
Van Gaal na Afisa mkuu wa klabu hiyo Ed Woodward wanahaha kusaka saini ya Vidal baada ya kumaliza kusajili Angel Di Maria jana.
United imekuwa ikipinga kumhitaji Vidal kwa kipindi kirefu lakini sasa wanadaiwa kuanza mazungumzo kama wanayofanya dhidi ya Ajax Amsterdam kwa ajili ya kumsajili Daley Blind.
Majeruhi pekee ndiyo yalioonekana kumzuia Van Gaal kumsajili nyota huyo wa kimataifa wa Chile ambaye ana thamani ya paundi milioni 30 lakini kutokana na matokeo mabovu ya hivi karibuni klabu imeona hakuna jinsi bali kutumia fedha ili wajiimarishe.
Upasuaji wa goti msimu uliopita ulimzuia Vidal kuitumikia Juventus toka mwishoni mwa Machi mwaka huu ingawa baadae alipona na kupata muda wa kuwepo katika kikosi cha Chile katika michuano ya Kombe la Dunia.
Ujio wa Vidal, 27 United kutasaidia kuimarisha safu ya kiungo ambayo imeonekana kuyumba na kupelekea kipigo cha mabao 4-0 jana dhidi ya timu ya daraja la chini ya MK Dons katika mchezo wa Kombe la Ligi.
Kama United wakifanikiwa kumsajili Vidal watakuwa wamefikisha kiasi cha paundi milioni 150 walizotumia msimu huu kwa ajili ya usajili baada ya kuvunja rekodi nchini Uingereza kwa uhamisho wa Di Maria.
No comments:
Post a Comment