STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, July 4, 2014

Coastal Union yazidi kuzoa nyota wapya

 

Aliyekuwa beki wa kulia wa timu ya Rhino Rangers ya Tabora, Amani Juma kulia akisaini mkataba wa kipindi cha miaka miwili kuitumika timu hiyo katika msimu mpya wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara kushoto ni katibu
Mkuu wa Coastal Union Kassim El Siagi.???????????????????????????????Aliyekuwa beki wa kati wa timu ya Mgambo Shooting ya Tanga,Bakari Mtama akisaini mkataba wa kuijunga na timu ya Coastal Union ya Tanga jana wanaoshuhudia katikati ni Makamu Mwenyekiti wa Coastal Union, Steven Mguto wa kwanza kulia ni Katibu wa Coastal Union,Kassim El Siagi na wa pili kushoto ni mjumbe wa kamati ya usajili wa klabu hiyo, Salim Amiri.
???????????????????????????????Mshambuliaji Mpya wa timu ya Coastal Union,Husein Sued akisaini mkataba wa mwaka mmoja wa kujiunga na timu hiyo yenye makazi yake barabara ya kumi na moja jijini wanashuhudia katikati ni Katibu wa Coastal Union,Kassim El Siagi na wa kwanza kulia ni Meneja wa timu hiyo, Akida Machai.

NA OSCAR ASSENGA,TANGA.
BEKI wa Kulia wa timu ya Coastal Union,Amani Juma amesema atahakikisha
anashirikiana na wenzake ili kuweza kuipa mafanikio timu hiyo katika
michuano ya Ligi kuu Tanzania bara lengo likiwa kuiwezesha kuchukua
kombe hilo na kuweza kushiriki mashindano makubwa.

Juma ambaye alisajiliwa na Coastal Union kwa mkataba wa miaka miwili
alisema ni wajibu wake kujituma na kupambana vilivyo kuiwezesha timuhiyo kufikia malengo yao waliojiwekea msimu ujao ya kumaliza ligi hiyo
 wakiwa mabingwa.
Alisema katika kutimiza suala hilo wachezaji waliosajiliwa na timu hiyo hawana budi kushikamana na kuwa kitu kimoja kwa kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mechi zao za nyumbani na ugenini wakati ligi
 hiyo itakapoanza.

Aidha aliwashukuru viongozi wa klabu hiyo kwa kuthamini mchango wake
kwa kumpa ridhaa ya kuichezea timu hiyo katika kipindi hicho na kuahidi kupambana kufa na kupona kwa ajili ya kufikia mafanikio
 yatokanayo na soka hilo.

Katika hatua nyingine wachezaji wote waliosajiliwa na timu hiyo
 wanatakiwa kuwasili mkoani Tanga Kesho(leo) kwa ajili ya kuanza
 maandalizi ya kuelekea msimu mpya bila kukosa kwani watakaochelewa kuwasili watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Barcelona wamruhusu Xavi kuhama

KLABU ya Barcelona kupitia Rais wake, Josep Maria Bartomeu imesema ipo tayari kumsaidia Xavi Hernandez kuondoka kama atataka kuihama klabu hiyo.
Nyota huyo wa timu ya taifa ya Hispania amekuwa gwiji tangu alipoanza kuichezea klabu hiyo mwaka 1998, lakini veterani huyo mwenye umri wa miaka 34 alijikuta akikosa nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza chini ya kocha Gerardo Martino msimu uliopita.
Aliachwa pia nje ya kikosi cha kwanza kilichocheza mechi ya kuamua bingwa wa La Liga dhidi ya Atletico Madrid, ambayo kama Wacatalunya hao wangeshinda wangetwaa ubingwa.
Tangu wakati huo amehusishwa na klabu kadhaa, ikiwamo ya Al-Arabi ya Qatar, na bosi huyo wa Barca amemfungulia milango ya kuondoka Camp Nou.
"Amedumu katika kikosi cha kwanza kwa miaka mingi na anayo haki ya kuamua (kubaki ama kuondoka). Tutaheshimu maamuzi yake," Bartomeu alisema.
"Siku atakayoondoka, ataacha historia kama mchezaji bora kuliko wote waliopitia (Barcelona). Kama anataka kubaki nasi, tutafurahi, kama anataka kuondoka tutamsaiddia.
"Xavi atarejea hapa kwasababu atakuwa kucha mkubwa," aliongeza.
Barca ilimtambulisha kiungo mpya Ivan Rakitic Jumanne waliyemsajili kwa euro milioni 20 kutoka Sevilla.

Algeria waoinyesha mfano wa kuigwa

KATIKA mafundisho ya Qur'an na Hadithi za Mtume Muhammad (SAW) inasema Muislam ndugu na Uhurumiana wenyewe kwa wenyewe.
Hiyo imethibitishwa na timu iliyoonyesha soka la kusisimua nchini Brazil, Algeria iliyong'oka kishujaa mbele ya Ujerumani.
Mshambuliaji nyota wa timu ya taifa ya Algeria Islam Slimani aliyepo kwenye orodha ya wafungaji bora akiwa na mabao mawili amebainisha kuwa kikosi kizima cha nchi hiyo kinatarajiwa kutoa msaada wa posho zao kwa watu wa Gaza. 
Timu ilirejea nyumbani wakiwa mashujaa na wachezaji wameamua kutoa posho zao kwa wale ambao wanazihitaji zaidi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa miongoni mwa Ibada ndani ya Uislam.
Hatua hiyo ya Algeria imekuja huku wawakilishi wengine wa Afrika katika michuano hiyo kama Ghana, Nigeria na Cameroon kukumbwa na msuguano katika kambi zao kutokana na posho hatua iliyochangia kwa kiasi kikubwa kuenguliwa mapema.
Algeria ni nchi ya Kiislam iliyopo Kaskazini mwa Afrika na inaelezwa kufungwa kwa mabao 2-1 katika hatua ya lala salama na Ujerumani ilitokana na swaumu.

Ujerumani, Ufaransa hapatoshi leo Brazil

* Wenyeji Brazil na Colombia kumaliza udhia

* Neymar shakani, akiwaonya majirani zao

Wenyeji Brazil

Wakali wa Colombia
UTAMU wa Fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea nchini Brazil unatarajiwa kuanza kunoga leo wakati michezo ya Robo Fainali itakapochezwa kwa timu wenyeji Brazil kuvaana na majirani zao Colombia, huku mabingwa wa zamani Ujerumani na Ufaransa wakikumbushia nusu fainali ya mwaka 1982 nchini Hispania.
Ujerumani walionyakua taji hilo la Dunia mara tatu itawavaa mabingwa hao wa mwaka 1998 katika mechi ya kwanza ya hatua hiyo kwenye uwanja wa Maracana, kuanzia saa 1 usiku kwa saa za Afrika Mashariki huku kila timu ikitambia nyota wake na kuwa na kiu ya kusonga mbele katika nusu fainali.
Ni mechi ambayo haraka inaleta kumbukumbu ya mwaka za mechi ya nusu fainali ya Kombe la Dunia baina ya timu hizo mwaka 1982, pale Ujerumani iliposhinda kwa "matuta" baada ya sare ya 3-3  inayokumbukwa kwa rafu mbaya ya Harold Schumacher dhidi ya mshambuliaji wa Ufaransa, Patrick Battiston.
Ujerumani watakuwa wakicheza robo fainali yao ya tisa mfululizo ya Kombe la Dunia, lakini kikosi cha Joachim Low kimeshindwa kuonyesha ubora nchini Brazil tangu kiliposhinda 4-0 dhidi ya Ureno katika mechi ya ufunguzi.
Katika mechi yao iliyopita, walishinda kwa shida 2-1 dhidi ya Algeria katika muda wa nyongeza na kuzua mijadala mizito nyumbani kwao kuhusu kiwango cha timu hiyo, mbinu na staili ya uchezaji.
Moja ya mijadala ni kwa kocha Low anapojadili kikosi chake kwamba amchezeshe Philipp Lahm kama kingo ama beki wa kulia. Mijadala mingine ni kiwango cha chini cha wachezaji kama Mesut Ozil na Mario Gotze.
Wajerumani watapata nguvu kwa kurejea kikosini kwa beki Mats Hummels baada ya kuikosa mechi dhidi ya Algeria kutokana na kuwa mgonjwa kambini, lakini Shkodran Mustafi ameaga mashindano hayo kutokana na maumivu ya misuli ya nyuma ya paja.
Katika ushambuliaji, Andre Schurrle anatarajiwa kuanza baada ya kufunga goli akitokea benchini dhidi ya Algeria, wakati Thomas Muller ataongoza mashambulizi, jambo linalomaanisha kwamba Miroslav Klose atalazimika kuanzia benchi kama atahitaji kuvunja rekodi ya dunia ya kufunga magoli mengi zaidi.
Wakati Ujerumani wanaonekana kuwa na uchovu baada ya ratiba ngumu kaskazini, Ufaransa wanakuja kwenye mechi wakiwa na nguvu zaidibaada ya kuifunga Nigeria 2-0 katika raundi iliyopita.
Ufaransa hawakuwa katika kiwango cha kutisha katika hatua ya 16-Bora lakini wamecheza soka zuri mara moja moja katika michuano hiyo, huku kocha Didier Deschamps akiwatumia washambuliaji wake kiwerevu.
Uwanja ni wake Paul Pogba kuonyesha kwanini anatajwa kama mmoja wa viungo bora zaidi duniani akiwa na umri wa miaka 21 tu. Nyota huyo wa Juventus amekuwa na kiwango kinachopanda na kushuka katika fainali zake hizi za kwanza za Kombe la Dunia lakini tayari ameonyesha ishara za uwezo wake wa kuwa mchezaji mshindi kwa kufunga goli la kwanza dhidi ya Nigeria.
Bila shaka mechi hiyoya mapema itakuwa ni 'tamu' kuliko inavyotarajiwa kutokana na kuwepo kwa mchuano wa kimya kimya wa ufungaji baina ya Karim Benzema wa Ufaransa dhidi ya Thomas Muiller ambao wanatofautiana kwa bao moja, Muiller akiwa na manne sawa na Neymar na Messi, huku Benzema akiwa na matatu akilingana na Arjen Robben, Robin van Persie wa Uholanzi, Enner Valencia wa Ecuador na Xherdan Shaqiri wa Uswisi.
Katika mechi itakayopigwa baadaye saa tano usiku, wenyeji Brazil ambayo awali kulikuwa na hofu ya kukosa huduma za nyota wao Neymar aliyekuwa akisumbuliwa na maumivu ya misuli, itashuka dimbani kuwakabili Colombia waliopo kwenye kiwango cha hali juu katika fainali hizo.
Colombia iliyoshinda mechi zake zote za makundi kwa asilimia 100 na kuing'oa Uruguay kwa mabao 2-0 katika muda wa kawaida, itawakabili wenyeji wakiwa wanafahamu wapo nyumbani na wakipewa sapoti na maelfu ya mashabiki vichaa wa soka wa taifa hilo lenye watu wanaokadiriwa Miliioni 200.
Wakimtegemea nyota wao mpya anayeongoza kwenye safu ya Ufungaji Bora wa Fainali hizo za Brazil, James Rodriguez, Colombia bila shaka itakuwa na kiu kubwa ya kutinga hatua hiyo ya Nusu fainali ili kuzidi kuboresha reklodi yao baada ya kipindi cha muda mrefu. Kwani haikuwahi kutinga hatua ya Riobo Fainali waliyopo sasa wala kunusa Nusu Fainali tangu ianze kushiriki michuano hiyo.
Hatua kubwa kwake ni kutinga 16 Bora katika fainali za mwaka 1990 zilipofanyika nchini Italia, na mara zote ilikuwa ikikwamia katika hatua ya makundi na kwa kasi waliyoonyesha msimu huu ni wazi Brazil inapaswa kujichunga la sivyo watashuhudia wakibaki kuwashangilia wageni na wao kuwa watazamaji.
Rodriguez aliyefunga mabao matano na kufunika kabisa pengo lililokuwa likitarajiwa kuiathiri nchini baada ya Radamel Falcao kuumia na kuondolewa kikosini, anatazamwa kama tumaini ya Colombia kuweka historia kubwa zaidi kwa nchi hiyo ambayo pia ina wakali kadha wanaotamba duniani kama Jackson Martinez, Adrian Ramos na kipa mkongwe aliyeweka rekodi mpya ya kuwa mchezaji mzee kucheza Fainali za Kombe la Dunia akimpiku Mcameroon, Roger Milla. Faryd Mondragon mwenye miaka 43.
Hata hivyo Brazil siyo rahisi kwao kukubali kufanywa daraja na majirani zao hao katika mchezo huo na nyota wake Neymar amenukuliwa kujiandaa kumfunika Rodriguez na Colombia kwa ujumla.
Neymar alisema Brazil imedhamiria kutinga nusu fainali ya Kombe la Dunia kwa ushindi dhidi ya Colombia mjini Fortaleza, licha ya kumsifu  James kwa kiwango chake katika michuano hiyo akimtaja kama 'Mchezaji Mkubwa', ila akisistiza kuwa yeye na wachezaji wenzake watahitimisha safari nzuri ya wapinzani wao hao katika michuano hiyo leo.
"Colombia ni timu nzuri, wamekuwa wakishinda sana, wameonyesha wana nguvu wakati wa mechi zao. James ni bonge lamchezaji: yeye ni nyota, ingawa ni mdogo sana, miaka 22 kama mimi. Amekuwa akionyesha namna alivyo mchezaji mkubwa na tunapaswa kumpongeza kwa kila anachokifanya.
"Lakini natumai safari yake katika Kombe la Dunia hili imefikia tamati sasa na Brazil iendelee – kwa heshima yote, hakika."
Mbali na Neymar, Brazil pia inatambia nyota kama Fred, Davud Luis, Oscar, na kipa aliyegeuzwa 'Mungu' kwa sasa akiabudiwa kwa kuivusha timu yao hatua hiyi kwa kudaka penati mbili za Chile, Julio Cesar.
Je ni Ujerumani au Ufaransa zitakazotangulia Nusu fainali ma vipi wenyeji Brazil watatibua rekodi ya Colombia ya kushinda mechi kwa asilimia 100? Tusubiri kuona hiyo usiku.

Wambura wenzake wapigwa 'stop' Simba

UONGOZI wa klabu ya soka ya Simba umetangaza rasmi kumsimamisha uanachama aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Urais katika uchaguzi uliofanyika Jumapili, Michael Wambura, pamoja na wengine 70 kutokana na kwenda kufungua kesi kwenye mahakama za kawaida za nchi, imeelezwa jijini Dar es Salaam jana.
Akizungumza kwenye makao makuu ya klabu hiyo yaliyoko mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini jana, Rais wa Simba, Evans Aveva, alisema kuwa maamuzi ya kumsimamisha Wambura na wenzake yametolewa na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambao walikutana kwa mara ya kwanza juzi.
Aveva alisema kuwa kamati hiyo imechukua maamuzi ya kuwasimamisha kwa kufuata ibara ya 11 (1) (b) ya katiba ya Simba na kuongeza kuwa hatma yao itajulikana katika Mkutano Mkuu wa mwaka wa klabu unaotarajiwa kufanyika Agosti 3.
Rais huyo alisema kuwa wameamua kuchukua hatua hiyo ili kuilinda katiba ya Simba na uanachama wa klabu hiyo katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
"Suala la Wambura lilijadiliwa lakini hatukufikia mwafaka na kuamua lipelekwe katika mkutano mkuu ili wanachama waamue, tumewasimamisha wale 69 na katika kesi ya mwaka 2010 aliyofungua Wambura alishirikiana na Juma Mtemi, naye tumemsimamisha," alieleza Aveva.
Alisema kuwa katika mkutano mkuu unaokuja wanachama watajadili pia ripoti ya fedha na mabadiliko ya katiba ambayo yameonekana kuwa na mapungufu.
Kiongozi huyo pia aliwashukuru wanachama wote wa Simba waliompigia na wasiompigia kura kwa sababu kila mmoja ametekeleza haki yake ya kidemokrasia.
Alisema uchaguzi umekwisha sasa wanachama wote ni kitu kimoja waungane kuijenga klabu yao.
"Sasa tuungane kutekeleza ahadi zetu ambazo ni pointi tatu uwanjani, umoja na maendeleo, tusahau tofauti zetu, Simba ni muhimu kuliko sisi sote," alisema kiongozi huyo.

WACHEZAJI KULIPWA LEO
Aveva alisema kuwa uongozi wake unatarajia leo kuwalipa mishahara wachezaji wake ili kuwaweka tayari kwa ajili ya kuanza maandalizi ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Alisema kuwa kikosi cha timu hiyo kitaanza mazoezi yake Jumatano Julai 9 huku pia wakianza maandalizi ya tamasha la Simba Day litakalofanyika Agosti 8 mwaka huu.
Alisema kwamba kocha mkuu wa timu hiyo, Mcroatia, Zdravko Logarusic, atarejea nchini Jumatatu na taratibu za kumtumia tiketi ya ndege zimeshaanza.

WAJUME WAPYA, KAMATI MPYA
Aveva aliwataja wajumbe watatu wapya wa kuteuliwa watakaoingia katika Kamati ya Utendaji kuwa ni Mohammed Nassor, Musley Al Ruwey na Salim Abdallah huku wengine wawili waliobaki kwa mujibu wa matakwa ya katiba atawatangaza baadaye.
Uongozi huo mpya pia jana ulitangaza kamati tatu zitakazosimamia shughuli mbalimbali za kila siku lakini akisema Kamati ya Usajili itakuwa ni ya muda na itaongozwa na Hanspoppe Zacharia, Kassim Dewji, Saidi Tulliy, Musley Al Ruweh, Crescentius Magori na Rodney Chiduo.
Aliwataja wajumbe wanaounda kamati ya mashindano itakayokuwa chini ya mwenyekiti, Mohammed Nassor, kuwa ni Iddi Kajuna, Jerry Yambi, Hussein Simba na Mohammed Omary.
Mwenyekiti wa Kamati ya Vijana ni Tulliy, Ally Suru, ambao wote ni wajumbe wa Kamati ya Utendaji, Patrick Rweyemamu, Mulamu Nghambi, Madaraka Suleiman na Amina Poyo.

NIPASHE

CHUJI ATUA AZAM, MCAMEOON AMKUBALI

BAADA ya kutangazwa kuachwa na Yanga, kiungo nyota wa zamani wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Athumani Iddi ‘Chuji’ amedaiwa kusajiliwa na mabingwa wa kandanda nchini, Azam kwa mkataba wa muda mfupi na tayari ameanza kujifua mazoezini na wenzake.
Hata hivyo bado uongozi wa Azam haujathibitisha taarifa hizo, ingawa kocha wa Azam Mcameroon amenukuliwa akimwagia sifa Chuji kwa jinsi alivyoshuhudia vitu vyake kwenye mazoezi ya timu hiyo yanayoendelea Chamazi, Dar es Salaam.
Kocha huyo alisema ameridhika na kiwango cha Chuji na kutokana na uzoefu alionao ataisaidia Azam katika msimu ujao na mashindano ya kimataifa watakayoshiriki.
Hata hivyo viongozi wa Azama wamekuwa wagumu kutjhibitisha taarifa hizo kwa madai mwenye maamuzi ya mwisho juu ya Chuji ni kocha ambaye ni wazi ameridhia mkali huyo aliyewahi kuichezea Simba na Polisi Dodioma kuitumikia timu hiyo msimu ujao na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Thursday, July 3, 2014

Suarez azigonganisha Liverpool, Barcelona

MSHAMBULIAJI nyota wa Uruguay aliyefungiwa na FIFA kwa kitendo cha kumng'ata beki wa Italia, Giorgio Chiellini, Luis Suarez amezigoinganisha klabu yake ya Liverpool na Barcelona inayowania saini yake.
Klabu hizo zinatarajia kuanza kufanya mazungumzo juu ya bei ya awali ya paundi milioni 80 ili kuuziana mshambuliaji  huyo.
Mtandao wa michezo wa Sportsmail unafahamu kuwa maofisa wa Liverpool, akiwemo mkurugenzi mtendaji, Ian Ayre, wamekubali kukutana na mkurugenzi wa michezo wa FC Barcelona, Raul Sanllehi,  mjini London ili kujadiliana thamani ya mchezaji huyo mwenye miaka 27.
Barcelona wanatazamiwa kutoa paundi milioni 60 kwa kuzingatia kuwa Suarez amefungiwa miezi minne kucheza soka baada ya kumng`ata beki wa Italia, Giorgio Chiellini.
Liverpool hawapo tayari kushusha bei ya Suarez, lakini wanataka kumhusisha mshambuliaji wa Barcelona Alexis Sanchez kama sehemu ya makubaliano hayo.
Barcelona wanasema mchezaji wao wa kimataifa wa Chile ana thamani ya paundi milioni 35, lakini tayari wameshakataa ofa ya paundi milioni 20 kutoka kwa Juventus ya Italia iliyokuwa na nia ya kumsajili nyota huyo mwenye miaka 25.

Domayo nje Azam kwa miezi minne kisa upasuaji

MABINGWA wa soka nchini, Azam Fc, imesema kiungo wake Frank Domayo atakuwa nje ya uwanja wa muda wa miezi minne kufuatia upasuaji wa mguu aliofanyiwa nchini Afrika Kusini.
Akizungumzia jiji Afisa Habari wa Azam, Jaffar Idd  amesema uchunguzi wa afya wa kiungo huyo aliofanyiwa na mganga mkuu wa klabu hiyo Dk Mwamkemwa ulibaini kuwa Domayo ana matatizo ya msuli wa mguu wake wa kushoto na kwamba atatakiwa kufanyiwa upasuaji.
Domayo alipekwa na uongozi wa Azam wiki iliyopita nchini Afrika Kusini akiambatana na Dk Mwankemwa ambapo juzi alifanyiwa upasuaji katika hospitali ya Vicent Parent na imeelezwa kuwa anaendelea vizuri huku akitarajiwa kurejea nchini Jumapili.
  Afisa Habari huyio amesema kiungo huyo atakuwa nje ya uwanja kwa kipindi miezi minne akiendelea kupata tiba na uangalizi wa karibu wa jeraha lake kabla ya kurejea uwanjani kuitumikia klabu yake hiyo mpya ambayo amejiunga nayo hivi karibuni.

Cameroon yachunguzwa kwa upangaji matokeo Brazil

TIMU ya soka ya taifa ya Cameroon, inachunguzwa kwa tuhuma za upangaji wa matokeo katika mechi zao za Kombe la Dunia waliotolewa hatua ya makundi nchini Brazili.
Maafisa wa Cameroon watapelelezwa kutokana na madai kwamba saba kati ya wachezaji wa timu ya taifa hilo walihusika katika kupanga mechi katika Kombe la Dunia linaloendelea nchini Brazil.
Kamati ya maadili ya shirikisho la kandanda la taifa hilo litachunguza shutuma za "udanganyifu" wa "wachezaji saba wabaya" katika mechi zao tatu za makundi.
Madai hayo yametolewa na gazeti moja la kijerumani na mtu aliyehukumiwa kwa kuhusika na kupanga mechi nchini Singapore.
Cameroon ilipoteza mechi zote za kundi A, ikiwemo ile waliolazwa na Croatia kwa mabao 4-0.
Mchezaji wa 'The Indomitable Lions' Alex Song, alionyeshwa kadi nyekundu kwa kumgota Mario Mandzukic mgongoni katika mechi hiyo, huku wachezaji wenzake Benoit Assou-Ekotto na Benjamin Moukandjo wakizozana baadaye katika mechi hiyo.
Ripoti kutoka katika shirikisho la kandanda la Cameroon lilisema: "Madai yaliyotolewa majuzi kuhusu udanganyifu katika mechi tatu za mwanzo za Cameroon katika Kombe la Dunia la 2014, hasa kati ya Cameroon na Croatia, na vile vile 'kuwepo na wacheza saba wabaya katika timu yetu ya taifa' hayaambatani na maadili na kanuni zinazopendekezwa na usimamizi wetu, pamoja na kanuni za Fifa na maadili ya taifa letu.
"Tuna nia kuu ya kutumia mbinu zote zinazostahili ili kutatua swala hili linalosumbua kwa muda mfupi iwezekanavyo."
Fifa haikusema iwapo ilikuwa ikichunguza swala hilo au la, kwani bodi hiyo inayosimamia kandanda ulimwenguni "ilitaka uchunguzi uwe wazi".

Mbeya City, Prisons kuzipima tiketi za Electronic

Mbeya City
Prisons-Mbeya
TIMU za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) za Mbeya City na Tanzania Prisons zinacheza mechi ya kirafiki Jumamosi (Julai 5 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Mechi hiyo ambayo itakuwa ya kwanza kuchezwa jijini Mbeya katika mfumo wa matumizi ya tiketi za elektroniki kwa washabiki wanaoingia uwanjani itaanza saa 10 kamili jioni.
Kiingilio ni sh. 3,000 kwa majukwaa yote ambapo tiketi zimeanza kuuzwa leo (Julai Mosi mwaka huu).
Wakati huo huo, keshokutwa (Julai 3 mwaka huu) kutakuwa na mafunzo ya matumizi ya tiketi za elektroniki yatakayofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya kuanzia saa 3 asubuhi.
Washiriki wa mafunzo hayo ni wasimamizi wa mechi katika uwanja huo, viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA), meneja wa Uwanja wa Sokoine na msaidizi wake, makatibu wa Tanzania Prisons na Mbeya City, maofisa habari wa Mbeya City na Tanzania Prisons, Ofisa Usalama wa MREFA na wasimamizi wa milangoni (stewards).

Stars yapigwa 4 Botswana kujiuliza kwa Lesotho

TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) juzi ilikubali kichapo cha mabao 4-2 kutoka kwa wenyeji wao timu ya Botswana katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika jijini Gaborone.
Mechi hiyo iliyochezwa kwenye uwanja wa Taifa wa Gaborone, ilishuhudiwa hadi mapumziko Stars ilikuwa nyuma kwa mabao 3-0 licha kuonekana timu zote zikishambuliana kwa zamu.
Mabao ya Stars katika mchezo huo wa kirafiki yalifungwa na wachezaji wa klabu ya Azam, Khamis Mcha 'Vialli' na John Bocco 'Adebayor' kwa njia ya penalti.
Kikosi hichio cha kocha Mart Nooij kitashuka dimbani tena siku ya Jumamosi kupepetana na Lesothio katika pambano jingine la kirafiki la kimataifa kabla ya siku inayofuata kurejea nyumbani kujiwinda na mechi yao ya kuwania kufuzu hatua ya makundi ya kucheza Fainali za Kombe la Afrika za mwakani.
Taifa Stars imeweka kambi ugenini kwa ajili ya kujiandaa na mechi yake ya kusaka tiketi ya kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Msumbiji itakayofanyika Julai 20 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Stars ambayo ilisonga mbele katika mashindano hayo baada ya kuifunga Zimbabwe mabao 3-2 na kama itafanikiwa kuing'oa Msumbiji katika mechi zao itaangukia kundi moja na timu za Zambia, Cape Verde na Niger ili kuwania kucheza fainali hizo za Afrika zitakazofanyika nchini Morocco.