STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, August 12, 2013

Kocha Liver amuwakia Suarez, amtaka aombe radhi

Kocha wa Liverpool

KOCHA wa Liverpool, Brendan Rodgers amemweleza mshambuliaji Luis Suarez kwamba ni lazima aombe radhi kwa kutaka kulazimisha kuihama klabu hiyo.
Suarez (26) amekuwa akifanya mazoezi peke yake baada ya kutaka kulazimisha kuhama Anfield katika kipindi hiki cha usajili.
"Kwanza anapaswa kuomba radhi kwa wachezaji wenzake na klabu," alisema Rodgers alipoulizwa kwamba nini kinachofuata anachopaswa kufanya mshambuliaji huyo.
Ofa mbili za Arsenal zikimekataliwa na Liverpool kwa ajili ya mshambuliaji huyo wa Uruguay.
"Nimemuona kwa muda. Najua huyu si Luis Suarez tunayemfahamu na ni kazi yangu kuwalinda mashabiki na wachezaji kwa sababu wanastahili zaidi ya hilo," aliongeza Rodgers.
Kocha huyo wa Liverpool alikuwa akizungumza baada ya timu yake kula kipigo, bila ya Suarez, cha goli 1-0 dhidi ya Celtic katika mechi yao ya mwisho ya ya kirafiki ya kujiandaa na msimu juzi.
"Amekuwa kwa siku kadhaa akifanya mazoezi peke yake," alisema Rodgers, ambaye atamkosa Suarez wiki hii kwa vile anasafiri na timu yake ya taifa ya Uruguay kwenda kucheza mechi ya kirafiki nchini Japan wiki hii.
"Atakaporejea kutoka katika mechi ya kimataifa tunamuangalia kuanzia hapo."
Pigo la karibuni zaidi katika matumaini ya Suarez' ya kuondoka Anfield lilikuja siku moja tu baada ya Rodgers kumtaka akubali kwamba hatauzwa, pale mmiliki wa Liverpool, John Henry aliposema kwamba nyota huyo hatauzwa kwa pesa yoyote kwa klabu yoyote hata nje ya Uingereza.
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, ameendelea kusema kwamba bado wanamhitaji mchezaji huyo huku ripoti zikisema kwamba klabu hiyo ya London inapanga kumfanya Suarez kuwa ndiye mchezaji anayelipwa pesa nyingi zaidi klabuni hapo kwa kumpa mshahara wa paundi 160,000 kwa wiki endapo atajiunga nao.
(Sunday Mirror)

Sunday, August 11, 2013

HILI NDILO TAMKO LA JESHI LA POLISI KUHUSU SHEIKH PONDA ISSA PONDA



1.  MNAMO TAREHE 10, AGOSTI ,2013 MAJIRA YA SAA 8 MCHANA, MAENEO YA SHULE YA MSINGI KIWANJA CHA NDEGE MANISPAA YA MOROGORO,  KULIFANYIKA KONGAMANO LA BARAZA LA EID LILILOANDALIWA NA UMOJA WA WAHADHILI MKOANI MOROGORO. DAKIKA KUMI KABLA YA KONGAMANO HILO KUMALIZIKA  ALIFIKA SHEKHE PONDA ISSA PONDA AMBAYE ALIZUNGUMZA KWA MUDA MFUPI.
 
2. KONGAMANO HILO LILIFUNGWA  MAJIRA YA SAA 12:05 JIONI AMBAPO WATU WALIANZA KUTAWANYIKA, BAADHI YAO WAKIWA WAMEZINGIRA GARI DOGO ALILOKUWA AMEPANDA SHEKHE PONDA. BAADA YA KUTOKA KATIKA  ENEO HILO, ASKARI WA JESHI LA POLISI WALIZUIA GARI HILO KWA MBELE KWA NIA YA KUTAKA KUMKAMATA SHEKHE PONDA AMBAYE MPAKA SASA  ANATUHUMIWA KWA KOSA LA KUTOA MANENO YA UCHOCHEZI SEHEMU MBALIMBALI HAPA NCHINI YENYE MLENGO WA KUSABABISHA UVUNJIVU WA AMANI.
 
3. BAAADA YA ASKARI KUTAKA KUMKAMATA, WAFUASI WAKE WALIZUIA UKAMATAJI HUO KWA KUWARUSHIA  MAWE ASKARI.  KUFUATIA PURUKUSHANI  HIYO, ASKARI WALIPIGA RISASI HEWANI KAMA ONYO LA KUWATAWANYA.
 
4. KATIKA VURUGU HIZO, WAFUASI HAO WALIFANIKIWA KUMTOROSHA  MTUHUMIWA. HIVI SASA IMETHIBITIKA KUWA SHEKHE PONDA YUKO KATIKA HOSPITALI YA TAIFA YA MUHIMBILI AKITIBIWA JERAHA KATIKA BEGA LA MKONO WA KULIA LINALODAIWA ALILIPATA KATIKA PURUKUSHANI HIZO.
 
5. KUFUATIA TUKIO HILO, TIMU INAYOSHIRIKISHA WAJUMBE KUTOKA JUKWAA LA HAKI JINAI IKIONGOZWA NA KAMISHINA WA JESHI LA POLISI  CP ISSAYA MNGULU IMEANZA KUFANYA UCHUNGUZI WA TUKIO HILO.
 
6. AIDHA, JESHI LA POLISI LINATOA  WITO KWA  WANANCHI KUWA WATULIVU WAKATI SUALA HILI LINASHUGHULIKIWA KISHERIA.
 
Imetolewa na:-
Advera Senso- SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.

TPBO Limited 'yamfungia' bondia kwa udanganyifu

Bondia Ramadhani Kido aliyefungiwa na TPBO
OGANAIZESHENI ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO-Limited) imemfungia kwa muda usiojulikana bondia machachari, Ramadhani Kido kwa madai ya kufanya udanganyifu katika pambano lake dhidi ya Chupaki Chipindi na kusababisha kutokea vurugu ukumbini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Rais wa TPBO-Limited, Yassin 'Ustaadh' Abdallah', Kido alifanya udanganyifu kwa kujiangusha ulingoni sekundu chache baada ya pambano lake na Chipindi kufanyika kwenye ukumbi wa Dar Live na kusababisha usumbufu mkubwa.
Ustaadh, alisema Kido alijiangusha na kugoma kuendelea na mchezo wakati mpinzani wake alipomrushia konde ambalo hata hivyo alikumpata na kufanya mashabiki waliofurika ukumbini kurusha chupoa za maji na kutukana kitu ambacho alisema TPBO haikikubali.
Alisema kilichofanyika ni udanganyifu kama aliowahi kuufanya Francis Cheka kwa kukataa kucheza na Japhet Kaseba na wao kumfungia kwa muda kabla ya kumasamehe, hivyo hata kwa Kido hali itakuwa hivyo kwa vile ameonyesha siyo wanamichezo.
Ustaadh alisema mara baada ya kumalizwa kwa pambano hilo kwa Kido kupigwa kwa KO ya sekunde 23, alimhoji sababu ya kufanya uhuni ule na kwa maelezo yake alimwambia kuwa mpinzani wake alipanda na 'jini' ulingoni lililomdhibiti kitendo alichodai ni kuingiza ushirikina katika michezo.
"Vitendo kama hivi huwa hatukubaliani navyo, tunaamini kabisa bondia huyu hakutaka kupigana ila aliingia mkataba na waratibu ambao ni Global Publishers, hivyo mbali na kumfungia pia tunamtaka arudishe fedha alizochukua kwa pambano hilo," alisema Ustaadh.
MICHARAZO halikubahatika kumpata Kido kusikia maoni yake juu ya tuhuma hizo na adhabu aliyopewa na TPBO, ingawa mashuhuda wa pambano hilo ambalo lilifuatiwa na pigano kali kati ya Francis Miyeyusho aliyemnyuka Mzambia Fidelis Lupapa, ni kwamba Kido alijiangusha.
"Sijawahi kuona bondia anaanguka na kugoma kucheza bila hata kuguswa na ngumi, huu ni uhuni na tumeibiwa fedha zetu. Mambo haya ndiyo yanayofanya ngumi za Tanzania zisiendelee kwa vile zinakatisha tamaa waaandaaji na mashabiki," alisema Ally Kisa 'Kingkong' mmoja wa mashuhuda wa michezo hiyo ya Eid Mosi aliyezungumza na MICHARAZO mapema leo.

Benchi la Ufundi linachekaaaaaa!


BENCHI la ufundi la klabu ya Yanga limeusifia usajili wao iliyofanya safari hii na kutamba kuwa hawaoni cha kuwazuia kutetea tena taji lao la Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Fred Felix Minziro, aliiambia MICHARAZO kuwa, kwa namna usajili wao ulivyofanywa kwa umakini mkubwa na hasa safu yao ya mbele kunawapa nafasi ya kuwa ya kutetea taji lao na kufanya vyema kwenye mechi za kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Minziro alisema, msimu wa 2013-2014 unaoatarajiwa kuanza wiki mbili zijazo utakuwa wao kwa kuringia wachezaji iliyonayo na namna wanavyojiandaa, huku wakiionya mapema Azam kwamba wajiandae na kipigo Jumamosi katika mechi ya Ngao ya Hisani.
Yanga na Azam zitaumana katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam kuashiria kuanza kwa msimu mpya, ambapo wana lamabalamba wenyewe walijichimbia Afrika Kusini na wanatarajiwa kuwasili kesho baada ya kambi ya wiki moja ugenini.
"Kikosi kipo imara na vijana wanatuma matumaini makubwa ya kufanya vyema msimu huu kuliko ilivyokuwa msimu uliopita. Kifupi tunaamini tutatetea taji letu kwa sababu hatuoni kitu cha kutuzuia kuanzia kikosi tulichonacho hadi maandalizi tuliyofanya," alisema.
Minziro aliongeza kushika kwa wepesi kwa maelekezo ya makocha kwa wachezaji wageni kikosini kunawafariji na kuwapa fursa ya benchi lao kumtumia mchezaji yeyote wakati wowote katika mechi yoyote bila tatizo.
"Wachezaji wageni wameshika haraka maelekezo kitu ambacho kimeturahisishia kazi na ndiyo maana tunaamini kwa silaha hizi tulizonazo sijui kama kuna timu itakayofua dafu mbele yetu," alisema Minziro beki wa zamani wa kimataifa wa Yanga na Taifa Stars.
Yanga inatarajiwa kukata utepe wa Ligi Kuu kwa kuumana na Ashanti United ambayo imejichimbia Kigoma na mwishoni mwa wiki wanatarajiwa kucheza mechi mbili na timu za nchini Burundi walikozifuata ili kujiweka fiti kabla ya kuwavaa watetezi hao wa ligi.
Jioni ya leo iliendeleza ubabe katika mechi zake za kirafiki za kujipima nguvu kwa kuilaza SC Villa ya Uganda kwa mabao 4-1 ikiwa ni ushindi wa tatu mfululizo baada ya awali kuilaza Mtibwa Sugar 3-1 kisha kuikamua kiduchu 3 Pillars ya Nigeria kwa bao 1-0.

Cheka abadilishiwa bondia pambano la WBF

Francis Cheka

Bondia Phil Williams ndiye atakayepigana na Cheka,

WAKATI akiendeleza rekodi yake ya kutopigwa katika ardhi ya Tanzania kwa karibu miaka 10 sasa, bondia Francis Cheka 'SMG' amebadilishiwa mpinzani atakayepigana naye Agosti 30 kuwania ubingwa wa WBF ulio wazi kwa sasa kutoka Findley Derrick hadi Phil Williams.
Mabondia wote hao wawili waliobadilioshana ili kupigana na Cheka anayeshikilia ubingwa wa IBF Afrika na mikanda minginje inayotambuliwa kimataifa wanatokea Marekani.
Rais wa Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO-Limited), linalosimamia pambano hilo la kimataifa litakalochezwa kwenye ukumbi wa Dimaond Jubilee,  Yassin Abdallah 'Ustaadh' alisema Derrick ameondolewa kwa kukosa sifa za kupigana a Cheka.
Ustaadh alisema baada ya kupitiwa kwa rekodi za mabondia wote ilionekana Cheka amemuacha mbali Derrick na hivyo WBF ikamteua Williams anayeshikilia nafasi ya 45 duniani kati ya mabondia zaidi ya 900 wa uzito wa Super Middle kupigana na Mtanzania huyo.
Cheka yeye yupo nafasi ya 34 duniani katika uzito huo tofauti na ilivyokuwa kwa Derrick anayeshikilia nafasi ya 95 kati ya mabondia 1220 wa uzani wa kati, kitu ambacho kingempa nafasi nzuri Cheka kumshinda kirahisi mpinzani wake kwa wasifu na vigezo hiovyo.
Rais huyo wa TPBO-Limied alisema kutokana na hali hiyo ndiyo ikaamuliwa Derrick aenguliwee na nafasi yake kupewa Williams ambapoa tayari Cheka ameshataarifiwa juu ya mabadiliko hayo na anapaswa kujiandaa vyema ili kuipeperusha vizuri bendera ya Tanzania.
"Haya ni mabadiliko ya kawaida, hivyo kila kitu kinaendelea vyema juu ya maandalizi ya mchezo huo ambao ufasindikizwa na  mingine kadhaa ukiwamo wa kuwania ubingwa wa Afrika wa WBF kati ya Thomas Mashali na Mada Maugo," alisema Ustaadh.
Wakati akibadilishiwa mpinzani, Cheka juzi alimfumua Mmalawi Chiotcha Chimwemwe kwa pointi na kuendeleza rekodi ya kutipigwa katika ardhi ya Tanzania tangu Agosti 2013.
Cheka alimshinda Mmalawi huyo katika pambano lisilo la ubingwa lililofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro lililokuwa la raundi nane, ingawa baadhi ya mashabiki wanaamini kuwa Mtanzania huyo alibebwa mbele ya Chiotcha.
Hiyo ni mara ya pili kwa Cheka kumpiga Mmalawi huyo na kuibua hisia hizo baada ya awali kufanya hivyo Desemba 24 jijini Arusha walipokuwa wakiumana kuwania taji la IBF Afrika, ambapo Cheka alishinda na kutetea taji hilo kwa pointi huku akiachiwa majeraha makubwa.

Ajali nyingine ya basi, safari hii basi la Meridian

MATUKIO ya ajali za barabarani kwa mabasi ya abiria yameendelea baada ya leo tena basi la kampuni ya Meridian kupata ajali mbaya katika  eneo la Mbwewe, mjini Bagamoyo.
BASI la Meridian linalofanya safari zake Dar es Salaam na Rombo limepata ajali mbaya eneo la Mbwewe Bagamoyo
mkoani Pwani likiwa safarini kuelekea jijini Dar es Salaam likitokea Rombo.
Abiria kadhaa wamepoteza maisha katika ajali hiyo japo idadi kamili bado haijafahamika.

Chanzo: Jamii Forum
Baadhi y abiria walinusurika wakisaka mizigo yao baada ya ajali hiyo iliyopoteza uhai wa watu kadhaa

Hatimaye yathibitika Sheikh Ponda kujeruhiwa kwa risasi angalia picha zake

Jeraha la Sheikh Ponda linavyoonekana kwa karibu

Sheikh Ponda akiwa hospitalini


Sheika Ponda akiwa wodini Muhimbili

BAADA ya danadana ya Polisi kukwepa ukweli juu ya tukio la kupigwa risasi na kujeruhiwa kwa Sheikh Ponda Issa Ponda, ukweli sasa upo hadharani baada ya kiongozi huyo wa Umma wa Kiislam kuonesha jeraha hilo hadharani akiwa kalazwa Muhimbili.
Awali Polisi mkoa wa Morogoro kupitia Kamanda wake Faustin Shilogile lilikuwa likidai halijui lolote kuhusu tukio hilo, licha ya kukiri kwamba ilitaka kumkamata kiongozi huyo kipenzi wa waislam walio wengi.
Tangu jana vyombo vya habari vikitumia vyanzo vyake vya habari kutoka mjini humo ikiwemo MICHARAZO viliripoti juu ya tukio hilo ambalo lilitokea jioni mara baada ya Sheikh huyo kuhutubia kwenye Kongamano la Kiislam, lakini Polisi ikawa inavunga kuwa haujui lolote.
Hatimaye sheikh huyo alitua jijini mchana kwa matibabu katika hospitali ya Muhimbili na 'kuwaumbua' wale waliokuwa wakikanusha taarifa hizo kwamba hakuna kilichotokea juu ya kujeruhiwa kwake.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amezungumza jijini Dar leo na kumtaka Rais Jakaya Kikwete na IGP Saida Mwema kuangalia namna ya kuthibiti jeshi la Polisi juu ya matumizi ya risasi za moto kwa raia wasio na silaha yoyote.
Matukio ya polisi kuwatwanga risasi raia kwa sasa imekuwa kama fasheni, kitu ambacho kinawatia hofu raia juu ya umakini wa askari wa jeshi hilo ambalo ni la usalama wa raia na mali zao.

Yanga kama Simba, Ngassa atupia moja wakiiua Sc Villa 4-1

Na Prince Akbar YANGA SC imetuma salamu Johannesrbug, Afrika Kusini ambako Azam FC wameweka kambi kujiandaa na msimu mpya- kufuatia ushindi wa mabao 5-1 leo katika mchezo wa kirafiki dhidi SC Villa ya Uganda, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Yanga na Azam zitamenyana Jumamosi ijayo Uwanja wa Taifa, katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii, kuashiria ujio wa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. Azam imeweka kambi Afrika Kusini kujiandaa na mechi hiyo ya kufungua msimu na Yanga wanaendelea na maandalizi yao Dar es Salaam, wakitarajiwa kuingia kambini baada ya mechi ya leo kisiwani Pemba, au Bagamoyo, Pwani.
Akaunti mpya; Ngassa amefungua akaunti
mpya ya mabao Yanga leo
Katika mchezo wa leo, hadi mapumziko, tayari Yanga SC walikuwa mbele kwa 3-1, mabao yake yakifungwa na Mrisho Ngassa dakika ya saba, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ dakika ya 27 na Didier Kavumbangu dakika ya 30, wakati la nne lilifungwa kipindi cha pili na Haruna Niyonzima dakika ya 62. Bao la kufutia machozi la Villa ambayo jana ilifungwa 4-1 pia na Simba Uwanja huo huo wa Taifa, lilifungwa na Moses Ndaula dakika ya 18.    Katika mechi zake za awali za kujiandaa na msimu, Yanga SC ilitoa sare ya 2-2 na URA ya Uganda kabla ya kuzifunga 3-1 Mtibwa Sugar na 3Pillars ya Nigeria 1-0.  Azam nayo imekwishacheza mechi tatu za kujipima nguvu Afrika Kusini, imeshinda moja tu dhidi ya Mamelodi Sundwons 1-0, imefungwa mbili, 3-0 na Kaizer Chiefs na 2-1 na Orlando Pirates na kesho itacheza mechi ya mwisho na Moroka Swallows kabla ya kurejea nyumbani keshokutwa. Kikosi cha Yanga SC leo kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, David Luhende/Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan/Rajab Zahir, Athumani Iddi ‘Chuji’/Bakari Masoud, Mrisho Ngassa, Salum Telela, Didier Kavumbangu, Jerry Tegete/Hussein Javu na Haruna Niyonzima/Said Bahanuzi. 

SEMINA YA MAKAMISHNA YAANZA DAR, MWANZA


Na Boniface Wambura
SEMINA kwa ajili ya makamishna wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) pamoja na mtihani wa utimamu wa mwili (physical fitness test) kwa  waamuzi wote wa daraja la kwanza (Class I) wanaotaka kuchezesha VPL msimu wa 2013/2014 vinaanza kesho (Agosti 12 mwaka huu) katika vituo vya Dar es Salaam na Mwanza.

Mafunzo hayo yatakayomalizika Agosti 14 mwaka huu yatakuwa chini ya wakufunzi Leslie Liunda, Joan Minja na Riziki Majara kwa kituo cha Dar es Salaam wakati kituo cha Mwanza kitakuwa na Alfred Rwiza na Omari Kasinde.

Kwa Dar es Salaam mafunzo yatafanyika Uwanja wa Taifa wakati Mwanza itakuwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Kituo cha Mwanza kitakuwa na makamishna na waamuzi kutoka mikoa ya Geita, Kagera, Katavi, Kigoma, Manyara, Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Singida na Tabora.

Kituo cha Dar es Salaam kitahusisha waamuzi na makamishna kutoka mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Kilimanjaro, Lindi, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Njombe, Pwani, Ruvuma na Tanga.

Washiriki wote wanakumbushwa kuwa ni lazima wafuate utaratibu huo wa vituo, na si vinginevyo.

Kagera Sugar yatakata Uganda, kesho kuivaa URA

Kikosi cha Kagera Sugar

KAGERA Sugar iliyosafiri mpaka Uganda jioni ya leo imeanza vyema michezo yao ya kujiandaa na Ligi kuu Tanzania Bara baada ya kuikwanyua Bunawaya Fc kwa bao 1-0 katika pambano la kirafiki la kimataifa lililochezwa jijini Kampala.
Kocha Msaidizi wa Kagera, Mrage Kabange wimba wa zamani wa Simba na Taifa Stars, alisema kikosi chao kilionyesha soka la kuvutia katika pambano hilo licha ya ugeni na kujipatia bao katika kipindi cha kwanza lililofungwa na Juma Mpola.
Timu hiyo itashukla tena dimbani kesho kuumana na URA katika pambano jingine kabla ya kuangalia mechi nyingine na kurejea Kagera tayari kujiandaa na mechi yao ya fungua dimba ya ligi kuu msimu wa 2013-2014 dhidi ya 'wageni'  Mbeya City mechi itakayochezwa uwanja wa Sokoine, Agosti 24.

MAKOCHA 32 KUSHIRIKI KOZI YA FIFA COPA COCA-COLA

 
Na Boniface Wambura
MAKOCHA 32 kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Visiwani wanashiriki kozi ya Copa Coca-Cola inayoanza kesho (Agosti 12 mwaka huu) jijini Dar es Salaam chini ya Mkufunzi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA).

Kozi hiyo itakayomalizika Agosti 17 mwaka huu itafunguliwa saa 3 kamili asubuhi kwenye ukumbi wa Msimbazi Centre na washiriki wote tayari wameshawasili Dar es Salaam. Mkufunzi wa kozi hiyo ni Govinder Thondoo kutoka Mauritius.

Washiriki wa kozi hiyo ni Ahazi Ibrahim Kasegese (Mbeya), Aloyce Mayombo (Pwani), Andrew Zoma (Tabora), Asuri Msakamali (Simiyu), Bakari Khamis Kilambo (Kaskazini Pemba), Chacha Sambulo (Mara), Charles Rwezaura (Kagera), Daniel Sambala (Njombe), Dudu Haruni (Iringa) na Emmanuel Kapurata (Rukwa).

Faki Makame Haji (Kaskazini Unguja), Fatawi Khamis Sheha (Kusini Pemba), Hamisi Omary Mabo (Kigoma), Hussein Maulid (Morogoro), Issa Lugaza (Kilimanjaro), James Gaspar (Shinyanga), James Wambura (Arusha), Jomo Jackson Puccey (Lindi), Joseph Sihaba (Dodoma), Kelvin Haule (Ruvuma) na Kessy Juma Abdallah (Tanga).

Kessy Mziray (Mwanza), Menswi Mchwampaka (Kinondoni), Mohamed Abdallah Kweka (Singida), Nurdin Gogola (Temeke),  Pius Kamande (Rukwa), Ramadhan Abrahman Ramadhan (Mjini Magharibi), Ramadhan Salum Mnyoti (Manyara), Raphael Ngeleja (Geita), Samuel Edgar Maokola (Ilala), Shaweji Nawanda (Mtwara) na Vuai Abdul Haji (Kusini Unguja).

Fainali za U15 Copa Coca-Cola ngazi ya Taifa zitafanyika Septemba mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Sheikh Ponda aletwa Muhimbili? Ukweli kuweka hadharani Alasiri Msikiti wa Mtambani

 
HABARI zilizotufikia hivi punde zinasema Sheikh Ponda Issa Ponda ameletwa Dar na kukimbizwa Hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu na tayari kuna habari kwamba Polisi wakiwa kwenye madifenda yao wameshatimba hospitalini hapo.
MICHARAZO inafuatilia taarifa hizo zilizopenyezwa hivi punde kujua ukweli na ikiwezekana kuwatupia na picha kama ni kweli Sheikh huyo machachari na kiongozi wa umma wa waislam walio wengi amepelekwa hospitalini hapo.
Pia taarifa rasmi kuhusu hali ya Sheikh Ponda inatarajiwa kutolewa Alasiri hii katika Msikiti wa Mtambani na Amir wa Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Mussa Kundecha baada ya kuwepo kwa mkanganyiko juu ya hali ya kiongozi huyo wa umma wa waislam Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda juu ya tukio la kujeruhiwa kwa risasi begani na Polisi wakati alipotaka kukamatwa, japo Polisi wanaendelea kukomaa kwamba hawajui lolote.

Yanga, Sc Villa hapatoshi leo taifa, Javu kuendeleza dozi?

Kikosi cha Yanga
TIMU ya soka ya Yanga, inatarajiwa kushuka dimbani jioni ya leo kuvaana na SC Villa ya Ugannda huku mashabiki wakielekeza macho yao kwa Hussein Javu kuona atawafanyizia vipi wageni hao katika mechi hiyo ya leo.

Javu aliyetua Jangwani hivi karibu akitokea Mtibwa Sugar, ameanza na moto kwa kufunga katika mechi zake mbili za awali akiisiaidia Yanga kuisulubu Mtibwa kwa mabao 3-1 na kuizamisha 3 Pillars ya Nigeria kwa bao pekee katika mechi iliyoichezwa katikati ya wiki.

Villa iliyochezea kichapo cha aibu jana toka kwa Simba, itaikabili Yanga itakayotumia mchezo huo kujiweka vyema kabla ya pambano lake la Ngao ya Hisani dhidi ya Azam litakalofanyika siku ya Jumamosi.

Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema jana kuwa maandalizi ya mechi hiyo yamekamilika na kila mchezaji yu tayari kuonesha uwezo wake.

Kwa upande wa Yanga, si tu itaitumia mechi hiyo kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu itakayoanza Agosti 24, pia kunoa makali ya kuikabili Azam FC katika mechi ya Ngao ya Hisani itakayochezwa Agosti 17.

Mechi ya Ngao ya Hisani ambayo ni ishara ya ufunguzi wa Ligi Kuu, itachezwa ikiwa ni siku nne tangu Azam warejee nchini wakitokea nchini Afrika Kusini walikokwenda kusaka makali kwa ajili ya msimu mpya tangu Agosti 3, wakicheza mechi za kirafiki.

Wakati Azam wakitokea Afrika Kusini, Yanga wao tofauti na msimu uliopita ambapo walikwenda kujinoa nchini Uturuki kabla ya kuanza kwa ligi hiyo, safari hii wameamua kujifua nyumbani.

Kwa mujibu wa tovuti ya Yanga, Kocha Mkuu wake, Ernie Brandts, amefurahia kwisha salama kwa mazoezi ya nyota wake hadi jana asubuhi, huku akisema hakuna majeruhi hata mmoja kuelekea mechi ya leo.

“Mechi ya kesho (leo) dhidi ya Villa, itakuwa kipimo kizuri kwetu kwani itakuwa ya mwisho kabla ya kuikabili Azam katika mechi ya Ngao ya Hisani na kuanza kwa Ligi Kuu ya Vodacom,” alisema Brandts.

Kwa mujibu wa tovuti ya Yanga, viingilio vya mechi ya leo ni sh 20,000 kwa jukwaa la VIP A; sh 15,000 kwa VIP B; sh 10,000 kwa VIP C na sh 5,000 kwa viti vya rangi ya machungwa, bluu na kijani.

Wapenzi wa soka na mashabiki wa klabu ya Yanga wameombwa kujitokeza kwa wingi kujionea uwezo wa timu yao kuelekea vita ya kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu ya Vodacom ambao iliutwaa msimu uliopita.

Wakati Yanga iliyoanzishwa mwaka 1935 ikimaliza msimu uliopita na ubingwa ukiwa wa 24 tangu mwaka 1965, Villa ni mabingwa mara 16 tangu ianzishwe mwaka 1975, ambapo mara ya mwisho kuonja ubingwa wa Uganda ni mwaka 2004.