STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, November 10, 2013

Meshack Abel kurejea Simba?

Meshack Abel wakati akiiichezea Simba
BEKI wa kimataifa wa Tanzania anayecheza soka la kulipwa nchini Kenya, Abel Meshack ameanza mazungumzo na timu yake ya zamani ya Simba ili kurejea kuja kuichezea katika duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza na MICHARAZO, beki huyo wa kati mwenye mwili mkubwa, alisema viongozi wa Simba wamekuwa wakizungumza naye ili kurejea tena kuichezea timu hiyo ambayo imemaliza duru la kwanza ikiwa nafasi ya nne.
Meshack, alisema kwa jinsi mazungumzo hayo yanavyoendelea kuna uhakika wa kuichezea timu hiyo duru lijalo, licha ya kukiri mkataba wake na timu anayoichezea ya Bandari-Mombasa umebakisha miezi sita.
"Natarajia kurejea nchini Ijumaa ijayo kwa ajili ya mapumziko kwa vile Ligi Kuu Kenya imeisha na tumemaliza tukiwa nafasi ya sita, lakini tayari nimeanza mazungumzo na Simba ili kujiunga nayo," alisema Meshack.
Beki huyo aliyewahi kuzichezea pia timu za Ashanti United na African Lyon, alisema yeye binafsi angependa kuja kucheza nyumbani baada ya misimu miwili ya kucheza Kenya katika Bandari.
"Napenda kuja kucheza nyumbani baada ya kuwa nje ya nchi kwa muda, japo suala la masilahi ni kitu kitakachonishawishi zaidi," alisema.
Uongozi wa Simba haukupatikana kueleza juu ya taarifa hiyo, lakini gazeti la NIPASHE la leo lilinukuu taarifa kwamba benchi la ufundi likiwa linasaka beki wa kati ili kuimatisha safu yake ya ulinzi.
Kabla ya kwenda Kenya, Meshack alitibuana na Simba kwa kugoma kitendo cha kumpeleka kwa mkopo katika timu ya Ruvu Shooting wakati huo akiwa amepata timu ya kuceza soka la kulipwa nchini Botswana.

No comments:

Post a Comment