STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, November 9, 2013

MAJANGA! MAITI YAKUTWA NA KETE 65 ZA 'BWIMBWI' POLISI WAIZUIA!

  





 Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani, akitoa taarifa kwa waandishi wa habari nje ya ofisi yake huku akiwa na baadhi ya askari wa jeshi hilo mkoani hapa.


 Pasi ya kusafiria kijana huyo alizokutwa nazo...





 Kete zilizokutwa tumboni mwa kijana huyo baada ya kufan yiwa upasuaji katika hospitali ya Rufaa ya Mbeya.


 Kete inayosadikika kumuua kijana huyo baada ya kupasukia tumboni.






 Kulia ni kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani, akiwa amevalia mavazi maalum, kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya rufaa ya Mbeya kwa ajili ya kuona maiti hiyo.





 Maiti ya kijana Kassim Said Mboya ukiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya rufaa ya Mbeya baada ya kufanyiwa upasuaji na kutolewa dawa zinazodhaniwa kuwa ni za kulevya.




MAITI ya kijana Kassim Said Mboya(36), mkazi wa Jijini Dar es Salaam, imekutwa na kete 65 za zinazodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya.

Taarifa zilizolifikia Tanzania daima tangu jana jioni, zilieleza kuwa maiti ya kijana huyo, ilikutwa katika basi la kampuni ya Taqwa eneo la Kasulumu lililokuwa likitokea Jijini Dar es Salaam nchini Tanzania na kuelekea nchini Malawi.
PAPARAZI blog ilifuatilia na kujua ukweli wake kisha kuwasiliana na kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani leo asubuhi, ambaye pia alikiri kuwepo kwa maiti hiyo na kumwambia mwandishi wakutane eneo la chumba cha maiti cha hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwa ajili ya kuona mwili wa marehemu huyo.


Kamanda wa polisi wa mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani, alisema kuwa kijana huyo kabla hajafariki, alikamatwa Novemba 7, mwaka huu akiwa ndani ya basi hilo lenye namba za usajili T 319 BLZ akiwa na tiketi yenye jina la Kassim Mueck Michael.

‘’Awali basi hilo kabla ya kufika mpakani Kasumulu na abiria kushuka na kuanza kufanya taratibu za kuvuka mpaka na kuingia nchini Malawi, marehemu alibaki kwenye gari huku afya yake ikizidi kudhoofika’’ alisema Kamanda Dwani Athumani.

Alisema baada ya kuona hivyo, wahusika wa basi hilo walitoa taarifa kituo cha polisi ambapo kijana huyo alichukuliwa na kupelekwa katika hospitali ya wilaya ya Kyela na kabla hajapata matibabu alifariki dunia.

Alieleza kuwa, kwa kuwa kijana huyo kabla hajapasuka alikuwa na dalili zilizogundulika kuwa alikuwa na dawa za kulevya, iliamuliwa mwili huo kusafirishwa mpaka hospitali ya Rufaa ya Mbeya ambako ulipasuliwa na kukutwa na pipi 65 zinazodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya na moja ikiwa imepasuka.
‘’Natoa rai kwa wananchi wa mkoa wa Mbeya nan chi nzima kwa ujumla kufika hospitali ya rufaa ya Mbeya kwa ajili ya utambuzi wa mwili wa marehemu na kwamba ijulikane kuwa usafirishaji na utumiaji wa dawa za kulevya ni hatari kwa afya ya mtumiaji’’ alisema Kamanda Diwani.


Alipoulizwa kuwa kutokana na mkanganyiko uliowahi kujitokeza katika upotevu na kuwa dawa zilizowahi kukamatwa awali hazikuwa dawa, alisema kuwa kikosi kazi chake kimejipanga vema na jitihada za kupeleka kwa mkemia mkuu zinafanywa chini ya kikosi kidogo cha ulinzi na usalama cha mpaka wa Kasumulu.


Hii ni maiti ya tatu kukamatwa na dawa zinazodhaniwa kuwa ni za kulevya mkoani Mbeya, ambapo shehena ya kwanza ya dawa hizo ilikamatwa mwaka mjini Tunduma mkoani hapa mwaka 2006 ikiwa kwenye tumbo la marehemu Kombo Siriri.


Shehena ya pili ya dawa hizo ilikamatwa Desemba 5, 2011 katika hotel ya High Class mjini Tunduma, ikiwa katika tumbo la maiti ya Mshanga Mwasala.

Licha ya ukamataji wa dawa hizo na baadhi ya watuhumiwa wakiwa hai, hakuna mtuhumiwa aliyewahi kupatikana na hatia tangu mfululizo wa ukamata dawa hizo zinazodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya mkoani Mbeya.

UHAI CUP KUANZA NOV 17, TANZANITE YATUA SALAMA MAPUTO

Michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha wachezaji wenye umri chini ya miaka 20 wa klabu za Ligi Kuu inaanza kutimua vumbi Novemba 17 mwaka huu katika viwanja vya Karume na Azam Complex, Dar es Salaam.

Droo ya michuano hiyo inayodhaminiwa na Maji Uhai imefanyika leo (Novemba 8 mwaka huu) mbele ya waandishi wa habari katika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambapo timu zimepangwa katika makundi matatu.

Kundi A linaundwa na timu za Azam, Coastal Union, JKT Ruvu Stars, Mbeya City na Yanga, wakati kundi B ni Ashanti United, Mgambo Shooting, Oljoro JKT na Ruvu Shooting. Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Rhino Rangers na Tanzania Prisons ndizo zinazounda kundi C.

Mechi za ufunguzi kundi A Novemba 17 mwaka huu ni kati ya Azam na Coastal Union (saa 2 asubuhi- Karume), Yanga na Mbeya City (saa 8 mchana- Karume). Kundi B ni Ruvu Shooting na Ashanti United (saa 4 asubuhi- Karume), Oljoro JKT na Simba (saa 10 jioni- Karume).

Kagera Sugar na Mtibwa Sugar (saa 2 asubuhi- Azam) na Rhino Rangers na Tanzania Prisons (saa 10 jioni- Azam) ndizo zitakazocheza mechi za ufunguzi Novemba 17 mwaka huu katika kundi C.

Robo fainali ya michuano hiyo itachezwa Novemba 24 na 25 mwaka huu wakati nusu fainali itapigwa Novemba 26 na 27 mwaka huu. Mechi ya kutafuta mshindi wa tatu na ile ya fainali zitachezwa Novemba 30 mwaka.

TANZANITE YATUA SALAMA MAPUTO
Kikosi cha timu ya Taifa ya wanawake chini ya miaka 20 (Tanzanite) kimewasili salama jijini Maputo, Msumbiji tayari kwa mechi ya marudiano ya raundi ya kwanza ya Kombe la Dunia itakayochezwa kesho (Novemba 9 mwaka huu).

Kwa mujibu wa kiongozi wa msafara wa Tanzanite, Kidao Wilfred ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), timu hiyo chini ya Kocha wake Rogasian Kaijage ilifanya mazoezi yake ya kwanza jana asubuhi.

Tanzanite itafanya mazoezi yake ya mwisho leo (Novemba 8 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa wa Zimpeto ambao ndiyo utakaotumika kwa mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 10 kamili jioni kwa saa za Msumbiji.

Nao wachezaji waliobaki kumalizia mtihani yao ya kidato cha nne wameondoka leo saa 11 jioni kwa ndege ya LAM wakiongozwa na naibu kiongozi wa msafara, Khadija Abdallah Nuhu ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA).

KESSY KUSIMAMIA MECHI YA KOMBE LA DUNIA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Lina Kessy kuwa kamishna wa mechi ya Kombe la Dunia Kanda ya Afrika kwa wanawake chini ya umri wa miaka 20 kati ya Afrika Kusini na Botswana.

Mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya kwanza itachezwa nchini Afrika Kusini, Novemba 9 mwaka huu. Waamuzi kutoka Zambia ndiyo watakaochezesha mechi hiyo namba kumi.

Waamuzi hao wataongozwa na Glads lengwe atakayepuliza filimbi wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Bernadette Kwimbira kutoka Malawi, namba mbili ni Mercy Zulu na mezani atakuwepo Sarah Ramadhani, wote wa Zambia.

Afrika Kusini ilishinda mechi ya kwanza ugenini mabao 5-2. Mshindi wa mechi hiyo atacheza raundi ya pili na mshindi wa mechi kati ya Tanzania na Msumbiji.

MECHI YA JKT RUVU, COASTAL YAINGIZA LAKI 2/-
Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya wenyeji JKT Ruvu na Coastal Union ya Tanga iliyochezwa juzi (Novemba 6 mwaka huu) Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam imeingiza sh. 201,000.

JKT Ruvu iliibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi hiyo namba 85 na kushuhudiwa na watazamaji 67 waliokata tiketi kwa viingilio vya sh. 3,000 na 10,000.

Kila klabu ilipata mgawo wa sh. 39,010 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 30,661.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 19,835, tiketi sh. 38,100, gharama za mechi sh. 11,901, Bodi ya Ligi sh. 11,901, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 5,950 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 4,628.

Nayo mechi kati ya Ashanti United na Simba iliyochezwa juzi Uwanja wa Taifa imeingiza sh. 24,931,000 ambapo kila klabu ilipata mgawo wa sh. 5,333,590.

Wakati huo huo, mechi za jana (Novemba 7 mwaka huu) kati ya Yanga na Oljoro imeingiza sh. 34,902,000 kutokana na watazamaji 6,045 ambapo kila klabu imepata sh. 7,812,477.95. Mechi ya Azam na Mbeya City iliyochezwa Azam Complex yenyewe imeingiza sh. 15,973,000 kwa watazamaji 4,857 na kila klabu imepata sh. 3,953,162.

WATATU WAOMBEWA ITC KUCHEZA UJERUMANI
Watanzania watatu wameombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) na Chama cha Mpira wa Miguu Ujerumani (DFB) ili wacheze mpira wa miguu nchini humo.

Wachezaji hao ni Charles Mishetto na David Sondo wanaombewa hati hiyo ili waweze kujiunga na timu ya SpVgg 1914 Selbitz, wakati Eric Magesa ameombewa kibali hicho ili achezee timu ya klabu ya SC Morslingen.

Hata hivyo, katika maombi hayo DFB haikuleza hapa nchini walikuwa wakicheza katika klabu zipi. Wachezaji wote wameombewa hati hiyo kama wachezaji wa ridhaa.

KIUNGO WA YANGA HAROUNA NIYONZIMA NDIYE MWANASOKA BORA WA MWANASPOTI 2013

Haruna akiwajibika uwanjani

Haruna na tuzo zake tatu

KIUNGO wa Yanga SC, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima raia wa Rwanda, ameshinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa gazeti la Mwanaspoti, akiwashinda Amri Kiemba, Shomary Kapombe wa Simba SC na Themi Felix wa Kagera Sugar. 


Katika hafla iliyofana kwenye ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wachezaji wengi, mgeni rasmi akiwa Naibu Waziri wa (TEKNOHAMA) Januari Makamba, mchezaji Niyonzima aliondoka na tuzo tatu, nyingine ya mchezaji wa kigeni na 11 Bora wa Mwanaspti.

Haruna akipokea tuzo yake ya Mwanasoka Bora wa Kigeni kutoka kwa Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Afrika Kusini (SAFA)

Katika tuzo ya mchezaji bora wa kigeni, Niyonzima aliwashinda mchezaji mwenzake wa Yanga, mshambuliaji wa Kiganda, Hamisi Friday Kiiza na mshambuliaji wa Azam kutoka Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche. Mchezaji wa Azam FC, Joseph Kimwaga aliwashinda Juma Luizio wa Mtibwa Sugar na Ramadhani Singano ‘Messi’ katika kinyang’anyiro cha tuzo ya Mchezaji Chipukizi.


Mwanahamisi Omar wa Mburahati Queens aliwashinda Shelida Boniface na Fatuma Mussa katika ya Mchezaji Bora wa kike, wakati Mbwana Samatta aliwashinda Henry Joseph aliyekuwa anacheza Kongsvinger ya Norway kabla ya kurejea Simba SC msimu huu na mshambuliaji mwenzake wa TP Mazembe ya DRC, Thomas Ulimwengu katika tuzo ya mwanasoka anayecheza nje.
Haruna akipokea hundi ya Sh. Milioni 5 kutoka kwa Naibu Waziri wa TEKNOHAMA, Januari Makamba. Wengine kulia ni Zuhura Muro, Mwenyekiti wa Bodi wa MCL na Tido Mhando kushoto, Ofisa Mtendaji Mkuu wa MCL.


Oden Mbaga aliwashinda Martin Sanya na Ibrahim Kidiwa katika tuzo ya Refa bora, wakati Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ aliwashinda Muingereza Stewart Hall wa Azam na Mholanzi Ernie Brandts wa Yanga katika tuzo ya kocha bora.


Thomas Ulimwengu alishinda tuzo ya bao bora alilofunga katika mechi dhidi ya Ivory Coast kuwania tiketi ya Kombe la Dunia, wakati Kipre Tchetche ameshinda tuzo ya Mfungaji bora. 

Juma Kaseja, Mbuyu Twite, Shomary Kapombe, Kevin Yondan, David Mwantika, Amri Kiemba, Thomas Ulimwengu, Haruna Niyonzima, Themi Felix, Mbwana Samatta na Kipre Tchetche wameteuliwa katika ’11 Bora’ wa Mwanaspoti.
 
Zilizotolewa pia tuzo za heshima kwa wachezaji wa zamani nchini akina Nicholas Akwitende, John Lyimo, Mbwana Abushiri, Omar Zimbwe, Jellah Mtagwa na mtangazaji wa zamani maarufu, Mshindo Mkeyenge. Mkeyenge aliyeanza kutangza tangu miaka ya 1960 Radio Tanzania (RTD) aliwahuzunisha wengi baada ya kuwasili jukwaani akiwa amebebwa kutokana na kukatwa mguu kwa sababu ya maradhi ya kupooza. 

Hadhara Charles alipewa tuzo ya kipaji maalum, wakati Rais wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Leodegar Tenga alipewa tuzo ya Utawala Bora katika soka. 

Washindi walipewa na zawadi za fedha, Niyonzima Sh. Milioni 5, wengine Sh. Milioni 1 na wengine 500,000. Kwa ujumla tuzo hizo zilizosindikizwa na burudani ya wanamuziki Juma Nature, Joh Makini na King Kiki zilifana.


BIN ZUBEIRY 

Thursday, November 7, 2013

Kocha Azam abwaga manyanga, kisa...!

Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
KOCHA Muingereza, Stewart John Hall ameamua kujiuzulu kufundisha klabu ya Azam FC baada ya kukubaliana na wamiliki wa timu hiyo na leo hii amewaaga wachezaji wa timu hiyo.
Stewart aliwaaga wachezaji na benchi la Ufundi mara tu baada ya mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baina ya timu hiyo na Mbeya City ulioisha kwa sare ya kufungana mabao 3-3 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Amebwaga manyanga; Stewart Hall amewaaga wachezaji na benchi la Ufundi baada ya sare ya 3-3 na Mbeya City leo Camazi

“Ni kweli nimewaaga wachezaji na wenzangu katika benchi la Ufundi, nimewaambia imebidi niondoke kwa sababu nimepata kazi sehemu nyingine. Lakini pia wamiliki wa timu wameridhia niondoke na ninaondoka vizuri, nawatakia kila heri,”alisema Stewart alipozungumza na BIN ZUBEIRY jioni hii.
Hii inakuwa mara ya pili, Stewart kuondoka Azam, baada ya awali Agosti mwaka jana kuondolewa kiasi cha mwaka mmoja tu tangu aajiriwe akitoka kufundisha timu ya taifa ya Zanzibar.
Stewart alifukuzwa baada ya kuiwezesha Azam kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu na Kombe la Kagame, Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati pamoja na kuiwezesha kutwaa Kombe la Mapinduzi na nafasi yake ikachukuliwa na Mserbia, Boris Bunjak.
Hata hivyo, baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu uliopita, Stewart aliyehamia Sofapaka ya Kenya, alirejeshwa Azam kufuatia kutimuliwa kwa Mserbia, Bunjak.
Stewart akarudia kuipa nafasi ya pili Azam katika Ligi Kuu na kuipa Kombe la Mapinduzi pamoja na kuiwezesha kutwaa taji la Ngao ya Hisani, michuano iliyofanyika mjini Kinshasa, DRC, Desemba mwaka jana. 
Bado haijajulikana sasa Azam itaangukia mikononi mwa kocha gani, ikiwa sasa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu umemalizika na wachezaji wanakwenda mapumzikoni.
Stewart ni kocha wanne kuondolewa Azam tangu ianze kucheza Ligi Kuu msimu wa 2007/2008 baada ya Wabrazil Neider dos Santos na Itamar Amorin na Mserbia Bunjak.
Azam imemaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, ikiwa katika nafasi ya pili kwa pointi zake 27 sawa na Mbeya City, nyuma ya mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 28.

Yanga yarejea kileleni, Azam, Mbeya City zawekwa rekodi zikitoka sare ya 3-3,Mwagane Yeya apiga hat trick

Azam wakishangilia moja ya mabao yao msimu huu

Mbeya City wakiomba dua kuwasaidia wafanye vyema katika mechi zao
MSHAMBULIAJI Mwagane Yeya ameingia kwenye rekodi ya wafungaji wa hat trick msimu huu baada ya jioni ya leo kutupia mabao matatu wavuni wakati timu yake ya Mbeya City ikilazimisha sare ya mabao 3-3 na Azam.
Mchezaji huyo anakuwa wa tatu kufunga mabao matatu katika mechi moja na mzawa wa pili baada ya Abdallah Juma wa Mtibwa Sugar kuvunja rekodi iliyokuwa imedumu kwa misimu miwili tangu iwekwe na Juma Semsue wa Polisi Dodoma mwaka 2010-2011.
Yeya alifunga mabao hayo katika pambano la funga nikufunge baina ya timu yake na Azam lililochezwa kwenye uwanja wa Chamazi na kuzifanya timu hizo kugawa pointi na kuipisha Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi.
Mabao yake aliyafunga katika dakika ya 30, 50 na 73 na kuwafanya washambuliaji wa Azam kuwa na kazi ya kuyarejesha ambapo John Bocco 'Adebayor' alifunga bao la kusawazisha la pili kabla ya Mcha Khamis Vialli kuchomoa bao la tatu dakika ya 83 na kuzifanya timu hizo zigawane pointi na kuweka rekodi ya kutofungika duru zima la kwanza.
Timu hizo ndizo pekee hazijafungwa katika ligi mpaka sasa na zikiwa zimemaliza mechi zake zikiwa na ponti 27 kila mmoja wakizidiwa na Yanga waliorejea kileleni wakiwa na pointi 28 baada ya kuinyuka Oljoro JKT mabao 3-0 kwenye uwanja wa Taifa.
Bao la tatu la Azam lilifungwa na Humphrey Mieno aliyetangulia kufunga dakika ya 13 tu ya mchezo kwa kichwa kabla ya Yeya kusawazisha na kwenda mapumziko wakiwa nguvu sawa ya bao 1-1.
Katika uwanja wa Taifa Yanga ilipata mabao yake kupitia Simon Msuva aliyefunga katika dk ya 23 kabla ya Mrisho Ngassa kufunga bao la pili dakika ya 30 na Jerry tegete kuongeza bao jingine dakika ya 54 na kuhitimisha ushindi wa mechi nne mfululizo wote ukiwa kwa timu za maafande na kurejea kileleni hadi mwakani.
Katika mechi nyingine ya mjini Tabora matokeo ni kwamba timu ya Rhino Rangers ikiwa nyumbani imeshindwa kufurukuta kwa kulazimishwa suluhu na Prisons ya Mbeya.

Kiiza kumkamata Tambwe lna kutimiza ahadi yake leo Taifa?

Hamis Kiiza wa Yanga

Amissi Tambwe wa Simba

Kipre Tchetche wa Azam
MSHAMBULIAJI wa kiganda, Hamis Kiiza 'Diego' hivi karibuni alinukuliwa kwamba angependa kumaliza mechi za duru la kwanza kwa kufunga jumla ya mabao 10, na kabla ya pambano la leo la timu yake ya Yanga dhidi ya Oljoro JKT, tayari anayo mabao nane.
Mabao hayo ni pungufu ya mabao mawili na aliyonayo mkali wa Msimbazi, Mrundi Amissi Tambwe anayeongoza orodha ya wafungaji bora kwa sasa katika Ligi Kuu akiwa na mabao 10, nusu ya mabao aliyoahidi kuyafunga katika msimu wake wa kwanza akiwa na Wekundu wa Msimbazi.
Kiiza, ili kutimiza ahadi yake ya kufunga mabao 10 anapaswa leo kutumbukiza wavuni mabao mawili ambapo mbali na kumkamata mpinzani wake, pia itamfanya kuuaga mwaka 2013 akiwa na furaha na kusubiri kuona mwaka ujao wa 2014 utakuwa wa aina gani kwake na wote wanaokifukizia kiatu cha dhahabu.
Mganda huyo mbali na kutaka kumkamata Tambwe, pia atalazimika kufunga mabao zaidi ikiwezekana ili kumpita Elias Maguri anayeshika nafasi ya pili akiwa na mabao 9 na pia kuwaacha mbali Kipre Tchetche wa Azam mwenye mabao 7 na Juma Luizio wa Mtibwa aliyefunga mabao nane na kulingana naye.
Iwapo atatoka kapa, basi ile ahadi yake ya kufikisha mabao 10 itaambulia patupu na pia kuwaacha wapinzani wake wakimcheka kwa mbaaali kwani itambidi asubiri hadi mwakani panapo majaliwa kuwakimbiza tena.
Wakati Mganda akiwaza hivyo, Kipre Tchetche leo atakuwa na wasaa nzuri wa kuthibitisha kuwa hakubahatika kuwa Mfungaji Bora kwa msimu uliopita wakati atakapovaana na Mbeya City.
Tchetche mwenye mabao saba kwa sasa akishika nafasi ya nne ya wafuingaji inayoongozwa na Tambwe na kufuatiwa na Maguri kisha Kiiza na Luizio, ana kazi nghumu mbele ya Mbeya City ambayo kama ilivyo kwa Azam haijapoteza mechi yoyote msimu huu.
Mashabiki wa soka wangependa kuona 'vita' ya mapro hao ikinoga kama Tchetche atatupia mabao kambani kadfhalika kwa Kiiza na kukimbizana na Tambwe, japo wazawa Muguri na Luizio hawana chao kwa sasa mpaka mwakani kwa vile shughuli yao waliimaliza jana walipozifungia timu zao mabao.
Mbali na mechi za Azam na Mbeya City na ile ya Yanga na Oljoro, leo pia kuna mechi nyingine kati ya Rhino Rangers ya Tabora dhidi ya Prisons Mbeya mechi inayochezwa uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ambayo matokeo yake yataweza kuvuruga tu msimamo wa timu zilizopo chini tofauti na mechi hizo mbili za awali ambazo zinaweza kubadilisha taswira ya msimamo wa Tatu Bora wakati ligi ikienda mapumzikoni.
Azam wanaoongoza msimamo ikiwa na pointi 26 sawa na Mbeya City wakizidiana idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa na watetezi Yanga wapo nafasi ya tatu na pointi zao 25 na mechi yao na Oljoro inaonekana kama nyepesi, japo katika soka hakuna kitu kama hicho.

Arsenal, Chelsea zaua, Barca yaichinja Milan, Atletico Madrid dah!

Samuel Eto'o aliyeifungia Chelsea mabao mawili

Ramsey akishangilia bao lake na Mesut Ozil

KOCHA Arsene Wenger huenda sasa anapumua na kuondokana na presha juu ya uwezo wa kikosi chake baada ya usiku wa kuamkia leo kuwatungua Borussia Dotmund ya Ujreumani ikiwa kwao kwa bao 1-0 na kujiweka pazuri kwenye kundi lake katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Bao pekee lililowekwa na kiungo Aaron Ramsey katika dk ya 62, lilitosha kuzima ngebe wa wanafainali hao wa msimu uliopita na kuipa Arsenal ushindi huo na kuifanya ilingane pointi na Napoli walioinyuka Olympique Maseille mabao 3-2 zote zikiwa na pointi 9 na kutofautiana uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Katika mechi nyingine zilizochezwa jana  Barcelona ikiwa nyumbani iliisulubu AC Milan kwa mabao 3-1, huku nyota wa Argentina,  Lionel Messi akifunga mawili na jingine likizamishwa na Busquets, huku Gerrard Pique akijifunga na kuizawadia wageni bao la kufutia machozi.
Chelsea ilifuata nyayo za Arsenal kwa kuizabua Schalke 04 ya Ujerumani mabao 3-0 kayika pambano lililoshuhudia Samuel Et'oo na mbadala wakem Demba Ba wakifunga mabao hayo yote na kuwapa ushindi muhimu vijana wa Jose Mourinho.
Eto'o alifunga mabao mawili na alipotoka na kuingizwa Ba naye alitupia moja na kufanya Chelsea kutakata ikiwa nyumbani, huku Atletico Madrid ikiwa nyumbani ikiidadavua Viena kwa mabao 4-0, Ajax ikiizima Celtic kwa bao 1-0  na timu za Basel vs Steau Bucharest na Porto na Zenit zikishindwa kutambia katika michezo yao kwa kutoka sare ya baoa 1-1.

Wednesday, November 6, 2013

MAAFA! WATU SITA WAUWAWA, 35 WALAZWA MAPIGANO YA WAFUGAJI NA WAKULIMA MVOMERO

http://www.herald.co.zw/wp-content/uploads/2013/08/knife-blood.jpg
WATU sita wamefariki baadhi watatu wakiwa wamechinjwa, huku watu wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa vibaya katika mapigano ya kugombea ardhi kati ya wafugaji na wakulima huko kijiji cha Lukindo wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro.
Taarifa zinasema kuwa, chanzo cha vita hivyo ambavyo vimeleta athari kubwa ikiwemo familia kuparaganyika kwa hofu ya mapigano hayo ni mifugo ya wafungaji kuingia katika shamba moja la mkulima na kula mazao.
Baada ya kitendo hicho kilichotokea jana kinaelezwa kuwa, mifugo ya wafungaji ikikamatwa na wakulima na kisha kutaka walipwe fidia ya Sh Milioni 3 na kushindwa kupatikana muafaka kabla ya Polisi kuja kuingilia kati.
Hata hivyo mbele ya polisi makundi hayo mawili yanadaiwa yalianza kupigana mawe na kufanya Polisi walienda kusuluhisha kutimka na ugomvi huo kuibuka upya mapema leo na kusababisha maafa hayo makubwa.
Inaelezwa watu sita wanne wakiwa ni wakulima wameuwawa wengine wakichinjwa kama kuku na wawili wakiwa ni wafungaji na watu 35 wamejeruhiwa vibaya katika miili yao kwa silaha za jadi na kulazwa hospitali ya Bwagala huko huko Mvomero kwa sasa.
Jeshi la Polisi linaelezwa limefanikiwa kutuliza mapigano hayo, lakini watu waliojeruhiwa wakiwa hoi baadhi wakijeruhiwa vibaya na kulazimisha kufanyiwa upasuaji kunusuru maisha yao, ingawa mashuhuda wanasema huenda idadi ya vifo vilivyotokana na mapigano hayo vikaongezeka.

Yanga, Azam, Mbeya City nani kukaa kileleni kesho


Wageni Mbeya City kuweka rekodi kesho kwa Azam?

Mabingwa watetezi watamaliza vipi kesho kwa Oljoro?
PAZIA la duru la kwanza la Ligi Kuu Tanzania Bara linatarajiwa kufungwa rasmi kesho kwa mechi tatu, huku mechi mbili kati ya hizo zitakuwa zikitupiwa macho ili kujua ni timu hiyo kati ya zilizopo kwenye Tatu Bora, Azam, Mbeya City na mabingwa watetezi watakaomaliza kileleni kuuaga mwaka 2013?
Yanga itaikaribisha Oljoro JKT kutoka Arusha kwenye uwanja wa Taifa, huku Azam na Mbeya zilizopo juu ya Yanga zikiumana zenyewe kwa wenyewe katika pambano litakalochezwa kwenye uwanja wa Chamazi.
Vinara Azam watafanya nini kesho kwa Mbeya City?
Matokeo yoyote katika mechi hizo mbili yatatoa nafasi kwa timu hizo tatu moja wapo kukaa kileleni kutokana na kuwa na pointi zisizopishana sana.
Azam wanaongoza msimamo kwa tofauti na yamabo ya kufungwa na kufunga licha ya kulingana pointi na Mbeya City iliyoipanda daraja msimu huu zote zikiwa na pointi 26 kila moja, wakati Yanga wenyewe waliopo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 25.
Kutokana na hali hiyo iwapo Yanga itashinda na wapinzani wake kutoka sare watakalia kiti cha uongozi, lakini kama itashinda na Azam au Mbeya City ikashinda ina maana Yanga itashika nafasi ya pili na moja kati ya timu hizo mbili itaangukia katika nafasi ya tatu na nyingine kukalia kiti cha uongozi.
Tayari kumekuwa na tambo kwa timu za Azam na Mbeya City kuhusiana na pambano lao, lakini Yanga wenyewe wanaombea waendelee rekodi yao ya kutoa dozi kwa timu za maafande kwa kuikwanyua Oljoro JKT katika pambano lao huku wakiombea wapinzani wake kutoka sare.
Mechi nyingine kwa kesho itawakutanisha Rhino Rangers yua tabora itakayovaana na maafande wa Prisons ya Mbeya kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.
Je, ni Yanga, Azam au Mbeya City watauaga mwaka kileleni hadi mwaka 2014 au watauvuruga vipi msimamo wa ligi hiyo katika nafasi ya Tatu Bora? Tusubiri tuone hiyo kesho!

Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2013-2014    
                                  P    W     D     L      F     A    GD  PTS
01.Azam                    12   07    05    00   20    07    13   26
02.Mbeya City           12   07    05    00   16    07    09   26
03.Yanga                    12   07    04    01   28    11    17   25
04.Simba                    13   06    06    01   26   13     13   24
05.Kagera Sugar         13   05    05    03   14   09     05   20
06.Mtibwa Sugar         13   05    05    03   19   17     02   20
07.Ruvu Shooting        13   04    05    04   15   15     00   17
08.Coastal Union         13   03    07    03   10  07     03    16
09.JKT Ruvu               13   05    00    08   10  16    -06   15
10.Rhino Rangers        12   02    04    06   09  16     -05   10
11.Oljoro                    12   02    04    06   09  16     -07   10
12.Ashanti                  13   02    04    07   12   24    -12    10
13.Prisons                  12   01    05    06    05  15    -10    08
14.Mgambo               13   01    03    09    03  23    -20    06
 
Wafungaji:

10- Tambwe Amisi (Simba)
9- Elias Maguri (Ruvu Shooting)
8- Hamis Kiiza (Yanga), Juma Luizio (Mtibwa Sugar)
7- Kipre Tchetche (Azam)
6- Themi Felix (Kagera Sugar)
5- Tumba Sued (Ashanti Utd), Didier Kavumbagu, Mrisho Ngassa (Yanga)
4- Peter Michael (Prisons), Jerry Santo (Coastal Union), Jerry Tegete (Yanga), Betram Mombeki (Simba), Bakar Kondo (JKT Ruvu)
3- Haruna Chanongo, Jonas Mkude (Simba), Paul Nonga (Mbeya City), Salum Machaku (JKT Ruvu), Jerry Santo (Coastal Union),  Mcha Khamis (Azam), Amir Omary (Oljoro), Ramadhani Singano (Simba)
2- Haruna Moshi, Crispian Odulla (Coastal Union), Saady Kipanga (Rhino Rangers), Mwagani Yeya, Jeremiah John, Peter Mapunda,(Mbeya City), Godfrey Wambura (Kagera Sugar), Shaibu Nayopa (JKT Oljoro), Joseph Kimwaga (Azam), Shaaban Nditti, Shaaban Kisiga (Mtibwa Sugar), Said Dilunga (Ruvu Shooting)
1- Abdi Banda, Danny Lyanga (Coastal Union), Henry Joseph, Joseph Owino, Gilbert Kazze (Simba), Haruna Niyonzima, Nizar Khalfan, Simon Msuva, Frank Dumayo, Mbuyi Twitte, Oscar Joshua (Yanga), Iman Joel, Salum Majid, Mwalimu Musuku, Kamana Salum, Hussein Abdallah, Abbas Mohammed (Rhino Rangers), Gaudence Mwaikimba, Seif Abdallah,  Aggrey Morris,  John Bocco, Faridi Maliki, Hamphrey Mieno, Salum Abubakar, Erasto Nyoni (Azam), Steven Mazanda, Richard Peter, Deo Deus  (Mbeya City), Laurian Mpalile (Prisons-OG), Shaaban Susan, Jerome Lembeli, Cosmas Ader  (Ruvu Shooting), Masoud Ally, Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Shaaban Juma, Anthony Matangalu, Paul Maono(OG), Samir Luhava (OG), John Matei, Mwinyi Ally, Hussein Sued, Said Maulid (Ashanti Utd), Abdallah Bunu, Emmanuel Switta, Amos Mgisa (JKT Ruvu), Fully Maganga, Hamis Msafiri (Mgambo JKT), Seleman Kibuta, Daud Jumanne, Maregesi Marwa, Clement Douglas, Salum Kanoni (Kagera Sugar), Paul Malipesa, Expedito Kidulo, Nurdin Mohammed, Fikiri Mohammed (Oljoro JKT)

Matokeo yote ya mechi za Duru la KwanzaDURU LA KWANZA
Agosti 24, 2013
Yanga vs Ashanti United (5-1)
Mtibwa Sugar vs Azam (1-1)
Oljoro JKT vs Coastal Union (0-2)
Mgambo JKT vs JKT Ruvu (0-2)
Rhino Rangers vs Simba (2-2)
Mbeya City vs Kagera Sugar (0-0)
Ruvu Shooting vs Prisons (3-0)

Agosti 28, 2013
Mtibwa Sugar vs Kagera Sugar (1-0)
Rhino Rangers vs Azam (0-2)
JKT Ruvu  vs Prisons (3-0)
Mbeya City vs Ruvu Shooting (2-1)
Mgambo  vs Ashanti United (1-0)
Oljoro JKT vs Simba (0-1)
Yanga  vs Coastal Union (1-1)

Sept 14, 2013
Simba  vs Mtibwa (2-0)
Coastal Union  vs Prisons (0-0)
Ruvu Shooting va Mgambo JKT (1-0)
Oljoro JKT vs Rhino Rangers (1-1)
Mbeya City  vs Yanga (1-1)
Kagera Sugar vs Azam (1-1)
Ashanti United  vs JKT Ruvu (0-1)

Sept 18, 2013
Prisons vs Yanga (1-1)
Simba vs Mgambo JKT (6-0)
Kagera Sugar vs JKT Oljoro (2-1)
Azam  vs Ashanti United (1-1)
Coastal Union  vs Rhino Rangers (1-1)
Mtibwa Sugar  vs Mbeya City (0-0)
Ruvu Shooting vs  JKT Ruvu (1-0)

Sept 21, 2013
Mgambo JKT vs Rhino Rangers (1-1)
Prisons vs Mtibwa Sugar (1-1)
Simba vs Mbeya City (2-2)
Kagera Sugar vs Ashanti United (3-0)

Sept 22, 2013
JKT Ruvu vs Oljoro JKT (0-1)
Azam  vs Yanga (3-2)
Coastal Union v Ruvu Shooting (1-0)

Sept 25, 2013
Rhino Rangers vs Ashanti Utd (2-0)

Sept 28, 2013
Yanga vs Ruvu Shooting (1-0)
Rhino Rangers v Kagera Sugar (0-1)
Mbeya City vs Coastal Union (1-1)
Mgambo JKT vs Oljoro JKT (0-0)

Sept 29, 2013
Ashanti Utd vs Mtibwa Sugar (2-2)
JKT Ruvu vs Simba (0-2)
Prisons vs Azam (1-1)

Okt 05, 2013
Ruvu Shooting vs Simba (1-1)
JKT Ruvu vs Kagera Sugar (2-1)
Coastal Union vs Azam (0-0)
Oljoro JKT vs Mbeya City (1-2)

Okt 06, 2013
Mgambo JKT vs Prisons (0-1)
Yanga vs Mtibwa Sugar (2-0)

Okt 09, 2013
Rhino Rangers vs Mbeya City (1-3 )
Oljoro JKT vs Ruvu Shooting (2-2)
Azam vs Mgambo JKT (2-0)
Mtibwa Sugar vs JKT Ruvu (2-1)

Okt 12, 2013
Kagera Sugar vs Yanga (1-2)
Simba vs Prisons (1-0)
Ashanti Utd  vs  Coastal Union (2-1)

Okt 13, 2013
Ruvu Shooting vs Rhino Rangers (1-0)
Mgambo JKT vs Mbeya City (0-1)
Azam vs JKT Ruvu (3-0)
Mtibwa Sugar vs Oljoro JKT (5-2)

Okt 16, 2013
Ashanti Utd vs Prisons (2-1)

Okt 19, 2013
Kagera Sugar vs Coastal Union (1-0)
Oljoro JKT vs Azam (0-1)
Mtibwa Sugar vs Mgambo JKT (4-1)
Mbeya City vs JKT Ruvu (1-0)
Ashanti Utd vs Ruvu Shooting (2-2)

Okt 20, 2013
Simba vs Yanga (3-3)

Okt 23, 2013
Coastal Union vs Simba (0-0)
Prisons vs Kagera Sugar (0-0)
Yanga vs Rhino Rangers (3-0)

Okt 28, 2013
Simba vs Azam (1-2)
Ruvu Shooting vs Kagera Sugar (1-1)
Coastal Union vs Mtibwa Sugar (3-0)
Oljoro JKT vs Ashanti Utd (0-0)

Okt 29, 2013
Prisons vs Mbeya City (0-2)
Rhino Rangers vs JKT Ruvu (1-0)
Yanga vs Mgambo JKT (3-0)

Okt 31, 2013
Simba vs Kagera Sugar (1-1)

Nov 1, 2013
JKT Ruvu vs Yanga (0-4)

Nov 2, 2013
Mgambo JKT vs Coastal Union (0-0)
Azam vs Ruvu Shooting (3-0)
Mtibwa Sugar vs Rhino Rangers (1-0)
Mbeya City vs Ashanti Utd (1-0)

Nov 3, 2013
Prisons vs Oljoro JKT (0-1)

Nov 06, 2013
JKT Ruvu vs Coastal Union (1-0)
Ashanti Utd vs Simba (2-4)
Ruvu Shooting vs Mtibwa Sugar(2-2)
Kagera Sugar vs Mgambo JKT (2-0)

Nov 07, 2013
Azam vs Mbeya City (-)
Rhino Rangers vs Prisons (-)
Yanga vs Oljoro JKT (-)

Elias Maguri, Juma Luizio wazidi kukifukizia kiatu cha dhahabu Mtibwa, Ruvu zikitoka sare Mabatini


Juma Luizio 'Ndanda'
MABAO mawili ya mshambuliaji nyota wa Ruvu Shooting, Elias Maguri yaliyoisaidia timu yake kupata sare ya 2-2 na Mtibwa Suigar yamefanya mbio za kuwania kiatu cha dhahabu kuzidi kuwa ngumu baada ya mchezaji huyo kufikisha bao la tisa na kumjongelea Amissi Tambwe wa Simba anayeongoza orodha hiyo.
Maguri amefunga mabao hayo katika pambano la timu yake kufungia duru la kwanza kwenye uwanja wa Mabatini, Mlandizi na kuonyesha dhamira yake ya kunyakua kiatu hicho cha dhahabu ambacho msimu uliopita kilichukuliwa na 'Pro' Kipre Tchetche.
Mabao ya wapinzani wao yaliwekwa kimiani na mshambuliaji anayezidi kuja juu nchini, Juma Luizio'Ndanda' ambaye alifikisha bao lake la nane msimu huu na kumfikia Hamis Kiiza huku akibakisha mawili kumkamata Tambwe.
Bao jingine la Mtibwa liliwekwa kimiani na kiungo mzoefu nchini, Shaaban Kisiga 'Marlon' na kuifanya timu yao ya Mtibwa kupata pointi moja na kufikisha pointi 20 na kushika nafasi ya sita ikiipisha Kagera kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

JKT Ruvu wazinduka waikwanyua Coastal, Kagera yaua 2-0

JKT Ruvu iliyozinduka leo Chamazi

Kagera iliyoikwanyua Mgmabo mabao 2-0
BAADA ya kupokea vipigo mfululizo maafande wa JKT Ruvu leo wamezinduka kwenye uwanja wa Chamazi, jijini Dar es Salaam baada ya kukwanyua Coastal Union kwa bao 1-0, huku Kagera Sugar wakiishikisha adabu MKatika pambano la Chamazi, bao pekee la maafande hao linalowafanya wafikishe pointi 15 liliwekwa kimiani na Bakar Kondo.
Nako Kaitaba mabao mawili ya Themi Felix na Seleman Kibuta yalitosha kuizima Mgambo JKT iliyosafiri hadi mjini Bukoba baada ya kuwanyuka mabao 2-0 katika pambano jingine la Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kwa matokeo hayo Kagera imefikisha pointi 20 huku JKT Ruvu ikifikiosha pointi 15 na kusalia kwenye nafasi ya tisa katika msimamo  wa ligi hiyo. Huku bao la Themi anayewania Tuzo ya Mwanasoka Bora inayoendeshwa na gazeti la MWANASPOTI imemfanya afike jumla ya mabao sita, huku Bakar Kondo akifika bao lake la nne katika orodha ya wafungaji inayoongoza na Amissi Tambwe wa Simba mwenye mabao 10 na kufuatiwa na Elias Maguri wa ruvu Shooting kisha Hamis Kiiza 'Diego' mwenye mabao nane akiwa na nafasi ya kuongeza idadi kwa vile timu yake ya Yanga itashuka kesho dimbani kuvaana na Oljoro JKT.

MAKAMBA MGENI RASMI TUZO ZA MWANASOKA BORA


NAIBU Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, Mh. January Makamba anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji wa tuzo kwa mwana soka bora wa mwaka katika ligi kuu ya Vodacom mwaka 2013, itakayofanyika katika ukumbi wa  Mlimani City jijini Dar es Salaam.
 
Tuzo hiyo itashuhudia wachezaji walioingia hatua ya Tano bora, AMRI KIEMBA, HARUNA NIYONZIMA, SHOMARI KAPOMBE, THEMI FELIX, na KELVIN YONDANI wakichuana kuwania umwamba wa soka Tanzania,  Baada ya kupigiwa kura na mashabiki na Kamati maalum chini ya Mwenyekiti wake Zamoyoni Mogela kuchambua majina hayo kulingana na kura walizopata.
 
Akizungumza juu ya hafla hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano Kelvin Twissa amesema, wanafurahi kuwa sehemu ya  maendeleo ya soka nchini na siku zote kampuni yake imekuwa msitari wa mbele katika kuunga mkono michezo nchini, hususani mchezo wa soka na kuhakikisha unakuwa moja ya ajira muhimu kwa watanzania.
 
“Vodacom tumeendelea kuwa wadau muhimu katika mapinduzi ya soka la Tanzania, sasa mpira umekuwa zaidi ya burudani kwa watanzania kutokana na chachu ambayo tumeiweka tangu tuanze kudhamini ligi kuu, ambayo sasa imekuwa na ushindani mkubwa na thamani yake inazididi kupanda siku hadi siku,” alisema Twissa.
 
Aidha Twissa amesema kampuni yake itaendelea kushirikiana na wadau wengine wote wanaopenda maendeleo ya soka bila kusita kutokana na namna ambavyo kampuni yake imejidhatiti katika kuinua michezo nchini.
 
“Mafanikio yanayopatikana katika soka letu sasa hayajapatikana hivivi ni kutokana na dhamira tuliyoiweka katika kuinua mchezo huu wa soka na uwekezaji mkubwa tulioufanya hadi sasa, watu ambao wanaleta mafanikio haya ni wachezaji ambao wamekuwa wanapambana kufa na kupona kutoa burudani kwa Watanzania, Ni lazima tuwaenzi wachezaji hawa kwa njia tofauti tofauti,” alisema Twissa.
 
Kwa upande wake Meneja Masoko wa MCL Bernad Mukasa amesema kuwa, wamefurahi kushirikiana na Naibu waziri Mh. Makamba katika utoaji wa tuzo hizi, ambazo zinatambua mchango wa wanasoka nchini.
 
“Tuzo hizi zinatambulika rasmi kwa jina la zitaitwa MWANASPOTI BORA WA SOKA WA VODACOM 2013. Ni za kipekee na za kwanza kabisa nchini kwa wigo wa wachezaji wanaohusishwa, ushirikishwaji wa uteuzi wa mshindi, na vigezo husika.” alisema Mukasa na kuongeza.
 
“Kwa mwaka huu, licha ya kumpata Mwanaspoti Bora wa soka wa mwaka , pia tutatoa Tuzo kwa “categories” zaidi ya 10 ikiwemo kocha bora, mwamuzi bora, mchezaji bora wa kike, mchezaji bora chipukizi, “1st eleven”, goli bora, mchezaji bora wa kigeni, Mchezi bora wa kulipwa anayecheza nje, na Kipengele kingine kitajulikana siku ya ijumaa,” alisema Mukasa.
 
Mukasa alihitimisha kwa kutoa wito kwa Watanzania kuendelea kuwapigia kura wachezaji hao  kwa  kuandika ujumbe mfupi unaoanza na neno KURA kisha jina la mchezaji anayemchagua kati ya hao waliotajwa na kisha kutuma kwenda namba 15678.

Simba yamaliza hasira zake kwa Ashanti, Tambwe, Mombeki nouma

Mombeki akitafuta njia ya kumtoka beki wa Ashanti huku, Haruna Shamte akiwa tayari kwa msaada (picha: Lenzi ya Michezo)

KAMA walivyoanza ndivyo walivyomaliza duru la kwanza, Ashanti United 'Wana wa Jiji' wameshindwa kuhimili hasira za 'mnyama' baada ya jioni hii kukubali kipigo cha aibu cha mabao 4-2 kutoka kwa Simba.
Ashanti Utd iliyorejea Ligi Kuu msimu huu, ilikumbana na kipigo hicho kwenye uwanja wa Taifa ikiwa ni miezi karibu mitatu tangu walipolala kwa mabao 5-1 na Yanga katika mechi ya kufunga dimba la ligi hiyo.
Mabao mawili ya Betram Mombeki na mengine ya Ramadhani Singano 'Messi' na Amissi Tambwe yalitosha kuiangamiza Ashanti Utd ambayo kabla ya pambano hilo waliapa kutoa kisago kwa wapinzani wao hao.
Messi, ndiye aliyeanza kufungua karamu ya mabao ya Simba katika dakika ya 8 kabla ya Ashanti kusawazisha kwenye dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza kupitia kwa Hussein Sued.
Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kucharuka kwa kupata mabao ya harakaharaka kupitia Tambwe aliyefunga dakika ya kwanza tu ya kipindi hicho na kufikisha jumla ya mabao 10 katika orodha ya ufungaji bora.
Dakika ya nne baadaye Mombeki alifunga bao la tatu kabla ya kuongeza jingine dakika ya 15, wakati huo Ashanti ikiwa imerejesha bao jingine na la pili kwao kupitia mkongwe Said Maulid 'SMG' aliyevurumusha kombora lililomshinda kipa Abuu Hashim.

Kwa matokeo hayo Simba imefikisha jumla ya pointi 24 na kumaliza mechi zake za duru la kwanza, Ashanti ikisaliwa na pointi 10, huku pia ikijikuta ikimaliza pambano hilo bila kipa wake, Amani Simba kuwepo uwanjani kwa kulimwa kadi nyekundu na mwamuzi Andrew Shamba.
Kipa huyo alipewa kadi hiyo baada ya kuudaka mpira nje ya eneo lake akizuia kupigwa kanzu na nyota wa mchezo wa leo, Ramadhani Singano Messi.

NEWZ ALERT: MFANYAKAZI TBC APIGWA RISASI NA KUFARIKI

No comments

MFANYAKAZI  wa Shirika la Utangazaji Nchini  TBC, pichani, RAMADHAN GIZE ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaosaidiwa kuwa ni majambazi usiku wa kuamkia leo katika eneo la UBUNGO Maziwa Jijini DSM.

Tukio hilo limetokea baada ya watu hao kuvamia duka moja katika eneo hilo la UBUNGO MAZIWA kwa lengo la kupora, ambapo mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la MWARAMI RAJABU amejeruhiwa na watu hao wanasadikiwa kuwa ni majambazi.
Chanzo:MICHUZI

Msiba! DJ RANKEEM RAMADHANI HATUNAYE DUNIANI


KWA mujibu wa taarifa zilizopatikana jioni ya leo, zinaeleza kuwa mmoja wa Ma Dj Maarufu sana hapa jijini Dar na Tanzania kwa ujumla ,Dj Rankeem Ramadhani amefariki mchana huu.
Inaelezwa kuwa DJ Rankeem aliyewahi kufanya kazi Radio One Stereo na vituo vingine mbalimbali alifariki kwenye hospitali ya Mwananyamala baada ya kufanyiwa upasuaji kutokana na tatizo la kidole utumbo.
Mwili wa mkali huyo katika kupangilia muziki aliyetingisha kwa miaka kadhaa, umehifadhiwa kwenye hospitalini hiyo ikifanywa mipango ya mazishi yake.
Taarifa zaidi juu ya msiba huu zitaletwa kwenu kadri tukavyopata kwa undani zaidi ikiwemo kujua atazikwa lini na wapi, ingawa inaelezwa huenda akazikwa kesho jijini Dar es Salaam.
MICHARAZO inatoa pole kwa familia, ndugu jamaa na wadau wote wa habari na muziki kwa msiba wa gwiji hilo, na kuwataka kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu kwa kukumbuka kuwa Sote tu wa Allah (SW) na Kwake Tutarejea.
Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi-AMEN

Manchester City yaweka rekodi Ulaya, Juve, Man Utd wabanwa

Aguero akishangulia moja ya mabao yake ya jana kwa CSKA
Bale akiwatungua Juve walipopata sare ya 2-2
 KLABU ya Manchester City kwa mara ya kwanza katika michuano uya Ligi ya Mabingwa Ulaya imevuka salama hatua ya makundi na kuweka rekodi kwao baada ya kuwadungua 'wabaguzi wa rangi' CSKA ya Urusi kwa mabao 5-2 katika pambano kali ya michuano hiyo ya Ulaya.
Mabao mawili ya Sergio 'kun' Aguero na hat trick ya Alvaro Negredo yalitosha kuwavusha wakali hao wa EPL mbele ya Warusi hao.
Bapa la kwanza la Aguero lilitokana na mkwaju wa penati baada ya David Silva kuchezwa vibaya kisha kuongeza jingine kabla ya Negredo kufunga mabao mengine, huku yale ya wageni yote mawili yakifungwa na Doumbia.
Katika mechi nyingine za kundi hilo, Mabingwa watetezi Bayern Munich ilipata ushindi kiduchu wa bao 1-0 na kuendeleza rekodi ya kushindwa kwa asilimia 100 mbele ya Victoria, Juventus ya Italia ikiwa nyumbani ilijitutumua na kuibana Real Madrid na kutoka nao sare ya 2-2, japo walishindwa kuwazuia Cristiano Ronaldo na Bgareth Bale kuwatungua kwani wote wawili walifunga mabao ya wahispania hao.
Manchester United ikiwa ugenini ililazimishwa suluhu na Real Sociedad, huku Shakhtar Doneksk na Bayer Leverkusen nao wakitoka suluhu na mabinhwa wa Ufaransa PSG na Anderletch zikitoka pia sare ya 1-1.
Benfica ikiwa ugenini ililala kwa bao 1-0 kwa Olympiakos na Galatasaray ilikubali kichapo cha ugenini cha bao 1-0 toka kwa Kobenhavn.
Ligi hiyo itaendeela tena usiku wa leo kwa michezo minane baadhi ikiwakutanisha Arsenal itakayokuwa ugenini dhidi ya Borussia Dotmund, Barcelona dhidi ya Ac Milan na Ajax itaikaribisha Celtic.
Mechi nyingine ni kati ya Chelsea dhidi ya Schalke 04, Napoli watakaoumana na Olympique Marseille, Zenit na Porto na Atletico Madrid itakayoumana na Viena.