STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, March 7, 2013

Kagera Sugar, JKT Ruvu vitani leo Chamazi

Kikosi cha JKT Ruvu

Kikosi cha Kagera Sugar


BAADA ya kupoteza mechi yake ya mwisho dhidi ya Yanga, timu ya Kagera Sugar jioni ya leo itashuka dimbani kujaribu bahati yake kwa kuumana na maafande wa JKT Ruvu katika mechi ya mfululizo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kagera wanaonolewa na nyota wa zamani wa Simba, King Abdallah Kibadeni na Mrange Kabange wakavaana na vijana wa winga wa zamani wa Yanga, Charles Kilinda ambao mechi yao ya mwisho walipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Toto Afrika.
Kila upande umejinafasi kufanya vema katika poambano hilo la leo litakjalochezwa kwenye uwanja wa Chamazi, nje kidogo ya Dar es Salaam.
Kibadeni alisema kiu yao ni kusaka pointi muhimu ugenini kabla ya kurejea nyumbani kwao Kagera kwa mechi nyingine zijazo.
Kocha huyo alisema kikosi chake kipo tayari kwa pambano hilo na ana imani kubwa ya kupata ushindi licha ya kukiri pambano litakuwa gumu kwa vile JKT Ruvu sio timu ya kubeza hasa ikizingatiwa msimuu huu hawajawa na matokeo ya kuvutia kama misimu miwili iliyopita.
Kwa upande wa JKT Ruvu baadhi ya nyota wake wamedai kama walivyofanya kwa Toto ndiyo itakavyokuwa kwa Kagera katika mechi hiyo kwa nia ya kuipa timu yao ushindi na kuondoka eneo la mkiani wanakochuana na timu nyingine tatu kuwania kuepuka kushuka daraja.
 

Mtibwa yatakata yazikamata Simba, Coastal Union

Kocha wa Mtibwa, Mecky Mexime

BAO lililofungwa dakika za lala salama kwenye uwanja wa Mkwakwani Tanga, imeiwezesha mabingwa wa zamani wa soika nchini, Mtibwa Sugar kuzikamata timu za Simba na Coastal Union kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mtibwa iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mgambo JKT na kuifanya ifikishe jumla ya poiinti 31 sawa na wapinzani wake hao watakaovaana Jumapili jijini Dar japo wabakia nafasi tano.
Bao hilo pekee la Mtibwa lilifungwa na 'muuaji' wa Simba, Salvatory Ntebe katika dakika ya 90 na kuwafanya vijana wa Mecky Mexime kupumua baada ya kuanza duru la pili vibaya.
Katika mechi nyingine zilizochezwa jana kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid wenyeji JKT Oljoro iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa katika kipindi cha pili na Paul Nonga na kuilaza Prisons ya Mbeya ambapo kocha wake Jumanne Chale alilalamikia mchezo huo.
Kocha huyo alidai wenyeji walibebwa kutokana na kukataliwa bao lao safi lililofungwa na mchezaji wake, huku akidai kulikuwa na maamuzi yasiyomvutia kwenye pambano hilo.
Nao maafande wa Ruvu Shooting ya Pwani waliendelea kuizamisha Aficna Lyon kwa kuilaza baio 1-0 na kuifanya timu hiyo kubakia mkiani mwa msimamo wa lihi hiyo itakayoendelea tena leo.
Bao lililoiweka pabaya Lyon katika kuwepo kwake katika Ligi Kuu msimu ujao lilifungwa na Abdulrahman Mussa katika dakika ya 29 katika mechi kali iliyochezwa kwenye uwanja wa Chamazi, jijini Dar.

TFF yabanwa na serikali, hofu yatanda


Waziri Dk Mukangara

WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara ameliagiza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhakikisha kuwa linaitisha uchaguzi wake mkuu kabla ya Mei 25 mwaka huu; amri ambayo inazidi kuiweka Tanzania katika hatari ya kufungiwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ambalo haliruhusu masuala ya soka kuingiliwa na serikali.
Amri hiyo ni moja kati ya maagizo matatu yaliyotolewa na serikali katika kikao cha pamoja kilichofanyika jana baina ya viongozi wa wizara, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na TFF.
Kikao hicho kilichofanyika jana asubuhi badala ya leo kama TFF walivyokuwa wameomba katika barua yao ya Jumatatu Februari 4 kilihudhuriwa na Dk. Mukangara, naibu wake Amos Makalla, katibu mkuu wa wizara Seth Kamuhanda, mkurugenzi wa michezo Leonard Thadeo, mwenyekiti wa BMT, Dioniz Malinzi na katibu wa BMT, Henry Lihaya.
TFF iliwakilishwa na katibu mkuu Angetile Osiah, mjumbe wa kamati ya utendaji Alex Mgongolwa na mkurugenzi wa ufundi, Sunday Kayuni.
Baada ya kikao hicho, Dk. Mukangara aliwaambia waandishi wa habari kuwa amewaandikia barua TFF kuwapa maagizo matatu aliyoyataja kuwa ni; kuhakikisha shirikisho hilo la soka linatangaza hadharani kuwa limekubaliana na maelekezo yaliyotolewa na wizara na kwamba tamko hilo litolewe kabla ya Machi 11 mwaka huu.
Barua hiyo ambayo ilionwa nakala yake jana imeitaka TFF katika agizo la pili kuitisha mkutano mkuu wa marekebisho ya katiba ndani ya siku 40 kuanzia jana (kabla ya Aprili 15, 2013).
Katika agizo la tatu, serikali imeitaka TFF iitishe mkutano mkuu kwa kuzingatia katiba ya mwaka 2006 na kwamba, kwenye mkutano huo wajumbe wapitishe marekebisho yaliyofanywa hadi mwaka 2008.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alikaririwa akisema jana kuwa hawezi kuzungumzia lolote kuhusiana na matokeo ya kikao chao cha jana na serikali kwa sababu mwenye mamlaka ya kuzungumzia suala hilo ni Rais wa TFF, Leodger Tenga ambaye hakuwapo nchini.
Maagizo hayo ya serikali yametolewa katika kipindi ambacho tayari serikali imeshatangaza kuifuta katiba mpya ya TFF (ya mwaka 2012) na kuamuru itumike ya 2006, bila kujali ahadi ya FIFA kutuma ujumbe wake katikati ya mwezi huu kujaribu kutatua mgogoro wa uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo.
Hata hivyo, kwa mujibu katiba ya TFF ambayo inazingatia maelekezo ya FIFA, ibara ya 25(1) na (2), mwenye mamlaka ya kuitisha mkutano mkuu wa TFF ni kamati ya utendaji ya shirikisho hilo au theluthi mbili ya wajumbe wa mkutano mkuu ambao hutakiwa kuomba kuitishwa mkutano mkuu kwa maandishi.
Katiba hiyo ya TFF haitoi nafasi kwa serikali kuamuru kuitishwa mkutano mkuu.

Rais wa TFF, Leodger Tenga

HATARI YA KUFUNGIWA
Ingawa hadi kufika jana haikufahamika kama TFF watatekeleza maagizo hayo ya serikali,
lakini uzoefu katika maeneo mengine unaonyesha kuwa utekelezaji wa amri hiyo utaiweka Tanzania katika hatari kubwa ya kufungiwa na FIFA ambayo inapinga vikali serikali kuingilia masuala ya soka.
Novemba 2006, Kenya ilifungiwa na FIFA kutokana na serikali kuingilia masuala ya soka na kushindwa kufuata taratibu za chombo hicho cha kusimamia mchezo wa soka duniani.
FIFA waliiondolea Kenya kifungo hicho Machi 9, 2007 baada ya Waziri Kamanda 'kuinua mikono' kwa kutangaza hadharani kuwa kamwe hawataingilia tena masuala ya KFF kufuatia 'mashinikizo' makubwa kutoka ndani na nje ya taifa hilo.
Ujumbe wa FIFA ulienda Kenya kutoa mwongozo wa kurejesha soka la Kenya katika hali ya kawaida ikiwamo kumtaka waziri wa michezo akiri kutoingilia tena uendeshaji wa KFF.
Rais wa Nigeria, Jonathan Goodluck aliamuru nchi yake isishiriki tena michuano yoyote ya soka ya kimataifa kwa nia ya kujipanga upya baada ya timu yao ya taifa ya soka kuondoshwa kwa aibu kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010.
Hata hivyo, ilifahamika baadaye kuwa maamuzi hayo ya rais yalikuwa na nia ya kumdhibiti mmoja wa viongozi wa juu wa shirikisho la soka la nchi hiyo (NFF), Amos Adam aliyekuwa mbioni kuwania tena uongozi.
Kutokana na kitendo hicho cha serikali kuingilia soka, FIFA iliipa serikali ya Nigeria saa 48 kufuta agizo lake na kwamba, vinginevyo ingefungiwa. Saa chache baadaye, serikali ya Nigeria ilisalimu amri kwa kutangaza kufuta agizo lake baada ya rais Jonathan kuteta ikulu na Adam.

MGOGORO TFF
Chanzo cha mgogoro wa uchaguzi wa TFF ni kuenguliwa kwa baadhi ya wagombea, wakiwamo Jamal Malinzi anayewania kugombea urais na Michael Wambura anayeutaka umakamu wa rais.

Wednesday, March 6, 2013

Ronaldo aizamisha Manchester United na kuing'oa Ulaya

Kocha wa Real Madrid, Jose Morinho akimtuliza Nani baada ya kulimwa kadi nyekundu
Luca Modric akisawazisha bao la Real Madrid jana


 

'Muuaji' Real Madrid akiwajibika uwanjani jana OT

MSHAMBULIAJI nyota wa zamani wa Manchester United, Cristiano Ronaldo usiku wa kuamkia leo alikuwa mwiba mbali kwa vinara hao wa Ligi Kuu ya England baada ya kufunga bao la ushindi na kuiondosha Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ronaldo aliyepata mafanikio makubwa akiwa na klabu hiyo ya Old Trafford, jana alirejea kivingine kwa kuifungia Real Madrid bao la pili na la ushindi na kuifanya timu yake kufuzu robo fainali za Ulaya kwa jumla ya mabao 3-2.
Katika mechi ya awali iliyoisha kwa sare ya bao 1-1 mjini Madrid, Ronaldo ndiye alifunga bao la kuasawazisha na jana alionyesha alivyo muhimu kwa kikosi hicho cha Morinho kwa kufunga bao lililoipa Real ushindi wa 2-1 uwanja wa Old Trafford.
Madrid waliwapa matumaini vijana wa Sir Alex Ferguson alimuanzishia benchi Wayne Rooney, baada ya Sergio Ramos kujifunga bao baada ya kipindi cha pili kabla ya kurekebisha kosa lake kwa kusaidia kupatikana kwa bao la kusawazisha lililofuingwa na Luca Modric aliyetokea benchi.
Manchester United iliyomuanzisha benchi nyota wake, Wayne Rooney ilijikuta ikimpoteza winga wake mahiri, Luis Nani aliyemchezea rafu Alvaro Albeloa kadi iliyolalamikiwa na Sir Ferguson kabla ya Ronaldo kuja kuwazamisha.
Katika mechi nyingine iliyochezwa jana mabingwa wa Ujerumani, Borussia Dotmund iliungana na Real baada ya kuing'oa Shakhtar Donetsk kwa jumla ya mabao 5-2 baada ya kupata ushindi nyumbani wa mabao 3-0 wiki mbili tangu walipolazimisha sare ya mabao 2-2 ugenini.
Michuano hiyo itaendelea tena usiku wa leo kwa mechi nyingine mbili, Juventus ya Italia itakuwa nyumbani kuialika Celtic walioitungia kwao mabao 3-0 na Valencia itaifuata PSG nchini Ufaransa wakiwa nyuma ya mabao 2-1 iliyofungwa ilipocheza nyumbani Hispania.

 

 

Tuesday, March 5, 2013

ZFA yaridhia Aman Makungu kujiuzulu Urais

Aman Ibrahim Makungu; Si rais tena ZFA

Na Ally Mohamed, Zanzibar
HATIMAYE Kamati ya Utendaji ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), imekubali ombi la Rais wake, Aman Ibrahim Makungu kujiuzulu nafasi hiyo.
Katika Barua iliyoandikwa na ZFA Machi 4, mwaka huu, yaani jana, ikisainiwa na Makamu wa Rais Kisiwani Unguja, ambaye pia ni Kaimu Rais wa ZFA kikatiba, Alhaj Haji Ameir, ikiwa na Kumbukumbu namba. ZFA/PRESIDENT/VOL.11/05, ombi hilo limekubaliwa.
Barua hiyo imesema Kamati ya Utendaji ya ZFA Taifa, imekaa na kujadili kwa kina ombi la kujiuzulu kwa Makungu, na kutafakari kwa makini na hatimaye kufikia uamuzi wa kulikubali ombi hilo.
Aidha katika barua hiyo, ZFA Taifa wamemshukuru Aman Makungu kwa msaada wake alioutoa huku wakimuomba aendelee kuwa na chama hicho wakati wowote atakapohitajika.
Nakala za barua hiyo zimetumwa kwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Michezo la Zanzibar pamoja na Msaidizi Katibu ZFA Kisiwani Pemba.
Kwa mujibu wa Katiba ya ZFA, sasa ni wazi kuwa kunalazimika kufanyika uchaguzi mwingine ndani ya siku 90.
Itakumbukwa kuwa miezi miwili iliyopita, Rais wa ZFA, Aman Ibrahim Makungu aliandika barua ya kuomba kujiuzulu nafasi hiyo kwa kile kilichoelezwa katika barua hiyo kuwa ni kuchoshwa na baadhi ya viongozi wa chama hicho wasiotaka mabadiliko huku wakionekana kuwagawa baadhi ya wajumbe wa ZFA kwa kisingizio cha U-Unguja na U-Upemba, ambapo Kamati ya Utendaji ya ZFA Taifa walilikataa ombi hilo kwa madai kuwa litachangia kurejesha nyuma soka la Zanzibar.


Imehamishwa:Bin Zubeiry


TFF yawasilisha barua ya kutaka kuonana na Waziri




NA BONIFACE WAMBURA
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewasilisha rasmi maombi ya kuonana na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara ili kuzungumzia uamuzi wake wa kutengua usajili wa Katiba ya 2012.
Maombi hayo yaliwasilishwa rasmi Wizarani jana (Machi 4 mwaka huu) ambapo TFF imependekeza kikao hicho kifanyike keshokutwa (Machi 7 mwaka huu) au Machi 13 mwaka huu.
Kamati ya Utendaji ya TFF iliyokutana Machi 2 mwaka huu kujadili tamko ya Waziri kutengua matumizi ya Katiba ya 2012 ndiyo iliyopendekeza kikao hicho kwa lengo la kusikiliza upande wa TFF katika suala hilo.
TFF imeamua kuchukua hatua hiyo kufuatia tamko la serikali kutangaza kuifuta katiba mpya ya shirikisho hilo iliyorekebishwa kwa njia ya waraka na iliyotumika kuwaengua baadhi ya wagombea kwenye uchaguzi wake uliokuwa ufanyike Februari 24 mwaka huu.
Hatua ya serikali imekuwa ikielezwa na wadau kama tisho la Tanzania kuadhibiwa na Shirikisho la Soka Duniani, FIFA linalopinga serikali kuingilia vyama wanachama wake.

Hatma ya Lyon kesho Chamazi, Ligi Kuu ikiendelea




NA BONIFACE WAMBURA
HATMA ya African Lyon kuendelea kushika mkia au la kwenye Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inajulikana kesho wakati itakapokuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
Lyon yenye pointi 13 kutokana na mechi 19 inabidi iifunge Ruvu Shooting kama inataka kuirejesha mkiani Toto African yenye pointi 14. Kama kweli inazitaka pointi zote tatu itabidi ifanye kazi mbele ya Ruvu Shooting inayotiwa makali na Kocha Charles Boniface Mkwasa.
Hiyo itakuwa mechi ya 18 kwa Ruvu Shooting inayoshika nafasi ya saba ikiwa na pointi 26 ikitanguliwa na vinara wa ligi hiyo Yanga, Azam, Simba, Coastal Union, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar yenye pointi 28 ikinolewa na nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Mecky Maxime.
Mechi hiyo namba 139 itachezeshwa na mwamuzi Amon Paul kutoka Musoma wakati wasaidizi ni Anold Bugado wa Singida na Milambo Tshikungu kutoka Mbeya. Mwamuzi wa mezani atakuwa Shafii Mohamed wa Dar es Salaam.
Nayo Tanzania Prisons ya Jumanne Chale itakuwa mgeni wa Oljoro JKT katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha wakati Mgambo Shooting itaoneshana kazi na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Keshokutwa (Machi 7 mwaka huu) Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya JKT Ruvu ya Kocha Charles Kilinda na Kagera Sugar.
Ligi hiyo itaendelea tena Jumamosi ya Machi 9 mwaka huu kwa mechi mbili; Yanga vs Toto Africans (Uwanja wa Taifa), na Azam vs Polisi Morogoro (Azam Complex, Chamazi).

 

Simba kurejea kinyonge nyumbani leo usiku

Na Ezekiel Kamwaga, Kwanza Sul, Angola
TIMU ya Smba inarejea nchini Tanzania kesho usiku ikitokea Angola ambako jana ilitolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Libolo ya hapa.
Wachezaji wa Simba leo asubuhi wamefanya mazoezi katika Uwanja wa Libolo uliopo hapa ambako mechi hiyo ilichezwa na mchana itasafiri kwenda mji mkuu wa Angola, Luanda, itakapolala kusubiri safari ya kesho.
Hali katika kambi ya Simba iliyopo katika Hoteli ya Ritz, ilikuwa ya huzuni kutokana na kipigo hicho kikubwa zaidi cha ugenini ambacho Simba imewahi kukipata katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Mara ya mwisho Simba kupata kipigo kikubwa ilikuwa mwaka 2009 ilipofungwa mabao 5-1 na Harass Al Hadoud ya Misri katika michuano kama hii kwenye mechi iliyopigwa jijini Alexandria, Misri.
Kwa ujumla, Simba ilicheza vizuri katika mchezo huo isipokuwa katika dakika 10 za mwisho ambazo iliruhusu mabao matatu kati ya manne iliyofungwa.
Hata hivyo, matokeo hayo ya 4-0 hayatoi tathmini halisi ya mechi hiyo kwa vile katika sehemu kubwa ya mchezo huo, Simba na Libolo zilikuwa zimetoshana nguvu.
Libolo walikuwa na faida ya kuwa na wachezaji wenye uzoefu mkubwa wa mechi za kimataifa kama vile kiungo Ruben aliyekuwa nyota wa mchezo huo ambaye pamoja na kufunga bao la tatu, ndiye aliyekuwa akiichezesha timu hiyo.
Ruben ametoka kuichezea klabu ya Braga ya Ureno iliyokuwa ikishiriki katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na tofauti za wachezaji kama hao na wale wa Simba ilionekana katika namna ambavyo wenyeji walitumia nafasi zao.
Saa moja kabla ya mechi kuanza, mvua kubwa ilinyesha katika mji wa Calulo na kuathiri hali ya uwanja jambo lililosabisha mpira kuchezwa katika mazingira magumu.
 

TFF YAIPONGEZA AZAM KUSONGA MBELE AFRIKA


NA BONIFACE WAMBURA
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa timu ya Azam ya Tanzania Bara kwa kufanikiwa kusonga mbele katika michuano ya Kombe la Shirikisho iliyo chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Ushindi wa jumla ya mabao 8-1 ambao Azam imeupata dhidi ya Al Nasir Juba ya Sudan Kusini si fahari kwa timu hiyo tu, bali Tanzania kwa ujumla, na unaonyesha jinsi klabu hiyo ilivyojipanga kiushindani katika michuano hiyo ya Afrika.
Hata hivyo, ni vizuri Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, benchi la ufundi na wachezaji wa timu hiyo wakautazama ushindi huo kama changamoto kwao kuhakikisha wanajipanga vizuri zaidi kwa raundi inayofuata.
Timu ya Azam inayofundishwa na Mwingereza John Stewart Hall ilishinda nyumbani mechi ya kwanza mabao 3-1, na juzi kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 ugenini jijini Juba.
Kwa kufanikiwa kuing’oa Al Nasir Juba, Azam sasa watacheza raundi ya kwanza (raundi ya 16 bora) ya michuano dhidi ya Barrack Y.C.II ya Liberia ambayo katika raundi ya awali iliitoa Johansens ya Sierra Leone. Barrack ilishinda bao 1-0 nyumbani katika mechi ya kwanza na kulazimisha suluhu katika mechi ya marudiano jijini Freetown.
 
Azam itaanzia mechi hiyo ugenini kati ya Machi 15,16 na 17 mwaka huu wakati mechi ya marudiano itachezwa Tanzania kati ya Aprili 5,6 na 7 mwaka huu.

Monday, March 4, 2013

Azam sasa kuvaana na Waliberia, kurejea leo kishujaa

Wakali wa Tanzania, Azam Fc
USHINDI wa mabao 5-0 iliyopata Azam jana na kuiwesha kuing'oa Al Nasir Juba ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 8-1 imeifanya klabu hiyo kuweka historia na sasa inatarajiwa kuvaana na tiu ya Barrack Young Controllers Fc ya Liberia  katika mechi yao ya raundi wa kwanza katikati ya mwezi huu.
Azam iliyoshinda mchezo huo wa Sudan Kusini kwa mabao ya Mcha Khamis 'Vialli', aliyefunga mabao matatu na mengine kupitia kwa John Bocco 'Adebayor' na Salum Abubakar 'Sure Boy' itakutana na wapinzani wao klabu iliyoanzisha mwaka 1997.
Wapinzani wao walipata nafasi hiyo baada ya kuing'oa timu ya Johansens ya Sierra Leone kwa jumla ya bao 1-0  baada ya juzi kutoshana nguvu kwa kutofungana wiki tangu BYC II kupata ushindi wa bao 1-0 nyumbani.
Kwa kufuka hatua hiyo Azam imezidi kuweka rekodi katika michuano mikubwa ya kimataifa inayoishiriki kwa mara ya kwanza, kwani ni hivi karibuni tu iliweka rekodi ya kufika fainali za Kombe la Kagame na kutwaa ubingwa wa michuano ya Hisani ya nchini DR Congo.
Klabu hiyo iliyopanda Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2008-2009, ndiyo wawakilishi pekee wa Tanzania waliosalia kwenye michuano ya Afrika baada ya Simba na Jamhuri ya Pemba kung'olewa jana kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika kwa vichapo vya aibu.
Simba wenyewe walinyukwa mabao 4-0 na Recreativo do Libolo ya Angola na hivyo kung'oka kwa mabao 5-0 wakati wenzao walinyukwa mabao 5-0 jana mjini Addis Ababa, Ethiopia na wenyeji wao Kedus Giorgi.
Katika mechi ya awali iliyochezwa visiwani Zanzibar, Jamhuri ilinyukwa mabao 3-0 na hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 8-0.
AAzam inatarajiwa kuwasili leo nchini kishujaa kusubiri kujiandaa na mechi yao ya Ligi Kuu ikiufukuzia ubingwa kwa mara ya kwanza, na pia kwa pambano la kwanza la raundi ya kwanza dhidi ya Barrack Y. C. II ya Liberia mechi itakayochezwa kati ya Machi 15-17.

Ndomba: Mkali wa ngumi anayeota makubwa kimataifa

Bondia Pascal Ndomba



Bondia Pascal Ndomba akiwa Marekani
WAKATI mabondia wengi nchini, wakiwamo wenye majina makubwa, wakilia juu ya mchezo wa ngumi kutowapa mafanikio ya kujivunia, kwa Pascal Ndomba hali kwake ni tofauti.
Bondia huyo anayefahamika zaidi kama 'Kimondo', anasema ngumi zimempa mafanikio ya kujivunia kiasi kwamba hajutii kuucheza mchezo huo.
Ndomba anasema mbali na ngumi kumwezesha kuzitembelea nchi mbalimbali duniani, lakini pia zimemfanya ajenge nyumba Kimara Suka, akimiliki kiwanja eneo la Mbezi Beach pamoja na kuitunza vema familia yake.
Bingwa huyo wa zamani wa Taifa wa TPBC na Afrika Mashariki na Kati, anasema na hivi karibuni ameingia mkataba nchini Marekani ambao unamfanya azidi kuuheshimu mchezo huo.
Anasema mkataba huo wa muda wa miaka minne aliingia mwishoni mwa mwaka jana na kampuni ya Nelson Boxing Promotion na umeanza kutumika mwaka 2013 hadi 2017.
"Ingawa ni kweli ngumi kwa hapa nchini na hata kanda ya Afrika Mashariki zimekuwa hazina tija kutokana na ubabaishaji uliopo, nashukuru Mungu zimenisaidia kwa mengi," anasema.
Anasema siri ya kufanikiwa kupitia mchezo huo ni kujitambua kwake na kuwa na nidhamu kwa kila senti anayoipata, huku akimwagia sifa 'bosi' wake Humoud M. Sumry, anayemfadhili.
"Bosi wangu Humoud Sumry, ndiye kila kitu kwangu kwa msaada anaonipa chini ya kampuni yake ya mabasi ya Sumry," anasema.


SIRI
Bondia huyo anafichua siri kwa kusema kuwa chanzo cha mabondia wengi nchini na hata Afrika kushindwa kufanikiwa kimaisha na kimichezo kupitia ngumi inatokana na ubabaishaji uliopo katika sekta hiyo.
Anasema mapromota na viongozi wa ngumi wamekuwa wakiwanyonya mabondia kwa kutumia udhaifu wao wa kuwa na elimu ndogo ama kushindwa kujitambua wapo katika mchezo huo kwa ajili ya nini.
Pia anasema kumekuwa na hila zikifanywa kati ya viongozi wa vyama na mapromota wa nje wa kutaka mabondia dhaifu ndiyo wapelekwe nje kuicheza na hata kama ni wakali basi hulazimishwa wacheze chini ya kiwango.

Pascal Ndomba akiwa nje ya nchi
"Hufanya hivyo kwa lengo la kutaka mabondia wao kuendeleza rekodi zao na ikitokea bondia anayepelekwa huko akashinda kama alivyofanya Karama Nyilawila basi huzua tafrani baina ya pande mbili zilizokubaliana," anasema.
Akaongeza hiyo ndiyo sababu inayofanya mabondia wengi wa Tanzania au barani Afrika kupigwa kila wanapoenda nje.
"Ni 'dili' tu zinazofanywa na baadhi ya watu wachache kwa tamaa za fedha," anasema.
Ndomba anayependa kula ugali au ndizi kwa nyama na kunywa Fanta, pia anasema mabondia wamekuwa wakidhulumiwa haki zao na baadhi ya viongozi wa ngumi kwa kuwapunja fedha za malipo tofauti na makubaliano.

Pascal Ndomba akiwa na 'bosi' wake, Humoud Salim
Anasema inawezekana bondia ameitwa kwenda kucheza nje kwa dola 5,000, lakini huishia kulipwa 3,000 au nusu ya hapo kwa kisingizio hiki na kile, wakati mwingine asipewe kabisa.
Bondia huyo aliyeingia kwenye ngumi kwa kuvutiwa na bingwa wa zamani wa dunia, Mike 'Iron' Tyson, anasema ni vema kungekuwa na utaratibu chini ya serikali kuhakiki mikataba na kujua kinachompeleka bondia nje ya nchi.
"Japo hizi ni ngumi za kulipwa, ni vyema kungekuwa na chombo cha namna hiyo kusimamia safari za mabondia nje kuepusha kudhulumiwa na kuichafua nchi nje kwa vile hupeperusha bendera ya taifa," anasema.

MATAJI
Ndomba, mume wa Ikupa aliyezaa naye watoto wawili, Michael (8) na Abel (5) wanaosoma Shule ya Msingi Makuburi, anasema alianza rasmi ngumi mwaka 1996 katika klabu ya Kiwira iliyopo Kyela Mbeya.
Kocha aliyemnoa anaitwa Said Tambwe na alishiriki michuano kadhaa ya ngumi za ridhaa na alipoona hazina tija yoyote, mwaka 2000 aliamua kuhamia ngumi za kulipwa.
Anasema akizcheza ngumi hizo aliweza kunyakua ubingwa wa mkoa wa Mbeya na kupata fursa ya kupigania ubingwa wa Taifa wa TPBC mwaka 2005 kwa kumpiga Fike Wilson.
Aliendelea kutoa vipondo kwa wapinzani wake kabla ya mwaka 2009 kutwaa taji la Afrika Mashariki na Kati kwa kumchapa kwa KO Mkenya Joseph Odhiambo.
Pia amewahi kuwania mikanda ya kimataifa inayotambuliwa na WBC, WBO na IBF, uzito wa Cruiser mara ya mwisho ikiwa Desemba, 2012 alipoenda Ghana kupigana na Mghana asiyepigika Braimah Kamoko na kunyukwa.

Pascal Ndomba (Kushoto) akichapana na Mghana Braimah Bamoko
Ndoto zake kubwa ni kuja kutwaa ubingwa wa dunia akiamini ana uwezo wa kufanya hivyo, pia akitamani kuja kumiliki gym na klabu ya kufunzia vijana mchezo huo.
"Napenda nije kuwafunza na kuwarithisha vijana kipaji changu, najua siwezi kusalia kuwa bondia milele," anasema.
Licha ya kucheza mapambano mengi, Ndomba analitaja pambano la kuwania ubingwa wa vijana wa IBF uzani wa 'cruiser' dhidi ya Mswisi, Agron Dzila, kuwa ndilo gumu kwake na asiloweza kusahau kwa 'kisago' alichoikipata.

CHIMBUKO
Pascal Ndomba alizaliwa mwaka 1983, Kyela Mbeya akiwa ni mtoto wa nne kati ya watano wa familia yao na alisoam  Shule ya Msingi Lema ya Kyela kabla ya kujiunga Tabora Boys kwa masomo ya Sekondari.
Tangu shuleni alipenda michezo, ila alivutiwa na ngumi na kujifunza kabla ya kuanza kuzipiga ulingoni na mabondia kama akina Bagaza Mwambene, George Sabuni, Hassani Matumla, Karama Nyilawila na Maneno Osward.
Ndomba anasema hana furaha mpaka atakapopanda ulingoni kupigana na Japhet Kaseba aliyenukuliwa hivi karibuni akidai amekuwa akikwepa na baadhi ya mabodnia kwa umahiri wake.
"Kwa kweli kiu yangu ni kuzichapa na Kaseba, dai lake kwamba amekuwa akikimbiwa na mabondia siyo kweli kwa vile nimekuwa nikiomba kucheza naye bila mafanikio," anasema.
Ndomba anayeiomba serikali itupie macho mchezo wa ngumi kwa madai umekuwa ukiiletea sifa Tanzania nje ya nchi kwa mabondia waliowahi kutwaa mataji ya kimataifa.

Pascal Ndomba (kushoto) akiwa kwenye kazi yake ya uwakala wa mabasi kituo cha mabasi cha Ubungo
Bondia huyo anayependa kusikiliza muziki na kuangalia runinga mbali na kucheza ngumi pia ni wakala wa kampuni ya mabasi ya Sumry, akiishabikia Simba na Manchester United, na anawazimia Shomari Kapombe na Patrick Evra.
Tukio la furaha kwa Ndomba, ambaye anamkubali sana bondia mkongwe Mbwana Matumla, ni siku mkewe alipojifungua mtoto wake wa kwanza mwaka 2005. "Tukio la huzuni nisilolisahau ni kifo cha baba yangu kilichotokea mwaka 2002," anasema.

Pascal Ndoma (kushoto) akiwa na wakala mwenzake wa mabasi ya Sumry

TOTTENHAM  YAINYUKA ARSENAL, MANCHSTER CITY DIMBANI LEO

Garreth Bale akifunga bao la kwanza la Tottenham katika mechi ya jana


KIKOSI cha vijana wa Andre Villas Boas, Tottenham Hotspur, jana waliendeleza  makali na ubabe kwa klabu za London ya Kaskazini baada ya kuwanyuka wapinzani wa Arsenal kwa mabao 2-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya England.
Katika pambano hilo lililochezwa kwenye uwanja wa White Hart Lane nyumbani kwa Spur, Arsenal ilishtukizwa kwa bao la mapema lililofungwa na Garreth Bale kabla ya Aaron Lennon kuongeza bao la pili dakika mbili kabla ya mapumziko.
Arsenal waliocheza kichovu kipindi cha kwanza na kurejea toka mapumziko walifanikiwa kupata bao la kufutia machozi lililofungwa na beki wake 'ngongoti' Mertesacker.
Ushindi huo umeifanya Spur kurejea kwenye nafasi yake ya tatu iliyokuwa inaishikilia kabla ya kuenguliwa Jumamosi na Chelsea waliopata ushindi dhidi ya West Brom kwa bao 1-0.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena usiku wa leo kwa pambano moja la timu za Aston Villa itakayoikaribisha mabingwa watetezi wa Li litakalowakutanisha mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Manchester City waliopo nafssi ya pili.