nchini pamoja na wadhamini husika," alisema Osiah.
Alisema kuwa hiyo itaongeza ubora wa ligi na kuweka hali ya uwazi wa mikataba ya kudhamini ligi kuu hapa nchini.
Osiah alisema katika mkataba na mdhamini wa sasa wa ligi kuu, kampuni ya huduma za simu ya Vodacom, kuna kipengele kinachotoa nafasi ya kufanya mapitio ya mkataba huo kila msimu unapomalizika.
Alisema kuwa kamati ya ligi imekuwa ikikutana na klabu za ligi kuu na hivikaribuni kamati hiyo itatoa msimamo wake juu ya udhamini wa Vodacom.
Katika msimu uliomalizika hivi karibuni, klabu iliyoshuka daraja ya African Lyon iliingia kwenye msuguano na TFF baada ya kuingia mkataba wa kudhaminiwa na kampuni ya Zantel ambao ni washindani wa kibiashara na Vodacom.
TFF iliiamuru African Lyon kutotumia nembo ya kampuni hiyo ya Zantel kwa kuwa tayari jezi zote za timu za ligi kuu zina nembo ya Vodacom kama mdhamini mkuu wa ligi.

Ufaulu Kiadto cha sita waongezeka 'kiduchu'

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEi4wTtUyMRmkPrNtJ_YP5QyVIBrnZSzDWWrb6c0dI3nXm2Ag6H8HZPwgV9fUwi9-b3vStZJ9d9HqAtB_xSOxuQsVeNKt0_09WSNwkBHVUnfO18aXRtSkXP_emGk-F-k1Om3TPSUhYmH_Fl6/s320/DSC_8458.JPG
Wanafunzi wakifanya mitihani
UFAULU wa wahitimu wa Kidato cha Sita mwaka huu umeongezeka kwa asilimia 0.20 kutoka asilimia 87.65  mwaka jana hadi asilimia 87.85.
Kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyotangazwa jana jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania, Dk. Charles Msonde kwa niaba ya Katibu Mtendaji,  jumla ya watahiniwa 44,366 sawa na asilimia 87.84 ya waliofanya mtihani wamefaulu.
Alisema kati ya watahiniwa hao, wasichana waliofaulu ni 14,622 na wavulana ni 29,744 sawa na asilimia 87.2.
Akifafanua alisema jumla ya watahiniwa 52,513 waliandikishwa kufanya mtihani huo,  50, 611 sawa na asilimia 96.38 waliufanya huku 1,902 sawa na asilimia 3.62 hawakufanya.
Aliongeza kuwa, watahiniwa wa shule waliofaulu ni 40,242 sawa na asilimia 93.92.
Alisema idadi ya wasichana ni 14,622 na wavulana ni 29,744 sawa na asilimia 87.2 ambapo kwa mwaka jana watahiniwa 40,775 sawa na asilimia 92.30  walifaulu.
Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea alisema waliofahulu ni 4,124 sawa na asilimia 53.87 wakati kwa mwaka jana walikuwa ni 5,883 sawa na asilimia 64.96 .
UBORA WA UFAULU
Kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa wa shule, alisema unaonyesha jumla yao ni 35,880 sawa na asilimia 83.74 wamefaulu katika daraja la 1 -111 wakiwemo wasichana  12,108 sawa na asilimia 87.30 na wavulana 23,772 sawa na asilimia 82.04.
Akifafanua  alisema idadi ya ufaulu daraja la kwanza ni 325 sawa na asilimia 0.76 ambapo wavulana ni 188 sawa na asilimia 0.65 wakati wasichana ni 137 sawa na asilimia 0.99.
Alisema idadi ya ufaulu daraja la pili ni 5,372 sawa na asilimia 12.54 ambapo wavulana ni 3,142 sawa na asilimia 10.84 na wasichana 5,372  sawa na asilimia 12.54.
Katika daraja la tatu jumla ya idadi ni 30,183 sawa na asilimia 70.45 ambapo wavulana 20,442 sawa na asilimia 70.55 na wasichana ni  9,741 sawa na asilimia 70.24.
Alisema katika daraja la nne jumla ya idadi ya watahiniwa ni 4,362 sawa na asilimia 10.18 wavulana ni 3,184 sawa na asilimia 10.99 na wasichana ni 1,178 sawa na asilimia 8.49.
Kwa upande wa daraja sifuri jumla ya idadi ni 2,604 sawa na asilimia 6.08 ambapo wavulana ni 2,021 sawa na asilimia 6.97 na wasichana ni 583 sawa na asilimia 4.20.
MASOMO YALIYOFANYWA VIZURI
Aliyataja kuwa ni Historia, Jiografia, Kiingereza, Kemia, Biolojia, Kilimo, Sayansi ya Kompyuta, Uchumi na Uhasibu ambapo alisema yamefanywa vizuri tofauti na mwaka uliopita.
SHULE KUMI BORA
Alitaja kundi la shule zenye watahiniwa 30 na zaidi na maeneo zilizopo kwenye mabano kuwa ni  Marian girls (Pwani),  Mzumbe (Morogoro), Fedha Boys Dar es Salaam), Ilboru (Arusha), Kisimiri Arusha), St Mary Mazinde Juu (Tanga), Tabora Girls (Tabora), Igowele (Iringa), Kibaha (Pwani) na Kifungilo Girls (Tanga).
SHULE KUMI ZA MWISHO
Alizitaja kuwa ni Osward Mang’ombe (Mara), Green Acres (Dar es Salaam), Bariadi (Simiyu),
Pemba Ismail College (Pemba), Mazizini, High View International, Mwanakwerekwe, Hamamni, Dunga na Lumumba  zote za Unguja.
Akitaja shule kumi zenye watahiniwa chini ya 30 kuwa ni Palloti Girls (Singida), Itamba (Njombe), Kibara (Mara), St. Luise Mbinga Girls (Ruvuma) St. Peter Seminari (Morogoro), Peramiho Girls (Ruvuma), St. James Seminari, Masama Girls, Parane na Sangiti zote za Kilimanjaro).
SHULE ZA MWISHO
Alizitaja kuwa ni St. Mary’s na Mzizima za Dar es Salaam, Mbarali Preparatory, Philter Federal, Mpapa Al-Falaah Muslim zote za Unguja, Hijra Seminari (Dodoma),  Tweyambe (Kagera), Presbyterian Seminari   (Morogoro) Nianjema (Pwani).

TANO BORA KITAIFA
Naibu  huyo alitaja watainiwa watano bora kitaifa katika masomo ya Sayansi kuwa ni Erasmi Inyase (Ilboro Arusha), Maige Majuto (Kisimiri Arusha), Gasper Mung’ong’o (Fedha Boys Dar es Salaam), Gasper Setus (St. James Seminari Kilimanjaro) na Lucylight Mallya (Marian Girls Pwani).
 Pia alitaja wasichana watano bora kitaifa kwa masomo ya Sayansi  kuwa ni Mallya , Edna Kibango (Msalato Dodoma), Sarah Kimario (St. Mary’s Mzinde Juu Tanga), Veronica Mwamfupe (Marian Girls Pwani) na Beatrice Issara (St Marys Goreti Kilimanjaro).
Kwa upande wa wavulana ni Inyase, Majuto , Mung’ong’o, Setus na  Christopher Stanslaus (Mzumbe Morogoro).
Alitaja watahiniwa watano bora kitaifa kwa masomo ya biashara ni Eric Mulogo (Tusiime Dar es Salaam), Alicia Filbert (Nganza Mwanza), Evart Edward  (Kibaha Pwani), Annastazia Renatus (Tambaza) na Peterson Meena  (Mbezi Beach).
Wasichana ni Alicia, Anastazia, Mary Bujiku (St. Anthony’s), Getruda Patrick (Barbor-Johansson (Dar es Salaam) Leticia Kayange (Weruweru Kilimanjaro).

Wavulana ni Mulogo, Edward, Meena, Frank Bunuma (Kibaha Pwani) na Abdallah Juma (Kazima Tabora).
 Watahiniwa watano bora kitaifa kwa masomo ya lugha na Sayansi ya jamii ni Asia Mtini (Barbro-Johansson (Dar), Godlove Ngowo (Majengo Kilimanjaro), Johnason Macha (Njombe), Hamis Mwita Ilboru, Sia Sandi (Marian Girls Pwani).
Alitaja wasichana watano bora katika masomo hayo kuwa ni Aisa, Sia, Jacqueline Agrippa (Masama Girls (Korogwe), Dhulfa Kangungu (Korogwe Girls) na Angelika Chengula (Msalato).
Kwa upande wa wavulana ni Ngowo, Macha,  Mwita, Abubakar Msangule  (Swilla Mbeya) na Alex Mkunda (Kibiti Pwani).

YALIYOZUIWA

Alisema baraza limeyazuia matokeo ya watahiniwa 89 wa shule ambazo hawajalipa ada ya mitihani na kwamba yatatolewa pindi wahusika watakapolipa ada na faini.
Alisema wapo watahiniwa kumi waliopata tatizo la kiafya na kufanya baadhi ya mitihani na wengine 17 walishindwa kufanya mitihani yote kutokana na tatizo hilo ambao watapata fursa ya kuifanya ile ya 2014.
UDANGANYIFU
Alisema wamefuta matokeo yote ya mtihani wa mtahiniwa mmoja wa shule na watahiniwa watatu wa kujitegemea baada ya kubainika kufanya udanganyifu.
Alisema jitihada za serikali katika kukabiliana na tatizo la udanganyifu zimefanya tatizo hilo kupungua kutoka wanafunzi sita mwaka jana na kufikia wanne mwaka huu.
Katika mtihani wa mwaka huu watahiniwa wa shule  43,231 waliosajiliwa, 42,952 sawa na asilimia 99.35 walifanya ambapo wasichana ni 13,883 sawa na asilimia 99.54 na wavulana ni 29,069 sawa na asilimia 99.27.
Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea kati ya 9,282 waliosajiliwa, 7,659 sawa na asilimia 82.51 walifanya mtihani na watahiniwa 1,623 sawa na asilimia 17.49 hawakufanya.

Friday, May 31, 2013

AJALI: AFA KWA KUANGUKIA KICHWA AKIPANDA DALA DALA ILALA

afariki-akidandia-daladala-0
afariki-akidandia-daladala
Add caption


MTU mmoja ambaye jina lake bado halijafahamika, amefariki dunia baada ya kuteleza na kuanguka wakati alipokua akijaribu kudandia Daladala maeneo ya Ilala Boma, Jijini Dar es Salaam leo. Marehemu huyo baada ya kuanguka na kupiga kichwa kwenye lami, alipasuka kichwa na kuvuja damu nyingi kichwani, na kufariki katika eneo la tukio.
 
Credit:Superstarstz

Mwili wa Ngwair sasa kuwasili J'pili, mazishi yake J'4

Ngwair enzi za uhai wake


MWILI wa marehemu Albert Mangwea 'Ngwair', aliyekuwa nyota wa muziki wa kizazi kipya kupitia miondoko ya Hip Hop, hautawasili tena kesho kama ilivyokuwa imepangwa na badala yake utawasilia siku ya Jumapili na kuagwa Jumatatu kabla ya kusafirishwa kwenda kuzikwa siku ya Jumanne mjini Morogoro.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hivi punde na Kamati ya Mazishi ya msanii huyo aliyefariki nchini Afrika Kusini, imesema sababu ya mwili wa Ngwair kurejeshwa kesho umetokana na watanzania waliopo nchini humo kuomba wapewe nafasi ya kumuaga kesho ndipo usafirishwe kuja Tanzania.
Taarifa inasema kuwa watanzania hao ambao kwa namna moja au nyingine wamekuwa mstari wa mbele katika kuratibu shughuli zote tangu Ngwair apelekwe hospitali mpaka kufariki kwake na kuhamishwa hospitali aliyokuwa amehifadhiwa na kupelekwa hospitali ya Serikali hivyo wameona ni vyema nao wakamuaga mpendwa wao.
Kutokana na ratiba hiyo kupanguliwa utaratibu kwa sasa ni kwamba Jumamosi mwili huo wa Ngwair utaagwa Afrika Kusini na kusafirishwa kurejeshwa Tanzania ambapo utawasilia Jumapili saa 8 mchana kabla ya kupelekwa moja kwa moja Muhimbili kuhifadhiwa.
Jumatatu kuanzia saa 2 mpaka saa 6 mashabiki wa muziki watauaga mwili huo kabla ya kuanza safari ya kupelekwa Morogoro kwa mazishi.
Kamati hiyo imesisitiza watanzania waendelea kujitolea michango kwa ajili ya kufanikisha mazishi ya Ngwair kwa kutuma fedha kwa simu ya kaka wa marehemu Kenneth Mangwea 0754-967738 au katika akaunti ya namba 2012505840 Benki ya NMB kwa jina la Kenneth B Mwangweha.
Katika hatua nyingine, msanii aliyekuwa hoi pamoja na Ngwair, M2P anaendelea vyema ambapo hivi punde amehojiwa 'live' na Clouds FM na kusema anaendelea vizuri japo anasumbuliwa na maumivu ya kichwa na kifua na ameanza kunywa vitu vyepesi  na anamshukuru Mungu hali yake inatengemaa.
Hata hivyo ni kwamba M2P hajui chochote kinachoendelea juu ya kifo cha Ngwair kwa vile walimuongopea kwamba rafikie amerejea Tanzania wakati yeye akiwa katika hali mbaya ya kiafya.

Neymar: Nahisi kutetemeka kucheza na Messi

http://upload.wikimedia.org/wikipedia/commons/3/3e/Messi_with_Neymar_Junior_the_Future_of_Brazil.jpg
Messi na Neymar
RIO DE JANEIRO, Brazil
MSHAMBULIAJI mpya wa Barcelona, Neymar amesema anajihisi "kupagawa" kila anapofikiria kuja kucheza pamoja na Lionel Messi.
Mbrazil huyo mwenye umri wa miaka 21, ambaye alibainisha wiki iliyopita kwamba anajiunga na mabingwa wa La Liga kwa dili la uhamisho la paundi milioni 28, alisema kuwa wakati umefika wa kuja kuwa nyota wa soka la Ulaya.
Akizungumza katika uzinduzi wa viatu vya Nike Hypervenom, Neymar alisema: "Najisikia kupagawa. Hii ni ndoto iliyokuwa kweli. Kucheza na Messi na wachezaji wengine wenye vipaji pale Barcelona ni jambo lililonifanya nichague kujiunga nao."
Nyota huyo pambo la soka la Brazil alipata ofa kutoka katika klabu kadhaa zikiwamo Real Madrid na Chelsea lakini alichagua kwenda kucheza na 'fundi' wa Kiargentina Messi klabuni Nou Camp baada ya kujadiliana na familia yake.
"Yalikuwa maamuzi magumu lakini niliamua pamoja na familia yangu,” alibainisha. “Walinisaidia sana. Nina furaha lakini pia huzuni kwa kuondoka katika timu (Santos) ambayo nimekuwa kwa miaka mingi. Natakiwa kuitumia fursa."
Neymar aliongeza kwamba baada ya uhamisho wake sasa anaweka akili zake katika kuitumikia timu ya taifa ya Brazil, huku michuano ya Kombe la Shirikisho ikitarajiwa kuanza Juni 15.
"Kuvaa jezi ya njano ni majukumu lakini unatakiwa kuivaa na kucheza kama vile unacheza uani kwako,” alisema. “Unatakiwa uwe na furaha.
“Daima nimekuwa nikitaka kuchezea Brazil na kuwa mchezaji kama Ronaldo, Ronaldinho na pia Robinho na Kaka - kuna wachezaji wengi sana ninaopwapenda."

RONALDINHO
Mwanasoka bora wa zamani wa dunia, Ronaldinho (33) amepongeza uhamisho wa Neymar kutua katika klabu yake ya zamani ya Barcelona.
Ronaldinho anaamini kwamba Neymar atafurahia soka la Ulaya kwa sababu ana kipaji kinachohitajika kuwa mmoja wa wachezaji bora duniani.
Macho yote yameelekezwa kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 baada ya kukamilisha uhamisho wake wa kwenda Barcelona, na Ronaldinho, ambaye aliichezea barca kwa miaka mitano, anaamini kwamba yosso huyo atatamba Ulaya
"Itakuwa jambo zuri kumuona akiichezea Barcelona," Ronaldinho aliwaambia waandishi wa habari wa Brazil. "Barca ni klabu kubwa katika moja ya ligi bora duniani.
"Atazoea kwa sababu ana kila kitu kinachohitajika kumfanya awe bora duniani."
Neymar anatarajiwa kutambulishwa Barcelona mapema mwezi ujao kabla ya kurejea kuatika maandalizi ya kuiwakilisha Brazil katika michuano ya Kombe la Shirikisho Juni 15.
Ronaldinho ameachwa nje ya kikosi cha kocha Luiz Felipe Scolari kitakachoshiriki michuano hiyo.

NEYMAR HABARI NYINGINE
Kocha wa timu ya taifa ya Hispania, Vicente Del Bosque amemsifu Neymar akisema ni "habari nyingine" na akiongeza kuwa "ni fundi mwenye uwezo mkubwa. Atafanya makuibwa."
Del Bosque pia anaamini kwamba yosso huyo Mbrazil hatapata shida kucheza pamoja na 'supastaa' wa Barca, Lionel Messi. "Tulikuwa na majina makubwa mengi katika chumba cha kuvalia wakati naifundisha Real Madrid na tulifanikiwa sana."

UTATA WA JEZI
Miamba hao wa Catalunya watalazimika kutafuta namba ambayo Mbrazil huyo anaipenda, jambo ambalo litakuwa gumu kwa sababu namba zinazomvutia ni 7 inayovaliwa na David Villa, 11 inayovaliwa na Thiago Alcantara.
Duka la klabu hiyo limeshaanza kuuza jezi zenye jina la Neymar lakini zikiwa na namba zote hizo mbili.

Mzee Yusuf kupamba Miss Arusha Juni 8

http://www.gushit.com/files/bookmark_photos/7a6b3e0e06L.jpg
Mzee Yusuf
KUNDI la muziki wa taarabu linaloongozwa na muimbaji nyota wa miondoko hiyo nchini, Mzee Yusuf, Jahazi Modern inatarajia kuinogesha usiku wa kumsaka mlimbwende wa mkoa wa Arusha (Redds Miss Arusha) inatarajiwa kufanyika June 8 katika ukumbi wa triple A uliopo jijini humo.
Akizungumza na waandishi wa habari muandaaji wa shindano hilo Phidesia Mwakatalima alisema kuwa shindano hilo litafanyika usiku wa jumamosi june nane katika uwanja wa ukumbi wa Triple A uliopo ndani ya jiji la Arusha.
Alisema kuwa jumla ya walibwende kumi na tano 15 kutoka katika vitongoji vitatu vya jiji la Arusha ambapo alivitaja kuwa ni pamoja na kitongoji cha Njiro,Arusha mjini(Arusha city cetre)pamoja na kitongoji cha Monduli.
Alibainisha kuwa mpaka sasa warembo wameshaingia kambini wameanza kujifua kwa ajili ya shindano hilo huku akibainisha kuwa kwa mwaka huu lazima mrembo wa Tanzania (Redds Miss Tanzania )atokee mkoa wa Arusha.
Alisema kuwa zawadi mbalimbali zitatolewa ikiwemo kuwasomesha warembo katika vyuo mbalimbali lungha ya kiswahili, kingereza pamoja na kifaransa.
Kwa upande wa wadhamini waliothamini shindano hili walisema kuwa ni pamoja na perfect choice super markety, libeneke la kaskazini blog, triple A FM, Radio 5 FM, Sunrise FM, Mambo Jambo FM, Alayance france,Geo Securty,Cassaranda wear,Meru Spring Water Pamoja na Otakef
Motel.

HII NDIYO HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI ILIYOLETA VURUMAI JANA




HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHE. EZEKIAH DIBOGO WENJE (MB) KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014
1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika bajeti ya wizara hii mwaka 2012/13, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA ilibaini mapungufu mengi ya kiutendaji na kiuwajibikaji katika wizara hii, na hivyo kuitaka Serikali kufanya mambo yafuatayo ili kuboresha utendaji na ufanisi:
1. Kuziwezesha balozi zetu nje kwa kuzitengea fedha za kutosha  ili ziweze kufanya kazi kwa ufanisi
2. Kutoa idadi ya majengo ya balozi zetu nje (nyumba za mabalozi, nyumba za maafisa wa balozi na ofisi za balozi) kwa mchanganuo wa idadi ya nyumba katika nchi na kama nyumba hizo zina hati miliki au la.
3. Kutoa taarifa ya namna kila ubalozi ulivyotekeleza sera ya Diplomasia ya uchumi kwa kuzingatia kwamba balozi nyingi ziko hoi kifedha kiasi cha kwamba waambata wa kiuchumi wanakosa fedha za kusafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa ajili ya upelelezi wa masuala ya kiuchumi.
4. Kulikarabati jengo la ubalozi wa Tanzania huko Msumbiji lililokuwa limechakaa kwa kutofanyiwa ukarabati tangu 1975 ingawa jengo hilo tulipewa bure na Serikali ya Msumbiji chini ya FRELIMO.
5. Kujenga kitega uchumi katika kiwanja  cha Tanzania kilichopo Dubai na kukiendeleza kiwanja namba 19 tulichopewa bure na Serikali ya Uingereza kilichopo Uingereza (Central London) ambavyo vimekuwa maficho ya wezi kwa kutoendelezwa kwa muda mrefu na kusababisha Serikali za nchi hizo kutaka kutaifisha viwanja hivyo.
6. Kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma za balozi zetu nchini China, na Uingereza kutoa hati za kusafiria kwa mataifa mengine hasa ya Afrika Magharibi ili kubaini ukweli na kuliondolea taifa aibu kutokana na tuhuma hizi.
7. Kukarabati jengo la ubalozi wetu nchini China ambalo lilikuwa na nyufa na kuvuja nyakati za mvua, na kununua samani  na vifaa vya ofisi kama mashine za nukushi na za kurudufu ambazo zilikuwa hazipo,
8. Kununua magari mapya ya ofisi ya ubalozi wetu nchini China kwa kuwa  magari matatu yaliyokuwepoyalikuwa yameshapitiliza muda wa miaka 10 ambao kwa mujibu wa sheria za China hayapaswi kutumika tena,
9. Kupeleka mwambata wa kiuchumi (economic attaché)  nchini China ili kufuatilia fursa mbalimbali za kiuchumi katika kutekeleza diplomasia ya uchumi kutokana na mahusiano makubwa ya kibiashara  kati ya nchi yetu  na China
10. Kuwawekea zuio wahusika wa kashfa ya rada kuwa viongozi wa shughuli za kiserekali ili walau kuonesha uwajibikaji wa kimaadili (moral accountability) baada ya kushindwa kuwawajibisha kisheria, ili kuondoa dhana iliyojengeka miongoni mwa jamii kwamba dola imetekwa na mafisadi.
11. Kuchunguza na kuwachukulia hatua watanzania (wafanyabiashara na wanasiasa) waliotorosha kiasi kikubwa cha fedha za nchi yetu (zaidi ya shilingi bilioni 315) na kuzificha katika mabenki ya uswisi
12. Kutoa mchanganuo wa jinsi fedha za rushwa ya rada (chenji ya rada) zilivyotumika
13. Kueleza bayana faida za kiuchumi tunazopata kama taifa kwa kushirikiana na jumuiya mbalimbali za kimataifa ili kuthibitisha kwamba mashirikiano hayo hayatumiki kupora rasilimali za nchi yetu kwa hila ya “uwekezaji”
Mheshimiwa Spika, kabla sijajielekeza kwenye mambo mahsusi kwa kipindi hiki cha bajeti ya 2013/2014, napenda kuchukua nafasi hii kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA, kuitaka Serikali kutoa majibu mbele ya Bunge hili tukufu, kwamba imetekeleza kwa kiwango gani masuala yaliyoorodheshwa hapo juu, tuliyoitaka iyatekeleze (moja baada ya jingine) kwa mwaka wa fedha unaomalizika wa 2012/2013?
1.1 Upotevu wa Fedha za Safari za Rais, Shilingi bilioni 3.5
Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu ya mwaka 2012/2013 nilihoji kuhusu serikali Kuchunguza na kuchukua hatua kwa waliohusika na upotevu wa shilingi bilioni 3.5 kwa ajili ya safari “hewa” za Rais nje ya nchi, ili waweze kubainika na kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria zetu.
Mheshimiwa Spika, fedha hizi ni nyingi sana na hasa  ikikukumbukwa kuwa mwaka jana 2012 wapo mawaziri ambao walichukuliwa hatua na Bunge hili kutokana na upotevu ama madhaifu yaliyofanyika kwenye wizara zao, wapo ambao walihukumiwa kutokana na kupotea kwa Twiga kwenye wizara zao, wapo waliohukumiwa kutokana na udhaifu katika kusimamia wizara zao na taasisi zilizoko chini yao. 
Kambi rasmi ya upinzani, inahoji iweje leo waziri aliyeshindwa kusimamia wizara yake na kusababisha upotevu wa fedha hizi mpaka leo bado yupo, wakati wapo mawaziri wengine walioshughulikiwa kutokana na udhaifu walioonyesha kwenye kusimamia wizara zao, au ndio kusema kuwa Serikali hii ya CCM inafanya upendeleo na kuonea baadhi ya mawaziri na kuwaacha wengine? “This clearly indicates the “double standard” nature of this Government in the performance of its functions”
1.2. Kuanzishwa kwa Ubalozi Mdogo Guangzhou -China
Mheshimiwa Spika, mwaka jana Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilipendekeza kuwa serikali ianzishe ubalozi mdogo katika Jiji la Guangzhou kwa ajili ya kurahisisha biashara kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na wale wa China. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inatambua kuwa serikali imelifanyia kazi wazo hili na imeamua kuanzisha ubalozi mdogo katika mji huo ,ila tunataka kujua ni lini ubalozi huu utazinduliwa rasmi, kupata watendaji na vitendea kazi ili uweze kuanza kufanya kazi .
2.0 DIPLOMASIA YA UCHUMI
Mheshimiwa Spika, moja ya matarajio ya ushirikiano wa kimataifa ni kuweza kutafuta, na kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazoweza kupatikana katika mashirikiano hayo ili kama Taifa, tuweze kujikwamua kiuchumi na kujitegemea.
Mheshimiwa Spika, kinyume na matarajio hayo mazuri, sasa nchi yetu imegeuzwa kuwa kitega uchumi cha nchi zilizoendelea kwa kisingizio cha “ushirikiano wa kimataifa” chini ya mwavuli wa “uwekezaji”. Matokeo ya ushirikiano huu wa kinyonyaji (exploitative relationship) ni kwamba kiwango cha umasikini katika nchi yetu kimeongezeka na hivyo kuifanya nchi yetu kuwa tegemezi zaidi kuliko ilivyokuwa hapo kabla.
Mheshimiwa Spika, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikerwa na unyonyaji na unyanyasaji uliokuwa ukifanywa na wakoloni, hali iliyompelekea kusema maneno yafuatayo:
“Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, tumepuuzwa kiasi cha kutosha. Unyonge wetu ndiyo uliotufanya tuonewe, tunyonywe na kupuuzwa. Sasa tunataka kufanya mapinduzi”
Mheshimiwa Spika, baada uhuru, Mwalimu akaanzisha siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Ujamaa ulilenga kujenga umoja wa kitaifa  na umoja wa bara la Afrika dhidi ya unyonyaji wa kibeberu, wakati kujitegemea  kulimaanisha kujenga uchumi endelevu ili kulijengea taifa heshima na nguvu ya maamuzi mbele ya mataifa mengine, na kuliepusha taifa na fedheha ya kuombaomba.
Mheshimiwa Spika,  Kambi Rasmi ya Upinzani imesikitishwa sana na kitendo cha Serikali kulidanganya taifa, kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010 kwamba: “Katika kipindi cha miaka mitano 2010 -2015, Serikali ya Chama cha Mapinduzi itatekeleza Sera ya Diplomasia ya Uchumi” wakati Ibara ya 98 (i) ya Ilani hiyohiyo ya CCM inasema kwamba Serikali ya CCM itaendelea kushinikiza nchi tajiri kutekeleza ahadi yao ya kutenga asilimia 0.7 ya pato la taifa la nchi zao kwa ajili ya misaada kwa nchi masikini”.
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba ahadi hii ya asilimia 0.7 ya pato la taifa la nchi tajiri ambayo Serikali ya CCM inakodolea macho ni fedha za walipa kodi wa nchi hizo kama ambavyo wananchi wetu wanavyolipa kodi. Aidha ni aibu kwa Serikali hii ya CCM kuchukua ahadi za wahisani na kuziweka kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM kama ahadi kwa wananchi ili kubembelezea kura.
Mheshimiwa Spika, kutokana na uvivu wa kufikiri na kubuni mbinu za kuikwamua nchi hii na umasikini, Serikali hii ya CCM sasa hivi imeachana kabisa na sera ya kujitegemea, ambayo Mwalimu kupitia Azimio la Arusha alisema kwamba “ … Hakika ni ujinga na upumbavu zaidi kwetu sisi, kufikiri kwamba tutaondokana na umasikini wetu kwa misaada ya fedha kutoka nje kuliko rasilimali zetu wenyewe”
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza bunge hili, kama inatekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa kutegemea ahadi ya misaada ya fedha kutoka kwa wahisani na kama hilo ndio suluhisho la matatizo yanayokumba uchumi wetu kama taifa kwamba tutaweza kuendelea kwa kutegemea hisani na fadhila za wafadhili huku tukishindwa kuzitumia rasilimali zetu kwa ajili ya kujikomboa kiuchumi.
Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani imejiridhisha kwamba kauli mbiu ya ‘Diplomasia ya  Uchumi’ imeendelea kubakia kama ilivyo kauli mbiu ya ‘Kilimo Kwanza’ ambayo imebakia kutamkwa na viongozi bila kuwa na mkakati wa utekelezaji wala vigezo vya kupima kiwango cha utekelezaji wake.
3.0.  VYAMA VYA SIASA NA MISAADA KUTOKA NJE YA NCHI.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa ‘United Nations University’(UNU-WIDER) ya mwezi Aprili 2012 iliyoandaliwa na Aili Mari Tripp ilionyesha kuwa misaada ya wahisani kutoka nje katika mabadiliko ya kisiasa Tanzania ‘Donor Assistance and Political Reform in Tanzania’, inaonyesha kuwa Tanzania imepokea misaada kutoka nje yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 26.85 toka mwaka 1990-2010.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti hiyo ni kuwa Tanzania ni nchi inayoongoza kusini mwa jangwa la Sahara kwa kupokea misaada mingi kutoka nje ya nchi na hasa kutoka mataifa ya Ulaya na taasisi za nchi za Uingereza, Marekani, Ujerumani, Uholanzi, Norway, Canada, Sweden, na taasisi kama Benki ya Dunia, IMF ,UNDP ,UNICEF na mengineyo. 
Pamoja na misaada yote hiyo, bado tumeendelea kuwa nchi maskini sana duniani pamoja na kuwa na rasilimali lukuki ambazo tumepewa na Mungu ila tunashindwa kuzitumia kwa manufaa ya watanzania na badala yake tumeendelea kudanganywa na vimisaada vidogo vidogo na kubadilishana na rasilimali zetu kama madini, misitu ,wanyama nk kwa ajili ya misaada hiyo.
Mheshimiwa Spika, pamoja na misaada hiyo kwa serikali hii ya CCM bado vyama vya siasa vimekuwa na mahusiano na baadhi ya vyama vingine vya siasa katika mataifa ya magharibi na vimekuwa vikipokea misaada ya aina mbalimbali kama fedha , nyenzo na mengineyo kadiri ya makubaliano na mirengo ya kiitikadi ya vyama husika.Pamoja na ukweli huo bado vipo vyama vya siasa vinavyopotosha umma kuhusiana na misaada vinayopokea kutoka nje ya nchi na vyama hivi vimekuwa mstari wa mbele kueneza propaganda za uongo kuwa vyenyewe havipokei misaada kutoka nchi za magharibi.
Mheshimiwa Spika, CCM wao ‘wanajiita’ kuwa wapo mrengo wa kijamaa/kikomunisti na wamekuwa wakipokea misaada mingi sana ya fedha na nyenzo kutoka Umoja wa Vyama vya Kikomunisti Ulimwenguni ‘Socialist International’ kutoka katika nchi kama za Ujerumani kupitia SDP ,Uingereza kupitia chama cha Labour,China kupitia chama cha Kikomunist ,Marekani kupitia chama cha Democrats. Pamoja na misaada ya kifedha na kiufundi ambayo CCM imekuwa ikipata kutoka nje wamekuwa hawatangazi hadharani hata mara moja kuhusiana na kiasi ambacho wamekuwa wakipokea na hivyo kila kitu kwao imekuwa ni siri kuu ya viongozi wao.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa chama cha CUF, kutokana na itikadi zake za mrengo wa Kiliberali ambazo miongoni mwa misingi yake mikuu ni pamoja na “kupigania haki za ndoa ya jinsia moja, usagaji na ushoga”. Hii ni kwa mujibu wa tangazo lao kwenye mtandao wao wa umoja wa maliberali ulimwenguni, likiungwa mkono na Waziri wa Haki na Usawa wa Uingereza, Lynn Featherstone kutoka chama cha Liberal Democrats wakati chama hicho([url]www.liberal-international.org[/url])  kilipokuwa kinapitisha azimio la kuruhusu ndoa za jinsia moja kama haki ya mtu mmoja mmoja, wanashirikiana na vyama kama vile LPC ya Canada, Det Radikale Venstre cha Norway, FDP cha Ujerumani, Israel Liberal Group cha Israel,PDS cha Senegal na Liberal Democrats cha Uingereza.
Kutokana na umoja huo, CUF wamekuwa wakipata msaada wa kifedha na nyenzo nyingine mbalimbali kutoka kwa vyama hivyo vya mrengo wa Kiliberali na msaada wa mwisho ni hivi majuzi mwezi Machi 2013 waliposaini makubaliano na chama cha Kiliberali kutoka Norway.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa CHADEMA, wapo kwenye Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Ulimwenguni (International Democratic Union - IDU). Huu ni umoja wa vyama ambavyo vipo kwenye mrengo wa kati na ambavyo msingi wake mkuu  ni pamoja na kuwa na familia, kama taasisi muhimu katika jamii, ikimaanisha kwamba: “tunapinga vitendo vyote vya ushoga na usagaji”. Tunatetea demokrasia, haki za binadamu na kupambana na ufisadi katika serikali. Vyama wanachama wa umoja huu ni pamoja na Conservative Party cha UK, CPP cha Norway, Republican cha Marekani na vingine vinavyofuata   mrengo huo.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya upinzani Bungeni, inavitaka vyama vyote ambavyo vimekuwa na mahusiano na vyama vya nje viweke wazi mikataba yao na malengo ya mahusiano hayo ikiwa ni pamoja na misaada ambayo vimekuwa vikipokea kutoka kwenye nchi hizo .
4.0 MPANGO WA KUJITATHIMINI KIUTAWALA BORA (APRM)
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa mnamo mwezi Januari, 2013 ulifanyika mkutano wa 20 wa wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa ,Ethiopia na ni katika mkutano huo Mhe. Rais Kikwete aliwasilisha taarifa ya nchi yetu kuhusu kujitathimini katika utawala bora kwenye mpango wa nchi zinazojitathimini katika utawala bora (APRM).
Mheshimiwa Spika, baada ya taarifa hiyo (randama uk.15) nchi yetu ilitakiwa kutafutia ufumbuzi changamoto zifuatazo;
i. Migogoro baina ya wakulima na wafugaji
ii. Imani za kishirikiana (uchawi)
iii. Kuhakikisha kuwa manufaa ya kukua kwa uchumi yanawafikia wananchi
iv. Kutoa elimu kwa umma kuhusu mipango na sera za serikali
Mheshimiwa Spika, changamoto hizi ambazo nyingine zinatia aibu taifa letu mbele ya mataifa mengine kama vile sisi kuonekana ni wachawi na hivyo kutakiwa kuchukua hatua dhidi ya uchawi !ni fedheha na aibu kubwa kwa taifa letu .
Aidha , Kambi rasmi ya upinzani Bungeni inataka kujua serikali na wizara imechukua hatua gani mpaka sasa katika kukabiliana na changamoto hizi na hasa tatizo la wakulima na wafugaji na kuhakikisha kuwa manufaa ya kukua kwa uchumi wetu yanawanufaisha wananchi na sio kuwanufaisha baadhi ya viongozi na mafisadi wachache.
5.0 MLIPUKO WA BOMU ARUSHA NA BARAZA LA USALAMA LA UMOJA WA MATAIFA.
Mheshimiwa Spika, mwaka huu tarehe 05 Mei,   Kanisa Katoliki Parokia ya Olasiti  huko Arusha lililipuliwa  kwa bomu.  Tukio hili lilitokea wakati akiwepo balozi wa Vatican Nchini na ambaye ndio alikuwa mgeni wa heshima kwenye tukio la kuzindua Parokia hiyo.
Mheshimiwa Spika, mara baada ya tukio hilo, Balozi wa Vatican nchini aliwasilisha taarifa hiyo kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuonyesha kuwa Tanzania sio nchi salama sana kutembelewa na wageni na kama wakitembelea basi wanapaswa kuchukua tahadhari kubwa kwa kipindi chote watakapokuwa hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kujua nini kauli ya serikali kuhusiana na tukio hili na hasa kuhusiana na taarifa za hali ya usalama wa nchi yetu na wageni zilizowasilishwa kwenye Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa .
6.0 SAFARI ZA VIONGOZI NJE NA MISAFARA MIKUBWA
Mheshimiwa Spika, tangu mwaka 2011/2012 Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikihoji suala la misafara ya Viongozi wa kitaifa kuwa mikubwa kutokana na kuambatana na watu wengi ambao wengine wanakuwa hawana hata majukumu ya msingi ya kufanya wakati wa ziara hizo huku wakiliongezea taifa gharama kubwa ya kuwasafirisha na na kulipia malazi yao na starehe zao.
Aidha , tumekuwa tukipendekeza na kushauri kuwa sasa ni wakati muafaka kwa Rais wa nchi kuamua kutuma wasaidizi wake kwenye baadhi ya ziara za nje kama wanavyofanya viongozi wengine wa nchi jirani kama Rais Kagame wa Rwanda na hata Mwai Kibaki,  Rais mstaafu wa Kenya alivyokuwa anafanya akiwa Rais, kwani kwa kufanya hivyo atapunguza msururu wa maafisa na viongozi mbalimbali wa kuambatana naye. Tunashauri tena kuwa rais awe anatuma wasaidizi wake kwenye ziara za kawaida na yeye awe na jukumu la kushiriki kwenye ziara rasmi za kiserikali ‘State Visits’ na mikutano maalum ya Kimataifa kama UN na AU.
Hivyo basi Kambi rasmi ya Upinzani inashauri mambo yafuatayo yafanyike ili kupunguza gharama hizi kubwa za kuwasafirisha viongozi na misafara isiyokuwa na tija kama ifuatavyo;
i. Serikali itengeneze kanuni za kuthibiti idadi ya maafisa na watu ambao watakuwa wakiambatana na Rais kwenye ziara za nje (idadi ya wajumbe kwenye misafara iwe wazi na ijulikane)
ii. Pawepo na kanuni za kuainisha kuwa ni nani watapaswa kupanda ndege daraja la kwanza na wale wenye haki ya kulala kwenye hoteli za daraja la kwanza wajulikane.
6.1. Idara ya Protocol na Mabilioni ya Fedha za Safari za Nje.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/2012 fungu 221100 ‘travel out of country’zilitumika shilingi 36,121,942,870.00 kwa ajili ya safari za nje ya nchi kwa viongozi wakuu. Katika mwaka wa fedha uliopita wa 2012/2013 kifungu 1010 ambacho ni kwa ajili ya protocol walitengewa shilingi 8,372,581,824 na fedha ambazo zilikuwa zimepokelewa na wizara mpaka mwezi Februari 2013 zilikuwa jumla ya shilingi 26,081,860,727.16! (randama uk.4)jedwali la 2 na zilitumika kwa ajili ya kugharamia safari za viongozi nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013 Bunge lilikuwa limetenga na kuidhinisha kiasi cha shilingi 8,372,581,824 kwa ajili ya kifungu hiki cha Protocol ‘travel out of Country’kwa mujibu wa kitabu cha matumizi ya kawaida juzuu ya pili (volume II). Jambo  la kushangaza ni kwamba, wizara iliieleza kamati na Bunge hili kuwa walishatumia zaidi ya bilioni 26.081 kutokana na fedha walizokuwa wamejitengea wenyewe wizara ambazo hazikuidhinishwa na Bunge kiasi cha bilioni 29.404
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA, inataka maelezo ya kina kuhusiana na mamlaka ya wizara hii kwenda kutenga na kutumia fedha nyingi kuliko zilizokuwa zimeidhinishwa na Bunge hili na zilikuwa fedha kwa ajili ya safari za kwenda nje ya nchi, ni nani aliipa wizara mamlaka hiyo na kiburi hicho kiasi cha kupuuza maamuzi ya Bunge hili tukufu.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha 2013/2014 kitengo hiki cha Protocol kimetengewa jumla ya shilingi 15,155,377,400.00 kwa ajili ya matumizi mengineyo ,ambazo katika mchanganuo wake kwenye kifungu 1010 kifungu kidogo cha 221100 ‘travel out of Country’ zimetengwa shilingi 9,381,328,850.00 kwa ajili ya kugharamia safari za kikazi za viongozi wa Kitaifa nje ya nchi.
Aidha, katika kifungu kidogo cha 220700 ‘rental expenses’ zimeombwa jumla ya shilingi 2,925,445,000.00 kwa ajili ya kukodisha ndege ,magari na kumbi za mikutano kwa ajili ya viongozi wa kitaifa.
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, haikubaliani na kamwe haitakubaliana na ufujaji huu wa fedha za walipakodi maskini wa Tanzania . Tunamtaka waziri atoe maelezo ya kina kwa watanzania ni kwanini nchi maskini kama yetu tutumie fedha nyingi kiasi hicho kwa ajili ya safari za viongozi nje ya nchi? Aidha , hatukubaliani na kitendo cha kutenga fedha kwa ajili ya kukodi ndege  wakati  Rais ana ndege yake ambayo ilinunuliwa na mabilioni ya fedha za watanzania. 
Ikumbukwe kwamba ndege hii ya Rais ilinunuliwa kwa mbwembwe nyingi kiasi kwamba Waziri wa Fedha wa wakati huo Ndugu Bazili Mramba alisema watanzania wafunge mkanda, hata kama watakula majani, lazima ndege ya Rais inunuliwe. Watanzania hawa wamekula majani sasa kiasi cha kutosha, bado tena Serikali inaendelea kuwanyonya ili ipate pesa za kukodisha ndege wakati Rais ana ndege? Hivi Serikali sasa inataka watanzania wale mawe ndio ijue kwamba watu wamefunga mkanda kiasi cha kutosha?
6.2 Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje
Mheshimiwa Spika, mwaka 2012 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama, ilifanya ziara kwenye balozi takribani zote na iliona matatizo yanayozikumba balozi zetu huko na ilikuwa matumaini yetu kuwa baada, ya ziara ile ya kamati ingehakikisha kuwa fedha zinaongezwa kwenye wizara hii na hasa kwenye fungu la maendeleo ili tuweze kuboresha mazingira ya balozi zetu. Kinyume na matumaini hayo, ni kwamba hakuna jitihada zilizofanyika kuongoeza bajeti ya wizara hasa katika fedha za maeendeleo.
Mheshimimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka kamati ya Bunge ya Ulinzi na usalama, kuishinikiza Serikali ili kuhakikisha kuwa katika mwaka huu wa fedha wizara hii inaongezewa fedha kwa ajili ya kuboresha mazingira ya balozi zetu , na hiyo ndio njia pekee ya kuonyesha kuwa kamati haikuenda kufanya utalii bali ilienda kuona matatizo ya balozi zetu na kuchukua hatua.
7.0 UFISADI KATIKA UNUNUZI WA JENGO LA OFISI NA MAKAZI KATIKA UBALOZI WA TANZANIA JIJINI PARIS – UFARANSA.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha kwa mujibu wa randama ya wizara ni kuwa mwaka huu wa fedha kiasi cha shilingi bilioni 28 (28,000,000,000.00) zimepangwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo na kati ya hizo kiasi cha shilingi bilioni 24 na milioni 188 (24,188,000,000.00) ni kwa ajili ya ununuzi wa jengo la ofisi na makazi ya balozi jijini Paris ,Ufaransa (randama uk 25) na kiasi cha shilingi bilioni 3 na milioni 812 (3,812,000,000.00) ni kwa ajili ya gharama za ukarabati wa majengo ya ofisi na makazi yaliyopo Ubalozi wa Tanzania Maputo,Msumbiji. 
Mheshimiwa Spika, ukisoma randama ya wizara (uk.120) katika kasma 6391 ,kifungu kidogo 411100 kiasi cha fedha kilichoombwa ni shilingi bilioni 23 na milioni 900 (23,900,000,000) kwa ajili ya ununuzi wa jengo la ofisi na makazi ya Balozi jijini Paris, Ufaransa na shilingi bilioni 3 namilioni 700 (3,700,000,000.00) kinaombwa kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya ofisi na makazi yaliyopo ubalozi wa Tanzania Maputo,Msumbiji.
Hata hivyo, katika mwaka huu wa fedha 2013/2014 kwenye kasma 6391 katika fungu la Maendeleo (randama uk.120) wizara inaomba kutengewa kiasi cha shilingi milioni 400 (400,000,000.00) (kifungu 221100 ) fedha ambazo hazipo kwenye kitabu cha matumizi ya kawaida juzuu ya pili (volume II) kwa ajili ya posho ya kujikimu na gharama za usafiri kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Wizara, miradi yenyewe ni miwili mmoja wa kununua nyumba Ufaransa na kukarabati jengo Msumbiji.
Mheshimiwa Spika, mkanganyiko huu wa kimahesabu unatia mashaka makubwa sana kuhusiana na dhamira ya serikali na wizara hii hasa fedha zinapotengwa bila kufuata utaratibu wa kibajeti na bila kuingizwa kwenye vitabu vya fedha na mafungu husika.
Kambi rasmi ya Upinzani, inajiuliza tunapitisha mafungu yapi? Kwani kwenye randama fedha zinatofautiana kwenye fungu moja la maendeleo baina ya (ukurasa 25 na 120) , vilevile kwenye kitabu cha matumizi ya kawaida hali ni tofauti kwenye fungu la travel out of the Country kwani sasa wizara imejiongezea shilingi milioni mia nne kwa ajili ya kufuatilia miradi miwili ambayo ni kununua jengo Paris na kukarabati Jengo la ubalozi - Maputo,Msumbiji.
Mheshimiwa Spika, utata wa fedha unaendelea kuonekana kwenye randama ya wizara katika kiambatanisho Na.1 ‘utekelezaji wa ushauri na mapendekezo ya kamati ya kudumu ya Bunge ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa’ katika ushauri/mapendekezo Na.5 kamati iliitaka ‘Wizara itoe mchanganuo wa matumizi ya fedha za bajeti ya maendeleo zilizopokelewa kutoka hazina katika mwaka wa fedha 2012/13’
Maelezo ya wizara yalikuwa kama ifuatavyo; nanukuu randama ya wizara “katika mwaka wa fedha 2012/2013 ,hadi kufikia mwezi Machi ,2013 wizara imepokea kutoka Hazina kiasi cha shilingi 13,261,281,600.00 ambapo kati ya fedha hizo kiasi cha shilingi 9,660,000,000.00 zimetumika kwa ajili ya kulipia malipo ya awali ya ununuzi wa Jengo la Ofisi na Makazi ya Balozi Paris,Ufaransa;shilingi 995,930,000.00 zimetumika kwa ajili ya ukarabati wa jengo la serikali lililopo Maputo,Msumbiji ;shilingi 626,899,155.00 zimetumika kwa ajili ya ukomboaji wa vifaa vya ujenzi bandarini vilivyotumika katika ujenzi wa kituo cha mikutano cha kimataifa cha Julius Nyerere na safari ya kikazi ya wataalam katika balozi za Maputo,Pretoria na Lusaka kwa ajili ya kazi ya upembuzi yakinifu wa miradi ya maendeleo iliyopo katika Balozi hizo; na shilingi 1,978,452,485.20 bado hazijatumika na zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya kulipia gharama za ukarabati wa jengo la Serikali lililopo Maputo’
Mheshimiwa Spika, baada ya kufuatilia na kufanya tathimini ya kina kuhusiana na majibu hayo ya wizara kuhusu fedha za maendeleo kwa ajili ya ukarabati wa Jengo la Maputo na kununua Jengo la Ofisi na Makazi ya Balozi Ufaransa na kukuta kuwa ni fedha nyingi sana kuliko uhalisia wenyewe , kwa mfano waziri anataka Bunge na taifa tuamini kuwa kufanya ukarabati wa jengo moja la ofisi Maputo Msumbiji tunahitaji kutumia kiasi cha shilingi 4,695,930,000.00 kwa kutumia fedha inayoombwa mwaka huu wa fedha na zile ambazo tayari zilishalipwa katika mwaka wa fedha wa 2012/2013. 
Aidha wakati wizara inawasilisha majibu yake kwenye kamati ya kudumu ya Bunge walisema kuwa (swali 12 uk.5) ‘kiasi cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya Serikali yaliyopo Maputo ni shilingi 3,812,000,000.00……kiasi hicho cha fedha kinatosheleza kukamilisha kazi ya ukarabati wa majengo hayo ya Serikali yaliyopo Maputo, Msumbiji’
Aidha, kununua jengo moja la ofisi na makazi katika Jiji la Paris Ufaransa tunahitaji kutumia kiasi cha shilingi bilioni 33 na milioni 560 33,560,000,000.00.
Mheshimiwa Spika, kwa majibu haya ya wizara ni kuwa tayari wizara imeshafanya malipo ya shilingi bilioni 9.66 kama malipo ya awali kwa ajili ya ununuzi wa jengo la ofisi na makazi huko Paris Ufaransa , na kuwa tayari tumeshafanya malipo ya awali kiasi cha shilingi milioni 995.930 kwa ajili ya ukarabati wa jengo la ubalozi huko Maputo,Msumbiji.
Mheshimiwa Spika, hakika kiasi hiki ni kikubwa kupitiliza na hata utafiti na tathimini ambayo ilifanywa na Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni ilionyesha kuwa kununua jengo la ofisi katika jiji la Paris kwenye mji wa bei ghali kama Co’te d’Azur (most expensive area in Paris) huwezi kutumia fedha nyingi kiasi hicho kwa ajili ya manunuzi ya jengo la ofisi na makazi.
Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tunakumbuka sakata la ununuzi wa jengo la ubalozi lililomkumba balozi Prof.Mahalu huko Roma - Italia na yaliyofuatia mpaka kesi na fedha zetu tulizoambiwa kuwa zimepotea hazikuweza kurejeshwa baada ya Prof.Mahalu kushinda kesi hiyo mahakamani.
Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kupata majibu kuhusiana na mambo yafuatayo;
i. Ni eneo gani ambalo tumepata jengo la kununua kwa ajili ya ubalozi na makazi ya balozi huko Paris, Ufaransa, na ni nyumba ya aina gani .
ii. Je, Serikali inaweza kuonyesha mkataba wa manunuzi wa nyumba hizo (Paris) kwa Bunge na tutalipa kiasi gani kununua jengo hilo?
iii. Ni nani au wakala gani wa serikali aliyefanya tathimini ya hayo majengo na kuamua kuwa tulipe kiasi hicho cha fedha?
iv. Ni kampuni gani iliyohusika katika kufanya makubaliano ya mauziano ya nyumba hizo na tunawalipa kamisheni ya shilingi ngapi?
v. Nani, aliidhinisha kutumika kwa kiasi kikubwa hivyo kwa ajili ya kununua jengo la Ubalozi na makazi huko Paris, je Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, ilishirikishwa katika manunuzi haya?
vi. Ukarabati unaofanywa kwenye jengo la Maputo Msumbiji ni wa aina gani, au tunajenga upya nyumba hizo?
vii. Ni kampuni gani ya ujenzi inayofanya ukarabati wa jengo letu huko Msumbiji na mkataba wa ukarabati huo uko wapi, tungetaka uwekwe hadharani.
Aidha , kambi rasmi ya Upinzani Bungeni , inatoa hoja ya kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya uchunguzi maalum (Special Audit) kuhusiana na ununuzi wa majengo haya na ukarabati unaofanyika kwenye jengo letu huko Maputo, Msumbiji, na kuona kama thamani halisi ya fedha imezingatiwa , na kama sheria ya manunuzi ya umma imefuatwa kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, Vile vile, tungetaka sehemu ya fedha hizi zitumike kwa ajili ya kukarabati jengo letu la zamani la ubalozi lililopo Washngton ambalo kwa sasa halitumiki baada ya kutekelezwa kwani likikarabatiwa litaweza kuliongezea taifa mapato kutokana na matumizi ya kibiashara ya jengo hilo.
8.0 MPANGO WA WIZARA WA KUTOA VISA KWENYE BALOZI TU
Mheshimiwa Spika, mpango wa Wizara kutoa visa kwenye balozi tu haukubaliki. Kwa Mujibu wa majibu ya wizara kwenye kamati ya kudumu ya Bunge ya Mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa ilionyesha kuwa ili wizara iweze kukusanya fedha za kutosha kwenye balozi zetu ni kwa kurudisha utaratibu wa utoaji wa viza kufanywa na Balozi zetu tofauti na utaratibu unaotumika hivi sasa ambapo wageni huweza kupatiwa viza pindi wanapowasili katika vituo vya kuingilia nchini (viza on arrival).
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, haikubaliani na wazo hili la wizara kwani badala ya kuongeza wageni kuja nchini litapunguza sana hasa ikizingatiwa kuwa ni nchi chache sana ambako tuna ofisi za Balozi na pia kuna nchi nyingine kama Marekani ambapo, kama mgeni yupo Carlifonia na anataka kusafiri kuja Tanzania atalazimika kwanza kusafiri kwenda Washington ambako ndiko kwenye ubalozi atafute visa na ndipo aweze kuja nchini.  Utaratibu huu utaongeza gharama kubwa za usafiri kwa wageni na watalii na hivyo kulipotezea taifa mapato yataokanayo na utalii kwani wageni watapungua.
Aidha, tunaikumbusha wizara kuhusiana na Itifaki ya kuwa na“Single Tourist Destination Protocol” na uwepo wa hati ya kusafiria na visa moja ya utalii “Single Tourist Visas” kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo kama sisi tukifanya huo uamuzi basi wenzetu Kenya wataendelea kupata wageni wengi zaidi kutokana na visa ya pamoja na wageni wataingia Tanzania kutokana na visa za Kenya chini ya Itifaki hiyo.
8.1 Mkutano wa Mabalozi wa Mwaka 2013/2014
Mheshimiwa Spika, wizara inahitaji kiasi cha shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kufanikisha mkutano wa mabalozi kwa mwaka wa fedha 2013/2014 , na wizara iliwasilisha maombi ya fedha hizo Hazina kama sehemu ya kipaumbele lakini hazikuweza kupatikana .
Kambi rasmi ya upinzani Bungeni, inaitaka serikali kuiondoa aibu hii na kutenga hizo fedha kwa ajili ya kufanikisha mkutano huo na tunapendekeza kuwa katika fungu la protocol safari za nje ndipo fedha hizo zipunguzwe na kutumika kwa ajili ya mkutano wa mabalozi wetu ili waweze kupeana ushauri na uzoefu,ili kuboresha ufanisi wa majukumu yao.
8.2 Utaratibu wa Kupeleka Fedha kwenye Balozi
Mheshimiwa Spika, kutokana na utaratibu wa kupeleka fedha kwenye balozi zetu kuwa na mlolongo mrefu wa kwanza kutoka Hazina na kupelekwa Wizarani, ndipo wizara isambaze fedha hizo kwenye balozi zetu mbalimbali umesababisha fedha kuchelewa kufikishwa kwa wakati kwenye balozi zetu na hivyo kusababisha usumbufu mkubwa na ucheleweshaji wa kazi kwenye balozi zetu.
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka serikali kubadilisha utaratibu huu na hazina iwe inapeleka fedha hizo moja kwa moja kwenye balozi husika badala ya kuzipitisha wizarani kama ilivyofanya kwenye fedha za Halimashauri mbalimbali nchini ili kupunguza usumbufu huo.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya kambi rasmi ya Upinzani naomba kuwasilisha.
________________________________
Ezekiah Dibogo Wenje
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
NA
WAZIRI KIVULI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA

Ufaulu Kidato cha Nne waongezeka

Waziri wa Elimu na Ufundi Stadi, Dk Shukuru Kawambwa aliyetangaza matokeo hayo leo
SERIKALI imetangaza matokeo mapya ya mtihani wa kidato cha nne ya mwaka 2012 na kuwaokoa watahiniwa 30,057 kati ya 240,903, ambao katika matokeo yaliyotangazwa Februari 18, mwaka huu, walipata daraja sifuri.

Matokeo hayo mapya yalitangazwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.

Dk. Kawambwa alisema kiwango cha ufaulu kimeongezeka kutoka asilimia tisa hadi 43.

Waziri Kawambwa alitangaza matokeo hayo mapya, ikiwa ni wiki chache tangu serikali iyafute matokeo ya mtihani huo yaliyoyatangazwa na waziri huo, Februari 18, mwaka huu na kuliagiza Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kuyaandaa upya.

Kwa mujibu wa matokeo hayo mapya, jumla ya watahiniwa waliopata daraja sifuri ni watahiniwa 210,846, wavulana wakiwa 104,259 na wasichana ni 106,587.

Mbali na kuwaokoa watahiniwa hao, matokeo hayo mapya, yanaonyesha kuwa idadi ya watahiniwa waliopata daraja la kwanza wameongezeka kutoka watahiniwa 1,641 waliotangazwa Februari 18, hadi watahiniwa 3,242 waliotangazwa jana.

Kati ya watahiniwa hao, ambao jumla yao ni 3,242, wavulana ni 2,179 na wasichana 1,063.

Pia idadi ya watahiniwa waliopata daraja la pili imeongezeka kutoka watahiniwa 6,453 waliotangazwa Februari 18, mwaka huu, hadi watahiniwa 10,355 waliotangazwa jana.

Kati ya watahiniwa hao, ambao jumla yao ni 10,355, wavulana ni 7,267 na wasichana 3,088.

Vilevile, idadi ya watahiniwa waliopata daraja la tatu imeongezeka kutoka watahiniwa 15,426 waliotangazwa Februari 18, mwaka huu, hadi watahiniwa 21,752 waliotangazwa jana.

Kati ya watahiniwa hao, ambao jumla yao ni 21,752, wavulana ni 14,979 na wasichana ni 6,773.

Kadhalika, idadi ya watahiniwa waliopata daraja la nne imeongezeka kutoka watahiniwa 103,327 waliotangazwa Februari 18, mwaka huu, hadi watahiniwa 124,260 waliotangazwa jana.
Kati ya watahiniwa hao, ambao jumla yao ni 124,260, wavulana ni 74,433 na wasichana ni 49,827.

Alisema kuanzia sasa matokeo ya kidato cha nne hadi cha sita yatachakatwa kwa kutumia mfumo wa viwango vya aina moja ambao hutumika kuchakata matokeo kwa masomo yote bila kujali kiwango cha kufaulu kwa somo husika.

Serikali iliyabatilisha matokeo hayo baada ya Necta kutumia mfumo mpya wa viwango vya ufaulu ambao ulisababisha wanafunzi takribani asilimia 60 kufeli.
Matokeo hayo yalilalamikiwa sana na makundi mbalimbali ya jamii.

Aidha wanafunzi kadhaa walijinyonga kutokana na kupata matokeo mabaya ambayo hawakuyatarajia na kuilazimisha serikali kuunda tume ya kuchunguza sababu za kufeli.
Hata hivyo, kabla ya tume hiyo iliyoongozwa na Profesa Sifuni Mchome, kuwasilisha ripoti, Baraza la Mawaziri lilikutana na kuiamuru Necta kuyafuta na kuyaandaa upya kwa kutumia mfumo uliotumika mwaka 2011.

Yanga yamwagiwa manoti

Add caption

KAMPUNI ya bia Tanzania (TBL), jana iliwakabidhi mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, Yanga ya jijini Dar es Salaam hundi ya Sh. milioni 25 ikiwa ni motisha ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo wa msimu uliomalizika wa mwaka 2012/ 2013.
Akizungumza jana jijini, meneja wa bia ya Kilimanjaro, George Kavishe, alisema kwamba wanaipongeza Yanga kwa kutwaa ubingwa huo na wanaamini udhamini wao kwa klabu hiyo ndiyo umesaidia kupatikana kwa matunda ya ushindi.
Simba ambao pia wanadhaminiwa na Kilimanjaro wamekosa kitita cha Sh. milioni 15 msimu huu kutoka TBL kutokana na kumaliza katika nafasi ya tatu kama ilivyokuwa kwa Yanga mwaka jana.
Kavishe alisema kuwa anafahamu ubingwa huo wa Yanga umetokana na klabu kuwa na mikakati imara ya ushindi ambayo waliipanga kuanzia mwanzo wa msimu.
Alisema kuwa kiasi hicho cha fedha TBL walichokiweka baada ya kuwapatia vifaa vya mazoezi na jezi, waliamini itakuwa ni chachu kwao kupambana na kumaliza kwenye nafasi mbili za juu na kwa msimu huu Yanga walifanikiwa kutwaa ubingwa.
"Tunafurahi kuona matunda na ushirikiano wa udhamini wetu umefanikiwa, tunajua kwamba klabu hizi mbili za Simba na Yanga tunazodhamini zinashindana kila mwaka na msimu huu umekuwa ni wa Yanga," alisema Kavishe.
Aliwataka wahakikishe msimu ujao pia wanafanya vizuri katika ligi hiyo licha ya kuwapo kwa changamoto kubwa katika kuubakiza ubingwa huo wanaoushikilia kutoka kwa timu nyingine.
Katibu mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako, aliwashukuru TBL kwa kutimiza ahadi yao waliyoiweka kwenye mkataba na kuongeza kwamba ubingwa wao ulipatikana baada ya kukubali kukosolewa kila walipokosea.
Mwalusako alisema kwamba waliyafanyia kazi maoni na ushauri na kujirekebisha pale walipokosea na hicho ndiyo siri ya wao kutwaa ubingwa.
Alisema katika kujiandaa na msimu ujao, kikosi chao kitaanza mazoezi Jumapili huku pia kocha mkuu, Ernie Brandts, akitarajiwa kurejea nchini siku hiyo hiyo kutoka kwao Uholanzi alikokwenda kwa ajili ya mapumziko ya wiki mbili.

King Kibadeni awaondoa Wakongo Simba


https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEijN4dvadffLpnswPFysC5UmxMrrwBhG9qrUePA72-ldgNezJYJHRnT2PymiqUCtD1ySI8YI3ku3iwNGYeuWbWu7o4LmjPTtyHFbnktdOu7ZIe2kI9GWfaGDlPY5kc9nw2mDC4FGWGpTro/s400/Kin1.jpg
King Kibadeni akiwangalia wachezaji wake mazoezini

WAKATI kocha mpya wa timu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, Abdallah 'King' Kibadeni akiahidi kuanza kurejesha heshima ya kikosi hicho katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), tayari amewapiga 'panga' wachezaji wa kimataifa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambao walikuwa wakifanya majaribio.
Wachezaji hao ambao Kibadeni na wasaidizi wake hawajaridhishwa na viwango vyao ni Fabrice Baloko, Fabian Tshiyaz, Patrick Milambo na Joe Fills.
Akizungumza jana, Kibadeni ambaye aliiongoza Simba kufikia fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993, alisema kuwa bado amewapa nafasi wachezaji wengine wawili, kiungo mkabaji kutoka Ivory Coast, Kouakou Martial na beki anayetoka Nigeria, Youssouf Gabra.
Aliongeza kuwa bado milango iko wazi katika kuangalia wachezaji wa kuwasajili na jana jioni zaidi ya nyota watatu kutoka klabu za Prisons, JKT Ruvu na JKT Oljoro, walitarajia kuanza mazoezi chini ya mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba.
Kocha huyo alisema kwamba anataka kufanya usajili kwa umakini ili kuhakikisha msimu ujao Simba inafanya vizuri na anarejesha imani kwa mashabiki wake.
Kocha huyo mkongwe alisema kuwa kikosi hicho ambacho kiko katika mabadiliko kinahitaji muda ili kuweza 'kusimama' na kucheza kama timu hasa kufuatia uamuzi uliofanyika wa kujenga upya timu yenye mchanganyiko wa wachezaji chipukizi na wazoefu.
"Timu hii ina wachezaji wakubwa ambao wanatakiwa kuelimishwa na kubadilishwa kidogo na wachezaji vijana nao wanahitaji kuelimishwa ili kujua nini wanatakiwa kufanya kukabiliana na ushindani," alisema kocha huyo.
Aliongeza kwamba kikubwa anachokiangalia yeye ni wachezaji kuwa na nidhamu huku akisisitiza kutowarudisha wachezaji waliosimamishwa kwa kosa la utovu wa nidhamu.
Simba tayari imeshawasajili Issa Rashid kutoka Mtibwa, Zahoro Pazi (Azam), Andrew Ntalla (Kagera Sugar), Ibrahim Twaha (Coastal Union) na Mganda Samuel Ssenkoomi wa URA ya Uganda.
Wakati huo huo, Simba inatarajia kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa Juni 12 mwaka huu dhidi ya Sofapaka inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka ya Kenya.
Mratibu wa mchezo huo,George Wakuganda, alisema kuwa mchezo huo utatumiwa na Simba kutambulisha wachezaji wapya.