STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, August 11, 2013

Azam yaanza kuingiwa mchecheto kwa Yanga

Na Mahmoud Zubeiry, Johannesburg, Afrika Kusini, IMEWEKWA AGOSTI 11, 2013 SAA 5:05 ASUBUHI
KOCHA Muingereza wa Azam FC, Stewart John Hall ameridhishwa na maandalizi ya timu yake katika kambi ya kujiandaa na msimu hapa Afrika Kusini, lakini kuelekea mchezo dhidi ya Yanga SC Jumamosi ijayo kuwania Ngao ya Jamii, mwalimu huyo anahofia sana juu ya marefa.
Stewart ameiambia BIN ZUBEIRY leo mjini hapa kwamba ana imani na timu yake imenufaika mno na kambi ya Afrika Kusini na inaweza kwenda kuwapa burudani nzuri wapenzi wa soka Tanzania baada ya hapa.
Marefa watende haki; Kocha Stewart Hall kulia akiwa na Msaidizi wake, Kali Ongala. Amemba marefa watende haki Agosti 17 Taifa dhidi ya Yanga.

Hata hivyo, Stewart amesema mchezo wa kufungua pazi la Ligi Kuu dhidi ya Yanga, Agosti 17, wasiwasi mkubwa ni marefa kuwabeba wapinzani wao siku hiyo.
“Nina wasiwasi na marefa, tena sana. Mara ya mwisho tulipocheza na Yanga, walitufunga 1-0, lakini refa alitunyima penalti na akakataa bao letu lililofungwa na John Bocco,”.
“Imekuwa kawaida unapocheza na Simba SC au Yanga, marefa wanakuwa upande mwingine. Sasa kama na kwenye mechi ya Ngao itajirudia hivyo, itakuwa mbaya. Naomba marefa watakaopangwa wachezeshe kwa haki,”alisema Stewart.
Azam ipo hapa tangu Agosti 3, kwa ajili ya kujiandaa na msimu- ambapo wataanza na mechi ya kuwania Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga SC, Agosti 17, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwaka jana, Azam FC ilifungwa 3-2 na Simba SC katika mechi ya kuwania Ngao, licha ya kuongoza kwa mabao 2-0 hadi mapumziko, lakini kocha Stewert amepania kubeba ‘Ubao’ safari hii.  
Kikosi kazi; Kikosi cha Azam katika moja ya mechi zake hapa Afrika Kusini

Tangu iwasili hapa, Azam, ambayo imekuwa ikijifua katika viwanja vizuri vya Chuo Kikuu cha Wits, ikitokea kwenye hoteli ya nyota tano, Rundburg Towers, imekwishacheza mechi tatu na kufungwa mbili, ikishinda moja.
Ilifungwa 3-0 katika mchezo wa kwanza na Kazier Chiefs, ikashinda 1-0 katika mchezo uliofuata na Mamelodi kabla ya kufungwa 2-1 na Orlando Pirates, wakati kesho itacheza mechi ya mwisho na Moroka Swallows kabla ya Jumanne kurejea Dar es Salaam.

Yathibitika Sheikh Ponda yu hai na kisa cha kupigwa risasi hiki hapa!



KATIBU wa Jumuiya ya Kiislamu nchini , Shekhe Ponda Issa Ponda, alijikuta katika wakati mgumu baada ya kuumizwa na kitu kinachodhaniwa kuwa ni risasi kwenye bega lake la kulia wakati akiekelea katika Msikiti wa Mungu Mmoja Dini Moja wa Mjini Morogoro baada ya kumalizika kwa kongamano ya Dini ya Kiislamu.

Mkasa huyo ulitokea jana Jumamosi Augosti 10, mwaka huu majira ya saa 12: 15 za jioni eneo la barabara ya Tumbaku karibu na Fire, mara baada ya kumaliza kwa Kongamano la Kiislamu lililofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Kiwanja Cha Ndege, Kata ya Saba Saba , Manispaa ya Morogoro.
 

Shekhe  Ponda alishiriki katika Kongamano hilo lililoandaliwa na Umoja wa Wahadhiri wa Dini ya Kiislamu Mkoani Morogoro na kufanyika siku ya Idd Pili kuanza saa nane mchana hadi kumi na mbili jioni ya siku hiyo. 
 

Kongamano hilo lilipata baraka zote na Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro, ambalo lilitoa  masharti kadhaa ya kuzingatiwa na wazungumzaji ikiwa ni kutokashifu dini nyingine wala viongozi wa serikali. 
 

Sakata la kutaka kutiwa mbaroni kwa Shekhe Ponda lilikuja baada ya yeye kudaiwa kukiuka masharti ya Mahakama aliyopewa baada ya kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja nje wa  kutakiwa asitende kosa lolote la jinai anapotumikia adhabu hiyo. 

Mwenyekiti wa Kamati ya Maadalizi ya Kongamano hilo, Ustaadh Idd Msema, alidai kuwa Shekhe Ponda baada ya kutoka ndani ya gari eneo la Uwanja wa Shule ya Msingi Kiwanja Cha Ndege aliofika mita chache katika barabara ya Tumbaku aliteremka na wakati akitaka kuingia garini ilifyatuliwa risasi iliyompiga begani. 
 

Ustaadh Msema alidai kuwa baada ya kupigwa risasi begani waumini waliokuwa wameambatana naye walimchukua na kumpakiza kwenye Piki Piki hadi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ili kupatiwa matibabu. 
 

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, baada ya kufika hospitali, waliona anacheleweshwa kupatiwa matibabu na ndipo walipoamua kumwondoa na kumpekea kwenye Hospitali binafsi ambayo hakupenda kuitaja. 
 

Akizungumzia kwa kina hali ya Shekhe Ponda baada ya kujeruhiwa huko, alisema kuwa yu hai licha ya kuumia vibaya begani na kwamba wanatarajia kumpekela eneo jingine hususani Jijini Dar es Salaam kupata matibabu zaidi.
 

Alisema viongozi wa Umoja huo hauwezi kuweka wazi sehemu anakotibiwa kwa kuwa jambo hilo ni la kiusalama zaidi hasa wakati huu ambapo kumekuwa na sinto fahamu.
 

Baadhi ya walinzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro waliozungumza juu ya tukio hilo , walikiri kuwa Shekhe Ponda aliletwa hapo kwa usafiri wa Piki piki zikiambatana na nyingine zaidi ya 50 na kuishia getini. 
 

Walisema walimwingiza hadi mapokezi na kwamba walipoona umati mkubwa upo getini waliamua kutoa taarifa Polisi kuwa wamevamiwa na watu ambapo muda si mrefu Polisi wa FFU waliwasili na gari lao Hospitalini hapo.  
 
Hata hivyo walinzi hao walisema, baada ya kuona Askari wamefika Hospitalini hapo, baadhi ya wafuasi wa Shekh Ponda waliamua kumnyanyua na kumbeba mabegani na kutoka naye mlango mwingine wakimlazimisha mlinzi kuwafungulia mlango na baadaye wakatokomea naye kwa usafiri wa Pikipiki kusikojulikana. 

Kufikishwa kwa Sheikh Ponda katika Hosipitali ya Rufaa kulithibishiwa pia na Mwenyekiti huyo ambaye alidai  kuwa waliamua kumwondoa baada ya kuchekewa  kupatiwa huduma. 
 

Baada ya tukio hilo, uvumi ulisambaa maeneo mbalimbali nchini ukidai kuwa Sheikh Ponda amepigwa risasi na Polisi na kufariki dunia. 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Feustine Shilongine akizungumza na Mwandishi wa Habari hizi majira ya saa tatu usiku wa Augosti 10, baada ya kutokea kwa tukio hilo, alisema kuwa hapakuwa na taarifa juu ya kutokea kifo cha Shekhe Ponda. 
 

“ Nimepigiwa simu zaidi ya 50 , zikiulizia jambo hili...kuwa Ponda amefariki dunia ...Binafsi nami ninazisikia , ujumbe umesambazwa kwenye simu za watu mbalimbali...tumezunguka kila mahali hakuna kifo wala maiti yake ...na vijana wangu wanaendelea kulifuatilia suala hili” alisema Kamanda huyo. 

Juhudi za kufuatilia sakata la uvumi kifo cha Sheikh Ponda uliendelea kufanyiwa kazi na Ripota wetu huyu na usiku wa saa tano Mwenyekiti wa Kamati huyo aliweka wazi kwa kusema kuwa Sheikh huyo machachari yu hai isipokuwa ameumia vibaya sehemu ya bega . 
 

 “ Nipo katika eneo ambalo Shekhe Ponda anapatiwa matibabu...sehemu ambayo hatuwezi kupataja kiusalama , isipo kuwa ameumia vibaya kwenye bega lake.

 "Lakini yu hai wala hajafa” alisema Msema.

 Askari wa FFU wakijisogeza kati kati ya uwanja mara baada ya muda wa kongamano kumalizika.

 Kutambulishwa jukwaani Shekh Ponda.

 Kikosi cha FFU uwanjani

 Shekh Ponda akikaribishwa kwenye jukwaa kuu baada ya kuwasili kwenye viwanja vya shule ya Msingi Kiwanja Cha Ndege , mjini Morogoro

 Shekh Ponda akisalimiana na Mhadhiri wa Mihadhara nchini, Ustaadhi Abubakari

 Shekh Ponda akisisistiza jambo mbele ya waumini wa Dini ya Kiislamu kwenye Kongamano , Augosti 10, mwaka huu mjini Morogoro

 Shekh Ponda akiteta jambo na baadhi ya Viongozi wa umoja wa Wahadhiri wa Dini ya Kiislamu Mkoa wa Morogoro

 Shekhe Ponda akiwa meza kuu kwenye kongamano hilo

 Shekhe Ponda akiwa amezingirwa na waumini

 Umati wa waumini wa Kiislamu wakimsikiliza Shekh Pond




Waumini wa Dini ya Kiislamu wa mjini Morogoro wakimsikiliza Shekh Ponda


Waumini wa Kiislamu wakitawanyika uwanjani baada ya muda wa kongamano kufikia tamati


The Choice

Huyu alijeruhiwa vurugu za msikitini Kyela Mbeya

HUYU ni mmoja ya watu waliojeruhiwa katika vurugu wakati wa sala ya Idd zilizotokea jana katika msikiti wa Kyela mkoani Mbeya. Anatambuliwa kwa  jina la  Khamis Hussein na alijeruhiwa na kitu chenye ncha kali na kushonwa nyuzi tatu.

Pichani akiwa hospitali mara ya kupewa matibabu.

Kiza kinene chatanda sakata la kupigwa risasi Sheikh Ponda

Katibu wa Kamati ya Kutetea Haki za Waislam Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda.
MPAKA muda huu bado hatujaweza kupata taarifa nyingine zozote kuhusu tukio la kupigwa kwa risasi kwa Sheikh Ponda Issa Ponda lililotokea mjini Morogoro.
Juhudi zetu zimeishia kupata taarifa kama tulizowafahamisha mapema, huku jeshi la Polisi likisisitiza kutohusika na kitendo hicho, licha ya mashuhuda kueleza kwamba Polisi walifyatua mabomu ya machozi na risasi za moto ambayo moja ilimpata Ponda begani.
Kadhalika hakuna ukweli wowote kwamba Sheikh Ponda amefariki dunia kama baadhi ya watu wanavyovumisha, kwa sababu mpaka tunapoandika taarifa hii kwenu tumefahamishwa kuwa sheikh huyo alikuwa kajeruhiwa na hakukuwa na yeyote kati ya vyanzo vya habari au hata Polisi wenyewe kuthibitisha juu ya Ponda kuaga dunia.
Hivyo wasomaji wa MICHARAZO, endeleeni kuvuta subira kupata ukweli wa kinachoendelea badala ya kupandwa presha kwamba Kiongozi huyo wa Umma wa Kiislam anayependwa kila kona ya nchi kwa harakati zake za kupigania haki za waislam walio wanyonge huenda amefariki.
Pia kama ni kweli Sheikh Ponda atakuwa amefariki basi ni mipango ya Mungu kwa vile kila nafsi itaonja mauti, ila ukweli ulivyo ni kwamba hakuna taarifa za kupoteza kwake maisha zaidi ya hizo za kujeruhiwa na pia haifahamiki kwa sasa yupo wapi, kitu ambacho hata Polisi kimesema na kutangaza kumsaka na kutaka wenye taarifa juu ya alipojichimbia Sheikh huyo watoe taarifa haraka. Vuteni subira.

Cheka aendeleza ubabe katika Masumbwi amtwanga Mmalawi mjini Morogoro

Francis Cheka 'SMG'

BINGWA wa IBF Afrika, Francis Cheka ameendeleza ubabe mbele ya mabondia wenzake baada ya usiku huu kumshinda kwa pointi Mmalawi Chiotcha Chimwemwe katika pambano lisilo la ubingwa lililochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.
Cheka amepata ushindi huo katika pambano hilo la raundi 8 japo baadhi ya mashabiki wamedai Mtanzania huyo amebebwa tena kama ilivyokuwa mjini Arusha alipomtwanga Chimwemwe na kutetea taji lake la IBF Desemba mwaka jana.
Ushindi huo umeendeleza rekodi ya Cheka ya kutopigwa katika ardhi ya Tanzania tangu Agosti, 2003 na kwa sasa atakuwa akijiandaa na mchezo wake mwingine lakini wa kimataifa kuwania mkanda wa WBF dhidi ya Mmarekani, Phil Williams atakayepigana naye Agosti 30 katika ukumbi wa Diamond Jubilee.
Pia ushindi huo wa Cheka umekuja saa chache baada ya Mtanzania mwingine na bingwa wa UBO Afrika, Francis Miyeyusho kumtwanga Mzambia Fidelis Lupapa katika pambano lisilo la ubingwa lililofanyika jana kwenye ukumbi wa Dar Live, Mbagala Dar es Salaam.
Miyeyusho alimtwanga Mzambia huyo kwa KO ya raundi ya 8 kati ya 10 zilizopangwa zichezwe katika kusindikiza sherehe za sikukuu ya Eid el Fitri.

Saturday, August 10, 2013

Arsenal yaikamua Man City 3-1, Liver ikizama kwa Celtic

Hands on: Carl Jenkinson accidentally catches Samir Nasri in the face with an arm
Wachezaji wa Arsenal na Manchester City
KLABU ya Arsenal jioni hii imeizabua Manchester City kwa mabao 3-1 katika pambano lililofanyika  kwenye Uwanja wa Olimpiki mjini Helsinki ukiwa ni mchezo wa kirafiki.
Arsenal inayohaha kumsaka mshambuliaji wa Liverpool, Luis Suarez, walipata mabao yao kupitia kwa Theo Walcott dk ya 9, Aaron Ramsey dk 59 na Olivier Giroud dk 62.
Bao la kufutia machozi la City liliwekwa kimiani 'jioni' kabisa na Negredo dk 80.
Nayo Liverpool imejikuta ikiwashwa bao 1-0 na Celtic ya Scotland huku Tottenham ikitoshana nguvu na Espaniol katika mechi zingine za kirafiki zilizochezwa leo.

Utata sakata la Sheikh Ponda, Polisi waruka kimanga

clip_image001
TUKIO la kupigwa risasi na kujeruhiwa kwa Sheikh Ponda Issa Ponda mjini Morogoro ni utata mtupu wakati baadhi ya waumini wa kiislam wa mjini humo wakithibitisha taarifa hizo kwamba Sheikh wao kapigwa risasi begani, jeshi la Polisi mkoani humo limekanusha tukio hilo, japo linalikiri walitaka kumkamata jioni hii.
Kamanda wa Polisi wa mkoani humo, Faustine Shilogile, amenukuliwa hivi punde na Radio One Stereo na kudai jeshi lake lilikuwa likimvizia kumkamata Sheikh Pondaa ya kuhudhuria Kongamano la Wahadhiri wa Kiislam mkoani Morogoro na kuhutubia, lakini wakazidiwa ujanja na waumini waliomkinga na kumtorosha Sheikh wao huyo machachari asiishie mikononi mwa dola.
Kamanda Shilogile, alisema suala la Ponda kupigwa risasi na kujeruhiwa au kuuwawa kama habari hizo zilivyozagaa mjini humo ni uzushi kwa vile sheikh huyo hajafikishwa kituo chochote cha polisi au hospitali kama ni kweli kajeruhiwa.
Kamanda Shilogile

"Hizi ni habari zilizozagaa mjini hapa wengine wakidai ameuwawa, ila ukweli ni kwamba Polisi hawajafanya kitendo chochote dhidi ya Ponda zaidi ya kwamba tulitaka kumkamata mara baada ya kuhutubia kwa dakika kama 5 kwa kutambua kuwa anasakwa," alisema Shilogile.
Aliongeza wakati wanamvizia Sheikh Ponda liyechelewa kwenye kongamano hilo likliwa kama dakika 10 limalizike waumini wa kiislam aliodai walikuwa wengi mno walimtorosha na hivyo wao kumkosa na kudai kuwa wanafuatilia mahali alipofichwa na kama ni kweli alijeruhiwa wajue anatibiwa wapi.
Utata unakuja wakati Shilogile akisema hawakufanya tukio lolote la kupiga risasi, je wanafuatilia mahali anapotibiwa kwa sababu zipi? Kadhalika waumini waliozungumza kwa njia ya simu na MICHARAZO wamedai tukio hilo limetokea wakati Polisi walipovamia taksi iliyomleta Sheikh Ponda na katika purukshani walifyatua mabomu ya machozi na risasi za moto ambapo ilimpata begani na kumjeruhi.
"Hawa watu wanatuchokoza Waislam ili tuonekane wakorofi tunasherehekea sikukuu yetu kwa amani wanatuletea mambo ya kihuni walitaka kumkamata Sheikh wetu nasi tukasimamia kidete na kuwagomea ndipo wataamua kutumia nguvu kupiga risasi na kwa bahati ikampiga risasi ya bega na kumjeruhi wanakanusha nini," alisema mmoja wa mashuhuda hao.
Hata hivyo bado imekuwa vigumu kujua mahali alipo sheikh huyo inayedaiwa alikimbizwa Hospitali ya mkoa na kabla ya kuanza kupata matibabu baada ya kubainiwa Polisi wanamfuatiliwa alitoroshwa na waumini hao na kutofahamika kapelekwa hospitali gani kupata matibabu, japo Polisi wanasema wameanza upelelezi wa mahali alipo kupata ukweli wa uvumi huo ambao umesambaa nchi nzima kama moto wa nyikani.
MICHARAZO bado inafuatilia kujua ukweli wa taarifa hizi na kila tukipata habari mpya tutawapenyezea.

Simba yawapa raha mashabiki wao 'Simba Day' wapiga mtu 4-1

Kiungo wa Simba, Amri Kihemba akimtoka beki wa Sports Club Villa ya Uganda katika mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo., Siomba imeshinda 4-1. (Picha na Habari Mseto Blog) 
 Kipa wa Sports Club Villa ya Uganda, Elungat Martins akiota mpira katika nyavu la lango lake baada ya mshambuliaji wa Simba, Betram Mombeki kuifungia timu yake bao la tatu katika mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam
Tunda Man, akitumbuiza katika tamasha hilo.

Breaking News: Sheikh Ponda kapigwa risasi Morogoro

Sheikh Ponda katika harakati zake za kidini


TAARIFA zilizotufikia muda huu kutoka Morogoro ambazo hata hivyo bado hazijathibitishwa rasmi zinasema kuwa Katibu wa Kutetea Haki za Waislam Tanzania na Sheikh maarufu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda amepigwa risasi.
Habari zilizotumwa kwa njia ya ujumbe mfupi toka mkoani humi zinadai kuwa Sheikh Ponda alipigwa risasi hiyo na wanaodaiwa askari Polisi na kujeruhiwa.
MICHARAZO ilijaribu kuwasiliana na masheikh kadhaa ili kuthjibitisha taarifa hizo, ambapo mmoja wa viongozi wa Baraza la Habari za Vijana la Kiislam (BAHAKITA) Sheikh Sadick Godegode alisema hata yeye kazipata taarifa hizo ila bado anaendelea kuzifuatilia toka Morogoro.
"Ni kweli hata mimi nimezipata taarifa hizo kwamba Sheikh wetu, Ponda Issa Ponda kapigwa risasi ya bega, ila bado hatujathibitisha japo jana alikuwa mmoja wa walihudhuria Baraza la Idd lililofanyika msikiti wa Kichangani," alisema Sheikh Sadick.
Blogu hii inafanya jitihada za kupata ukweli wa taarifa hizo ambazo huenda zisiwe nzuri kwa waumini wa Kiislam ambao wapo katika sherehe za sikukuu ya Eid.

Zaidi ya Mil 100 kutumika mazishi wa Bilionea na Tanzanites

Mwili wa Erasto Msuya baada ya kupigwa risasi.
 

IKIWA ni takribani siku tatu zimepita tokea mfanyabiasha wa madini ya Tanzanite na mmiliki wa hotel kitali ya S.G Resort iliyopo jijini Arusha aliyefahamika kwa jina la Erasto Msuya kupigwa risasi 21 na kumsababishia kifo papo hapo katika eneo la njia panda ya KIA wakati akitoka Mirerani kuelekea Arusha mjini majira ya mchana.
Habari kutoka katika kamati ya mazishi inayoundwa na wafanyabiashara wa madini ya Tanzanite, ikiongozwa na kaka mkubwa marehemu Gady Msuya, anasema zaidi ya shilingi milioni mia moja (100,000,000/=) inatarajiwa kutumika kugharamia mazishi ya mfanyabiashara huyo bilionea wa madini yav Tanzanite. Na kaka wa Marehemu  (Gady) aliendelea kusema kuwa gari maalumu la kubeba mwili wa marehemu na jeneza vimeagizwa kutoka Nairobi, nchini Kenya kwa gharama ya Shilingi milioni nane (8,000,000/=).
 Kiasi hicho cha zaidi ya milioni mia moja kinarajiwa kuchangwa na wafanyabiashara wenzake wa madini . Pia wanatarajia kulipia magari maalumu yatakayotumika kwenye msafara wa mazishi ya Erasto Msuya yanayotarajiwa kufanyika nyumbani kwake Mirerani, wilayani Simanjiro siku ya jumanne ya tarehe 13 August 2013. 

Leo ni Simba Day, Msimbazi kutambulisha mpya ikiivaa SC Villa ya UgandaSimba kutambulishja

Kikosi kipya cha Simba
Kocha Kibadeni akisalimiana na wadau wa Simba
TIMU ya soka ya Simba leo itatambulisha nyota wake wapya wakati itakapocheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya SC Villa ya Uganda.
Mechi hiyo itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sehemu ya maadhimisho ya tamasha la Simba Day, ambalo hufanyika kila mwaka kabla ya kuanza kwa ligi kuu.

Katibu Mkuu wa Simba, Evod Mtawala alisema jana kuwa, wachezaji watakaotambulishwa leo ni pamoja na mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Hamisi Tambwe na beki wa kimataifa wa nchi hiyo, Kaze Gilbert.

Wachezaji wengine wapya watakaotambulishwa leo ni beki Joseph Owino na mshambuliaji, Betram Mombeki.

Mtawala alisema mechi hiyo itapambwa na burudani kutoka kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya wa kundi la TMK Wanaume Family na Snura, anayetamba kwa kibao chake kipya cha Majanga.

Wakati huo huo, Coastal Union ya Tanga leo itawatambulisha nyota wake wapya wakati itakapocheza mechi ya kirafiki dhidi ya kombaini ya Polisi.

Mkurugenzi wa Ufundi wa Coastal Union, Nassor Bin Slum alisema jana kuwa,mechi hiyo itapigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

Aliwataja wachezaji wapya watakaotambulishwa leo kuwa ni Haruna Moshi 'Boban', Juma Nyoso, Yayo Lutimbi kutoka URA ya Uganda na Crispin Odula kutoka Bandari ya Kenya.

Sheikh ashambuliwa msikitini wakati wa Swala ya Eid, kisa....!


Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Diwani Athumani

WAUMINI wa dini ya Kiislamu waliokuwa katika ibada ya Swala ya Idd El Fitri katika msikiti mkuu wa Ijumaa uliopo Wilayani Kyela mkoani Mbeya jana walikumbwa na taharuki baada ya Shekhe wao aliyekuwa akiongoza ibada kuvamiwa kibla wakati akiendesha ibada na kujeruhiwa.
Tukio hilo la aina yake limetokea majira ya asubuhi ambapo Shekhe huyo aliyetambuliwa kwa jina la Nuhu Mwafilango alishambuliwa akiwa katikati ya sijida baada ya mtu mmoja aliyedaiwa kuwa ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya kutwa Kyela Ally Mwangosi kumpiga Shekhe huyo na kitu chenye ncha kali kichwani.
Taarifa kutoka msikitini hapo zinadai kuwa mara baada ya mwanafunzi huyo kupita upande wa Kibla na shekhe huyo na kupigwa chenye ncha kali alipiga ukelele wa kuomba msaada na hivyo kuibua taharuki miongoni wa waumini waliokuwa wakiswali msikitini hapo.
Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Wilayani Kyela Bw. Daudi Mwenda alisema kuwa mara baada ya Shekhe huyo kuvamiwa na kupigwa waumini walimuokoa na kumkimbiza katika Hospitali ya Wilaya kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Bw. Mwenda alisema kuwa Shekhe huyo ameumizwa vibaya eneo la kichwani ambapo damu nyingi zilivuja mara baada ya kupigwa na kwamba mbali na Shekhe huyo waumini wengine wawili waliokuwa wakijaribu kumuokoa walijeruhiwa kwa kuchomwa na visu.
Wengine waliojeruhiwa katika tukio hilo ni pamoja na mweka hazina wa BAKWATA wilaya Ustadhi Khamis Husein aliyejeruhiwa kichwani na sikioni.
Baadhi ya waumini waliokuwepo katika ibada hiyo walisema kuwa tukio hilo lilitokea wakati waumini wote wakiwa wamesujudu ndipo waliposikia kelele na vurugu ambapo aliinuka mtu mmoja aliyekuwa na kitu mfano wa nondo na kumpiga nayo Shekhe kichwani.
Mmoja wa waumini aliyejitambulisha kwa jina la Idd Husein alisema kuwa wakati kijana huyo aliyekuwa na kitu kinachofanana na nondo liliibuka kundi la watu wengine waliomsaidia na hivyo kuibuka vurugu kubwa iliyosababisha ibada ya swala ya Idd kuvunjika.
Akizungumzia tukio hilo Katibu wa BAKWATA mkoa wa Mbeya Shekhe Juma Killah alisema kuwa vurugu hizo zimetokea katika swala ya Idd na wahusika wa vurugu hizo ni waislamu ambao wanaipinga BAKWATA.
 ‘’Hiki ni kikundi cha waislamu waliotoka Jijini Dar es salaam kimekuja huku na kimesambaa katika wilaya zote za mkoa wa Mbeya kinashawishi watu kuipinga BAKWATA na  kinafanya mambo ambayo BAKWATA hatukubaliani nayo,’’alisema Shekhe Killah.
Alisema kuwa kikundi hicho kilikuwa kikimtuhumu Shekhe wa Wilaya kuwa ni mshirikina na kwamba kutokana na hali hiyo hakupaswa kuongoza ibada msikitini na badala yake wao ndio waliopaswa kuongoza ibada msikitini hapo.
Kwa upande wake Shekhe wa BAKWATA mkoa wa Mbeya Mohamed Mwansasu alisema kuwa kitendo hicho kimeudhalilisha Uislamu na kwamba kilichofanywa na kundi hilo la watu si mafundisho ya dini ya Kiislamu.
Hata hivyo Shekhe Mwansasu alienda mbali zaidi na kusema kuwa katika kikundi hicho wapo  baadhi ya waumini wanaodaiwa kuwa ni askari polisi ambapo inadaiwa kuwa katika moja ya swala ya Ijumaa wiki iliyopita imamu aliyekuwa akiswalisha alivutwa kanzu yake na kutakiwa kutoka eneo la kuongozea ibada ili kuwapisha wao waendeshe ibada hiyo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Bw. Athumani Diwani amekiri kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema kuwa watu sita wanashikiliwa na Polisi kufuatia vurugu hiyo iliyotokea majira ya saa 2:30 katika msikiti mkuu wa Ijumaa wakati wa swala ya Idd el Fitri.
Kamanda Diwani alisema kuwa kundi la waislamu wanaojiita kuwa ni wenye itikadi kali walivamia msikitini wakati waumini wengine wakiwa wameinama wakisujudu na kumvaa imamu kwa kumpiga kwa mateke na ngumi huku wakiwa na nondo, mikasi na visu.
Alisema waumini hao walikuwa na madai kuwa hawamtaki Shekhe huyo na kwamba uwezo wake ni mdogo katika dini.
Alisema kuwa Shekhe huyo aliokolewa na baadhi ya waislamu ambapo aliwataja walioshikiliwa na polisi kuwa ni pamoja na Mashaka Kassim(30)Issa Juma(37),Ahmed Kassim Magogo(35) Ibrahimu Shaaban(17) ambaye ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya kutwa ya Kyela anayesoma kidato cha Nne,Ambokile Mwangosi,(19)mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya sekondari Kyela, Sadick Abdul(28).

Kamanda Diwani alisema kuwa taratibu zinafanyika ili watuhumiwa wafikishwe mahakamani.

Polisi Zanzibar watangaza 'bingo' kwa waliowajeruhi Waingereza


 
KAMANDA wa Polisi, Kamishna Musa Ali Musa amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeahidi kutoa Shilingi milioni 10/= kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwa watu waliowashambulia mabinti wawili kutoka Londona, Uingereza,  Kirstie Trup na Katie Gee.

Mabinti hao walishambuliwa kwa tindikali usoni, kifuani na mikononi siku ya Jumatano walipokuwa njiani kuelekea kwenye chakula cha jioni.


Kwa sasa raia hao wameshapelekwa kwa Uingereza kwa ajili ya matibabu zaidi huku vyombo vya habari nchini humo vikilitia chumvi tukio hilo kiasi cha kuitia doa Tanzania mbele ya uso wa dunia.

Bomoabomoa ya maghorofa Dar yanza

ASKARI POLISI WAKIWA KATIKA DORIA WAKATI WA UBOMOAJI WA MAGOROFA KATIKA BARABARA YA SAMORA LEO


ENEO LA MAGOROFA YANAYOBOMOLEWA KATIKATI YA MJI BARABARA YA SAMORA JIJINI DAR ES SALAAM MAGOROFA HAYO YALE AMBAYO YAMESHA KUWA MAGOFU LEO

JIMMY MASTER NA UJIO MPYA WA DOUBLE J FINAL

Nguli wa filamuza (Action) nchini Jimmy Master akiwa ameshika
moja ya tuzo yake katika tuzo zilizoandaliwa na kampuni maarufu ya filamu 
nchini Steps.
YULE muongozaji na mwigizaji Jimmy Mponda 'Jimmy Master' aliyetikisa na mfululizo wa filamu za misuko iliyotoka sehemu ya kwanza hadi ya tatu na baadaye kujiongezea jina lingine akiitwa
J Plus.
Kwa sasa nyota huyo amefunguka  kuwa yukombioni kutoa muvi ya mwisho inayoitwa Doble J Final  huku ujio huo ukiwa ni wa mwisho kutoka baada ya kutangulia  na Doble J sehemu ya kwanza na yapili zilizotoka mwaka jana.
"Mwaka jana nilifanikiwa kukonga nyoyo za mashabiki wa filamu hususani wanaopagawa 
na filamu za mapigano na kujawa mambo ya  kipelelezi,"alisema J Plus.
Alisema Doble J Final pia ni ujio wake wa filamu nyingine ya mapigano na kuna heka heka za kipelelezi ndani. J Plus aliyezoeleka sasa katika kuonesha ubabe wa kufa mtu , kwa sasa ujio wake huo unao tazamiwa kuingia sokoni mapema tu , mwezi ujao .
Pia amemshirikisha mbabe mwingine katika filamu za mapigano Ibrahim Mbwana  'Bad Boy' na pia wamo nyota wengine katika dulu la filamu kama Charles Magari , Hashim Kambi na Veronica Viankero.

Miyeyusho amchapa Mzambia kwa KO Dar Live


Bondia Mtanzania Francis Miyeyusho (kulia)  akionyeshana kazi na Fidelis Lupupa wa Zambia wakati wa  mpambano wao wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika wakati wa Idd katika ukumbi wa Dar Live Mbagal, ambapo Miyeyusho alishinda kwa K.O ya raundi ya nane.

Bondia Kassim Rajabu akiumana na Kelvin Fabian katika pambano lao uliofanyika jana Dar Live, ambapo Fabian aliibuka mshindi kwa pointi.
Bondia Godfrey Pancho kushoto akioneshana ufundi wa kutupiana makonde na Hamisi Mohamedi wakati wa mpambano wao uliofanyika sikukuu ya Idd mosi katika ukumbi wa Dar Live Mbagala
Bondia Godfrey Pancho kulia akioneshana ufundi wa kutupiana makonde na Hamisi Mohamedi wakati wa mpambano wao uliofanyika sikukuu ya Idd mosi katika ukumbi wa Dar Live Mbagala
Bondia Chipaki Chipindi akiwa na mashabiki wake baada ya kumkarisha raundi ya kwanza bondia Ramadhani Kido

Bondia Fidelis Lupupa wa Zambia akiwa chini amekaa akijifikilia kuwa aendelee au asienderee baada ya kupigwa na bondia Mtanzania Francis Miyeyusho wakati wa mpambano wao uliofanyika katika ukumbi wa Dar Live Mbagala Dar es salaam Miyeyusho alishinda kwa KO ya raundi ya nane 
Bondia Mtanzania Francis Miyeyusho kulia  akipambana na Fidelis Lupupa wa Zambia wakati wa  mpambano wao wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika wakati wa Sikuku ya Iddi katika ukumbi wa Dar Live Mbagala Miyeyusho alishinda kwa K.O ya raundi ya nane 
Bondia Fidelis Lupupa wa Zambia akiwa chini amekaa akijifikilia kuwa aendelee au asienderee baada ya kupigwa na bondia Mtanzania Francis Miyeyusho wakati wa mpambano wao uliofanyika katika ukumbi wa Dar Live Mbagala Dar es salaam Miyeyusho alishinda kwa KO ya raundi ya nane 
Bondia Mtanzania Francis Miyeyusho kushoto  akipambana na Fidelis Lupupa wa Zambia wakati wa  mpambano wao wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika wakati wa Sikuku ya Iddi katika ukumbi wa Dar Live Mbagala Miyeyusho alishinda kwa KO ya raundi ya nane 

MIYEYUSHO AKISHANGILIA USHINDI

MIYEYUSHO AKIWA KATIKA POZI